You are on page 1of 34

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA

Sheria Katika Lugha Rahisi

Kimetolewa na Chama Cha Wanasheria Tanzania Bara

JUNI, 2015

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA i


KIMEANDALIWA NA

Kamati ya Utafiti na Machapisho ya Chama Cha Wanasheria


Tanganyika ambayo ina wajumbe wafuatao:

Cyriacus Binamungu Mwenyekiti


Daniel Welwel Mjumbe
Madeline Kimei Mjumbe
Alex Makulilo Mjumbe
Ally Possi Mjumbe
Lilian Mongella Mjumbe
Frank Mirindo Mjumbe
Elifuraha Laitaika Mjumbe
Judith S. Kapinga Katibu wa Kamati

Mratibu
1. Seleman Pingoni
2. Kaleb Gamaya (CEO-TLS)
3. TEPHEN mSECHU (PO-RPA
4. Selemani Pingoni (M & E Officer)

HAKIMILIKI 2015 TLS


Kijarida hiki ni mali ya Chama cha Wanasheria Tanzania Bara
na ni kosa kurudufu au kuchapa au kutumia kwa namna yoyote
itakayo kuwa kinyume hakimiliki ya Chama Cha Wanasheria
bila idhini au ruhusa ya maandishi ya Chama Cha Wanasheria
Tanzania Bara.

ii IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


YALIYOMO

Mirathi Ni nini?

Sheria Zinazohusu Urithi na Wosia Tanzania

Taratibu za Ufunguzi wa Mirathi

Wajibu wa Msimamizi wa Mirathi

Wosia Ni Nini?

Aina na sifa za wosia

Faida za wosia

Mahali pa kuhifadhi wosia

Mfano wa Jinsi ya Kuandika Wosia

Pingamizi kwa Maombi ya Mirathi

Wajibu wa Mtekelezaji au Msimamizi wa Mirathi

Haki za Warithi Dhidi ya Mtekelezaji/Msimamizi wa Mirathi

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA iii


SHUKRANI

Kamati ya Utafiti na Machapisho ya Chama Cha Wanasheria


Tanzania Bara kwa niaba ya Baraza la Uongozi la Chama inatoa
shukrani za dhati kwa wadau wote na wanachama wa Chama
Cha Wanasheria Tanzania Bara kwa kushiriki kikamilifu katua
hatua mbalimbali za kuandaa kijaridi hiki.
Kwanamna ya pekee, Kamati inapenda kuishukuru pia
Sekretariati ya chama kwa kazi kubwa walioifanya na inashuruku
wanachama wa Chama Cha Wanasheria kwa ushirikiano
wanaoendelea kutoa katika kufanikisha kazi za chama.

iv IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


UTANGULIZI

Chama Cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society) ni


chama kilichoanziahwa na Sheria ya Bunge ya 1954 Sura Na.307.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, Chama kinawajibu wa kuisaidia
serikali katik amasuala yahusuyo sheria na pia kuieleimisha
jamii kisheria katika kupata haki zao za msingi.

Katika kutimiza jukumu lake kwa wanajamii Cham Cha Sheria


Tnaganyika kimeeandaa kijarida hiki cha sheria katika lugha
Rahisi kiitwacho “Ijue Sheria ya Urithi, Mirathi na Wosia’’.

Kijarida hiki kinalengo la kuijengea jamii uwezo wa kufahamu


dhana ya urithi na taratibu za ufunguzi wa mirathi. Katika
Kijarida hiki mwanajamii atapata elimu ya Maana ya urithi na
mirathi, Sheria zinazohusu urithi na mirathi hapa Tanzania,
Taratibu za ufunguzi wa mirathi, Wajibu wa msimamizi wa
mirathi, Wosia na aina za wosia, Faida za kuandika wosia na
Haki za wanawake katika mirathi.

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA v


vi IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA
Mirathi Ni nini?
Mirathi ni mali aliyoacha marehemu kwa ajili ya kurithishwa
warithi wake halali. Sheria imeweka taratibu maalum
zinazoongoza ukusanyaji, uangalizi, usimamizi, ugawaji na
umiliki wa mali za marehemu pamoja, na kulipa madeni aliyoacha
marehemu wakati wa uhai wake au gharama zitokanazo na
mazishi yake.
Sisitiza kuwa lengo kuu la sheria za mirathi ni kutoa utaratibu
wa kusimamia mali za marehemu baada ya kifo chake ikiwamo
kuhamisha umiliki wa mali hizo kutoka kwa marehemu kwenda
kwa watu wenye haki ya kuzipata mali hizo. Nia hasa ni kwamba
mali alizoacha marehemu zisibaki zikiharibika na kupotea bure,
au warithi halali au watu wenye maslahi na mali za marehemu,
kwa mfano wale wanaomdai hawapotezi haki hiyo. Awepo mtu
ambaye atazisimamia na kuzigawa kwa wahusika wakiwamo
wadai kuepusha mgongano katika jamii husika.

Sheria Zinazohusu Urithi na Wosia Tanzania


Sheria zinazohusu urithi na wosia (mirathi) hapa Tanzania
zimegawanyika katika sheria za aina tatu ambazo ni;
• Sheria ya Serikali
• Sheria ya Mila
• Sheria ya Dini ya Kiislam

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 1


Sheria ya Serikali
Sheria ya Kiserikali ni Sheria ya Urithi ya India ya mwaka 1865.
Sheria hii ilianza kutumika nchini India tangu mwaka 1865
lakini ililetwa Tanzania (wakati huo Tanganyika), na Serikali
ya Wakoloni wa Kiingereza. Sheria hii inaongoza na kusimamia
mgawanyo wa mali za marehemu pale ambapo itaonekana
kwamba marehemu alikuwa hafuati Sheria za Kiislam wala
Sheria za Kimila au kama ni waislamu hawataki sheria ya dini
yao kutumika katika mirathi.

Mgawanyo wa mali kwa kutumia sheria hii huwa hivi;


• Kama marehemu ameacha mjane na watoto, mjane atapata
1/3 na watoto 2/3 ya mali yote ya marehemu.
• Lakini kama marehemu hakuacha watoto, basi mjane
atapata ½ na ½ ya mali na nyingine inayobaki hugawanywa
sawasawa kati ya wazazi, kaka, na dada za marehemu.

Angalizo: Mgawanyo wa mali kwa mujibu wa sheria hii


hufanyika pale tu ambapo marehemu hakuacha wosia. Kama
kuna wosia mali zitagawanywa kwa mujibu wa wosia.

