HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KATIKA KILELE CHA SHEREHE ZA SIKUKUU YA WAKULIMA

, NANE NANE KWENYE UWANJA WA NZUGUNI - DODOMA, TAREHE 08 AGOSTI, 2010 Mhe. Stephen Wassira, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika; Waheshimiwa Mawaziri; Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa; Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa TASO; Mwenyekiti wa TASO Taifa; Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika; Washiriki kwenye Maonesho; Waheshimiwa Viongozi wa Serikali, Vyama vya Siasa, Vyama vya Ushirika; Mashirika ya Dini na Asasi nyingine za Wananchi; Wakulima, Wafugaji, Wavuvi na Wanaushirika; Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana: Nakushukuru sana Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mheshimiwa Stephen Wassira kwa heshima kubwa uliyonipa ya kunialika katika kilele cha Maadhimisho ya 17 ya Sherehe za Wakulima, maarufu kwa jina la Nane Nane ya mwaka 2010. Nawashukuru na kuwapongeza kwa namna ya kipekee Mhe. Eng. James Msekela, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Mhe. Paseko Ole Kone, Mkuu wa Mkoa wa Singida pamoja na viongozi na wananchi wa Mikoa hii kwa maandalizi mazuri ya sherehe za mwaka huu. Hii ni mara ya tatu mfululizo sherehe hizi zinafanyika katika kanda ya kati na hapa hapa kwenye Uwanja wa Maonesho wa Nzuguni katika Manispaa ya Dodoma. Sherehe zimefana sana na najiandaa kufaidi zaidi nitakapotembelea mabanda ya maonesho. Ndugu zangu, Nawashukuru kwa mapokezi mazuri na burudani. Pia nakushukuru Mwenyekiti wa TASO kwa hotuba yako nzuri na wewe Mheshimiwa Waziri kwa maelezo yako ya utangulizi. Lakini shukrani kubwa zaidi nazitoa kwa wale wote walioshiriki maonesho haya kwa kujenga mabanda na kutuonesha shughuli mzifanyazo katika kuleta mapinduzi ya kilimo, ufugaji na uvuvi nchini. Nawapongeza sana wale wote walioshinda na kupata zawadi mbalimbali. Hongereni sana! Tuzo mtakazopewa ni uthibitisho wa kiasi gani mmefanikiwa katika kuendeleza kilimo nchini. Ni kitendo cha kutambua kazi nzuri mliyoifanya katika kutumia maarifa ya kisasa na teknolojia zinazosaidia kuongeza tija, uzalishaji na ubora wa mazao ya kilimo na mifugo. Wapo pia wanaopata tuzo kwa kutambua mchango wao katika kutoa huduma zinazosaidia kuongeza tija, uzalishaji na ubora wa mazao. Huduma hizo ni pamoja na zile za upatikanaji wa zana za kilimo na ufugaji pamoja na pembejeo muhimu kama vile mbolea, mbegu bora, madawa na teknolojia mbalimbali. Wapo wanaotambuliwa kwa huduma za masoko na kwa kuongeza thamani mazao ya wakulima na wafugaji. Ni matumaini yangu kwamba tuzo hizo zitakuwa kichocheo cha kuongeza juhudi na maarifa zaidi katika kazi zenu. Aidha, ninyi mlioshinda mtakuwa darasa la mafunzo kwa wengine. Ndugu Wakulima, Wafugaji na Wanaushirika, Baada ya kumaliza kutoa zawadi nitatembelea baadhi ya mabanda ya maonesho nami nione kwa kiasi gani tunapiga hatua katika safari yetu ya kuleta mapinduzi ya kijani nchini. Nimeambiwa kuwa katika maonesho haya unaoneshwa jinsi utaalamu na teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na kuanza kutumiwa katika shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi zinavyoweza kuongeza tija. Kwa kweli taarifa hizo zinanifurahisha na kunipa faraja kubwa kwamba ipo kazi nzuri inayoendelea kufanywa kuleta mageuzi katika kilimo chetu na ufugaji wetu nchini. Nachukua nafasi hii kuwapongeza wataalam wa kilimo, mifugo na uvuvi kwa kazi nzuri ya kubuni, kuandaa na kuifikisha teknolojia na maarifa kwa walengwa. Aidha

nawashukuru wenzetu wa sekta binafsi kwa mchango wao mkubwa unaowezesha zana na pembejeo za kilimo kupatikana. Pia nawapongeza kwa huduma ya masoko na kuongeza thamani mazao yetu.

