You are on page 1of 5

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI

Simu: 255-26-2323201-7 Jengo la LAPF Ghorofa ya 6,


Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barabara ya Makole
Barua pepe: gcu@nje.go.tz
Tovuti : www.foreign.go.tz S.L.P. 2933,
Nukushi: 255-26-2116600 DODOMA ,
Tanzania.

TAARIFA KWA UMMA

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa katika baadhi ya vyombo vya habari na


kutoka kwa baadhi ya wanasiasa kuishutumu Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kufuatia hatua ya kukamata na kupiga mnada
mifugo iliyoingizwa nchini bila kufuata sheria. Aidha, taarifa hizo zinajenga
sintofahamu kuhusiana na suala la vifaranga vya kuku vilivyoteketezwa
kufuatia kuingizwa nchini bila kufuata sheria. Baadhi ya taarifa hizo
zimeenda mbali zaidi na kudai kuwa hatua hizi zinaweza kudhoofisha
mahusiano yetu na nchi jirani.

Kadhalika, kufuatia suala hilo la kupigwa mnada kwa ngombe walioingia


nchini kinyume cha sheria, na wenye ngombe hao kukaidi kuondoa mifugo
yao hata baada ya kupewa muda kufanya hivyo, na kufuatia kuteketezwa
kwa vifaranga vilivyoingia nchini kinyume cha sheria na kanuni, Serikali ya
Kenya ilimwita Balozi wetu aliyeko Nairobi kutaka maelezo. Balozi wetu
alisikiliza maelezo ya Serikali ya Kenya na akatumia fursa hiyo kuelezea
masuala haya kwa Serikali ya Kenya. Vile vile Serikali imepokea barua
kutoka Serikali ya Kenya kuhusu masuala haya, na Serikali itaijibu barua
hiyo kutoa ufafanuzi.

Serikali inapenda kuufahamisha umma kwa ujumla kuwa uingizwaji wa


mifugo na bidhaa zake nchini Tanzania huongozwa na sheria za nchi,
makubaliano ya kikanda na kimataifa.

Sheria na taratibu hizi ni pamoja na:


(i) Sheria ya Magonjwa ya Wanyama (Animal Disease Act) Na. 17 ya
mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2007 na 2010, ambazo

1
zinatumika kudhibiti na kukagua uingizaji wa mifugo na mazao yake
katika maeneo ya mpakani, bandarini na viwanja vya ndege;
(ii) Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali ya Vyakula vya Wanyama
(Grazing-land and Animal Feed Resources Act) Na. 13 ya mwaka 2010
ambayo inasimamia nyanda za malisho na ubora wa malighafi za
kusindika vyakula vya mifugo;
(iii) Zuio (quarantine) la uingizaji ndege na mazao yake nchini la mwaka
2006, kutokana na uwepo wa ugonjwa hatari wa Homa ya Mafua
Makali ya Ndege katika nchi mbalimbali duniani. Ugonjwa huo
umejitokeza kwenye nchi jirani ya Uganda mwanzoni mwa mwaka
2017 na hivyo kuiweka nchi yetu katika hatari ya kuambukizwa
ugonjwa huu iwapo zuio hili litakiukwa. Zuio hilo halijaondolewa hadi
leo.
(iv) Ukweli kwamba katika Jumuiya ya Afrika Mashariki mifugo na bidhaa
za mifugo zinavuka mipaka kwa utaratibu maalum kupitia kwenye vituo
vya mipakani ambapo maofisa mifugo kutoka pande zote za mipaka
hufanya shughuli ya udhibiti.
Utekelezaji wa sheria na makubaliano haya hufanyika bila ubaguzi wa uraia
wa mwingizaji wa mifugo au nchi inakotoka mifugo hiyo. Nchi zote duniani,
zikiwemo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, zinadhibiti
uingizwaji wa mifugo na mimea katika nchi zao. Udhibiti huu hufanyika
katika viwanja vya ndege, bandari na vituo vya mipakani. Kwa mfano, katika
Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani cha Namanga, wapo maofisa wa
mifugo na kilimo kutoka Kenya na Tanzania wanaodhibiti uingizwaji wa
mifugo na mimea kwenye nchi zao.

