You are on page 1of 3

P.O. Box 78172, Tel: +255 22 2762167, Fax: +255 22 2762168, E-Mail: misatanzania@gmail.

com ,Dar es Salaam,


Tanzania
SIKU YA KIMATAIFA YA HAKI YA KUPATA TAARIFA
SEPTEMBA 28, 2014
MAELEZO MAFUPI JUU YA SIKU HIYO NA MATOKEO YA UTAFITI WA UPATIKANAJI
TAARIFA KWENYE OFISI ZA UMMA, TANZANIA
Mwenyekiti wa MISA-TAN - Bwana Simon Berege.
Siku ya kimataifa ya haki ya kupata taarifa iliasisiwa mnamo Septemba 28 mwaka 2002 baada
ya mashirika mbalimbali ya kutetea uhuru wa habari duniani kukutana mjini Sofia, Bulgaria
na kuunda mtandao wa watetezi wa haki ya uhuru wa habari.
Malengo ya mtandao huu ni kutetea na kuhakikisha uhuru wa habari unatambulika na Katiba
mbalimbali za nchi kama haki ya msingi na pia kuhamasisha umuhimu wa uwazi na
uwajibikaji serikalini.
Kwa mantiki hiyo, tokea kuasisiwa kwa siku hii haki ya kupata taarifa, nchi mbalimbali
duniani zimekuwa zikiazimisha siku hii kwa namna tofauti.
Kwa sisi Tanzania kwa mwaka huu tunaadhimisha kwa kuzindua Ripoti ya Utafiti wa
upatikanaji taarifa katika ofisi mbalimbali za umma na kutoa TUZO kwa mshindi wa mwaka
2014 (Idara iliyofanya vizuri zaidi katika utoaji taarifa kwa umma) na TUZO ya Idara iliyofanya
vibaya zaidi katika utoaji taarifa.
Kimsingi, Utafiti huu hufanywa kila mwaka na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa
Afrika (MISA) katika nchi 11 wanachama wa Shirika la Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Hiyo ni kusema kwamba leo Ripoti hii inazinduliwa katika nchi hizo.
Lengo kubwa la kufanya utafiti huu ni kuona jinsi gani wananchi wa kawaida wanaweza
kupata taarifa muhimu ili ziwasaidie katika kufanya maamuzi sahihi yanayohusu maisha yao
binafsi na Taifa kwa ujumla.
Utafiti huu pia hutumika kama chombo cha kuwakumbusha walio madarakani hususan
katika ofisi mbalimbali za umma kutimiza wajibu wa kutumikia umma kwa uwazi na ukweli ili
kuleta maendeleo stahiki nchini.
Inafahamika kwamba mataifa mbalimbali yaliyoendelea kiuchumi na kijamii ni yale ambayo
watu wake wamemakinika kitaarifa. Watu hawa huusika sana ama kuchangia kwenye
mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ripoti za aina hii hutumika pia kama vyombo vya uzengezi (Advocacy) ili kuishawishi serikali
kutunga sheria ya haki ya kupata taarifa kwa wananchi wote.
Aidha ripoti hizi zinalenga kuhamasisha serikali zetu kuondokana na dhana ya USIRI ambayo
kwa kiasi kikubwa imechangia kurudisha maendeleo yetu nyuma.
Kutokana na usiri huo, watumishi wa umma wamekuwa wakitumia vibaya nafasi zao hata
pale pasipo stahili. Sio ajabu kupata barua za mialiko ya shughuli za serikali ama hata
kalenda zikiwa na mhuri wa SIRI.
UTAFITI NA VIGEZO VYAKE
Utafiti huu umehusisha idara nane za serikali. Kati ya hizo, 2 zinatoka kwenye utafiti
uliofanyika mwaka jana, ambapo alichukuliwa mshindi wa kwanza wa mwaka jana, ambaye
alikuwa ni Wizara ya Nishati na Madini ili kuona maendeleo yake toka ashinde na Yule wa
mwisho ambaye alikuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuona pia kama kutakuwa na
mabadiliko yoyote.
Taasisi nyingine zilizohusika ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Kituo cha Taifa
