THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

· Nia yake ya kuendeleza masomo ya hisabati na sayansi ·Rais Kikwete amesema Serikali itachukua hatua ili kianzishwe haraka · Akutana na Mkurugenzi wa Chuo kinachojulikana kama AIMS Chuo Kikubwa cha kufundisha na kuendeleza masomo ya Hisabati na Sayansi duniani imeamua kufungua Kampasi yake ya kuandaa wataalamu wa kuendeleza masomo hayo katika Tanzania kwa njia mbali mbali ikiwa ni pamoja na ufundishaji wa masomo hayo kwenye ngazi mbali mbali za elimu. Uamuzi wa kuanzishwa kwa Kampasi hiyo katika Tanzania ulitangazwa jana, Ijumaa, Septemba 20, 2013, wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipokutana kwa mazungumzo na Mwenyekiti wa Chuo hicho kijulikanacho rasmi kama Taasisi ya African Institute for Mathematical Sciences (AIMS), Profesa Neil Turok anbaye pia tokea mwaka 2008, amekuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Perimeter Institute for Theoretical Physics ambayo inahusiana na AIMS. Rais Kikwete alikutana na Profesa Neil Turok kwenye Chuo Kikuu cha Guelph cha Toronto nchini Canada baada ya Rais Kikwete kuwa ametunukiwa na kupokea Shahada ya Uzamivu ya Udaktari wa Sheria (Honorary Doctor of Laws – Honoris Causa) na chuo hicho jana, Ijumaa, Septemba 20, 2013. Profesa Turok alikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria sherehe za tunuku hiyo kwa Mheshimiwa Rais na kwenye chakula cha jioni kilichofuatia sherehe ya tunuku. Profesa Turok ambaye alipata kuishi Tanzania wakati akiwa mdogo alimwambia Rais Kikwete kuwa AIMS imeamua kuanzisha Kampasi yake mpya katika Tanzania ambayo itaanza kazi kwa kasi itakayokwenda kwa kasi ya kutolewa jengo ambako

Kampasi hiyo inaweza kuanzishwa. AIMS inaomba Serikali kutoa jengo hili kwa ajili ya kuanzishwa kwa Kampasi hiyo. AIMS yenye makao yake Muizeberg, Jimbo la Western Cape, Afrika Kusini ina matawi mawili katika Afrika – moja likiwa eneo la Mbour, karibu na Dakar, Senegal na nyingine ikiwa kwenye mji mdogo wa pwani ya Ghana wa Biriwa. AIMS ilipata kuwa na Kampasi kwenye Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Afrika cha African University of Science and Technology (AUST) iliyojulikana kama AIMS-Abuja, Nigeria. Baada ya kupewa maelezo ya jitihada za kuanzisha Kampasi hiyo katika Tanzania, Rais Kikwete alimhakikishia Profesa Turok kuwa Serikali yake itaiwezesha Taasisi hiyo kuanzisha Kampasi katika Tanzania na kuwa itachangia raslimali za kufanikisha uanzishwaji na uendeshaji wa Kampasi hiyo. AIMS ilianzishwa Septemba, mwaka 2003, Afrika Kusini ikiwa ni ushirikiano baina ya Vyuo Vikuu vya Stellenbosch, Cape Town na Western Cape vya Afrika Kusini, Vyuo Vikuu vya Oxford na Cambridge vya Uingereza na Chuo Kiku cha Paris-Sud cha Ufaransa kwa nia ya kuendeleza masomo ya Hisabati na Sayansi katika Afrika. Taasisi hiyo ilianzishwa na Profesa Turok wakati alipokuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Hisabati na Fizikia (Mathematical Physics) kwenye Chuo Kikuu cha Cambridge. Profesa Neil Turok ni mtoto wa Mheshimiwa Ben Turok, Mbunge wa Chama cha African National Congress (ANC) katika Bunge la Afrika Kusini. Mheshimiwa Turok alipata kuwa mpigania uhuru na kuishi katika Tanzania. Profesa Neil Turok alipata elimu yake ya Msingi ya Bunge, mjini Dar Es Salaam. Katika mazungumzo na Rais Kikwete, Profesa Turok alisema kuwa Taasisi yake imekuwa ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kuanzisha Kampasi ya AIMS kwenye eneo la Silver Sands, Dar es Salaam lakini mazungumzo yenyewe yamekuwa hayana kasi ya kutosha. Shabaha kubwa ya AIMS ambayo hutoa shahada za utatifi kwa ngazi mbali mbali inalenga kutoa wanafunzi wenye uwezo wa kufanya utafiti wenye ubora wa kiwango cha juu katika masuala ya sayansi. Mwaka jana, AIMS ilikuwa na jumla ya wanafunzi 75. Aidha, AIMS inalenga kutoa mwanayansi maarufu duniani kama alivyokuwa Albert Einstein chini ya mpango wake wa Next Einstein Initiative. Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya siku tatu ya kikazi katika Canada ameondoka mjini Toronto asubuhi ya leo, Jumamosi, Septemba 21, 2013, kwenda mjini New York, Marekani ambako atakutana na viongozi mbali mbali duniani na pia kuhudhuria na kuhutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) mwaka huu.

Imetolewa na: Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, DAR ES SALAAM. 21 Septemba, 2013

Sign up to vote on this title
UsefulNot useful