You are on page 1of 27

HOTUBA YA MH.

JANUARY Y MAKAMBA YA
KUTANGAZA NIA YA KUOMBA RIDHAA YA CHAMA
CHA MAPINDUZI KUMTEUA KUGOMBEA URAIS
KATIKA UCHAGUZI MKUU 2015
Kama ilivyo ada, tunaanza kwa kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa baraka zake na kibali chake cha
kutukunanisha siku hii ya leo.
Nawashukuru
wote
mliofika
hapa
na
nyote
mnaonisikiliza kupitia luninga na redio. Nawashukuru
pia wana-CCM na Watanzania waliokusanyika katika
mikoa mbalimbali ambao wataunganishwa nasi moja
moja wakati wa kipindi cha maswali na majibu.
Nimeonelea nitumie siku na fursa hii kuwajulisha
kwamba, baada ya tafakuri ya kina ya changamoto za
sasa nchi yetu na mahitaji ya uongozi wa aina mpya,
nimeamua kuomba nafasi ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Kwa ajili hiyo, keshokutwa, nitasafiri kwenda Dodoma
kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya wana-CCM ili
niweze kuteuliwa na Chama chetu kuwa mgombea kwa
nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Nafanya hivyo nikitambua ukubwa na utakatifu wa
dhamana ninayoiomba.
Naiomba nafasi hii nikiwa nimejiridhisha bila shaka
yoyote kwamba ninao uwezo, ukomavu, uzalendo,
uadilifu, uzoefu, hekima, busara, maarifa na ubunifu wa
kuishika nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.

Naiomba nafasi hii nikielewa kiu ya Watanzania ya


kupata uongozi mpya, wa zama za sasa, unaotoa
matumiani mapya, yatakayozaa Tanzania mpya.
Naiomba nafasi hii nikiwa naelewa misingi iliyoijenga
nchi yetu misingi ya haki, umoja, amani, mshikamano
na upendo miongoni mwa Watanzania na haja ya
kuilinda misingi hiyo.
Nchi yetu iko katika njia panda. Katika miaka 10 ijayo,
Tanzania inaweza kuchukua njia mojawapo kati ya hizi
mbili: inaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo na
hali ya maisha ya wananchi wote kuboreka.
Lakini vilevile, ipo hatari ya taifa letu kupasuka
kutokana na dalili za mpasuko wa kidini, mmomonyoko
wa maadili kwenye jamii, kuporomoka kwa imani ya
wananchi kwa dola, dalili za ufa katika Muungano,
umaskini na tofauti kubwa ya kipato baina ya wananchi.
Aina ya uongozi tutakaouchagua mwaka huu ndio
utaamua mustakabali wa nchi yetu. Baada ya miaka 50
ya uongozi wa kizazi kilichopita, sasa ni wakati wa nchi
yetu kuongozwa na viongozi wa aina mpya, wenye
mtazamo mpya, fikra mpya, maarifa mapya na
majawabu mapya.
Ndugu zangu, Watanzania wenzangu,
Nimesimama hapa kuwahakikishia kwamba nimefanya tafakuri ya
kina na za muda mrefukuhusu mwelekeo wa nchi yetu. Na niko tayari
kutengeneza na kuongoza timu madhubuti ya Watanzania wazalendo
na waadilifu watakaounda Serikaliitakayojenga kesho njema.
Nimesimama hapa kuwakaribisha wana-CCM wenzanguna
Watanzania wote kwenye kampeni hii. Tunayo dhamira na uwezo wa
2

kushinda na kuongoza mabadiliko makubwa ambayo Watanzania


wanayatarajia.
Kwa mambo niliyoyaona na kujifunza kuanzia kufanya
kazi na Rais Kikwete Ikulu, kwenye uongozi wa Chama,
Bungeni na Serikalini, nimepata matayarisho ya
kutosha ya kuiongoza nchi yetu.
Naiomba nafasi hii nikiwa naijua vyema sana nchi yetu,
nikiwa nayajua kwa kina matatizo ya Watanzania katika
kila kona ya nchi yetu, na nikiwa nimejiridhisha
kwamba ninao ubunifu na maarifa ya kutosha ya
kutafuta majawabu mapya kwa ajili ya kuinua hali za
maisha za Watanzania.
Siko mbele yenu kuwasimulia kuhusu matatizo ya nchi
yetu ambayo sote tunayajua. Niko mbele yenu kuelezea
namna tukavyotatua matatizo ya nchi yetu. Katika
kuomba nafasi hii nimefikiria na nitaelezea baadhi ya
majawabu mapya ambayo yananitofuatisha mimi na
wengine wanaoomba nafasi hii.
Natambua kwamba nikiteuliwa na Chama changu,
nitakabidhiwa Ilani ya Uchaguzi itakayoelekeza mambo
ya kufanywa na Serikali ijayo. Nitainadi Ilani hiyo na
kuitekeleza kwa nguvu zangu zote.
Hata hivyo, kama wasemavyo waswahili, ziada njema
haigombi. Kuwepo kwa Ilani hakuzuii kuwa na mambo
ya ziada ya msingikwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Kwa msingi huo, nianze kwa kusema kwamba Serikali
nitakayounda itaendeshwa na falsafa ya uwezeshaji
mpana wa wananchi kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Kwa miaka mingi sasa, Watanzania wamepewa ahadi
nyingi na viongozi wa siasa. Badala ya kuwaahidi
3

wananchi kwamba tutawafanyia kila kitu, Serikali


nitakayoiunda itawajengea uwezo na nguvu ya
maamuzi kuhusu maisha yao. Serikali yangu itajikita
katika kuwajengea nguvu ya kiuchumi ya kuendesha
maisha yao, na kuamua waishi wapi, wapeleke watoto
shule wapi, waanzishe biashara gani, wajenge nyumba
za aina gani, wakatibiwe wapi.
Tutawajengea uwezo wa kuwa na sauti katika maamuzi
ya Serikali yao.Tutaondokana na dhana ya wananchi
kubaki watazamaji tu katika masuala ya nchi yao.
Sitaunda Serikali ya waporaji na wabinafsi. Nitaunda
Serikali yenye utu nainayowasikiliza na kuwajali watu.
Serikali inayotimiza wajibu wake bila chembe ya
uzembe wala ulegevu. Nitaunda Serikali yenye Mawaziri
wasiozidi 18 ambayo haitakuwa na mtu hata mmoja
anayetiliwa shaka kuhusu uwezo na uadilifu wake.
Serikali yetu itakuwa na vipaumbele vikubwa vitano:
Kwanza ni kukuza kipato cha watu. Msingi wa
maendeleo ya nchi yetu sio mapato ya Serikali, bali
ukubwa na uhakika wa kipato cha Watanzania. Kama
nilivyosema awali, nitataka Watanzania tuwe na nguvu
na uwezo wa kiuchumi wa kuendesha maisha yetu.
Kwahiyo, kwa wale wenye shughuli za kufanya iwe ni
kilimo, uvuvi, ufugaji au biashara tutaweka mazingira
ya kisera, kisheria na kikodi ili shughuli hizo zipanuke,
zishamiri, ziwe na faida kwao na ziwanufaishe katika
maisha yao.
Falsafa yetu ni kwamba mtu yoyote anayetoa jasho
kutengeneza maisha yake na ya familia yake, ni lazima
anufaike na juhudi na jasho lake. Kwa wale wasio na
shughuli za kipato, tutafanya jitihada zote ili wawe na
4

