You are on page 1of 7

1

Msingi wa Makosa Katika Mchakato wa Kutafuta na Kupata Viongozi wa


Kisiasa Tanzania na Suluhisho Lake

Sehemu ya Pili
Katika sehemu ya kwanza ya makala haya, nilieleza ni kwa jinsi gani nchi yetu
ya Tanzania kwa muda mrefu imejikuta kwenye tatizo kubwa la kutafuta na
kupata viongozi katika ngazi zote za utawala wa nchi yetu. Nilionesha ni jinsi
gani uongozi wa kisiasa umegeuzwa kuwa mtaji mkubwa wa uwekezaji kwa
mafanikio ya watu binafsi na walio karibu nao. Kama vile haitoshi hali hii
imepelekea siasa kupanda mbegu mbaya na kuifanya jamii kutothamini
taaluma, utaalamu na uwajibikaji mwingine wa kimaendeleo kwa raia. Naomba
niendelee na sehemu hii ya pili.

Hatuna Misingi na Mfumo Imara wa Kudumu wa Kitaasisi na Kijamii wa
Kuwandaa Viongozi Waliobeba Maono ya Nchi

Nilipoanza kazi katika taasisi ya elimu ya juu niliambiwa kwamba; ukiwa katika
hatua ya awali kama mwanataaluma (mkufunzi) unakuwa bado hujafuzu
kufundisha madarasa ya shahada kwa kuwa unakua nawe ni mwanafunzi.
Katika kipindi cha ukufunzi, niliambiwa nitatakiwa kuwa chini ya mhadhiri
mwandamizi ili pamoja na mambo mengine nijifunze kutoka kwake uzoefu wa
kufanya tafiti, kufundisha (kutoa mihadhara) na kujishughulisha na utoaji wa
huduma za jamii. Niliambiwa natakiwa kujifunza haiba ya kitaaluma ili kuwa
mwanataaluma na nilielezewa kwa undani kwa nini sio sahihi kuichukulia kazi
ya taaluma kama mahali pa kutafutia utajiri. Kwamba nilipitia malezi hayo chini
ya waandamizi kama ilivyotakikana au vinginevyo, sio sehemu ya makala
haya.

Kwa mzazi yeyote yule anayewaangalia watoto wake kwa mtazamo wa ni aina
gani ya watu anataka kuwaona toka kwa watoto wake, ni lazima awaandae
watoto wake kwa mtazamo huo. Ni lazima ile picha au maono aliyonayo juu ya
watoto wake vitafsiriwe katika vitendo ili kuwajengea uwezo wa kutimiza yale
anayoyategemea kutoka kwao. Itakua ni kitu cha ajabu sana iwapo mzazi
huyu atategemea tu kuona watoto wake wanakua wa aina fulani au kufuata
mwenendo wake (kama ndio kaweka kuwa kielelezo) bila yeye kuwaonesha
njia. Kwa kufanya hivyo itakua ni kutotambua wajibu wa mzazi katika malezi
2

na makuzi na ni sawa na kuruhusu kichaka kikue nje ya nyumba huku
ukitegemea baadaye iwe ni miti ya matunda.

Familia za kifalme huwa ziko makini sana katika malezi ya watoto
wanaozaliwa katika familia zao. Kuanzia mtoto anavyozaliwa, kukua kwake,
elimu yake na yote yanayoendelea katika mazingira yake, vinalenga
kumuandaa kuwa mfalme. Anajengea haiba, ujuzi, akili, ustaarabu na kila
kinachotakikana kuonekana toka kwa mfalme. Wakati wa kurithisha ufalme
unapowadia ama kwa umri, ugonjwa au kifo kwa mfalme aliyeko, hakuna hofu
wala mashaka juu ya urithi wa kitu cha ufalme kwani kila mtu anajua ni akina
nani wameandaliwa na wanafaa kushika mamlaka ya kifalme.

