You are on page 1of 6

KISWAHILI NA CHANGAMOTO ZA KUJITAKIA

Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia pumzi na Afya, na kuweza kuandika
mawazo yangu haya machache.
Nikukumbushe kidogo japo kwa ufupi Kuhusu lugha ya Kiswahili ilipoanzia, Kiswahili kilikuwepo
toka karne za mwanzo kabisa kikiwa katika mfumo wa vilugha vidogovidogo vilivyoitwa lahaja.
“Lahaja ni vilugha vidogovidogo vya lugha moja ambavyo hubainika kijamii au kijiografia”,
mnamo mwaka 1930 kulizuka mjadala wa kutafuta lugha itakayotumika katika ukanda wa afrika
mashariki kwa ajili ya mawasiliano, biashara, na siasa. Kulianzishwa kamati ya lugha ya afrika
mashariki iliyokua na kazi ya kutafuta lugha itakayotumika, ndipo kiunguja kikachaguliwa kati
ya lahaja nyingi za lugha ya kiswahili na kusanifishwa kutokana na kuenea kwake kuanzia
unguja, bara mpaka kufika mashariki ya Kongo a idadi kubwa ya wasemaji.
Harakati ziliendelea baina ya wataalamu (wanaisimu) wa lugha katika kuongeza istilahi na
misamiati ili kuifanya lugha iweze kukidhi mahitaji ya kila sehemu, wasanii mashuhuri kama
Shaaban Robert walitumia sanaa kuieneza, kuitunza na kuikuza lugha ya kiswahili katika kila
kona ya afrika mashariki, wanaharakati wa kupigaia uhuru nao walichangia
kukisambaza/kuitangaza lugha. Baada ya uhuru serikali nayo haikua nyuma katika kuhakikisha
lugha ya kiswahili inatumika, inakua na kuenea kila sehemu kwa kuunda chombo kitakacho
simamia kiswahili (BAKITA), nao wataalamu kutoka taasisi ya uchunguzi wa kiswahili (TUKI)
kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam hawakua nyuma, walianzisha na kuchapisha kamusi
mbalimbali za kiswahili.
Tangu usanifishaji wake lugha ya Kiswahili kipindi cha ukoloni, Harakati na changamoto zake
katika kuikuza, kuieneza na kuisambaza kabla na baada ya uhuru mpaka kufikia leo 2016,
kiswahili kimekua kijografia na idadi ya wazungumzaji, sasa kiswahili kina wazungumzaji zaidi ya
milioni 100 dunia nzima, Kiswahili huzugumzwa katika nchi zaidi ya 15.

