You are on page 1of 2

WENYE SILAHA ZA NYUKILIA TUHAKIKISHIENI USALAMA TANZANIA

Na Mwandishi Maalum, New York


Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeungana na mataifa mengine wapenda
amani katika kuyachagiza mataifa yenye silaha za nyukilia kuonesha utashi na
utayari wa kweli wa kutekeleza mkataba unaodhibiti usambaaji holela wa silaha
hizo ( NPT).
Kauli ya kuyataka mataifa hayo yenye silaha za nyukilia kuutekeleza Mkataba
huo imetolewa siku ya jumanne na Balozi Ramadhan Mwinyi, Naibu Mwakilishi
wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa. Ilikuwa ni wakati Kamati ya
Kwanza ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ilipokuwa ikijadili ajenda inayohusu
silaha za nyukilia na tisho lake kwa usalama na amani ya dunia.
Katika mchango wake, Katika kamati hiyo inayohusika na masuala ya upokonyaji
wa silaha na Amani ya kimataifa,Tanzania licha ya kuyataka mataifa yenye silaha
hizo kuchukua hatua za kuzipunguza na kuzidhibiti, imekwenda mbali zaidi kwa
kuyataka pia kuihakikishia dunia usalama wake.
Akatoa wito kwa mataifa yenye silaha hizo kuzingatia masharti ya Mkataba wa
NPT.
Balozi Mwinyi amesema Tanzania kama ilivyo kwa mataifa mengine, pamoja na
kuunga mkono juhudi za upunguzaji na udhibiti wa silaha za nyukilia, pia inaunga
mkono umuhimu wa kuwapo kwa maeneo huru yasiyo na silaha za nyukilia kama
sehemu ya kuihakikishia dunia usalama.
Hata hivyo akasema, inasikitisha kuwa licha ya nia hiyo njema ya kuwa na maeneo
huru yasiyo na silaha za nyukilia bado kumekuwa na kusuasua katika majadiliano
ya kuanzishwa wa eneo huru katika Mashariki ya Kati.
Katika hatua nyingine Tanzania imelitaka Shirika linalohusika na masuala ya
nguvu za nyukilia kuhakikisha kuwa elimu na teknolojia inayohusiana na masuala
ya nyukilia inatolewa kwa mataifa yote pasipo ubaguzi.
Akasisitiza kuwa Tanzania inaunga mkono matumizi sahihi na salama ya nishati ya
nguvu za nyukilia na ni kwasababu hiyo inasisitiza kila taifa kuwa na haki ya
kupata elimu na teknolojia inayohusiana na eneo hilo.
Majadiliano kuhusu ajenda hiyo ya silaha za nyukilia mara zote inapojadiliwa
huwa na vuta nikuvute ya aina yake na malumbano ya hapa na pale , kutokana
na ukweli kuwa zile nchi ambazo hazina silaha hizo zimekuwa zikisisitiza haja na
umuhumu wa kutekeleza mkataba wa NPT huku mataifa yenye silaha hizo
yakitetea uhalali wa umiliki wa silaha hizo au zikiainisha hatua ambazo zimeaza
kuchukua katika kuzipunguza hatua ambazo Jumuiya ya Kimataifa inasema
hazitoshi.
Wapo baadhi ya wazungumzaji ambao walieleza wazi wazi kutoridhishwa na
baadhi ya nchi ambazo licha ya kuwa zinamiliki silaha hizo, lakini hadi sasa
hazijakiri hadharani kuwa zinamiliki na hivyo kuwa sehemu ya kikwazo katika
mchakato mzima wa kuzidhibiti.
Vile vile zipo nchi zinazomiliki silaha hizo ambazo zimeeleza bayana kwamba
hazitaacha utengenezaji wake au hata majaribio mpaka pale mataifa makubwa
nayo yatakapoonyesha utashi wa kweli wa nia ya kufanya hivyo
Hapana shaka kwamba kuendelea kuwapo kwa silaha hizo za nyukilia na
kutokuwapo kwa uwazi au utashi wa kisiasa wa kuzipunguza, dunia bado
itaendelea kukabiliwa na changamoto ya silaha hizo za maagamizi.

You might also like