You are on page 1of 3

1

SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA

TAARIFA YA MKURUGENZI MKUU WA NHC, BW. NEHEMIAH KYANDO MCHECHU, KATIKA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI WAKATI WA UZINDUZI KAMPENI YA UUZAJI WA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU NCHI NZIMA IJULIKANAYO KAMA NYUMBA YANGU - MAISHA YANGU, TAREHE 03, OKTOBA, 2013 Ndugu Wanahabari, Kwanza kabisa napenda kuwashukuru wote kwa kuitikia mwaliko wetu wa kuja kushiriki katika tukio hili muhimu. Tunatambua umuhimu wa Vyombo vya habari katika uendelezaji wa sekta ya nyumba hapa nchini na kwamba ushirikiano wenu mnaotupatia mara kwa mara umetuwezesha kubadili taswira ya sekta ya Nyumba na Shirika kwa ujumla na kwa hakika mmetutia moyo kufikia lengo la serikali la kuwapatia Watanzania nyumba bora. Ndugu wanahabari, Shirika linaendelea kutekeleza mpango mkakati wake kwa unaolenga kujenga nyumba15,000 kufikia mwaka 2015, ili kujaribu kukabiliana na uhaba wa nyumba unaokadiriwa kufikia nyumba milioni 3 hivi sasa ambao unaongezeka kwa nyumba 200,000 kila mwaka. Katika nyumba 15,000 zinazojengwa, nyumba 5000 zitakuwa za gharama nafuu kwa ajili ya watu wa kipato cha kati na chini. Kama mnavyokumbuka, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete Desemba 13, 2012 akiwa Kibada huko Kigamboni, alizindua mradi wa majaribio na kuanza kwa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika maeneo mbalimbali hapa nchini, ujenzi unaofanywa na NHC. Ndugu Wanahabari, Tangu Rais Kikwete alipozindua ujenzi wa nyumba za gharama nafuu huko Kibada, tayari shirika limeanza miradi mbalimbali katika mikoa 11 na leo ndiyo tunatangaza rasmi uzinduzi wa program ya ujenzi wa nyumba 5000 (elfu tano) ijulikananyo kama Nyumba Yangu Maisha Yangu. Program hii inalenga kuainisha na kutekeleza mpango mkakati wa Shirika la Nyumba. Katika program hii Shirika la Nyumba la Taifa litaendelea kushirikiana na Halmashauri mbalimbali ili kuhakikisha kuwa, kwa pamoja tunawawezesha walengwa kuwa na nyumba zao na hivyo kuboresha maisha yao.