Taifa letu halina mfumo sahihi unaojulikana wa kuandaa viongozi. Hili sio
tatizo la kisiasa au kiserikali tu, bali ni tatizo la kitaifa kwani hata katika ngazi
ya familia, ni wazazi wachache sana wanawandaa watoto wao kwa ajili ya
kubeba majukumu ya kesho. Familia nyingi zimebuni aina ya malezi ambayo
hayawaandai watoto kwa ajili ya maisha ya kesho kwanza kama wanafamilia
wawajibikaji na pili kama raia wazalendo na watumishi wa taifa na nchi yao.
Wazazi wengi wanadhani kuwapeleka watoto wao shule fulanifulani zenye
majina na gharama kubwa, ndio kipimo cha makuzi mazuri kwa watoto wao
huku wa kijitahidi kuwalea "kimayai" bila kuwaonesha "kadhia ya kufuga kuku".
Tatizo hili limetapaa kila eneo kuanzia kampuni binafsi, mashirika ya umma,
taasisi za dini,vyama vya siasa na uongozi wa nchi. Hakuna mfumo mzuri wa
kurithishana madaraka, malaka, ujuzi wala uzoefu na ndio mana kila
mabadiliko ya lazima ya kiuongozi huwa yanaleta mvutano na hofu kwenye
jamii.

Ukitaka kuelewa ninachomaanisha, anza kutazama familia yenu au nyingine
unayoijua, nini kilitokea baba ua mama au mtu mwingine yoyote aliyekua
anaonekana kama nguzo kwenye jamii alipofariki. Jaribu kukumbuka ni
biashara na makampuni mangapi yalifikia mwisho wa kukua kwake au yalikufa
kabisa siku kiongozi mkuu mwanzilishi alipolala uzingizi usio na mwisho.
Jaribu kukumbuka, kwenye dini yenu, nini kilitokea ilipolazimika kiongozi mkuu
aliyekuwepo alipolazimika kuondoka au kuondoshwa katika nafasi
aliyokuwepo. Tumekuwa tukisikia vita, mashindano na mivutano mikubwa
katika baadhi ya makanisa ya mahali pamoja, madhehebu ya dini, misikiti na
taasisi zao pale kunapotokea mabadiliko ya uongozi. Kwa nini? Hakuna
maandalizi ya uongozi na kama wapo ni ambao hawajaandaliwa kubeba
maono mapana ya tasisi husika.

Wakati huohuo, tasisi kama Kanisa Katoliki, wana mifumo imara sana ya
kuandaa viongozi na kurithisha maono ya tasisi yao toka kizazi hadi kizazi.
Ukienda nchi yoyote duniani, utendaji wa kanisa Katoliki ni kama unafanana.
Ukitoka Jimbo la Katoliki la Arusha ukahamia Jimbu Kuu la Sumbawanga,
huna kazi ya kujifunza namna mpya ya uendeshaji wa mambo, kwani mfumo
ni mmoja na viongozi wameandaliwa kubeba maono ya Kikatoliki. Sina
kumbukumbu ya kusikia vita vya uongozi ndani ya Parokia na Majimbo ya
3

kanisa Katoliki na kama kuna tofauti basi ni ndogo sana na wanaweza
kukabiliana nazo bila kutoka nje ya milango ya makanisa yao.

Tatizo hili pana, ndilo limetutafuna sana, kwani kwa muda mrefu na karibu
maeneo mengi ya uwepo wa nchi yetu, viongozi wanapatikana kwa
kubahatisha na hakuna mikakati mahsusi ya kuwaandaa na kuwaweka katika
nafasi stahiki. Wako watu ambao wanaweza kujenga hoja kwamba
ninachokiongea kina walakini na kudai kwamba viongozi wanaandaliwa. Iwapo
wako wenye hoja hii nina maswali kadhaa ya kuwauliza:

1. Ni mfumo gani rasmi tuliona wa kuanda viongozi katika nchi yetu?
2. Tunawaandaje viongozi wetu?
3. Tunatumia muongozo gani wa kitaifa kuwaandaa viongozi?
4. Ni kina nani wanatuandalia viongozi?
5. Wanaotuandalia viongozi wana haiba na maadili gani?
6. Tuliwapataje wanaotuandalia viongozi?
7. Wanaondaliwa ni akina nani na wanapatikanaje?

Nikiazima neno la msanii mcheshaji ajulikanaye kama Masanja Mkandamizaji,
"Enzi za Mwalimu" kulikua na utaratibu wa kuandaa viongozi. Pamoja na
taratibu zingine za kichama, kulikua na jitihada za wazi za kuandaa viongozi
kitaasisi zaidi na ndio maana tulikua na vyuo kama cha Magogoni ambacho
kilitumika kutoa mafunzo ya kiungozi na kusambaza sera na misingi ya
utawala wa chama kilichokua kimeshika hatamu. Pamoja na ukweli huu, bado
kulikua na kasoro kubwa pia katika utaratibu huu kwani kwa sehemu kubwa
chuo hiki kilitumika kufundisha (kuandaa?) watu ambao tayari walikua
wamepewa majukumu ya kiungozi na hivyo ilikua ni mahali pa kuwapa
mafunzo ya muda mfupi juu ya majukumu yaliyo mbele yao. Waliongia kwenye
chuo hiki na vingine kama vilikuwepo, walikuwa ni "wateuliwa" waliobahatika
kupewa nafasi kutokana na mazingira yaliyokuwepo. Bado hatukuwa na
maandalizi kwa maana ya kulea kizazi cha viongozi waliothibitika kuwa
wanafaa kubebeshwa "Utanzania" ndani ya mioyo yao, ambao wako radhi
kujitoa mhanga ili kuiona nchi yao inaboreka kila siku.4

