You are on page 1of 26

UCHAMBUZI WA BAJETI YA SERIKALI 2016/17

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto (Mb)


Kiongozi wa Chama

12 Juni 2016

Dar es Salaam

01. Utangulizi
Serikali ya Awamu ya Tano imewasilisha Bungeni Bajeti yake ya kwanza tangu
iingie madarakani. Bajeti hii inapaswa kutafsiri maono, malengo, shabaha
na ahadi kadha wa kadha ambazo zimekuwa zikitolewa tangu wakati
wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Katika uchambuzi wetu huu mfupi
tutatazama kama Serikali, kupitia Bajeti yake ya kwanza, imeweza kuweka
fedha kwenye maneno yake.
Serikali imependekeza kutumia jumla ya shilingi 29.5 trilioni ambapo kati ya
hizo shilingi 17.7 ni za matumizi ya kawaida na shilingi 11.8 ni za matumizi ya
Maendeleo. Hata hivyo uwezo wa Serikali kukusanya mapato yake ya ndani
(Mapato ya kodi, mapato yasiyo ya kodi na mapato ya Halmashauri) na
misaada kutoka nje ni shilingi 22.1 trilioni tu. Hivyo nakisi ya Bajeti
ni shilingi 7.4 trilioni sawa na asilimia 4.5 ya Pato la Taifa. Nakisi hii ya Bajeti
itazibwa kwa mikopo ya ndani na nje ya Nchi ambapo Serikali itakopa jumla
ya shilingi 7.4 trilioni ili kuziba nakisi hiyo ya Bajeti.
Serikali imependekeza kufanya marekebisho kadhaa kwenye kodi mbalimbali
ili kuweza kufikia malengo ya makusanyo ya kodi. Tutachambua baadhi ya
mapendekezo hayo na kuonyesha kama yatakidhi haja na kuwezesha kufikia
malengo husika.

Chama cha ACT Wazalendo kinafanya mapitio ya Bajeti ya


Serikali kwa lengo la kuainisha maeneo ambayo tunaamini Serikali
inafanya vizuri na maeneo ambayo yanahitaji kuangaliwa upya
na tunatoa mapendekezo mbadala. Tumeanza utaratibu mwaka
huu na utakuwa endelevu kila mwaka.

UTU. UZALENDO. UADILIFU

01

02. Dhana na misingi ya Bajeti ya Serikali

Bajeti ya serikali ndiyo tafsiri ya matamko ya kisera yanayotolewa na viongozi


wa serikali katika nyakati mbalimbali. Ni kupitia bajeti ambapo serikali hujaribu kutekeleza kwa vitendo ahadi zake mbalimbali. Aidha, bajeti ni nyenzo
muhimu kwa chama kilichoshinda uchaguzi kutafsiri ilani yake kwa vitendo.
Bajeti hujengwa katika misingi mikuu mitatu.

Mosi: bajeti ya serikali huanisha vyanzo vya mapato ya serikali, ikiwemo kodi
inayokusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali.

Pili: Bajeti ya serikali huanishi maeneo ambayo serikali inakwenda kutumia


makusanyo ya fedha. Matumizi haya hugawanywa katika makundi mawili:
matumizi maendeleo na matumizi ya kawaida.

Tatu: Bajeti ya serikali hutoa dira ya maendeleo ya nchi kwa kipindi cha mwaka
mmoja wa fedha na miaka mingi ijayo. Katika uchambuzi huu tunaangalia
maeneo ambayo serikali inakwenda kukusanya na kutumia mapato yake na
kwa kiasi gani maeneo haya yanajibu changamoto za nchi kwa sasa na muda
mrefu ujao.
02

UTU. UZALENDO. UADILIFU

03. Taswira halisi ya Bajeti ya Mwaka 2016/2017


Katika mwaka wa fedha wa 2015/2016, Serikali ilipanga kukusanya na
kutumia Shilingi 22.5 trilioni. Kama tulivyoona kwenye utangulizi, Serikali
ya Awamu ya Tano imepanga kukusanya na kutumia shilingi 29.5 trilioni
katika mwaka wake wa kwanza (2016/2017).
Ndiyo kusema Bajeti ya Mwaka huu imeongezeka kwa asilimia 31
ukilinganisha na Bajeti ya Mwaka jana. Hata hivyo, tangu Bajeti ya
mwaka jana thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani
imeporomoka kwa takribani asilimia 10. Kwa kuwa manunuzi yetu mengi
hasa kwenye miradi ya Maendeleo (ununuzi wa ndege, ujenzi wa Reli,
mikataba ya wakandarasi wa barabara nk ) hufanywa kwa fedha za
kigeni hususan dola ya Marekani, thamani halisi ya Bajeti itakuwa
imeongezeka kwa asilimia 21.
Aidha, mfumuko wa bei umeongezeka kwa takribani asilimia 5 kutoka
mwaka 2015/16. Ndiyo kusema uwezo wa kimanunuzi wa Bajeti ya mwaka
huu ni pungufu kwa uwezo wa Bajeti ya mwaka jana kwa asilimia 5. Hivyo
basi, ongezeko halisi la Bajeti ya mwaka huu ni takribani asilmia 16. Hata
hivyo tunaipongeza serikali kwa ongezeko hili, pamoja na kwamba, kama
tutakavyoonyesha, na kama ambavyo wachumi mbalimbali wamekwishaoonyesha, utekelezaji wake unatia shaka.

UTU. UZALENDO. UADILIFU

03

04. Bajeti inajibu Changamoto za Nchi?


Changamoto kubwa ya nchi yetu hivi sasa ni ukosefu wa Ajira kwa maelfu
ya Vijana wanaomaliza masomo na kuingia kwenye soko la Ajira. Ili kujibu
changamoto hii hatuna budi kutazama sera za kibajeti kwenye maeneo
yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira nyingi na kuona kama maamuzi ya
kibajeti yanapeleka rasilimali kwenye maeneo hayo.
Sekta yenye kuajiri Watanzania wengi kwa sasa ni sekta kubwa ya Uchumi wa
Vijijini (Kilimo, Mifugo na Uvuvi) ambapo kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya
Uchumi ya mwaka 2015 iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango tarehe 8
Juni 2016, asilimia 65 ya Watanzania wanajihusisha na ajira vijijini. Ajira katika
sekta rasmi ni 2.1 milioni chini ya 10% ya Watanzania wote wenye uwezo wa
kufanya kazi 22.3 milioni.
Katika ajira rasmi sekta inayoongoza ni Viwanda kwa kuchangia asilimia 20
ya ajira zote rasmi ikifuatiwa na Elimu 17% na Ulinzi na Utawala asilimia 15.
Mchanganuo huu unaonyesha kuwa Watanzania wengi (zaidi ya theluthi
mbili) wanaishi nje ya mfumo rasmi na hivyo juhudi kubwa inapaswa
kuwekwa kwenye Uchumi wa Vijijini ili kuboresha maisha yao na kuongeza
ajira rasmi huko huko vijijini.
Bajeti ya mwaka 2016/17 inajibu changamoto hii? Ili kujibu swali hili kwa
uhakika inabidi kutazama kwa ufupi hali ya sekta ya Kilimo (inayojumuisha
na Mazao, Misitu Ufugaji, Uvuvi nk) na kuona kama rasilimali za kutosha
zimeelekezwa kuikwamua sekta hiyo. Kiwango cha ukuaji wa shughuli za kilimo
umeporomoka mpaka asilimia 2.3 mwaka 2015. Sababu kubwa imeelezwa ni
tija ndogo, teknolojia duni, ukosefu wa masoko na uhaba wa viwanda vya
kusindika mazao ya kilimo (agroprocessing industries).
Kwa sisi wachumi tunatambua kuwa ili kupunguza umasikini wa Tanzania
kwa zaidi ya nusu ilihitajika sekta ya Kilimo kukua kwa kati ya asilimia 8 na
10 kwa mwaka. Kwa ukuaji huu tulionao sasa, maana yake itachukua miaka
mingi sana watanzania kuondoka kwenye dimbwi la umasikini. Baadhi ya
mazao yanayotarajiwa kuzalisha malighafi za viwanda uzalishaji wake
umeporomoka kwa kiwango cha kutisha.
04

