You are on page 1of 13

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO

KIKWETE, KWENYE UZINDUZI RASMI WA BUNGE LA KUMI LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,


DODOMA, 18 NOVEMBA, 2010

Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyo ada niruhusuni nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma kwa kutujaalia uzima na
kutuwezesha kushiriki na kushuhudia uzinduzi wa Bunge la Kumi tangu kuundwa kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Ni siku adhimu katika historia ya nchi yetu na Bunge letu ambapo sote hatuna budi kujipongeza.

Mheshimiwa Spika;
Niruhusu nikupongeze kwa kuchaguliwa kwako kwa kishindo kuwa Spika wa Bunge letu. Ni ushindi ulioustahili kufuatia
historia yako iliyotukuka ya miaka 35 ya kuwa Mbunge na miaka kadhaa ya utumishi wa umma nchini. Umefungua ukurasa
mpya katika maisha yako binafsi, Bunge letu na nchi yetu kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hii. Ni heshima
kwako na ni fahari kwa nchi yetu kwamba hatuna ajizi katika kuwapa fursa wanawake. Bila ya shaka umefungua milango
kwa wanawake kuweza kuaminiwa kushika nafasi ya juu zaidi ya uongozi wa nchi yetu, Inshaalah. Nakuahidi ushirikiano
wangu na ule wa wenzangu wote Serikalini katika kufanikisha majukumu yako na ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika;
Napenda kuchukua fursa hii pia kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Samuel Sitta kwa kazi nzuri aliyoifanya ya
kuliongoza Bunge la Tisa. Atakumbukwa kwa mambo mengi mazuri aliyoyafanya katika kipindi chake. Tunamtakia kila la
heri katika kuwahudumia wananchi wa Urambo Mashariki na Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika,
Nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge, kwa kuaminiwa na wananchi na kuchaguliwa kuwa wawakilishi wao katika
Bunge hili. Hiyo ni heshima kubwa mliyopewa. Nawatakieni kila la heri hasa wakati huu mnapojiandaa kuonyesha kuwa
kweli mmestahili heshima hiyo. Napenda kuwakumbusha kuwa msijisahau kuwatembelea wapiga kura wenu kwa maelezo
kuwa mna shughuli nyingi za Bunge na Kamati zake. Wananchi hukasirishwa sana wasipowaona wawakilishi wao
wakiwatembelea na kuzungumza nao. Aghalabu hasira zao wanazionyesha kwenye uchaguzi. Mkumbuke miaka mitano si
mingi.

Shukrani kwa Wananchi Kuchagua CCM


Mheshimiwa Spika,
Narudia tena kutoa shukrani zangu kwa wananchi kwa kunichagua mimi, Dkt Mohamed Gharib Bilal na Chama Cha
Mapinduzi kuongoza nchi yetu kwa miaka mitano ijayo. Ushindi wetu ni ushahidi tosha kwamba Watanzania wanatambua na
kuthamini kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Chama chetu katika miaka mitano iliyopita. Aidha, kwamba wamekubaliana
na hoja tulizozitoa kuhusu mikakati yetu ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi yetu na kusukuma gurudumu la
maendeleo.

Nawashukuru wana-CCM wenzangu wote, kuanzia viongozi wa kitaifa hadi kwenye mashina pamoja na wapenzi na
washabiki wa CCM kote nchini kwa kuutafuta ushindi na kuupata. Kazi iliyo mbele yetu sasa ni kutimiza ahadi zetu kwa
Watanzania. Napenda kuwahakikishia kuwa chini ya uongozi wangu kazi hiyo ipo katika mikono salama.

 Shukrani kwa Waziri Mkuu


Mheshimiwa Spika,
Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kukubali uteuzi wangu wa Mheshimiwa Mizengo Peter Kayanza Pinda kuwa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano. Wengi wenu mnamjua vizuri. Mmekuwa nae kwa kipindi kilichopita na ndiyo maana
hapakuwa na taabu kumthibitisha. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge mumpe ushirikiano kama mlivyofanya kipindi
kilichopita.
Majukumu ya Msingi
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge,
Nilipozindua Bunge la Tisa, Desemba 30, 2005, nilifafanua majukumu yetu ya msingi, yaani kwangu, Serikali yetu, Wabunge
na wananchi wote kwa jumla. Niliainisha mambo makuu matatu: Kwanza, kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa nchi
moja na watu wake wanaendelea kuwa wamoja, wanaopendana na kushirikiana licha ya tofauti zao za rangi, makabila, dini,
maeneo watokayo na ufuasi wa vyama vya siasa. Aidha, nilisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kuwa nchi yenye
usalama, amani na utulivu. Pili, kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa nchi
yetu na watu wake. Na, tatu, kuhakikisha kuwa demokrasia yetu inazidi kustawi na Serikali inaendeshwa kwa kuzingatia
misingi ya utawala bora, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na
maovu katika jamii.

Mheshimiwa Spika;
Leo miaka mitano baadaye, tunapozindua Bunge la 10 bado naamini kuwa mambo haya matatu yanastahili kuendelea kuwa
ndiyo majukumu yetu ya msingi. Yanafaa kuendelea kuwa mwongozo kwetu katika kupanga vipaumbele vyetu, kubuni sera
na kutengeneza mipango ya maendeleo. Safari ile nilisema tutatekeleza majukumu yetu kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu
mpya, safari hii nasema tutafanya hivyo kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi.

Vipaumbele 13
Mheshimiwa Spika,
Kwa ajili ya hiyo basi, Serikali nitakayoiunda siku chache zijazo itakuwa na vipaumbele 13 vifuatavyo:

1. Kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kuwa yenye umoja, amani na usalama, na Muungano wetu unaendelea kudumu
na kuimarika;

2. Kuendeleza juhudi za kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini kwa kuchukua hatua thabiti za kuharakisha
mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda. Aidha, tuboreshe mazingira ya uwekezaji na biashara nchini ili tuvutie
wawekezaji wengi wa ndani na nje kuwekeza katika sekta mbalimbali;

3. Kuongeza jitihada za kuwawezesha kiuchumi wananchi wa makundi yote ili waweze kushiriki na kunufaika na uchumi
wetu unaokua. Tuboreshe mipango iliyopo ya kusaidia wajasiriamali wadogo na wote wanaotaka kujiajiri. Aidha, tuweke
mipango thabiti ya kuwatambua na kuwawezesha wajasiriamali wa tabaka la kati ili wastawi na waweze kushiriki katika
uwekezaji mkubwa ndani na hata nje ya nchi yetu;

4. Kuendelea kujenga na kuimarisha sekta binafsi nchini na kutengeneza mazingira mazuri zaidi ya ushirikiano na sekta ya
umma. Aidha, tuimarishe uwezo wa Serikali kupanga mipango ya maendeleo na kusimamia utekelezaji wake bila kuingilia
isivyostahili shughuli za sekta binafsi;

5. Kutumia fursa ya kijiografia ya nchi yetu na kuifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi za
Afrika ya Mashariki na Kati. Kwa ajili hiyo hatuna budi kuboresha miundombinu ya barabara, reli, bandari, viwanja vya
ndege na teknohama. Aidha, tuongeze ufanisi katika utendaji na utoaji wa huduma wa miundombinu hiyo;

