You are on page 1of 2

HOTUBA YA MHE. DKT.

ASHA-ROSE MIGIRO (MB), WAZIRI WA KATIBA NA


SHERIA KATIKA HAFLA FUPI YA KUKABIDHI NAKALA ZA KATIBA
INAYOPENDEKEZWA KWA TAASISI MBALIMBALI KATIKA UKUMBI WA
KARIMJEE, TAREHE 16 MACHI, 2015

Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria;


Bi. Maimuna Tarishi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria;
Dkt. Florens Turuka, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu;
Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa;
Ndugu Viongozi wote wa Serikali, Vyama Vya Siasa na Taasisi mbalimbali;
Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo wa Wizara ya Katiba na Sheria;
Ndugu Wahariri na wanahabari;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
As-salamu alaykum
Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mwingi wa rehema kwa kutujalia kuwa wenye
siha njema siku hii ya leo. Pili, Niwashukuru wote kwa kukubali mwaliko wetu wa
kuhudhuria hafla hii fupi ya kukabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa. Nakala hizi
zitakabidhiwa kwa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu,
taasisi za kidini na asasi za kiraia. Kufika kwenu katika hafla hii ni ishara kuwa
mnatambua umuhimu wa Katiba kwa mustakabali mwema wa Taifa letu. Pia ni ishara
kwamba mmedhamiria kushiriki kikamilifu katika zoezi zima la upatikanaji wa Katiba
Mpya ya nchi yetu.
Mabibi na Mabwana,
Kabla ya kukabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa, nichukue fursa hii kueleza kwa
kifupi kuhusu hatua iliyofikiwa katika zoezi la kuchapa na kusambaza nakala za Katiba
Inayopendekezwa. Kama nilivyosema wiki kadhaa zilizopita, jumla ya nakala milioni 2
za Katiba Inayopendekezwa zimechapishwa na kusambazawa katika mikoa yote ya
Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa upande wa Zanzibar, nakala laki mbili (200,000) zilisambazwa kwa wananchi
kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. Kwa upande Tanzania Bara, jumla ya nakala
1,141,300 zimesambazwa ambapo kila kata imepelekewa nakala mia tatu (300) chini ya
uratibu wa uongozi wa mikoa na wilaya. Nakala 658,700 zilizobaki ndiyo zinasambazwa
kwa Wizara, Taasisi za Serikali, asasi za kiraia na makundi mbalimbali. Ni matumaini
yangu kuwa wananchi wengi wamepata nakala hizo ambazo zimesambazwa katika
maeneo yao. Napenda kuwashukuru viongozi wa mikoa na wilaya waliofanikisha
zoezi hili hadi sasa.
Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana
1

Pamoja na kusambaza nakala za Katiba Inayopendekezwa kwa wananchi kupitia mikoa,


wilaya na kata zao, Serikali pia ilichapisha Katiba Inayopendekezwa katika magazeti
mbalimbali nchini na kuweka katika tovuti za taasisi zake ikiwemo tovuti ya Wizara ya
Katiba na Sheria (www.sheria.go.tz); tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(www.agctz.go.tz) na tovuti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
(www.habari.go.tz). Aidha, baadhi ya vyombo vya habari ikiwemo TBC1 na TBC Taifa
vimekuwa vikirusha matangazo mbambali kuhusu Ibara za Katiba Inayopendekezwa.
Jitihada zote hizi zinalenga kuwawezesha wananchi kupata fursa za kuielewa Katiba
Inayopendekezwa. Kwa niaba ya Serikali, nichukue fursa hii kuvipongeza vyombo vya
habari kwa kutekeleza jukumu hili muhimu la taaluma ya habari la kuelimisha umma.
Mabibi na Mabwana,
Baada ya maelezo hayo, niruhusuni niseme machache kuhusu hafla yetu ya leo.
Mchakato wa kuandika Katiba Mpya unamhusu kila mwananchi. Ni kutokana na sababu
hii, Serikali imesambaza nakala za Katiba Inayopendekezwa moja kwa moja kwa
wananchi. Hata hivyo, Serikali inatambua umuhimu na mchango wa taasisi mbalimbali
katika kuongeza uelewa wa wananchi wa maudhui ya Katiba Inayopendekezwa.
Hivyo, tumekutana hapa ili Serikali iwakabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa
ambazo mtazigawa kwa wadau wenu. Wito wangu kwenu ni kuwasihi wadau wenu
waisome kwa makini Katiba Inayopendekezwa ili kuielewa vizuri na hatimaye kushiriki
katika Kura ya Maoni muda utakapowadia.
Kwa upande wa Zanzibar, nakala za Katiba Inayopendekezwa kwa ajili ya Wizara,
Taasisi za Umma na binafsi, asasi za kiraia na makundi ya kijamii zitasambazwa kwa
uratibu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Mabibi na Mabwana,
Pamoja na kukabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa ambazo zimechapishwa katika
maandishi ya kawaida, leo pia tutakabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa
zilizochapishwa katika maandishi ya nukta nundu na maandishi yaliyokuzwa kwa ajili ya
ndugu zetu wenye mahitaji maalum. Lengo la kuchapisha nakala hizi ni kuwawezesha
watu wenye mahitaji maalum kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata Katiba
Mpya. Wito wangu kwa viongozi wao ni kuwa wahakikishe nakala hizi zinawanufaisha
wenzao wengi kadri iwezekanavyo.
Mwisho, kupitia kwenu na hadhara hii, ninawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi
katika zoezi la kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura linaloendelea ili watumie haki
yao ya kidemokrasia ya kupiga Kura ya Maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa muda
utakapowadia.
Asanteni kwa kunisikiliza