UTU. UZALENDO. UADILIFU

Kwa mfano Zao la Pamba, uzalishaji na mauzo ya nje ya zao hili yameshuka
kwa asilimia 45 kwa mujibu wa Taarifa ya hali ya Uchumi iliyosomwa na
Serikali bungeni tarehe 8 Juni 2016.
Hata hivyo, katika Bajeti yote ya Maendeleo ya Tshs 11.8 trilioni, ni shilingi
100 bilioni tu zimetengwa kwa ajili ya sekta ya Kilimo sawa na asilimia 1
ya Bajeti nzima ya Maendeleo. Ni dhahiri kwamba ili kujenga uchumi
shirikishi ni muhimu kufanya jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba
kilimo kinaanza kuchangia vya kutosha katika kasi ya ukuaji wa Uchumi.
Kwa Uchumi wa Tanzania, ujenzi wa Sekta ya Viwanda hauwezi kufanikiwa
bila kukua kwa sekta ya kilimo. Kilimo ndio sekta Kiongozi katika kutokomeza
umasikini kwani inachangia theluthi moja ya Pato la Taifa na kuajiri theluthi
mbili ya Watanzania wote. Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano
imeshindwa kufungamanisha Sekta ya Kilimo na ndoto ya maendeleo ya
Viwanda. Ushahidi wa kisayansi unaotokana na Taarifa za Serikali yenyewe
unaonyesha kuwa hakuna mahusiano kati ya mipango ya maendeleo ya
viwanda na mipango ya maendeleo ya wananchi.
Maeneo mengine ambayo yanaweza kuzalisha ajira za kutosha ni Sekta ya
Utalii ambayo kwa kiasi kikubwa inazalisha ajira kwenye sekta za usafirishaji,
malazi na huduma za vyakula. Sekta ya Utalii ililiingizia Taifa Mapato ya kigeni ya
Dola za Kimarekani 2.3 bilioni. Ikumbukwe kuwa kila Mtalii anayeingia nchini
anatarajiwa kula, kulala na kusafiri na yote hayo ni huduma zinazotolewa na
Watanzania wanaoajiriwa kwenye mahoteli na magari ya Watalii.
Hata hivyo Serikali katika hotuba yake ya kwanza kabisa ya Bajeti imeamua
kurudisha nyuma juhudi zote za kukuza Sekta ya Utalii kwa kuanzisha kodi
ya VAT kwenye huduma zote za Utalii. Kodi hii itaifanya Tanzania kuwa ghali
kuliko washindani wake kama Kenya ambayo imeifuta kodi hii na kuongeza
Bajeti ya kutangaza Utalii. Utalii ndio sekta inayoongoza kwa kuingiza
mapato mengi ya fedha za kigeni na kawaida inapaswa kuangaliwa
kama sekta ya nje (export sector). Sekta za nje hazina kodi ya Ongezeko la
Thamani yaani VAT lakini cha kushangaza ni kwamba Serikali imeweka kodi
hii kwa sekta ya Utalii.
UTU. UZALENDO. UADILIFU

05

Vile vile maamuzi ya Serikali kubana matumizi kwa kufanya mikutano yake
kwenye majengo ya Serikali yatapelekea mahoteli mengi nchini kufunga
shughuli zao na kuachisha kazi mamia ya Watanzania wanaofanya kazi
kwenye mahoteli hayo. Hatua hii itakosesha Serikali mapato yatonayo na
Kodi na PAYE ambayo hulipwa na Wafanyakazi.
Kwa Ujumla Bajeti ya mwaka 2016/17 haitaweza kutatua kero ya ajira
nchini na badala yake itapelekea Watanzania wengi zaidi kukosa ajira kwa
waajiri kupunguza wafanyakazi ili kubana matumizi. Tumeanza kusikia
waajiri mbalimbali wakipunguza wafanyakazi. Hali itakuwa mbaya zaidi
kwa wenye mahoteli na miji kama Arusha itaumia zaidi kwani inategemea
sana Biashara ya Utalii. Kuanguka kwa sekta ya Utalii ni kuanguka kwa
uchumi wa nchi kwa ujumla.

06

UTU. UZALENDO. UADILIFU

05. Viwanda Vitajengwa?


Kauli mbiu ya Bajeti ya mwaka 2016/17 ni kuongeza uzalishaji viwandani ili
kupanua fursa za ajira. Kama tulivyoainisha hapo juu, Viwanda vinachangia
asilimia 20 ya ajira zote rasmi nchini na kwamba thuluthi mbili ya Watanzania
wameajirwa na sekta isiyo rasmi. Hivyo juhudi za kuongeza uzalishaji viwandani
ni muhimu sana ili kuwaondoa Watanzania wengi kutoka sekta isiyo rasmi na
kuwaingiza kwenye sekta rasmi. Ili kupima nia hii ya Serikali inabidi kutazama
hatua mbalimbali za kisera kuwezesha sekta binafsi kufungua viwanda vingi
zaidi nchini na kuajiri watu wengi.
Moja ni jambo la kupongeza sana kwamba Bajeti ya mwaka 2016/17 imelenga
kuondoa changamoto ya miundombinu kwa kiwango kikubwa sana. Wenye
viwanda wengi wamekuwa wakilalamika kuhusu kutokuwepo kwa
umeme wa uhakika, gharama kubwa za usafirishaji wa malighafi na
bidhaa na mawasiliano ya intaneti yasiyo na kasi ya kutosha. Katika
Bajeti ya mwaka 2016/17 Serikali imeelekeza rasilimali nyingi sana kujibu
changamoto hizo. Kwa mfano, Bajeti za Miundombinu ya Usafirishaji na
Umeme zimechukua asilimia 53 ya Bajeti yote ya Maendeleo. Jumla ya
shilingi 6.2 trilioni ya Bajeti imetengwa kwa ajili ya miradi ya miundombinu na umeme. Huu ni mwelekeo mzuri katika kujibu changamoto hizo.
Hata hivyo inawezekana kabisa kuwa uwekezaji kwenye Viwanda ukakumbwa
na changamoto ya soko maana katika Bajeti ya Mwaka huu Serikali imebana
matumizi na hivyo watu hawatakuwa na fedha za kutumia kununua bidhaa
na huduma. Miundombinu inaweza kujengwa lakini ikawa haina watu
wa kuitumia wala bidhaa za kusafirisha kwa sababu hakuna vivutio vya
kuanzisha viwanda pia. Ikumbukwe kuwa Serikali haianzishi viwanda bali
inajenga mazingira mazuri ya wawekezaji kuanzisha viwanda. Bajeti ya
mwaka 2016/17 haijaweka hivyo vivutio vya kaunzisha viwanda na imeminya uwezo wa walaji kutumia kwa kudhibiti matumizi na pia kutoza
kodi nyingi zinazopunguza uwezo wa kutumia bidhaa na huduma.
Ni vema kukumbusha kuwa kasi ya ukuaji wa shughuli za uzalishaji viwandani ni
ndogo kwa kiwango cha asilimia 6.5 na mchango wake katika Pato la Taifa
ni mdogo sana, wa asilimia 5.2 tu.
UTU. UZALENDO. UADILIFU