shughuli za kiuchumi za kufanya. Tutatengeneza fursa


za kiuchumi ili mtu yoyote kama hana shughuli ya
kufanya basi awe ameamua mwenyewe. Maendeleo ya
nchi yatapatikana kwa nguvu ya uchumi ya wananchi,
sio kwa hisani ya wafadhili.
Kipaumbele cha pili kitakuwa ni kupatikana kwa
huduma bora za jamii na kiuchumi. Kazi kubwa
imefanywa na viongozi waliotangulia, lakini bado
Watanzania wengi wanahitaji kupata huduma ya
uhakika ya maji, afya, elimu bora, barabara za uhakika,
umeme, huduma za fedha na mawasiliano. Tutabuni
mbinu mpya za kumaliza matatizo haya.
Kipaumbele cha tatu ni utawala bora, wa haki na wa
sheria. Msingi wa amani ya nchi yetu ni haki. Wananchi
wengi hawana uhakika wa kupata haki zao waendapo
polisi au mahakamani. Serikali yangu italibadilisha hili.
Tutazijenga upya taasisi ya usimamizi wa utawala na
haki za watu, zikiwemo mahakama na jeshi la polisi.
Hatutakubali Mtanzania yoyote aonewe na watu au
mamlaka za umma. Lakini pia tutataka kila mtu afuate
sheria za nchi, hata ziwe ndogo kiasi gani.
Tutakabiliana na tatizo la ubadhirifu wa mali ya umma
kwa nguvu zote. Nampongeza Rais Kikwetekwa kufanya
jambo la kimapinduzi la kuelekeza Ripoti za Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ziwekwe
hadharani na kujadiliwa.
Serikali yangu itaenda mbele zaidi na kuhakikisha
kwamba ripoti ya CAG ikitolewa, viongozi ambao taasisi
zao zimekutwa na makosa wanakaa pembeni siku hiyo
hiyo na hatua za kisheria, za kipolisi, za kimahakama
zinaanza siku inayofuatia.
5

Kipaumbele cha nne ni usimamizi wa uchumi.Serikali


yangu taimarisha uwezo wa taasisi za usimamizi wa
uchumi ikiwemo Wizara ya Fedha, Tume ya Mipango,
Benki Kuu na Mamlaka ya Mapato. Nitazipa mamlaka na
rasilimali-watu ili ziweze kudhibiti mfumuko wa bei,
kuporomoka kwa thamani ya shilingi, nakisi ya bajeti,
kupungua kwa hifadhi ya fedha za kigeni, kukua kwa
deni la taifa na kusimamia uwekezaji wa kimkakati wa
sekta binafsi.
Kama ambavyo tuna Baraza la Usalama wa Taifa sasa,
nitaunda Baraza la Uchumi la Taifa litakalojumuisha
wataalam kutoka katika taasisi za umma za usimamizi
wa uchumi, wagwiji wa uchumi kwenye nchi yetu,
pamoja na wawakilishi wa sekta binafsi.
Baraza hili litakuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba
uchumi wetu unawekewa mikakati ya muda mrefu na
wakati wote hali ya uchumi wetu inaratibiwa kwa
weledi na changamoto zinazojitokeza zinarekebishwa
haraka.
Kipaumbele cha tano ni amani, umoja na usalama wa
mali na maisha ya Watanzania. Amani na umoja wa
nchi yetu ni tunu na urithi tulioachiwa na waasisi wa
nchi yetu. Marais wote waliopitawamefanya kazi kubwa
ya kuzilinda tunu hizi. Serikali yangu haitakubali urithi
huu upotee. Tutafanya jitihada zote ili kujenga
maridhiano mapya na upendo miongoni mwa makundi
mbalimbali katika jamii yetu. Nitawahusisha viongozi
wa dini zote katika hili. Nitaanzisha Jukwaa la Rais na
Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Jumuiya ya
Wakristo Tanzania (CCT) na Baraza la Waislam Tanzania
(BAKWATA) litakalokutana kila miezi miwili kujadili na
kupanga mikakati ya kuendeleza amani, umoja, upendo
na maadili ya jamii.
6

Pia tutachukua hatua mpya za kuimarisha Muungano


wetu na kuupatia uhalali mpya na wa ziada miongoni
mwa Watanzania.
Ndugu Watanzania wenzangu,
Naomba sasa nifafanue majawabu mapya ambayo
Serikali yangu itayatekeleza kwa changamoto mahsusi:
Naomba nianze na suala la ajira. Kwasasa, wapo zaidi
ya Watanzania milioni 23 kwenye soko la ajira leo hii.
Kila mwaka wanaongezeka vijana zaidi ya laki
tisakwenye soko la ajira.
Hawa ni watu wengi sana. Viongozi wengi wa siasa
wameliita tatizo la ajira kuwa ni bomu. Lakini kulielezea
tatizo sio kulitatua.
Serikali yangu itafanya nini?
Watanzania wengi wanajishughulisha na biashara
ndogo na za kati. Karibu zotezinaajiri mtu mmoja au
wawilina nyingi zinasuasua.Watalaamu wanatuambia,
asilimia 20 tu ya biashara na kampuni ndogo nchini
zikiongeza mfanyakazi mmoja kwa mwaka, ajira
400,000 za kudumu zitazalishwa kwa mwaka. Je
asilimia 80 za biashara hizi zikiongeza watu wawili
wawili tu kwa mwaka? Tutakuwa tumepunguza sana
kama sio kumaliza tatizo la ajira.
Kwahiyo, jawabu letu la kwanza litakuwa ni maendeleo
ya biashara ndogo na za kati. Zilizopo zifanye vizuri na
kuongeza waajiriwa na wale wanaotaka kuanzisha
biashara, iwe rahisi kufanya hivyo.
Ziko namna kadhaa za kufanya hivi. Kwa mfano, katika
nchi yetu, Serikali bado ndio mnunuzi mkuu. KIla siku,
7