Katika utekelezaji na usimamizi wa sheria hii, ilibainika kuwa idadi kubwa ya


mifugo kutoka nchi za jirani imeingizwa nchini pasipo kufuata sheria na
taratibu zilizopo. Serikali iliagiza mifugo hiyo irudishwe kwenye nchi ilikotoka
kwani ilikuwa inahatarisha mazingira na kuongeza uwezekano wa
kusambaa magonjwa ya mifugo. Serikali ilitoa muda wa kutosha kwa
wamiliki wa mifugo hiyo kuiondoa nchini. Tahadhari ilitolewa kwamba muda
uliotengwa ukifikia ukomo, mifugo hiyo itakamatwa na kushugulikiwa kwa
mujibu wa sheria za nchi.

Pamoja na agizo hilo, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na


Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilituma Waraka wa Kidiplomasia kwa
Serikali za Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda, ikizihimiza kuwataka raia
wao walioingiza mifugo nchini isivyo halali waiondoe. Wamiliki wengi walitii
agizo hilo la Serikali ya Tanzania na kuondoa mifugo yao nchini.

2
Hata hivyo, wapo wamiliki wachache kutoka nchi za jirani waliokaidi agizo
hilo na hivyo ngombe wapatao 1113 walikamatwa katika Wilaya ya
Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro na kupigwa mnada baada ya wamiliki wake
kushindwa kujitokeza. Katika mkoa huo wa Kilimanjaro wapo ngombe 74
ambao wamiliki wake walijitokeza, wakalipa faini kwa amri ya mahakama na
kuondoka na ngombe wao. Katika Mkoa wa Kigoma ngombe 324 ambao
wamiliki wake hawajajitokeza wamekamatwa na hatua stahiki
zinachukuliwa. Aidha, katika mkoa huo wa Kigoma ngombe 728
walikamatwa na wamiliki wao walijitokeza na kulipa faini kutokana na
maamuzi ya Mahakama. Katika mkoa wa Kagera jumla ngombe 1,536
ambao wamiliki wake bado hawajulikani wanashikiliwa na vyombo vya ulinzi
na usalama na sheria itachukua mkondo wake.

Kwa takwimu hizi ni wazi kwamba zoezi hili halijalenga nchi yeyote, kwa
sababu sio nchi moja tu imeathirika. Zoezi hili limelenga kutekeleza sheria
na kanuni za nchi yetu ili kulinda mazingira na kupunguza uwezekano wa
kusambaa kwa magonjwa ya mifugo. Hili suala halipaswi kusababisha
mgogoro wa kidiplomasia na nchi yeyote, labda tu mtu aamue kwa
makusudi yasiyo mema kupotosha na kuchochea mgogoro.