07

Serikali ilipaswa kuja na Sera mahususi za kufikisha asilimia 10 au zaidi ukuaji


wa uzalishaji viwandani. Hii maana yake ni kwamba matamshi mengi kuhusu
viwanda hayaendani na hali halisi ya viwanda nchini. Serikali haina budi kukaa na wenye viwanda na kupata mwafaka wa namna bora ya kuweka sera
mahususi zitazopelekea uwekezaji mkubwa wa wenye mitaji katika viwanda
na kuongeza uzalishaji. Vinginevyo, ahadi za Serikali hazitaweza kutekelezwa
kwa wakati. Vile vile viwanda vitahitaji muda mpaka kuanza uzalishaji, hivyo
juhudi kubwa ilipaswa kuwekwa kwenye uzalishaji wa malighafi za viwanda
ili wakati viwanda vinaanza kazi vikutane na malighafi.
5.1
Mapendekezo
Katika sekta hizi tatu nyeti kwa uchumi wa Tanzania, Chama cha ACT Wazalendo
tunapendekeza hatua zifuatazo kuchukuliwa
Serikali itunge mfumo wa kodi unaoeleweka na usiotetereka (stable
fiscal regime) kwa sekta ya kilimo ili kumwezesha mkulima kubakia na
sehemu kubwa ya mapato yake na kuvutia wananchi wengi kujishughulisha na uzalishaji katika kilimo.
II.
Serikali iharakishe kuanza kufanya kazi kwa soko la bidhaa (commodities
exchange) ili kupuguza watu wa kati katika sekta ya Kilimo
III. Serikali ianzishe mfumo wa hifadhi ya jamii kwa wakulima kwa kuanzisha
pia Fao la Bei ili kuhakikisha kuwa mkulima anarudisha gharama zake za
uzalishaji pindi bei katika soko zinapoterereka.
IV. Serikali ifute kodi zote za mazao (produce cess) na kuondoa vizuizi vya
aina yeyote ile ili kuhakikisha mkulima anauza bidhaa zake anapotaka
mwenyewe.
V.
Serikali ifanye maamuzi ya kisera ili kuhakikisha kuwa Viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi (agroprocessing
industries) vinapewa vivutio vya kikodi.
VI. Serikali iweke utaratibu kurahisisha taratibu za kufungua viwanda na
kuweka mfumo wa kisheria wa kufidia baadhi ya gharama za uzalishaji
kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumiwa na wananchi wengi
zaidi
VII. Serikali iondoe msururu wa kodi katika sekta ya Utalii ikiwemo
kuondoa kabisa wazo la kuweka VAT kwenye huduma za Utalii katika
I.

08

UTU. UZALENDO. UADILIFU

Bajeti ya 2016/17
VIII. Serikali itunge mfumo rahisi wa kikodi katika sekta ya utalii kwani ni

sekta inayoweza kuajiri vijana wengi sana na kupunguza kwa kiwango


kikubwa tatizo la ajira nchini.

06. Bajeti ina maana gani kwa Wananchi?


Tunapotazama maana ya Bajeti kwa wananchi hatuna budi kuangalia mambo ya msingi kama bei za bidhaa za huduma. Iwapo shilingi 1000 aliyonayo
mwananchi leo itanunua bidhaa nyingi zaidi kuanzia Mwezi Julai mwaka
2016, tutasema hali ya maisha ya mwananchi imeboreka. Iwapo shilingi
1000 aliyonayo mwananchi leo itanunua bidhaa chache zaidi kuanzia mwaka
mpya wa fedha tutasema hali ya wananchi imeporomoka.
Serikali imepandisha kodi mbalimbali kwenye bidhaa zinazoagizwa
kutoka nje na ushuru wa bidhaa mbalimbali. Hii itapelekea bei ya bidhaa na huduma kupanda na kusababisha mfumuko wa bei tofauti na
malengo ya Serikali. Serikali inatarajia mfumuko wa bei kuwa katika
tarakimu moja. Hata hivyo uchumi wetu unategemea sana uchumi wa
dunia kwa sababu tunaagiza zaidi ya uwezo wetu wa kuuza nje. Bei ya
Mafuta katika soko la dunia imeanza kupanda taratibu na sasa imefikia
$50 kwa pipa moja kutoka chini ya $30. Uzalishaji wa kilimo umekuwa hauridhishi kwani chakula ni sehemu kubwa ya mfumuko wa bei
(huchangia takribani asilimia 52 ya kapu la bidhaa na huduma). Kuna
mwelekeo mkubwa kwamba mfumuko wa bei utaongezeka mpaka
kwenye taratimu mbili na hivyo kupelekea hali za wananchi kuwa mbaya.
Kodi za miamala ya kutuma fedha kwenye mabenki au simu za mkononi
inabidi zitazamwe upya ili kuhakikisha kuwa malengo ya Serikali ya
kuwaingiza wananchi wengi katika mfumo wa kibenki yanafanikiwa.
Serikali imeamua kubana matumizi kwenye baadhi ya maeneo, ni jambo jema sana. Hata hivyo uamuzi huo utaendana na biashara nyingi
kufungwa na watu wengi kupoteza ajira na kuingia mtaani. Hii inaweza
kuongeza ugumu maisha kwa wananchi wengi wa kawaida.
UTU. UZALENDO. UADILIFU

09

Serikali inabidi kuaianisha hatua inazochukua na madhara yake katika


kuhakikisha jamii inabaki salama. Ni vizuri Serikali ikatazama ni maeneo
gani ambayo matumizi yake yanachochea ukuaji wa sekta binafsi na
kuyaachia badala ya kubana na kukumbatia fedha zote. Madhara yake
ni kwamba uchumi hautapata multiplier effect na hivyo kuendelea
kudumaa badala ya kukua mpaka kufikia tarakimu mbili.
Kwa ujumla, Bajeti ya mwaka 2016/17 itapelekea maisha ya mwananchi
wa kawaida kuwa magumu zaidi kwa sababu gharama za maisha
zitapanda na kipato kupungua. Sera za Bajeti zimeshindwa kutazama
Bajeti kama Sera (policy instrument) na badala yake imekuwa nyenzo
tu ya kukusanya mapato na kuyatumia.

