You are on page 1of 142

MIONGOZO MIWILI

KUPAA NA KUTUNGULIWA KWA


AZIMIO LA ARUSHA

Yamekusanywa na kuhaririwa na:

Bashiru Ally
Saida Yahya-Othman
Issa Shivji

NYERE
RE

DA CHA T
A
GO
KI

U
IM
AL

A CHA M
W
UM
AL

CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM


Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere katika Umajumui wa Afrika
S. L. P. 35091, Dar es Salaam, Tanzania Simu: +255 22 2410 763
Barua pepe: mwalimuchair@udsm.ac.tz Tovuti: nyererechair.udsm.ac.tz
Kitabu hiki kimechapishwa kwa ufadhili wa Shirika la HakiElimu katika maadhimisho
ya Tamasha la Tano la Kitaaluma la Julius Nyerere, Aprili 10-12, 2013, lililoandaliwa
na Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere katika Umajumui wa Afrika,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

NYERE
RE

DA CHA T
A
GO
KI

U
IM
AL

A CHA M
W
UM
AL

CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM


Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere katika Umajumui wa Afrika
S. L. P. 35091, Dar es Salaam, Tanzania Simu: +255 22 2410 763
Barua pepe: mwalimuchair@udsm.ac.tz Tovuti: nyererechair.udsm.ac.tz
Kitabu hiki kimechapishwa kwa ufadhili wa Shirika la HakiElimu katika maadhimisho
ya Tamasha la Tano la Kitaaluma la Julius Nyerere, Aprili 10-12, 2013, lililoandaliwa
na Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere katika Umajumui wa Afrika,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

ISBN 978-9987-9418-2-7

YALIYOMO
Dibaji

Utangulizi: Ujio na uzito wa Miongozo Miwili


Kingunge Ngombale Mwiru

11

Sura ya Kwanza

Azimio la Arusha la 1967

23

Sura ya Tatu

Mwongozo wa CCM wa 1981

55

Sura ya Pili

Mwongozo wa TANU wa 1971

43

Sura ya Nne

Maamuzi ya Zanzibar ya 1991

116

Sura ya Tano
Miongozo Miwili ya Chama na tabaka lililopindua Ujamaa
Issa Shivji

MIONGOZO MIWILI

132

DIBAJI
Kitabu hiki kimeandaliwa na Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere
kwa ajili ya kuweka kumbukumbu ya matukio muhimu katika historia
ya nchi yetu tangu Uhuru. Kuna nyaraka nne katika kitabu hiki: Azimio
la Arusha la 1967, Mwongozo wa 1971, Mwongozo wa 1981 na Maamuzi
ya Zanzibar ya 1991, ambayo ni hotuba ya Mzee Ali Hassan Mwinyi. Kwa
nini tumechagua nyaraka hizo na sio nyengine? Kwa sababu kila nyaraka
ina muhula wa kihistoria wa kuhadithia. Muongo mmoja kati ya 1971
na 1981 ni kipindi cha uzalendo wa hali ya juu, uzalendo wa mrengo wa
kushoto, uliozaliwa na itikadi ya Umajumui wa Afrika (Pan-Africanism).
Kipindi hiki kilipewa jina rasmi la kipindi cha Ujamaa na Kujitegemea.
Mwongozo wa 1981 ni waraka wa kipekee ambayo inafanya uchambuzi
wa miaka 14 ya Azimio kwa mtazamo wa kitabaka, ambao, lazima tukiri,
haukuwa mtazamo wa Chama wala Mwalimu.
Muongo wa 1981 mpaka 1991 ni kipindi cha mpito kutoka muhula
wa kizalendo na kuingia muhula wa uliberali mambo-leo. Maamuzi ya
Zanzibar ya 1991 (kwa msamiati wa kisiasa huitwa Azimio la Zanzibar),
ni hotuba ya Rais wa Awamu ya Pili, inayoelezea na kuhalalisha mtazamo,
mwelekeo, itikadi na sera za uliberali mambo-leo.
Baada ya kuchagua nyaraka hizi, tukamuomba Mzee Kingunge Ngombale
Mwiru, kutuandikia Utangulizi wa Miongozo Miwili. Mzee Ngombale
anajulikana kwa sifa yake ambayo anaistahili - ya kuzungumzia itikadi
na nadharia ya Chama kwa ufasaha, na kwa undani; ni kingunge hasa
wa itikadi ya Chama. Yeye amekuwa mwanaitikadi (ideologue) wa Chama
kwa miongo kama minne hivi. Umahiri wake wa kiitikadi unadhihirishwa
vema na ukweli usiopingika kwamba amekuwa msemaji mkuu wa itikadi
ya Chama katika awamu zote za utawala wa kisiasa nchini kuanzia
awamu ya Mwalimu, ambayo ilikuwa awamu ya kizalendo; kupitia awamu
ya Mzee Ali Hassan Mwinyi ambayo ilikuwa awamu ya mpito kuelekea
kwenye uliberali mambo-leo; ikifuatiwa na awamu ya Mheshemiwa
Benjamin William Mkapa, ambayo ilikuwa awamu ya kuiimarisha bila
vikwazo misingi mikuu ya uliberali mambo-leo, au kwa msamiati wake
4

MIONGOZO MIWILI

mwenyewe, utandawazi; kufikia kipindi cha kwanza cha Mheshemiwa


Jakaya Mrisho Kikwete ambaye amefuata nyayo za Mzee Mkapa na kwa
mara ya kwanza utawala wake umeanza kuonja joto kali la uchumi wa
ubepari wa kimataifa.

Ili tuweze kuelewa kwa ufasaha na kwa kina, hasa chimbuko la


Miongozo Miwili na umuhimi wake wa kihistoria, tumeweka makala
ya mwanazuoni Issa Shivji, iliyoandikwa kwa mara ya kwanza mnamo
2009, inayochambua Miongozo hii kwa mtazamo wa kitabaka.

Azimio la Arusha, 1967

Miaka sita tu baada ya Uhuru wetu mnamo 1961, chama tawala,


TANU, ambacho kwa asili na hulka yake tunaweza tukakiita chama
cha ukombozi, kilitangaza Azimio la Arusha (ang. Sura ya Kwanza).
Azimio lilikuwa ni dalili ya kutambua kwamba uhuru wa nchi na watu
wake haukamiliki kutokana na kupata wimbo na bendera ya kitaifa au
mawaziri na viongozi wazawa.
Uhuru wa kinchi kilichotawaliwa na wakoloni ni hatua ya kwanza, ya
awali kabisa, katika mchakato wa ukombozi. Ukombozi katika jamii kama
yetu una pembe tatu. Kwanza kuna uhuru wa nchi, kwa maana kwamba,
huwezi ukawa huru katika nchi ambayo inatawaliwa kimabavu na nchi
ya nje. Pili, kuna uhuru wa watu au jamii katika nchi. Unaweza ukawa na
nchi huru bila ya watu kuwa huru, kwa maana kwamba hawana uwezo
wa kujiamulia mambo yao wenyewe. Ingawa nchi yao ni huru, lakini bado
wanajikuta kwamba kuna kundi au tabaka dogo la watu wanaowatawala
na kufanya maamuzi kwa niaba yao au kwa ajili ya waliowengi. Katika
hali yetu halisi, tabaka-tawala la ndani linakuwa bado chini ya himaya ya
ubeberu na kwa hiyo watawala hao wanakuwa vibaraka wa matabakatawala ya kibeberu. Na hali hii inasababisha, sio tu tabaka-tawala la ndani
kuwa tegemezi, lakini hata nchi yenyewe inakuwa tegemezi kwa sababu
inakosa uongozi unaojitegemea na kufanya maamuzi kwa manufaa na
maslahi ya watu wake.
Pembe ya tatu ya ukombozi ni ukombozi wa wavujajasho kutoka makucha
ya unyonyaji na ukandamizaji. Na ukombozi wa kijamii-tabaka (social
MIONGOZO MIWILI

emancipation) hauwezi kupatikana bila kufanya mapinduzi ya mfumo


wenyewe wa uzalishaji na utawala; kwa sababu unyonyaji na ukandamizaji
havitokani na nia, dhamira au lengo la mtu binafsi. Hakuna mtu anayezaliwa
akiwa mnyonyaji. Tabaka la wanyonyaji linatokana na nafasi yao katika
mfumo wa uzalishaji. Ukiwa bepari, bila kujali usamaria mwema wako,
lazima utakuwa mnyonyaji. Ndivyo ulivyo mfumo wa kibepari.