Ni matarajio yangu kwamba mambo yanayooneshwa hapa yatapatikana kwa urahisi mtu anapoyahitaji. Pia yatapatikana kwa bei au gharama nafuu. Ni matumaini yangu pia kwamba, kwa wakulima wenzangu na wafugaji wenzangu tuliobahatika kutembelea maonesho haya au kupata habari zake kupitia vyombo vya habari kwamba tuliyojifunza hapa tutayazingatia na kuyatumia kubadili kilimo chetu na ufugaji wetu. Na njia pekee ya kuthibitisha hayo ni kuongeza tija, uzalishaji na ubora wa mazao yetu ya kilimo, mifugo na uvuvi. Ndugu Wananchi, Tukifanya hivyo tutakuwa tumetimiza wajibu wetu kwa mujibu wa kaulimbiu ya mwaka huu isemayo KILIMO KWANZA “Mapinduzi ya Kijani – Uhakika wa Chakula na Kipato”. Kauli mbiu hii ni mwendelezo wa ile ya mwaka 2009. Inafanyika hivyo kwa sababu nzuri ya kusisitiza umuhimu wa kilimo kwa mkulima, jamii na taifa. Kwa mkulima kilimo kinamhakikishia chakula na ni chanzo cha mapato yatakayomwezesha kupata mahitaji yake ya msingi ya maisha na hivyo kuinua hali yake ya maisha. Kwa jamii na taifa, licha ya kuhakikisha upatikanaji wa chakula, kilimo ni kichocheo kwa sekta nyingine za uchumi kukua na hivyo kukuza pato la taifa na watu wake. Ukweli ni kwamba mataifa mengi ambayo sasa ni tajiri yalianzia kwenye kuleta mageuzi ya kilimo. Kilimo ndiyo mwanzo wa kila kitu kwa mwanadamu, jamii na mataifa. Bila ya shaka mtaelewa kwa nini wadau wa Serikali na sekta binafsi tulikuja na Azimio la Kilimo Kwanza mwaka jana. Kwa sisi, Tanzania asilimia 80 ya watu wetu wanaishi vijijini na wanategemea kilimo kwa maisha yao. Lakini wanategemea kilimo cha kujikimu tu ndiyo maana wengi wao ni maskini na nchi yetu ni maskini. Ndugu Wananchi, Sherehe za mwaka huu ni za tano tangu Serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani. Pia ni za mwisho kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2010. Vile vile Sherehe hizi zinafanyika mwaka mmoja tangu nilipozindua Azimio la Kilimo Kwanza katika Uwanja huu huu mwaka jana. Hivyo basi, Maadhimisho ya mwaka huu yanatoa fursa ya pekee kwetu kuangalia tulikotoka, tulipo sasa na tunakoelekea katika juhudi zetu za kuendeleza kilimo nchini katika miaka 5 ya Serikali yetu. Aidha inatupa fursa ya kupima utekelezaji wa Azimio la Kilimo Kwanza. Ndugu Wakulima Wenzangu, Wafugaji Wenzangu, Wana-Ushirika na Wananchi Wenzangu, Leo, naona fahari kusema kuwa tumepata mafanikio ya kutia moyo katika azma yetu ya kuendeleza sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi. Matokeo yake yanaonekana mahali mbalimbali. Tumetekeleza kwa ufanisi malengo ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo yaani Agricultural Sector Development Programme – ASDP na Azimio la KILIMO KWANZA. Kwa nia ya kujenga uwezo zaidi na kuleta mageuzi katika kilimo chetu nchini tarehe 8 Julai, 2010 Serikali yetu imeridhia Programu Kabambe ya Kuendeleza Kilimo Barani Afrika yaani Comprehensive Africa Agriculture Development Programme – CAADP itekelezwe nchini. Utekelezaji wa Programu hii unalenga kutoa msukumo mkubwa zaidi kwa utekelezaji wa dira yetu ya kuendeleza kilimo kama ilivyofafanuliwa katika ASDP na Azimio la Kilimo Kwanza. CAADP inasisitiza mageuzi ya kilimo kama yalivyo malengo ya ASDP, pia inasisitiza ushiriki wa sekta binafsi kama ilivyo katika Azimio la Kilimo Kwanza. Kuna mambo matatu mapya yanatiliwa mkazo na CAADP ambayo hatukuyapa mkazo kama huo katika ASDP na Kilimo Kwanza. Mambo hayo ni matumizi ya matrekta, upatikanaji wa mikopo kwa wakulima na lishe.

