You are on page 1of 7

1

Risala ya MVIWATA kwa Mgeni Rasmi, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma


Mheshimiwa SAIDI MWAMBUNGU
Kilele cha Maadhimisho ya Nane Nane, Tarehe 8 Agosti, 2014 katika
uwanja wa John Mwakangale Mkoani Mbeya
Ndugu Mgeni Rasmi, kwanza tunatoa shukrani zetu za dhati kwako
binafsi kwa kukubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi katika kilele hiki
cha maadhimisho ya siku kuu ya wakulima, yaani Nane Nane.
Tunatambua uzito na ukubwa wa majukumu yako na kwa hiyo
tunashukuru kwa kutupa heshima hii sisi wakulima ya kuwa nasi leo hii
katika maadhimisho haya.
Pili tunatoa shukrani kwa viongozi wote waliofikilia kuwepo kwa
maonesho ya wakulima kila mwaka ili kutoa fursa kwa wakulima
kujifunza, kutangaza shughuli zao za kilimo na kukutana na watoa
huduma mbali mbali za kilimo. Tunawashukuru waandaaji wa
maadhimisho ya Nane Nane kwani kwa kweli yamefana sana.
Ndugu Mgeni Rasmi, pili, tunapenda kutambua na kumpongeza Rais
wetu kwa kuanzisha mchakato wa uandishi wa Katiba mpya ya Tanzania
kwani umetoa mwanya kwetu sisi wananchi kujadili na kuchangia
mustakabali wa Taifa letu, tunaamini mchakato unaoendelea hivi sasa
utatoa katiba inayolinda maslahi ya wakulima wadogo.
2

Ndugu Mgeni Rasmi, tunapenda pia kuipongeza serikali yetu ya awamu
ya nne kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo na tunatambua
juhudi mbalimbali za serikali yetu za kukuza sekta ya kilimo ili iwe
injini ya ukuaji wa uchumi wetu.
Ndugu Mgeni Rasmi, MVIWATA ni chombo cha wakulima
kilichoundwa kwa lengo la kuwaunganisha wakulima wadogo ili kuwa
na sauti moja yenye nguvu katika kutetea maslahi yao kiuchumi, kijamii,
kiutamaduni na kisiasa. Mtandao huu ulianzishwa mwaka 1993 na
wakulima wadogo walioungana ili kuwa na sauti ya pamoja, kwa sasa
MVIWATA inawanachama katika mikoa yote ya Tanzania bara na
visiwani.

Ndugu Mgeni Rasmi,kama chombo cha wakulima, MVIWATA
imefanikiwa kufanya mambo mengi ya mafanikio ikiwemo;
1. Kuunganisha wakulima wadogo katika vikundi na mitandao
inayohusisha wanachama takribani 150,000 na wanufaikaji zaidi
ya milioni mbili.
2. Kuwezesha utoaji wa huduma za akiba na mikopo kwa
kuhamasisha uanzishaji wa SACCOS zisizopungua 100 ambazo
zimewezesha mikopo ya takribani shilingi bilioni 5 kwa mwaka.
3. Kushughulikia masuala mtambuka
Ndugu Mgeni Rasmi, Kama kauli mbiu ya mwaka huu ya
maadhimisho ya nane nane inavyosema
MATOKEO MAKUBWA SASA Kilimo ni biashara
3

