You are on page 1of 2

MUKHTASARI WA TAARIFA YA UTAFITI WA VIFO VINAVYOTOKEA KATIKA

HOSPITALI YA TANZANIA

Utangulizi

Taarifa za vifo ni moja ya vyanzo muhimu vya takwimu katika kupanga


mipango na kuandaa sera ya afya. Kuainisha vyanzo vya vifo katika hospitali
zetu ni muhimu ili kufuatilia ongezeko la matukio ya vifo na kuweka vipaumbele
katika kuboresha huduma za afya. Hata hivyo, kumekuwa na uhaba mkubwa
wa takwimu za vifo vinavyotokea katika hospitali zetu zilizoainishwa kama
inavyostahili.

Utafiti huu ulifanywa kuainisha matokeo ya vifo katika hospitali 39 za Tanzania


ili kubaini maradhi yanayoathiri jamii yetu. Utafiti huu pia ulichunguza uwepo,
upatikanaji na ubora wa takwimu za vifo hospitalini.

Mbinu za utafiti: Utafiti huu ulifanyika kati ya Julai na Desemba 2016 na


ulihusisha jumla ya hospital 39. Hospitali hizo ni pamoja na hospitali ya Taifa
Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Kanda na Mikoa, Hospital Maalum na hospitali
za Wilaya. Takwimu hizi zilipatikana kutoka kwenye rejesta za hospitali na za
Wakala wa Vizazi na Vifo katika ofisi za Mikoa na Wilaya. Taarifa
zilizokusanywa zilihusu wasifu wa jinsia ya mgonjwa na chanzo cha kifo.

Vyanzo vya vifo viliwekwa katika makundi 45 kulingana na utaratibu wa


makundi ya magonjwa uliowekwa na Shirika la Afya Duniani.

Matokeo: Kwa ujumla kulikuwa na ugumu katika upatikanaji wa takwimu.


Utunzaji wa takwimu katika hospitali nyingi ulikuwa na mapungufu makubwa,
na baadhi ya takwimu hazikupatikana katika baadhi ya hospitali au baadhi ya
miaka iliyokusudiwa. Utunzaji wa takwimu ulikuwa mzuri kiasi katika hospitali
za kanda kuliko za mikoa na wilaya. Matumizi ya majina ya magonjwa kwa
kufuata mwongozo wa kimataifa yalikuwa hafifu.

Jumla ya vifo 247,976 vilitolewa taarifa katika kipindi cha miaka 10 (2006-
2015). Kulikuwa na tofauti kubwa katika idadi ya vifo kati ya jinsia ya kiume na
ya kike. Vifo vingi viliathiri zaidi wanaume kuliko wanawake. Vifo vingi
vilitokea katika hospitali za Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza.

Vifo katika kundi la watoto chini ya miaka 5 vilichangia 20% ya vifo vyote. Vifo
vingi viliathiri kundi la watu wenye umri wa miaka 30-45. Kwa wastani, watu
wengi hufa wakiwa na umri wa miaka 31 (wanaume miaka 33 na wanawake
miaka 29).

Magonjwa yaliyoongoza kusababisha vifo ni malaria (12.8%), magonjwa ya


mfumo wa hewa (10.1%), UKIMWI (8.0%), upungufu wa damu (7.8%) na
magonjwa ya moyo na mfumo wa damu (6.3%).

Vifo kwa baadhi ya magonjwa vilipungua katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Kati ya mwaka 2006 na 2015; vifo kutokana na malaria vilipungua kwa 47%,
UKIMWI kwa 28% na Kifua Kikuu kwa 26%. Hata hivyo, kumekuwa na ongezeko
kubwa la vifo vilivyosababishwa na magonjwa yanayoathiri kundi la watoto
wachanga (chini mwezi mmoja) kwa 128%.

Hospitali za mkoa wa Dar es Salaam zilikuwa na wagonjwa wengi waliokufa


kutokana na malaria, UKIMWI, ajali, maambukizi ya bakteria kwenye damu,
upungufu wa damu, saratani na kifua kikuu. Mkoa huu ulifuatiwa kwa karibu
na Morogoro ambao ulikuwa na vifo vingi vilivyotokana na malaria na kifua
kikuu. Malaria na upungufu wa damu ulichangia vifo vingi kwenye kundi la
watoto chini ya miaka mitano. Vifo vingi kutokana na UKIMWI na Kifua Kikuu
viliathiri watu wazima. Ajali ziliathiri kundi kubwa la vijana; wakati saratani
ziliathiri makundi ya umri wote.

Uchanganuzi wa maradhi katika makundi ya magonjwa ya kuambukiza,


magonjwa yasiyoambukiza na kundi la ajali na majeraha ulionesha tofati
kubwa kati ya mikoa na mikoa. Mikoa ya Pwani, Geita na Katavi iliathirika
zaidi na magonjwa ya kuambukiza na utapia mlo. Vifo kutokana na ajali na
majeraha viliathiri zaidi mikoa Rukwa, Tabora, Singida na Kigoma. Kundi la
magonjwa yasiyoambukiza limeathiri zaidi mikoa ya Ruvuma, Manyara, Dar es
Salaam na Mwanza.

Hitimisho: Utafifi umeianisha changamoto katika ukusanyaji, uchanganuzi na


matumizi ya takwimu katika hospitali zetu. Kumekuwa na matumizi hafifu ya
majina ya magonjwa kwa kutumia mwongozo wa kimataifa. Vyanzo vikuu vya
vifo nchini Tanzania ni malaria, maradhi yanayoathiri mfumo wa kupumua,
UKIMWI, upungufu wa damu na magonjwa ya moyo na mfumo wa damu.
Kumekuwa na ongezeko kubwa la vifo vya watoto wachanga, na ongezeko la vifo
kutokana na magonjwa ya mfumo wa kupumua katika kipindi cha miaka 10
iliyopita.

Mapendekezo: (i) Serikali iandae mwongozo wa ukusanyaji, matumizi, utunzaji


na uhifadhi bora wa takwimu za afya; (ii) Kujenga uwezo wa watumishi wa afya
katika uchanganuzi ili kuboresha matumizi ya takwimu; (iii) Kuimarisha mfumo
wa takwimu wa kielektroniki; (iv) Kuimarisha mafunzo ya madaktari katika
utumiaji wa mwongozo wa kimataifa wa kuanisha magonjwa na vyanzo vya
vifo.