6. Kuongeza jitihada za kuhakikisha Taifa letu linanufaika zaidi na maliasili zake zilizopo juu na chini ya ardhi. Tutahakikisha
kuwa tunazo sera na sheria za uvunaji na matumizi ya rasilimali hizo zinazonufaisha taifa letu sawia;

7. Kuboresha zaidi ukusanyaji wa mapato ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa pamoja na kuimarisha nidhamu ya matumizi
ya fedha na mali za umma;

8. Kuendeleza juhudi za kupanua fursa za elimu kwa vijana wetu tangu elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu ya
juu. Aidha, tutoe msukumo na kipaumbele maalum kwa masomo ya sayansi katika ngazi zote. Pia, tuweke mkazo maalum wa
kuboresha elimu ya msingi na sekondari ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto nyingi;

9. Kuongeza jitihada za kupanua na kuboresha huduma muhimu za kiuchumi na kijamii hususan afya, maji, umeme, barabara,
reli, bandari, anga, simu, teknohama na huduma za fedha;

10. Kuimarisha utawala bora, demokrasia, utawala wa sheria, haki za binadamu na kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya
rushwa, dawa za kulevya, matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa mali ya umma. Kwa ajili hiyo tutaendelea
kuvijenga na kuviwezesha kirasilimali, kimuundo na kisheria vyombo vinavyoongoza mapambano hayo na vile vya kutoa na
kusimamia haki nchini;

11. Kuendelea kuimarisha uhusiano mzuri uliyopo baina ya nchi yetu na majirani zetu pamoja na mataifa mengine duniani na
mashirika ya kimataifa. Aidha, tutaendelea kutafuta marafiki wapya na kuboresha diplomasia ya uchumi kwa manufaa ya
nchi yetu;

12. Kuongeza maradufu juhudi za kuhifadhi mazingira hasa wakati huu ambapo makali ya athari za mabadiliko ya tabia nchi
yanazidi kutuumiza sote; na

13. Kulinda mafanikio tuliyoyapata katika kipindi cha miaka mitano iliyopita pamoja na yale ya tangu uhuru mpaka sasa.
Aidha, tukamilishe yale tuliyoyaahidi mwaka 2005 ambayo hatukuweza kuyakamilisha.

Tudumishe Umoja wa Nchi yetu


Mheshimiwa Spika,
Nguvu ya mnyonge na maskini ni umoja. Hivyo basi, na sisi hatuna budi kudumisha umoja wa nchi yetu kwa gharama yoyote
ile. Umoja wa nchi yetu una sura tatu kuu. Kwanza ni mipaka inayotambulisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa
salama. Nafurahi kusema kuwa mipaka ya nchi yetu iko salama na wala hakuna tishio lolote la kutoka ndani au nje ya nchi
yetu dhidi ya mipaka yetu.

Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange, Maafisa na askari
wote wa JWTZ kwa kazi nzuri waifanyayo ya kulinda mipaka ya nchi yetu. Nawaomba waendelee na moyo wao huo wa
uzalendo. Napenda kuwahakikishia kuwa kazi tuliyoianza ya kuliimarisha Jeshi letu kwa kulipatia zana na vifaa vya kisasa
vya utendaji kivita tutaiendeleza bila ajizi. Aidha, tutaendelea kuboresha maslahi ya wanajeshi wetu pamoja na mazingira yao
ya kuishi na kufanyia kazi.

Muungano

Mheshimiwa Spika;
Sura ya pili ya umoja wa nchi yetu ni Muungano wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika uliozaa nchi
moja mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964. Tunalo jukumu la kihistoria la kuhakikisha kuwa
Muungano wetu unadumu na unazidi kuimarika. Nafurahi kusema kuwa Muungano wetu ni imara licha ya changamoto za
hapa na pale. Na, kinachonipa faraja zaidi ni ule ukweli kwamba pande zetu zote mbili za Muungano zinayo dhamira ya dhati
ya kutatua kero zilizopo kwa lengo la kuuimarisha.
Mheshimiwa Spika;
Nafurahi kwamba dhamira yangu ya kuimarisha kamati ya pamoja ya Serikali zetu mbili kuhusu masuala ya Muungano
imefanikiwa. Kamati hiyo imefanya kazi nzuri sana na mambo mengi yaliyokuwa yanaleta usumbufu na misuguano
yamezungumzwa kwa uwazi na kupatiwa majawabu. Yale machache yaliyosalia tutaendelea kuyapatia ufumbuzi ulio
muafaka kwetu sote.

Mheshimiwa Spika;
Niruhusu nimshukuru na kumpongeza kwa dhati aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed
Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, wakati akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa uongozi wake mzuri. Aidha, nawapongeza kwa namna ya kipekee Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa
na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda na Mheshimiwa Edward Lowassa kabla yake, kwa upande wa Serikali ya
Muungano na aliyekuwa Waziri Kiongozi, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar. Nawapongeza kwa umakini wao, moyo wao wa uzalendo na kwa juhudi zao zilizozaa matunda mema.
Umoja wa Watu
Mheshimiwa Spika;
Sura ya tatu ya umoja wa nchi yetu ni ile ya wananchi wetu kuwa wamoja, wanaopendana, kushirikiana na kushikamana.
Pamoja na changamoto za hapa na pale, Watanzania wameendelea kuwa watu wamoja, wanaopendana na kushirikiana licha
ya tofauti zao za rangi, makabila, dini, maeneo wanayotoka na ufuasi wa vyama vya siasa. Kubaguana na kuchukiana kwa
sababu za tofauti zao hizo ni mambo mageni kabisa kwao. Nafurahi kwamba hata pale waliposhawishiwa wengi wao
walikataa na waliunga mkono kwa wingi sana juhudi za kutafuta suluhu.

Mheshimiwa Spika;

Bila ya shaka sote tunaikumbuka hali tete ya kisiasa na kiusalama iliyokuwepo Zanzibar katika miaka ya hivi karibuni.
Katika hotuba yangu ya Desemba 30, 2005, nilielezea kusononeshwa na hali hiyo na kuahidi kushirikiana na viongozi wa
kisiasa wa pande zote kulitafutia ufumbuzi. Nafurahi kwamba ahadi hiyo imetimia. Zanzibar sasa ni shwari na watu wanaishi
kindugu. Serikali ya umoja wa kitaifa imeundwa na hasama zimeisha.
Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid
Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Mheshimiwa Seif Shariff Hamad ambaye sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar kwa uongozi wao thabiti uliowezesha kupatikana maridhiano ya kisiasa yaliyomaliza mzozo Visiwani humo.
Nawapongeza wananchi wa Unguja na Pemba kwa kuwaunga mkono viongozi wao. Zanzibar sasa ni nzuri kwa kila mtu
kuishi.

Mheshimiwa Spika;

Kwa mara nyingine nampongeza Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi. Nampongeza Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad kwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais. Tunawatakia heri katika kazi yao ya kujenga Zanzibar
mpya. Nawahakikishia utayari wangu wa kushirikiana nao kwa lolote watakaloona naweza kuwa wa manufaa. Ahadi yangu
hiyo ni ahadi ya Serikali ya Muungano pia.

