You are on page 1of 16

1

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH


MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA,KWENYE MAADHIMISHO YA SIKUKUU
YA WAFANYAKAZI DUNIANI, MBEYA, TAREHE 1 MEI, 2019

Ndugu Tumaini Nyamhokya, Rais wa Shirikisho


la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu


wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania;

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu


wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Jamhuri


ya Muungano wa Tanzania;

Mwakilishi wa Jaji Mkuu wa Tanzania;

Mheshimiwa Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya


Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi,


Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;

Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri


wengine mliopo;

Mheshimiwa Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa


wa Mbeya pamoja na Wakuu wa Mikoa mingine mliopo;

Waheshimiwa Wabunge mliopo;

Ndugu Makatibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu


mliopo;
2

Jaji Mfawidhi wa Divisheni ya Kazi ya Mahakama Kuu pamoja na


Waheshimiwa Majaji wengine mliopo;

Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani nchini;

Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania;

Waheshimiwa Mabalozi mliopo;

Ndugu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya;

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

Ndugu Qambos Sulle, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya


Wafanyakazi;

Dkt. Yahya Msigwa, Katibu Mkuu wa Shirikisho


la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA);

Viongozi Wengine mliopo wa Vyama Vishiriki vya TUCTA;

Viongozi Wengine wa Serikali mliopo;

Viongozi wa Vyama vya Siasa na Viongozi wa


Dini mliopo;

Ndugu Wafanyakazi Wenzangu;

Ndugu Wana-Mbeya, Mabibi na Mabwana:

Najisikia furaha kubwa sana, kwa mara nyingine tena, kuweza

kushiriki Siku hii muhimu ya Wafanyakazi, ambayo huadhimishwa

duniani kote kila mwaka. Napenda kwanza kabisa, kumshukuru

Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutuwezesha kuiona siku ya leo.


3

Aidha, kwa namna ya pekee, napenda kutoa shukrani zangu nyingi

na za dhati kwa Uongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi

Tanzania (TUCTA), wakiongozwa na Rais wa Shirikisho, Ndugu

Tumaini Nyamhokya, kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi kwenye

Maadhimisho haya. Leo ni mara yangu ya nne TUCTA wamenialika

kuwa Mgeni Rasmi tangu nimekuwa Rais. Mialiko hiyo ni ishara

kwamba, vyama vya wafanyakazi nchini, vinaiunga mkono Serikali

ninayoiongoza. Ninawashukuru sana na napenda niwahakikishie kuwa

Serikali itaendelea kushirikiana nanyi katika kushughulikia masuala

yenu pia kwa lengo la kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika

Taifa letu.

Napenda pia kutumia fursa hii kuungana na wote walionitangulia

kuzungumza kuwashukuru na kuwapongeza Waratibu wa shughuli hii,

Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao wa

Mawasiliano Tanzania (TEWUTA) kwa maandalizi mazuri ya Sherehe

hizi. Hongereni sana. Sherehe zimefana.

Vilevile, nawashukuru wenyeji wetu, wananchi wa Mbeya

mkiongozwa na Mkuu wenu wa Mkoa, kwa makaribisho yenu mazuri na

kwa kujitokeza kwenu kwa wingi kwenye Maadhimisho haya. Ahsanteni

sana wana-Mbeya. Waswahili husema “shughuli ni watu”.

Nawashukuru pia Viongozi wengine wa Serikali ambao

wamehudhuria Maadhimisho haya, wakiongozwa Mheshimiwa


4

Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu; Mheshimiwa Spika na

Naibu Spika, Waheshimiwa Mawaziri, Waheshimiwa Wabunge,

Viongozi wa Ulinzi na Usalama, n.k. Uwepo wenu hapo unadhihirisha

kuwa mnawapenda sana wafanyakazi.

Ndugu Wafanyakazi Wenzangu,


Mabibi na Mabwana;
Siku ya Wafanyakazi au maarufu Mei Mosi, ni siku ambayo dunia

huitumia kuenzi na kutambua mchango unaotolewa na wafanyakazi

katika kuleta maendeleo. Na hii ni kwa sababu, kama mjuavyo,

maendeleo; katika ngazi yoyote ile, iwe mtu mmoja mmoja, familia,

taasisi, au nchi; huwa ni matokeo ya kufanya kazi. Waingereza wana

usemi usemao “all wealth is the product of labour” na mwingine unasema

“Without labour, nothing prospers”. Hii yote ni katika kudhihirisha kuwa

kazi na wafanyakazi ni muhimu sana katika kuleta maendeleo.

Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii, kwa niaba yangu binafsi na

kwa niaba ya Serikali na Watanzania wote; kuwapongeza wafanyakazi

wote hapa nchini kwa kuungana na wafanyakazi wengine duniani katika

kuadhimisha Siku hii muhimu. Aidha, nawapongeza kwa mchango

wenu mkubwa mnaoutoa katika kuiletea maendeleo nchi yetu. Napenda

niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nanyi, ikiwa ni

pamoja na kushughulikia changamoto zenu mbalimbali. Ni imani yangu

kuwa mtaendelea kufanya kazi kwa bidii, kama Serikali ya Awamu wa

Tano inavyosisitiza kuwa “Hapa Kazi tu”. Tukifanya kazi kwa bidii,

tutafanikiwa katika lengo letu la kuiletea maendeleo nchi yetu.


5

Ndugu Wafanyakazi, Mabibi na Mabwana;


Hivi punde tumetoka kusikia Risala nzuri ya TUCTA iliyosomwa

na Katibu wake Mkuu, Bwana Msigwa. Kupitia Risala hiyo, Katibu

TUCTA ameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua katika

kujenga miundombinu na kuboresha huduma za jamii. Aidha, Risala

imetaja baadhi ya kero za wafanyakazi pamoja na kutoa mapendekezo

yenye nia ya kuchochea ukuaji uchumi nchini.

Namshukuru Katibu Mkuu wa TUCTA kwa Risala hiyo nzuri; na

leo napenda nimpongeze kwa kujitahidi kuisoma kwa muda mfupi. He

was brief and very clear. Hongera sana. Napenda nikuhakikishie Ndugu

Katibu Mkuu wa TUCTA pamoja na wafanyakazi wote nchini kuwa,

Serikali imepokea Risala yenu na tunaahidi kuwa yote yaliyomo kwenye

Risala, tutayafanyia kazi. Hata hivyo, naomba mniruhusu nizungumzie

baadhi ya masuala machache yaliyomo kwenye Risala hiyo.

Ndugu Wafanyakazi, Mabibi na Mabwana;

Baadhi ya hoja zilizotolewa kwenye Risala ni pamoja na maombi ya

kutaka Bodi za Mishahara kukutana; kupunguza viwango vya kodi kwa

watumishi wote; suala la watumishi wa darasa la saba na uboreshaji wa

mazingira na usalama sehemu za kazi.

Napenda niseme kuwa, binafsi, sina tatizo na Bodi za Mishahara

kukutana; na kusema kweli, sielewi ni kwa nini hazikutani. Kwangu

mimi hata wakitaka kukutana leo, sina shida. Hivyo basi, namwagiza
6

Waziri mwenye Dhamana kuhakikisha Bodi hizo zinakutana. Hata hivyo,

napenda kutoa angalizo kuwa vikao vyao visiwe kichochoro cha kutumia

fedha za Serikali vibaya.

Kuhusu suala la kupunguza viwango vya kodi na lenyewe sina

matatizo nalo. Kama tuliweza kushusha kodi kutoka asilimia 11 had

asilimia 9 kwa watumishi wa kima cha chini; bado tunaweza kuendelea

kujadiliana kwa ngazi nyingine. Jambo la msingi na muhimu kwa

Viongozi wa TUCTA na wafanyakazi ni kutambua kuwa Serikali ina

sababu za msingi za kutofautisha viwango vya kodi kulingana na

madaraja ya mishahara.

Kuhusiana na suala la watumishi wa darasa la saba, napenda

niwahakikishie kuwa, Serikali hii haina ubaguzi kwenye suala la ajira.

Katika kuthibitisha hilo, kati ya Watumishi 525,506 ambao Serikali

imeajiri nchi nzima, wenye elimu ya darasa la saba wapo 98,615.

Kuhusu suala la uboreshaji wa Mazingira na Usalama sehemu za

Kazi, natoa wito kwa waajiri wote kuhakikisha wanazingatia Sheria za

Kazi, ikiwemo Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi. Aidha, Waajiri

hawana budi kutekeleza matakwa mengine ya kisheria, ikiwemo kutoa

mikataba ya ajira na pia kuruhusu uwepo wa vyama vya wafanyakazi

sehemu zao za kazi. Kama mtakavyokumbuka, suala hili nimelieleza

mara nyingi. Hivyo, kwa mara nyingine tena, naziagiza mamlaka husika

kuhakikisha masharti hayo ya sheria yanatekelezwa.


