HOTUBA YA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHE. MIZENGO P.

PINDA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA WAZEE DUNIANI, UWANJA WA JAMHURI, MOROGORO 1 OKTOBA 2010

2

HOTUBA YA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHE. MIZENGO P. PINDA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA WAZEE DUNIANI, UWANJA WA JAMHURI, MOROGORO 1 OKTOBA 2010

Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kazi Ajira na Maendeleo ya Vijana, Mheshimiwa Katibu Mkuu TAMISEMI, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Waheshimiwa Wakuu na Wakurugenzi wa Wilaya, Waheshimiwa vingozi wengine wa Serikali, Mheshimiwa Mkurugenzi Mkazi wa HelpAge International, Mweshimiwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika ya Wazee Waheshimiwa wazee toka mikoa mbalimbali Kamati ya maadalizi. Mabibi na mabwana
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha tukakutana hapa Morogoro katika maadhimisho haya ya siku ya Wazee duniani. Kwa wale ambao tumefikia miaka 60 tunakila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuishi mpaka dakika hii na kufikia uzee wetu. Kwa dunia ya leo kufikia umri wa uzee ni kazi kwelikweli, kuna changamoto nyingi hasa kutokana na matatizo mbalimbali yanayojitokeza duniani yakiwepo maradhi. Hata kwa wale ambao hawajafikia miaka 60 ni vizuri wote kutambua kwamba wote ni wazee watarajiwa tu.
3

Malalamiko yanayotolewa na wazee ni bora tuyasikilize kwa makini na tusiyafumbie macho wala masikio. Ndani ya muda mfupi nasi tutakuwa huko huko. Kwa muungwana siyo vizuri kusubiri kunung’unika pale wewe mwenyewe utakapoaanza kukabiliana na changamoto za uzeeni, ni muhimu kuchukua hatua madhubuti kwa sasa hasa kwa yale mambo tuliyo na uwezo kwa manufaa ya wazee waliopo na wanaokuja. Nawashukuru sana Wazee kwa kuona inafaa kunialika kuja kushiriki nanyi katika shughuli hii muhimu. Lakini nitumie nafasi hii vile vile na zaidi niwashukuru walioiandaa hafla hii. Najua kila mahali ukishaambiwa Waziri Mkuu ama Mheshimiwa Rais anakuja lazima ujitahidi nami nina hakika Wazee hawa watakuwa wamehangaika kwelikweli. Napenda kuwashukuru Wazee kwa ujumla na kamati nzima ya maadalizi chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa kwa kufanikisha maadhimisho haya. Niwashukuru kwa namna ya pekee wale wazee waliotoka mikoa mbalimbali. Hongereni sana na poleni kwa safari. Niwatakie safari njema mtakapokuwa mnarudi, kwa kweli tunawashukuruni sana.

SIKU YA WAZEE DUNIANI
Ndugu zangu, Umoja wa Mataifa ulifikia uamuzi wa kutenga siku hii maalumu ya wazee duniani kwa sababu nyingi. Sababu mojawapo kubwa ni kutoa nafasi kwa mataifa yote duniani kutafakari hali ya maisha ya wazee wake, na kuangalia mapungufu yaliyopo katika mipango yakushughulikia kundi hili kwa lengo la kuiboresha. Lengo likiwa ni kuwafanya wazee wetu kuishi maisha ya heshima kwa kuwapatia mahitaji yao muhimu. Ni siku pia inayotumika kumkumbusha kila mwanadamu kwamba yeye ni mzee mtarajiwa na hivyo kumtaka ajiandae kwa maisha ya uzeeni ambayo hayakwepeki. Ukitaka kujua ukweli wa dunia mtoto anapozaliwa huwa anabebwa tu mara nyingi na mama, baba mara chache sana na baadaye anaanza kutambaa. Na baada ya muda anaanza kutembea, anaenda shule, kisha anaoa au anaolewa na akishafika hapo juu uzeeni anaanza kushuka. Hatembei bila fimbo huo ndiyo ukweli wa maisha na hata fimbo yenyewe baadaye inakuwa ni nzito. Wakifikia wakati huo huanza pia kushambuliwa na maradhi kwa wingi mara mgongo, kiuno, mfupa, miguu nk Kwa sasa lipo tatizo kubwa lilitokana na ugonjwa wa UKIMWI. Wazee ambao inakadiriwa kuwa ni asilimia 5.7 wanatunza karibu asilimia 50 ya yatima wote. Lazima tutafakari haya tuone jinsi gani tunaweza kuwasaidia wazee kuwapunguzia matatizo.