Mheshimiwa Spika;

Kwa upande wa Tanzania Bara uchaguzi wa mwaka huu umeacha nyufa za mgawanyiko hatari wa kidini ambao hatuna budi
tuchukue hatua haraka kuziziba. Nawahakikishia utayari wangu wa kushirikiana na wanasiasa wenzangu, viongozi wa dini na
wa kijamii kulitafutia ufumbuzi suala hili. Si vyema na siyo busara kuliacha likaota mizizi na kulimong’onyoa taifa letu.
Naomba wenzangu mkubali tuinusuru nchi yetu.

Usalama wa Raia
Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano iliyopita, tumefanikiwa kuimarisha usalama wa raia. Kama mjuavyo, tulianza kazi wakati nchini kuna
wimbi kubwa la ujambazi ulioonekana kama vile umeshindikana. Nashukuru kwamba Jeshi letu la Polisi kwa kushirikiana na
wananchi na vyombo vingine vya usalama limefanikiwa kudhibiti ujambazi. Uhalifu huo bado upo, lakini upo kwa kiwango
cha kudhibitika. Katika miaka mitano ijayo tutaendeleza maradufu juhudi za kupambana na uhalifu huu na wa aina zote
nchini.

Mheshimiwa Spika;
Niruhusu pia nitoe pongezi za dhati kwa Jeshi la Polisi chini ya uongozi wa Inspekta Jenerali Saidi Mwema kwa kazi kubwa
na nzuri wanayoendelea kufanya. Wananchi wanajisikia kuwa salama. Tutaendelea kuliimarisha Jeshi letu hili kwa kuwapatia
zana na vifaa vya kisasa vya kazi pamoja na kuboresha maslahi na mazingira ya kufanyia kazi na makazi ya Maafisa na
Askari.

Kukuza Uchumi
Mheshimiwa Spika;
Miaka mitano iliyopita ilikuwa migumu sana kwa kazi ya kujenga uchumi wa nchi yetu na kupunguza umaskini. Uchumi
wetu ulipata misukosuko mikubwa ikiwemo ukame mkubwa wa mwaka 2005 – 2006 uliokausha mazao mashambani na
kusababisha njaa kubwa iliyoifanya Serikali kulisha watu zaidi ya 3,776,000. Ukame huo pia ulikausha maji katika mabwawa
yote ya kuzalisha umeme na kusababisha upungufu mkubwa sana wa umeme. Kwa ajili hiyo uzalishaji viwandani na utoaji
wa huduma muhimu kwa maisha ya Watanzania uliathirika sana.

Mwaka 2007 tukakumbwa na tatizo la kupanda sana kwa bei za mafuta na bei za vyakula duniani. Kana kwamba hiyo
haitoshi mwaka 2008 – 2009 kukaja tatizo la kuyumba kwa masoko ya fedha ya kimataifa na kudorora kwa uchumi wa dunia
kulikoathiri nyanja zote za uchumi wetu.

Matokeo ya misukusuko yote hiyo ni kudumaa kwa uwekezaji, kudorora kwa shughuli za uzalishaji, biashara na utalii,
kupanda sana kwa mfumuko wa bei, kupungua kwa mauzo nje, kushuka kwa mapato ya fedha za kigeni na mapato ya
Serikali pamoja na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi. Kwa sababu hiyo pia kasi ya kupunguza umaskini nayo ilikuwa
chini ya lengo tulilojiwekea katika MKUKUTA I.

Mheshimiwa Spika;
Tulilazimika kufanya kazi ya ziada kuzuia uchumi wetu usiporomoke na nafurahi kwamba juhudi zetu zilifanikiwa. Hivi sasa
uchumi wetu umekuwa tulivu tena. Kasi ya ukuaji ni nzuri (asilimia 7.1), mfumuko wa bei umeshuka sana kutoka wastani wa
asilimia 12.1 mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 4.2 hivi sasa. Watalii wameongezeka, shughuli za viwanda na biashara
zinarejea katika hali ya zamani. Tunategemea mambo kuwa mazuri zaidi katika miaka mitano ijayo, labda kama kutatokea
misukosuko mingine ambayo hatuwezi kuitabiri sasa. Tutaendeleza juhudi hizo za kukuza uchumi ili uchumi wetu uzidi
kutengemaa.

Kuendeleza Sekta za Uzalishaji Mali


Mheshimiwa Spika,
Pamoja na changamoto mbalimbali zilizokuwepo juhudi kubwa ilielekezwa katika kuendeleza sekta ya kilimo, ufugaji, uvuvi,
viwanda na madini. Mafanikio ya kutia moyo yalipatikana na dhamira yetu ni kuyadumisha na kupata ufanisi zaidi miaka
mitano ijayo.

Kilimo na Mifugo
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa kilimo na ufugaji, mwaka 2006 tulianzisha programu kubwa ya kuendeleza sekta hizo. Baadaye mwaka 2009
kwa kushirikiana na sekta binafsi tukatengeneza mkakati wa Kilimo Kwanza kuongeza kasi na ufanisi wa utekelezaji wa
malengo ya kuleta mapinduzi katika kilimo chetu na ufugaji wetu.

Mheshimiwa Spika;
Matunda ya juhudi zetu hizo yameanza kuonekana. Mavuno kwa mazao ya chakula na biashara yameendelea kuongezeka na
mwaka huu tunacho chakula cha kutosha nchini. Tutaendeleza juhudi hizo maradufu katika miaka mitano ijayo. Kwa ajili
hiyo vipaumbele vyetu vitakuwa vifuatavyo:

1. Kuendelea kuongeza mgao wa fedha katika bajeti ya sekta ya kilimo na kufikia asilimia 10 ya bajeti ya Serikali;

2. Kuharakisha uanzishwaji wa Benki ya Kilimo ili wakulima, wafugaji na wavuvi wapate mikopo itakayowawezesha kukuza
na kuboresha shughuli zao, hivyo kuongeza tija na mapato yao;

3. Kutengeneza na kutekeleza programu maalumu ya kuendeleza ufugaji itakayojumuisha pia uendelezaji wa malisho na
kukabiliana na athari za ukame;

4. Kuendeleza utafiti wa kilimo na mifugo;

5. Kuendelea kuhimiza kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya kanuni bora za kilimo, mbolea, mbegu bora, zana za kisasa za
kilimo, uboreshaji wa masoko na miundombinu;

6. Kupanua mafunzo ya wataalamu wa kilimo na mifugo wa ngazi mbalimbali ili kupata maafisa ugani wa kutosha wa
kuelimisha wakulima na wafugaji; na

7. Kuendeleza mikakati ya kuanzisha kanda za kilimo na kuhamasisha kilimo cha mkataba katika kanda hizo na kwingineko
itakapowezekana.

Uvuvi
Mheshimiwa Spika,
Kuhusu uvuvi, tutaendeleza kazi nzuri tuliyoifanya katika miaka mitano iliyopita ya kuendeleza shughuli za uvuvi na
kuwaendeleza wavuvi wa baharini na katika maziwa na mito. Tutaendelea na jitihada za kulinda hazina yetu ya samaki dhidi
ya uvuvi haramu. Ni makusudio yetu kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010-2015 ya kutengeneza
programu kabambe ya kuendeleza sekta ya uvuvi nchini kama tulivyofanya kwa kilimo.