Kwa muda mrefu kumekua na mijadala miongoni mwa wasomi na hata
wananchi wa kawaida iwapo ni kweli Baba wa Taifa aliandaa watu sahihi wa
kurithi kuongoza nchi. Mijadala na lawama hizi zimejengwa katika ukweli
kwamba; tangu Mwalimu aondoke kizazi alichokiacha madarakani na
kilichofuata, kwa sehemu kubwa kimeshindwa kabisa kusimamia yale
aliyoyaamini na kuyasimamia kwa muda wote wa maisha yake ya uongozi na
ujenzi wa taifa letu. Watu wanahoji, iweje hawa walioandaliwa kuwa
waungwana na wasimamizi wa maadili wabadilike kuwa watu wa kuleta majuto
kwa watanzania; kuleta maumivu kwenye maisha na kukatisha tamaa huku
wao na familia zao wakineemeka na kuishi katikati yetu kwa viwango vya
"kimbingu" huku sisi tukiteseka. Sina lengo la kumkosoa Baba wa Taifa letu
Mwalimu Nyerere kuwa hakuandaa vionogi, bali najenga picha pana ya
chanzo na uzito wa tatizo la uongozi katika nchi yetu. Maswali kama haya
yanwasumbua pia raia wa Afrika Kusini kwani hawaoni kama Mzee Madiba
Mandela amewaachia warithi waliobeba maono yake kuhusu ustawi wa watu
weusi.

Mjadala huu unaongezea nguvu hoja yangu kuwa Tanzania hatujawa na
mifumo mizuri ya kitaasisi ya kuandaa viongozi kwa ajili ya kushika nafasi za
kitaifa na kitaasisi kwa maendeleo ya nchi yetu. Tumekuwa taifa la kuongozwa
na viongozi wacheza bahati nasibu na mara nyingine tumejikuta twaongozwa
hata na watu ambayo hawako tayari kutuongoza na wanaona nafasi
walizopewa sio jambo la kufurahia kwao na ni mzigo kwenye maisha hayo;
lazima mradi liende. Katika shauku yangu ya kufuatilia viongozi mbalimbali
kuna kipindi nilijipa kazi ya kufahamu ni kwa njia gani nchi kama China wasio
na uchaguzi wa kidemokrasia kwa maana ya kupata rais kupitia sanduku la
kura wanavyopata kiongozi wap bila ugomvi wala vita. Nilisoma kwa undani
kidogo ni jinsi gani Rais wa sasa wa China aliandaliwa kushika nafasi
aliyonayo. Nilishangazwa na mfumo wa chama cha kimomunisti cha watu wa
China unaotumika kuandaa viongozi.


Marais wa Chinaaliyepita na wa sasa (Hu J untao na Xi J inping)
5

Mara kadhaa tumeambiwa kuwa nchi kama China, India, Malaysia, Indonesia,
Korea na nyingine nyingi, zilikua na hali mbaya ya kiuchumi karibu sawa na
sisi miaka 40 au 50 iliyopita. Tumekua tukiimba sana huu wimbo na tumeusikia
sana toka kwa wanasiasa huku kukiwa hakuna wazo mbadala la kututoa sisi
hapa tulipo. Ukifuatilia vizuri, utagundua kuwa maaendeleo ya nchi hizi
yamejengwa katika maono na misingi ya uendeshaji taifa iliyowekwa na
viongozi waliokuwepo miaka ya 1950 hadi 1970. Utagundua kile
kinachoendelea sasa ni mwendelezo wa fikra na maono yaleyale. Bila shaka
utakubaliana na mimi kuwa, mataifa haya yaliandaa mifumo ya kitaasisi ya
kutengeneza viongozi wa kubeba maono na mipango yao ya kimaendeleo na
ndio maana wamefanikiwa kwa sehemu kubwa. Sio tu kwamba wana mipango
mizuri, lakini wameandaa watu wa kubeba mipango hii na kuiweka katika
utekelezaji kitaasisi zaidi. Na kinachofurahisha zaidi ni kuwa, watu hawa wana
mifumo inayoandaa viongozi bila kujali mitazamo na mapenzi yao ya kisiasa
na hivyo haijalishi sana ni nani atakua madarakani, bado ana maono na uwezo
wa kuilea ndoto ya nchi yake.