Kiswahili sasa kimekua miongoni mwa lugha zinazozungumzwa sana duniani, ni moja kati ya
lugha 7 zinazozugumzwa zaidi duniani, Afrika kinashika nafasi ya pili, lugha ya kiswahili imekua
na mafanikio makubwa duniai, ni lugha rasmi ya umoja wa afrika, mashirika mbalimbali
makubwa ya utagazaji duniani yameanzisha redio za kurusha matagazo yao kwa lugha ya
kiswahili ili kufikia jamii zinazozungumza kiswahili, Mfano BBC Swahili, Dira ya Dunia, Sauti ya
Amerika nk.
Kiswahili kimekua kikiwavutia wengi, imefikia hatua sasa kinafundishwa katika vyuo vikubwa
duniani, vyuo kama chuo kikuu cha mawasiliano ya habari china, chuo kikuu cha lugha za kigeni
cha Beijing, chuo cha Glasgow, chuo cha Cambridge, Harvard, Stanford na vingine vingi.
Kwa Juhudi zote hizo zinazofanywa na wanaofanya kukikuza na kufanya kiswahili kiwafikie watu
wengi zaidi duniani bado zinaonekana kutoendani na kasi ya ukuaji wa lugha yenyewe,
wahusika wakuu wa lugha ambao ni nchi za afrika mashariki bado jitihada zetu kukifanya kiwe
kikubwa zaidi ni ndogo, bado raia wake hatukizugumzi ipasavyo, bado hatujaamka kutumia
fursa zilizopo mbele yetu Kupitia lugha yetu ambayo ndio inaonekana kubeba tamaduni za watu
wa afrika mashariki, kiswahili ni moja ya tanzu za mila, tamaduni na desturi zetu watu wa afrika
mashariki hasa Tanzania.
Dhana ambayo ipo katika vichwa vyetu ni kua lugha yetu adhimu ya kiswahili haijitoshelezi
kimsamiati, inakosa istilahi kukidhi matakwa ya taaluma mbalimbali, lakini ukweli ni kwamba
kiswahili kimejitosheleza kimsamiati, kiswahili ni kipana, kiswahili ni kikubwa. Tatizo ni kukosa
wazungumzaji ambao wako tayari kujua na kujifunza zaidi kufahamu vizuri maneno yake.
“Kweli penye miti hapana wajenzi” kuna wengine wanakutana na maneno tofauti ya kiswahili
ambayo hawakuwahi kuyaona, ila kwakua tu wameshazoea kuyapatia mbadala wake kwa
kingereza basi utasikia “bora kiingereza”. Watu wa zamani wanakwambia “fimbo ya jirani haiui
nyoka”. Wakiwa na maana kwamba, matatizo yako usitegemee jirani yako akutatulie, onesha
kwanza mweyewe unataka kujisaidia ili wa pembeni waweze kukusaidia.
Wa kuikuza lugha ni sisi wenyewe kwa mikakati thabiti na uhamasishaji wa hali ya juu katika
kuifanya lugha ya kiswahili kua tishio zaidi duniani. Tunaposema tunataka kuipeleka mbele

Tanzania kiuchumi ili hali tamaduni zetu ziko nyuma, itakua jambo la kustaajabisha sana,
kiswahili ni tamaduni yetu watanzania.
Najua hatupendi itolewe mifano ya nchi kama China, ila sidhani kama China walisema kwakua
sisi bado hatujaendelea ndio kwanza tunajenga nchi basi tutumie kingereza kwanza mapaka
hapo tutakapo kua imara, la hasha, walipokua wanajenga nchi na tamaduni zao pia walikua
wakizidumisha. Ndio maana mpaka leo hii hawajui historia za nchi zigine zaidi ya zao wenyewe.
Haya turudi kwenye Dhumuni kuu la hii makala fupi, changamoto kadhaa ambazo zikiangaziwa
kwa stakiri hakika tutajivunia zaidi na lugha yetu adhimu hadi wanaokikosoa watuunge mkono,
fid q aliwahi kusema “wafurahishe waliokaribu wa mbali watasogea”
Tanzania kuna vyuo vikuu na vishirika vyake vitoavyo stashahada, shahada, shahada za uzamili
na uzamivu za kiswahili (chuo kikuu huria cha Tanzania, chuo kikuu cha Dar es salaam, chuo
kikuu kishiriki cha Dar es salaam, chuo kikuu cha Dodoma, chuo kishiriki cha Mkwawa, hii
inamaanisha kuna wawakufunzi/wahadhiri wa lugha ya kiswahili katika hivi vyuo wanaojituma
na kuhakikisha wanadahili na kutoa wahitimu watakao kidhi uhitaji wao katika maeneo
mbalimbali yanatakiwa kua na wanaisimu.
Maswali ni mengi nayojiuliza katika ngazi hii ya vyuo, sawa vyuo vina toa wahitimu wengi wa
kiswahili lakini wanaishia wapi? Na ni kipi hasa wanafundishwa? Wanafundishwa ili waje kua wa
kina nani baadae? Wanaandaliwa vizuri kweli kuja kukabiliana na soko la ajira mtaani? Soko
lenyewe ni lipi, wanaoneshwa au wanatakiwa wajioneshe? Mtanijibu.
Tumeanzisha hizi taaluma za kiswahili Tanzania, afrika na dunia kwa ujumla ili tukuze lugha na
kuisambaza na kua na watu wengi wanaojua kiswahili sanifu, wenye ufahamu yakinifu wa sarufi
ya lugha yetu adhimu, Lakini wanaisambaza? Au Je, Wanatumika ipasavyo?
Kwanini vyuo Kupitia wakufunzi wao, kwa sababu (ni wanafunzi wengi wanamaliza) Kwanini
wasikae wakabuni njia mbadala ya kuwatafutia ajira hawa watu? Mfano, kuna taaluma kadhaa
ambazo hua zinachangia moja kwa moja kuisambaza elimu katika jamii, taaluma za uandishi wa
habari na utangazaji, ukweli ni kwamba waandishi wa habari na watangazaji wanachangia kwa
kiasi kikubwa kuharibu lugha, Kwanini vyuo na wizara husika wasikae na kufikiria kudahili hawa