Kuleta Mapinduzi ya Viwanda


Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano iliyopita tumeanzisha mkakati wa dhati wa kuendeleza viwanda nchini. Tumeunganisha mamlaka mbili
za uendelezaji wa maeneo maalum ya uchumi, yaani Special Economic Zones (SEZ) na Export Processing Zones (EPZ) kuwa
chini ya Wizara moja na chini ya uongozi mmoja. Kufanya hivyo kumeimarisha upangaji na utekelezaji wa mipango ya
kuendeleza viwanda nchini. Mikoa yote na Wilaya nyingi nchini zimetenga maeneo ya kujenga viwanda yatakayosimamiwa
na mamlaka ya Export Processing Zones Authority (EPZA).

Mheshimiwa Spika;
Kwa jumla juhudi zetu za kuendeleza viwanda nchini zina muelekeo mzuri. Sekta ya viwanda inakua kwa kasi nzuri ya
karibu asilimia tisa, na inatoa mchango wa zaidi ya asilimia nane katika pato la taifa. Katika miaka mitano ijayo tutaongeza
maradufu juhudi za kukuza na kuendeleza viwanda nchini. Tutaongeza uhamasishaji wa uwekezaji katika ujenzi wa viwanda
vipya na kufufua vilivyopo. Aidha, tutaboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo pia kuboresha upatikanaji wa umeme na
maji pamoja na kurahisisha taratibu za utoaji wa leseni za biashara na upatikanaji wa malighafi na ardhi.

Mheshimiwa Spika;
Tutaendelea kuimarisha Benki ya Rasilimali ili iwe chachu ya kukuza viwanda nchini kwa kutoa mikopo ya muda wa kati na
mrefu kwa wawekezaji, hasa wazawa. Pia, tutachukua hatua za makusudi za kuliimarisha Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO)
ili liweze kuwafikia na kuwawezesha watu wengi zaidi. Tutaitazama na kuiboresha ipasavyo Sheria iliyoanzisha SIDO.

Madini
Mheshimiwa Spika;
Tanzania imejaliwa kuwa na maliasili nyingi yakiwemo madini ya aina mbalimbali. Katika miaka mitano iliyopita tulielekeza
nguvu zetu kwenye kurekebisha mapungufu yaliyokuwemo kwenye mikataba ya madini, sheria na kanuni mbalimbali ili taifa
linufaike inavyostahili. Tumefanikiwa kurekebisha mikataba hiyo na makampuni yenye migodi mikubwa yamenza kulipa
kodi. Tumetunga Sera Mpya ya Madini (2009) na Sheria Mpya ya Madini (2010). Pia tumeunda kitengo cha Ukaguzi wa
Madini. Viwango vya mrabaha vimerekebishwa, ushiriki wa wazawa na Serikali umeainishwa vizuri. Maeneo kwa ajili ya
wachimbaji wadogo yameanza kutengwa na leseni zinatolewa. Kutokana na hatua hizo mwelekeo wetu sasa ni mzuri na
tunahakika taifa litanufaika inavyostahili kwa madini yake. Katika miaka mitano iliyopita madini yameliingizia taifa dola za
Kimarekani milioni 4,725.4 na kushika nafasi ya pili nyuma ya utalii kwa tofauti ndogo sana.

Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano ijayo, tutaendelea kutatua changamoto ambazo bado hazijapata ufumbuzi. Aidha, tutaliimarisha Shirika
la Taifa la Madini (STAMICO) ili kwa niaba ya Serikali liweze kushiriki katika umiliki wa migodi mikubwa na ya kati na
hivyo taifa kunufaika zaidi. Tutaendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika utafutaji na uchimbaji wa
madini, gesi asilia, mafuta ya petroli pamoja na kuongeza thamani ya rasilimali hizo.

Utalii
Mheshimiwa Spika;
Utalii ni sekta inayoongoza katika kuliingizia taifa letu fedha za kigeni. Kwa mfano, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita
(2005-2009) sekta hii iliingiza jumla ya dola za Kimarekani 4,987.5 milioni. Mafanikio haya yametokana na juhudi kubwa ya
kuitangaza Tanzania na vivutio vyake ndani na nje ya nchi. Katika miaka mitano ijayo tutaendelea na juhudi hizo kwa
kuongeza rasilimali na kupanua wigo wa aina za utalii kuhusisha utamaduni, mazingira, historia/makumbusho na michezo.
Pia tutaboresha miundombinu na mazingira ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji kwenye mahoteli ya hadhi ya nyota 3 hadi 5.

Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi


Mheshimiwa Spika;
Katika kujenga uchumi wa nchi yetu, hatutafanikiwa bila ya kuwawezesha wananchi na sekta binafsi ya ndani kushiriki na
kunufaika. Katika miaka mitano iliyopita tulifanya jitihada kubwa ya uwezeshaji wa wananchi kwa kuanzisha mifuko, taasisi
na programu mpya na kuziboresha zilizokuwepo ikiwa ni pamoja na TASAF na MKURABITA. Aidha, tuliwahimiza
wananchi kujiunga katika vikundi na kuanzisha vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) ili iwe rahisi kukopesheka.
Wamefanya hivyo na wengi wamenufaika sana kupitia SACCOS na VICOBA.

Mheshimiwa Spika;
Ahadi yetu ya kuanzisha Benki ya Wanawake imetimia. Benki hiyo imeanza kazi na tayari inatoa huduma. Katika miaka
mitano ijayo, tutaendelea kuijengea uwezo zaidi Benki ya Wanawake, pamoja na kuongeza fedha katika mifuko iliyopo,
kuimarisha Benki ya Rasilimali na kuanzisha Benki ya Kilimo. Lengo letu ni kuongeza na kuwawezesha watu wengi kupata
mikopo ili waendeleze shughuli zao za ujasiriamali. Pia tumedhamiria, kama nilivyosema awali, kutengeneza mkakati
maalum wa kuwawezesha wafanyabiashara wa kati washiriki katika uwekezaji mkubwa.

Kukuza Ajira
Mheshimiwa Spika;
Tutaongeza jitihada za kuwajali vijana wetu wanaoongezeka kila mwaka mijini na vijijini kutafuta ajira na riziki. Tutaboresha
mikakati ya kukuza ajira nchini ili watu wengi zaidi hususan vijana waajiriwe na kujiajiri. Tutaongeza kasi ya kujenga
majengo ya wafanyabiashara wadogo (Machinga) kama tulivyofanya pale Ilala, Dar es Salaam ili wawe na mazingira mazuri
ya kufanyia shughuli zao. Tutaendelea kujenga majengo ya namna hiyo Dar es Salaam, Mwanza na baadaye katika miji
mingine mikuu ya Mikoa hatua kwa hatua. Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha wajasiriamali wadogo kujiunga
kwenye vikundi ili waweze kutambuliwa na kukopeshwa kwa urahisi.