Kwa mujibu wa sheria hii watoto wa nje ya ndoa hawana haki


ya kurithi isipokuwa tu kama kuna wosia na katika wosia huo
wawe wamerithishwa mali.

Ikumbukwe kuwa mgawanyo wa mali kwa mujibu wa sheria


hii hufanyika tu pale ambapo imethibitika kwamba ni kweli
marehemu alikuwa ameacha kabisa kuishi kwa kufuata mila na
desturi za jamii yake na pia hakuacha wosia unaolekeza namna
mali yake itakavyogawanywa pindi atakapofariki.

Sheria ya Mila
Mwaka 1963, serikali ilitoa tamko la kuzitambua sheria za mila
za urithi na wosia kupitia Tangazo Rasmi la Serikali Namba

2 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


436 la mwaka 1963. Sheria hii hutumika kwa wananchi wote
wa Tanzania ambao si wa asili ya Asia, Ulaya au Wasomali na
ambao katika maisha yao walifuata taratibu au sheria za kimila.
Hivyo basi, ikibainika na kuiridhisha mahakama kwamba wakati
wa uhai wake marehemu aliishi kwa kufuata mila na desturi za
kabila lake, basi mirathi itafuata sheria za mila za hilo kabila.

Ikiwa sheria ya kimila itatumika, urithi hufuata upande wa ukoo


wa kiumeni. Warithi huwa ni watu wanaoangukia katika vyeo
vya aina tatu;
• Daraja la kwanza
• Daraja la pili
• Daraja la tatu

Daraja la Kwanza
Cheo hiki hushikwa na warithi wafuatao;
• Mtoto wa kiume wa kwanza kutoka katika nyumba ya
kwanza (kama ilikua ndoa ya wake wengi), au;
• Mtoto wa kiume aliyezaliwa kwanza kutoka nyumba
yoyote, iwapo marehemu hakuacha mtoto wa kiume katika
nyumba ya kwanza.

Daraja la pili
Cheo hiki hushikwa na watoto wote wa kiume waliosalia ambao
hurithi sehemu kubwa kuliko watoto wa kike ambao huhesabika
kama daraja la tatu.

Daraja la Tatu
Cheo hiki ndio cha mwisho na kinajumuisha watoto wa kike wote
bila kujali tofauti ya umri na nafasi ya mama zao katika ndoa.
Hawa hupata sehemu ndogo kuliko watoto wa kiume. Kama
watoto wa kiume hawapo basi watoto wa kike huongezewa
urithi.

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 3


Zingatio Muhimu: Sheria ya ardhi ya vijiji Na. 5 ya mwaka 1999
imesahihisha utaratibu wa umiliki ardhi wa kimila (urithi wa
ardhi) kwa kuondoa ubaguzi wa aina yeyote kwenye umiliki wa
ardhi na kuweka usawa kwa wanawake na wanaume.

Sheria hiyo ya Ardhi inaeleza kuwa sheria yoyote ya kimila


inayowanyima wanawake, watoto au watu wenye ulemavu
uhalali wa kumiliki mali, kutumia au kupata ardhi, basi sheria
hiyo ya mila itakuwa batili. Kwa misingi hiyo, cheo cha tatu
cha urithi kwenye sheria za kimila kinakuwa batili pale urithi
wa mali ya marehemu unapogusa suala la ardhi (wanaume na
wanawake watagawana sawa ardhi ya urithi) kwa mujibu wa
sheria ya ardhi ya mwaka 1999.

Nafasi ya mjane
Utaona kuwa katika sheria ya kimila ambayo iko katika Tangazo
la Serikali Namba 436 la Mwaka 1963, wajane hawaruhusiwi
kurithi mali za marehemu waume zao. Sheria hiyo inasema kuwa
mjane mwenye watoto inabidi aishi kwa kutegemea watoto
wake. Mjane ambaye hana watoto atabaki katika nyumba ya
marehemu na kupewa asilimia 20 ya nusu ya mali ya marehemu
na kuitumia wakati wa uhai wake. Akifariki au akiolewa na mtu
mwingine nje ya ukoo mali hiyo na nyumba aliyokuwa anakaa
hugawiwa kwa warithi halali wa marehemu mume wake. Sheria
hii pia inasema, mume hawezi kurithi mali ya mke wake katika
urithi usio na wosia, isipokuwa pale tu ambapo mke hakuacha
watoto na hakuacha kabisa mtu yoyote katika ukoo wake.
Sheria hii kwa sasa inakosa uhalali wa Kikatiba kwa kuwa haki
za binadamu zinataka usawa bila ya ubaguzi.

Sheria ya mila inatamka kuwa watoto waliozaliwa nje ya ndoa


hawaruhusiwi kurithi ila wanaweza kurithi endapo marehemu
aliacha wosia unaowapa haki ya kurithi au ikiwa walihalalishwa
na marehemu kabla ya kufa. Hata hivyo, mtoto wa kwanza wa

4 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


kiume aliyezaliwa nje ya ndoa na kuhalalishwa, hawezi kuwa
mrithi daraja la kwanza bali atarithi katika daraja la pili.

Sheria ya Kiislamu
Sheria ya Kiislamu ya Mirathi ni kama ilivyoanishwa katika
vifungu mabalimbali vya Kuruani Tukufu na kufafanuliwa
katika Makala mbalimbali za wanazuoni wa Kiislamu. Hapa
Tanzania Bara, Sheria ya Kiislamu ya mirathi imeanishwa katika
Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1967 (The Statements of
Islamic Law, GN 222 of 1967). Tamko hili pamoja na kwamba
halijawahi kutumika rasmi, ni mwongozo mzuri wa hizo sheria.
Kama mirathi yeyote ile, mgawanyo wa mali ya marehemu kwa
mujibu wa Sheria ya Kiislamu, huzingatia mambo muhimu
matatu yafuatayo,
Kwamba:
i. Mwenye mali awe alishakufa (maut al–muwarith)
ii. Pawepo na warithi halali wa marehemu (hayat al-warith),
yaani watoto wa marehemu ndugu wengine wa marehemu.
Warithi hawa ni lazima wawepo na wawe ni warithi hakika
wanaotambulika kisheria wakati wa mauti ya marehemu
iii. Marehemu ameacha mali (al- tarikah I al–mauruth)
iv. Urithi utokane na mali halisi na halali za marehemu na sio
nje ya hizo.