Azimio la Arusha lilizungumzia pembe zote tatu za ukombozi. Mosi,


lilitambua kwamba uhuru wa nchi hautakuwa na maana wala hautakuwa
salama kama tukiendelea kuwa tegemezi, yaani, kutegemea misaada,
mikopo na uwekezaji kutoka nje. Kwa sababu mikopo haitapatikana
ya kutosha na hiyo kidogo itakayopatikana itaambatana na masharti
yatakayoididimiza nchi zaidi. Isitoshe, hata kama tungepata misaada,
mikopo na uwekezaji kwa ajili ya maendeleo, vitahatarisha uhuru
wetu. Kujitawala ni kujitegemea. Kujitawala kwa kweli hakuwezekani
ikiwa Taifa moja linategemea misaada na mikopo ya Taifa jingine kwa
maendeleo yake. (ang. Sura ya kwanza, uk) Ukweli huu unajidhihirisha
wazi tukiangalia mwenendo wetu wa kama miongo miwili iliyopita.
Tumekuwa tegemezi sana kiasi kwamba leo hii hatuna uhakika kwamba
tunajitawala au tunatawaliwa na wawekezaji na wafadhili wa nje, yaani,
nchi za kibeberu.
Pili, Azimio liliainisha matabaka-nyonyaji na matabaka-nyonywaji mabepari na makabaila kwa upande mmoja na wakulima na wafanyakazi
kwa upande mwingine. Nchi yenye Ujamaa kamili ni nchi ya wafanyakazi:
haina ubepari wala ukabaila. (ang. Sura ya kwanza, uk.25)

Hata hivyo, mkakati wa Azimio wa kujikomboa kutokana na unyonyaji


ulikuwa ni kutaifisha njia kuu za uchumi kwa maana ya serikali kumiliki
na kudhibiti viwanda vikubwa, migodi, mabenki, taasisi nyingine za
fedha, na biashara za nje na ndani. Ni ukweli usiopingika kwamba Azimio
lilitambua kwa dhati kuwa haitoshi serikali kumiliki njia za uchumi
kama serikali yenyewe sio ya kidemokrasia, kwa maana ya kudhibitiwa
na kuwajibika kwa wananchi. Hata hivyo, kama tutakavyobainisha hivi
punde, katika suala la demokrasia Azimio halikufanikiwa, pamoja na
kuwa na nia njema ya kukomboa wanyonge. Wanyonge hujikomboa wao
wenyewe kupitia vyombo vyao na huendeleza mapambano ya kitabaka
6

MIONGOZO MIWILI

kwa ustadi na kwa kutumia mikakati yao wenyewe. Mapinduzi kamwe


sio fadhila ya wakubwa au wasamaria wema.

Mwongozo wa 1971

Baada ya miaka minne tu ya Azimio, TANU ikapitisha nyaraka nyingine


ya kihistoria, Mwongozo wa TANU (ang. Sura ya Pili). Msimamo wa
Mwongozo ulikuwa wa kimapinduzi zaidi kuliko ule wa Azimio. Mzee
Ngombale, katika Utangulizi wake wa kitabu hiki anaeleza kwa ufasaha
chimbuko la Mwongozo wa 1971 na maudhui yake. Aidha anasisitiza
ibara muhimu za Mwongozo kuhusu ulinzi wa Taifa dhidi ya ukoloni wa
Kireno na Kikaburu ambao waliendelea kukalia nchi za Afrika ya kusini.
Kwa msimamo thabiti wa Mwalimu, vita vya ukombozi katika nchi za
Msumbiji, Angola na Afrika ya kusini, viliungwa mkono na Tanzania
kwa hali na mali. Kwa hivyo, Tanzania yenyewe ilikuwa katika hatari ya
kuvamiwa au kushambuliwa. Ili kujilinda dhidi ya uwezekano huo, ndipo
Mwongozo wa 1971 ukaweka sera ya kuwa na Jeshi la Wananchi, kwa
maana ya mgambo.
Kama anavyoeleza Mzee Ngombale, wananchi, hasa wafanyakazi
viwandani, walishawishika sana na wakajitolea kujiunga na mgambo. Ni
sahihi kabisa kwa Mzee Ngombale kusisitiza kwamba sera hii ilifanikiwa
kiasi kwamba wakati nchi yetu ilipovamiwa na nduli Iddi Amin Dada,
dikteta wa Uganda, askari wa mgambo walipigana kwa ustadi na ujasiri.
Mchango wao kamwe hauwezi kusahaulika.

Lakini, kwa mtazamo wa kitabaka, nafasi mahsusi na ya kihistoria ya


Mwongozo inatokana na ibara yake ya 15. Ibara hii ambayo ilishutumu
tabaka chipukizi wakati huo la warasimu viwandani na serikalini ilikuja
kuwa panga na ngao ya tabaka la wafanyakazi kuibua na kuendeleza
mapambano yao dhidi ya tabaka la vibwenyeye wa kirasimu. Katika
historia ya mapambano ya tabaka la wafanyakazi nchini mwetu, hakuna
kipindi kilichokuwa na msisimko mkubwa kama hiki (1971-1975). Kwa
sababu ambazo haziko wazi, Mzee Ngombale, ingawa anagusia ibara
ya 15 katika Utangulizi wake, hakuchambua kwa undani umuhimu
wa kipekee wa ibara hii katika mapambano ya kitabaka. Hata hivyo,
MIONGOZO MIWILI

wasomaji wanaweza wakaangalia makala ya uchambuzi ya Shivji (ang.


Sura ya Tano) kuhusu mapambano hayo. Mapambano hayo, hatimaye,
yalidhoofishwa na kukosa nguvu na uhalali kwa tamko la Mwenyekiti wa
Chama, naye sio mwingine isipokuwa Mwalimu. Katika hotuba yake ya
Mei Mosi mwaka 1974 Mwalimu alihoji: Mnapogoma mnamgomea nani?
akiwa na maana kwamba kwa kuwa viwanda na mashirika yalikuwa
mali ya umma, wakiwemo wafanyakazi wenyewe, basi walikuwa
wanajigomea wenyewe!
Jibu la swali la Mwalimu kwamba wafanyakazi walikuwa wanamgomea
nani lilipatikana katika uchambuzi wa Mwongozo wa 1981.