THAMANI YA WAZEE
Wazee ni rasilimali na ni hazina kubwa ya maendeleo lakini tukubali vilevile uzee ni dawa. Mkiwa mmekorofishana na mkeo au mumeo mnaenda kwa wazee. Hata purukushani nyingi zinapotokea huwa tunakwenda kwa wazee kupata ushauri na mara nyingi linakwisha. Wao, kwa busara na hekima zao ni dawa, kwa hiyo lazima tujue wazee hawa ni muhimu sana katika maisha yetu na tuendelee kuwaenzi na tuwatumie kwa kadri itakavyowezekana. Lakini lazima tutambue wanatuhitaji sana ili tuweze kuwawekea mazingira mazuri zaidi ya kuishi ili kama Taifa tuendelee kunufaika na mchango wao. Tukumbuke hawa ndiyo wametujengea Taifa hili letu tunalojivunia.
4

Ni vizuri tukatambua kwamba wazee wetu akinababa na akinamama, wengi wao hasahasa wametokana na maisha ya vijijini, wamepita kwenye msukosuko ya kilimo, ufugaji au uvuvi. Kwa Mtanzania hilo halikwepeki maana mnaposema asilimia 80 ni wakulima ni kweli kwamba ndiyo hiyo asilimia 80 ya wazee wanaotokea vijijini sehemu ndogo sana isiyozidi asilimia nne tunatoka maofisini. Ni lazima tukubaliane kwamba Wazee hawa lazima tutakuwa nao na ni jukumu la nchi kutambua kuwa uzee utakuwepo siku zote. Lazima jamii ngazi zote kuanzia vitongoji na vijijini tuweze kuwatambua Wazee hawa katika maeneo yetu. Hili ni jambo muhimu na hatuwezi kuwatupa wala kuwaacha pasipo msaada.

KAULIMBIU
Kaulimbiu ya mwaka huu ni nzito kidogo, Wazee na mafanikio ya Milenia. Kaulimbiu yao inatukumbusha na kutuuliza Serikali mmefikia wapi kwa malengo ya milenia hasa yale yanayotugusa sisi wazee? Nadhani ndiyo mtihani wanaotupa. Ndugu wananchi, yapo malengo 8 ya milenia, lakini kwa maana ya Wazee hawa, zaidi lengo la kwanza ambalo linazungumzia kuondoa umaskini uliokithiri pamoja na njaa ndilo linalowagusa kweli. Tanzania tunalo hilo tatizo lakini kwenye uzee ni zaidi hasa unapokutwa na mzigo wa kulea watoto yatima hali inakuwa ngumu sana na umasikini wanaouzungumza Umoja wa Mataifa ni wale wanaosema wanaishi chini ya sh. 1,500/= kwa siku. Huu ndiyo umaskini uliokithiri. Siku 10 ni sawa na sh. 15,000/-; siku nyingine 10 unatumia sh. 15,000 na siku 10 zilizobaki unatumia sh. 15,000/- jumla sh. 45,000/- kwa mwezi. Kama hujavuka hapa wewe uko bado kwenye umaskini mkubwa sana. Tungekuwa na muda tungewauliza mzee mmoja mmoja hivi mzee hizo sh. 45,000/unazipata kwa mwezi? Pengine Wazee wangesema hata ile sh. 500/- kwa mwezi naisikia tu, hasa vijijini; kwa hiyo tatizo ni kubwa siyo dogo. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa tulitakiwa ifikapo mwaka 2015 tuwe tumepunguza tatizo hili angalau kwa asilimia 50, kazi ni kubwa kidogo ila penye nia hapakosi njia. Vivyo hivyo kwa upande wa njaa, kwa nini tatizo la njaa linakuwa kubwa kwa Wazee? Tukishafikisha umri mkubwa jamani tupende tusipende unaweza ukawa unajitahidi kulima eka zako tatu, nne au tano kwa jembe lako la mkono. Ukishafikisha miaka 65 au 70 hata kulima ile eka moja ni tatizo, sasa njaa itakukimbiaje? Na kama huna mtu wa kukujali ni mbaya zaidi. Kwa hiyo na kwenye njaa nayo Wazee hawa ni lazima tukubali ipo changamoto kubwa ya kuishughulikia ili nao angalau waweze kusema si haba kuna kitu Serikali inafanya angalau kidogo tu.