Kabla ya mirathi lazima matatizo yafuatayo yawe yametatuliwa kwanza:


• Madeni yanayokabili mali za marehemu
• Gharama za Mazishi
• Utatuzi wa madeni mengine
• Wosia uwe umefuatiwa
• Warithi halali

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 5


Kulingana na mafundisho ya dini ya Kiislamu, wanazuoni wote
kwa ujumla wanaafiki kuwepo kwa makundi yafuatayo kuwa
ndio warithi halali kwa mujibu wa dini ya Kiislamu;

a. As’hab Al – Furud: Hili ni kundi la watu wanaopata urithi


wao kufuatana na muainisho wa bayana uliotolewa ndani
ya KuruaniTukufu. Hawa kwa kawaida wapo kumi na mbili
(12). Kati yao, wawili (2) hupatikana kwa njia ya mahusiano
ya kinyumba yaani mke na mume, wengine hutokana na
undugu wa damu na uhusiano wa ukaribu kidugu, yaani
jamaa. Kwa ujumla wao, ni kama ifuatavyo: (i) Mume, (ii)
Mke, (iii) Mtoto wa kiume, (iv) Mtoto wa kike, (v) Mama,
(vi) Dada, (vii) Kaka, (viii)Mpwa, (ix) Dada wa kambo, (x)
Kaka wa kambo, (xi) Babu mzaa baba
b. Asabah: Hawa ni wale wenye kupata urithi kutokana na
albaki ya mali yote baada ya wale warithi waliobainishwa
kwenye Qur’an kupata sehemu yao.
c. Hazina ya Umma: Kwa mujibu ya wanazuoni wa Kiislamu,
kuna mgawanyiko wa mawazo katika kuthibitisha uhalali
wa kuchukuliwa sehemu ya mali ya marehemu na kutolewa
kama hazina ya umma. Mfano kundi linaloongozwa na
Iman Hanafi na Hanbal, wanapinga mali za marehemu
kupelekwa katika hazina kusaidia jamii. Lakini wale wenye
mtazamo wa mawazo kama ya Malik na Shafii wanaafiki
suala la mali ya marehemu kuchukuliwa na kurithishwa
kwenye hazina ya jamii. Mali za namna hii huwa ni mali
ya jamii nzima na huwa chini ya msimamizi wake mkuu
aliyechaguliwa na jamii yenyewe. Mfano katika serikali
ya mapinduzi Zanzibar, mali zitolewazo kama Baitul Mal
(hazina ya umma), zimewekwa chini ya uangalizi wa
Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana.
d. Dhawl -Arham: hili ni lile kundi la wale ndugu wasiotokana
na damu ya marehemu moja kwa moja.

6 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


e. Angalizo: Izingatiwe kwamba mgawanyo wa mali kwa
mujibu wa dini ya Kiislamu, hufuata matabaka kama
yalivyobainishwa hapo juu. Kulingana na Sheria ya Kabidhi
Wasii Mkuu, endapo mtu atakufa bila kuwa na mrithi,
au kwamba mali yake inaweza kupotea, basi hiyo mali
itawekwa chini ya Kabithi Wasii Mkuu, na endapo utapita
muda wa miaka kumi na mbili (12) bila mtu yeyote kudai
kitu chochote kuhusu mirathi hiyo, basi KabidhiWasii
Mkuu ataihamishia mali hiyo Serikalini.

Taratibu za Ufunguzi wa Mirathi


Taratibu za kufungua mirathi ikiwa hakuna wosia
i. Itokeapo kifo, taarifa ya kifo itolewe na kusajiliwa kwenye
ofisi ya mkuu wa Wilaya ndani ya siku (30) thelathini toka
kifo kitokee. Kumbuka kupewe hati ya kifo.
ii. Kikao cha wana ukoo kifanyike ili kumchagua au kumteua
msimamizi wa mirathi na uamuzi huo uwekwe katika
dondoo za maandishi.
iii. Msimamizi aliyeteuliwa na wanaukoo apeleke maombi ya
kupata barua/hati ya usimamizi wa mirathi mahakamani
akiambatanisha na;
• Cheti cha kifo, na
• Dondoo za kikao cha wana ukoo kilichomteua muombaji
kuwa msimamizi
iv. Kiutaratibu Mahakama itatoa taarifa kwa kubandika
katika ukuta wa mahakama au gazetini juu ya maombi
ya usimamizi wa mirathi na kutoa muda wa siku tisini
kuruhusu mtu yeyote kutoa pingamizi kama ana sababu
za kufanya hivyo. Kama hakuna pingamizi basi mahakama
itatoa barua ya usimamizi wa mirathi kwa mwombaji.
v. Msimamizi wa mirathi hugawa mali ndani ya miezi sita
na hatimaye kurejesha mahakamani nakala ya fomu
inayoonyesha jinsi mgawo ulivyofanyika na kutiwa sahihi
na kila mrithi. Mahakama itafunga jalada.

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 7


Barua ya kuomba usimamizi wa mirathi lazima itaje;
a. Familia ya marehemu na anwani zao na ndugu waliokuwa
wakimtegemea.
b. Idadi na aina ya mali iliyoachwa.
c. Juhudi zilizofanyika kuhakikisha kwamba ni kweli
marehemu hakuacha wosia.
d. Maelezo kuhusu maskani yake.

Hata hivyo, endapo kunahitajika kufungua mirathi, ni vizuri


kwenda mahakamani ili kupata fomu maalum ya kujaza. Mtu
anaweza kufungua mirathi katika mahakama ya mwanzo,
Wilaya au hata ya Hakimu Mkazi.

Maombi ya usimamizi wa mirathi lazima yaeleze bayana juu ya


yafuatayo;
a. Kiasi na aina ya mali iliyoachwa na marehemu.
b. Majina na anwani za warithi.
c. Sehemu atokayo marehemu na mahali mali zilipo (hii ni
muhimu kwani husaidia kuamua ni mahakamani gani
stahiki inaweza kupokea maombi ya ufunguzi wa mirathi).

Wajibu wa Msimamizi wa Mirathi


Msimamizi wa mirathi anawajibika;
a. Kufungua shauri la maombi ya usimamizi wa mirathi.
b. Kuainisha na kutambua mali zilizoachwa na marehemu.
c. Kulipa na kukusanya madeni yaliyoachwa na marehemu.
d. Kugawanya mali kwa warithi kulingana na sheria husika
(sheria zisichanganywe).
e. Baada ya mgawanyo wa mali, msimamizi atawasilisha Hati
inayoonyesha orodha ya mali na jinsi zilivyogawiwa katika
mahakama ambayo shauri lilifunguliwa.
f. Kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha Kanuni za uendeshaji

8 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


mirathi katika mahakama za mwanzo GN Na. 49/1971
baada ya msimamizi wa mirathi kuchaguliwa na mahakama,
ndani ya muda usiozidi miezi sita (6) tangu achaguliwe,
msimamizi huyo aieleze mahamama kwa kutumia fomu
Na. 5 jinsi alivyogawa mali ya marehemu na kulipa madeni
ya marehemu.