Mwongozo wa 1981

Mchakato wa kuandaa Mwongozo wa 1981, kama ulivyoelezwa na Mzee


Ngombale, ni wa kipekee na ni tofauti na taratibu za Chama zilizozoeleka.
Kwanza, tuuelewe muktadha wa mchakato wenyewe. Kipindi cha
mwisho cha utawala wa Mwalimu, 1980-85, kilikuwa kigumu kupita
kiasi kutokana na sababu mbalimbali. Hapa sio mahali pake kuangalia
kwa undani sababu hizo isipokuwa kusisitiza tu kwamba ilikuwa katika
hali hii ndipo Mzee Ngombale mwenyewe alipoonyesha dhamira yake
ya kupendekeza kwamba Chama hakina budi kuzungumzia hali hii. Kwa
hivyo, mchakato wa Mwongozo haukuanzia katika sekretariati ya Chama
wala Kamati Kuu. Badala yake, ulianza kutokana na pendekezo lililotolewa
na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama (NEC), yaani Mzee Ngombale
mwenyewe. Pili katika kikao hikihiki cha NEC, kamati ya kuandaa
Programu, ikiwa ni pamoja na kufanya uchambuzi kosoa, ilichaguliwa.
Na kinyume na taratibu zilizozoeleka za Chama, aliyewasilisha Programu
katika Mkutano Mkuu alikuwa Mzee Ngombale na sio Mwenyekiti,
yaani Mwalimu mwenyewe. Kwa mujibu wa Mzee Ngombale, Mwalimu
alipendekeza kwamba nyaraka iitwe Mwongozo badala ya programu
kwa sababu wanachama walikuwa hawajazoea msamiati wa Programu.

Katika Utangulizi wake, mwandishi anaweka mkazo katika ibara za


Mwongozo wa 1981 zinazozungumzia suala la demokrasia katika
Chama na muundo wa Chama. Pia anatuarifu kwamba vyombo vya
Chama vilizungumzia Mwongozo. Kwa kadri ninavyokumbuka mimi,
8

MIONGOZO MIWILI

Mwongozo wa 1981 haukuwa gumzo la wananchi katika ujumla wao


kama ulivyokuwa ule wa 1971. Kwa kiasi kikubwa, Mwongozo wa 1981
ama ulisahaulika au ulisahaulishwa. Hakuna kumbukumbu zozote
zinazoonyesha kwamba Mwongozo wa 1981 ulipigiwa debe au kufanyiwa
kampeni au kuzungumziwa mitaani na matawini. Wazee wengi wa
chama waliokuwepo wakati ule, ukiwauliza juu ya Mwongozo wa 1981,
wanakuwa ama wanachanganya mambo au wanajifanya hawaukumbuki.
Hatuna ushahidi wa moja kwa moja, lakini ushahidi wa mazingira na
hali halisi unatulazimisha kujenga hoja kwamba Mwongozo wa 1981
haukuwa utashi wa viongozi wakuu wa CCM. Mwongozo wa 1981
unatahadharisha kwamba tayari kulikuwa na watu/wanachama ambao
walikuwa wananungunika na kusema kichinichini kwamba Ujamaa
ulishindwa na kulikuwa na haja ya kubadili mtazamo na mwelekeo wa
nchi. Mwongozo ulisema kwa ufasaha kwamba chini ya mwavuli wa
Azimio na sekta ya umma lilijengeka tabaka la vibwanyenye wa kirasimu
(bureaucratic bourgeoisie) ambalo lilikuwa linahujumu Ujamaa. Kwa
mara ya kwanza katika nyaraka ya Chama, mapambano ya kitabaka
yalizungumziwa waziwazi bila kutafuna maneno.
Makala ya Shivji (ang. Sura ya Tano) inajaribu kufanya uchambuzi
wa ibara muhimu za Mwongozo wa 1981. Hitimisho la makala hiyo
ni kwamba tabaka linaloshutumiwa katika Mwongozo kuhusiana na
hujuma dhidi ya Ujamaa ndilo likawa kinara wa kubeba mtazamo, itikadi
na sera za uliberali mambo-leo. Bila shaka, kama kawaida ya nchi zetu
ambamo matabaka-tawala ya ndani ni dhaifu, tabaka hili liliungwa
mkono na taasisi za kifedha za kimataifa na nchi za kibeberu wakiwemo
eti wafadhili. Kinadharia na kiitikadi, wasomi wa Chuo Kikuu, hususan
wachumi waliosoma Marekani, ndio wakawa wasemaji wakuu wa sera
za uliberali.
Hatimaye, Mwalimu akangatuka kwa hiari yake, na labda pia kwa
kutambua kwamba sera zake hazingefua dafu tena, na viongozi wa
awamu ya pili ndio wakakumbatia, hatua kwa hatua, sera za ulegezaji wa
masharti ya biashara, uwekezaji na ubinafsishaji.
Sura ya Nne inaashiria kuzikwa kwa Azimio na mambo yote yalosimamiwa
MIONGOZO MIWILI

na Azimio. Bila shaka, Mzee Ruksa bado anajitangaza kuwa muumini wa


Azimio. Kwake yeye, maamuzi ya Zanzibar yalipitishwa ili kupanua tafsiri
ya Azimio na sio kulizika. Kila zama ina Mwongozo wake, anasema Mzee
Mwinyi katika hotuba yake, na mwongozo wa zama ya uliberali mamboleo ni Azimio la Zanzibar! Naam.

Hitimisho

Sio nia yangu kuendelea kuchambua historia yetu ya miongo miwili


tangu Maamuzi ya Zanzibar. Ni juu ya vijana-wanazuoni wetu kuchambua
hali halisi na hasa zama zetu hizi za misukosuko na zahma za kisiasa
na kiuchumi. Jukumu mojawapo la Kigoda ni kuibua mijadala juu ya
masuala muhimu na magumu ambayo watawala hupenda kuyakwepa
au kuyazika. Nia yetu ya kuchapisha upya toleo hili la nyaraka muhimu
katika historia yetu ni kuwakumbusha vijana-wanazuoni kwamba
huwezi ukaelewa kwa undani na ufasaha hali iliyopo bila kuelewa na
kuchambua hali iliyotangulia na iliyozaa hali ya leo.

Shukrani

Kwa mara nyingine tena ningependa kuishukuru taasisi ya HakiElimu na


hasa Mkurugenzi Mtendaji wake Bi. Elizabeth Missokia kwa kuwezesha
uchapishaji wa kitabu hiki. Ninapenda pia kumshukuru Mzee Ngombale
kwa kutuandikia Utangulizi. Namshukuru kwa namna ya kipekee
mchoraji mashuhuri wa katuni , Masudi Kipanya kwa kutuchorea katuni
murua.
Mwisho, bila ya ushupavu, ukereketwa na uchapakazi wa wanakigoda,
hasa Mwalimu Bashiru Ally, Profesa Saida Yahya-Othman na Walter
Rodney Luanda, tusingeweza kukamilisha kitabu hiki. Asanteni sana na
kila la heri.
Issa Shivji
Profesa wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Aprili 2013
10

MIONGOZO MIWILI

UTANGULIZI
UJIO NA UZITO WA
MIONGOZO MIWILI
Kingunge Ngombale Mwiru

Mwongozo wa TANU wa 1971


Mwongozo wa TANU wa 1971 ni mwendelezo wa moyo wa Azimio la
Arusha. Waandazi wa Mwongozo huu ni watu waliojazwa hisia kali za
uzalendo zilizotamka: tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa
kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio
uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka kufanya
mapinduzi, ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na tusipuuzwe tena!
Katika moyo ule ule wa Azimio la Arusha, Mwongozo wa TANU wa 1971
unapalilia ari ya mapambano ya Waafrika dhidi ya Ukoloni, UkoloniMamboleo na Ubeberu na dhidi ya Waafrika wanaotumia madaraka
kufifisha Uhuru na kudhalilisha utu wa wananchi.