cha Takwimu (NBS), Idara ya Mahakama na Bunge.
Barua za maombi ya taarifa zilitumwa kwenye taasisi hizi na zilitolewa siku ishirini na moja
(21) kupata majibu. Pia tovuti (websites) za mashirika na taasisi hizi zilitafitiwa ili kuona ni
aina gani ya taarifa za umma hutolewa na kwa namna gani.
Zaidi ya hayo, watafiti pia walitembelea ofisi hizi na kupiga simu kwa nyakati tofauti kama njia
ya kujihakikishia upatikanaji wa taarifa mbalimbali kutoka kwa watumishi wa umma.
Kwa kila njia iliyotumika alama zilitolewa kwa kila taasisi na hivyo kupata mshindi. Kwa
mfano, kama taasisi ilijibu barua ndani ya siku 7 baada ya kupokea maombi, alama zake ni
tofauti na waliojibu siku 14 baadae na pia ni tofauti na ambao hawakujibu kabisa hata baada
ya siku 21 kupita.
Kuna ofisi ambazo ukipiga simu saa za kazi haiwezi kupokelewa, na wakati mwingine unaweza
kudhani labda mhusika katoka kidogo. Lakini unapopiga simu mara kadhaa kwa nyakati na
siku tofauti bila majibu, inatia shaka sana.
Hata hivyo jambo la kutia moyo sana ni matumizi ya tovuti. Taasisi nyingi zimefanya vizuri
katika eneo hili. Hata hivyo katika baadhi ya Idara, unaweza kupiga simu kuulizia taarifa
fulani, ukaambiwa haipo ama wahusika hawana ruhusa kuitoa, lakini ukienda kwenye tovuti,
unaikuta taarifa hiyo.
CHANGAMOTO:
Bado utamaduni wa kutoa mrejesho wa mawasiliano hauko vizuri. Kwa mfano umepata
baruapepe ama umepokea barua ya kawaida kutoka kwa mtumaji haujazoelekana sana
kurudisha majibu japo kusema kwamba umeipata.
Kadhalika, kuna watumishi ambao hawataki kutia sahihi vitabu vya kupokelea barua
zinapopelekwa kwenye ofisi husika, hii inajenga picha kwamba bado kuna watu hawataki
kuwajibika iwapo kutatokea barua kutoonekana baada ya kupokelewa. Na tumepambana na
kesi za aina hiyo kwenye tafiti zetu.
Bado utamaduni wa USIRI hata mambo ya kawaida kabisa upo na ni changamoto kubwa
kwenye utekelezaji wa mipango na miradi mbalimbli ya maendeleo.
HITIMISHO:
Kwa zaidi ya miaka mitano (5) ambayo utafiti huu umekuwa ukifanyika, kumekuwa na
mabadiliko makubwa kwenye taasisi husika kwa jinsi na namna wanavyofanya kazi na hasa
katika kuupatia umma taarifa muhimu pale zinahitajika.
Kwa mfano, utafiti ulifanywa kwenye tovuti ya Taasisi iliyokuwa ya mwisho mwaka jana
umeonesha mabadiliko makubwa kwenye utoaji wa taarifa kwa umma kwa njia ya mtandao.
PENDEKEZO:
MISA Tanzania inapendekeza mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi na hasa wale ambao
wanahusika moja kwa moja na utoaji taarifa kwa umma ili kujenga imani na wale wanaofika
kwenye taasisi hizo kwa nia ya kupata huduma mbalimbali. Hapa tunasisitiza sana maafisa
habari, watumishi wa mapokezi na wale wa masjala.
Kuzindua Ripoti
Baada ya kutoa maelezo hayo, naomba sasa kukata utepe kuzindua ramsi chapisho hili kwa
matumizi halali ya umma.
Kutangaza Washindi:
Baada ya kuzindua Chapisho hili napenda sasa kuwatangazia kuwa Taasisi inayochukua
TUZO ya KUFULI LA DHAHABU kwa kubana sana taarifa kwa mwaka 2014 kuwa ni Idara ya
Mahakama.
Na Taasisi inayochukua TUZO ya UFUNGO WA DHAHABU kwa kufunguka sana kwa umma
kwa mwaka 2014 ni Idara ya Taifa ya Takwimu (NBS).

You might also like