Fahamu Kuwa: msimamzi wa mirathi sio lazima awe ndugu


na awe binadamu. Msimamizi wa mirathi aweza kuwa taasisi
au ofisi fulani kama vile Benki ili mradi taasisi hiyo iweze
kufanya zoezi la kugawanya mali za marehemu kadri ndugu
na warithi watakavyopenda kwa kuzingatia haki na sheria.
Hata hivyo, taasisi za serikali kama vile Kabidhi Wasii Mkuu au
Mdhamini wa Umma hawezi kuteuliwa kushughulikia mirathi
inayotawaliwa na sheria za kimila au kiislamu. Kwa mujibu
wa Sheria ya Kabidhi Wasii Mkuu, Sura ya 27 na Sheria ya
Mdhamini wa Umma, Sura ya 31 taasisi hizo zinashughulikia
mirathi ambayo sheria inayotumika sio ya kimila au kiislamu
bali ni sheria ya kiserikali.

Taratibu za kufungua mirathi pale ambapo kuna wosia


Mambo yafuatayo sharti yazingatiwe katika kufungua mirathi
endapo kuna wosia;
i. Mtu akifariki, kifo kiandikishwe kwa Mkuu wa Wilaya
katika muda wa siku 30;
ii. Kama wosia umemtaja mtu atakayekuwa msimamizi wa
mirathi, msimamizi huyo afungue mirathi mahakamani
akiwa na;
• Wosia ulioachwa, na
• Cheti cha kifo
iii. Ikiwa hakuna mtu aliyetajwa kuwa msimamizi wa mirathi,
utaratibu wa wana ndugu kukaa kikao ufanyike na kumteua
mtu atakayekuwa msimamizi wa mirathi;

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 9


iv. Mahakama hutoa tangazo la mirathi kwa muda wa siku 90
na kama hakuna pingamizi lolote msimamizi hukabidhiwa
barua ya kuhalalisha kugawa urithi na kulipa madeni;
v. Msimamizi hugawa mali kwa mujibu wa wosia.
vi. Baada ya ugawaji wa mali, msimamizi hupeleka taarifa ya
ugawaji mali mahakamani na mahakama hufunga jalada.

Barua ya kuomba usimamizi wa mirathi lazima itaje;


a. Jina la marehehemu,
b. Orodha ya mali za marehemu,
c. Majina na anwani za wasimamizi,
d. Maskani ya marehemu, hii ni muhimu kwani mirathi
hufunguliwa kufuatana na maskani yake.
e. Viambatanisho: Cheti cha kifo na wosia.

Hata hivyo, ni vyema kufahamu kuwa;


a. Msimamizi wa mirathi si lazima awe ndugu wa marehemu,
bali awe mtu yeyote mwenye tabia nzuri na mwadilifu
ambaye amechaguliwa na wana ukoo au mahakama.
Msimamizi wa mirathi sio lazima awe mtu mmoja,
wanaweza kuchaguliwa watu hata wawili kushirikiana
kufanya usimamizi wa mirathi.
b. Endapo anachaguliwa mtoto chini ya miaka 18 au mtu
mwenye ulemavu kuwa msimamizi wa mirathi, inashauriwa
wawepo wasimamizi wa mirathi wawili, ili kusaidia
kuhakikisha kuwa usimamizi wa mali za marehemu
unafanyika kwa busara.
c. Endapo unaona msimamizi wa mirathi hakutendei haki,
unaweza kupeleka lalamiko lako mahakamani na kuomba
amri ya mahakama ya kuhakikisha haki inatendeka au
kuomba msimamizi aondolewe madaraka ya kusimamia
mirathi.
d. Kesi za mirathi zifunguliwe pale marehemu alipokuwa
anaishi, yaani kama marehemu alikuwa anaishi Dodoma

10 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


lakini sehemu aliyozaliwa ni Kigoma basi kesi hiyo
ifunguliwe katika mahakama yenye mamlaka na sehemu
hiyo, yaani Dodoma.
e. Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali (WAUU/RITA)
pamoja na mambo mengine inajishughulisha katika
usimamizi wa mirathi katika mazingira yafuatayo:
• Kama marehemu ameacha wosia kwamba mirathi yake
isimamiwe na ofisi hii,
• Endapo mahakama itateua ofisi hii kuwa msimamizi
wa mirathi. Hii hutokea endapo kuna pingamizi dhidi
ya wasimamizi wa mirathi.
f. Ikiwa marehemu amefariki bila kuacha ndugu yeyote au
mtoto, mali zake zitasimamiwa na Kabidhi Wasii Mkuu wa
Serikali.
g. Mali zenye wakfu kama vile msikiti, kanisa pamoja na mali
ambazo serikali ina maslahi nazo kama hospitali, shule, nk.
zinabakia chini ya usimamizi wa kabidhi wasii mkuu wa
serikali.

Angalizo: Baadhi ya sheria za urithi zinawakandamiza


wanawake, wajane na watoto wa kike. Ni vema wakati wa
kugawa mali ya urithi kuachana na mila na desturi ambazo
zinabagua na kumkandamiza mwanamke.

Kumbuka: Sheria ya Ardhi inaeleza kuwa sheria yoyote ya


kimila inayowanyima wanawake, watoto au watu wenye
ulemavu uhalali wa kumiliki mali, kutumia au kupata ardhi,
basi sheria hiyo ya mila itakuwa batili.

Zingatia: Mirathi inayofuata sheria za mila na au dini ya Kiislamu


hufunguliwa katika mahakama za mwanzo.

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 11


Wosia

Kutokana na ukweli kwamba mwanadamu hapa duniani ni


kiumbe wa kupita tu na kwamba mara nyingi kifo hutokea kwa
kushtukiza, ni vyema mwanadamu akajitayarisha kwa kuusia
mali yake, ili pindi kifo kikimchukua, mali hiyo igawiwe kadri
muusia alivyotaka na hivyo kuwaondolea warithi migogoro
isiyokuwa ya lazima. Njia pekee na nzuri ya kuusia mali ni kwa
kuacha wosia.

Mara nyingi wosia huchukuliwa na baadhi ya watu kama ni


uchuro, kwa maana kwamba unaanza kujitabiria kifo. Wengine
huona kuwa wosia hauna umuhimu kwa kuwa kuna uwezekano
mkubwa wa kuvuja. Fikra hizi sio sahihi na hazisaidii chochote
kwani kuandika wosia sio kufungua mlango wa mauti bali ni
kuhakikisha utashi wako unafuatwa katika kurithisha mali zako
kwa watu unaofikiri wanastahili.