Serikali yetu inanunua bidhaa nyingi - kuanzia kuni,


karatasi, matofali, mabati, vyakula na huduma nyingine
nyingi. Katika kuzijengea uwezo kampuni ndogo na za
kati, Serikali yangu itaweka Sheria ya kuwezesha
asilimia 30 ya thamani ya manunuzi ya umma kupewa
makampuni madogo na ya kati yatakayokidhi vigezo
rahisi yanayomilikiwa na vijana na wanawake. Jambo
hili litawezesha biashara nyingi ndogo kujenga uwezo,
kupanuka na kuajiri watu wengi zaidi.
Lakini, ili hili litokee, lazima tuwe na taasisi madhubuti
ambayo itashughulika na ustawi wa biashara na
makampuni madogo na ya kati.
Kwahiyo, nitaanzisha Mamlaka mahsusi ya Maendeleo
ya Biashara Ndogo na za Kati. Pamoja na mambo
mengine, Mamlaka hii itapewa majukumu ya
kuwezesha, kurahisisha na kusimamia biashara ndogo
kuanzishwa kwa urahisi, kuendeshwa bila bughudha, na
kupata fursa ya kukua.
Ndugu Wananchi,
Viwanda bado ni tegemeo kubwa la ajira. Kwa
viwanda vikubwa vilivyopo sasa, tutaweka motisha ya
kikodi kwa yoyote ambaye ataweza kuongeza ajira
mpya angalau500 au zaidi za kudumu kwa mwaka.
Haipaswi kumgharimu kikodi mtu mwenye biashara
kuongeza wafanyakazi.
Kwa waajiri ambao nibiashara au kampuni mpya ndogo
na za kati, yaani SMEs, Serikali yangu itatoa motisha ya
kupunguziwa kodi hizi kwa kila kazi mpya tano au zaidi
kwa mwaka. Ukweli hapa ni kwamba kunawiri kwa
uchumi hakutokani na kodi inayokusanywa na Serikali
bali kunatokana na kipato na uwezo wa manunuzi
8

walionao wananchi na kipato cha wafanyabiashara


kuweza kukuza biashara zao na kutoa ajira nyingi zaidi.
Vilevile,
katika
kukabiliana
na
tatizo
hili
la
ajira,tutawezesha sekta binafsi kujenga na kufufua
viwanda vya nguo, katani na korosho nchini. Huko
nyuma tulishawahi kuwa na viwanda vingi vya aina hii,
vikichangia asilimia 25 ya pato la Taifa na kuajiri
asilimia 25 ya wafanyakazi wote nchini. Kwa sasa, ni
asilimia 30 tu ya pamba yetu ndio inayotumika nchini.
Pamba tunayo ya kutosha kukidhi mahitaji ya viwanda
vikubwa zaidi ya hamsini. Ndani ya miaka mitano ijayo
tutahakikisha tunajenga na kufufua viwanda 11 vya
nguo vitakavyotoa ajira mpya zaidi 100,000
viwandani tu, huku asilimia zaidi ya 80 ya wafanyakazi
hawa wakiwa ni wanawake. Lengo ni sekta nzima ya
pamba kuajiri walau asilimia 10 ya nguvu kazi (kazi
milioni 2.5).
Katika kuwezesha hili, Serikali nitakayoiongoza
itachukua hatua za muda mfupi za kikodi na kiushuru ili
kuwezesha viwanda hivi kukabiliana na ushindani wa
kanga, vitenge, mitumba na vitambaa kutoka nje ya
nchi.
Ndugu wananchi,
Shughuli za ujenzi wa nyumba na miundombinu
huongeza chachu katika uchumi na kuongeza ajira
nyingi sana. Tuna mahitaji makubwa ya nyumba na
tuna mahitaji makubwa ya ajira. Nitahakikisha
tunatengeneza mazingira mazuri ya uanzishwaji na
uimarishaji wa makampuni madogo na ya kati
yanayojihusisha na biashara katika sekta ya nyumba.
Tutahakikisha kwamba, ndani ya miaka kumi ya uongozi
wangu, sekta ya ujenzi inachangia zaidi ya asilimia 25
ya Pato la Taifa na kuajiri zaidi za watanzania milioni 5.
Hii itawezekana kwa kupunguza gharama za ujenzi. Na
9

hili litawezekana kwa uwekezaji kwenye viwanda vya


vifaa ya ujenzi, kama vile viwanda vya nondo, mabati,
simenti, vigae na vioo.
Hii itaenda pamoja naujenzi wa miundombinu mikubwa,
hasa ya usafirishaji. Tutaweka jitihada za makusudi
kuongeza kasi na ukubwa wa miradi ya miundombinu
nchini ambayo itaajiri watanzania wengi zaidi na
kuingiza fedha nyingi zaidi kwenye mzunguko wa
uchumi. Tutahakikisha kwamba wakandarasiwa miradi
hii ni makampuni ya ndani yatakayohifadhi na
kuwekeza fedha hizo hapa ndani. Lengo langu ni
kuwezesha wakandarasi wa ndani kiufundi, kiutawala
na kifedha na kuwawezesha kupata walau asilimia 80
ya miradi yote ya miundombinu inayojengwa kwa fedha
za umma ndani ya miaka kumi ijayo.
Shughuli za sanaa na michezo zikisimamiwa vizuri zina
uwezo wa kuajiri asilimia kubwa ya watanzania.
Mapema kabisa kwenye serikali yetu tutarasimisha
shughuli za sanaa ikiwemo sinema, muziki na kazi zote
za ubunifu. Tutatunga Sheria kali zaidi kulinda
hakimiliki. Kupitia Mfuko wa Sanaa wa Taifa
tutakaouunda upya, tutatoaruzuku na mikopo ya
masharti nafuu kwa wazalishaji, waendeshaji na
wasanii wenyewe kwenye kuendeleza ubunifu na
kuzalisha, kutangaza na kuuza kazi mpya kwa njia za
kisasa. Tukiweza kuongeza maradufu uwekezaji kwenye
tasnia ya sanaa na ubunifu hapa nchini, tutatengeneza
ajira mpya zaidi ya milioni mbili.
Sita, kwa vijana wasomi na wanataaluma ambao
hawatakuwa wamebahatika kupata ajira katika sekta
rasmi, tutawawekea utaratibu wajiunge na kuanzisha
makampuni na biashara za kitaaluma wahandisi,
wanasheria, wasomi katika fani za siasa na utawala, na
10