Katika kukifanya kilimo kuwa biashara MVIWATA imekuwa
ikifanya mambo yafuatayo:
Kutoa mafunzo kwa wakulima juu ujasiriamali na kilimo
biashara
Kutoa elimu ya uzalishaji bora wa mazao ya kilimo
Kuunganisha wakulima na masoko kwa kuboresha miundo
mbinu ya masoko ambapo mpaka sasa masoko tisa yamejengwa
likiwemo Igagala wilaya ya wangingombe mkoani Njombe,
soko la mchele Igurusi wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, soko
la mahindi la Matai na soko la samaki Kasanga yaliyopo
wilayani Kalambo mkoani Rukwa, soko la kibaigwa Kongwa
Dodoma, masoko matatu ya matunda yaliyopo Morogoro vijini
na Mvomero mkoani morogoro na soko la Mkata handeni
Tanga. Tathimini zinaonyesha masoko haya yameweza
kuchangia kukuza kipato cha wakulima
Kuanzisha mfumo wa taarifa za masoko ambao kwa miaka
mitatu tangu uanze umenufaisha takribani watu 90,000
MVIWATA pia imekuwa ikiwezesha vikao mbali mbali kati ya
wakulima, wanunuzi na wadau wengine katika biashara ya
mazao. Na kama njia ya kuwaunganisha wakulima na masoko
MVIWATA imekuwa ikishiriki maonyesho ya Nane Nane kila
mwaka katika Viwanja mbali mbali.
Ndugu mgeni rasmi, kutokana na shughuli hizi kumekuwa na
mafanikio mengi kwa wakulima kujipanga na kufanya mambo yao
kwa pamoja, kwa kutumia mifumo ya masoko iliyotajwa, wakulima
katika baadhi ya maeneo wameweza kuongeza kipato chao. Na kwa
4

kushiriki Nane Nane wakulima wanaweza kujifunza, kutangaza
biashara yao, kukutana na watoa huduma za kilimo wanaotoa ushauri
na bidhaa pembejeo za kilimo. Mafanikio haya yamechangiwa kwa
kiasi kikubwa kwa upande mmoja na ari ya wakulima wenyewe
katika kujiletea maendeleo na kwa upande wa pili changamoto
mbalimbali zinazowakabili.
Ndugu Mgeni Rasmi, licha ya mafanikio hayo na licha ya juhudi za
serikali kukuza sekta ya kilimo; wakulima wadogo wanakumbana na
changamoto nyingi sana.
Kwanza; migogoro ya mara kwa mara ya ardhi ambayo
tunaogopeshwa na kasi ya ongezeko la migogoro hiyo. Aghalabu,
migogoro mingi inasababishwa na msongamano na mbanano wa
wazalishaji wadogo wakiwemo wakulimana wafugaji, msongamano
na mbanano huo unatokana na kuongezeka kwa ugawaji wa maeneo
mengi yenye rutuba kwa makampuni na wakulikma wakubwa. Kwa
miaka kadhaa hivi karibuni tumeshuhudia kasi ya ugawaji wa maeneo
mengi yenye rutuba kwa makampuni na wakulima wakubwa kama
njia ya kuongeza uwekezaji wa kilimo. Licha ya kutambua umuhimu
wa uwekezaji katika kilimo, mashaka yetu ni kwamba katika maeneo
mengi, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali yamewabakiza wakulima
wadogo kama wahanga badala ya kuwaendeleza.
Kuna taarifa na ushahidi wa makampuni na wawekezaji ambao
wanatafuta ardhi kwa lengo la kuhodhi tu na sio kutumia kwa
kuzalisha. Baadhi ya makampuni na wawekezaji wanatumia ardhi
hiyo kukodisha kwa bei ya juu, inayofikia shilingi 120,000 kwa ekari
kwa wakulima wadogo na wafugaji waliopoteza ardhi zao, licha ya
wao wenyewe, yaani makampuni na wawekezaji, kupata ardhi hizo
kwa bei nafuu na kulipa serikalini kodi ya ardhi ndogo tu.
5