7

Ndugu Rais wa TUCTA;


Ndugu Katibu Mkuu wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi Wenzangu;
Sambamba na hayo, kama nilivyoeleza awali, kwenye Risala yenu

mmetoa mapendekezo yenye nia ya kukuza uchumi na kuongeza fursa

za ajira. Mmeshauri tuongeze bidii kwenye ujenzi wa viwanda

vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini; kuongeza bidii katika

kutangaza vivutio vyetu vya utalii; kusimamia vizuri masuala ya uchumi

wa bahari, ikiwemo kununua meli ya mizigo itakayotoa huduma

baharini, n.k.

Mapendekezo yenu yote ni mazuri; na tunakubaliana nayo kwa

asilimia 100, japokuwa mengine, utekelezaji wake utategemea

upatikanaji wa fedha. Hata hivyo, napenda niwaarifu kuwa, baadhi ya

mapendekezo tumeanza kuyafanyia kazi. Mathalan, kuhusu uchumi wa

bahari; tumeanza kuchukua hatua za kulifufua Shirika letu la Uvuvi

(TAFIRI), ambapo marafiki zetu wa Japan na Korea, wameonesha nia ya

kutuunga mkono. Na kuhusu ununuzi wa Meli ya Mizigo, hilo na

lenyewe halina shida. Tumeshaanza kujenga meli mpya za mizigo Ziwa

Nyasa; na tunaendelea na ujenzi wa meli nyingine Ziwa Victoria na

Tanganyika. Tukishishamaliza huko, tutaelekeza nguvu zetu katika

Bahari ya Hindi.

Kwa upande wa utalii, ninyi wenyewe ni mashahidi. Tunajitahidi

sana kutangaza vivutio vyetu vya utalii, vikiwemo vilivyo kwenye

Ukanda huu wa Nyanda za Juu Kusini; ambavyo kwa bahati mbaya, kwa
8

muda mrefu vilikuwa havitangazwi. Na kutokana na jitihada tulizoanza

kuzifanya, idadi ya watalii imeendelea kuongezeka. Mwaka juzi

tulipokea watalii milioni 1.2; lakini mwaka jana tumepokea watalii

milioni 1.5.

Hivi majuzi mmeshuhudia wenyewe tumepokea takriban watalii

1,000 kutoka Israel. Aidha, Bodi yetu ya Utalii imeingia makubaliano na

Kampuni moja ya China kuleta watalii 10,000 kwa mwaka, ambapo kundi

la kwanza la watalii 342 linatarajiwa kuwasili nchini tarehe 12 mwezi

huu.

Lakini katika juhudi hizo hizo za kuvutia watalii wengi zaidi; na

kwa kutambua kuwa watalii wengi husafiri kwa ndege; tunafanya

upanuzi wa viwanja vya ndege 11 na tayari tumenunua ndege mpya 8

kwa mpigo. Juzi mmeona, kwa mara ya kwanza, ndege ya abiria imetua

kwenye Uwanja wa Ndege wa Nduli, Iringa, baada ya Uwanja kufanyiwa

matengenezo.

Ndugu Wafanyakazi, Mabibi na Mabwana;

Ni kweli pia kuwa, kutokana na jitihada mbalimbali tulizozifanya

kwa kushirikiana na ninyi wafanyakazi, Serikali imeweza kuongeza

ukusanyaji wa mapato. Kwa mfano, mapato ya kodi yameongezeka

kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwezi mwaka 2015 hadi

kufikia shilingi trilioni 1.3 hivi sasa. Mapato yasiyo ya kodi pia

yameongezeka, na hasa baada ya kudhibiti wizi wa rasilimali zetu na pia


9

kuyabana mashirika na kampuni kulipa gawio. Mathalan, mwaka jana,

Wizara ya Madini ilipanga kukusanya maduhuli ya shilingi bilioni 190;

lakini wakakusanya shilingi bilioni 301. Aidha, mashirika na kampuni

zilitoa gawio la shilingi bilioni 717.56 kwa Serikali; kutoka shilingi

bilioni 130.686 Mwaka 2014/2015.