Mara kadhaa familia nyingi zimejikuta zikiingia kwenye


mogogoro juu ya mali aliyoiacha marehemu mara baada ya kifo
chake, pengine hata kupelekea kuwepo na uhasama na hatimaye
kuharibu hata uhusiano kati ya wanandugu. Mara nyingi
watoto na mjane au wajane ndio huathirika zaidi na migogoro
ya mirathi.

Maana ya Wosia
Wosia ni kauli inayotolewa na mtu wakati wa uhai wake kwa
hiari yake kuonyesha nia yake jinsi gani angependa mali yake
igawanywe baada ya kufa kwake.

12 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


Aina na sifa za wosia
Wosia unaweza kuwa wa namna mbili;
a. Wosia wa maandishi (ulioandikwa)
b. Wosia wa mdomo (usio wa maandishi)
Wosia wa maandishi
Wosia wa maandishi ni lazima;
• Uandikwe kwa kalamu ya wino na sio kalamu ya risasi
(inayoweza kufutwa futwa);
• Anayetoa wosia (Muusia) awe na akili timamu;
• Utaje tarehe ulipoandikwa (Tarehe ya wosia);
• Utaje kuwa muusia anayo akili timamu na anausia kwa
hiari yake mwenyewe;
• Ushuhudiwe na mashahidi wanaojua kusoma na kuandika
angalau wawili (mmoja wa ukoo na mwingine mtu baki),
kama muusia anajua kusoma na kuandika;
• Ushuhudiwe na mashahidi wasiopungua wanne (wawili
wa ukoo na wawili watu baki), kama muusia hajui kusoma
na kuandika;
• Wanaotarajia kurithi hawaruhusiwi kushuhudia wosia huo;

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 13


• Usainiwe na muusia mbele ya mashahidi wake wakiona,
kutia sahihi yake au kama hajui kusoma, aweke alama ya
dole gumba la kulia;
• Utiwe sahihi za mashahidi;
• Mashahidi wawe wamechaguliwa na muusia mwenyewe.

Angalizo: Wosia wa maandishi waweza kubadilishwa kwa


wosia mwingine wa maandishi unaotaja kubadilisha wosia wa
kwanza na unaofuata hatua zile zile kama ilivyoainishwa hapo
juu.

Wosia wa Mdomo
Wosia wa mdomo lazima;
• Ushuhudiwe na mashahidi wanne (wawili wa ukoo na
wawili watu baki);
• Muusia awe na akili timamu;
• Kama mashahidi watakufa kabla ya muusia kufa, basi wosia
hautakubalika na urithi utagawanywa kadri ya mpango wa
urithi usio wa wosia. Mwenyewe kama anataka kuusia mali
zake, atoe wosia mpya;
• Mashahidi wawe wamechaguliwa na muusia mwenyewe.

Ikumbukwe kuwa: Sheria inaweka bayana kwamba kuandikisha


wosia sio lazima, bali ni hiari ya muusia. Pia kwamba wosia wa
mdomo hauwezi kufuta au kubadilisha wosia wa maandishi,
lakini wosia wa maandishi waweza kufuta au kubadilisha wosia
wa mdomo ikiwa waliokuwa mashahidi wa wosia wa mdomo
watashiriki.

Kubatilishwa Wosia
Wosia waweza kubatilishwa ikiwa itathibitika kwamba muusia
amepungukiwa akili kwa sababu ya wazimu, ugonjwa, ulevi au
hasira ya gafla. Ni muhimu kukumbuka kwamba ni wahusika tu

14 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


(warithi), wanaoruhusiwa kupinga wosia kwa sababu zilizotajwa
hapo juu,

Jinsi ya Kurithisha Wosia


Kulingana na Sheria ya Usimamizi wa Haki na Matumizi ya
Sheria mbali mbali, Sura ya 358, muusia anaweza kuusia mali
yake yote bila kutaja kila kitu alichonacho wakati wa kufa kwake.
Ikiwa muusia anapenda kuusia sehemu tu ya mali yake, basi
sehemu iliyobaki itagawanywa kulingana na masharti ya urithi
usio na wosia.

Mrithi Kunyimwa Urithi na Muusia


Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Haki na Matumizi ya
Sheria mbalimbali, Sura ya 358, muusia anaweza kumnyima
mrithi urithi wake ikiwa mritihi;
• Amezini na mke wa mtoa urithi;
• Amejaribu kumuua, amemshambulia, au amemdhuru
vibaya mtoa urithi au mama mzazi wa mrithi;
• Bila sababu ya haki, hakumtunza mtoa wosia kutokana na
njaa na ugonjwa;
• Ameharibu mali ya muusia, uharibifu wake utahesabika
katika kukadiria kiwango cha urithi atakaostahili kupata.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kusimamia Mirathi ya Mali


Ndogondogo, Sura ya 30, dini sio sababu ya kumnyima mrithi
urithi.

Ikumbukwe kuwa: Muusia akimnyima mrithi urithi wake,


lazima ampe nafasi ya kujitetea mbele yake au Baraza la Ukoo,
na lazima atoe sababu za kumnyima urithi. Mrithi baada ya kujua
amenyimwa urithi akikaa kimya bila ya kujitetea mbele ya mtoa
urithi au Baraza la Ukoo, hawezi tena baadaye kupinga huo wosia.
Kama mrithi hakuwa na habari za kunyimwa kwake urithi, atatoa
malalamiko yake kwenye Baraza la Ukoo ambalo litamsikiliza na

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 15


linao uwezo wa kukubali au kukataa. Ikibainika kwamba muusia
alimnyima mrithi urithi kimakosa, wosia utabadilishwa na urithi
utagawanywa kulingana na urithi usio na wosia

Faida za wosia
Wosia una faida zifuatazo;
a. Mwosia anapata fursa ya kufanya mgawo wa mali yake
kwa kadri anavyotaka kabla ya kufariki.
b. Mwosia anapata fursa ya kuamua ni nani awe msimamizi
wa mirathi yake.
c. Wosia huepusha ugomvi wa wanafamilia na kuimarisha
amani miongoni mwa warithi na wanandugu halali.
d. Wosia ni chombo cha kuhakikisha kwamba urithi
unakwenda kwa watu ambao marehemu aliwaridhia.