wataalamu wa lugha kuja kua watangazaji, wahariri au waandishi wa habari, au kupitishwe
sheria vyuo vikuu kwamba lugha ya kiswahili iwe ni lazima kwa kila ngazi ya uandishi wa habari.
Hawa wataweza kueneza istilahi na maneno mengi sahihi ya lugha yetu na kufanya itumike zaidi
kwani watu watakua wanasikia na kusoma mara kwa mara.
Mzizi wa wanafunzi wa shule za msingi kujua kiswahili fasaha ni walimu, na ukweli ni kwamba
walimu wetu wanaofudisha kiswahili sio wanaisimu/wataalamu wa kiswahili, ni wanafunzi walio
faulu vizuri kiswahili na kuamua kurudi kufundisha kiswahili. Sasa tumepata kuanzisha taaluma
ya kiswahili, Kwanini hawa wanaomaliza kusomea kiswahili ndio wasiwe walimu wa kiswahili
kuanzia ngazi ya msingi mpaka elimu ya juu? Au wapelekwe wakasomee ualimu na kurudi
kufundisha wadogo na watoto wetu. Je, Kuna ushirikiano kati ya wahadhiri wa hapa nchini na
wa huko nje wanaofundisha taaluma hii ya kiswahili? Je wanaofundisha kiswahili huko nje ni
kweli wanataaluma ya ualimu au walisomea kiswahili? Isijekua kuna walimu huko nje lakini
hawajui vizuri sarufi ya lugha na kupotosha watu. Niishie hapo nisijetoka nje ya mada.
Turudi serikalini na taasisi zinazo linda na kutunza kiswahili Tanzania, Wizara ya Habari,
Utamaduni, Wasanii na Michezo, wizara ya elimu, sayansi, na teknolojia na Baraza la Kiswahili
Tanzania.
Wizara zenye majukumu ya moja kwa moja katika kuhakikisha kiswahili kinakua na mizizi halisi
yenye kuenea katika kila idara ni wizara ya elimu, sayansi, na teknolojia pamoja na wizara ya
habari, utamaduni, sanaa na michezo, Je zinafanya nini? Kasi waliyonayo katika kushughulikia
masuala ya lugha ina akisi kasi ya ukuaji na uhitaji wa kiswahili chenyewe duniani? Je, kuna
ushirikiano thabiti baina ya hizi wizara katika usimamizi wa hii lugha? Maana usijitape na minazi
kama huwezi kuikwea.
Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu, Tuseme wakaamua kushirikiana kwa pamoja kupitisha
sera mpya na sheria mpya za matumizi ya lugha (sera na sheria za lugha katika elimu pamoja na
shughuli mbalimbali za kibiashara na uchumi, hata kijamii) haya mabadiliko ukitoa tu kwa jamii
husika kubadilika. Chachu ya mabadiliko lazima ianzishwe na serikali Kupitia sera zake pamoja
na sheria ili kuongeza uhamasishaji wa matumizi ya kiswahili nchini. Serikali Kupitia wizara hizi