Haya ni mafanikio makubwa, ingawa changamoto bado zipo. Na

changamoto kubwa iliyopo ni kwamba, gharama za uendeshaji wa

Serikali bado zipo juu. Kwa mfano, kila mwezi inatulazimu kutumia

takriban shilingi bilioni 580 kulipa mishahara; na wakati huo huo

tunatakiwa kulipa madeni ya mikopo ya nyuma, kutekeleza miradi ya

maendeleo pamoja na kulipia OC. Hivyo, mnaweza kujionea wenyewe,

ni kiasi gani kinabaki baada ya matumizi hayo.

Na hapo ndiyo tumekuwa tukijiuliza maswali mengi kuhusu

namna ya kutumia kiasi hicho kinachobaki. Tumekuwa tukijiuliza sana,

kama ambavyo mkulima mwenye mbegu hujiuliza wakati wa njaa. Je,

azitumie mbegu zake kwa chakula na baada ya muda mfupi arudi tena

kwenye njaa; ama azitunze kusubiri msimu wa mvua ili azipande na

kumletea mavuno mengi. Tumekuwa pia tukijiuliza kama ambavyo

mfanyabiashara hujiuliza wakati wa mtikisiko wa kiuchumi au biashara;

je, autumie mtaji wake wote kutatua shida alizonazo kwa wakati huo,

ama atafute biashara au shughuli nyingine itakayomwongezea mapato.

Tumekuwa tumejiuliza sana maswali hayo.


10

Na kama nilivyoeleza kwenye Sherehe za Mei Mosi mwaka jana,

baada ya kutafakari kwa kina, sisi mliotupa dhamana ya kuwaongoza,

tuliona ni busara tutumie kiasi kidogo tunachobakiwa nacho kuwekeza

kwenye miradi ya maendeleo itakayosisimua na kuchochea uchumi

shughuli za kiuchumi. Shughuli ambazo zitasaidia kuongeza fursa za

ajira na kukuza uchumi kwa kasi.

Ni kwa kuzingatia hayo yote, tuliamua kutumia fedha inayobaki

kuanza kujenga reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa

gharama ya shilingi trilioni 7.026. Tunajenga pia barabara; na napenda

nitumie fursa hii kuwaarifu kuwa, jana Benki ya Maendeleo ya Afrika

imeidhinishia nchi yetu mkopo wa shilingi bilioni 415.3 kwa ajili ya

kujenga barabara ya mzunguko ya njia nne katika Jiji la Dodoma yenye

urefu wa kilometa 110.

Zaidi ya hapo, tumeamua kukarabati na kujenga meli mpya

kwenye Maziwa yetu Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa kwa

takriban shilingi bilioni 287.9 na pia tunapanua Bandari zetu kuu tatu za

Dar es Salaam, Mtwara na Tanga kwa zaidi ya shilingi trilioni 1.2.

Tunafanya upanuzi wa viwanja vya ndege 11 na tumenunua ndege mpya

8. Aidha, tunatekeleza mradi mkubwa wa umeme katika Bonde la Mto

Rufiji ambao utagharimu zaidi ya shilingi trilioni 6.5.

Ni imani yetu kuwa, miradi hii yote itakapokamilika, itarahisisha

na kupunguza gharama za usafiri na upatikanaji wa nishati ya umeme;


11

na hivyo, kuchochea shughuli za kiuchumi, ikiwemo viwanda, kilimo,

biashara, uvuvi, ufugaji, utalii, uchimbaji madini. Na hayo yakitokea,

uchumi wetu utaimarika na mapato ya Serikali yataongezeka.

Ndugu zangu Wafanyakazi, sambamba na kutekeleza miradi hiyo ya

miundombinu, tunaendelea kuimarisha na kuboresha upatikanaji wa

huduma muhimu za jamii, hususan elimu, afya na maji. Kwa mfano, kwa

upande wa afya, tunajenga Hospitali za Wilaya 67 kwa gharama ya

shilingi bilioni 105, tumekarabati vituo vya afya 352 kwa shilingi bilioni

184.67 na kuzipatia vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 41.6.

Tumeongeza pia bajeti ya afya kutoka shilingi bilioni 31 hadi shilingi

bilioni 270. Kwenye elimu nyote mnafahamu kwamba tunatoa elimu bila

malipo, tunajenga miundombinu na tumeongeza mikopo ya vyuo vikuu.

Kwa upande wa maji, tunayo miradi mingi mikubwa tunaitekeleza,

ikiwemo Mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenye miji ya

Nzega, Igunga, Tabora na Sikonge pamoja na mradi mwingine katika Jiji

la Arusha, ambayo kwa pamoja tunatumia zaidi ya shilingi trilioni 1.

