You are on page 1of 14

1

Utenzi wa Mamlaka Kamili ya Zanzibar


1. Ilahi kwa jina lako Leo twatoa tamko Lifike tukutakako Nako liweze pokewa 2. Lipokewe kwa hishima Adabu na taadhima Sababu tunolisema Hadhi yake twalijuwa 3. Tamko hili hakika Linahusu Mamlaka Kamili yasiyo shaka Ya Taifa la Visiwa 4. Ni Mamlaka Kamili Ya Watwani Zinjibari Ndiyo kwa sasa kauli Sote tunayoitoa 5. Ni tamko la kusudi La nia kuiradidi La kuilinda ahadi Na hishima ya uzawa 6. Ni tamko la kiapo Nacho hakitangukipo Wala hakitaangukapo Na wala kugeukiwa 7. Ni tamko la fakhari Ya kuwa Wazanzibari Tamko la ujuburi Na kwalo hatuna haya 8. Wakati twalitamka Ya Rabbi tuna hakika Ni Wewe uliyetaka Sisi hapa kuzaliwa 9. Ni Wewe Muumba wetu Ulotaka pawe petu

2 Zinjibari iwe yetu Ndipo ukatugaiya 10. Tangu zamani za kale Zama hizo za wavyele Ulitaka iwe vile Zinjibari biladiya 11. Waliotutangulia Nchi wakatuachia Na wanaofuatia Wajibu kuikutia 12. Ndipo kwa huo wajibu Leo hii twakutubu Tunayo kila sababu Watani kuutetea 13. Twatetea nchi yetu Kwamba hapa ndipo petu Ikenda hatuna chetu Tuwezacho kiringia 14. Mtu kupenda Watani Si tendo la kihaini Bali li kwenye imani Ni wajibu kisheria 15. Tutaulinda Watani Kwa nguvu na kwa imani Kwa kudura ya Manani Zenji yangu tabakia 16. Na kushinda ni lazima Nchi ibaki salama Tuwarithishe na wana Kitu cha kujivunia 17. Wana wairithi kheri Ya kuwa Wazanzibari Kamwe wasirithi shari Adha ya kutawaliwa 18. Waurithi utukufu Kheri ya umaarufu Wasirithi udhaifu 2

3 Uyatima na ukiwa 19. Uyatima si kukosa Baba na mama kwa sasa Uyatima ni kufisa Nchi yako ya uzawa 20. Mayatima ndio hao Watu wasio na kwao Waso chao waso lao Waso mava kuzikiwa 21. Nasi hilo hatutaki Wenetu wapate dhiki Kisha wakose rafiki Na bega la kulilia 22. Mtu hasa rafikiye Si yule alaye naye Walakini ni nchiye Kitovu ilozikiwa 23. Watwani ndiye swahibu Watwani ndiye muhibu Watwani ndiye tabibu Ndiye ponyo ndiye dawa 24. Ndipo twataka wenetu Wairithi nchi yetu Na warithi neno letu La nchi kupigania 25. Wasipiganie mali Wala vyeo na magari Wapiganie kauli Nchi yao ya uzawa 26. Rabbi kwa rehema zako Lilinde hili tamko Lende mbele nyuma mwiko Lipe nguvu na satuwa 27. Lisimamishie kweli Madhubuti mihimili Na liwe sauti kali Isiyodharauliwa 3

28. Lipe nguvu ya ajabu Ulizompa Habibu Kwenye Badri harubu Ushindi akachukua 30. Lipe kila mantiki Naliwe halipingiki Naliwe halianguki Hata linapotishiwa 31. Lifanye liwe ni hoja Wapemba na Waunguja Wote wajile pamoja Nchi yao kukomboa 32. Liwe ni neno la wote Wazenji wawe popote Wakiuzwa wasisite Tamko hili kutoa 33. Salama usalimini Tusikwame safarini Tuwashinde mafatani Rabbi Wewe wawajua 34. Rabbi tulinde wajao Kwa kheri ya ulinzio Na hao tuwambiao Nao walinde sawia 35. Linda viongozi wetu Walobeba ajenda yetu Wavushe taifa letu Lende tulikoridhia 36. Baba wa Maridhiano Wawili waso mfano Sefu, Karume ni wano Dua tunowaombea 37. Mpe nguvu Malimu Sefu Aongoze hii safu Kwenda kwenye utukufu Wa nchi hii aliya!