Ujio wa Mwongozo

Mwongozo wa TANU wa 1971 ulitolewa na kutangazwa na Halmashauri


Kuu ya Taifa ya TANU ya dharura mwanzoni mwa mwezi wa Februari,
Dar es Salaam. Mwezi wa Januari mwaka 1971 Jeshi la Uganda chini
ya Iddi Amin Dada, liliangusha serikali ya Rais Milton Obote na kutwaa
madaraka. Kufika Agosti kitendo cha uchokozi kisicho cha kawaida kikosi
cha Jeshi la Iddi Amin kilikivamia kikosi cha doria cha polisi wa Tanzania
mpakani Mutukula na kumteka nyara Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC)
na kumtoroshea Uganda.

Kitendo hiki cha uhasama kutoka kwa nchi jirani kilihitaji kupatiwa
jibu la haraka na la kimkakati. Ndipo nilipoitwa Ofisini kwa Makamu
MIONGOZO MIWILI

11

wa Pili wa Rais, Ndugu Rashid Mfaume Kawawa, ambaye nilimkuta na


Meja Hashim Mbita (wakati ule Katibu Mtendaji Mkuu wa TANU). Ndugu
Kawawa alinieleza kwa kifupi kuwa Mwalimu alimwagiza aniarifu
kuwa ameamua mimi niongoze timu ya viongozi wa vijana kadhaa wa
TYL kwenda Mkoa wa Ziwa Magharibi kufanya kazi ya kuhamasisha
wananchi kisiasa na kiulinzi na usalama ili waweze kukabiliana ipasavyo
na chokochoko zozote zile kutoka nchi jirani.

Pamoja na kukubali jukumu nililopewa na kuahidi kuanza maandalizi


mara moja, nilitoa rai kwa Makamu wa Pili wa Rais kwamba kwa kuwa
tishio kwa usalama wa nchi kutoka Uganda ni sehemu tu ya tishio
kwa taifa maana kuna tishio kubwa zaidi kwenye Ukanda wa Kusini
la majeshi ya Wareno na uhasama wa Wareno na uhasama wa dola za
Afrika ya Kusini na Rhodesia, ingekuwa busara kuitisha kikao cha NEC
kutafakari juu ya ulinzi na usalama wa Taifa. Ndugu Kawawa alikubaliana
na pendekezo langu na palepale aliondoka akifuatana na Ndugu Hashim
Mbita, kwenda kuonana na Mwalimu Ikulu. Walirejea baada ya nusu saa
na kunitaarifu kuwa Mwalimu amekubali pendekezo nililolitoa na tayari
ameagiza NEC iitishwe kwa dharura.
Kikao cha NEC kilipoketi wiki moja baadaye mimi nilipata fursa ya
kufungua dimba la mjadala baada ya hotuba fupi ya ufunguzi ya
Mwenyekiti. Pamoja na kuchangia mawazo kuhusu mapambano ya
ukombozi wa Afrika na suala muhimu wakati ule la kuunga mkono vyama
halisi vya ukombozi wa nchi za Afrika, nilitumia muda kujenga hoja ili
NEC iikubali dhana ya msingi ya ulinzi na usalama wa Umma ambapo
wananchi wenyewe ndio wanaokabidhiwa jukumu la ulinzi na usalama
wao. Wananchi wote wanahusika na ulinzi na usalama wao kwa njia ya
ulinzi wa mgambo na majeshi ni sehemu ya mstari wa mbele wa ulinzi na
usalama huo wa Umma.

Utekelezaji wa Mwongozo wa TANU na mafanikio yake

Kupitishwa na kutangazwa kwa Mwongozo wa TANU wa 1971 kulipokewa


kwa shangwe kubwa sana hasa Dar es Salaam. Matawi mengi ya chama
12

MIONGOZO MIWILI

wakati huo jijini Dar es Salaam yalianzisha utaratibu wa wanachama wote


kukutana baada ya kazi ili kuzijadili ibara moja moja za Mwongozo. Matawi
mengine yalianzisha madarasa ya itikadi ili kujadili Mwongozo. Maelfu ya
wafanyakazi wa jijini Dar es Salaam walijiunga na mafunzo ya ulinzi wa
mgambo kuitikia wito wa Mwongozo wa TANU. Wakati wa mafunzo ya
mgambo muda kidogo ulitengwa kujadili ibara za Mwongozo.

Makada waliohamasisha wakazi kujiunga na ulinzi wa mgambo walijenga


hoja za uzalendo. Basi msimamo na lugha iliyotawala miongoni mwa
wanamgambo ilikuwa ya kizalendo na kuihami nchi. Wanazuoni wa
historia watakuja kufanya tathmini na kutoa kauli lakini sisi wenye
busara za kawaida tu tunaweza kutamka bila kukosea kwamba uamuzi
wa NEC ya TANU ya Februari 1971 kukubali sera ya ulinzi wa mgambo
na kuagiza itekelezwe ulikuwa mwafaka na ulisaidia sana kuyafanya
matokea ya vita ya Kagera kuwa yalivyokuwa.
Hali ilivyo hivi sasa ni kwamba tunahitaji kuifanyia uchambuzi na tafakuri
ya kina hali ya sasa ya ulinzi wa mgambo tukizingatia hoja za ibara za 21,
22 na 23 za Mwongozo wa 1971 zilizotufikisha kwenye uamuzi wa kuwa
na sera ya ulinzi wa mgambo nchini.

Katika kuhitimisha sehemu hii napenda kusisistiza kuwa suala la sera


ya ulinzi na usalama wa Umma ambalo ndilo linaloibeba sera ndogo
sahihi ya ulinzi wa mgambo ndio uamuzi mkuu wa Mwongozo wa
TANU wa 1971. Dhana na nadharia ya ukombozi wa Mwafrika na hasa
kama ilivyochambuliwa katika ibara ya 28 ya Mwongozo wa 1971 ina
umuhimu wa kipekee hasa kwa viongozi na watafutao madaraka ya
kisiasa nchini kwetu. Ibara ya 28 inatuambia kuwa kwa watu waliotokana
na mifumo kandamizi kama Utumwa, Ukoloni, Ukabaila au/na Ubepari,
maendeleo ni ukombozi. Na ukombozi unaainishwa kama kitendo
kinachowaongezea watu uhuru wa kuamua mambo yao wenyewe na
kutawala maisha yao wenyewe.
Mwongozo katika ibara hii ya 28 unaendelea kusema kwetu sisi
maendeleo yenye maana ni yale yanayotuondolea kuonewa, kunyonywa,
MIONGOZO MIWILI

13

kunyanyaswa na mawazo ya kufungwa, na kutuongezea uhuru na utu


wetu.

Mwongozo unalileta suala la maendeleo ya watu kwa kutamka: Kwa hiyo


katika kufikiria maendeleo ya Taifa letu na katika kupanga mipango ya
maendeleo wakati wote mkazo mkubwa uwekwe kwenye maendeleo ya
WATU na sio ya vitu. [W]atu wenyewe lazima washiriki katika kufikiria,
kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo yao.