Kinyume na wenzetu hawa, sisi tumekua tukiendeshwa na maono ya
wanaopata uongozi ambao nao tunawapata ama kwa kubahatisha au kupewa
na waliowandaa kwa maslahi yao. Kila anayepata uongozi wa nchi au taasisi,
anakuja na maono na taratibu zake za kufanya mambo na mara nyingi ama ni
tofauti sana na za aliyemtangulia au vinapingana kabisa ili naye aonekane
kafanya kuliko aliyemtangulia. Na hii imepelekea nchi yetu na taasisi zake
kuendeshwa kimajaribio kwa kuwa eneo la kufanyia tafiti wa mawazo ya nani
yanafanya kazi zaidi tofauti na mwingine. Kwa mwenendo huu, tumekuwa na
nchi na taasisi za umma zisizo na dira inayoeleweka na wingi wa miradi ya
muda mfupi ambayo sio tu inashindwa kuendelezwa na wanaorithi uongozi
bali hata walionzisha wanashindwa kuiendeleza ndani ya uongozi wao na
mara nyingine hata wanasahau kuwa walinzisha kitu cha namna hiyo.

Kati ya madhara mengi yatokanayo na tatizo hili kubwa la kitaifa, ni kupata
viongozi wasio na uwezo wa kuyafikia matarajio yetu. Tunapata viongozi
ambao wamejiandaa wao wenyewe au wameandaliwa na kikundi fulani
chenye maslahi yao ambayo mara nyingi sisi kama taifa hata hatuyajui na
tunakuja tu kuona utekelezaji pindi viongozi husika wanapoanza wajibu wao.
Tumekuwa na viongozi wasioogopa mfumo wala watu wanaowaongoza.
Kuanzia ngazi ya vijiji, kwa sehemu kubwa nchi inaongozwa na watu
wanaosimamia maslahi yao binafsi na wengi wao hawana hofu kabisa kwa
kushindwa kutimiza matarajio ya wanaowangoza. Na kwa kuwa hatuna mfumo
wa kuandaa viongozi wanaobeba maono ya kitaifa na kitaasisi, tunakosa
nguvu ya kimaadili na kisheria kuwawajibisha au kuhoji utendaji wao na hata
tukifanya hivyo wana uwezo wa kutujibu wapendavyo...kwa nini?...uongozi
walionao ni mradi wao binafsi na waliwekeza rasilimali zao kuupata hivyo
hakuna wa kuwahoji wala kuwalazimisha wasimamie maono wasiyoyajua.
Hawakuandaliwa kwa hayo, hivyo hawawajibiki kwa lolote zaidi ya maono
yaliyowapelekea kuutafuta uongozi.

6

Itakua ni ndoto ya ajabu sana kutarajia makubwa na miujiza toka kwa viongozi
hawa ambao hawakuwahi kuandaliwa na sisi kutuongoza na kubeba
utambulisho wetu. Kwa kutarajia miujiza toka kwao, ni sawa na mzazi ambaye
wakati wa malezi ya watoto wake, alikua anakula bata apendavyo na hafuatilii
makuzi na malezi ya watoto wake halafu atakapostaafu ategemee kuwa na
watoto waliofanikiwa na kufikia kiwango cha kumsaidia yeye na kumuonesha
mapenzi katika uzee wake na kustaafu kwake.