Jambo lingine la manufaa kwa Tanzania kujiunga na CAADP ni uwezekano wa kupata misaada ya kuendeleza kilimo kutokana na mfuko maalum ulioanzishwa katika mkutano wa G20 wa Laquila, Italia mwaka 2008. Ndugu Wakulima, Wafugaji na Wanaushirika, Ukiacha hayo ya kuwa na dira inayoeleweka kwa mujibu wa ASDP, Kilimo Kwanza na sasa CAADP, tumechukua hatua za makusudi za kuongeza bajeti ya Sekta ya Kilimo kutoka shilingi 233.3 bilioni mwaka 2005/06 hadi kufikia shilingi 903.8 bilioni kwa mwaka 2010/2011. Kwa ongezeko hilo, bajeti ya kilimo kwa sasa imefikia asilimia 7.8 ya bajeti ya Serikali. Hii ni hatua nzuri kuelekea kwenye lengo la asilimia 10 lililoamuliwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC mwaka 1998 katika mkutano uliofanyika Dar es Salaam na Wakuu wa Nchi za Afrika kule Maputo, Msumbiji, mwaka 2003. Kutokana na ongezeko hili la bajeti malengo ya ASDP na Kilimo Kwanza yameweza kutekelezwa vizuri. Naamini kama uwezo ungekuwa mkubwa zaidi tungefanya makubwa zaidi hasa kutokana na ukweli kwamba kazi iliyo mbele yetu ni kubwa zaidi. Kilimo cha umwagiliaji kimepanuliwa kutoka hekta 264,388 mwaka 2005/2006 hadi 326,492 Desemba, 2009. Kwa kuongeza fedha za ruzuku ya pembejeo kama mbolea, mbegu bora na madawa ya kilimo na mifugo kutoka shilingi 7.5 bilioni mwaka 2005/06 hadi shilingi 143.8 bilioni mwaka 2010/11 upatikanaji na matumizi ya pembejeo hizo umeongezeka sana sasa. Faida yake imeanza kuonekana kwenye kuongezeka kwa tija na uzalishaji wa mazao ya mpunga, mahindi na pamba. Tanzania inaweza kujitosheleza kwa chakula kwa wastani wa asilimia 95. Lakini mwaka huu tumejitosheleza kwa asilimia 112 kwa maana kuwa tuna ziada ya asilimia 12.Uzalishaji wa pamba na mazao mengine ya biashara nayo kama vile kahawa na tumbaku umeongezeka sana. Mpango wa kugawa pembejeo za kilimo kwa kutumia vocha nao umesaidia sana kuwafanya walengwa kunufaika moja kwa moja. Hali kadhalika wafugaji nao wamenufaika. Ng’ombe 11,134,000 wamepatiwa chanjo ya homa ya mapafu na chanjo nyingine zinaendelea kutolewa. Majosho mapya 543 yamejengwa nchi nzima na Shs.13.5 bilioni zimetumika kwa ajili ya dawa za majosho ya mifugo. Tutaendelea kuongeza fedha za ruzuku ili wakulima wengi zaidi wapate pembejeo za kisasa zitakazoongeza uzalishaji na kuwahakikishia wakulima usalama wa chakula na kuwaongezea mapato. Hata hivyo, tunakusudia kuwajengea wakulima mfumo utakaowawezesha kupata kwa urahisi mikopo ya kununua pembejeo na zana za kilimo kama vile, mbolea, mbegu bora, madawa, matrekta n.k. Kwa ajili hiyo kwanza, tumetilia mkazo na kuhimiza wakulima kuanzisha SACCOS ambazo ndizo zitawarahisishia wakulima kupata mikopo kwa shughuli zao za kilimo, ufugaji na uvuvi. Lakini, SACCOS zinaweza kutoa mikopo midogo midogo tu, hivyo wakulima wanaotaka kupanua shughuli zao na kununua zana bora zaidi SACCOS hazitaweza kuwasaidia sana. Kwa sababu hiyo, tumeamua kuanzisha Benki ya Kilimo ambayo matayarisho yake yanaendelea. Katika bajeti hii tumetenga shilingi 50 bilioni katika Fungu Maalum kwa ajili hiyo. Tangu mwaka jana tulianzisha utaratibu maalum wa kutoa mikopo ya shughuli za kilimo. Tumeanzisha dirisha