Zingatio: Wosia ugusie mali za marehemu tu. Wosia wowote


ambao unarithisha mali zisizokuwa za marehemu au ambazo
zilikuwa zinamilikiwa na marehemu pamoja na mtu mwingine
kwa namna ya maslahi yasiyogawanyika wosia huo hautakuwa
halali.

Mahali pa kuhifadhi wosia


Wosia waweza kutunzwa mahali popote palipo na usalama
na ulinzi wa kutosha, ili kuepuka kughushiwa. Watu wengi
huchagua kutunza katika sehemu zifuatazo;
a. Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu(RITA/WAUU);
b. Kwenye vyombo vya kutoa msaada wa kisheria;
c. Asasi za kidini kama kanisa au msikiti;
d. Katika Kampuni ya uwakili;
e. Kwa mtu yeyote asiye mrithi katika wosia husika na ana
sifa za kutunza siri;
f. Benki;
g. Mahakamani;

16 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


Mfano wa Jinsi ya Kuandika Wosia
1. Huu ni wosia wangu wa mwisho mimi ….......…… wa
S.L.P………………………………………………………....…

2. Namchagua ……......……………………………………………..
wa S.L.P. …………………………………………………............
Simu………………………………………………………………
ambaye anaishi ………………….kuwa msimamizi wa
mirathi yangu.

3. Nitakapokufa mwili wangu ukazikwe ………………………


Wilaya ya ……………………… Mkoa wa ………………………

4. Mali yangu ni:


(a) ……………………………………………….……............…
.……………………………………………………………………
(b) Nina akaunti zifuatazo: ……………………………………

5. Natamka kwamba mali zangu zote zinazohamishika na


zisizohamishika zitamilikiwa na mke/ mume wangu
aitwaye ……………………… iwapo atakuwa hai baadaya
kufa kwangu.

6. Iwapo mke/ mume wangu aitwaye


………………………………….. atafariki mapema kuliko
mimi , mali zangu zitarithiwa katika mafungu yaliyo
sawasawa na watoto wangu wafuatao;

a) ………………………………………......………………....…
S.L.P………………………………………………………….
Simu …………………………………………………………

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 17


b) ………………………………………......…………………....
S.L.P……………………………………………............…….
Simu …………………………………………………………
c) ………………………………………......………………....…
S.L.P………………………………………………………….
Simu …………………………………………………………
d) ………………………………………......………………....…
S.L.P………………………………………………………….
Simu …………………………………………………………

Imetiwa saini hapa ……………………………………………………


Siku ya …………………………………………………………………
Mwezi wa…………………………… mwaka ……….....……….….
Saini ya mwosia……………………………………………...…….…

Shahidi wa Kwanza
Jina: ……………………………………………………………………
Saini: ………………………………………………………….….……
Anuani: ……………………………………………………………….
Kazi: ……………………………………………………….…………

Shahidi wa Pili
Jina: ……………………………………………………….…….….….
Saini: ……………………………………………………………….….
Anuani: …………………………………………………………….…
Kazi: ……………………………………………………………….…..

Mbele ya …………………………………………………..…..........…
Mshuhudi viapo/Saini : ………………………………………………

18 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


Mirathi pasipo Wosia
Ifahamike kuwa ndani ya siku thelathini (30) tangu alipofariki
marehemu wahusika wanapaswa kusajili kifo cha marehemu
kwenye Ofisi ya Vizazi na Vifo ambayo iko kwa Mkuu wa Wilaya
wa kila wilaya Tanzania Bara. Kama wahusika watachelewa
kusajili kifo ndani ya siku (30), basi wafike kwenye Ofisi hiyo ya
vizazi na vifo kwa maelezo.

Kifo kinasajiliwa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya iliyopo


mahali kilipotokea, na sio katika wilaya yeyote ile. Kama kuna
matatizo kuhusu wapi kifo kisajiliwe, wahusika wanaweza
kuwasiliana na msajili Mkuu wa Vizazi na Vifo, Makao Makuu,
Dar es Salaam.

• Msimamizi au wasimamizi wa mirathi huteuliwa au


kuchaguliwa na kikao cha wanandugu au ukoo
• Mwombaji hupeleka maombi yake mahakamani akiomba
kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi. Maombi hayo
huambatanishwa na vitu vifuatavyo;
◊ nakala ya cheti cha kifo cha marehemu;
◊ nakala ya kikao cha wanandugu cha kumchagua
msimamizi wa mirathi;
◊ tamko la mwombaji kwamba atasimamia mirathi kwa
uaminifu;
◊ kiapo cha wanandugu kwamba wanamteua mwombaji
kuwa msimamizi wa mirathi;
◊ kiapo cha mashahidi wakimdhamini mwombaji na
kwamba wako tayari kutoa fidia - endapo mwombaji
atashindwa kusimamia vizuri.

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 19


Ili mwombaji aweze kupewa usimamizi wa mirathi lazima
maombi yake yazingatie na kutaja kwa kiwango cha kuithibitishia
mahakama haya yafuatayo;
• Tarehe na mahali kilipotokea kifo cha marehemu;
• Familia na ndugu wengine wa marehemu,
• Haki au mamlaka ambayo kwayo mwombaji anapata uwezo
wa kuleta maombi mahakamani,
• Orodha ya mali/madeni ya marehemu anayoweza
kukusanya,
• Kwamba amefanya utafiti wa makini na kujiridhisha
kwamba hakuna wosia halali ulioandikwa au wa mdomo,
• Kwamba maombi kama hayo yamewahi kufanyika katika
mahakama yoyote ndani au nje ya nchi au la.

Baada ya kuwasilisha maombi ya mirathi, mahakama kwa


kawaida hutoa tangazo la mirathi kwa muda wa siku 90
kwenye Gazeti la Serikali linalosomwa na watu wengi au katika
mbao za matangazo za mahakama. Lengo ni kuwawezesha
wale wasioridhika na usimamizi huo kupeleka pingamizi
mahakamani. Vile vile mahakama ina uwezo wa kufupisha
kipindi hiki cha Tangazo la siku 90, kwa kutoa tangazo la muda
mfupi zaidi,

Baada ya kuwasilisha maombi ya mirathi mahakamani,


mahakama kwa kawaida hujaza fomu za “Taarifa ya Kawaida”
kulingana na mahakama ambako mirathi hiyo imefunguliwa.
• Kama mirathi imefunguliwa katika mahakama za chini
ya mahakama kuu (mahakama ya mwanzo, mahakama
ya wilaya), tangazo hutolewa katika gazeti la kawaida
linalosomwa na watu wengi au katika mbao za matangazo
za mahakama na mirathi hutolewa baada ya siku thelathini
(30) tangu tangazo kutolewa.
• Kama mirathi imefunguliwa katika Mahakama Kuu, tangazo
hutolewa katika gazeti la serikali na mirathi hutolewa baada
ya siku tisini (90) tangu tangazo kutolewa.