Tanzania Kuwa Lango Kuu la Biashara


Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu imejaaliwa kuwa mahali ambapo jiografia yake ni rasilimali ya kiuchumi. Tanzania inapakana na nchi za Malawi,
Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda ambazo zinategemea bandari, reli, barabara na
anga yetu kusafirisha bidhaa zao ziendazo na zitokazo nje.

Bado hatujaitumia kwa ukamilifu rasilimali hii ingawaje biashara ya usafirishaji (transit trade) inazidi kukua na inatuingizia
fedha nyingi zaidi za kigeni kuliko kilimo. Tunataka tuikuze zaidi biashara hii ili tunufaike zaidi. Kwa ajili hiyo tutaendeleza,
kwa kasi zaidi kazi ya kuimarisha miundombinu ya bandari, reli, barabara, viwanja vya ndege na teknohama katika miaka
mitano ijayo.

Bandari na Reli
Mheshimiwa Spika;
Tunao mpango wa kupanua na kuimarisha bandari ya Dar es Salaam ili iweze kupitisha bidhaa nyingi zaidi na kwa ufanisi
zaidi. Tutafanya hivyo hivyo kwa bandari za Mtwara, Tanga, Kigoma na Mwanza. Vile vile tutaimarisha bandari za Kasanga,
Mbamba Bay, Lindi, Musoma na Bukoba. Pamoja na mchango wa Serikali, tunakusudia kushirikisha sekta binafsi katika
juhudi hizi.

Mheshimiwa Spika;
Tutaongeza kasi ya kutatua matatizo yanayozikabili reli zetu mbili yaani TRL na TAZARA. Kwa upande wa reli ya kati
tunategemea kuanza ujenzi wa reli mpya ya upana wa kimataifa kutoka Isaka kwenda Rwanda na Burundi na kuboresha reli
yetu kutoka Isaka hadi Dar es Salaam iwe ya kiwango hicho. Aidha, tutaanza mchakato wa kuboresha reli kutoka Isaka
kwenda Mwanza na kutoka Tabora kwenda Kigoma ili iwe ya kimataifa. Ni matumaini yangu pia katika kipindi hiki
tutafanikiwa kupata wabia wa kushirikiana nasi kwa ujenzi wa reli ya Tanga hadi Musoma.

Barabara
Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano iliyopita tumejitahidi sana kuimarisha miundombinu ya barabara. Tumejenga barabara za lami, za
changarawe na za udongo kote nchini na kuwezesha maeneo mengi hata ya vijijini kufikika. Ni makusudio yetu kuendeleza
juhudi hizo maradufu katika miaka mitano ijayo. Tutakamilisha ujenzi wa barabara unaoendelea hivi sasa na kuanza ujenzi
wa barabara nyingine zilizoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka huu. Kwa ajili hiyo tutaendelea kutoa
kipaumbele cha juu kwa bajeti ya sekta ya miundombinu kama tulivyofanya katika miaka mitano iliyopita.

Kuboresha Huduma za Kijamii na Kiuchumi


Elimu
Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano iliyopita tumefanikiwa kupanua fursa za watoto na vijana wetu wengi sana kupata elimu ya awali,
msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu. Katika miaka mitano ijayo tutaendelea na upanuzi wa fursa za kupata elimu lakini
mkazo mkubwa tutauelekeza katika kuboresha elimu inayotolewa.

Mheshimiwa Spika;
Tutaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa bajeti ya elimu ili tufundishe na kuajiri walimu wengi zaidi, tupate vitabu na
vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Tutaongeza matumizi ya teknohama katika utoaji wa mafunzo pamoja na kujenga uwezo
wa wanafunzi na waalimu kiteknolojia ili kwenda sambamba na karne hii ya utandawazi. Aidha, tutajenga maabara za sayansi
katika sekondari zetu zote.

Katika kipindi hiki pia tutachukua hatua thabiti za kuboresha maslahi na mazingira ya kufanyia kazi ya walimu na watumishi
wa sekta ya elimu. Kwa ajili hiyo, tutakamilisha na kuanza kutekeleza mpango kabambe wa kujenga nyumba za walimu kote
nchini. Tutahakikisha kuwa mpango huo unatengewa pesa ya kutosha.

Mheshimiwa Spika;
Tutaendelea kujenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya kwa ajili ya kuandaa vijana wetu kwa stadi mbalimbali za kazi. Kwa
upande wa elimu ya juu, katika miaka mitano ijayo tutatekeleza Mpango wetu mpya wa Maendeleo ya Elimu ya Juu ambao
malengo yake makuu ni kupanua fursa za elimu ya juu na kuongeza ubora wa elimu ili ikidhi viwango na utashi wa soko la
ajira nchini na kimataifa. Tutaimarisha na kupanua vyuo vilivyopo na kujenga vipya.

Mheshimiwa Spika:
Katika miaka mitano ijayo, tutakamilisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma na kuanza mchakato wa ujenzi wa Chuo Kikuu
cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere huko Butiama, Musoma. Katika kipindi hicho pia, tutajenga makazi mapya kwa ajili ya
Chuo Kikuu cha Udaktari cha Muhimbili yatakayokuwa Mloganzila. Tutaendeleza mchakato wa kuipandisha hadhi Taasisi ya
Teknolojia ya Mbeya kuwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia. Ni dhamira yetu pia kutengeneza mpango wa muda wa
kati na muda mrefu wa ujenzi wa vyuo vikuu nchini. Kwa maoni yangu Serikali iwe na Chuo Kikuu katika kila kanda hapa
nchini.

Afya
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2007 tulitunga Sera Mpya ya Afya na kutengeneza Mpango wa miaka 10 wa Maendeleo ya Afya ya Msingi
(MMAM) wa kutekeleza sera hiyo. Shabaha yetu ni kufanya mambo manne: Kwanza, kusogeza huduma ya afya karibu na
wanapoishi watu. Lengo letu hasa ni kuona Watanzania hawatembei zaidi ya kilometa tano kufuata huduma ya zahanati.
Aidha, kuwa na vituo vya afya katika kila kata na kuboresha huduma katika hospitali za Wilaya, Mikoa na Kanda ili matatizo
mengi yamalizwe huko. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iimarishwe ili iweze kushughulikia matatizo makubwa zaidi
yanayohitaji taaluma za kibingwa na vifaa bora zaidi.

Pili, kujenga uwezo wetu wa ndani wa kutibu maradhi ili tupunguze watu wanaopelekwa nje kwa matibabu. Tatu, kuongeza
uwezo wetu wa kupambana na maradhi hasa yale yanayoathiri na kuua watu wengi. Na, nne kuongeza ajira ya madaktari,
wauguzi na wataalamu wengine wa afya ili kupunguza tatizo la uhaba mkubwa wa watumishi wa afya.

Mheshimiwa Spika;
Nafurahi kusema kuwa utekelezaji wa shabaha zote za MMAM umeanza na unaendelea vizuri. Huu ni mwaka wa pili tu wa
utekelezaji na mwelekeo wake ni mzuri. Sina shaka kabisa kuwa tutafanikiwa kutekeleza malengo yetu katika muda wa
miaka 10 ya mpango huu.