5 38. Tuepushe Bwana wetu Yalopatwa nchi yetu Tangu sitini na tatu Na yaliyofuatia 39. Tukinge na kuchuuzwa Kama dagaa kauzwa Na shimoni kaingizwa Kwenye mdomo wa chewa 40. Mwaka sitini na nne Mzee wetu Karume Aliendewa kinyume Kumvini akapetewa 41. Yeye na Mchongameno Walifanya mapatano Wakayeta Muungano Jamhuri Tanzania 42. Hilo lekuwa ni pigo Kubwa mno sio dogo La kuitia upogo Zinjibari baladiya 43. Karume akajitosa Mtegoni akanasa Hata lipojitikisa Eshindwa kujinasua 44. Masikini hakujua Muunganoni kungia Kwekuwa nyengine nia Nyerere alonuia 45. Kule kwenye nia yake Nyerere yuli na lake Alimtega mwenzake Na mwenzake akangia 46. Ushahidi mwingi mno Kuthibitisha maneno Hakutaka Muungano Nyerere twakuapia 47. Alitaka aishike 5

6 Mikononi isitoke Nchi hii iwe yake Na wanawe alozaa 48. Etaka aidhibiti Zenji isijizatiti Choyoche na dhulumati Zipate kutimilia 59. Aliwahi kutamka Angeweza alitaka Zinjibari kuifyeka Baharini kuitia 60. Lakini uwezo huo Nyerere hakuwa nao Ndipo akafanya mbio Makuchani kuitia 61. Akamtisha Karume Kuungana aungame Sivyo angoje aone Atakavyopinduliwa 62. Msiba ukatufika Nchi kufanywa sadaka Ikapewa Tanganyika Na bure-ghali ikawa 63. Hivyo ndivyo livyokuwa Madaraka kutwaliwa Zenji ikapokwa pawa Na nguvu za kuamua 64. Sivyo wanavyotamka Udugu wa Afrika Ndiyo sababu hakika Nchi yetu kunyakuwa 65. Sivyo wanavyotamka Kwamba ati Tanganyika Na Unguja zilitaka Udugu wao kukua 66. Na sivyo wanavyosema Sababu ni usalama 6

7 Zinjibari ingekwama Bila ya kuegemea 67. Vilivyo ndivyo ni kuwa Walikwisha kuamua Zinjibari kunyakuwa Vyovyote vitavyokuwa 66. Wemfadhili Karume Wakamtisha kiume Kusudi mwisho akwame Nchi wapatwe itwaa 67. Na kwenye hili hakika Karume eghafilika Wakapata walotaka Muradi wao ukawa 68. Wakabadilisha mambo Ya mijini na viambo Wakatunga na uongo Na njia za kulindia 69. Kazi ikawa kulinda Uongo waliounda Kusudi tuwe mapanda Wana wa Zinjibaria 70. Mkubwa ubaya wao Walofanya watu hao Ni kugeuza kibao Cha tarikhi ya Visiwa 71. Tarehe ikageuzwa Ubaguzi katukuzwa Na chuki kapandikizwa Kwenye vichwa na vifua 72. Tukalazwa usingizi Wazenji tusimaizi Kamsahau Mwenyezi Na dini yake Nabiya 73. Tukalazwa usingizi Kwayo kali hino dozi Mwishowe wake majambazi 7

8 Nchi wakaikwapua 74. Ndipo leo tukasema Haya yapaswa kukoma Nchi hii ina zama Na enzi za kuenziwa 75. Naukome ukoloni Uliopangwa zamani Uliotuweka duni Na bado ukabakia 76. Ikome hii alama Waziwazi inosema Kwamba Zenji si salama Wala huru haijawa 77. Kikome hiki kichonge Cha ukoloni mkongwe Uhusiano mazonge Na wenye dhamira mbaya 78. Ikome hii ishara Ioneshayo hasara Kupoteza kwetu dira Na hishima ya uzawa

79. Sasa na ije hishima Ya taifa lenye dhima Ya imara kusimama Liwezalo jiinua 80. Sasa tuwe na kauli Ya mambo kuyaamili Na Mamlaka Kamili Kwayo nchi ya uzawa 81. Sasa tuwe kila kitu Kale kilokua chetu Kikatwawa na wenzetu Kwa maguvu na kwa riya 82. Tunacho tulobakisha 8

9 Kuweza kuijulisha Ingalipo haijesha Nchi yetu ya uzawa 83. Tunayo hiyo imani Na mapenzi kwa Watwani Yametuganda nyoyoni Wameshindwa kuyatoa 84. Mungu katubakishia Dhamira na njema nia Na viongozi shujaa Wa mbele kuelekea 85. Hiyo ndiyo nguvu yetu Nao ndio mwanzo wetu Kwenendea lengo letu Hako wa kutuzuia 86. Ndipo tukasema basi Kugeuzwa matopasi Basi kunyimwa nafasi Na nguvu za kuamua 87. Na hino ndilo tamko Na ni kwetu litokako Tunasema sasa mwiko Nchi hii kuonewa 88. Sasa twasema hakika Jambo tunalolitaka Ni mamlaka haraka Kamili yasiyo doa 89. Mamlaka tusemayo Twayataka leo leo Wala si mtondogoo Ndivyo tushavyoamua 90. Vipi hilo lifanyike Litimu likamilike Tutawapa njia yake Na vituo vya kutua 91. Awali isimu yake Lazima ifahamike 9