Ndugu Mgeni Rasmi, tunaishauri serikali yetu ichuje na kuchunguza
mfumo uliopo wa uwekezaji katika ardhi ambao tunaona unahitaji
kurekebishwa. Aidha tunashauri njia muafaka itumike ili kuhakikisha
ulinzi wa wakulima unaimarishwa kwani tunaamini uwekezaji
endelevu unamtambua, unamlinda na kumweka katika kipaumbele
mkulima mdogo kama mwekezaji wa kwanza.
Ndugu Mgeni Rasmi, pili ni suala la masoko ya mazao. Tungependa
kutambua na kuipongeza hatua ya Rais wetu Dkt. Jakaya Kikwete ya
kuondoa marufuku ya kuuza mazao ya wakulima nje kadri
wanavyoona soko linafaa. Hatua hiyo ya Mheshimiwa Rais
itakamilika kwa kurekebisha Sheria ya mwaka 1991 Sura ya iii
sehemu ya 8 kifungu kidogo cha 2 h) ambacho bado kinatoa nguvu ya
kisheria ya kurejesha marufuku ya kuuza mazao nje.
Hata hivyo, suala la uhakika wa soko la mazao bado ni changamoto
kubwa sana, ikiwemo uwepo wa vikwazo vingi vinavyokwamisha
mkulima kuuza kwa bei bora. Tunaishauri serikali yetu kuondoa
vikwazo vilivyobaki, ikiwemo, ushuru kwa mazao ya wakulima
wadogo pamoja na vikwazo vya barabarani.
Ndugu Mgeni Rasmi, tatu ni suala la ushiriki mdogo wa wakulima
wadogo katika maamuzi na uundaji wa sera mbalimbali za kilimo; na
aghalabu ushiriki huo mdogo ni katika hatua za mwisho mwisho tu za
kuhitimisha uundaji wa sera hizo. Tunaamini kwamba ni ushiriki
kamili wa wakulima wadogo katika uundaji wa sera ndio utapelekea
kuwa na sera zinazoangalia maslahi ya wakulima wadogo.
Ndugu Mgeni Rasmi, pembejeo bado ni changamoto kubwa sana.
Mfumo wa usambazaji wa pembejeo umekumbwa na hujuma ambapo
pembejeo za kilimo zisizo halisi (feki) kama vile mbegu, madawa na
mbolea zimezagaa bila udhibiti. Hujuma hii imesababisha hasara
6

kubwa na usumbufu kwa wakulima. Sambamba na hilo, mfumo wa
usambazaji wa pembejeo za ruzuku bado ni tatizo kubwa na
unakabiliwa na ufisadi mkubwa katika ngazi mbalimbali. Ni
mapendekezo yetu kwamba mfumo huu ufutwe na itafutwe njia
mbadala ya kuwawezesha wakulima kupata pembejeo wanazohitaji
ambayo haitakuwa uchochoro mwingine wa ufisadi.
Ndugu Mgeni Rasmi, changamoto nyingine ni kukosekana kwa mitaji
ya kutosha kwa wakulima wadogo. Tunatambua na kupongeza juhudi
za serikali yetu za kuanzisha benki ya wakulima ambayo tuna taarifa
za ujumla kwamba mchakato huo unaendelea. Mfumo wa sasa wa
kibenki bado haujatoa fursa kwa wakulima wadogo kutumia huduma
za kibenki. Hapa tunatoa mfano wa wamiliki binafsi wa mashine za
kukoboa mpunga katika soko jipya la Mchele la Igurusi wilayani
Mbarali ambao licha ya kuanza kwa kuweka mitaji yao kidogo,
wameshindwa na masharti ya kuwawezesha kupata mikopo ya
kuendeleza usindikaji wa mchele. Suala ambalo lina mchango
mkubwa kwa kilimo cha mpunga. Hii ni fursa kubwa yenye manufaa
makubwa katika sekta ya kilimo cha mpuga lakini bahati mbaya
haijasaidiwa.
Kwa upande mwingine ingawa wakulima wenyewe wamefanya bidii
ya kuanzisha vyombo vyao vya kifedha, limeibuka suala jipya la
kutoza kodi SACCOS zinazoanza kuamka ni changamoto mpya
ambayo inatishia uhai na maendeleo ya SACCOS hizo. Suala hili
linaleta utatanishi kwa sababu kwa upande mmoja wenye mitaji
mikubwa wanapewa misamaha ya kodi na kwa upande mwingine
wale wanyonge wanaoanza kuinuka ndiyo wanaobanwa kulipa kodi.
Ndugu Mgeni Rasmi, mwisho tunapenda kukushukuru kwa mara
nyingine kuwa mgeni wetu rasmi, tunashukuru uongozi wa mkoa
7

wetu wa Mbeya, Tunashukuru TASO kanda ya Nyanda za juu kusini
kwa kusimamia na kuratibu shughuli hizi za Nane Nane kwa mwaka
2014
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki
wakulima wadogo.
Mwenyekiti MVIWATA Mbeya