You are on page 1of 2

HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI

jumapili, 6 februari 2011 Yaliyopita Pekua Tovuti

JK alifanyia siasa sakata la Dowans


• AKANA KUWA NA HISA KATIKA KAMPUNI HIYO

na Mwandishi wetu

RAIS Jakaya Kikwete ameungana na wananchi wanaopinga hukumu ya Mahakama ya


Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) inayolitaka Shirika la Umeme nchini
(TANESCO) kuilipa Kampuni ya Dowans fidia ya dola za Marekani milioni 94 kwa kosa la
kuvunja mkataba.
Kikwete alitoa kauli hiyo yenye mwelekeo wa kupoza hasira za makundi mbalimbali ya
kijamii na kisiasa yanayoendelea kujitokeza kupinga hukumu hiyo ambayo utekelezaji wake
unaweza ukaanza siku chache zijazo iwapo juhudi za kuzuia kusajiliwa kwake zitagonga
mwamba.
“Nataka kuwahakikishia kuwa na mie ni miongoni mwa wale wasiotaka TANESCO ilipe,
hivyo kauli za kuhusika na Dowans zinanishangaza, maana nisingeamua hivyo katika Kamati
Kuu na Kamati ya Wabunge wa CCM. Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi,” alisema
Kikwete.
Awali kabla ya kutoa hitimisho hilo, Kikwete alitoa kauli iliyoonyesha kuielezea Dowans kama
kampuni ambayo ilifanikiwa kuleta mitambo ya kuzalisha umeme ambayo baada ya kuwasili
nchini ilisaidia kupunguza makali ya tatizo la mgawo wa umeme.
“Baada ya hapo Kampuni ya Richmond ikauza mkataba wake kwa Kampuni ya Dowans
ambayo ilileta mitambo na uzalishaji wa umeme ukafanyika na kupunguza kabisa makali ya
mgawo,” alisema.
Kikwete ambaye alikuwa akihutubia wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya
kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema tayari wameshawaelekeza wanasheria
kushirikiana na wale wa TANESCO kutafuta namna ya kukwepa kulipa kiasi hicho kikubwa
cha fedha.
Alisema uamuzi wake wa kulizungumzia suala hilo la Dowans umekuja baada ya kuwapo
kwa watu wengi ambao wamekuwa wakihoji juu ya ukimya wake.
Akizungumzia madai kwamba amekuwa kimya kwa kuwa kampuni hiyo inahusishwa na rafiki
yake ambaye hata hivyo hakumtaja, Kikwete alisema hilo lisingeweza likamfanya
akashindwa kuchukua hatua.
“Sina ajizi wala kigugumizi cha kuchukua hatua kwa sababu ya rafiki yangu au hata kama
angekuwa ndugu yangu kahusika… “Maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu na Kamati ya
Chama ya Wabunge wa CCM yalifanywa chini ya uongozi wangu. Ni uthibitisho tosha wa
ukweli huo. Waliokuwepo kwenye vikao hivyo wanajua ukweli wa haya ninayosema.
Ningekuwa na masilahi au hofu tusingefanya uamuzi ule,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kueleza historia ya sakata zima la Dowans kuanzia katika Kampuni ya
Richmond ambayo ilishindwa kutimiza mkataba hata kulazimika kuuza.
Pasipo kuingia kwa undani, Kikwete alisema kabla ya mkataba ulioipa ushindi Richmond
kupita taratibu za kisheria za ukodishwaji wa mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura
zilifuatwa na serikali ikaombwa kugharamia ukodishwaji huo.
Akisimulia kuhusu kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa pasipo kumtaja
kwa jina, Rais Kikwete alisema tuhuma zilizoelekezwa kwake kwamba ndiye mwenye
kampuni hazikuthibitika.
Alisema Lowassa alilazimika kujiuzulu kwa sababu yeye ndiye aliyetoa kauli ya kukubali
Richmond ipewe tenda ili kuepusha nchi isiwe gizani.
Akizungumzia madai ya Katiba mpya, Rais Kikwete alisema mchakato wa kuitazama upya
katiba ya sasa ili kuihuisha na kupata kile alichokiita “Katiba mpya”, utaanzishwa mwaka huu.
Kwamba hivi sasa matayarisho yanaendelea serikalini ili kupeleka bungeni muswada wa
sheria wa kuanzisha mchakato huo, ikijumuisha pia kuundwa kwa tume ya kuongoza
mchakato huo.
“Napenda kuwahakikishia wananchi wenzangu kuwa sisi katika serikali na CCM ni miongoni
mwa wadau wakubwa wanaotaka Katiba ihuishwe kukidhi mahitaji ya wakati tulionao na
matarajio yetu ya baadaye.
“Sisi sote ni wadau wa mabadiliko ya Katiba yetu ya sasa…niwaombe kuwa wakati huo
ukifika Wana CCM na wananchi tujitokeze kwa wingi katika kutoa maoni na katika kupiga kura
ya maoni itakayoidhinisha Katiba hiyo”, alisema.

