You are on page 1of 3

MAHSUSI KWA WATU WA UJIJI TU

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na Mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo. Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu nyote. Sala na salam zimfikie Mtume wetu Muhammad (Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atushushie rehema zinazotoka kwake na atutengenezee uongofu katika jambo hili nililolikusudia AMINA. Ni muda mrefu sasa nimekuwa ninasongwa na jinsi mji wetu wa Ujiji unavyodidimia kana kwamba wenyewe hatuoni wala hatuna habari nao. Nimefanya subira huku nikitumaini kwamba si laiki yangu mimi kulisemea hili; isitoshe mimi si mweledi wa kuweza kujieleza kifasaha kiasi cha kweza kueleweka pasi na shaka yoyote. Muda umekuwa unapita kwa kasi mno; yalikuwa masiku, yakawa majuma, ikawa miezi na sasa miaka inapita. Jinsi muda unavyopita na mimi ndivyo ninavyozidi kusongwa. Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha leo hii kuliweka hadharani na ninatumaini litapokelewa na kutekelezwa kikamilifu. Sina sababu hata moja ya kuelezea UJIJI nini? Na ikiwa ni pamoja na watoto & wajukuu wote waliozaliwa na makundi haya. Yapo mambo mawili ambayo si vizuri kuacha kuyaweka bayana. Moja ni kwamba UJIJI ni mji unaoifanya Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/UJIJI. Pili, UJIJI pamoja na Kilwa ni miji miwili ya kwanza hapa Afrika Mashariki iliyokuwa imepimwa (surveyed towns) tokea wakati wa mkoloni. Kwa mshangao mkubwa UJIJI hiyo iliyokuwa mji uliopimwa tokea ukoloni hadi leo bado inasuasua sana kimaendeleo. Makazi duni, miundo mbinu mibovu, fursa za ajira au kujiajiri hazipo na mengineyo mengi kama kukosekana kwa hamasa ya elimu kwa vijana wetu na tatizo sugu la kupata mimba watoto na wajukuu zetu ilihali wakiwa na umri mdogo pamwe na kuwa masomoni (ngono zembe). Pamoja na mapungufu yote niliyoyataja hapa juu, nimeguswa sana na tatizo la makazi duni yaliyopo UJIJI. Miji mingine tatizo hili hujifuta lenyewe kwa sababu maendeleo huchukua mkondo wake hivyo suala la makazi duni hujifuta lenyewe. Kwa bahati nzuri UJIJI kila familia (kwa maana ya ukoo) inayo nyumba yao ya familia. UJIJI yote na nyumba zote zilikuwa za familia maalum. Nyingi ya nyumba hizo bado zipo ingawaje zimechoka sana au pamebakia viwanja. Kwa kupitia waraka huu ninaiomba kila familia (yaani ukoo) iimarishe numba yao (ya wazee wao) au waliyoachiwa na wazee wao kwa kutumia aidha matofali ya kufinya (yanayotumia udongo, simenti kidogo na mchanga kidogo), matofali ya kuchoma au matofali ya simenti. Kwa bahati mbaya ikiwa nyumba hiyo ya familia itakuwa imebomoka, basi ijengwe nyingine ili kuunusuru mji wetu wa UJIJI pia kuhuisha ukoo husika ambao ndiwo waasisi/wazawa wa UJIJI. Kwa taarifa tu, hivi sasa gharama ya tofali moja la kuchoma mpaka kulifikisha kwenye eneo la kujengea ni Shilingi150/= na gharama ya tripu moja yam awe kwa gari la tani 7 ni Shilingi 50,000/=. Kwa mtu mmoja kushughulikia ujenzi wa nyumba ya ukoo/familia inaweza kumwia vigumu ingawa kwa wengine inawezekana. Hivyobasi, kila wanaukoo/wanafamilia washirikiane ama kuiboresha au kuijenga nyumba yao hiyo moja tu.

