HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII MHE. DKT HUSSEIN ALI MWINYI (MB.

) KATIKA HAFLA FUPI YA KUGAWA VIFAA/NYENZO ZA KUJIMUDU KWA WATU WENYE ULEMAVU KATIKA, TAREHE 15/02/2013

      

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; Kaimu Mganga Mkuu; Kamishna wa Ustawi wa Jamii; Wakurugenzi wote; Wakurugenzi Wasaidizi; Ndugu Wanahabari; Mabibi na Wabwana.

Kwanza kabisa napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia uhai na afya njema na kutuwezesha kufika mwaka huu 2013 tukiwa wenye afya njema. Mabibi na Mabwana, Leo hii tumekutana hapa kwa dhumuni moja tu la kutoa vifaa vya kujimudu kwa watu wenye ulemavu kwa kuwa tunatambua kuwa tunao wajibu wa kufanya hivyo kwa watu wenye ulemavu. Mabibi na Mabwana, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii inao wajibu wa kusimamia utoaji wa huduma mbalimbali za ustawi wa jamii nchini zikiwemo huduma kwa makundi maalum wakiwemo watu wenye ulemavu. Huduma hizo zimekuwa zikitolewa kwa kuzingatia bajeti ya Serikali na kwa kutambua ufinyu wa bajeti.

Mabibi na Mabwana, Serikali ina dhamira ya kweli kuhakikisha kuwa maisha na usalama kwa watu wenye ulemavu yanaboreshwa. Kwa kutambua na kuthamini hilo serikali imetekeleza yafuatayo:
1

Mwaka 2004 serikali ilipitisha Sera ya maendeleo ya huduma kwa watu wenye ulemavu. Sera hii ni muhimu katika kuwatambua watu wenye ulemavu na ushiriki wao katika mipango mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni. Aidha, msingi wa Sera hii umejengwa kwa lengo la kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu katika jamii. Serikali pia imesaini mkataba wa Kimataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu (UN Convention on the Rights of Persons with Disabilities) mnamo mwezi Machi 2007 na mnamo tarehe 23 Aprili, 2009, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kikao cha Bunge iliridhia Mkataba wa Kimataifa juu ya haki za Watu Wenye ulemavu.

Mabibi na Mabwana, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na wadau wengine, imeandaa mwongozo wa utambuzi wa mapema wa watoto wenye ulemavu. Mwongozo huu utatoa mchango mkubwa katika kuwatambua watoto wenye ulemavu mapema pamoja na kupanga afua kulingana na mahitaji yao pia utambuzi huo wa mapema utasaidia kupunguza athari za ulemavu ukubwani.

Mabibi na Mabwana, Mwaka 2010 Serikali ilipitisha sheria Na.9 ya watu wenye ulemavu. Sheria hii inatoa mwongozo wa kisheria wa namna ya kutoa huduma za afya, misaada ya kijamii, kufikika na kupitika kwa huduma na mazingira ya kijamii, huduma za utengamao, elimu na mafunzo ya ufundi, mawasiliano, ajira na hifadhi za kazi pamoja na kudumisha haki za msingi za watu wenye ulemavu. Sheria hii ni muhimu kwa kuwa inaweka uhalali wa adhabu kwa watu wanaovunja haki za watu wenye ulemavu.

Mabibi na Mabwana, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inatoa huduma katika vyuo vya watu wenye ulemavu 5 na makazi 17 ya wazee na watu walemavu nchi. Hii yote ni katika kuboresha maisha na usalama wa watu wenye ulemavu. Serikali inatoa huduma ya chakula, matibabu, elimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika vyuo hivyo, huduma za utengamao, nyenzo za kujimudu na ushauri nasaha.

2

Mabibi na Mabwana, Serikali kupitia Wizara ya Afya na ustawi wa jamii imenunua vifaa mbalimbali kupitia Idara ya ustawi wa jamii ili kuwawezesha wazee walioko kwenye makazi yetu na watu wenye ulemavu kumudu maisha yao na pia kuweza kujongea kutoka sehemu moja hadi nyingine. Vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:

Na: 1. 2. 3. 4. 5. 6. 7. 8. 9. 10. 11. 12. 13. 14. 15.

Vifaa Magodoro (3x6x6) Mashuka Wheelchair Stretchers Vitanda vya Chuma Blanket Special Caps (Kofia) Bajaji Elbow Clutches Obstacle Detector Note taker Perking Braile Machine White cane Language Master Dictionary Computer with Dolfin Software

Idadi 1,292 4,000 30 20 117 1,000 100 10 100 1 10 1 100 5 10

Thamani ya vifaa hivi ni shilingi milioni mia tano (500,000,000/=).

3

Mabibi na Mabwana, Napenda kumalizia kwa kusema kuwa vifaa vitakavyogawiwa leo hii ni matokeo ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuwawezesha watu wenye ulemavu kumudu maisha yao binafsi na napenda kuwasihi msitumie vifaa hivi kibiashara au kuviuza. Aidha, napenda niwaombe wote mtakaopata vifaa hivi mvitunze vizuri mkijua kuwa kuna watu wengine wenye ulemavu kama nyie ambao nao wanahitaji vifaa hivyo lakini kulingana na uwezo wa serikali hatukuweza kuwapatia wote kwa pamoja. Napenda kuahidi kuwa vifaa hivi vitakuwa vinatolewa kadri bajeti ya serikali itakavyokuwa inaruhusu. Ahsanteni kwa kunisikiliza!

4

Sign up to vote on this title
UsefulNot useful