Aidha, tarehe 24 Oktoba, 2017 jumla ya vifaranga vya kuku wa mayai 6,400
vilikamatwa katika Mkoa wa Arusha kwa kuingizwa nchini bila kufuata sheria
na kanuni. Vifaranga hivyo vilikuwa kwenye maboksi 60 vikiwa kwenye gari
lenye namba za usajili T 285 BAY. Mmiliki wa vifaranga hivi alidai kwamba
ameviingiza nchini kutokea Kenya. Vifaranga hivi viliteketezwa kutokana na
msafirishaji wa vifaranga hivi kutokuwa na kibali cha aina yoyote kutoka
mamlaka husika ya udhibiti wa magonjwa ya mifugo hapa nchini ambayo ni
Idara ya Huduma za Afya Mifugo katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Pia,
mmiliki huyu alishindwa hata kuonesha kibali cha Serikali ya Kenya
kumruhusu kusafirisha vifaranga hivyo kutoka Kenya kuvileta Tanzania
pamoja na kwamba mmiliki huyu alidai kwamba vifaranga hivyo amevitoa
Kenya. Ni muhimu ikafahamika kwamba nchi zote duniani, ikiwemo
Kenya, hufuata miongozo ya WTO na Shirika la Afya ya Wanyama
Duniani (OIE) kwa kutoa vibali (export permit) kwa mtu yeyote
anayetaka kusafirisha mifugo nje ya nchi. Kosa jingine kubwa ni kwamba
vifaranga hivi havikupitishiwa kwenye vituo rasmi vya Ukaguzi wa Mifugo na
Mazao yake mipakani (zoosanitary border posts) kwa mujibu wa sheria na
kanuni husika.
3
Pamoja na yote haya, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania alimpigia
simu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo (Director of Veterinary Services) wa
Kenya kutaka kujua kama Mamlaka za Kenya zina habari kuhusu vifaranga
waliokamatwa na kama Kenya itakubali kuruhusu vifaranga hivyo
virudishwe Kenya. Mkurugenzi huyu wa Kenya alisema hana taarifa
kuhusu vifaranga hivyo na kwamba Kenya haiko tayari kuruhusu
vifaranga hivyo kurudishwa nchini mwao kwa sababu havina nyaraka
kulingana na miongozo ya kimataifa.

Ni vizuri umma ukajua kwamba hii si mara ya kwanza kwa Serikali


kuteketeza vifaranga vilivyoingizwa nchini bila kufuata sheria kanuni na
taratibu. Vipo vifaranga vingi tu vimeteketezwa kwa namna hiyo hiyo baada
ya kukamatwa kwenye viwanja vyetu vya ndege na sehemu nyingine.
Kadhalika vifaranga ambavyo vimekuwa vikiteketezwa havitokei nchi moja
tu. Vifaranga vyote vinavyoingizwa nchini bila kufuata sheria na kanuni
zinazotulinda dhidi ya uwezekano wa magonjwa vinateketezwa mara moja
bila kujali vinatoka nchi gani. Hatua hizi tumekuwa tukizitekeleza tangu
tuweke zuio mwaka 2006, na hazijaathiri kwa namna yeyote ile mahusiano
yetu na nchi yeyote. Hatua yeyote ya kujaribu kufanya jambo hili kuwa ni la
mgogoro wa kidiplomasia dhidi ya nchi yeyote ile ni hatua isiyo sahihi.

Serikali inawaasa wananchi na raia wa kigeni wazingatie sheria, kanuni na


taratibu pale wanapotaka kuingiza nchini au kusafirisha nje ya nchi mifugo
na mazao yake. Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia sheria, kanuni
na taratibu za nchi, kikanda na kimataifa zinazohusu utoaji na uingizaji wa
mifugo na mazao yake nchini. Tunapenda kuuhakikishia umma kwamba,
usimamizi wa sheria hizi hauwezi na hautakiwi kwa namna yoyote ile
kuathiri mahusiano yetu na nchi nyingine kwa sababu nchi zote
duniani zinasimamia sheria kama hizi.

Mojawapo ya misingi ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ni kujenga na


kuimarisha mahusiano na nchi nyingine pamoja na kudumisha ujirani
mwema. Hivyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea
kuhakikisha kuwa inalinda mahusiano mazuri yaliyojengwa kwa muda mrefu
kati yake na nchi nyingine duniani. Kadhalika, Serikali itaendelea kutumia
fursa mbali mbali, kama vile vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki na vikao
4
vya pande mbili kati yetu na jirani zetu, na pia vikao vya ujirani mwema
mipakani, kutatua changamoto zozote za kimahusiano zitakazo jitokeza kwa
nia ya kuendelea kuimarisha ujirani mwema.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
19 Novemba, 2017

You might also like