wengineo na tutawapa mikopo maalum ya kufanya


hivyo.
Kwa upande wa wamachinga, naelewa kwamba
wanazunguka kutwa nzima wakiuza bidhaa ambazo
hawazimiliki na huishia kupata pesa ya kula tu au nauli
au hawapati kitu kabisa.
Viongozi nitakaowateua
kuongoza Mamlaka mpya ya Biashara Ndogo na Za Kati
katika mwaka wao wa kwanza watapimwa kwa uwezo
wao wa kuhakikisha wamachinga wana sehemu salama
na zenye wateja za kufanyia shughuli zao na hawaishii
kuwa fremu tu barabarani kwa mali za watu wengine.
Jambo jingine kubwa tutakalofanya ni kutoa shilingi
milioni 50 kwa kila kijiji hapa nchini katika miaka
mitano kwa ajili ya wanavijiji kukopeshana kwa ajili ya
shughuli za uzalishaji mali. Mfuko huu utaendeshwa na
Kamati maalum zitakazoundwa na wanavijiji wenyewe
na wao ndio watakaomua nani akopeshwe na arudishe
baada ya muda gani. Mzunguko wa shilingi milioni 50
kwenye shughuli za uzalishaji mali kijijini utatoa chachu
ya maendeleo ya watu. Fedha zinazohitajika hazifiki
bilioni 700 katika miaka mitano. Kwa sasa tunakusanya
zaidi ya bilioni 800 kwa mwezi. Fedha hizi tutazipata na
nitaelezea ni. Utaratibu wa aina hii umebadilisha
maisha ya wananchi wa vijijini huko nchini Thailand.
Kilimo bado ndio nguzo ya ajira kwa Watanzania
wengi. Mambo mengi yamezungumzwa kuhusu
mapinduzi ya kilimokwa miaka mingi. Kila zao
linalolimwa nchini iwe ni pamba, korosho, chai,
kahawa, tumbaku, mkonge, au mboga na
matunda lina changamoto zake mahsusi.
Serikali
yangu
itabadilisha
namna
ya
kushughulikia maendeleo ya kilimo kwa kuweka
mkakati ya zao moja moja tofauti na ilivyo sasa
ambapo kuna mikakati ya jumla ya kilimo.
Tutabadilisha utaratibu wa sasa wa upatikanaji
11

wa pembejeo ambapo pesa nyingi zinapotea kwa


watu wa kati huku wakulima wakiwa hawapati
pembejeo za kutosha, kwa wakati na kwa bei
wanayoimudu.
Tutaweka
mkazo
kwenye
kurekebisha mfumo wa ununuzi wa mazao ambao
kwasasa unamkandamiza mkulima. Tutaanzisha
Soko Kuu la Kitaifa la Mazao, yaani Commodities
Exchange, litakalowezesha wakulima kuwa na
nguvu ya kujua na kuamua bei na wakati wa
kuuza mazao yao.
Kwenye uvuvi na ufugaji, mipango iliyopo
inatosheleza. Tutakachokifanya na kuitekeleza
kwa haraka na uhakika. Kwa maeneo ya uvuvi,
tutaanzisha mifuko ya kuwawezesha wavuvi
kukopeshwa nyavu, boti na mashine na majokofu
ili waweze kwenda mbali majini na kuhifadhi
samaki kwa muda mrefu ili wapate soko zuri na
bei nzuri. Hatutaacha wafugaji wakose malisho
ya mifugo yao. Kila mfugaji atamilikishwa eneo
ya malisho na kupewa hati. Hii itasaidia kumaliza
migogoro kati yao na wakulima.
Ndugu wananchi,
Jambo jingine ambalo ningependa kuliongelea ni suala
la elimu. Ni lazima kukiri kwamba, pamoja na
changamoto
zilizopo,
mafanikio
makubwa
yamepatikana kwenye Serikali ya Rais Kikwete kwenye
nyanja ya elimu, hasa kwenye udahili wa wanafunzi
kwa ngazi zote. Pamoja na mafanikio haya,
changamoto za elimu zipo lukuki na ndugu zangu
Watanzania mnazijua. Sasa nini kifanyike kuboresha
elimu? Katika serikali yetu, tutatekeleza yafuatayo.
Kwanza, Serikali yangu itaondoa shaka na kumaliza
kabisa mjadala kuhusu dira ya elimu yetu. Tutaongozwa
na dira ya elimu inayochochea vijana kujiajiri,
12

inayochochea
udadisi,
inayochochea
ubunifu,
inayochochea uthubutu, nidhamu, weledi na uzalendo.
Tutatengeneza mitaala mipya na thabiti kabisa
inayokidhi mahitaji ya mazingira na changamoto za
sasa na mahitaji ya uchumi wa kisasa, mahitaji ya jamii
na mahitaji ya taifa kwa ujumla. Hiyo ndio itakuwa
mihimili ya elimu tutakayowafundisha watoto wetu
chini ya uongozi wangu.
Tutawafundisha watoto wetu kwa lugha zote mbili, ya
Kiswahili
na
Kiingereza
kwasababu
ni
jambo
linalowezekana.
Rais Kikwete amefanya kazi kubwa katika kukabiliana
na tatizo la uhaba wa walimu. Bado changamoto ipo
kwenye walimu wa sayansi na hisabati. Tutaongeza
udahili kwenye vyuo vya ualimu vinavyofundisha
masomo
hayoili
kupata
walimu
wengi
zaidi.
Kama saikolojia ya mwalimu haijakaa sawa kutokana na
changamoto nyingi, tusahau kuhusu ubora wa elimu.
Tunasema ualimu ni wito lakini haipaswi kuwa adhabu.
Tutazitatua changamoto za walimu, ikiwemo mazingira
yao ya kazi, motisha na hamasa yao ya kufundisha
ikiwemo mishahara yao, kupandishwa madaraja,
mafunzo yao ya ziada ya kujiendeleza.
Tutaweka vipimo vipya ya maendeleo ya elimu nchini
kwa kupima uelewa na maarifa ya wanafunzi kwa
mambo wanayopaswa kuyajua katika ngazi husika ya
elimu. Hatutaishia tu kusheherekea ufaulu wa jumla
katika mitihani ya mwisho. Pia, tutaweka mfumo wa
motisha ya malipo au kupandishwa vyeo kwa walimu
wetu wa shule za Serikali wanaofanya vizuri
Vilevile, hatutaingiza siasa kwenye maendeleo ya
elimu. Tutaweka uongozi thabiti na wa kizalendo
13

kwenye sekta ya elimu utakaokabiliana na


changamoto za uendeshaji na utawala wa sekta ya
elimu, ikiwemo masuala ya ukaguzi, usimamizi wa
walimu, uidhinishaji na usambazaji vitabu kwenye
mashule, upelekaji na matumizi ya fedha za uendeshaji
wa shule na mambo mengineyo.
Ili kuchukua vijana wengi wanaoishia darasa la saba na
kidato cha nne, tutajenga Chuo kikubwa cha ufundi
kwenye kila Wilaya ya nchi yetu kwa kushirikiana na
sekta binafsi.
Kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Serikali
yangu itabadilisha utaratibu na kuweka utaratibu mpya,
wa wazi na wa haki ili kila anayestahili mkopo apate na
apate kwa kiwango kinachotosheleza. Tutaanzisha
Mfuko Maalum, yaani National Education Endowment
Fund, kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu kwa wenye
mahitaji maalum. Serikali pia itaweka dhamana ya
mikopo wanafunzi katika taasisi binafsi zitakazokuwa
tayari kukopesha wanafunzi. Zaidi ya hapo, tutaanza
utaratibu wa kuviwezesha vyuo na taasisi za elimu ya
juu viwe na mifuko kwa ajili ya kutoa mikopo na
misaada kwa wanafunzi.
Jambo jingine kubwa ambalo ningependa kulizungumzia
ni tatizo la rushwa. Limezungumzwa na wengi. Lakini
kulizungumzia na kulipigia kelele suala la rushwa pekee
hakulimalizi. Ziko namna mbili tutakazozitumia
kukabiliana na hili tatizo: njia ya kwanza ni kisheria,
kimfumo na kitaasisi; njia ya pili ni kijamii.
Kuhusu kimfumo, nitafanya mabadiliko makubwa
mawili. Kwanza, ni kuiwezesha TAKUKURU kuwa na
mamlaka kisheria ya kuwashitaki watuhumiwa wa
rushwa moja kwa moja mahakamani. Pia, tuanzishe
Mahakama Maalum ya Uhujumu Uchumi ambayo
14