10 Hapana mume na mke Na kwamba hii si ndoa 92. Waziwazi kwa maneno Zote kwenye Muungano Jamhuri kwa hizino Ziwe zinatambuliwa 93. Pili ni kwenye mipaka Si pa mdogo na kaka Kila taifa lataka Liweze jifaragua 94. Mpaka wa Tanganyika Utajwe ulipofika Wetu siye kadhalika Unapo lipoanzia 95. Tatu kwenye uraia Nchi inojivunia Ni watuwe kutambua Na pia kusimamia 96. Nne uraia wetu Tuwe pasipoti zetu Tano ni polisi yetu Na uhamiaji pia 97. Saba mbele ya dunia Wawe wanatutambua Na bendera kupepea Ya Dola Zinjibaria 98. Na tuwe na mabalozi Wa taifa lenye hadhi Wangie kwenye arudhi Na mikataba kutia 99. Nane ni sarafu yetu Pesa yetu wenye wetu Pamwe na benki zetu Uchumi kusimamia 100. Kumi mambo ya siasa Hatuyataki kabisa Tena kuyachanganyisha 10

11 Sababu yanatugawa 101. Kila nchi iwe navyo Vyamavye ivitakavyo Madaraka vishikavyo Kwa kura kwisha pigiwa 111. Mwisho yatayobakia Muunganoni kutiwa Lazima pawe na njia Namna ya kuyendea 112. Na hayo kila upande Uridhie uyapende Pasiwe kutiwa mbinde Na mtutu kushikiwa 113. Hayo ndiyo tutakayo Kwenye katiba ijayo Ila kinyume cha hayo Wallahi twaikataa 114. Kwenye kura ya maoni Haipiti asilani Katiba isodhamini Mamlaka yenye pawa 115. Hilo ndilo tusemalo Wazenji tulitakalo Kinyume na jambo hilo Hatukhofu kuamua 116. Laiti hayatokua Basi koti twalivua Hakuna tunochelea Wala tunachokhofia 117. Lau kama hawataki Muungano kuhakiki Kauli yetu ya haki Ni kuvunja hii ndoa 118. Hatuchelei kutoka Muunganoni hakika Lakini tunalotaka Pawe haki na usawa 11

12

119. Fitina naisitishwe Na vitisho tusitishwe Na wao nawakumbushwe Kwamba sisi meamua 120. Kama waja wa kusoma Basi waone alama Mbele zilizosimama Za wakati kufikia 121. Wasome nawaelewe Kisha nao waamuwe Kwamba ni sisi wenyewe Sasa tuliopania 122. Ni sisi Wazanzibari Ambao tunadhukuri Kwa kheri ama kwa shari Hatutaki tawaliwa 123. Hatukatai umoja Nasi kwao tuna haja Bali linalotufuja Ni huku kutawaliwa 124. Twakataa ukoloni Wa Dodoma uso soni Unaoua imani Na hishima ya raia 125. Hiyo ndiyo hoja yetu Ndio uamuzi wetu Haturudi nyuma katu Mbele tutaendelea 126. Dhamira ya Mapinduzi Ilikuwa iko wazi Uhuru na uamuzi Nchi kujiamulia 127. Mapinduzi kuyalinda Ni kwa nchi kuipenda Sio kuwacha ikenda Ikamezwa kapotea

12

13 128. Basi Ilahi wadudi Ilinde na mahasidi Ilinde na mafisadi Nchi waloikamia 129. Kile kilichobakia Kwenye yetu biladiya Kilinde kisijetwawa Nacho kikeshapotea 130. Ilahi tupe umoja Wapemba na Waunguja Tuweze kujenga hoja Ya nchi kujilindia 131. Ya Rabbi tupe mapenzi Tuchukie ubaguzi Tushikane kama wenzi Mapacha tuvyozaliwa 132. Ya Karima Mola wetu Hupungukiwi na kitu Ukitupa nchi yetu Kama vile livyokuwa 133. Kwako Bwana tuombacho Sio zaidi ya hicho Tufumbue yetu macho Na nuru kututilia 134. Tuwezeshe kungamua Kosa tulilokosea Kisha tuongoze njia Ya hapa kujinasua 135. Lau hii ni adhabu Kwa mambo tuloharibu Kwako Ghafaru twatubu Na toba zetu pokea 136. Zipokee toba zetu Ufanye ujira wetu Ni kutupa nchi yetu Kama vile livyokuwa 137. Wewe Bwana hufundishwi 13

14 Na wala hurekebishwi Na wala hulazimishwi Watenda unoamua 138. Ukitaka jambo kuwa Husema Kuwa likawa Sababu u mwenye quwa Na ilimu iso doa 139. Lakini hatuna budi Kukuomba Ya Majidi Sisi ni wako ibadi Tunaokutegemea 140. Kwa rehemazo Wadudi Na dua za Muhammadi Tumiminie suudi Bariki hivi Visiwa 141. Swala nyingi na salamu Zende kwa Abu Qassimu Na sahabaze kiramu Na wakeze wote pia 142. Na wote maiti wetu Wazazi nao wenetu Warehemu Mola wetu Kwa Fatiha tunotia

14