You are on page 1of 5

TAMKO LA MHESHIMIWA JANUARY Y.

MAKAMBA (MB), WAZIRI WA


NCHI - OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA
KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA KUHUSU MAADHIMISHO YA
SIKU YA KUPAMBANA NA KUENEA KWA HALI YA JANGWA NA
UKAME DUNIANI, TAREHE 17 JUNI, 2017

Ndugu Wananchi,

Mwaka 1994 Baraza la Umoja wa Mataifa liliazimia na kuitangaza tarehe


17 mwezi Juni ya kila mwaka kuwa ya maadhimisho ya siku ya
Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame. Kwa kutambua
umuhimu wa kuadhimisha siku hii, tarehe 17 mwezi Juni kila mwaka,
duniani kote huadhimishwa Siku ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya
Jangwa na Ukame. Madhumuni ya kuadhimisha siku hii ni kukuza uelewa
miongoni mwa jamii juu ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana
na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame na umuhimu wa utekelezaji
wake duniani, hususan katika nchi zilizoathirika zaidi na tatizo hili la kuenea
kwa hali ya jangwa na ukame hasa katika bara la Afrika.

Ndugu Wananchi,

Tangu mwaka 1994 nchi zilizoridhia Mkataba wa Kupambana na Kuenea


kwa Hali ya Jangwa na Ukame, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Mashirika
ya Kimataifa yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na wadau wengine,
huadhimisha siku hii kwa kufanya shughuli kadhaa zinazohusu kupambana
na tatizo hili. Mkataba huu ndiyo mkataba pekee wa Umoja wa Mataifa
unaolenga kupambana na tatizo la uharibifu wa ardhi katika maeneo kame,
na kufanya juhudi za kuhifadhi na kuleta matumizi endelevu ya ardhi. Kwa
kutambua umuhimu wa Mkataba huu, Nchi zipatazo 193 ulimwenguni
zimeridhia utekelezaji wake hadi sasa. Ni wazi kuwa mkataba huu una
umuhimu wa pekee kwa nchi kama Tanzania ambayo uchumi wake
unategemea ardhi kwa ajili ya kilimo ambacho kinatoa ajira kwa wananchi
wengi.

Ndugu Wananchi,

1
Kauli mbiu ya mwaka huu katika kuadhimisha siku ya Kupambana na
Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame inasema Ardhi ni Makazi yetu
Tuitunze kwa Manufaa ya baadaye (Our Land, Our Home, Our
Future). Kauli mbiu hii inayoadhimishwa mwaka huu ina malengo ya
kuhamasisha jamii kuitunza Ardhi kwa kuwa ndiyo makazi yetu hii ikiwa ni
pamoja na kuongeza juhudi zaidi kwa ajili ya manufaa ya baadaye kwetu
sisi na vizazi vijavyo. Malengo haya yanadhihirisha umuhimu wa utunzaji
wa ardhi na udongo kwa ajili ya matumizi endelevu hasa kuifanya iwe na
uwezo wa kuzalisha mazao ya kilimo na mifugo na kutoa huduma zingine
muhimu kama vile utalii wa wanyamapori, uwindaji, miti, vyanzo vya maji
na uwekezaji wa viwanda ili kuleta ustawi wa jamii kwa vizazi vya sasa na
vijavyo. Hali ya uharibifu wa mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji
inaongezeka kwa kasi na hivyo kuongezeka kwa tatizo la ukame, upungufu
wa mazao ya kilimo na kupungua kwa chakula mara kwa mara na
kuongezeka kwa umasikini miongoni mwa jamii. Ukataji wa miti kiholela na
uharibifu wa misitu unaosababishwa na utegemezi mkubwa wa binadamu
wa kupata mahitaji kutokana na mazao ya misitu pamoja na huduma
zingine muhimu, kunazidisha ukubwa wa tatizo hili. Makazi, Mikakati na
program zote muhimu za maendeleo ya nchi hufanyika kwa kutumia ardhi.

Ndugu Wananchi,

Nchi yetu inakabiliwa kwa kiasi kikubwa na hali ya kuenea kwa jangwa na
ukame. Takwimu zinaonyesha kuwa takriban asilimia sitini na moja (61) ya
eneo la nchi liko katika hatari ya kugeuka jangwa. Miongoni mwa mikoa
ambayo imeathirika zaidi ni pamoja na Singida, Dodoma, Shinyanga,
Manyara, Simiyu, Geita na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Arusha. Tayari
madhara mbalimbali ya kuenea kwa hali ya jangwa na ukame yameanza
kuonekana ikiwa ni pamoja na kukauka kwa vyanzo vya maji katika
maeneo mbalimbali, vifo vya mifugo na wanyama pori, upungufu wa mvua
kutokana na ukataji wa miti kiholela, migogoro baina ya wafugaji na
wakulima kutokana na kupungua kwa maeneo ya kilimo na malisho ya
mifugo.