Mheshimiwa Spika;
Tutaendelea kuongeza fedha katika bajeti ya sekta ya afya kama tulivyofanya katika miaka mitano iliyopita tulipoiongeza
kutoka shilingi bilioni 271 mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 1,205.9 mwaka huu. Aidha, tutaendeleza ushirikiano na
mashirika ya dini katika utoaji wa huduma ya afya. Vile vile, tutaendelea kutengeneza mazingira mazuri na kushawishi
wenzetu wa sekta binafsi wenye uwezo na wale wenye hospitali kubwa huko nje wajenge hospitali za aina hiyo hapa nchini.
Maji na Mazingira
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na juhudi kubwa tulizozifanya katika kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji nchini, uhaba wa maji bado ni tatizo
kubwa katika maeneo mengi. Tumedhamiria kulitatua tatizo hili kwa kuongeza mgao wa fedha za bajeti ya Serikali kwa ajili
ya huduma ya maji. Nilishaagiza kwamba tufanye kila tuwezalo ili bajeti ya sekta ya maji iongezwe kwa kiasi kikubwa
kuanzia mwaka ujao wa fedha.

Tutaendelea kuwaomba wabia wetu wa maendeleo waongeze mchango wao katika kuendeleza huduma ya maji nchini.
Napenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani maalum kwa Benki ya Dunia na wahisani wengine kwa msaada wao mkubwa
wanaoutoa kwa sekta ya maji. Ni matumaini yangu kuwa mchango wao na wadau wengine utaongezeka katika miaka mitano
ijayo.

Mheshimiwa Spika;
Lipo tatizo kubwa la kuendelea kupotea kwa vyanzo vya maji hapa nchini. Matendo yetu wenyewe ya uharibifu wa mazingira
ndicho chanzo kikubwa kilichotufikisha hapa. Sasa wakati umefika wa kutolifumbia macho jambo hili. Tutachukua hatua
thabiti za kuhakikisha kuwa miongozo mbalimbali iliyokwishakutolewa kuhusu hifadhi ya mazingira na utunzaji wa vyanzo
vya maji inatekelezwa.

Lazima mamlaka husika katika Mikoa, Halmashauri za Wilaya na Mabonde ya Mito zitimize ipasavyo wajibu wao kuhusu
suala hili muhimu. Wahenga wamesema “ajizi nyumba ya njaa”. Tukifanya ajizi na kuacha kuchukua hatua muafaka katika
miaka si mingi ijayo kutakuwa na uhaba mkubwa wa maji unaoweza hata kuhatarisha amani. Tuchukue hatua sasa kuepuka
janga hili.

Nishati
Mheshimiwa Spika;
Bila ya shaka sote tunakumbuka kuwa nilianza uongozi wa nchi yetu kukiwa na tatizo kubwa la upungufu wa umeme
kutokana na ukame mkubwa ulioikumba nchi yetu wakati ule. Tulilazimika kuchukua hatua za dharura za kukabiliana na
tatizo hilo ambazo zilitusaidia kupunguza ukali wa tatizo. Matatizo yale yalitufundisha kupunguza kutegemea mno umeme
wa nguvu ya maji na kuongeza mchango wa vyanzo vingine vilivyopo kama vile gesi asilia na makaa ya mawe.

Mheshimiwa Spika;
Tumefanya hivyo na tayari tumeongeza megawati 145 za umeme kwa kutumia gesi asilia. Mipango ya kuongeza megawati
100 za umeme unaotokana na gesi asilia imekamilika, imebaki kazi ya utekelezaji kuanza. Katika miaka mitano ijayo
tunategemea kuongeza megawati 640 za umeme unaotokana na gesi asilia, maji na makaa ya mawe.

Mheshimiwa Spika;
Tumepata mafanikio ya kuridhisha katika usambazaji wa umeme nchini. Kazi ya kuyapatia umeme makao makuu ya Wilaya
imeendelea vizuri. Tulikuwa tumebakiza Wilaya ya Namtumbo pekee ambayo nayo mchakato wake umekwishaanza. Hivi
sasa tunajipanga kutengeneza mipango ya kuzipatia umeme Wilaya mpya zilizoundwa ambazo hazitakuwa na umeme.

Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano ijayo tutaendeleza jitihada za kuiunganisha mikoa yote kwenye gridi ya taifa. Aidha, tutaongeza kasi ya
kusambaza umeme mijini na vijijini kwa lengo la kuwafikia asilimia 30 ya Watanzania ukilinganisha na asilimia 14 wa sasa
au asilimia 10 wa mwaka 2005. Naamini jitihada tunazozifanya za kuimarisha TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) pamoja na dhamira yetu ya kuongeza bajeti ya sekta ya nishati vitatuwezesha kutimiza malengo yetu ya kuongeza
uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini.

Kuimarisha Demokrasia
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tumeshuhudia kukua na kustawi kwa demokrasia nchini. Vyama vya siasa
vimeongezeka kwa idadi na kuimarika katika kufanya kazi za siasa. Asasi za kidemokrasia kama vile Bunge na Mabaraza ya
Madiwani zimeendelea kutimiza kwa ufanisi zaidi wajibu wao wa kuwa vyombo vya uwakilishi wa wananchi vya
kutumainiwa. Hali kadhalika sauti ya asasi za kiraia imeendelea kusikika kutoa maoni juu ya masuala muhimu kwa taifa letu
na watu wake. Vyombo vya habari navyo vimeendelea kufanya kazi zake kwa uhuru.

Mheshimiwa Spika;
Ni makusudio yangu na yetu Serikalini kuona kuwa demokrasia inazidi kustawi na raia wanapata fursa ya kutoa maoni kwa
uhuru na uhuru wa vyombo vya habari unaheshimiwa. Tutaendelea kusaidia na kuliwezesha Bunge na Mabaraza ya
Halmashauri kutimiza wajibu wao ipasavyo. Tumefanya hivyo miaka mitano iliyopita, naahidi kuwa tutajitahidi kufanya
vizuri zaidi katika miaka mitano ijayo.

Utawala Bora
Mheshimiwa Spika;
Katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge la Tisa tarehe 30 Desemba, 2005, niliahidi kuwa Serikali nitakayoiunda itahakikisha
kuwa demokrasia inastawi, itazingatia utawala bora, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu. Pia niliahidi
kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa na maovu katika jamii. Nafurahi kwamba katika miaka mitano iliyopita
tumetimiza ahadi zetu kwa kiasi kikubwa. Natambua wajibu wa kuimarisha mafanikio tuliyoyapata na kuongeza juhudi pale
ambapo hatuna budi kufanya vizuri zaidi. Natambua, pia, haja ya kuboresha utendaji kazi na uwajibikaji Serikalini: katika
Wizara, Idara na Taasisi za Serikali na, katika Halmashauri za Wilaya na Miji.

Tumejitahidi sana katika miaka mitano iliyopita kutoa mafunzo na kusisitiza nidhamu, uwajibikaji na ufanisi zaidi. Lakini
bado hatujafika pale tunapopataka. Naahidi kuwa tutajipanga vizuri zaidi na kusukuma kwa nguvu zaidi nidhamu na
uwajibikaji katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Naahidi pia kwamba tutaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa
maana ya mishahara, marupurupu, malipo ya uzeeni na mazingira ya kazi.