Mwongozo wa 1981

Mwongozo wa CCM wa 1981, kama ulivyokuwa mwongozo wa TANU


wa 1971, ulikuwa ni mwendelezo wa fikra na matarajio ya Ujamaa na
Kujitegemea uliotangazwa na Azimio la Arusha. Mwongozo huu ni
matokeo ya mila iliyokuwa imejengwa ndani ya Chama ya kutumia
vikao vikuu vyake, hususan NEC, kujadili na kuchambua masuala mazito
ya nchi, ya siasa, uchumi na jamii, na kuyatolea maelekezo ya kisera,
kiufafanuzi na kiutekelezaji.
Wakati Mwongozo wa TANU wa 1971 ulijielekeza kwenye mapambano
dhidi ya Ukoloni, Ukoloni-Mamboleo na Ubeberu ili kufanikisha
Ukombozi wa Afrika na wa Mwafrika na kuweka mkakati wa ulinzi na
usalama wa umma ili nchi iwe na uwezo wa kukabiliana na uvamizi
wowote kutoka kwa ubeberu au na vibaraka vyake, Mwongozo wa CCM
wa 1981 umejikita katika kufanya uchambuzi kosoa wa kina na mpana
juu ya hali ya kisiasa na kiuchumi iliyokuwepo nchini, hali ya maendeleo
ya demokrasia nchini na ndani ya chama, n.k., na kutoa mapendekezo ya
kuimarisha na kupanua demokrasia katika Chama na nchi.

Ujio wa Mwongozo

Mambo matatu yaliwezesha kikao kiamue kujadili yaliyomo katika


Mwongozo huu. La kwanza ni kuwa hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii
ilikuwa ngumu wakati ule na hivyo kuhitaji kuzungumzwa. Pili ni ujasiri na
umahiri wa mmoja wa wajumbe wa NEC ambaye kwa unyenyekevu kabisa
alitoa ombi la kusema jambo kabla shughuli kuanza. Aliporuhusiwa na kiti
14

MIONGOZO MIWILI

alisema kama hivi: Ndugu mwenyekiti na ndugu wajumbe naamini wote


mnafahamu hali yetu ya sasa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hali ni ngumu.
Ingefaa tutumie muda wa kikao hiki kutafakari na kufanya uchambuzi wa
kina juu ya hali ya sasa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ili tupate mikakati ya
kukipa chama chetu na serikali zake nguvu na msukumo mpya na uwezo
zaidi wa kuwahudumia wananchi. Naomba kikao chetu kijadili hali ya
nchi na ya chama chetu. Sababu ya tatu ni usikivu aliokuwa nao Mwalimu
Nyerere kwa mambo yaliyohusu watu na yanayoihusu nchi. Na katika
hili, mara mjumbe alipomaliza kusema na kukaa Mwalimu alinena naona
hili ni jambo jema, wakati umefika wa kuzungumzia hali yetu. Mnaonaje
wajumbe? Wajumbe wote wakaunga mkono.
Mjadala ulianza mara baada ya kikao kupitisha kumbukumbu za
mkutano uliotangulia pamoja na yatokanayo yake. Mimi niliyetoa hoja
ya kuomba mjadala huo maalum ufanyike nilipewa nafasi ya kuanzisha
mazungumzo. Wajumbe wengi wa kikao hicho walishiriki kwa kuchangia
mawazo katika mjadala ulioendelea kwa siku mbili.

Jioni ya siku ya pili, Mwenyekiti alipendekeza majina ya wajumbe


wa Kamati. Kutokana na pendekezo la msemaji wa kwanza kwamba
NEC iunde Kamati itakayoandaa Programu ya Chama yenye kuainisha
majukumu makuu (Central Tasks) katika kipindi ambacho kingeamuliwa
pamoja na mpangilio wa vipaumbele katika maeneo mbali mbali ya
kiuchumi na kijamii bila kusahau maendeleo ya chama chenywe, kamati
ikaitwa kamati ya Programu ya Chama.
Wajumbe wa kamati walikubaliana kumchagua Ndugu Peter Siyovelwa
(marehemu) kuwa Mwenyekiti wake na Kingunge Ngombale Mwiru
kuwa Katibu/Rapporteur. Wajumbe wengine walikuwa Ndugu Peter
Kisumo, Moses Nnauye (Marehemu), Getrude Mongella, Maalim Seif
Shariff Hamad, Isaac Sepetu, Pius Msekwa na Joseph Sinde Warioba
(hawa wawili wa mwisho walichaguliwa baadae).
Wajumbe wa Kamati ya Programu ya Chama walipiga kambi mjini Dodoma
ili kufanya kazi waliyopewa. Kwanza wajumbe walijadili mapendekezo ya
MIONGOZO MIWILI

15

sura ya Programu na dondoo za kila SEHEMU yake na kukubaliana nayo.


Baada ya hapo, kwenye kila hatua, wajumbe walipokea na kujadili kwa
kina rasimu ya maudhui ambayo Katibu wa Kamati aliwasilisha. Rasimu
mpya juu ya sehemu iliyojadiliwa iliandaliwa kwa msingi wa mwelekeo wa
michango ya wajumbe na uzito wa hoja.

Rasimu za kwanza ya Programu ya Chama iliwasilishwa kwenye NEC ya


Mwezi Septemba 1981. Mjadala wa NEC ulikuwa wa kusisimua kulingana
na mawazo chanya na changamfu yaliyobebwa na Programu hiyo.
Ilibainika waziwazi kuwa maudhui ya Programu yatahitaji marekebisho
makubwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na baadhi ya sheria. Kwa
hivyo, NEC iliona vyema kuwateua wajumbe wapya wawili wa Kamati ya
Programu, Ndugu Pius Msekwa na Ndugu Joseph Sinde Warioba.
Kamati iliagizwa kwenda kuandaa rasimu ya mwisho kwa ajili ya NEC
ya Desemba 1981. NEC ilikutana Mwezi Desemba 1981 ili kupitisha
Programu hiyo. Mambo mawili yalitokea. Kwanza Mwalimu alishauri
kuwa Programu ya chama tuiite Mwongozo wa chama wa 1981; neno
Programu ni jipya lingeweza kuwatatanisha watu bure. Na pili kutokana
na pendekezo la Mwenyekiti iliamuliwa kuwa Mwongozo wa CCM wa
1981 upitishwe na kutangazwa na Mkutano Mkuu wa dharura ambao
ungefanyika Tarehe 19 Januari, 1982, Dar es Salaam.
Mkutano Mkuu ulifanyika kama ilivyopangwa. Baada ya kuufungua
mkutano na kuwakaribisha wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa
Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere, alimwomba Katibu wa Kamati, Ndugu
Kingunge Ngombale Mwiru, awasilishe Mwongozo wa CCM wa Mwaka
1981 kwa niaba ya Halmashauri Kuu ya Taifa.
Mkutano Mkuu ulipokea Mwongozo wa 1981.

Mwongozo wa 1981: maudhui na utekelezaji


MWONGOZO wa CCM wa 1981 uliandaliwa ili kukiwezesha Chama cha
Mapinduzi kuikabili hali ngumu ya kiuchumi na kijamii ya wakati ule.
16

MIONGOZO MIWILI

Lakini ni muhimu ikumbukwe kuwa matarajio ya wananchi yaliyoibuliwa


na kutangazwa kwa Azimio la Arusha na Siasa ya TANU ya Ujamaa na
Kujitegemea yalichangia katika kuwasukuma Wajumbe wa NEC watoe
mawazo yaliyomo katika MWONGOZO huo. Ndiyo maana sehemu kubwa
ya maudhui ya MWONGOZO wa 1981 ni uchambuzi kosoa wa utekelezaji
wa Azimio la Arusha.

Waandazi wa MWONGOZO walikuwa na hisia kwamba sera za Chama na


hasa Azimio la Arusha, lilikuwa sahihi lakini mafanikio katika utekelezaji
wake ili yakidhi matarajio ya wananchi, yangehitaji Chama kiwe
madhubuti zaidi katika fikra, muundo na utekelezaji na serikali sawia.
Ili kufikia lengo hilo, walitumia methodolojia ya kufanya uchambuzi wa
kujikosoa kama Chama.