20 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


Angalizo: Lengo la kuweka muda huo wa tangazo ni
kuwawezesha wale wasioridhika na usimamizi huo kupeleka
pingamizi mahakamani na kuzuia mtu huyo asipewe usimamizi
wa mirathi au asiteuliwe kuwa mtekelezaji wa wosia (mirathi)
ya marehemu. Hata hivyo Mahakama ina uwezo wa kufupisha
kipindi hiki cha tangazo la siku 30 au 90, kwa kutoa tangazo la
muda mfupi zaidi.

Mwombaji ambaye sasa ni msimamizi wa mirathi ya marehemu


atalazimika kutekeleza, na/au kuendeleza taratibu za kugawa
mali za marehemu kama ifuatavyo;
• Kukusanya mali na madeni ya marehemu na pia kutambua
anaowadai,
• Kutayarisha taarifa ya awali ya maelezo / ufafanuzi wa mali
zote na madeni ya marehemu, na kuiwakilisha mahakamani
katika kipindi cha miezi sita tangu kuthibitishwa kwake
na mahakama. Hata hivyo mahakama inaweza kurefusha
muda huo kadri itakavyoona inafaa,
• Msimamizi wa mirathi atagawa mali kwa warithi halali
wa marehemu kama walivyobainishwa na kutajwa katika
maombi ya usimamizi wa mirathi, kwa mujibu wa sheria
husika yaani kama ni sheria ya mila, dini au serikali. •
Kutoa taarifa ndani ya miezi 6 ya ukamilishwaji wa zoezi la
ugawaji wa mali za marehemu mahakamani na mahakama
kujiridhisha kama zoezi hilo limeendeshwa sawa. Hata
hivyo mahakama inaweza kurefusha muda huo kadri
itakavyoona inafaa,
• Mahakama kufunga jalada la mirathi kama zoezi la ugawaji
limeendeshwa sawa na kukamilika

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 21


Pingamizi kwa Maombi ya Mirathi
Pingamizi
Lengo la kutoa tangazo la mirathi katika gazeti la serikali (Ndani
ya kipindi cha siku 90 au pungufu (chini ya hapo), au taarifa
ya kawaida (ndani ya kipindi cha siku 30 au pungufu (chini ya
hapo), ni kutoa fursa kwa yeyote asiyeridhika na kuthibitishwa
kwa mtekelezaji wosia ama kuteuliwa kwa msimamizi wa
mirathi, kupeleka pingamizi lake mahakamani.

Kwa njia ya pingamizi, mtoa pingamizi hutoa sababu za kupinga


uthibitishwaji au uteuliwaji wa mtekelezaji au msimamizi
wa mirathi ya marehemu. Baada ya kuwasilisha pingamizi
mahakamani, maombi ya mirathi huchukua mfumo wa shauri
la kawaida la daau na mwombaji wa mirathi hupewa muda
wa kujibu malalamiko ya mweka pingamizi. Hivyo mahakama
husikiliza pingamizi hilo na inaporidhika na sababu zitolewazo
katika pingamizi, inaweza kubatilisha uthibitishwaji wa
mtekeleza mirathi au kukataa uteuzi wa mwombaji usimamizi
wa mirathi.

Hata kama muda wa kuwasilisha pingamizi utapita na mahakama


ikamthibitisha au kumteua mtekelezaji au msimamizi wa
mirathi, endapo itathibitika kwamba kulikuwapo na kughushi
,au udanganyifu kuhusiana na usimamizi, au utekelezaji wa
mirathi, basi maombi yanaweza kupelekwa mahakamani kutaka
mtekelezaji au msimamizi aondolewe na/ au usimamizi wake
kutenguliwa.

Je, ni wakati gani Mahakama inaweza kubatilisha


uthibitishwaji wa Mtekeleza mirathi au kukataa uteuzi wa
Msimamizi wa mirathi?

Kifungu namba 49(1) cha Sheria ya Mirathi na Usimamizi wa


Mali ya Marehemu,

22 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


(Probate and Administration of Estate Act,) Sura ya 352 kinaeleza
kuwa Mahakama yaweza kubatilisha uthibitishwaji wa
mtekelezaji mirathi au kufuta uteuzi wa msimamizi wa mirathi,
endapo itabaini yafuatayo;
i. Kwamba mwenendo wa kupata utekelezaji au usimamizi
wa mirathi ulikuwa na dosari za msingi,
ii. Kwamba utekelezaji au usimamizi wa mirathi ulipatikana
kwa udanganyifu baada ya kutoa mapendekezo ya uwongo
au baada ya kuificha mahakama habari muhimu na za
msingi katika mirathi hiyo,
iii. Kwamba utekelezaji au usimamizi wa mirathi ulipatikana
kwa njia ya malalamiko ya uwongo juu ya jambo la muhimu
la kisheria ili kuthibitisha kupatikana kwa utekelezaji au
usimamizi wa mirathi, ingawa mlalamiko hayo yalifanywa
kwa kutojua au bila nia mbaya,
iv. Kwamba utekelezaji au usimamizi wa mirathi umekuwa
hauna maana na haitekelezeki,
v. Kwamba mtu aliyepewa utekelezaji au usimamizi wa
mirathi, kwa makusudi ameamua kutopeleka orodha
ya mali za marehemu kulingana na sehemu ya kumi na
mmoja ( XI) ya Sheria ya Mirathi na Usimamizi wa Mali
za Marehemu, Sura ya 352 au chini ya sheria hiyo hiyo,
amepeleka mahakamani orodha au taarifa ya uwongo ya
mgawanyo wa maliza marehemu.

Ikiridhika kwamba mirathi imeendeshwa kinyume na taratibu


sahihi zinazoongaza mirathi kisheria na /au kinyume cha
masilahi ya warithi, mahakama huwafutia uthibitishwaji au
uteuzi, mtekelezaji au msimamizi wa mirathi na badala yake
huagiza mtu mwingine ateuliwe na kupewa madaraka ya
usimamizi wa mirathi hiyo.

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 23


Maombi ya Kupewa Usimamizi wa Muda wa Mirathi
Wakati maombi ya kuomba usimamizi au utekelezaji wa mirathi
yanaendelea mahakamani, mwombaji anaweza kuiomba
mahakama impe usimamizi wa mirathi wa muda.