maalum la mikopo hiyo kwenye Benki ya TIB. Dirisha hili litakuwa ndiyo kitovu cha kuanzishia Benki ya Kilimo hapo wabia wetu watakapokuwa tayari. Ndugu wananchi, Kwa kutambua umuhimu wa kuongeza matumizi ya zana bora za kilimo hasa matrekta tulianzisha utaratibu wa kuzitaka Halmashauri za Wilaya kuagiza matreka na kuwauzia wakulima. Aidha, tumeongeza fedha katika mfuko wa pembejeo kutoka Shs. 4.9 bilioni hadi Shs. 30.1 bilioni. Kati ya fedha hizo Shs. 16.3 bilioni zilitumika kuagizia matrekta. Kwa jumla, hatua hizo tulizochukua kati ya mwaka 2006 na 2010 jumla ya matrekta 3,948 yameingizwa nchini. Huu ni sawa wa wastani wa matrekta zaidi ya 780 kwa mwaka ambayo ni mafanikio ya

aina yake ukilinganisha na wastani wa matrekta yasiyozidi 150 kwa mwaka yaliyokuwa yanaingizwa nchini miaka ya nyuma. Mipango ya kuagiza matrekta 3000 inaendelea vyema. Mbegu Bora Ndugu Wananchi, Kuhusu upatikanaji wa mbegu tumeanza kuchukua hatua thabiti za kujenga uwezo wetu wa ndani kuzalisha mbegu bora. Hivi sasa asilimia 75 ya mbegu bora tunazotumia tunaagiza kutoka nje. Katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha kiasi cha Shs. 30 bilioni maalum kwa ajili ya shughuli za utafiti na vituo vyetu vya utafiti wa kilimo hususan mbegu navyo pia vitanufaika. Tutaongeza fedha hizo kila mwaka mpaka tufikie lengo la asimilia 1 ya bajeti ya Serikali.

Tumefanya mambo mawili muhimu ya kujenga uwezo wetu wa ndani wa kuzalisha mbegu bora kwa kufanya mambo mawili. Kwanza, tumeanza kufufua mashamba ya mbegu ya Serikali ili yaweze kuzalisha mbegu bora kama ilivyokusudiwa. Pili, tumechukua hatua za makusudi za kuhusisha wadau wengine katika uzalishaji wa mbegu. Nilielekeza Jeshi la Kujenga Taifa na Idara ya Magereza kutumia ardhi yao kubwa ya kuzalisha mbegu. Nafurahi kwamba maelekezo yangu hayo yametekelezwa vizuri. Hivi sasa majeshi yetu hayo mawili yanazalisha mbegu kwa ajili ya wakulima nchini. Mpaka sasa mwelekeo ni mzuri. Tayari uzalishaji wa mbegu umeongezeka kwa asilimia 60 kutoka tani 10,477.17 mwaka 2005 hadi tani 16,144.79 mwaka huu. Lakini hii ni nyongeza ndogo sana ukilinganisha na mahitaji halisi hivyo lazima tuendelee kuwekeza katika uzalishaji. Lengo langu katika siku za usoni ni kuihusisha zaidi sekta binafsi katika uzalishaji wa mbegu bora. Wanaweza kuwa wenyewe au wanaweza kuwa wabia wa serikali. Tatu, ili kuhakikisha kuwa shabaha yetu ya kuongeza uzalishaji wa mbegu bora nchini inafanikiwa kama tulivyotaka tuliona hapana budi kuimarisha wakala wa Serikali wa mbegu (Agricultural Seed Agency – ASA). Tumeanza kuchukua hatua za kuimarisha chombo chetu hiki muhimu kwa rasilimali watu, fedha na vifaa ili chombo chetu hiki kiweze kufanyakazi ya kuongoza, kuratibu na kusimamia shughuli za uzalishaji wa mbegu bora nchini. Katika kipindi hiki pia tumechukua hatua za makusudi za kupanua upatikanaji wa huduma za ugani. Tumeongeza nafasi za ajira kwa mafisa kilimo na mifugo wa ngazi zote kuanzia wa Stashahada mpaka wa Shahada. Hatujaweza kujaza nafasi zote 15,000 tumeajiri watumishi 3,801 na kufikisha idadi 7,180 lakini bado tunalo pengo kubwa la Wataalamu wa Kilimo na Mifugo katika