Sehemu hii ya pili ya MWONGOZO ina umuhimu mkubwa sana. Kwa


upande mmoja inaonyesha upungufu wa Chama katika maeneo
mbalimbali na hatua za kurekebisha ili kukiimarisha na kwa upande
mwingine inatoa mchango wa mawazo ambao ni mwongozo katika
nadharia ya ujenzi wa Chama. Katika kila kipengele kilichoorodheshwa
kwenye sehemu hii ya pili kuna mchango mahsusi wa kukifanya Chama
kiwe madhubuti na chenye ufanisi.
Tuchukue kipengele cha pili (2) katika Sehemu ya Pili ya MWONGOZO
inayosema Wana-CCM ndio askari wa mstari wa mbele wa mapambano
Historia yetu inatuonyesha jinsi wanaTANU waliopigania uhuru wetu
walivyokuwa na hamasa za kuupinga ukoloni na kukataa kutawaliwa.
Wito wa TANU na ASP uliwafanya washikamane kwa kauli na vitendo.
Tanzania Bara haikuchelewa kunyakuwa uhuru wake.
Tangu tupate Uhuru na Mapinduzi ya Zanzibar hadi sasa pumzi ya
wanachama wetu ya kusukuma mapambano na kujenga jamii mpya
imepungua hasa kwa kuachia ubinafsi uwe na nafasi kubwa katika siasa
na jamii kwa ujumla. Kwa wana CCM sasa kuwa askari wa mstari wa
mbele wa mapambano yetu kutahitajika mageuzi ya msingi. Lakini hili
bado linawezekana.

Wasomi wa falsafa wanasema nadharia ni mwanga muhimu kwa


wanaohusika na kutekeleza mambo, kutenda. Nadharia ni mwanga
MIONGOZO MIWILI

17

unaoangaza ili wanaohusika na kutenda waangaziwe. Ndiyo maana kuna


vipengele juu ya umuhimu wa nadharia sahihi ya Chama na Mshikamano wa
nadharia na vitendo. Uchambuzi huu umefanywa kwanza ili kuwaonyesha
wanaodharau nadharia kuwa wanakosea na pili kusisitiza kuwa viongozi/
makada wasioandaliwa vizuri katika nadharia wana hatari ya kufanya
kazi ya Chama kwa kubahatisha. Viongozi na makada wanatakiwa wawe
watu wanaojiamini, wenye uhakika na wanayoyaeleza, wenye uwezo wa
kujenga hoja na kutumia nguvu ya hoja siyo hoja ya nguvu, kuwaelimisha,
kuwashauri na kuwavuta watu upande wa Chama.

Suala la chombo na maudhui yake

Mwaka 1981 ulikuwa mwaka wa kumi na nne (14) tangu Azimio la


Arusha. Utekelezaji wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ya TANU ulikuwa
umefikia kiwango kikubwa nchini. Sekta ya Umma iliyoundwa katika
kipindi hicho ilikuwa kubwa na anuai. Viwanda vya Umma na Mashirika
mbalimbali ya Umma ndiyo yaliyokuwa yakiongoza. Sekta hii ya Umma
ya uchumi ilikuwa inaajiri wafanyakazi wengi na kutarajiwa kuzalisha
mali na kutoa huduma kwa ufanisi.
Mwongozo pamoja na mambo mengine unajadili upungufu uliojitokeza
ndani ya sekta ya umma na kuhoji kama hali hiyo haianzishi mgongano
na makusudio ya kuundwa kwa sekta ya umma ambayo ndiyo ya ujamaa.
Itakumbukwa pia kuwa katika MWONGOZO wa TANU wa 1971 kuna
Ibara ya 15 ambayo inahoji viongozi wa kazi wenye tabia ya unyapara,
wasioheshimu watu, wakaripiaji n.k. katika sehemu za kazi.
Hapa pana suala kubwa kwa watu wanaoamini katika ujamaa na
wale wanaoamini katika uhuru na utu, na kuwa maendeleo yenye
maana ni maendeleo ya watu. Haitoshi katika nchi kuunda vyombo
vya ujamaa kama viwanda, mabenki, mashirika ya umma ya huduma n.k.;
lazima ndani ya vyombo hivyo kujenga uhusiano wa kijamaa yaani ule
unaoheshimu misingi ya usawa, haki, ushirikiano, mshikamano, kuchapa
kazi na uaminifu. Je, demokrasia ina nafasi ipi? Na nidhamu nayo?

MWONGOZO wa CCM wa 1981 katika kufanya uchambuzi kosoa


ulilenga kubainisha mapungufu katika maeneo ya uchumi, siasa
18

MIONGOZO MIWILI

na jamii ili kutoa mapendekezo chanya ya kukijenga Chama


na dola.

Watu wenye fikra za kimaendeleo tayari wakati ule walikuwa wanaona


haja ya kuleta mabadiliko makubwa ndani ya Chama ili kupanua
demokrasia na kuimarisha uongozi na utendaji. Kwa hiyo, MWONGOZO
ulisisitiza umuhimu wa kuwapata viongozi wa Chama kwa njia ya
uchaguzi badala ya uteuzi kwa lengo la kuunganisha uongozi wa chama
(Halmashauri Kuu za kila ngazi) na utendaji katika Chama. MWONGOZO
ulielekeza kuanzishwa kwa Sekretarieti za Halmashauri Kuu za kila ngazi
ambazo zingeongozwa na makatibu wa Halmashauri Kuu hizo.

Sekretarieti za Halmashauri Kuu ya Chama katika kila ngazi zilikusudiwa


ziwe timu za uongozi wa pamoja katika ngazi husika na chemchem za
fikra za chama, wakati kila mmoja ni kiongozi na msimamizi mahiri wa
shughuli za Chama katika idara yake.
MWONGOZO katika kusisitiza umuhimu wa kupanua demokrasia ndani
ya Chama umetilia mkazo uwakilishi wa wanawake na vijana kutokana
na uzito wa makundi haya katika jamii.
Waandazi wa MWONGOZO wa CCM wa 1981 hawakusita kujielekeza
kwenye suala la demokrasia katika dola. Ndiyo maana MWONGOZO
uliona umuhimu wa kuimarisha uwakilishi wa wafanyakazi, wakulima,
vijana na wanawake Bungeni. Aidha, ulisisitiza umuhimu wa uchaguzi
kama kigezo cha msingi cha demokrasia ya kijamaa na hivyo uchaguzi
uwe ndiyo njia kuu ya kuwapata wabunge na wawakilishi wengine
katika dola. MWONGOZO vile vile ulihimiza haja ya kupanua demokrasia
kwa kusisitiza umuhimu wa kuimarisha madaraka ya umma hadi
kwenye ngazi ya vijiji na ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za
maendeleo yao.

Mapokezi na utekelezaji

MWONGOZO wa CCM wa 1981 ulipata mapokezi makubwa ndani ya


Chama na katika jamii nzima nchini. Kitendo cha kuitishwa Mkutano
Mkuu wa Taifa wa CCM wa dharura ili kuupokea na kuupitisha
MIONGOZO MIWILI

19

MWONGOZO huo kilifanya ujumbe wa MWONGOZO ufike kwenye pembe


zote za nchi kwa ufanisi mkubwa. Jinsi masuala muhimu ya Chama na ya
Nchi yalivyochambuliwa kwa ufasaha na umahiri ilifanya MWONGOZO
kuwa gumzo la mabarazani na vijiweni na mada za kujadiliwa kwenye
vyuo vya Chama, madarasa ya itikadi na mijadala miongoni mwa wasomi.
Kwenye NEC ya Septemba 1981 ambapo Kamati ya Programu iliwasilisha
rasimu ya kwanza ya MWONGOZO wajumbe wawili wapya wa kamati
waliteuliwa, Ndg. Pius Msekwa na Ndg. Joseph Sinde Warioba, ili
kuiongezea Kamati uzoefu wa masuala ya kiufundi ya Chama na Dola
kama vile masuala ya Katiba.