Ndugu wana habari, Ni dhamira na Heshima ya kila mwanadamu kuwa na nyumba na sio nyumba tu bali nyumba iliyobora. Na mara nyingi ujenzi wa nyumba umekuwa ukichukua muda mrefu sana kwa watu kuweza kumaliza nyumba zao wanazokuwa wameamua kujenga. Tunatambua ya kwamba ujenzi kwa kutumia pesa zako unachukua muda mrefu wakati ukiendelea kulipa kodi pale unapoishi sasa. Mbali ya hayo, mara nyingi tunatambua ya kuwa ujenzi wa nyumba za mtu mojamoja kuna matatizo ya ulinzi na usalama, miundo mbinu, uhakika wa maji, na matatizo kedekede. Prorgam ya Nyumba yangu Maisha Yangu inakuwezesha kuishi maisha bora ukiwa kwenye makazi yaliyozingatia vitu vyote muhimu ambavyo hauvipati kwenye uendelezaji wa miji kwa sasa, na kukuwezesha uendelea kufaidi matunda ya nyumba yako kipindi cha maisha yako ukiwa na nguvu za kulitumikia Taifa. Inawezekana it is possible Ndugu wana habari, leo tumewaita ili muweze kuujulisha uma wa watanzania kwamba tarehe 13 October 2013 tutaanza rasmi kuuza nyumba za miradi mbali mbali iliyokwisha anza na imefikia katika hatua mbalimba nchi nzima. Tumeona ni vyema kuwajulisha na wao waanze maandalizi ili kuweza kumiliki Nyumba zao. Utekelezaji wa program ya Nyumba Yangu Maisha Yangu umeanza katika mikoa 11 na ni matarajio yetu kufikia mikoa yote kabla ya mwaka 2015 tutakapokamilisha utekelezaji wa awamu ya kwanza ya program hii. Tumeanza na nyumba (2000) elfu mbili maeneo yafuatayo ambazo zimefikia katika hatua tofauti, maeneo ambao miradi imeanza ni kama ifuatavyo: Maeneo yaliyoanza kunufaika na mpango huu ni pamoja na Mvomero (Morogoro), Mkinga (Tanga), Lindi, Mkuzo (Ruvuma), Bombambili (Geita), Mlole (Kigoma), Ilembo (Katavi), Kongwa (Dodoma), Unyankumi (Singida), Kibada ( Dar Es Salaam) na Mrara (Babati). Miji ambayo itafuatia hivi karibuni ni pamoja na Sumbawanga (Rukwa), Mwongozo na Kibada awamu ya pili (Dar Es Salaam), SafariCity (Mateves), Monduli, Longido (Arusha), Uyui, Nzega (Tabora), Manyara, Buswelu (Mwanza), Chalinze (Pwani) Kyerwa, Muleba (Kagera), Iwambi na Mbalali (Mbeya), Masasi (Mtwara). Maeneo tuliyoyataja ni yale ambayo upatikanaji wa ardhi na ushirikiano wa Halmashauri za Wilaya na Mikoa katika utekeleza wa mradi umekuwa wakuridhisha. Ndugu Wanahabari, Utekelezaji wa program ya Nyumba Yangu Maisha Yangu utakapokamilika utawapatia makazi bora wananchi wapatao 18,000 na kutoa ajira zipatazo 200,000 kwa ujumla wake.. Aidha, kutakuwa na huduma za kijamii ndani ya Estate hizo kama maduka, shule, hospitali, viwanja vya kuchezea watoto na vivutio vingine mbalimbali. Aidha, Halmashauri zitapata kodi mbalimbali na kuwezesha watumishi wa umma kuweza

kweza kutoa huduma maeneo mbalimbali ya nchi kwa kuwa sasa kutakuwa na nyumba za uhakika, tofauti na kabla ambapo wamekuwa wakikwepa kupangwa katika maeneo ya mbali. Uuzaji wa nyumba hizi utabebwa na kauli mbiu ya kampeni ya Nyumba Yangu; Maisha Yangu. Lengo la kaulimbiu likiwa ni kwanza kuwapa taarifa wananchi juu ya mpango huu wa Shirika, lakini pili ni kuwaandaa ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika manunuzi ya nyumba hizi zinazoendelea kujengwa katika maeneo takribani yote nchini. Aidha, kauli mbiu hii inaweka mbele thamani ya maisha ya mwanadamu anapokuwa na nyumba yake, kwa kuwa muda na mipango mingi ya maisha ya binadamu hufanyika akiwa katika nyumba yake. WITO: Ningependa kusisitiza kwamba Halmashauri mbali mbali zishirikiane na Shirika la Nyumba la Taifa katika shughuli za unjenzi wa makazi bora, upangaji wa miji, upatikanaji wa miundo mbinu kwenye maeneo yanayojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa na muhimu zaidi zinunue nyumba zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa kwa ajili ya wafanyakazi wa sekta muhimu kama walimu na madaktari. Kwa maelezo zaidi wananchi wanaweza kufanya mawasiliano na Makao Makuu ya Shirika, Ofisi zetu za Mikoa au kupitia baruapepe ili kuweza kujiandaa mapema kwa ajili ya kuweza kuingia kwenye mchakato ulio wazi wa manunuzi ya nyumba hizo. Baada ya kusema hayo sasa ninayo furaha na heshima kubwa kuwaomba nyie wanahabari, mkawaandae wananchi ili waweke akiba zao za kununua nyumba mara tutakapowatangazia Oktoba mwaka huu.

Ahsanteni kwa kunisikiliza. Ndugu Wanahabari,

You might also like