07. Mambo ya Kushangaza katika Bajeti 2016/17


Bajeti ya kwanza ya Serikali ya awamu ya Tano imeshindwa kutoka na jambo
kubwa la kisera ambalo lingeamsha ari ya wananchi ya kufanya kazi na kujenga
Taifa lao. Jambo kubwa la kushangaza ni kwamba Bajeti hii ni ya kawaida
mno na haina tofauti kubwa na Bajeti zilizopita. Tofauti na matamko makali
makali ya Serikali kabla ya Bajeti, kimsingi Bajeti hii inathibitisha kauli
kwamba watawala ni wale wale na inaonyesha kuwa Utawala wa Awamu
ya 5 utachoka mapema sana kabla hata kazi haijaanza. Hii inathibitishwa
na ukweli kwamba hakuna ubunifu katika kutafuta vyanzo vipya vya mapato.
Yafuatayo ni mambo ambayo yanashangaza katika Bajeti ya mwaka 2016/17
i.

Serikali imeamua kupandisha nakisi ya Bajeti mpaka 4.5% ya Pato la


Taifa na kuziba nakisi hiyo kwa kukopa kutoka ndani na nje. Mwaka
2016/17 Serikali itakopa shilingi 7.5 trilioni ambapo kati ya hizo mikopo
ya masharti ya kibiashara itakuwa shilingi 2.1 trilioni. Mikopo ya ndani
itapelekea Serikali kugombania vyanzo hivyo na wafanyabishara wa
ndani na kupelekea wafanyabiashara kupata tabu kubwa kupata fedha
za kuendesha biashara (crowd out effect). Mikopo ya nje nayo itaongeza
gharama za kuhudumia Deni la Taifa ambapo hivi sasa nusu ya mapato
yote ya Serikali itakwenda kulipa madeni (Wakati Mapato yote ya Ndani
ya Serikali ni shilingi 17.7 trilioni, mwaka Huu Serikali italipa madeni
10

UTU. UZALENDO. UADILIFU

shilingi 8 trilioni). Hata hivyo, Serikali haina uhakika wa kupata mikopo


hii kwa sababu inategemea na jamii ya kimataifa ya mabenki yao yanaonaje Serikali yetu. Mwaka 2015/16 Serikali ilipanga kukopa shilingi
2.1 trilioni na ikaambulia shilingi 1.1 trilioni tu. Kwa namna Serikali ya
awamu ya tano inavyohusiana na mataifa ya nje na hatua mbalimbali
za kuonekana kuvunja mikataba ya kibiashara na kampuni za uwekezaji za nje, inawezekana Serikali isipate hata theluthi ya mikopo hii kutoka nje. Jambo la kushangaza ni kwamba matamko ya Viongozi wa
Serikali yalionyesha kuwa Tanzania haitahitaji misaada kutoka nje lakini
Bajeti kwa kiwango kikubwa inategemea fedha kutoka nje (Misaada na
Mikopo shilingi 3.6 trilioni na mikopo ya kibishara kutoka nje shilingi
2.1 trilioni kufanya jumla ya shilingi 5.7 trilioni).
ii.

Serikali inategemea kukusanya shilingi 17.8 trilioni kutokana na kodi na


mapato yasiyo ya kikodi. Hata hivyo, Serikali inatarajia kutumia shilingi
8 trilioni kulipia deni la Taifa na shilingi 6.6 trilioni kulipia mishahara ya
wafanyakazi. Jumla ya Matumizi haya shilingi 14.6 trilioni sawa na
asilimia 82 ya mapato yote ya Serikali. Hii maana yake ni kwamba
katika kila shilingi 100 ambayo Serikali inakusanya, shilingi 82 zinalipia
deni na mishahara na hivyo Serikali kubakia na shilingi 18 tu kwa ajili
ya matumizi mengineyo na matumizi ya maendeleo. Uamuzi wa Serikali kutenga shilingi 11.82 trilioni kwa ajili ya Maendeleo unategemea
misaada ya wafadhili na mikopo ya ndani na nje jambo ambalo Serikali haijawaambia wananchi kwani inajua ni jambo gumu kutekelezeka.
Kutenga asilimia 40 ya Bajeti kwenye maendeleo ni jambo jema lakini ni
siasa zaidi kuliko uhalisia kwani hakuna fedha za uhakika kwenye Bajeti
kuweza kulipia miradi hiyo ya maendeleo.

iii.

Serikali imeamua kutoza kodi ya asilimia5 kwenye Kiinua Mgongo cha


Wabunge wanapomaliza miaka yao mitano. Kwanza, ni jambo jema
sana kuwa Serikali inataka kuwaweka wabunge sawa na wafanyakazi
wengine wowote ambao kiinua mgongo hutozwa kodi. Hata hivyo
jambo la kushangaza ni kwamba kodi hii haina nyongeza yeyote ya
mapato katika mwaka wa fedha 2016/17. Chama cha ACT Wazalendo
tulitarajia Serikali ama kufuta posho za vikao katika mfumo mzima wa
UTU. UZALENDO. UADILIFU

11

utumishi wa umma au kutoza kodi posho hizi angalau kwa kiwango cha
kodi zuio ya asilimia 10. Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba Mapato
ya Viongozi wakuu wa Serikali kama Rais, Makamu wa Rais nk hayapo
wazi na hayatozwi kodi yeyote ile. Serikali ingeanza kwa kutoza kodi
mishahara ya viongozi wakuu wa Serikali akiwemo Rais ili kuonyesha
mfano wa uzalendo kwa wananchi.
iv.

Serikali imeamua kushusha kiwango cha chini cha kodi ya mapato


(PAYE) kutoka asilimia 11 mpaka asilimia 9. Nafuu anayopata mfanyakazi ni tshs 3800 tu. Jambo la kushangaza ni kwamba Serikali imebakiza
kiwango cha kutozwa kodi kuwa kile kile cha zaidi ya shilingi 170,000.
Tulitaraji kuwa kipato cha chini ya shilingi 360,000 kisingetozwa kodi
na kiwango cha juu kingeongezwa mpaka kufikia zaidi ya shilingi 15
milioni. Rais mara kwa mara amekuwa akizungumza kuhusu dhamira
ya kupunguza malipo makubwa wanayopata watu (wanaoishi kama
malaika kuwashusha waishi kama mashetani). Serikali inapaswa kurekebisha tofauti ya kipato kati ya wenye nacho na wasio nacho kwa
kupitia sera za kodi. Tulitarajia Serikali ingetumia Bajeti yake ya kwanza
kurekebisha tofauti hizo. Chama cha ACT Wazalendo kinapendekeza
mfumo mbadala wa kodi ya Mapato katika majumuisho ya mada hii
(Angalia kiambatanisho namba 1).

v.

Serikali haikugusia mabadiliko ya mfumo wa kodi kwa kampuni za


kimataifa zinazowekeza nchini (Multinational Corporations). Jambo la
kushangaza ni kwamba Serikali imeshiriki katika mkutano wa kimataifa
wa rushwa uliofanyika nchini Uingereza ambapo ajenda yake kubwa
ilikuwa kuzuia makampuni makubwa kukwepa kodi katika nchi wanazozalisha faida. Serikali ya awamu ya tano imeshindwa kabisa kuja
na sera za kibajeti kuzuia ukwepaji huu mkubwa wa kodi ambao kwa
hapa Tanzania ni zaidi ya asilimia 5 ya Pato la Taifa (yaani zaidi ya nakisi
ya Bajeti ya mwaka huu).