itahusika na makosa ya rushwa; ubadhirifu wa mali ya


umma; ukwepaji kodi; kuiba, kunufaika au kutaka kuiba
au kutaka kunufaika na mali ya umma; na makosa
mengine ya aina hii.
Mahakama ambayo itakuwa na jopo maalum la majaji
ambalo litafanya kazi mwaka mzima na kusikiliza na
kuhukumu kesi hizi haraka. Kesi za uhujumu uchumi
ziendeshwe wazi na mfululizo na adhabu ziwe kali sana,
kwa mfano ya kifungo cha maisha. Pia tutaanzisha
Kurugenzi ya Uchunguzi na Mashtaka ya Uhujumu
Uchumi. Tutaiwezesha Mahakama hii na Kurugenzi hii
bila ukomo wa kirasilimali kuifanya kazi hii vizuri.
Kuhusu kijamii, kwa kushirikiana na viongozi wa dini
na wengine wa kijamii, nitaanzisha na kuwezesha
mjadala mpana kwenye jamii yetu kuhusu maadili ya
jamii. Jamii yetu ijengwe kwenye misingi ya kuchukia
rushwa, ulaghai na njia za mkato za kupata mali.
Inapofika mahala jamii inasheherekea mali ambazo
hazina maelezo, inapofika mahali ambapo jamii
inawatukuza wachache ambao wametumia ujanja
kufanikiwa, inapofika mahala ambapo jamii inakuita
mjinga unapostaafu ukiwa hujilimbikizia mali, hapo lipo
tatizo ndani ya jamii. Lazima kujenga jamii tofauti,
ambayo wala rushwa wanajiona kama wanatembea
uchi, jamii ambayo inatoa adhabu za kijamii, yaani
social sanctions, ikiwemo kutengwa, ambazo ni kali
kuliko adhabu za kisheria. Mwalimu Nyerere alijaribu
kujenga jamii ya aina hii: jamii ambayo kiongozi wa
umma hapaswi kungoja mahakama itamke kwamba ni
mla rushwa. Tunapaswa kuendelea kujenga jamii ya
aina hii. Viongozi wa dini wana nafasi kubwa. Maadili na
malezi na makuzi kwenye familia pia yana nafasi yake.
Ndugu zangu Watanzania, bila kudhibiti rushwa na wizi
hatuwezi kupata maendeleo. Kwa hiyo, kwa kiongozi
15

yoyote, kama anataka kuacha rekodi nzuri ya


maendeleo, kuitokomeza rushwa ni jambo la kufa na
kupona.
Katika uchaguzi huu, tunayo fursa ya kuanza safari ya
kumaliza tatizo hili. Rekodi ya uadilifu sio sifa pekee ya
uongozi. Lakini pia sio jambo la kupuuzwa hata kidogo.
Namna viongozi wanavyotafuta uongozi ndio namna
watakavyotawala. Tunayo fursa ya kuchagua viongozi
ambao hawatapata kigugumizi kupambana na rushwa.
Tunayo fursa ya kuchagua viongozi ambao hawatakuwa
na madeni ya kulipa. Sina shaka kabisa kwambamimi ni
kiongozi wa aina hiyo.
Ndugu wananchi,
Napenda pia kuzungumzia suala la ardhi. Hili pia ni
muhimu kwasababu mbili: kwanza, ardhi, kwa maana ya
umiliki na matumizi yake, ndio msingi wa yote; na pili, zimeanza
kuonekana dalili ya watu wachache kuhodhi ardhi kubwa na kuanza
kuirudisha nchi yetu kwenye zama za ukabaila. Hakuna maendeleo
ya kilimo kama hakuna uhakika wa matumizi bora ya ardhi na kama
hakuna uhakika wa mfumo wa umiliki wa ardhi.
Lazima sasa kuondoa migogoro ya ardhi isiyoisha kati ya
wakulima, wafugaji, wawekezaji na Serikali na kuipa
ardhi thamani halisi inayostahili. Kama tunavyobainisha
kisheria na kulinda hifadhi za misitu na mbuga za
wanyama lazima maeneo ya kilimo na mifugo na
makazi ya watu nayo yawe hivyo. Lazima wakulima
wamiliki ardhi yao kisheria. Lazima kutenga maeneo
maalumu ya wafugaji yanayomilikiwa na wafugaji
kisheria na bila kusahau korido mahususi za kupitisha
mifugo kutoka upande mmoja wa nchi mpaka
mwingine.

16

Serikali yetu itatumia teknolojia mpya ya satellite


katika kupima na kupanga matumizi ya ardhi nchini.
Tutajenga kituo cha kupokea picha za satellite ambacho
kitawezesha kila kipande cha ardhi katika nchi yetu
kupimwa, na hati ya umiliki, yenye picha na mipaka
isiyo na shaka, kutolewa na matumizi ya ardhi
hiyokujulikana.Kituo hiki hakigharimu fedha ambazo
tunazishindwa.
Kuhusu huduma ya afya, Watanzania wengi, hasa wa
vijijini, bado wana changamoto kubwa kuipata. Kazi
nzuri imefanywa na Serikali ya Rais Kikwete kusogeza
huduma hii karibu na wananchi na kuiboresha. Kazi
hiyo tutaiendeleza. Tutaitazama huduma ya afya
kimfumo zaidi na kurekebisha uendeshaji wake.
Lakini kubwa tutakalofanya ni kuhakikisha kwamba kila
Mtanzania ana bima ya afya na anapata matibabu bila
kujali uwezo wa kipato chake. Moja ya namna ya
kufanya hili ni kutengeneza Sheria mpya ya
kuiunganisha mifuko yote ya Bima na kurahisisha
ukusanyaji na matumizi ya pesa kwenye vituo vya afya
ya msingi. Nchi nyingine za Afrika wamefanya hivi na
kufanikiwa. Na sisi hatuwezi kushindwa. Tutaondoa
ukiritimba na urasimu wa Bohari ya Madawa ya Taifa
katika kusambaza madawa katika vituo vya huduma
vya Serikali.
Kwa wananchi wa Tanzania, ukiwauliza leo ni huduma
ipi ya jamii bado ni kero kubwa. Jibu litakuwa ni huduma
ya maji. Watanzania wanaopata huduma hii hawafiki
asilimia 60. Maeneo ya vijijini hali ni mbaya zaidi. Ni
jambo la kawaida kwa kina mama vijijini kutumia siku
nzima na kwenda umbali mrefu kupata nusu ndoo kwa
familia nzima. Tatizo kubwa ni uwekezaji mdogo katika
sekta ya maji. Ili kukabiliana na tatizo hili, tutaanzisha
Mfuko wa Maji Vijijini pamoja na Wakala wa Maji Vijijini.
17