Halmashauri. Tumepanua na tunaendelea kuongeza nafasi za mafunzo katika vyuo vyetu ili kukidhi mahjitaji ya wataalam nchini. Aidha tutajenga vingine. Wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM nilielezea nia yangu ya kushirikiana na mkoa wa Mara kujenga Chuo Kikuu cha Kilimo kule Musoma katika miaka mitano ijayo. Uvuvi Ndugu Wananchi; Katika awamu hii Serikali imetoa umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya uvuvi. Niliunda Wizara mpya ya Mifugo na Uvuvi ili kuupa uvuvi umuhimu unaostahili. Kwa uamuzi ule shughuli za uvuvi zimepata uhai mpya na tumeweza kufanya mambo kadhaa mazuri. Kumekuwepo uhamasishaji mkubwa kuhusu uvuvi endelevu na hifadhi ya mazingira ya mazalia ya samaki ili wakati wote samaki wawepo na uvuvi uwepo. Tumeondoa kodi ya zana za uvuvi zikiwemo boti,

nyavu, na injini ili kuwawezesha wavuvi kupata zana za kisasa za uvuvi. Tumeanzisha Mamlaka ya Bahari Kuu (Deep Sea Authority) kwa ajili ya kuongoza, kusimamia na kuratibu shughuli za uvuvi katika bahari kuu ndani ya mipaka yetu ya majini. Hivi sasa usimamizi haupo na uendelezaji wake hauna mpango wala mpangilio unaoeleweka. Ni matarajio yangu kuwa Mamlaka hii tuliyounda na mpango mkakati wa kukabili mapungufu yaliyopo utaendeleza uvuvi baharini. Ndugu Wananchi, Kati ya mwaka 2006 na mwaka 2009 tulivuna samaki wenye thamani ya shilingi 783.3 bilioni, ambapo samaki wenye thamani ya shilingi 597.5 bilioni waliuzwa nje ya nchi na kulipatia Taifa letu fedha za kigeni. Kwa nchi yetu yenye maziwa makubwa matatu ukanda wa bahari wa urefu kwa Km.1,000 na mito mingi, maziwa mengi madogo na mabwawa kadhaa, uvuvi ungeweza kuwa sekta muhimu sana kiuchumi. Bahati mbaya kwa sasa haiko hivyo. Hatua tulizochukua zimetupa msingi mzuri na makusudio yetu katika miaka mitano ijayo tufanye mambo mazuri zaidi kuendeleza uvuvi. Miongoni mwa mambo tuliyokusudia kuyapa msukumo maalum ni ufugaji wa samaki. Wenzetu wanafanya hivyo na wamenufaika sana na sisi tufanye hivyo. Mwelekeo Wetu Ndugu Wananchi; Ninakiri kwamba mafanikio tuliyoyapata katika miaka mitano hii katika kilimo, ufugaji na uvuvi yametuweka mahali pazuri pa kuwa na matumaini makubwa, kwamba mapinduzi ya kijani Tanzania yanawezekana. Kinachotakiwa ni kuwa na sera sahihi na kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake ipasavyo. Katika miaka mitano ijayo, tukipata ridhaa ya Watanzania kuwatumikia tena, dhamira yetu inabaki kuwa ile ile kwamba wakulima na wafugaji ndiyo nguzo yetu, hatutawatupa mkono hata kidogo. Tutakuwa nao bega kwa bega kuongeza uzalishaji na kipato chao kwa kuleta mapinduzi ya kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ari zaidi, nguvu zaidi, na kasi zaidi. Tutaendelea kutekeleza mipango yetu ya kuendeleza kilimo, ufugaji na uvuvi iliyopo na kubuni mipya. Hususan tutahakikisha tunatekeleza kwa ukamilifu ASDP, Azimio la Kilimo Kwanza na Programu ya CAADP. Lengo letu ni kuona kuwa mapinduzi ya kijani kwa maana ya mageuzi makubwa yanatokea katika kilimo chetu na ufugaji wetu, tija inaongezeka, uzalishaji wa mazao unakuwa mkubwa, nchi inajitosheleza kwa chakula na kunakuwepo na mali ghafi ya kutosha kwa ajili