You are on page 1of 3

CHAMA CHA MAPINDUZI

OFISI NDOGO YA MAKAO MAKUU

e-mail:katibumkuu@ccmtz.org

s. L. P. 9151 OAR ES SALAAM, TANZANIA, FAX: 022 - 2185245

__________________

Barua zote zipelekwe kwa Katibu Mkuu

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Jana tarehe 27/7/2016 Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
walitoa kauli kwa Waandishi wa Habari kupitia Mwenyekiti wa Chama
hicho Taifa Ndugu Freeman Mbowe (Mb). Tamko hilo kama ilivyo kawaida
ya CHADEMA lilijaa uongo mwingi na ghiliba nyingi za kibabaishaji na
kuthibitisha ukweli kuwa kwa hakika kutokana na kasi ya Serikali ya
Awamu ya Tano chini ya Dr. John Pombe Magufuli wapinzani nchi hii
wamekosa ajenda na hivyo njia peke yake wanayoona inafaa ili waendelee
kufanya utapeli ni kutunga uongo, kujiaminisha katika uongo huo na
kuusambaza uongo huo ili kujaribu kupata wafuasi.
Katika uongo na uzushi huo walioutangaza jana, CHADEMA wanasema
wameamua kufanya mikutano na maandamano nchi nzima kwa tarehe
waliyoitaja na maandamano hayo yatafanyika chini ya operesheni
waliyoiita UKUTA. Kimsingi hoja walizozitumia kufikia uamuzi wao bila
kuzirudia zimejaa upotoshaji na uongo uliokithiri. Kwa mfano wanadai
Serikali imezuia mikutano yote ya vyama vya siasa, huku wakijua kuwa ni
uongo kwani Serikali haijazuia mikutano kwenye majimbo yao, Wabunge
wako huru kufanya shughuli zao kwenye majimbo yao, na tumeona
Wabunge wakifanya shughuli zao majimboni bila shida wakiwemo hao wa
vyama vya upinzani.
Lakini vyama vya siasa kufanya shughuli kwa mujibu wa katiba ya vyama
vyao sio jambo lililozuiliwa pia, ndiyo maana tumeshuhudia vyama
vikifanya mikutano yao ya kikatiba bila tabu.
Lakini mfano mwingine wa hoja za uongo na uzushi, ni hoja eti ya Serikali
hii ya Awamu ya Tano kuwa ya kidikteta. Udikteta hasa unaosemwa na
Chadema ni upi? Ni huu wa kushughulikia watumishi hewa? Ni huu wa
kuwabana wakwepa kodi? Ni huu wa kupunguza na kudhibiti safari za nje?
Ni huu wa kubana matumizi ya Serikali? Ni huu wa kufukuza wabadhirifu
na wazembe kazini? Hivi udikteta huo ni huu wa kushughulikia mafisadi
mpaka kuanzisha mahakama yao? CCM inaamini Watanzania walio wengi
wanaunga mkono hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli na Serikali
yake, sasa kama kwa Chadema hatua hizi ndiyo tafsiri yake ni udikteta
basi bila shaka wao ni sehemu ya mfumo mbovu ndiyo maana wako tayari
kuleta vurugu ili wautetee.

Kwa kuwa CHADEMA wamezoea kujenga Chama chao kwa harakati


zinazohusisha kumwaga damu za Watanzania wasiokuwa na hatia, ukweli
huu wa maelekezo ya Serikali hawausemi, isipokuwa wanafanya juhudi
kubwa kuhakikisha wanafanya mambo ambayo mwisho wa siku
yatasababisha vurugu, uvunjifu wa amani na umwagaji damu.
Lakini pengine ni muhimu Watanzania na wapenda amani nchini na
duniani wakajiuliza ni kweli kuwa lengo la hizi vurugu na maandamano
haya ni la kujenga na si kubomoa? Kwa nini kila operesheni ikifanywa na
CHADEMA huwa inaambatana na umwagikaji wa damu za Watanzania
wasiokuwa na hatia? Wakati wa Maandamano hayo inapotokea madhara ni
kwa nini waathirika huwa sio viongozi waanzilishi wa maandamano hayo
wala wake au waume zao au watoto wao au hata ndugu zao wa karibu bali
huwa ni watu wengine nje ya hao ndugu zao wa karibu? Mpaka lini damu
za Watanzania wasio na hatia zitaendelea kutumika kutafuta umaarufu wa
CHADEMA na viongozi wake?
Hii ni kwa faida ya nani hasa? Kwa nini pamoja na kuelekezwa namna bora
ya kufanya siasa wao huwa hawataki kufuata utaratibu? Hivi ni kweli kuwa
hawajui bila kufuata utaratibu jambo lolote huwa ni vurugu?
Chama Cha Mapinduzi kinapenda kuwakumbusha Watanzania kuwa ni
vizuri kutafakari na kujiuliza maswali ya msingi kabla ya kuamua kushiriki
au kuruhusu watoto wetu kwenda kuwa kafara ya walafi wachache wa
madaraka. Ni vizuri tukayakumbuka matukio kwenye operesheni kama hizi
yaliyopoteza maisha ya vijana wetu na matokeo ya kila operesheni.
Pamoja na ukweli kuwa hakuna operesheni yeyote kati ya zote zilizowahi
kufanywa na Chadema ambayo imewahi kuwasaidia Watanzania wa
kawaida zaidi ya kujenga umaarufu wa viongozi wachache wa Chadema
na kuneemesha matumbo yao na ya familia zao, operesheni zote
zimepoteza maisha ya Watanzania kadhaa wasiokuwa na hatia wala
wasiofaidika kwa lolote na operesheni hizo.
Kama nia ni njema kwa nini hawataki kufuata Sheria na taratibu
tulizojiwekea? Demokrasia gani isiyokuwa na mipaka? Demokrasia bila
mipaka ni fujo. Tunaomba vyombo vinavyohusika visisite kuchukua hatua
zinazostahili bila kumuonea mtu lakini bila kufumbia macho vitendo
vyenye lengo la kuwahujumu Watanzania waliowengi walioamua kuchapa
kazi kuitikia wito wa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano ya kufanya kazi.
Lakini pia tunawashauri Watanzania, wapenda amani, utulivu na
maendeleo kupuuza wito wa vurugu na uvunjifu wa amani badala yake
wajikite kwenye kuchapa kazi na kujitafutia maendeleo yao kwa kufanya
kazi kwa bidii.
Maendeleo hayaji kwa maandamano, maendeleo huja kwa kuchapa kazi
kwa bidii. Maendeleo hayaji kwa vurugu na fujo nchini, bali amani na
utulivu ni vichocheo muhimu vya maendeleo ya kweli.
Imetolewa na:-

Christopher Ole Sendeka (MNEC),


MSEMAJI WA CHAMA
28/07/2016