KUONDOKANA NA UMASKINI
Ukiniuliza mimi nitakwambia kwa hakika kama Watanzania hatuwezi kuweka nguvu kubwa katika sekta hii ya kilimo ambako ndiko Watanzania wengi waliko tukakibadilisha kiwe kilimo chenye tija, umaskini si rahisi kututoka. Ni lazima tukubali kwamba kilimo ndiyo mkombozi wetu na kama mnataka kuondokana na umaskini hapa ndiyo tuweke nguvu kubwa. Serikali ya Rais Kikwete pamoja na kauli mbiu ya kilimo kwanza tumeshaanza kuona dalili nzuri, lakini nasema haitoshi ndiyo maana tunaendeleza juhudi ili tutoke kwenye jembe la mkono twende angalau kwenye matrekta madogo na baadaye tupande ngazi kwenda kwenye matrekta makubwa. Lazima pia tuimarishe utafiti na tuwe na wataalamu wa ugani wa kutosha na tuimarishe kilimo cha umwagiliaji. Lazima tuhakikishe tuna masoko na kwenye masoko ni lazima tuingize mipango mahususi wa kuhakikisha mazao yote yale tunayoyalima yanasindikwa ili tuweze kuongeza thamani
5

na kuwaongezea wananchi kipato chao. Kwa njia hii, ndiyo tunaweza kushughulika na wazee inavyotakiwa. Kwa sasa lazima tukubali changamoto bado kubwa pamoja na jitihada kidogo ambazo zimeanza kuzaa matunda mazuri lakini bado lazima tufanye kazi ya ziada. Safari hii kwa maana ya msimu tuliomaliza faraja ninayoiona leo ni kwamba sasa kilio ni kwamba mahindi ni mengi tutayapeleka wapi? Ukienda Iringa, Mbeya, Ruvuma, nenda Rukwa, Morogoro safari hii wamelima kwelikweli. Kwangu mimi naona heri hilo kuliko lile lililokuwa likijitokeza kabla, hili ni rahisi kushughulika nalo kuliko unapokuwa na njaa.

WAZEE NA MAGONJWA
Ndugu wananchi, lengo lingine linalowagusa sana Wazee hawa ni lengo namba 6, linalohusu kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI, MALARIA, na magonjwa mengine kama vile KIFUA KIKUU, n.k. Kwa nini tunasema linawagusa? Linawagusa kwa sababu kwa hali ilivyo sasa, wazee ndiyo walezi wa watoto yatima kwa sehemu kubwa, kwa hiyo lazima jitihada kubwa zifanywe kuhakikisha hili jambo linasimamiwa kikamilifu kabisa. Tumejitahidi kupunguza maambukizi kiasi tumefikia kama asilimia 5.8. Ni lazima tuendelee kuwasaidia watoto hawa walioko katika mikono ya hawa wazee. Jitihada nyingi pia zipo katika kudhibiti malaria kwa sababu pamoja na kwamba maradhi ni mengi lakini wataalamu wanatuambia malaria inaua zaidi kuliko magonjwa mengine yote hata ukiyachanganya pamoja. Kwa wazee hawa tatizo linakuwa ni kubwa zaidi kwa vile nguvu zao za kupambana na maradhi zimepungua. Pia tukumbuke kuwa malaria inashambulia watoto hao pia wanaolelewa na wazee. Ndugu wananchi, kwa mwaka huu tumejipanga kuendelea kutoa vyandarua milioni 14, vitasambazwa maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kila kaya, tumeanza na akinamama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano mwisho tukasema twende kwenye kaya. Hili tuna hakika linaweza kusaidia kupunguza tatizo la malaria. Kwa magonjwa kama kuharisha na kipindupundu; tutajitahidi kufanya vizuri zaidi kwa kadri uwezo wa Serikali utakavyozidi kukua. Nimefarijika kwamba wazee wenyewe wamekubali kwamba ziko dalili za kuwajali ambazo zimeanza kuchukuliwa na serikali, tuna kila sababu ya kuongeza juhudi hizi kwa manufaa ya taifa.