Ndugu Wananchi,

2
Kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kuna madhara makubwa sana katika
uchumi wa taifa letu. Kama inavyoeleweka asilimia themanini (80) ya
Watanzania inategemea kilimo ambacho kwa kiwango kikubwa
kinategemea mvua. Kutokana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame ni
dhahiri kuwa uzalishaji wa mazao unapungua kwa kiasi kikubwa. Hali hii
inachangia kuathiri kushuka kwa uchumi hasa unaotegemea uuzaji wa
mazao ya chakula na biashara. Hali hii itapunguza pia upatikanaji wa
kipato katika ngazi ya kaya na ngazi ya taifa kiujumla. Kuenea kwa hali ya
jangwa na ukame pia kunasababisha upotevu wa rasilimali zingine kama
misitu, vifo vya wanyama pori ambao ni chanzo kikubwa cha fedha za
kigeni kupitia utalii. Aidha, kuenea kwa hali ya jangwa na ukame
kunasababisha tabaka la juu la ardhi kuwa wazi na hivyo kutoa nafasi kwa
mmomonyoko wa udongo kwa njia ya maji na upepo. Hali hii inasababisha
kupungua kwa rutuba katika udongo na hivyo kupunguza uzalishaji wa
mazao kwa kiasi kikubwa.

Ndugu Wananchi

Ili kupambana na hali ya kuenea kwa jangwa na ukame serikali imechukua


hatua mbalimbali. Hatua hizo ni pamoja kuandaa taarifa ya hali ya kuenea
kwa jangwa na ukame (Status of Land Degradation) ya mwaka 2014;
Mpango kazi wa Kitaifa wa Kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na
ukame (National Action Program to Combat Desertification) ya mwaka
2014-2018. Taarifa na Mpango kazi huu vimetoa maelekezo mbalimbali
kwa mamlaka husika, maelekezo ambayo utekelezaji wake ni wa muda
mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Maelekezo haya ni pamoja na
programu za upandaji miti, kuandaa mpango wa matumizi bora wa ardhi,
kulima kilimo kinachofuata njia za kisasa, ufugaji bora na wa kisasa,
kuanzisha maeneo ya hifadhi na kuyalinda yale yaliyopo, kusisitiza
matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa,
kuendeleza njia bora kuhifadhi maji na uvunaji wa maji hasa kipindi cha
mvua na kuelekeza wananchi kuwa na shughuli zingine za uzalishaji mali
(Other income generating activities) ili kupunguza utegemezi katika
maliasili. Kwa mfano, programu ya kitaifa ya upandaji miti ya mwaka 2016
hadi 2021 inalenga kupanda miti zaidi ya milioni 280 kila mwaka na
3
inalenga hasa maeneo yaliyo katika hatari za kukabiliwa na hali ya jangwa
na ukame.

Ndugu Wananchi,

Ili kukabiliana na tatizo hili na kwa ajili ya kutunza na kuhifadhi maliasili,


Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Kupanda na Kutunza miti wa
mwaka 2016 2021. Mkakati huu unalenga kupunguza kasi ya uharibifu
wa ardhi kwa njia ya kupanda na kutunza miti na kuhakikisha kwamba kila
mwananchi anahusika katika utaratibu huu. Aidha, pamoja na mambo
mengine, Mkakati wa kupambana na ukame na Jangwa na mikakati
mingine ya Mazingira inaendelea kutekelezwa. Pia serikali inaandaa
mkakati wa kupunguza matumizi ya nishati ya Mkaa itokanayo na miti ya
misitu ya asili. Kuongeza juhudi za matumizi ya Usimamizi Endelevu wa
Ardhi. Kufanya Tathmini za Athari kwa Mazingira na Tathmini za Mazingira
Kimkakati. Malengo yote haya ni kutaka kufikiwa wadau wote na endapo
wadau wote katika sekta ya mbalimbali watahusika katika utunzaji wa
mazingira na matumizi endelevu ya Ardhi malengo ya baadaye yatafikiwa.

Ndugu Wananchi;
Matumizi endelevu ya Ardhi, Kupanda na kutunza Miti ni mojawapo ya
mikakati inayoweka ulinganifu katika shughuli za kilimo, ufugaji, misitu,
uhifadhi wa vyanzo vya maji na kuhakikisha kuwa mifumo ya ikolojia
inayotegemeana haiingiliwi. Juhudi hizi zitasaidia katika utekelezaji wa
Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya
Jangwa na Ukame (UNCCD) kwa kuhakikisha kwamba Mpango wa Taifa
wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (NAP) 2014
unakuwa nyenzo muhimu ya kuongeza uzalishaji katika kilimo; kuondokana
na tatizo la uharibifu wa ardhi; kuongoa maeneo yaliyoharibika na
kurejesha misitu katika maeneo ya nyanda kame; na hivyo kupunguza
umasikini.

4
Ndugu Wananchi,
Ninaomba kutoa rai kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika
kutekeleza kauli mbiu ya mwaka huu 2017 ya siku ya kupambana na
kuenea kwa hali ya jangwa na ukame ili kuhakikisha ardhi yetu inatunzwa,
ardhi iliyoharibika imeongolewa, kwa ajili ya kizazi cha sasa na vizazi
vijavyo. Hii inawezekana `ikiwa kila mmoja wetu atashiriki kikamilifu katika
eneo Lake.

Asanteni kwa kunisikiliza.