ya viwanda vya kusindika mazao ya kilimo. Kwa kufanya hivyo tutaongeza mapato ya wakulima na wafugaji na hivyo kuwapunguzia umaskini na kuwafanya wawe na maisha bora. Pia tutaongeza mapato yetu ya fedha za kigeni na pato la taifa kwa jumla. Ndugu Wananchi, Tutaendelea kwa ari zaidi, kasi zaidi na nguvu zaidi kuchukua hatua za kuendeleza ukulima wa kisasa. Tutasisitiza matumizi zaidi ya pembejeo za kisasa na kuhakikisha upatikanaji wa mbolea, mbegu bora, madawa ya kuua wadudu, n.k. Aidha, tutahimiza matumizi ya zana za kilimo na kuhakikisha matrekta, plau na zana nyingine za kisasa za kilimo na ufugaji zinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu. Tutaongeza huduma za ugani ili kuhakikisha wakulima na wafugaji wanatumia utaalam na mbinu za kisasa. Tutaongeza fedha ili tuweze kupanua maeneo ya kilimo cha umwagiliaji nchini na kuendeleza malisho ya mifugo ili hatua kwa hatua tupunguze ufugaji wa kuhama hama. Kuendeleza malisho na maji ya mifugo ni miongoni mwa mambo tutakayoyapa uzito maalum katika Mpango Kabambe wa Kuendeleza Mifugo tunaendelea kuutayarisha. Ndugu Wakulima, Wafugaqji na Wana Ushirika, Tutaendeleza maradufu juhudi za kuimarisha masoko kwa mazao ya wakulima na wafugaji kwa lengo kuu la kutaka wanufaike kutokana na jasho lao. Upande mmoja kuna upatikanaji wa masoko ya uhakika na upande wa pili kuna kupata bei nzuri kwa mazao ya mkulima na mfugaji. Katika miaka mitano mafanikio yanaonekana. Masoko ya mazao yamekuwa mazuri na

bei pia imekuwa nzuri kwa karibu mazao yote ya kilimo na mifugo kiasi cha kuwa mzigo mkubwa kwa watu waishio mijini hasa wale wa kipato cha chini. Tutaendela kuchukua hatua zaidi za kuimarisha Vyama vya Ushirika wa mazao na kuangalia uwezekano wa kuanzisha vyama vya ushirika vya wafugaji. Hatua tulizochukua za kubeba madeni ya vyama vya ushirika imesaidia sana kuvipa uhai mpya vyama vya ushirika na hivyo kuwapatia wakulima masoko ya uhakika na yenye bei nzuri kwa mazao yao. Mfumo wa stakabadhi ghalani umekuwa na manufaa makubwa. Tutaimarisha zaidi kitengo cha ukaguzi wa vyama vya ushirika kwa kuongeza watu na vitendea kazi. Hata hivyo narudia kuwaomba wana ushirika kutokuwachagua watu wasiokuwa waaminifu kuongoza na kuendesha vyama vyao. Watu hao ndiyo waliokuwa chanzo cha matatizo yote ya vyama vya ushirika huko nyuma – tusirudie tena kufanya makosa hayo. Sekta Binafsi Ndugu Wananchi; Kama ilivyo dhamira ya Kilimo Kwanza na sasa ya CAADP tutaishirikisha sekta binafsi kwa nguvu zaidi. Bahati nzuri sera na sheria ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi vimekamilika. Sasa mambo yatakuwa mazuri zaidi. Tunataka wenzetu wa sekta binafsi washiriki kulima mashamba makubwa ya kilimo na mifugo. Tunataka washiriki katika shughuli za utafiti na uzalishaji wa mbegu bora za mazao na mifugo. Tunataka wanunue mazao ya wakulima tena wawe na masoko ya uhakika na watoe bei nzuri. Tunataka wenzetu wa sekta binafsi wahakikishe kuwa mahitaji ya pembejeo za kilimo na ufugaji zinapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu. Wafanye biashara ya kuagiza na kusambaza pembejeo hizo. Kwa kweli tunataka wazalishe pembejeo hizo