HUDUMA KWA WAZEE HOSPITALINI
Ndugu madaktari wetu, daktari makini na mzuri ni yule ambaye kila baada ya muda atatoka chumbani mwake akawasalimie wagonjwa wake walioko kwenye mstari. Anachoangalia pale ni kumtafuta mzee mwenye fimbo mkononi, amwambie mzee njoo huku, mama mjamzito njoo huku kwa maana kwamba unawatoa kwenye adha ya foleni kwa sababu wamechanganyika na vijana mwenye nguvu. Angalau fanyeni hilo tu, litawapa heshima lakini kubwa mtakuwa mmewasaidia sana Wazee hawa. La pili, tunaomba kila hospitali ya Wilaya na Mkoa tengeni maeneo maalumu ya kuwahudumia Wazee hawa. Mimi wilayani kwangu Mpanda tunafanya na tumeweza, Wizara ya Afya wanajua. Tumemweka daktari wa Wazee anaitwa Dk. Mwita. Tumetenga kabisa chumba cha Wazee tukahakikisha registration ya Wazee hawa iko hapo hapo. Tukahakikisha pharmacy na yenyewe iko hapo hapo. Tumewawekea makochi mahali pa kumsubiri daktari. Naomba hospitali za wilaya nyingine zote pia kuweka makochi na
6

kuboresha sehemu ya wazee kumgojea mganga. Haya yanawezekana. Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya wapo hapa. Ndugu wananchi, mara ya mwisho nilipoomba taarifa kujua wilaya ngapi na mikoa mingapi imeanza kutoa huduma bure za afya kwa wazee wote na kuwatengea maeneo yao ya huduma, tulikuta kuna mapengo mengi kwa vile wengine bado wanasuasua. Nasema hakuna sababu ya kutofanya haya niliyowaagiza. Kumbuka ipo siku yatakupata hayahaya kwa hiyo tujitahidi. Tunajipanga tuweze kuona kama jambo hili linaweza kufanyika kwenye hospitali zetu zote za rufaa, tulichukua muda kidogo kwa sababu ya mazingira ya hospitali hizi za rufaa - specialization ya maeneo yao tofauti na kule ambako ni mchanganyiko. Tutakapofikia mwisho na kupata ufumbuzi tutaitolea maelekezo yake nini kitawezekana, kubwa ni kutuepusha na hali ambayo kwenye hizi hospitali za rufaa unamkuta mzee wa miaka 70 anazunguka wee utafikiri hakuna watu wanaomwona. Ndugu wananchi, Mkutano ule wa mwaka jana nilisema kwa upande wa vituo vya afya na zahanati, wazee wapewe huduma ya matibatu bure. Hili halina mjadala, hakuna sababu ya kununa maana halikuhusu. Sera imeamua, Mkuu wa Nchi amesema, sisi tunalipigia kelele, wewe mpe dawa aondoke aende zake, wewe cha kufanya ni kutoa taarifa kwa wakubwa zako nimemhudumia mzee fulani na kumpa dawa bure, wao watajua la kuufanya. Tusilifumbie macho! Kazi yetu TAMISEMI ni kufuatilia na kuona suala linafanyika kikamilifu. Kwenye suala ili nataka niongezee kidogo kwa kuiomba Wizara ya Afya ione ni namna gani tunaweza kuwa na utaratibu wa kupeleka waganga kutoka hospitali za wilaya na mikoa kwenda kwenye maeneo ya vijijini na kupiga kambi kwa siku kadhaa ili kupima afya za wazee na kuwapatia huduma hasa kwa yale magonjwa ambayo hayawezi kutibiwa na waganga tulionao katika ngazi ya zahanati na kituo cha afya. Kwa kuanzia, tukifika angalau katika ngazi ya tarafa, itasaidia sana. Tukumbuke wapo wazee wengi wasioweza kumudu gharama kufika katika hospitali za wilaya na mikoa kupata matibabu wanayostahili. Ni bora tukatumia muda na posho ya Halmashauri kidogo kwa jambo hili, hakuna atakayekulalamikia hata kidogo. Na huo utaratibu ukishaanzishwa sasa uwe wa kudumu kila mwezi lazima mtaalamu aende kupiga kambi kwa siku tatu au nne. Napenda niamini tunaweza. Naomba Wizara ya Afya na TAMISEMI mshirikiane, ili tuone jambo hili ndani ya muda mfupi ujao linafanyika kwa mafanikio.