Zaidi ya hapo, tumepata mkopo kutoka India wenye thamani ya shilingi

trilioni 1.2 kwa ajili ya miradi ya maji kwenye miji 28, ambapo Mkoa wa

Mbeya umepata miradi miwili yenye thamani ya shilingi bilioni 22.5.

Tunatekeleza pia miradi ya kusambaza umeme vijijini.

Ni wazi kuwa uboreshaji huu wa huduma hizi muhimu za jamii

utasaidia kupunguza gharama za maisha kwa Wafanyakazi na


12

Watanzania kwa ujumla. Hii ni kwa sababu huduma za maji, afya na

elimu sasa zinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

Ndugu Viongozi wa TUCTA;


Wafanyakazi Wenzangu;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kwa kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo na kuboresha huduma

za jamii, haina maana kuwa tumeacha kushughulikia masuala ya maslahi

ya wafanyakazi. La hasha! Tumeendelea kuyashughulikia. Mathalan,

baada ya kukamilisha zoezi la uhakiki wa wafanyakazi hewa na wenye

vyeti feki, tangu Mwaka wa Fedha uliopita, tumeanza kutoa nyongeza ya

mwaka ya mshahara (annual increment) kwa watumishi 505,985 kwa

gharama ya shilingi bilioni 72.8 ambapo shilingi bilioni 37.2 zimelipwa

kwa walimu 270,878 na kiasi kingine cha shilingi bilioni 35.7 kwa

watumishi wengine wapatao 235,107.

Mbali na nyongeza ya mwaka ya mshahara, kuanzia mwezi

Novemba 2015, tumelipa malimbikizo ya mishahara yenye thamani ya

shilingi bilioni 75.5 kwa watumishi 50,386. Kati yao, walimu ni 28,115 na

wamelipwa shilingi bilioni 27.9. Vilevile, tumelipa shilingi bilioni 9.5

kwa watumishi wastaafu 1,829, ambao nao walikuwa wakiidai Serikali.

Ndugu Wafanyakazi wenzangu, miongoni mwa mabango ya Mei Mosi

mwaka huu, mojawapo limeandikwa “tupandishe madaraja ili na sisi

tupande bombardier”. Napenda niwaarifu kuwa, tangu mwezi Novemba

2015, tumewapandisha madaraja/vyeo watumishi 118,989 kwa gharama


13

ya shilingi bilioni 29.5, ambapo walimu ni 75,502 na wamelipwa shilingi

bilioni 16.3 na watumishi wasio walimu ni 43,487 na wamelipwa shilingi

bilioni 13.2. Kwenye Mwaka ujao wa Fedha, tumepanga kuwapandisha

vyeo watumishi 193,116. Sambamba na hayo, tumelipa madai mbalimbali

yasiyo ya mishahara yenye thamani ya shilingi bilioni 291.3. Na mengi

ya madai hayo, yalikuwepo kwa zaidi ya miaka 10.

Kama mlivyoona, kwenye maeneo mengi nimeamua kutofautisha

kati ya watumishi walimu na wasio walimu, kwa kuwa walimu ni zaidi

ya asilimia 50 ya watumishi wote Serikali.

Ndugu zangu Wafanyakazi;


Ukiachilia mbali hayo niliyoyaeleza, Serikali imelipa kiasi cha

shilingi trilioni 1.5 kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Kabla ya kulipa

fedha hizo, Mifuko hiyo ilikuwa ikidai Serikali kiasi cha shilingi trilioni

1.6 kwa kushindwa kupeleka michango ya watumishi wake tangu

mwaka 2013. Hii iliifanya Mifuko ishindwe kulipa mafao ya wastaafu.

Lakini baada ya kulipa deni hilo sasa wanawalipa wastaafu.