12

UTU. UZALENDO. UADILIFU

ACT Wazalendo ingefanya nini katika mwaka wake wa Kwanza?


Chama cha ACT Wazalendo kinapendekeza mabadiliko makubwa ya mfumo
wa kodi kufanyika ikiwemo kuwa na mtazamo kuwa Kodi sio tu ni sera ya
mapato bali ni sera ya kuchochea ukuaji uchumi wa sekta teule. Bajeti ya
kwanza ya Serikali ya awamu ya Tano haipelekei kujenga Tanzania ambayo
hakuna unyonyaji wala kujenga Uchumi Imara, shirikishi na unaosimamiwa na
Dola. Serikali ya awamu ya tano inaendeleza vikundi vya kinyonyaji (cartels)
ama kwa kuziimarisha cartels zilizopo au kujenga vicartel vipya kwa faida za
watawala. Kwa mfano, Serikali imeshindwa kuvunja vikundi maslahi kwenye
sekta ya Sukari na bidhaa zingine zinazoagizwa kutoka nje ikiwemo mafuta
ya kula na mchele licha ya kelele ambazo zimepelekea bei ya sukari kupanda
maradufu na kuwapa wananchi ugumu wa maisha. Wakulima wa mpunga
nchini hivi sasa wanapata ushindani mkubwa kutoka mchele unaotoka nje ya
nchi kama Vietnam na Pakistani na hivyo kupelekea bei ya wakulima kuporomoka na kushindwa kulipa mikopo waliyochukua kuendesha kilimo.
Tunapendekeza Wabunge wazingatie masuala machache yafuatayo kwenye
mjadala wa Bajeti na hatimaye kuweza kuifanya Serikali kuepuka madeni
makubwa inayokwenda kuchukua na kuanza kujitegemea.
I.

Katika sheria ya Fedha ya mwaka 2016, kuwe na kifungu cha Sheria


kinachoweka ukomo wa misamaha ya kodi mpaka asilimia 1 ya Pato
la Taifa. Misamaha ikaguliwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali, na misamaha yenyewe na taarifa ya ukaguzi viwekwe wazi
kwa umma. Mfumo ambao Serikali imependekeza sasa unaweza kuwa
na madhara makubwa sana kwa kuongeza urasimu na hasa ukizingatia kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania haina utamaduni wa kurudisha
fedha (tax refunds). Uamuzi wa kutunga sheria tunayopendekeza unaweza kuwezesha Serikali kukusanya shilingi trilioni 1.8 ya kodi.

II.

Serikali irekebishe sheria ya Kodi ya Mapato na kuweka vifungu vinavyohakikisha kuwa kila Mtanzania anajaza Tax Returns kila mwaka. Hii
itawezesha kila Mtanzania kuwa na wajibu wa kujaza fomu inayoonyesha kipato chake na TRA kutambua walipa kodi. Rais aongoze hili kwa
kujaza Tax Returns kila mwaka na kuweka wazi. Fomu zaweza kutolewa
UTU. UZALENDO. UADILIFU

13

kupitia mfumo wa Serikali za Mitaa kwa Watendaji wa Mitaa na Vijiji.


III.

Serikali ifanye marekebisho ya sheria mbalimbali za kodi zinazohusisha


makampuni ya kimataifa (MNCs) ili kuzuia kumomonyoa wigo wa kodi
(Base Erosion and Profit Shifting) kunakofanywa na kampuni hizi. Hili
linawezekana kwa Serikali kuchukua hatua ya kupitia mikataba ya kikodi (double taxation treaties) ambayo Tanzania iliingia na nchi nyingine
duniani. Tafiti mbalimbali katika eneo hili zinaonyesha kuwa Tanzania
hupoteza asilimia 5 ya Pato la Taifa kutokana na vitendo vya kampuni
kubwa kukwepa kodi kwa kutumia mbinu za kihasibu (tax planning
measures). Iwapo Serikali ikichukua hatua kwenye eneo hili haitahitaji
kukopa kabisa shilingi 7.5 trilioni inazopanga kukopa mwaka 2016/17,
ama itakopa kidogo sana kwa sababu hatua hizi zitaingiza fedha nyingi
kwa mara moja.

IV.

Kodi za Majengo ziendelee kukusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuziwezesha kuwa na mfumo wa kielektroniki wa kukusanya
kodi hizi kupitia kwa Watendaji wa Mitaa. Mamlaka ya Mapato Tanzania
haina uwezo wala nyenzo za kukusanya kodi hii kwa ufanisi.

V.

Michango ya Hifadhi ya Jamii ishushwe mpaka asilimia 14 kwa Waajiri


kuchangia asilimia 7 na Waajiriwa kuchangia asilimia 7 ya mishahara
yao. Hii itasaidia kupunguza gharama za kuajiri kwa Waajiri. Tozo ya
SDL ishushwe mpaka asilimia 3 pia. Eneo hili ni muhimu liangaliwe kwa
muktadha wa kukuza ajira nchini hivyo ajira zinapoongezeka mapato
kwenye maeneo haya yanaongezeka pia.

VI.

Fedha za uwezeshaji wananchi ( 50m kila kijiji) zitumike kujenga mfumo


wa hifadhi ya jamii wa taifa kwa kuchangia nusu ya michango ya wananchi watakaokuwa tayari kuingia kwenye hifadhi ya jamii kupitia vikundi vya uzalishaji mali. Hii itawezesha wananchi wengi kuwa na bima
ya afya na usimamizi wa mikopo kwneye vikundi kuwa mkubwa maana
utatokana na mfumo wa hifadhi ya jamii badala ya mpango ulivyo hivi
sasa. Kuna hatari kubwa ya fedha hizi kutumika vibaya kwa kuzigawa
kwa watu watakaozichezea tu kama ilivyokuwa kwa mabilioni ya JK.

14

UTU. UZALENDO. UADILIFU

VII.

Msamaha wa kodi kwenye maduka ya Majeshi na Taasisi za Dini iendelee kama ilivyo sasa kwani misamaha hii ni chini ya asilimia 1 ya misamaha yote inayotolewa nchini. Taasisi za Dini zinatoa huduma nyingi
kwa jamii hasa maeneo ambayo Serikali imeshindwa kutoa huduma
kama vile Elimu, Afya nk. Kuwapa posho wanajeshi ili wanunue bidhaa
kunaweza kuwaweka wanajeshi katika hatari ya kununua bidhaa zisizo
na ubora na hata kuwaweka kwenye hatari ya kudhuriwa. Vikosi vyetu
vya ulinzi na usalama havipewi misamaha kwa ajili ya mapato tu bali ni
kwa ajili ya kuimarisha usalama na ustawi wao kijamii.

VIII. Pendekezo la kodi ya VAT kwa huduma za utalii liondolewe ili Tanzania
iendelee kuwa shindani kwenye sekta ya utalii.
IX.

Pendekezo la kodi kwenye karatasi kutoka nje litazamwe upya kwani


litaongeza gharama za uzalishaji wa vitabu nchini. Tanzania haina viwanda vya karatasi vya kulinda ukiachana na Mgololo ambacho karatasi zake hazitumiki hapa nchini kwa kiasi kikubwa.

X.

