You are on page 1of 1

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu: 255-22-2114512, 2116898 OFISI YA RAIS,
E-mail: press@ikulu.go.tz IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
Tovuti : www.ikulu.go.tz
11400 DAR ES SALAAM.
Faksi: 255-22-2113425
Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 28 Desemba, 2017 amewasilisha fomu yake ya tamko kuhusu rasilimali na
madeni katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo Mtaa
wa Ohio, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuwasilisha fomu hiyo Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Sekretarieti ya


Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kazi inazofanya na amemtaka Kamishna wa
Maadili Jaji Mstaafu Harold Nsekela kutopokea fomu ya kiongozi yeyote ambaye
atakuwa hajawasilisha tamko lake ifikapo tarehe 31 Desemba, 2017.

“Mhe. Jaji Nsekela ikifika tarehe 31 Desemba, ambayo ni siku ya mwisho kwa Mujibu
wa Sheria, weka mstari na usipokee fomu zingine, halafu tuone sheria itafanyaje,
nakutakia kazi njema” amesisistiza Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela amemshukuru na


kumpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kutekeleza matakwa ya kisheria
yanayomlazimu kujaza fomu hizo na amesisitiza kuwa ujazaji wa fomu hizo kwa
viongozi wa umma sio ombi.

“Viongozi hawaombwi kujaza fomu hizi, kuna baadhi wanadhani labda kutuletea hilo
tamko ni fadhila, hapana, sheria ya nchi inahitaji hivyo na kuna sababu zake za msingi”
amesema Mhe. Jaji Mstaafu Nsekela.

Aidha, Mhe. Jaji Mstaafu Nsekela amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa
kuwasilisha taarifa ya akaunti yake ya benki sambamba na tamko hilo, na amekiri
kuwa ameonesha mfano wa kuigwa na viongozi wengine.

Tamko la viongozi wa umma kuhusu rasilimali na madeni linatolewa kwa mujibu wa


kifungu cha 9 na cha 11 cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya
mwaka 1995.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Desemba, 2017