Msimamizi aliyepewa usimamizi wa muda anakuwa na


majukumu sawa na msimamizi aliyethibitishwa au kuteuliwa
na mahakama ya kukusanya na kutunza mali ya marehemu,
isipokuwa hawezi kugawa mali ya marehemu kwa warithi.

Lengo la kutoa usimamizi huu wa muda, ni kuwawezesha


kutimiza majukumu ya haraka kama vile matunzo kwa watoto
na mjane.

Wajibu wa Mahakama Katika Kuthibitisha Mtekelezaji au


Kuchagua] Msimamizi wa Mirathi
Endapo mtu ameomba kuthibitishwa au kuteuliwa kuwa
mtekelezaji au msimammizi wa mirathi, mahakama inao wajibu
wa kuchunguza kwa makini na kujiridhisha kwamba mtu huyo
anayeomba kuthibitishwa au kuteuliwa kuwa mtekelezaji au
msimamizi wa mirathi, anayo maslahi katika mirathi hiyo na
ataweza kufanya kazi hiyo kwa makini na uaminifu mkubwa
kulingana na matakwa ya marehemu (kama yanaweza
kubainika) katika kusimamia mali hizo.

Wajibu wa Mtekelezaji au Msimamizi wa Mirathi


Kadiri ya Jedwali la tano la Sheria ya Mahakama za Mahakimu
na fungu la 99 la Sheria ya Mirathi na Usimamizi wa mali
za marehemu, mtekelezaji au msimamizi wa mirathi ya
marehemu ndiye mwakilishi wa marehemu kisheria na mali
zote za marehemu ziko mikononi mwake. Hivyo mtekelezaji
au msimamizi wa mirathi ya marehemu anao wajibu na au
majukumu kama inavyoainishwa hapa chini;

24 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


• Kukusanya mali zote za marehemu kwa uaminifu na
uangalifu mkubwa,
• Kupeleka orodha ya mali ya marehemu au madeni
alivyoweza kukusanya,
• Kupokea na kulipa madeni halali ya marehemu, ikiwani
pamoja na kulipa gharama zitokanazo na usimamizi,
• Kugawanya mali iliyobaki kwa warithi halali wa marehemu,
• Kuifahamisha mahakama juu ya ugawaji wa mali za
marehemu ulivyofanyika na kama umekamilika au muda
zaidi uongezwe ili aweze kukamilisha ugawaji wa mali ya
marehemu na kuiwezesha mahakama kufunga jalada la
mirathi,
• Kulingana na fungu la 100 la Sheria ya Mirathi na Usimamizi
wa Mali za Marehemu, mtekelezaji au msimamizi wa mirathi
anaweza kushitaki au kushitakiwa katika shauri lolote jipya
au ambalo marehemu ama alianzisha au lilifunguliwa dhidi
yake,
• Kadri atakavyoona inafaa, na kadiri ilivyo kwa masilahi
ya warithi, mtekelezaji au msimamizi wa mirathi, anaweza
kuuza mali inayohamishika kutoka katika mirathi ya
marehemu,
• Mtekelezaji au msimamizi wa mirathi hawezi kutengeneza
au kupata faida kutokana na usimamizi wake,isipokuwa
kama wosia umesema hivyo.

Angalizo Muhimu: Msimamizi wa mirathi yeye siyo mrithi wa


mali ya marehemu. Maana kumekuwepo na dhana potofu kwa
watekelezaji au wasimamizi wa mirathi walio wengi, kwamba
baada ya mtu kuthibitishwa au kuteuliwa kuwa mtekelezaji au
msimamizi wa mirathi, basi amerithishwa mali hizo moja kwa
moja na anaweza akafanya anavyotaka juu ya mali hizo. Kisheria
jambo hilo si la kweli na hiyo ni dhana potofu. Baada ya kuteuliwa
au kuchaguliwa kuwa msimmizi wa mirathi, anao wajibu wa
kukusanya mali na kuzigawa kwa warithi halali wa marehemu,

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 25


katika muda uliopangwa na kutoa taarifa mahakamani kwamba
zoezi hilo limefanyika salama na limekamilika. Kinyume na
hapo, anatenda kosa la jinai.

Haki za Warithi Dhidi ya Mtekelezaji/Msimamizi wa Mirathi


Endapo mtekelezaji au msimamizi wa mirathi amesimamia
au ametumia mirathi ya marehemu vibaya, warithi halali wa
marehemu, pamoja na mambo mengine, waweza kufanya
yafuatayo;
a. Kulingana na fungu namba 49(1)(e) na (2) cha Sheria ya
Mirathi na Usimamizi wa Mali za Marehemu, Sura ya 352,
warithi hao, wanaweza kuiomba mahakama kumfutia
utekelezaji au usimamizi wa mirathi na hivyo kulazimika
kurudisha mahakamani hati zote zilizotolewa na mahakama
kuthibitisha utekelezaji au usimamizi wake wa mirathi, ili
mahakama iweze kumchagua mtu mwingine,
b. Kama amekataa kurudisha mahakamani hati zote
zilizotolewa na mahakama kuthibitisha utekelezaji au
usimamizi wake wa mirathi, warithi wanaweza kumshitaki
chini ya fungu namba 51 kifungu cha pili, na akikutwa na
hatia anaweza kutozwa faini au kifungo kisichozidi miezi
mitatu au vyote faini na kifungo,
c. Kama mtekelezaji huyo na/au msimamizi wa mirathi
amesimamia vibaya au ameharibu mali ya marehemu,
warithi au mtu yeyote mwenye maslahi na usimamizi huo,
anaweza kumfikisha mahakamani akimtaka alipe fidia kwa
uharibifu au hasara aliyosababisha. Mfano mzuri ni katika
shauri la Safiniel Cleopa dhidi ya John Kadeghe (1984)
Mahakama Kuu, kupitia Mheshimiwa Jaji Chua, ilisema
kwamba msimamizi ambaye ameharibu, kutumia vibaya
au kusababisha hasara kwenye mali ya marehemu, lazima
arekebishe hasara au uharibifu huo.

26 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA


Hitimisho
Hapa Tanzania mambo yanayohusu mirathi hayapo katika
sheria moja, ingawa hiyo ni sheria nyeti na ina mguso mkubwa
katika jamii. Jambo hili limesababisha utata mkubwa katika
kuchagua sheria ipi itumike na wakati mwingine kusababisha
baadhi ya wanajamii hasa wajane na wanawake kupoteza haki
yao ya urithi.

IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA 27


28 IJUE SHERIA YA URITHI, MIRATHI NA WOSIA

You might also like