Kwa upande wa Chama, utekelezaji wa maelekezo ya MWONGOZO


ulijikita kwenye mambo makubwa matatu. La kwanza, ni kufanya
marekebisho ya Katiba ili kimsingi viongozi wote katika Chama
wapatikane kwa kuchaguliwa na katika ngazi zote. La pili, mpangilio
wa vikao na majukumu yake uliwekwa wazi zaidi. Mikutano mikuu ni
vikao vya kutoa sera na maamuzi elekezi na kuchagua wajumbe walio
wengi wa Halmashauri Kuu; Halmashauri Kuu za kila ngazi kuwa
vyombo vya kusimamia na kuongoza utekelezaji wa katiba, sera na
maamuzi katika ngazi zao na Kamati za Siasa kwa kila ngazi kusimamia
utekelezaji wa Chama wa siku hadi siku. La tatu, ili kuunganisha uongozi
(Halmashauri Kuu) na utendaji katika Chama ziliundwa Sekretarieti
za Halmashauri Kuu kwa kila ngazi. Katika ngazi ya Taifa wajumbe wa
Sekretarieti wanachaguliwa na NEC kutoka miongoni mwa wajumbe wa
NEC yenyewe na inaongozwa na Katibu Mkuu wa Chama. Katika ngazi
zilizobaki makatibu katika kila ngazi ndio wanaoongoza Sekretarieti za
ngazi zao. La nne, marekebisho ya katiba yaliweka nafasi maalum kwa
uwakilishi wa wanawake na vijana katika NEC na vikao vingine kama
MWONGOZO ulivyosisitiza.
Kwa upande wa dola maelekezo mengi ya MWONGOZO yalizingatiwa
katika maeneo mbalimbali. Hapa tutayataja yale ambayo yaliingizwa katika
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 kwa marekebisho
ya mwaka 1984. La kwanza ni lile la kulifanya suala la haki za binadamu,
kuwa ni sehemu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania badala
20

MIONGOZO MIWILI

ya kuwa sehemu ya Dibaji tu ya Katiba hiyo. Pili ni hatua ya kuimarisha


na kupanua demokrasia nchini kupitia uchaguzi ulio huru na wa haki
wa uwakilishi wa wananchi katika ngazi za Ubunge na Serikali za Mitaa.
Jambo la tatu linahusu madaraka ya umma. Mwongozo ulisisitiza juu ya
madaraka ya umma kuanzia vijijini hadi wilayani na mijini. Kutokana na
mwelekeo huo wa MWONGOZO marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano yaliyofanywa mwaka 1984 yalipanua dhana finyu ya Serikali za
Mitaa katika mtazamo nyumbufu wa madaraka ya umma na kusisitiza juu
ya haki ya wananchi kwa serikali zao katika maeneo yao.

Changamoto zinazohitaji tafakuri


Unapoisoma miongozo hii miwili, wa TANU wa 1971 na wa


CCM wa 1981, huwezi kukosa kubaini kuwa fikra, nadharia na
tafakuri kubwa zilitumika katika utunzi wake. Haya ni matokeo
ya viongozi wa chama wanapokaa pamoja na kufikiri pamoja.
Hii ni aina mojawapo ya uhai wa chama iliyo muhimu sana kwa
uhai wa jumla wa chama cha siasa.
Je, mila hii iliyokuwa imejengeka huko nyuma CCM yetu ya
sasa inaiendeleza? Je Vyama vingine vya siasa nchini vinajaribu
kujenga tabia ya viongozi wake kuketi pamoja na kufikiri
pamoja na kuchambua pamoja hali ya nchi yetu na namna
vitakavyozikabili changamoto mbalimbali?

Huu umaskini wetu wa sasa wa falsafa unaotuathiri vibaya


unatokana na nini?

Mwongozo wa TANU wa 1971, katika ibara zake za 21, 22 na


23 ulijenga msingi wa sera ya ulinzi na usalama wa umma, sera
iliyozaa ulinzi wa mgambo. Maandalizi sahihi ya wanamgambo,
yaani kuhamasishwa kwa mbinu ya uzalendo, uandikishaji na
mafunzo makini ya kijeshi chini ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania ndiyo yaliyowezesha wanamgambo kushiriki
bega kwa bega na wapiganaji wengine katika Jeshi la Tanzania
lilolishinda na kulitokomeza Jeshi la Nduli Iddi Amin wa Uganda.
Miaka 33 imekwishapita tangu vita vya Kagera viishe. Vita hivyo
vya kujihami dhidi ya uvamizi uliofanywa na majeshi ya Iddi

MIONGOZO MIWILI

21

22

Amini wa Uganda dhidi ya nchi yetu vilidhihirisha ubora wa sera


mkakati ya ulinzi wa usalama wa umma.

Wakati huu ambapo tumejumuika kumuenzi Mwalimu Nyerere


miaka 91 tangu azaliwe, ni jambo linalopendeza kujipa muda
wa kutathmini sera nzito alizozianzisha na ambazo zimetoa
mchango mkubwa kwa taifa kama ile ya ulinzi na usalama wa
umma iliyozaa ulinzi wa mgambo. Ni vizuri kupitia mazingira ya
wakati huo, misingi ya kuanzishwa kwake, taratibu zilizotumika
na matokeo/tija iliyopatika nchini. Je, hali ya ulinzi wa mgambo
ya sasa inakidhi matarajio ya sera za ulinzi na usalama wa umma
kama ilivyoasisiwa katika mwongozo wa TANU wa 1971?

Mjadala wowote wa maana kuhusu Mwongozo wa TANU


wa 1971 haukamiliki pasi na mjadala kuhusu ibara za 28.
Kwa watu ambao vizazi vyao vilivyotangulia viliishi katika
mifumo kandamizi ya utumwa, ukoloni, ukabaila na ubepari,
dhana kwamba maendeleo ni Ukombozi yenyewe inasaidia
kutukomboa kifikra.
Ibara hii inatoa muhtasari sahihi wa ujumbe wake inaposema
kwetu sisi maendeleo ya maana ni yale yanayotuondolea
kuonewa, kunyonywa, kunyanyaswa na mawazo ya kufungwa,
na kutuongezea uhuru na utu wetu. Na katika hitimisho ibara
hii imesema kwa hiyo katika kufikiria maendeleo ya taifa letu,
na katika kupanga mipango ya maendeleo, wakati wote lazima
mkazo mkubwa utiliwe kwenye maendeleo ya WATU na siyo ya
vitu. Ili maendeleo haya yaweze kuwa ya watu, watu wenyewe
lazima washiriki katika kufikiria, kupanga na kutekeleza
mipango ya maendeleo yao.
Mwongozo wa TANU wa 1971 ulitufikisha hapo katika nadharia.
Je, sisi wasomi na wanasiasa wa leo hatuna la kuchangia?