Mapambano Dhidi ya Rushwa


Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa mapambano dhidi ya rushwa katika miaka mitano iliyopita tumechukua hatua muafaka za kujenga uwezo wa
kisheria, kimfumo na kitaasisi wa kupambana na rushwa nchini. Tumetunga sheria mpya kali zaidi na yenye upeo mpana
zaidi wa kukabili tatizo hili. Pia tumetunga Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya kuzuia na kupambana na rushwa wakati wa
uchaguzi. Tumeunda chombo kipya cha kuzuia na kupambana na rushwa, TAKUKURU, chenye mamlaka zaidi kisheria na
chenye uwezo mkubwa zaidi wa rasilimali watu na vifaa wa kutekelezea majukumu yake.

Mheshimiwa Spika;
Ni ukweli ulio wazi kuwa katika kipindi hiki tuhuma nyingi zimeibuliwa, kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani.
Watuhumiwa wengi zaidi wamepatikana na hatia na kuhukumiwa. Rushwa kubwa zimeshughulikiwa na vigogo
wamewajibishwa bila kuonewa muhali. Pamoja na hayo bado ipo haja ya kufanya zaidi kwani tatizo la rushwa bado ni
kubwa.

Nimesikia, tumesikia na wamesikia kilio cha wananchi cha kutaka tufanye vizuri zaidi. Tutaongeza bidii katika mapambano
haya. Naomba wananchi waendelee kutuunga mkono na kututia moyo na hasa TAKUKURU. Kauli za pongezi pale
wanapofanya vizuri zinawaongezea ari vijana wetu ya kufanya vizuri zaidi. Lakini, tabia za kubeza hata pale walipofanya
vizuri zinawavunja moyo, kuwakatisha tamaa na kushuhsa morali wao wa kazi. Tuwapongeze wanapofanya vizuri,
tuwakosoe wanapokosea na lililo muhimu zaidi tuwape ushauri juu ya njia bora ya kupata ufanisi. Tukifanya hivyo tunajenga,
kinyume chake tunabomoa.

Utawala wa Sheria
Mheshimiwa Spika;
Tutaendelea kuimarisha na kuboresha mfumo wetu wa utoaji haki nchini. Serikali itashirikiana na Mahakama kupanga na
kutekeleza mipango ya kuongeza uwezo wa vyombo vya kutoa haki ili vitimize ipasavyo wajibu wao. Tutaendelea kuongeza
bajeti ya Mahakama nchini. Tutakamilisha mchakato wa kuanzisha mfuko wa Mahakama ambao utaongeza uhuru na uwezo
kwa masuala ya fedha na rasilimali. Tutaendelea kuongeza Majaji, Mahakimu na Mawakili wa Serikali. Aidha, tutahakikisha
kuwa mchakato wa kuboresha mfumo wa utawala katika Mahakama nchini unakamilishwa.

Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano hii tutalivalia njuga na kulipatia ufumbuzi muafaka tatizo kubwa la mlundikano wa wafungwa na
mahabusu magerezani. Mapema iwezekanavyo nakusudia kukutana na wahusika katika Wizara ya Mambo ya Ndani na Idara
ya Magereza kuelewana juu ya hatua za kuchukua .

Wanawake Katika Nafasi za Maamuzi


Mheshimiwa Spika;
Katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge lililopita na hata kabla, nilitoa ahadi ya kuchukua hatua za makusudi za kuongeza
ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi. Ninyi na mimi ni mashahidi kwa kiasi gani tumetimiza ahadi hiyo katika
Baraza la Mawaziri, utumishi wa umma na kwingineko. Aidha, tuliahidi kufikia asilimia 50 kwa 50 katika Bunge hili. Bado
hatujafikia lengo hilo, lakini ni ukweli ulio wazi kwamba Bunge hili ndilo la kwanza tangu Uhuru, Mapinduzi na Muungano
kuwa na uwakilishi mkubwa wa wanawake. Tutaendelea kutafakari namna bora ya kufikia lengo letu hilo adhimu.

Tume ya Mipango
Mheshimiwa Spika;
Mwaka 2008 niliunda upya Tume ya Mipango na kuipa muundo wake wa sasa ili kuirejesha nchi kwenye utaratibu mzuri wa
kupanga maendeleo yake ya muda mrefu, wa kati na mfupi. Tume itapanga mipango, kisha itaratibu, kufuatilia na kufanya
tathmini ya utekelezaji wa mipango hiyo na kuishauri Serikali ipasavyo. Nilipoteua watendaji wa Tume niliwataka watazame
upya shabaha na malengo ya Dira ya Maendeleo ya 2025 ili wahuishe panapostahili. Kisha watengeneze mkakati wa
kutekeleza Dira hiyo kwa miaka 15 iliyosalia. Niliwataka wagawe utekelezaji wa mkakati huo katika vipindi vitatu vya miaka
mitano mitano na kila kipindi kiwe na mpango wake wa maendeleo.

Mheshimiwa Spika;
Kwa sababu hiyo mwaka ujao tutazindua Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ya Miaka Mitano, kati ya hiyo mitatu ya
kutekeleza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025. Naiona njia hii kuwa ni ya uhakika zaidi ya kutekeleza Dira
hiyo badala ya kuacha kila Wizara, Idara au Taasisi kufanya inavyofikiria yenyewe inafaa. Ni matumaini yangu kuwa kila
mmoja wetu kote nchini ataipa Tume ya Mipango ushirikiano na msaada unaostahili ili waweze kutekeleza kwa ufanisi
jukumu lao hilo muhimu na la kihistoria.

Michezo na Utamaduni
Katika miaka mitano iliyopita tumeanza safari ya kuboresha michezo nchini ili tuwape fursa vijana wetu kuendeleza vipaji
vyao na Tanzania isikike katika medani za michezo duniani. Nilitimiza ahadi yangu ya kugharamia makocha wa michezo
mbalimbali watakaochaguliwa na vyama vya michezo husika. Hivi sasa tunao makocha wa mpira wa miguu, ndondi, riadha
na netiboli. Bado hatujapata mafanikio ya juu, lakini mwanga wa matumaini unaonekana. Kinachotakiwa sasa ni kuimarisha
uongozi na utendaji wa vyama na vilabu vya michezo husika ili muda mwingi utumike kuendeleza vipaji vya wana-michezo
wetu badala ya hali ilivyo sasa ambapo muda mwingi hutumika kugombania uongozi na maslahi binafsi.

Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki pia tumerejesha michezo mashuleni, lakini lazima tujipange vizuri zaidi kufanikisha michezo mashuleni.
Tufundishe walimu wa michezo na tuhakikishe viwanja na vifaa vya michezo vinapatikana mashuleni. Sasa wakati umefika
kwa vyama au vilabu vya michezo kuanzisha shule za michezo yao ili kukuza vipaji vya vijana mapema.