mbili wapitishe sheria kwa vyuo na kwenye mashirika ya utangazaji pamoja na taasisi zake
Kuhusu kutumia kiswahili.
Mfano. Kupitishwe sheria kwa waandishi wa habari na watangazaji wawe wamesomea lugha ya
kiswahili (wawe na vyeti). Ufudishwaji wa somo la lugha katika kila taalamu vyuoni, walimu wa
kiswahili wawe wamesoma lugha kwa ngazi kutokana na ngazi wanayofundisha. Serikali
iwauganishe wahadhiri wa kiswahili Tanzania na wale wa nje ya nchi ili kuleta usawa wa
ufundishaji duniani kote, mafunzo ya lugha yetu yalandane na kila upande wa dunia, kubuniwe
mashindano na Harakati mbalimbali za lugha duniani kote.
Sidhani kama ninayosema hayawezekani kama tukiamua kweli kuyafanya kwa minadhiri ya
kutunza utamaduni, mila na desturi. Kiswahili ni moja ya tanzu na njia za kutunza mila, desturi
na tamaduni zetu, kiswahili ni fahari ya mtanzania. Sija wasahau BAKITA, yawapasa serikali
kuliunda upya Baraza hili la kiswahili Tanzania liendane na wakati, vijana kutoka vyuoni
wanaosomea kiswahili wawekwe pale, Baraza liundwe upya lisimamie lugha ipasavyo,
lichapishe kamusi na vitabu vya sarufi ya lugha, vitabu vya hadithi, methali, misemo, misamiati
na semi zingine (wa kutunza kiswahili ni sisi wenyewe sio wageni). Wataalamu wapo, Kwanini
wasituthibitie ubora na utajiri wa lugha hii rahisi na tamu kinywani mpaka kichwani? Kiswahili
chenyewe kinatusikitikia “kweli penye miti hapana wajenzi” Hatuna sababu ya kushindwa
kuinyanyua na kuithamini hii lugha ikiwa tuna wanaisimu wasio na kazi mtaani na wengine
wapo mavyuoni. Eti jamani, wanamaliza vipi shahada bila kufanya uchunguzi Kuhusu jamii zetu
na lugha yetu tukazisoma?
Wa mwisho kabisa ni wanaisimu wenye, kweli mnamaliza na mnakosa cha kuifanyia hii lugha?
Mbona fursa zipo nyingi Kupitia hii lugha au ndio msemo wa mtaani “ukiwa nje ya mchezo
unaona kweli”? ila sidhani kama ni hivyo kweli, kiswahili bado kina mambo mengi ya kukifanyia,
ikiwa waliamua kusomea hii lugha maana yake wanaipenda, basi na wafanye yanayotakikana
kufanyika. Wakijiunga vikundi kwa vikundi wakagawana kazi. Mgaagaa na upwa hali wali
mkavu” wajuzi wa lugha wanasema, huwezi ukajituma na ukakosa hata chochote kitu, wajuzi
wa hii lugha wanaosema hawana kazi na waamke wafanye kitu kwa ajili ya hii lugha.

Ukitoa tu wasomi, serikali, vyuo na vyuo hata sisi wananchi hatuoneshi nia kweli ya kutaka
kujua kiswahili fasaha, tumejawa na kasumba nyingi za kutokuthamini lugha yetu, tumejawa na
shauku za kujua lugha za wenzetu pasi na kujali ya kwetu, tunaongea tu kiswahili kwa sababu
tumewakuta watu wanaotuzunguka wanakizungumza. Tumekua tukishangaa sana pale
tunapokutana na maneno ambayo hatukuwahi kuyasikia kabla na kuona bora kuyapatia
mbadala wake kwa lugha nyingine. Ila tukumbuke kisichotumika hupotea.
Ni rai yangu kwa wadau wote wa kiswahili kuungana kwa pamoja kuithamini na kutukuza lugha
hii adhimu ya kiswahili, ili kuifanya iwe ya kwanza duniani na kuweza kutunza utajiri wetu wa
lugha na jamii. Matumizi fasaha ya kiswahili huleta utulivu wa moyo na fikra. Matumizi fasaha
ya kiswahili huongeza hali ya unzalendo katika nyoyo na akili zetu.
Ningependa kuishia hapa maana wenyewe wanasema mwenye busara huweka akiba ya
maneno na siku zote akiba haiozi. Basi mi sina budi kuweka kalamu chini, Poleni sana na
samahani kama kuna nilio wakwaza.
Nimekosea basi nikosoe nijirekebishe siku yingine
BARAKA HEMEDI JEREKO
Twitter @jerekojr
Jereko98@gmail.com 0788121085
ALHAMDULILLAH