Pendekezo la tozo kwenye miamala ya simu za mkononi na ile ya kibenki iondolewe ili kuhakikisha Watanzania wanaendelea kutumia mifumo
ya kifedha ya nchi.

UTU. UZALENDO. UADILIFU

15

08. Hitimisho
Tanzania isiyo na unyonyaji na yenye uchumi shirikishi unaozalisha ajira nyingi haitajengwa kwa Bajeti ya mwaka mmoja. Hata hivyo ni muhimu juhudi
zianze kuonekana katika hatua za mwanzo kabisa.
Serikali ya awamu ya Tano ina maono ya kujenga Tanzania ya Viwanda. Hata
hivyo, Bajeti yake ya kwanza kabisa imeshindwa kuonyesha sera mahususi
ambazo zinaweza kupelekea watu wenye mitaji kuleta mitaji yao Tanzania
na kujenga viwanda. Bajeti ya kwanza ya Serikali ya awamu ya Tano imekosa
ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato na sera zitakazopelekea nchi yetu kusonga mbele kiuchumi. Maamuzi ya kibajeti yaliyotangazwa na Serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mipango hayana mvuto unaoonyesha nia ya
kujenga uchumi wa viwanda.
Chama cha ACT Wazalendo kimejaribu kuonyesha mapungufu kadhaa yaliyomo kwenye mfumo wa Bajeti ya mwaka 2016/17 na kutoa mapendekezo ya
namna ya kuboresha. Ni dhahiri kuwa mwaka unaoanzia Julai 2016 utakuwa
ni mwaka mgumu sana kwa Watanzania wa kawaida kwani Bajeti haijawapa
unafuu wa maisha na badala yake imeongeza machungu. Ni kweli kwamba
ili kupata maendeleo ni lazima kuumia katika mchakato, lakini kuumia huko
ni lazima kueleweke na umma. Hivi sasa Umma umebakia bumbuwazi bila
kuelewa. Bajeti na Serikali imekosa uwezo wa kuwasiliana na umma vizuri.
Chama cha ACT Wazalendo kinahimiza wananchi kufuatilia kwa kina
utekelezaji wa Bajeti ya Serikali na kupaza sauti pale wanapoumia ili Serikali
ipate kusikia na kurekebisha mapungufu. Tunaamini kuwa tunao uwezo wa
kujenga Uchumi shirikishi na usio na unyonyaji wa kidola au sekta binafsi.
Tuna uwezo wa kujenga Tanzania lenye Ujamaa wa Kidemokrasia yaani Taifa
lisilo na unyonyaji na lenye uchumi unaowashirikisha wananchi wengi.
Mungu ibariki Afrika,
Mungu ibariki Tanzania.
Ahsanteni kwa kunisikiliza na kunisoma!
16

UTU. UZALENDO. UADILIFU

09. Viambatanisho
Kiambatanisho namba 1
Mapendekezo ya ACT Wazalendo ya Viwango vipya vya Kodi ya Mapato (PAYE)
Mapato ya Jumla kwa mwezi yasiyozidi Shilingi 360,000/=

Asilimia sifuri 0%

Mapato ya Jumla yanayozidi shilingi 360,000/= lakini hayazidi


shilingi 720,000

Shilingi 36,000 + 11% ya kiasi


kinachozidi shilingi 360,000/=

Mapato ya jumla yanayozidi shilingi 720,000/= lakini hayazidi


shilingi 1,440,000

Shilingi 72,000 + 20% ya kiasi


kinachozidi shilingi 720,000/=

Mapato ya Jumla yanayozidi shilingi 1,440,000/= lakini hayazidi


shilingi 2,880,000

Shilingi 144,000 + 25% ya kiasi


kinachozidi shilingi 1,440,000/=

Mapato ya jumla yanayozidi shilingi 2,880,000/= lakini hayazidi


shilingi 15,000,000

Shilingi 288,000 + 30% ya kiasi


kinachozidi shilingi 2,880,000/=

Mapato ya jumla yanayozidi shilingi 15,000,000/=

Shilingi 3,000,000 + 40% ya kiasi


kinachozidi shilingi 15,000,000/=

UTU. UZALENDO. UADILIFU

17

Kiambatanisho namba 2
Mchango wa Ndg. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini
akichangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara 2016/17
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji amewasilisha
maombi ya Fedha ili Bunge lako Tukufu limuidhinishie Jumla ya Tshs 82 Bilioni
(Tshs 42 Bilioni za Matumizi ya Kawaida na Tshs 40 Bilioni za Maendeleo). Waziri
anaomba tumpe idhini kutumia Fedha hizi ili aanze kutekeleza Mpango wa Pili
wa Miaka Mitano ambao lengo lake kubwa ni kuwezesha Tanzania ya Viwanda.
Bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ni sawa na 0.3% ya Bajeti
nzima ya Serikali ya mwaka 2016/17.
Mheshimiwa Spika, Waziri Kivuli wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ameibua
hoja nzito sana kwenye hotuba yake ambazo naamini Serikali hainabudi kuzipatia majibu yanayostahili. Hoja kubwa ni ile inayohusu kuwepo kwa matamko
3 tofauti, yenye tarakimu tofauti kutoka Serikali moja. Mfano uliotolewa ni kufufua Kiwanda cha General Tyre ambapo Vitabu vya Bajeti vinaonyesha kutengwa
tshs 150 milioni, randama za Wizara zinaonyesha tshs 500 milioni na mpango
wa Maendeleo unaonyesha tshs 2 bilioni zimetengwa. Kisheria za Bajeti, kilichomo kwenye vitabu vya Bajeti ndio kitakachoidhinishwa na Bunge. Kwamba Serikali inataka kufufua Kiwanda cha General Tyre kwa kutenga tshs 150 milioni, ni
kichekesho cha karne. Mambo haya yanadhihirisha kuwa Serikali hii haitembei
kwenye maneno yake. Wananchi wapatiwe majibu ya uhakika kuhusu masuala
haya. Ni muhimu sana Serikali kuhakikisha kuna uratibu miongoni mwa Wizara
za Serikali ili kuwa na sauti moja inayokwenda kwa wananchi.
Kufungamanisha Sekta ya Viwanda na Sekta ya Kilimo
Mheshimiwa Spika, adhma ya nchi yetu kuwa ya Viwanda ni adhma yetu sote.
Jambo hili ni jambo la Maendeleo na halina ushabiki wa kivyama. Tumepitisha
Mpango wa Maendeleo katika Bunge hili na kwa hiyo ni Mpango wa Nchi sio
mpango wa vyama tena. Hivyo sote kwa pamoja tunafanya kazi ya kuhakikisha
tunafikia malengo. Sisi tulio kwenye upinzani jicho letu pamoja na kushauri na
18