Miaka kama mitano iliyopita nilibahatika kushiriki matukio makuu mawili ya
kitaifa kwa kuwa miongoni mwa watanzania walioalikwa kuwapokea/
kuwasikiliza wageni wa heshima waliotembelea nchi yetu. Wa kwanza ilikua ni
mapokezi ya Rais wa China wa kipindi kile Mheshimiwa Hu Jintao
yaliyofanyika pale Diamond Jubilee. Siku chache baadaye nilibahatika tena
kuwa miongoni mwa waliopata mwaliko wa kumsiliza Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon pale hoteli ya Serena kipindi hicho
ikijulikana kama Sheraton. Nakumbuka mapokezi ya Ban Ki Moon yalipelekea
waalikwa wamsubiri kwa zaidi ya lisaa limoja tofauti na muda aliokua kwenye
ratiba. Pamoja na adha ya kusubiri kwa muda mrefu ujio wake, nilipata bahati
ya kuwa na mazungumzo na mmoja wa viongozi wakongwe sana wa taifa letu
ambao kukaa nao meza moja na kuongea ilikua ni zaidi ya muujiza kwangu
kwani nilikua nawasoma kwenye vitabu na kumsikia kwenye vyombo vya
habari tu. Tulikua na mazungumzo marefu na kiongozi huyu na alinisimulia
sana mafanikio yake binafsi na taasisi nyingi za umma alizoziongoza ikiwa ni
pamoja na wizara kadhaa tangu enzi za Mwalimu. Katika maongezi yake yote,
nilisumbuliwa na mambo mawili makubwa. Alitumia muda mwingi kunieleza
mafaniko yake binafsi kuwa kiongozi na nafasi alizowahi kushika lakini katika
maelezo yake sikupata kusikia akinielezea ni jinsi gani alifanikisha jambo
muhimu katika nafasi hiyo. Jambo la pili, pamoja na kwamba amekua kwenye
uongozi kwa karibu miaka 50 nilipokua naongea naye, sikusikia akinitajia jina
la mtu yeyote aliyemfunda/aliyemwandaa/aliyemlea ili kua kiongozi bora
maana wengi aliofanya nao kazi bado ni watendaji maeneo mengi serikali.

Baada ya kusikiliza maelezo yake kwa kirefu, nilimkatiza na kumuuliza swali
lililojengwa kwenye jambo la pili hapo juu. Nilimuuliza, kati ya mawaziri,
makatibu wakuu na viongozi wengine walioko sasa, ni nani ambaye ulifanya
naye kazi na ulimwandaa vema na unapomtizama leo unajivunia kazi yako
nzuri ya kumlea? Kiongozi huyu alikwepa kujibu swali hili mara kadhaa na
baadaye alianza kujifanya hakunielewa. Nikaendelea kusisitiza aniambie
alimwandaa nani ili kuendeleza kazi nzuri aliyofanya. Alipoona ninambana
sana, aliniuliza mimi nafanya kazi gani, ni mtoto wa nani na baba yangu
anafanya kazi gani. Nilimjibu kuwa nafanya kazi chuo kikuu na niko ngazi ya
chini kabisa katika taaluma na baba yangu ni mkulima ambaye alikuwa
hajulikani hata nje ya kijiji chake, na kwa wakati huo nilikua nakumbuka
mwaka mmoja wa kifo chake. Baada ya majibu haya kiongozi huyo mzoefu
hakujibu swali langu na badala yake aliinuka na kuniacha na dakika chache
zilizofuata Ban Ki Moon aliwasili na tukaendelea na zoezi la kumsikiliza na
kumuuliza maswali.
7

Nilichojifunza toka kwa kiongozi huyu na melezo yake, ni kwamba nafasi zote
alizokua amezishika hadi aliyokuwa nayo kipindi hicho, zilikua ni mafanikio
yake binafsi na watoto wake (alinitajia wote na mafaniko yao) na somo la
kuandaa viongozi wa kurithi na kuendeleza maono ya nchi, lilikua ni jipya
kabisa kwake. Kuna uwezekano mkubwa kabisa kuwa hali hii ya viongozi
walioko kuwa madarakani kutokujua wajibu wao wa kuhamisha maono kwa
wnaowarithi iko kwa viongozi wengi walio kwenye taasisi na maeneno mengi
ya uongozi wa nchi. Na unaweza kuliona hili pale ambapo waziri fulani
mchapa kazi anapobadilishwa wizara, au mkurugenzi fulani wa taasisi ya
umma napoondoka, kila kitu kizuri kinabadilika na kinabadilishwa na walewale
aliokua anafanya nao kazi.

Mtaalamu maarufu duniani kwa maswala ya uongozi na mwandishi wa vitabu
kadhaa vya uongozi ajulikanaye kama John Maxwell, katika moja ya vitabu
vyake aliwahi kusema, "Kama unadhani unaongoza na hakuna anayefuata,
basi wewe huna tofauti na mtu anayefanya matembezi tu ya kawaida".


Katika sehemu ya tatu ya makala haya, nitaendelea na kuchambua eneo
lingine lililotulemea na kutuletea shida kabla sijaanza kujadili suluhisho.

Nitapenda kusikia maoni yako na unaweza kuniandikia kupitia
mmmwalimu@gmail.com

Mwalimu MM