Tuachane kabisa na ujenzi wa nyumba za udongo (za fito, kamba, kukandika na kuchapia). Tuepukane na uezekaji wa manyasi kwenye paa za nyumba. Tujenge vyoo bora na ambavyo havina gharama kubwa ili tukomeshe matumizi ya vyoo vya shimo na visivyokuwa na vibanda. Tupige vita nyua za makuti na manyasi. Haya shime WANAUJIJI, tuliangalie suala hili kwa mtazamo chanya. Kwa wale tulio nje ya UJIJI na Kigoma kwa ujumla, tusirubunike na hali bora iliyopo huko tuliko. Tunayo kila sababu ya kuimarisha na kukumbuka kwetu. Tuhamasishane bila ya kudharauliana, kusimangana au kunyanyasana. Tupitiane mtu kwa mtu, familia kwa familia, nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa, kata kwa kata na kitongoji kwa kitongoji. Suala hili halina utajiri wala ufukara. Wazazi wetu walikuwa wanatofautiana kimapato lakini kila familia ilikuwa inamiliki nyumba yake. Endapo familia husika itashirikiana kwa dhati (wale walio nje ya UJIJI) itafanikisha ujenzi wa nyumba yao hiyo ya familia kwa urahisi zaidi na matokeo yake yatakuwa ni ya kukumbukwa milele. Tuwachukulie wageni waliohamia kwa kasi UJIJI kuwa ni changamoto na fursa ya maendeleo mjini kwetu. Vile vile na sisi wazawa wa UJIJI hususan wale tulio nje ya UJIJI pia ni changamoto na fursa ya maendeleo ya UJIJI. Tunawajibika kurudisha shukurani kwenye mji ambao umetulea sisi na wazazi wetu. Ni jambo la aibu UJIJI kutufia mikononi mwetu (yaani katika kipindi chetu) ilihali mababu na mabibi zetu pamoja na baba na mama zetu walijitahidi kwa nguvu zao zote kuuimarisha. Suala hili ni sawa na mbio za vijiti. Hivi sasa ni zamu yetu kukimbiza kijiti hiki. Mbona inaonekana dhahiri kuwa aidha tumekata tamaa au tunazembea kwa sababu zisizokuwa na mashiko. Tukiiachia hali hii ya kuipa kisogo UJIJI iendelee kama ilivyofikia hivi sasa, sina shaka yoyote tutahukumiwa na kizazi chetu na kijacho kwa kuwafanya watu wasiokuwa na kwao kwa asili; ilihali papo na pa kuijivunia sana. Katika kuliuza suala langu hili kwenu wenzangu, nimesukumwa na utashi wa mapenzi na UJIJI. Sina wala sitarajii kuwa na azma yoyote ya kisiasa. Nitafarijika sana kama mtalipokea na kulifanyia kazi. Ninaomba wazo langu hili liwe chachu ya kuhamasisha mshawasha wa kuinusuru na kuiendeleza UJIJI; kusiwe na itikadi za dini, vyama vya siasa au ukabila katika zoezi hili. Nina wanasihi na kujinasihi mimi, tuziimarishe nyumba zile za familia zetu au tukiweza tujenge za kwetu wenyewe kasha tuone jinsi gani wale walio kwenye familia zetu (wake, waume, watoto na wajukuu wetu) watakavyokuwa wanamiminika kila mwaka kwenda UJIJI na wengine kuhamishia kabisa makazi yao UJIJI/Kigoma. Tusifanya ajizi katika kulitekeleza hili kama nilivyofanya mimi, kuchelewa kuufikisha ujumbe huu kwenu; kwani ladha ya mchuzi uunywe ukingali moto. Nichukue nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa wale wenzetu walioliona hili mapema na wakalifanyia kazi bila ya kusubiri kusukumwa na wengine. Nilitamani sana kuwataja majina yao lakini nimechelea mambo mawili; kwanza sikuwahi kupata ridhaa yao na pili isingekuwa vema kuwataja baadhi na baadhi kuwaacha. Itoshe kwamba wapo wenetu ambao wamekwishatuonesha njia; hivyo ni jukumu letu sasa sisi tuliosalia kuwafuata. Katika kuhamasisha, nimeweka kwenye kitongoni.blogspot.Com picha chache za ujenzi bora zilizojengwa na wenzetu ndani ya mji wa UJIJI.

Ninamwombna kila atakayeupata ujumbe huu, asikose kuufikisha kwa MWANAUJIJI mwenzake, pia amhamasishe kulitekeleza hili. Nitashukuru sana sana endapo watakuwapo watakaotoa nakala zaidi za ujumbe huu na kuwasambazia wengine ili uwafikie, kwani ukilifahamu tatizo upo nusu ya kulitatua.

Nimeona ninukuu semi chache ambazo zitasaidia kutuhamasisha kulitekeleza jambo hili:Nyumbani ni nyumbani japokuwa pangoni Mkataa kwao ni mtumwa Mwenda kwao si mtumwa Ukarimu huanzia nyumbani East, West home is best Mabadiliko yoyote hayaji hadi pale wahusika wanapokuwa wamejizatiti kuondoa mapungufu yaliyomo kwenye eneo lao Mabadiliko ni MIMI, ni WEWE ni SISI sote Kando ya ziwa la maji, Tanganyika kuna mji, Unaoitwa UJIJI, Nilizaliwa ghulamu. Ninakushukuru sana kwa kutumia muda wako adhimu kuusoma ujumbe wangu huu. Kwa yule ambaye kwa bahati mbaya atakuwa hajauelewa vizuri ujumbe huu, ninamwomba aurudie tena na tena huenda akapata maudhui yake katika nyakati hizi za marejeo. Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu, ninakuombna ujalie wazo langu hili lipokelewe kwa mikono miwili na wenzangu wote wakazi wa UJIJI na wale wanaopendelea maendeleo ya UJIJI. Uwafanyie wepesi katika kulitekeleza suala hili zaidi ya nilivyotarajia AMINA YA RABBIL ALAMINA. Wabillah Tawfiq. MWANAUJIJI MWENZENU

(Bilal Y. R. KaBange)

You might also like