Lakini, kama mtakavyokumbuka, kufuatia uamuzi wa Serikali

kuunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, liliibuka sekeseke kubwa

kuhusu kikokotoo kipya kilichopendekezwa. Wafanyakazi wengi

hawakuunga mkono kikokotoo hicho. Hivyo, baada ya kutafakari kwa

kina, ilibidi tuchukue uamuzi mgumu wa kuendelea na kikokotoo cha

zamani. Nasema ulikuwa uamuzi mgumu kwa vile, kikokotoo hicho

kinachotumika nchini hakitumiki mahali kokote duniani. Ni sisi tu ndiyo


14

wenye kukitumia. Hata kwenye nchi zilizoendelea hawakitumii. Na hii

ndiyo sababu, Mifuko yote mitano ya Hifadha ya Jamii ilikuwa kwenye

hali ngumu kiuchumi. Na hali hiyo ilichangiwa zaidi na Mifuko hiyo

kujiingiza kwenye miradi isiyo na tija. Hata hivyo, kutokana na kilio cha

wafanyakazi, tuliamua kuubeba mzigo huo mzito ili kuwalinda

wafanyakazi wetu.

Masuala mengine ambayo Serikali imefanya kwa wafanyakazi ni

pamoja na kujenga nyumba za walimu 11,078 na za watumishi wa afya

301. Zaidi ya hapo, baada ya kukamilisha zoezi la uhakiki, tumeajiri

watumishi wapya 42,735 ambao kwa mwezi wanalipwa shilingi bilioni

25.8. Aidha, kwenye Mwaka wa Fedha 2019/2020 tumepanga kuajiri

watumishi wengine wapya wapatao 45,000. Zaidi hayo, miradi ya

miundombinu tunayoitekeleza (reli, umeme, viwanja vya ndege,

barabara, n.k.) imetengeneza ajira nyingine nyingi.

Haya yote yanadhihirisha kuwa Serikali inawapenda sana

Wafanyakazi. Hivyo basi, nawasihi wafanyakazi kuendelea kuchapa kazi

kwa bidii ili kuiletea maendeleo nchi yetu. Wazee wetu wa zamani

walijitoa mhanga kuikomboa nchi yetu kisiasa, ni jukumu letu kizazi cha

sasa, kujitoa mhanga kuikomboa nchi yetu kiuchumi.


15

Ndugu Viongozi wa TUCTA;


Wafanyakazi Wenzangu;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu inasema:

“Tanzania ya Uchumi wa Kati inawezekana, Wakati wa Mishahara na

Maslahi Bora kwa Wafanyakazi ni Sasa”. Na kutokana na kaulimbiu

hiyo, Katibu Mkuu wa TUCTA amenikumbusha kuhusu ahadi yangu

niliyoitoa mwaka jana, wakati wa Sherehe kama hizi zilizofanyika Iringa;

kwamba, kabla sijaondoka madarakani, nitaongeza mshahara.

Napenda, kwanza, nimkumbushe Katibu Mkuu wa TUCTA kuwa

bado sijaondoka madarakani. Aidha, kama nilivyoeleza, kutokana na

hatua tulizochukua na tunazoendelea kuzichukua, uchumi wa nchi yetu

umeanza kuimarika. Halikadhalika, miradi mingi tunayoitekeleza

imeanza kuwanufaisha Watanzania, wakiwemo Wafanyakazi. Hivyo

basi, nitumie fursa kuwasihi Wafanyakazi nchini kuendelea kuwa na

moyo wa subira, maana subira yavuta heri. Waingereza husema “Before

the reward there must be labour. You plant before you harvest”.

Ndugu Viongozi wa TUCTA;


Wafanyakazi Wenzangu;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha kwa kurudia tena kuwashukuru Viongozi

wa TUCTA kwa kunialika. Aidha, nawashukuru kwa ushirikiano

mkubwa mnaoutoa kwa Serikali. Hatuna budi kuendeleza ushirikiano

huu.
16

Nawashukuru pia wageni wetu walioungana nasi kwenye

Maadhimisho haya, wakiwemo Waheshimiwa Mabalozi. Lakini, kwa

namna ya pekee, namshukuru Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani

kwa kushiriki kwenye Maadhimisho haya. Napenda nimhakikishie kuwa

Tanzania itaendelea kuheshimu Mikataba yote ya Kimataifa inayohusu

masuala ya kazi, ambayo tumeisaini na kuiridhia.

Mwisho lakini sio kwa umuhimu, narudia tena kuwashukuru

wana-Mbeya kwa kujitokeza kwa wingi kwenye Maadhimisho haya.

Nawasihi mwendelee kuchapa kazi kwa bidii tukikumbuka kuwa “Hapa

Kazi tu” ndiyo kaulimbiu yetu kuu katika Awamu hii ya Tano.

Mungu Wabariki Wafanyakazi wa Tanzania!

Mungu Ibariki Tanzania!

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”