Tumeona jinsi Mfuko wa Barabara na Wakala wa


Barabara wa Taifa unavyofanya kazi nzuri kwenye
ujenzi wa barabara. Tumeona jinsi ambavyo Mfuko wa
Umeme Vijijini na Wakala wa Umeme Vijijini ulivyofanya
kazi nzuri kusambaza umeme vijijini. Tumeweza
kufanya kazi nzuri ya barabara na umeme kwa kutumia
fedha zetu wenyewe.
Utaratibu mpya na msukumo mpya wa kupeleka maji
vijijini utasaidia. Chanzo cha fedha kwa Mfuko wa Maji
kinaweza kuwa tozo maalum ndogo kwenye matumizi
ya maji mijini na maji ya kunywa kwenye chupa. Nina
uhakika kabisa kuwa ndani ya miaka kumi tunaweza
kusogeza maji safi, salama na ya uhakika karibu kabisa
na kaya zote nchini kote.
Nataka sasa niongelee kuhusu miundombinu. Suala hili
lazima tulipe umuhimu wa kipekee. Uchumi wa nchi
unaendeshwa na miundombinu ya usafirishaji. Rais
Kikwete amefanya kazi kubwa, hasa kwenye
miundombinu ya barabara. Na naamini kwamba kabla
hajamaliza muda wake ataweka jiwe la msingi la ujenzi
wa reli ya kati. Kazi hii nzuri tutaiendeleza lakini
tutaifanya kwa kazi zaidi na maarifa mapya. Barabara
ambazo hazijaisha tutazimalizia na tutaanza nyingine
mpya. Tutahusisha sekta binafsi katika ujenzi wa reli za
kutoka Mtwara hadi Mchuchuma hadi Mbamba Bay. Pia
tutafufua reli ya Tanga hadi Arusha na kuisogeza hadi
Musoma.Bandari ya Mtwara itakuwa bandari kubwa ya
uchumi wa gesi na chuma kutoka Liganga na makaa ya
m awe kutoka Mchuchuma.Nimebahatika kufika kwenye
bandari za Kemondo Bay, Mwanza, Nansio na Musoma
kwenye Ziwa Victoria; bandari za Kigoma na Kasanga
kwenye Ziwa Tanganyika; na bandari za Itungi, Manda,
Liuli na Mbamba Bay kwenye Ziwa Nyasa. Hizo zote ni
bandari za uchumi na zinahitaji matengenezo mapya
makubwa. Kazi hii tutaifanya. Bandari ya Mwambani
18

ambayo imeahidiwa kwa miaka mingi nayo tutaanza


kuijenga kwa kushirikisha sekta binafsi.
Ndugu wananchi,
Nimezungumzia mambo mengi na mabadiliko makubwa
ambayo tutayatekeleza. Ni dhahiri kwamba baadhi ya
haya mambo yatahitaji rasilimali-fedha za Serikali
kuyafanya. Kwa hakika hatuwezi kufanya mambo yote
haya bila uwezo wa Serikali kuongezeka na uchumi
kupanuka.
Kiongozi makini hawezi kuzungumzia mambo yote haya
bila kuzungumzia rasilimali za kuyatekeleza.Tofauti na
wenzangu, nataka niwahakikishie kwamba ninazo fikra
za namna ya kupata fedha za kufanya yote
niliyoyazungumzia.
Kwanza, tutaihusisha sekta binafsi kwa kina zaidi
kutekeleza ile miradi ambayo ni ya kimaendeleo lakini
pia ni ya kibiashara ambapo Serikali haina ulazima
kutumia fedha zake.
Kwa upande wa uwezo wa Serikali, nimefanya utafiti wa
kina kupitia taarifa za Serikali, ripoti za Bunge na sekta
binafsi kuhusu kuongeza uwezo wa Serikali kutimiza
majukumu
niliyoyaainisha.
Serikali
nitakayounda
itafanya
yafuatayo:(napenda
kwa
wale
wenye
calculator kwenye simu zao tupige hesabu kwa pamoja
hapa)
Kwanza, bila kusita wala kuchelewa, nitapunguza
misamaha ya kodi na kufikia kiwango cha asilimia 1 ya
Pato la Taifa. Hatua hii itaiwezesha Serikali kupata zaidi
ya shilingi bilioni 780kwa mwaka.

19

Ili kuwaingiza walipa kodi wengi wapya, hasa kutoka


sekta isiyo rasmi, Serikali yangu itapunguza kiwango
cha mapato kwa mwaka kwa walipa kodi wadogo
wanaolipa kodi kwa mtindo wa ukadiriaji. Hakuna
mfanyabiashara
atakayetozwa
kodi
kabla
hajatengeneza faida. Lakini pia tutaweka adhabu
kubwakwa wataoshindwa kulipa kodi. Tutakamilisha
vitambulisho vya taifana anuani za makazi ili kuweza
kuwatambua watu wote wanaofanya biashara na
kuwatoza kodi. Hatua hizi itawezesha Serikali kupata
fedha za ziada zaidi ya shilingi bilioni 860kwa mwaka.
Tutaongeza ufanisi wa Mamlaka ya Kodi Tanzania. Kwa
mujibu wa taarifa za Kamati ya Spika Kuhusu Mapato na
Matumizi Serikalini, TRA ikiongeza ufanisi kwa asilimia
10 tu, Serikali itapata mapato ya ziada ya shilingi bilioni
620 kwa mwaka. Kazi hiyo tutaifanya kwani sio ngumu.
Na fedha hizo tutazipata.
Tutakapokamilisha mradi mkubwa wa kufua chuma wa
Liganga, ifikapo mwaka 2020, Serikali itapata mapato
ya shilingi bilioni 960. Tutakapokamilisha mradi wa
makaa ya mawe Mchuchuma, Serikali itaweza kupata
zaidi ya shilingi bilioni 800.
Tutahakikisha kwamba ardhi yote inapimwa na kila
mwenye ardhi anayo hati na anatozwa kodi stahiki.
Hatua hii itaiwezesha Serikali kupata zaidi ya shilingi
bilioni 520.
Tukiwekeza kiasi kidogo cha fedha kwenye sekta ya
nyuki na kudhibiti uvunaji na biashara haramu ya
rasilimali za misitu, tutaweza kupata fedha za ziada
zaidi ya shilingi bilioni 130.
Meli nyingi za kigeni zinavua samaki katika eneo letu
bila kutozwa mrahaba, wala kukaguliwa, wala kutozwa
20