PENSHENI JAMII
Kuhusu pensheni jamii kwa wazee wote nataka niseme tu kwamba ni kweli mwaka jana wazee walituomba hili jambo tulilipokea lakini hatukuwa tumefanya utafiti wa namna yoyote. Baadaye tuliweza kufanya utafiti huo. Na ile ripoti sasa imetoka na tumeanza kujipanga. Jambo la msingi ni lazima tuhakikishe kwamba tutakapoanza kutoa pensheni jamii kwa wazee wote ni lazima tuhakikishe kwamba ni zoezi endelevu siyo unawaanzishia Wazee hawa kwa mwaka wa kwanza halafu mwaka wa pili unasema ngojeni kidogo. Lengo la serikali ni kwamba wakati muswada wa wazee ambao unafikishwa bungeni tuwe tumekamilisha mpango wa kutoa pensheni jamii kwa wazee wote, ili ndani ya
7

sheria itakayopitishwa iwe pia na mpango wa kutoa pensheni jamii kwa wazee, badala ya kwenda na maneno matupu hoo wazee tunawatambua, watu muhimu, tunajua ni dawa, nk. Lengo namba saba la milenia linahusu zaidi mazingira endelevu (sustainable environment). Na kwa mantiki yetu linahusu zaidi maji safi na salama kwa bibi na babu zetu. Lazima tuangalie hili suala la maji na tuhakikishe wazee wetu wanaweza kupata maji safi na salama wakati wote ili kuwaepusha na maradhi ambayo yatawaongezea matatizo makubwa ya kiafya. Ninaomba kuwashukuru kwa kutambua jitihada zilizofanywa na Serikali kuamua kusamehe kodi za majengo kwa wanamoishi Wazee zaidi ya miaka 60 ambayo siyo ya biashara. Tayari Serikali imefanya uamuzi kuhusu jambo hili. Naomba sasa TAMISEMI iweze kusimamia vizuri utekelezaji wake. Sheria iko wazi utaratibu wa kumtambua huyo mzee uko wazi, tatizo liko wapi? Wekeni mfumo na utaratibu mzuri kuwatambua hao Wazee ili utekelezaji wake uwe wa ufanisi.

MAUAJI YA WAZEE
Ndugu wananchi, Mauaji ya ‘Wazee vikongwe’ ni jambo la kusikitisha sana. Wakati tunahangaika na mauaji ya albino yaani walemavu wa ngozi, tulijaribu kufanya zoezi hilo sambamba na mauaji ya wazee akinababa na akinamama. Ukweli ni kwamba bado wanauawa sana ndiyo maana safari hii katika Mbio za Mwenge mwaka huu tukaamua katika kaulimbiu ya safari hii tukaongezea kuendelea kulaani ukatili wa mauaji ya walemavu wa ngozi na wazee. Hawa hawana dhambi hata kidogo, kasoro yao macho ni mekundu tu basi, huyu mwingine ngozi yake nyeupe anauawa kikatili. Hili si jambo jema, ni jambo la kijinga mbaya zaidi dhambi, kwa nini utoe roho ya mtu kwa sababu ya uzee au ulemavu wa ngozi? Anayeua lazima ajue atakuja kuwa mzee naye macho yatakuwa mekundu hivyo hivyo, ni jambo linakera sana. Tunamshukuru Mungu kwamba jitihada na kelele tulizozipiga tumeona dalili kidogo zimeanza kuonyesha kupungua kidogo kwa mauaji haya. Ndugu wananchi, tuendelee kulaani kila tunapopata mwanya, viongozi wa madhehebu ya dini wasiache kulisema hili kila wakipata nafasi na sisi viongozi wa kisiasa hasa kwenye mikoa ya Mwanza na Shinyanga lazima tuendelee kukemea suala hili. Na vilevile niwaombe sana Wazee na Watanzania wote kwa ujumla muendelee kutusaidia hasa katika kulea watoto wetu waweze kukua katika maadili mema. Lakini na hata sisi wazazi wenye nguvu zaidi ni lazima tujitajidi kuwalea watoto hawa vizuri kadri itakavyowezekana ili wasitumbukie katika uhalifu. Mwisho, nawaomba wazee muendelee kutusaidia hasa katika eneo la amani na utulivu. Ni kitu cha msingi sana msiruhusu hata kidogo, ukabila, udini, ubaguzi wa aina yoyote ukaanza kujitokeza na ninyi mpo. Ni jukumu lenu kutuelekeza na kushauri kuepukwa kwa mambo yote ambayo yataleta uvunjifu wa amani. Ninashukuru sana kwa kuadhimisha siku hii ya leo hapa Morogoro na niwaombe basi wale waliopewa heshima kuandaa sherehe hii mwakani wajiandae mapema ili iweze kuwa siku nzuri kama ilivyofanyika safari hii. Itakuwa ni vizuri kama tutajianda vema ili mikoa yote ipate kushiriki.

AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
8

Sign up to vote on this title
UsefulNot useful