UTU. UZALENDO. UADILIFU

kupendekeza ni kukosoa pale ambapo walio kwenye Serikali wanakosea. Kukosoa ni tendo la kizalendo na walio Serikalini wawe tayari kukubali kukosolewa
ili kuboresha zaidi. Kwa maoni yangu, kama tusipofanya marekebisho ya kimkakati mapinduzi ya Viwanda itakuwa ni nyimbo na ngonjera za kisiasa. Watakaoumia ni Wananchi ambao hawatapata ajira na Serikali yenyewe itakosa kodi
kuweza kutoa huduma kwa wananchi. Kama nilivyosema hapo awali Serikali
inahitaji kufanya uratibu ili kufikia malengo. Sekta ya Viwanda au Maendeleo
ya Viwanda yanapaswa kufungamanishwa na sekta nyengine za uchumi kwa
sababu kuna kutegemeana. Kwa Tanzania unahitaji Sekta ya Kilimo inayokua
kwa kasi ili kuzalisha malighafi kwenye viwanda. Sekta nyingine kama Elimu,
Afya, Nishati, Mazingira nk zinahusiana na Viwanda pia. Kwa leo tutazame
Sekta Kilimo na Viwanda kwa muktadha wa Hotuba ya Waziri wa Viwanda na
kulinganisha na Hotuba ya Waziri wa Kilimo.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Viwanda na Sekta ya Kilimo kwa pamoja zinachangia nusu ya Pato la Taifa ( GDP) na nusu nyingine ni sekta ya Huduma. Nadharia
za Uchumi zinatuambia kuwa Tija ikiongezeka kwenye ya Kilimo inawezesha
sekta ya Viwanda kukua na kisha sekta ya Huduma. Hapa Tanzania na nchi
nyengine nyingi za Afrika, sekta ya huduma iliruka hatua hizi na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa sana kwenye Pato la Taifa. Ndio maana tuna Kitendawili
nchini kwetu kuwa Uchumi unakua lakini umasikini haupungui; ni kwa sababu
sekta ya huduma haijiri watu wengi kama sekta ya Kilimo na hivyo uchumi unaokuzwa na sekta ya huduma ni nadra kuondoa umasikini. Tanzania bado inapambana na umasikini. Juhudi zote tunazofanya lengo lake ni kuondoa umasikini kwa watu wetu. Sekta za kuondoa umasikini ni Kilimo na Viwanda hivyo
lazima mikakati ya Serikali iendane na kufungamanisha haya. Ndio Maana Nchi
nyengine Wizara ya Kilimo hujumuisha uongezaji thamani ( Ministry of Agriculture and Agro-processing ). Hatuhitaji kufanya hivyo, tunachohitaji ni kufungamanisha. Hata hivyo Serikali imeshindwa kufanya hivyo katika mwaka wake
wa kwanza tu wa Bajeti. Nitaeleza kwa kutumia changamoto tuliyonayo kuhusu
Sukari, Mafuta ya Kula na Nguo.
Mheshimiwa Spika, Malengo ya Serikali kwenye Viwanda yapo uk.140 ibara ya
191 ya Hotuba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Serikali imepanga
kutekeleza mambo 9 na katika mambo yote hayo hakuna hata moja linalohuUTU. UZALENDO. UADILIFU

19

siana na Viwanda vya kuzalisha bidhaa zinazohudumiwa na wananchi wengi


zaidi kama Sukari na Mafuta ya kula. Bidhaa hizi ni bidhaa zinazoleta maneno
ya kisiasa ndani ya nje ya Bunge. Nadhani baada ya madawa ya kulevya, bidhaa
zenye mizengwe mingi zaidi katika duru za kisiasa ni Sukari na Mafuta ya kula.
Sukari na Mafuta ya kula imeangusha Mawaziri kadhaa hapa nchini katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Hata hivyo Wizara ya Viwanda na Biashara haina
mkakati kabisa kushughulika na Bidhaa hizi licha ya uwezo wake wa kutenegenza ajira na kuokoa fedha za kigeni kuziagiza. Wizara imezungumza kuhusu
viwanda vya nguo lakini haijafafanua changamoto kubwa zinazoikabili sekta
ya nguo nchini na hasusan biashara haramu ya magendo ya Nguo inayoathiri
sana ukuaji wa sekta ya nguo nchini.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ukitazama hotuba ya Waziri wa Kilimo ambayo
Bunge lako tukufu limeshapitisha bajeti yake kuna mikakati ya kulima Miwa
kwa ajili ya Sukari. Ukurasa wa 44 ibara ya 107 ya Hotuba ya Wizara ya Kilimo na
ukurasa wa 25 ibara za 63 na 64 zinaeleza mikakati ya kukabiliana na uhaba
wa Sukari nchini. Kiambatanisho namba 6 cha Hotuba hiyo kimeeleza kwa kina
changamoto nzima ya Sukari na miradi inayopaswa kutekelezwa ili kumaliza
kabisa suala la uhaba wa Sukari nchini. Nimejumlisha miradi ile kutoka kona
mbalimbali za nchi na nimekuta ni takribani Hekta 300,000 za kulima Miwa.
Kwa Hesabu ya chini ya wastani wa kuzalisha Sukari kwa kila Hekta, miradi hii
ikitekelezwa Tanzania itaweza kuzalisha Tani 1.5 milioni za Sukari. Ukiondoa Sukari tunayotumia nchini, ziada itakayouzwa nje inaweza kuliingizia Taifa Fedha
za Kigeni USD 500 milioni, sawa na 30% ya malengo ya Mpango wa Maendeleo
kwa sekta ya Viwanda katika mapato ya Fedha za kigeni ya USD 3bn. Hapo sijaeleza kiwango cha Ajira kitakachopatikana, ukuaji wa biashara kwenye sekta
nyengine na Umeme utakaozalishwa ( Multiplier effect ).
Mheshimiwa Spika, swali la kujiuliza, chukulia Wizara ya Kilimo inalima hiyo
miwa hekta 300,000 halafu Wizara ya Viwanda haina mpango wa hivyo viwanda, hii miwa itakwenda wapi? Sio kwamba inapaswa kufungaminisha Kilimo
cha Miwa na Viwanda vya Sukari? Ni kwa nini Wizara 2 zilizo chini ya Serikali
moja zinashindwa kusomana? Baraza la Mawaziri linajadili nini? Ndio maana
Rais anajikuta akitoa matamshi ya Mawaziri barabarani. Suala la Rais kutoa
matamko kuhusu Sukari sio sawa, hii ni Kazi ya Mawaziri maana mnamuexpose
20

UTU. UZALENDO. UADILIFU

Rais. Rais sio mtu wa kuhangaika na masuala ya kunywa Chai na Uji.