hapa nchini kadri inavyowezekana. Na kubwa zaidi tunataka wenzetu wa sekta binafsi wajihusishe na kuongeza thamani kwa mazao ya wakulima kwa kuanzisha viwanda vya kusindika mazao ya kilimo na ufugaji. Aidha, waanzishe viwanda kutengeneza bidhaa zainazotokana na malighafi ya mazao ya kilimo na ufugaji, nguo, viatu n.k. Ndugu Wananchi, Hatua tulizochukuwa kuongeza mtaji wa TIB kuanzisha dirisha dirisha la mikopo ya kilimo katika TIB na juhudi tunazofanya kuanzisha Benki ya kilimo zina lengo la kuwezesha hayo. Aidha kama nilivyogusia sheria mpya ya ubia wa sekta ya Umma na Binafsi ni ushahidi wa kiserikali kuwa tayari kuisaidia na kuiwezesha sekta binafsi kushiriki katika kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi nchini. Ndugu Wananchi, Tunataka pia kuleta mapinduzi ya uvuvi nchini kwa kuhimiza matumizi ya zana na maarifa ya kisasa katika uvuvi. Lengo kubwa ni kuwaongezea wavuvi kipato na kuiwezesha sekta hiyo kuchagia zaidi kwenye pato la taifa kupitia uvuvi endelevu na ufugaji wa samaki kwenye mabwawa. Tutaimarisha miundombinu ya uvuvi ikiwa pamoja na kujenga maabara za kisasa za uvuvi, kujenga mialo, masoko ya kisasa na vituo vya kutotolea vifaranga vya samaki. Ili kuharakisha mapinduzi ya sekta hii, ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu sana. Hivyo basi, tutaboresha mazingira ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje katika ujenzi wa viwanda vya mazao ya samaki na uvuvi kwenye bahari kuu. Vile vile tutawahamasisha wavuvi wetu na wafugaji wa samaki kuanzisha vikundi vya uvuvi na ushirika ili waweze kuunganisha nguvu zao na kutumia fursa zilizopo vizuri zaidi katika kuleta mapinduzi ya uvuvi nchini. Naamini tukitekeleza kwa dhati mwelekeo wetu huu, tutafika kule tunakotarajia. Kinachotakiwa kwa sasa ni kuongeza ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi na kutumia vizuri rasilimali tulizonazo kwa lengo la kuharakisha mapinduzi ya kilimo, ufugaji na uvuvi. Ni matarajio yangu kuwa katika miaka mitano ijayo Watanzania wengi watakuwa wamepata uwezo wa kuendesha shughuli zao za kilimo, ufugaji na uvuvi kibiashara na kisayansi kwa kutumia mbinu za kisasa, zana za kisasa na mbegu bora. Uwezo wetu wa kutengeneza

pembejeo za kilimo pia utakuwa umeongezeka na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yetu ya kilimo, mifugo na uvuvi vitakuwa vinaendelea kujengwa kwa kasi ya kuridhisha. Hitimisho Ndugu Wananchi; Katika kuhitimisha ujumbe wangu wa leo, napenda kuwashukuru tena wakulima, wafugaji, wavuvi, wanaushirika na wananchi wote nchini kwa juhudi kubwa mnazozifanya katika kuimarisha uchumi wa nchi yetu na kuhakikisha nchi yetu inakuwa na chakula cha kutosha. Mchango wenu katika kukuza uchumi wa Taifa letu; mimi na Serikali yangu tunautambua, tunauthamini na kuuheshimu sana. Hivyo, tuongeze juhudi zetu katika kukifanya kilimo chetu, ufugaji wetu, na uvuvi wetu uwe na tija zaidi ili Taifa letu liondoke kutoka kwenye kundi la nchi maskini duniani kwenda kwenye kundi la kipato cha kati. Ndugu Wananchi; Baada ya kusema hayo nawatakia Maadhimisho mema ya Sherehe za Nane Nane zinazoendelea. Ahsanteni kwa Kunisikiliza