faini. Tutarekebisha Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu na


kuimarisha Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ili
kuwezesha haya kufanyika. Hatua hii itaipatia Serikali
mapato ya ziada ya zaidi ya shilingi bilioni 350.
Tutadhibiti biashara ya madini ya vito na kuiwezesha
Mamlaka ya Mapato Tanzania kufanya kazi kwa pamoja
na urahisi na Mamlaka ya Ukaguzi wa Madini ili kuhakiki
taarifa za mapato ya madini. Hatua hii itaiongezea
Serikali mapato ya ziada ya zaidi ya shilingi bilioni 520.
Tutadhibiti uvujaji wa mapato yanayokusanywa katika
ngazi za Halmashauri. Hatua hii itaweza kutupatia
kipato cha zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa mwaka.
Sekta ya utalii kwa sasa inatuingizia shilingi karibu
trilioni 3 kwa mwaka. Kwa mujibu wa taarifa ya kina ya
Benki ya Dunia, ndani ya miaka kumi, sekta hii inaweza
kuingiza shilingi trilioni 30 kwa mwaka. Ili tuzipate
fedha hizo tunapaswa kufanya mambo manne yaliyo
ndani ya uwezo wetu. Kwanza, kufungua, kuwekeza na
kutangaza ukanda wa utalii wa kusini mwa Tanzania;
pili, kuongeza aina na idadi ya watalii wanaotembelea
Tanzania na kuainisha vivutio vipya na mbadala na
kuvitangaza. Tatu, kudhibiti mfumo wa kukusanya
mapato ya utalii, ambayo mengi yanapotelea kwa
wajanja wachache nchi au yanalipwa nje ya nchi kwa
makampuni ya kitalii ya nje. Mambo haya tunayaweza,
na tutayafanya ili tufikie lengo la mapato ya shilingi
trilioni 30 kwa mwaka ili tuweze kufanya kazi kubwa
tulizozianisha.
Pia, serikali ina mali na hisa kwenye biashara
mbalimbali ambazo thamani yake ni zaidi ya shilingi
trilioni 10. Tutaweka utaratibu mzuri zaidi kwa kufanya
mabadiliko makubwa kwenye ofisi ya Msajili wa Hazina
ili tunufaike na mali na hisa hizi. Pia, ndani ya miaka
21

mitano,
kwa
hatua
mbalimbali,
tutayaingiza
makampuni makuu manne ya Serikali kwenye masoko
ya hisa Shirika la Nyumba la Taifa, Shirika la Petroli
Tanzania, Shirika la Reli la Taifa, Kampuni ya Simu ya
Taifa na Shirika la Bandari Tanzania. Hatua hii
itawezesha Watanzania kumiliki sehemu muhimu ya
uchumi wa nchi lakini pia kupatikana mapato.
Ndugu Watanzania wenzangu,
Naweza kuendelea kuelezea ni kwa namna gani Serikali
nitakayoiongoza itaweza kuongeza uwezo wake wa
kutimiza majukumu niliyoyaainisha.Hapa bado sijagusia
hatua za kubana matumizi ya Serikali ambazo pia fikra
zake tunazo.
Tofauti na baadhi ya wenzangu waliotangulia
kuzungumza, sijazungumzia mapato ya gesi kwa
makusudi kwasababu ukweli ni kwamba Rais wa
awamu ijayo, hata akiwa madarakani kwa miaka kumi,
bado nchi yetu itakuwa haijaanza kupata fedha
kutokana na gesi. Hata hivyo, ni muhimu kuendelea na
maandalizi ya nchi yetu kunufaika na uchumi wa gesi.
Na pia, tofauti na wenzangu, sijazungumzia kukopa au
misaada ya wahisani kwa ajili ya maendeleo yetu.
Ukweli ni kwamba tunao uwezo wa kufanya mambo
yetu kwa kujitegemea huku tukidhibiti deni letu la
taifa. Ninachoweza kusema tu ni kwamba mambo haya
nimeyafikiria kwa kina. Katika kutafakari ni kwa namna
gani tutabadilisha hali za maisha ya watu wetu,
sikukurupuka.
Inawezekana
mambo
niliyoyazungumza
kwamba
tutayafanya yakaonekana kuwa ni mengi na ni mzigo.
Lakini waswahili wanasema tembo hashindwi na
mkonga wake. Kama nilivyoonyesha, tunao uwezo
22

kabisa wa kuyafanya. Katika nchi yetu yenye mahitaji


mengi, hatuna anasa ya kuchagua kipi kiwe kwanza.
Tunao wajibu kama viongozi wa ubunifu wa kufanya
mambo yote ya msingi kwa wakati mmoja. Tunazo
rasilimali na uwezo wa kuendeleza elimu na kilimo kwa
wakati mmoja, tuna uwezo wa kumaliza matatizo ya
madawati nchini, matatizo ya madawa katika hospitali
zetu, matatizo ya mikopo kwa wanafunzi, matatizo ya
maji, matatizo ya mishahara ya marupurupu ya
wafanyakazi na mambo mengi ambayo Watanzania
wanayatarajia kutoka katika Serikali yao.
Haya yote yatawezakana iwapo tutafumua na kusuka
upya mfumo wa utumishi na utendaji wa Serikali ili
kukomesha urasimu uliokithiri Serikalini, ili kurudisha
nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma, ili kuongeza
uwezekano na uharaka wa uwajibishaji wa watumishi
wa umma wanaokiuka maadili ya kazi zao lakini pia ili
kurudisha ari, morali na fahari na heshima kwa
watumishi wa umma.
Lakini napenda nirudie, pamoja na yote haya, tiba ya
uhakika ni kuutengeneza uchumi wetu ukue kwa
namna ambayo inawajumuisha Watanzania wa hali
zote. Tiba ya uhakikani kwa Watanzania kuumiliki
uchumi wao na kuwa na nguvu ya kiuchumi ya
kujiamulia
hatma
ya
maisha
yao.
Serikali
nitakayoiongoza italisimamia hili. Tiba kubwa ni
nidhamu ya kazi na uwajibikaji wa kila mmoja wetu.
Nasimama mbele yenu nikiwa na bahati kubwa ya
kupata malezi ya siasa na uongozi kwa viongozi
waliotangulia wa nchi yetu. Rais Mstaafu Benjamin
William Mkapa aliyefahamu uwezo wangu na kunisaidia
kupata elimu yangu ya Chuo Kuu na kuniwezesha
kupata kazi Wizara ya Mambo ya Nje. Na, Rais Jakaya
Mrisho Kikwete aliyeniona nikiwa naye Wizara ya
23