converted by Web2PDFConvert.com
Hata hivyo, mtindo huo wa kuihuisha au kuiboresha katiba ya sasa tayari umepingwa na
wasomi, wanaharakati na wananchi mbalimbali wanaotaka katiba iandikwe upya.
Akizungumzia wimbi la maandamano na migomo inayoendelea nchini, Rais Kikwete
alisema hali hiyo inasababishwa na kuwepo kwa mipango ya makusudi ya uvunjifu wa
amani kwa kutumia njia hiyo, huku akigusia vurugu zilizotokea jijini Arusha kati ya polisi na
wananchi kama mfano wa mipango hiyo aliyodai inasukwa na wanasiasa ili kujitafutia
ushindi mwaka 2015.
Hata hivyo, maelezo hayo yameonekana kutofautiana na hali halisi ya migomo na
maandamano hayo, kwani ajenda yake kuu imekuwa ni kudai haki na maslahi, yakiwamo ya
wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, walimu na wafanyakazi wa mashirika ya umma au ya
vyama vya siasa na wananchi kupinga ukiukwaji wa demokrasia kama ilivyotokea katika
uchaguzi wa umeya jijini Arusha.
Tafiti za wasomi na taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali nchini zimethibitisha kuwa uvunjifu
wa amani umekuwa ukifanywa zaidi na Jeshi la Polisi linapojaribu kusambaratisha
maandamano ya haki na ya amani yanayofanywa na wananchi.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alisema kuwa nguvu ya vyama vya upinzani
imeongezeka na kusababisha ruzuku ya CCM ipungue, hivyo aliwataka Wana CCM kubuni
vyanzo vingine zaidi vya mapato ili kuiimarisha kiuchumi.
Aidha, alikiri kuwa Wana CCM wamekuwa wakitishwa na kunyong’onyezwa na mafanikio ya
CHADEMAiliyoyapata katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Sanjari na kukiri hilo, Rais Kikwete alitumia sehemu ya hotuba yake hiyo kurejea tena
matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kwa kutoa maelezo ya kuwatia moyo Wana CCM,
akiwataka wasiwe wanyonge kwani bado chama chao kilijitahidi kupata ushindi mkubwa.
Akionekana kuiacha CUF na kuishambulia zaidi CHADEMAhuku akitumia maneno yenye
husuda ya kisiasa ndani yake, Rais Kikwete alisema: “Nadhani tunatishwa na kelele na
propaganda za chama fulani na bwana Fulani, ambazo zinajenga hisia kama vile wako wengi
sana na wamepata ushindi mkubwa sana hata kuliko CCM. “Hilo si kweli, ingawaje safari hii
wamepata viti vingi kuliko uchaguzi uliopita.
“Kwa nini tujisikie wanyonge baada ya kupata ushindi mnono kiasi hicho?” alisema Rais
Kikwete.

juu

Habari Mpya | Matangazo | Bei zetu | Wasiliana nasi | Tuma habari | Webmaster
Copyright 2011 © FreeMedia Ltd.

Wasomaji
© free media limited 2011
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233 • faksi +255-22-2126234 • selula 0713 296570
hit counter

converted by Web2PDFConvert.com

You might also like