Mheshimiwa Spika, nashauri Bunge lako tukufu leo lisipitishe Bajeti ya Wizara
ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ili Wizara hii ikakae na Wizara ya Kilimo
wawianishe mipango hii na kisha walete hapa Bungeni ndio tupitishe. Sukari ni
mfano mmoja tu katika suala hili. Hebu tumuunge mkono Rais kwa kuwarejesha mezani Wizara hizi mbili.
Mheshimiwa Spika, kwenye sukari kuna suala la low hanging fruits. Hivi tunavyozungumza kila Mwaka miwa yenye uwezo wa kuzalisha tani 50,000 ya Sukari huoza hapa nchini uko Kilombero na Mtibwa. Wakulima wanalima miwa
mingi kuliko uwezo wa Viwanda kununua. Bodi ya Sukari inapaswa kutoa leseni
ili vikundi vya wakulima au wawekezaji wadogo wazalishe Sukari. Bodi ya Sukari
haijatoa leseni na wala Serikali haijahamasisha Watanzania kuwekeza kwenye
viwanda vidogo vya Sukari ili kuwezesha miwa yote inayozalishwa kutoa Sukari.
Kama hili lingefanyika, leo tusingekuwa na ukali huu wa uhaba wa Sukari. Waziri wa Viwanda, hii ni low hanging fruits.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji wa bidhaa kama Sukari unahitaji vivutio maalumu kutoka Serikalini. Kule Uganda, Rais Museveni tangu aingie madarakani
aliweka vivutio maalumu kwa Viwanda kama Kakira Sugar ili wazalishe Sukari
ya kutosha. Viwanda vya Sukari Uganda hata umeme hulipiwa na Serikali kwa
Asilimia 50 ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuokoa kutokana na ushindani wa Sukari kutoka nje inayotupwa nchini ( dumping). Subsidies kwa ajili ya
kupunguza gharama za uzalishaji ili kuwezesha kuzalisha Sukari, kutengeneza
ajira na kupata faida nyengine ni jambo ambalo Lazima Serikali ianze kulifikiria.
Sisi Kigoma kuna mtu anataka kuzalisha Sukari tani milioni 1 kwa mwaka. Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda wanabishana kuhusu vivutio. Rais anahangaika na kuwafanya Watanzania wanywe Chai na Uji kwa bei rahisi, Mawaziri
wake wanabishana kuhusu vivutio vya mitambo ya kupanda miwa nakuzalisha
Sukari na kuzalisha Umeme. Serikali, hebu mtawale. Hebu muongoze. Utawala
sio kutoa matamshi ya barabarani. Uongozi ni kufanya maamuzi yanayomaliza
shida za wananchi kwa muda mrefu zaidi na sio matamko ya kupata Kurasa za
Mbele za magazeti ya siku moja au mbili.

UTU. UZALENDO. UADILIFU

21

Mheshimiwa Spika, suala la Mafuta ya Kula halina tofauti na suala la Sukari.


Ukipanda gari ukapita njia ya Singida unaona wananchi wamepanga madumu
ya mafuta ya Alizeti wanauza. Nguvu kazi hii ya Wananchi inapotea kwa sababu
Serikali imetoa unafuu mkubwa wa kodi kwa wanaoagiza mafuta ya kula kutoka nje ya Nchi. Leo kodi kwenye mafuta ya kula kutoka nje ni 18% tu. Tukiendelea
hivi tutaendelea kuwaona wananchi wetu wanapigwa na jua kuuza mafuta ya
Alizeti. Tunaposema mapinduzi ya Viwanda tunataka kumsaidia nani kama sio
huyu Mwananchi anayeshinda juani? Kama tunataka kubadilisha hali ya Wananchi ni lazima tuwawekee mazingira mazuri. Ni Aibu kubwa nchi hii kuagiza
mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. Tunatumia USD 340 milioni kila mwaka kuagiza mafuta ya kula kutoka nje. Leo hii bei ya lita ya mafuta ya Alizeti ni kubwa
kuliko bei ya lita ya petroli kwenye soko la dunia. Lakini wazalishaji wetu, wananchi wetu masikini tunawatazama tu tukipita na mashangingi yetu barabarani. Hali hii lazima ibadilike. Serikali ndio yenye wajibu wa kubadili hali hii kwa
kuweka kodi kubwa zaidi dhidi ya Mafuta ya kula kutoka nje na kuwekeza kwenye viwanda vya kukamua Mafuta kwa kutumia Alizeti na Mawese.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kigoma kuna Mradi tunaotaka kuanza wa kupanda Michikichi ili kuzalisha Mafuta ya Mawese. Tuna mpango wa kila familia 1 kupanda hekta 1 ya michikichi kwa lengo la kufikia familia 100,000. Uzalishaji huu
wa Mawese unaweza kuondoa kabisa suala la Tanzania kuagiza mawese kutoka
nje maana tutaweza kuzalisha Tani 200,000 za Crude Palm Oil (CPO) kwa mwaka, kuzalisha ajira nyingi, kupandisha hali ya maisha ya wananchi wakulima na
kukuza biashara nyengine. Tunahitaji watu watakaowekeza kwenye Viwanda
vya kuzalisha mawese. Wizara ya Viwanda ishirikiane na Uongozi wa Mkoa wa
Kigoma kuhakikisha tunazalisha mafuta ya Kula ya kutosha ili kuondokana na
uagizaji huu. Mawese na Alizeti ndio suluhisho la kudumu la suala la Mafuta
ya kula. Bunge liitake Serikali ikae upya kuandaa Bajeti ya Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji ili kuifungamanisha na Bajeti ya Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Spika, Suala la Mwisho ni sekta ya Nguo. Nchi nyingi duniani ambazo zimefanikiwa kuondokana na umasikini zimetumia sekta ya nguo ( textile
industry). Mnyororo wa thamani wa Sekta ya Nguo ni mrefu kuanzia kwa Mkulima mpaka kwenye nguo tunazovaa. Hii inapaswa kuwa sekta ongozi kwenye
suala zima la uchumi wa viwanda. Hata hivyo tuna tatizo la Pamba.
22

UTU. UZALENDO. UADILIFU

Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa Pamba umeporomoka kwa asilimia 47. Tutapata wapi Pamba ya kulisha viwanda vya nguo? Wizara ya Kilimo na Wizaara
ya Viwanda lazima zikae pamoja ili kuhakikisha kuwa tunafufua zao la Pamba.
Vinginevyo nchi hii itaishia kuagiza pamba kutoka nje au tutajikuta tunaunganisha nguo za kutoka China tu.
Mheshimiwa Spika, Viwanda vya Nguo nchini vinapata shida kubwa sana kutokana na magendo ya nguo. Kuna ukwepaji mkubwa sana wa kodi kwenye
bidhaa za nguo zinazoingizwa hapa nchini na hivyo kuua viwanda vya ndani.
Viwanda vinapata shida kubwa ya matumizi ya Umeme maana umeme hauna
uhakika na ni bei kubwa. Matokeo yake viwanda vingi vinafungwa na watu
wetu kukosa ajira. Serikali lazima ifanye kazi ya ziada ya kuzuia magendo ya
nguo vinginevyo viwanda vilivyopo vitakufa na hakuna atakayekubali kujenga
kiwanda hapa nchini kwani atajua kuwa Serikali haifanyi ziada kuhakikisha
tunalinda viwanda.
Mheshimiwa Spika, hakuna nchi duniani isiyolinda viwanda vyake. Leo Taifa
kubwa kama Uingereza linahangaika na kiwanda cha Chuma na kutaka hata
kuingiza mtaji wake ili kulinda ajira za Wanananchi wake. Tujifunze kwa wenzetu. Kama tunataka kupata ajira kwa watu wetu ni lazima kulinda viwanda
vyetu. Viwanda vya nguo nchini vipo kwenye tishio kubwa sana kutokana na
magendo ya nguo. Serikali ichukue hatua stahiki. Nguo zitatutoa kuanzia kwa
mkulima mpaka kwa wenye viwanda.
Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja kwamba Tuahirishe mjadala wa Wizara
ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ili kuiruhusu Serikali kuwianisha mipango
ya Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda. Wakiwa tayari ndio Bunge lije kupitisha Bajeti ya Wizara hiyo.
Zitto Zubeir Ruyagwa Kabwe
Mbunge Kigoma Mjini (ACT Wazalendo)
Mei 9, 2016
UTU. UZALENDO. UADILIFU

23

You might also like