Mambo ya Nje na kuniteua niwe Msaidizi wake kwenye


kampeni za Urais mwaka 2005, ambapo nilizunguka
naye nchi nzima tukizungumzia kero za Watanzania, na
baadaye kuniteua kuwa Msaidizi wake Ikulu, ambapo
nilipata fursa ya kuona na kujua nchi inaendeshwa vipi,
kushiriki katika mikutano yake yote na viongozi
wengine duniani na kuona diplomasia ya kimataifa
inaendeshwa vipi, na kushiriki katika vikao vya Baraza
la Mawaziri na kujua maamuzi makubwa ya nchi
yanafanywa vipi.
Namshukuru pia Rais Kikwete kwa kunipa fursa ya kuwa
kiongozi katika Chama chetu. Kwa kuwa Mjumbe wa
Sektretarieti ya Chama, Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Chama na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya
CCM, nimeshiriki kwenye uendeshaji wa shughuli za kila
siku za Chama chetu na nimekijua vizuri Chama.
Nimejua uimara na udhaifu wake. Na nimeyajua
yanayopaswa kufanywa ili kiendelee kuaminiwa na
Watanzania.
Nawashukuru wananchi wa Bumbuli kwa kuniamini
niwe Mbunge wao. Nawashukuru wa kunifanya
nionekane na kuendelea kunipenda. Bado nina deni
kubwa kwao kwa imani hiyo.
Napenda nifikie mwisho kwa kusema kwamba ninayo
dhamira, uwezo, maarifa na ubunifu wa kuiongoza nchi
yetu kukabiliana na changamoto mpya, za kizazi cha
sasa, changamoto zinazohitaji maarifa mapya.
Naishukuru sana familia yangu, ikiwemo wazazi na
ndugu na jamaa. Lakini zaidi mke wangu, ambaye
tumekuwa wote sasa kwa miaka zaidi ya kumi, na
watoto wetu wawili kwa upendo na uvumilivu.
Lakini kazi ya kuijenga nchi sio kazi ya mtu mmoja.
Kiongozi yoyote anayesema yeye ndio Masia na
24

amekuja
kama
mkombozi
wa
taifa,
atakuwa
anawalaghai. Mafanikio yangu katika nafasi hii
ninayoiomba na katika kutimiza majukumu yangu
yanategemea ushiriki na ushirikiano wenu. Nachukua
nafasi hii kuwaalika katika harakati hizi. Sigombei
nafasi hii kupambana na mtu. Nagombea kupambana
na changamoto za watu. Nikifanikiwa, nitasikiliza
mawazo mazuri kutoka kwa kila mtu, hata ambao sio
wana-CCM. Nitakuwa kiongozi wa watu wote bila
kujali dini zao, makabila yao, rangi zao, vyama vyao au
kanda wanazotoka. Nitaongoza kwa namna ambayo
Watanzania watajisikia fahari kuongozwa nami.
Sijawa kwenye siasa kwa miaka 30 au 40 kama baadhi
ya wagombea, ambao wamepata fursa nyingi na
madaraka makubwa ya kutekeleza yale wanayoyaahidi
leo. Lakini nimekuwepo kwenye uongozi kiasi cha
kutosha cha kujua matatizo yako wapi, nini cha
kufanya,na namna ya kufanya, kama ambavyo
nimeelezea kwa kirefu mchana huu. Mkinipa nafasi
hamtakuwa mnatumaini tu, balimtakuwa mnaonyesha
dhamira ya kutaka hakika ya mabadiliko makubwa.
Nafarijika kwamba kwenye Chama chetu wamejitokeza
wagombea wengi. Hili ni jambo jema sana kwani
kunaonesha ukomavu wa kidemokrasia. Lakini ni
muhimu sote tukaelewa kwamba kugombea sio
kugombana. Binafsi ndivyo ninavyoelewa na ndio
maana sikutumia muda wenu kumshambulia mtu
kwasababu jambo hili halisaidii Watanzania. Nina imani
kubwa kwamba, kwa ukomavu wa Chama chetu,
tutabaki wamoja na imara mara baada ya mchakato
huu.
Chama chetu kina dhamana kubwa na kina
historia adhimu barani Afrika. Dunia nzima inatazama
mchakato huu wa ndani ya Chama chetu. Matumaini ya
marafiki zetu na matumaini ya wanachama wetu ni
kwamba tutachagua mgombea wetu kwa msingi wa
25

kujiamini na sio
kusambaratika.

kwa

msingi

wa

woga

wa

Mkinichagua mimi kupeperusha bendera ya chama,


nitatumia nguvu zangu zote na utajiri mkubwa wa
hekima ndani ya chama chetu kuvunja makundi yote
yaliyojitokeza
kipindi
hiki
cha
uchaguzi
na
kuwaunganisha wana-CCM wote. Mwenyekiti wetu,
Makamu Wenyeviti na Katibu Mkuu na Sekretarieti
yakewamefanya kazi nzuri ya kukiimarisha Chama
chetu na kukijengea uwezo. Nitakapokuwa kiongozi wa
Chama chetu nitaanzia walipoishia. Nimekuwa chipukizi
wa Chama hiki. Nimekuwa kiongozi wa Umoja wa Vijana
wa Chama hiki. Na nimefikia hadi kuwa Mjumbe wa
Kamati Kuu wa Chama chetu. Nafahamu changamoto
za watendaji wa Chama na Jumuiya mikoani na
wilayani. Wanafanya kazi kubwa. Nitawatazama.
Nafahamu Wenyeviti wetu wa Mikoa na Wilaya, wana
mahitaji mahsusi ya kufanya kazi zao za uongozi wa
Chama chetu na usimamizi wa Ilani yetu katika ngazi
zao. Nayajua hayo mahitaji. Naelewa majukumu mapya
ya
Wajumbe
wa
NEC
yanahitaji
uwezeshaji.
Tutayazungumza na kuyafanya. Nafahamu Makatibu wa
Siasa na Uenezi na Makatibu wa Uchumi na Fedha wa
Mikoa na Wilaya wanafanya kazi kubwa na wanastahili
kutambuliwa. Chama chetu kitakuwa salama chini ya
uongozi wangu.
Tutaendelea na kazi nzuri inayofanywa sasa na viongozi
wetu ya kukiimarisha Chama chetu ili kiendelee kuwa
tumaini la Watanzania.
Nimalizie kwa kurudia kwamba sigombei nafasi hii
kupambana na mtu bali kupambana na matatizo ya
watu. Nataka kushirikiana nanyi wote tuijenge Tanzania
Mpya. Nataka uongozi wangu uwe mwanzo wa Tanzania
Mpya, ya miaka 50 ijayo. Tunataka tujenge taifa la
26

Watanzania ambao kila mmoja ana fursa, uwezo na


nguvu ya kiuchumi ya kupata mahitaji yake na
kuendesha maisha yake. Tunataka kujenga taifa ambalo
wananchi hawabebi mzigo wa maisha unawaelemea.
Tunataka kujenga taifa la watu wenye sauti na kauli juu
ya Serikali yao. Haya mambo sio ndoto. Yanawezekana
kabisa.
Viongozi huwekwa na Mungu. Ninapoomba uongozi
huu, namuomba Mungu anipe fursa ya kuwaongoza
watu wake kupitia ridhaa yao. Kama mgombea,
namuomba Mungu anipe uwezo, hekima na busara ya
kupokea matakwa yake katika mchakato huu. Na kama
kiongozi, namuomba anipe hekima ya kuwaongoza
watu wake na kushughulikia mashauri yao kwa haki na
ukweli.
Na kubwa zaidi, namuomba Mungu aendelee kuibariki
nchi yetunawatu wake.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.

27