Katika kipindi hiki pia tumeshuhudia maendeleo makubwa ya sanaa za maonyesho yaani muziki na filamu. Wameibuka
wanamuziki wengi wazuri wa muziki wa kizazi kipya, taarabu na rumba. Pia kuna maendeleo makubwa ya filamu na uigizaji.
Kuna haja ya kujipanga vizuri kusaidia kuendeleza sanaa hizo na wasanii wake. Mimi binafsi nimeanza kuchukua hatua za
hapa na pale za kujaribu kutatua baadhi ya matatizo yanayowakabili. Sasa wakati umefika wa kuwa na mipango thabiti ya
kuendeleza fani hizi na kuwawezesha wasanii kuendeleza vipaji vyao na kunufaika na kazi zao.
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Spika;
Tumepata mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa diplomasia na ushirikiano wa kimataifa katika miaka mitano iliyopita.
Jina la Tanzania linang’ara katika medani za kimataifa. Tunaheshimika na kushirikishwa katika mambo mengi ya kikanda na
kimataifa. Tumetembelewa na wageni wengi mashuhuri na tumepata misaada mingi ya maendeleo na kufutiwa baadhi ya
madeni yetu.

Tumeitangaza vyema nchi yetu na mafanikio yake yanaonekana. Mauzo yetu ya nje yanazidi kuongezeka, uwekezaji unakua
na watalii wanaongezeka. Tumekuwa wenyeji wa mikutano mikubwa ya kimataifa. Yote hayo yamekuwa chachu kwa uchumi
wetu kukua na kustawi. Katika miaka mitano ijayo tutaendeleza diplomasia yetu na ushirikiano wa kimataifa kwa ari zaidi,
nguvu zaidi na kasi zaidi.

Mheshimiwa Spika;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wabia wetu wa maendeleo, yaani nchi na mashirika ya
kimataifa kwa misaada yao ambayo imesaidia sana kuifikisha Tanzania hapa ilipo. Kwa vile bado tunahitaji na tunastahili
kusaidiwa, naomba wasituchoke, waendelee kutusaidia. Naamini miaka si mingi kutoka sasa hawatakuwa na ulazima wa
kufanya hivyo. Hata sasa wanauona ushahidi kwa kiasi gani mwaka hadi mwaka tunaongeza uwezo wetu wa kujitegemea.
Hiyo ndiyo dhamira yetu na mwelekeo wetu wa siku za usoni.

Mapato na Matumizi
Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano iliyopita tumeongeza mapato yetu kutoka wastani wa shilingi 177.1 bilioni kwa mwezi mwaka 2005
hadi shilingi 453 bilioni kwa mwezi hivi sasa. Tumepunguza kutegemea misaada kutoka asilimia 44 mwaka 2005 hadi
asilimia 28 mwaka huu. Tutaongeza maradufu jitihada zetu za kukusanya mapato na kuimarisha nidhamu ya matumizi.
Tutaboresha mfumo wa ukusanyaji mapato ya Serikali na kupanua wigo wa walipa kodi. Tutakuwa wakali kuhakikisha
mianya inayovujisha mapato inazibwa na pesa za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Uzembe, wizi na
ubadhirifu havitavumiliwa. Tutaendelea kuzipa uzito unaostahili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
na kuchukua hatua zipasazo kasoro zinapobainika.

Ushirikiano wa Kanda
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), SADC na Umoja wa Afrika (AU). Katika miaka mitano
iliyopita tumeshiriki kwa ukamilifu katika asasi hizo za kikanda na nchi yetu imenufaika kisiasa, kiuchumi na kiusalama.
Mauzo yetu katika nchi za EAC na SADC, ambayo yameongezeka sana, yamekuwa nguzo yetu kuu ya biashara ya nje ya
nchi yetu. Tumenufaika sana na ushirikiano huu wa kanda. Katika miaka mitano ijayo tutazidi kuimarisha ushiriki wetu kwa
maslahi ya nchi yetu na watu wake.

Mheshimiwa Spika;
Tutaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo yanayotokea katika Jumuiya hizo na hasa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki
ambapo kasi ya utangamano ni kubwa. Kama mjuavyo tarehe 1 Julai, 2010 Soko la Pamoja limeanza baada ya kukamilika
kwa mafanikio, ujenzi wa Umoja wa Forodha. Hivi sasa mchakato wa kuanzisha Umoja wa Sarafu unaendelea kwa kasi na
unategemewa kukamilika mwaka 2012. Lazima tuhakikishe kuwa tunashiriki kwa ukamilifu katika vikao vyote
vinavyozungumzia masuala ya utangamano wa Afrika Mashariki ili kutetea na kulinda maslahi yetu.

Mheshimiwa Spika;
Hatuna budi kuchangamka na kujipanga vizuri kwani muda si mrefu kutoka sasa mjadala kuhusu kukamilisha hatua ya
mwisho ya utangamano yaani Shirikisho la Kisiasa utaanza. Kwa nijuavyo mimi, kwa jinsi shauku ya kuwa na shirikisho
ilivyo, mjadala huo huenda ukaendeshwa kwa ari na kasi kubwa. Si vyema kwa Tanzania kubaki nyuma kwa jambo lenye
maslahi kwetu sote. Lazima tushiriki vizuri ili kuhakikisha kuwa maslahi yetu yanazingatiwa ipasavyo mchakato huo
utakapokamilika.

Mheshimiwa Spika;
Tutaendelea kudumisha urafiki na ujirani mwema na mataifa yote yanayotuzunguka. Ni jambo lenye maslahi kwa uchumi na
usalama wa nchi yetu. Tutaendelea kutoa mchango wetu katika masuala ya amani na maendeleo kwenye ukanda wetu, barani
Afrika na duniani kwa kiwango tutakachoweza. Tutaendelea kuwa wanachama waaminifu na kushiriki ipasavyo katika
shughuli mbalimbali za Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na ushirikiano wa Kanda.

Hitimisho
Mheshimiwa Spika,
Nimesema mengi, lakini pia kuna mengi sikuyasema. Ni vigumu, katika muda tulionao nikasema yote. Naomba mridhike
niishie hapa kwa leo. Nimetoa kwa muhtasari sana mwelekeo na baadhi ya vipaumbele vitakavyoongoza Serikali
nitakayoiunda.

Katika siku chache zijazo nitaunda Baraza la Mawaziri. Dhamira yangu ni kwamba tupate Serikali makini, yenye watu
waadilifu na wachapakazi hodari. Watu ambao wataongoza nchi yetu na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na
mipango ya Serikali kwa umahiri mkubwa. Watu ambao wataondoa urasimu katika Serikali, watakuwa karibu na watu na
watashirikiana vizuri na Waheshimiwa Wabunge bila kujali vyama vya siasa wanavyotoka.

Mheshimiwa Spika;
Narudia kuwaomba muwape ushirikiano ili sote kwa pamoja tutimize wajibu wetu kwa wananchi waliotuchagua. Wabaneni
kisawasawa panapostahili, wasahihisheni wanapoteleza, lakini pia msiwe wachoyo wa kuwapa sifa wanapofanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge,


Naomba nimalize kwa kuwahimiza Watanzania wenzangu kwamba sote, mmoja mmoja na kwa umoja wetu, tuamue kwa
dhati kukusanya nguvu zetu, akili zetu na maarifa yetu yote, kama ndugu wa Taifa moja, kuifanya Tanzania kuwa nchi bora
ya kuishi. Maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana. Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge


Asanteni sana kwa kunisikiliza.
Mungu Ibariki Afrika.
Mungu Ibariki Tanzania.

You might also like