MIONGOZO MIWILI

SURA YA KWANZA
AZIMIO LA ARUSHA
Ujamaa na Kujitegemea
(Lilipitishwa na Halmashauri Kuu ya TANU, mwezi Januari 1967, na
kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa TANU)
(Lilitolewa rasmi tarehe 5 Februari 1967)

SEHEMU YA KWANZA
IMANI YA TANU
Siasa ya TANU ni kujenga nchi ya Ujamaa. Misingi ya Ujamaa imetajwa
katika Katiba ya TANU, nayo ni hii:
Kwa kuwa TANU inaamini:

(a) Kwamba binadamu wote ni sawa;


(b) Kwamba kila mtu anastahili heshima;
(c) Kwamba kila raia ni sehemu ya Taifa na anayo haki ya kushiriki
sawa na wengine katika Serikali tangu ya Mitaa, ya Mikoa hadi
Serikali Kuu;
(d) Kwamba kila raia anayo haki ya uhuru wa kutoa mawazo yake,
wa kwenda anakotaka, wa kuamini dini anayotaka na wa
kukutana na watu mradi havunji Sheria;
(e) Kwamba kila mtu anayo haki ya kupata kutoka katika jamii
hifadhi ya maisha yake na ya mali yake aliyonayo kwa mujibu
wa Sheria;
(f) Kwamba kila mtu anayo haki ya kupata malipo ya haki kutokana
na kazi yake;
(g) Kwamba raia wote kwa pamoja wanamiliki utajiri wa asili wa
nchi hii ukiwa kama dhamana kwa vizazi vyao;
(h) Kwamba ili kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unakwenda sawa
Serikali lazima iwe na mamlaka kamili juu ya njia muhimu za
kuukuza uchumi; na

MIONGOZO MIWILI

23

(i) Kwamba ni wajibu wa Serikali, ambayo ni watu wenyewe,


kuingilia kati kwa vitendo maisha ya uchumi ya Taifa ili
kuhakikisha usitawi wa raia wote na kuzuia mtu kumnyonya
mtu mwingine au kikundi kimoja kunyonya kikundi kingine na
kuzuia limbikizo la utajiri kufikia kiasi ambacho hakipatani na
siasa ya watu wote kuwa sawa.

MADHUMUNI YA TANU

Kwa hiyo basi, makusudi na madhumuni ya TANU yatakuwa kama hivi


yafuatavyo:
(a) Kuudumisha uhuru wa nchi yetu na raia wake;

(b) Kuweka heshima ya mwanadamu kwa kufuata barabara kanuni


za Tangazo la Ulimwengu la Haki za Binadamu;

(c) Kuhakikisha kwamba nchi yetu inatawaliwa na Serikali ya watu


ya kidemokrasia na ya kisoshalist;

(d) Kushirikiana na vyama vyote vya siasa katika Afrika


vinavyopigania uhuru wa bara lote la Afrika;
(e) Kuona kwamba Serikali inatumia mali yote ya nchi yetu kwa
kuondoshea umaskini; ujinga na maradhi;

(f) Kuona kwamba Serikali inasaidia kwa vitendo kuunda na


kudumisha vyama vya ushirika;

(g) Kuona kwamba kila iwezekanapo Serikali inashiriki hasa katika


maendeleo ya uchumi wa nchi yetu;
(h) Kuona kwamba Serikali inatoa nafasi zilizo sawa kwa wote,
wake kwa waume, bila kujali rangi, kabila, dini au hali;
(i) Kuona kwamba Serikali inaondoa kila namna ya dhuluma,
vitisho, ubaguzi, rushwa na upotofu;

(j) Kuona kwamba Serikali ya nchi yetu inasimamia barabara njia


kuu za kuzalisha mali na inafuata siasa ambayo itarahisisha njia
ya kumiliki kwa jumla mali za nchi yetu;

(k) Kuona kwamba Serikali inashirikiana na dola nyingine katika


Afrika katika kuleta Umoja wa Afrika.
(l) Kuona kwamba Serikali inajitahidi kuleta amani na salama
ulimwenguni kwa njia ya Chama cha Umoja wa Mataifa.
24

MIONGOZO MIWILI

SEHEMU YA PILI
SIASA YA UJAMAA
(a) Hakuna Unyonyaji
Nchi yenye Ujamaa kamili ni nchi ya wafanyakazi: haina ubepari wala
ukabaila. Haina tabaka mbili za watu: tabaka ya chini ya watu wanaoishi
kwa kufanya kazi, na tabaka ya juu ya watu wanaoishi kwa kufanyiwa
kazi. Katika nchi ya Ujamaa kamili mtu hamnyonyi mtu, bali kila awezaye
kufanya kazi hufanya kazi, na kila mfanyakazi hupata pato la haki kwa
kazi aifanyayo na wala mapato ya wafanyakazi mbalimbali hayapitani
mno.

Katika nchi ya Ujamaa kamili watu peke yao ambao huishi kwa jasho
la wenzao, na ni haki yao kuishi kwa jasho la wenzao, ni watoto
wadogo, wazee wasiojiweza, vilema na wale ambao, kwa muda, Jumuia
imeshindwa kuwapatia kazi yoyote ya kujipatia riziki kwa nguvu zao
wenyewe.

Nchi yetu ni nchi ya Wakulima na Wafanyakazi, lakini si nchi ya Ujamaa


kamili. Ina misingi ya ubepari na ukabaila na vishawishi vyake. Misingi
hii ya ubepari na ukabaila yaweza ikapanuka na kuenea.

(b) Njia Kuu za Uchumi ni Chini ya Wakulima na


Wafanyakazi

Namna ya pekee ya kujenga na kudumisha ujamaa ni kuthibitisha kuwa


njia kuu zote za uchumi wa nchi yetu zinatawaliwa na kumilikiwa na
Wakulima na Wafanyakazi wenyewe kwa kutumia vyombo vya Serikali
yao na Vyama vyao vya Ushirika. Pia ni lazima kuthibitisha kuwa Chama
kinachotawala ni Chama cha wakulima na wafanyakazi.

Njia kuu za Uchumi ni: kama vile ardhi, misitu, madini, maji, mafuta na
nguvu za umeme; njia za habari, njia za usafirishaji; mabenki, na bima;
biashara na nchi za kigeni na biashara za jumla; viwanda vya chuma,
mashini, silaha, magari, simenti, mbolea; nguo, na kiwanda chochote
kikubwa ambacho kinategemewa na sehemu kubwa ya watu katika
kupata riziki zao au kinachotegemewa na viwanda vingine; mashamba
MIONGOZO MIWILI

25

makubwa na hasa yale yanayotoa mazao ya lazima katika viwanda


vikubwa.

Baadhi ya njia hizi na nyingine zisizotajwa hapa hivi sasa zinamilikiwa au


kutawaliwa na Serikali ya Wananchi.

(c) Kuna Demokrasi

Nchi haiwi ya Ujamaa kwa sababu tu njia zake kuu au zote za uchumi
hutawaliwa na humilikiwa na Serikali. Sharti Serikali iwe inachaguliwa na
kuongozwa na Wakulima na Wafanyakazi wenyewe. Serikali ya Makaburu
wa Rhodesia au Afrika ya Kusini ikitawala au kumiliki njia zote za uchumi,
hiyo itakuwa ni njia ya kukomaza Udhalimu siyo njia ya kuleta Ujamaa.
Hakuna Ujamaa wa kweli pasipo na Demokrasi ya kweli.

(d) Ujamaa ni Imani

Lakini Ujamaa hauwezi kujijenga wenyewe. Kwani Ujamaa ni imani.


Hauna budi kujengwa na watu wanaoamini na kufuata kanuni zake.
Mwana-TANU wa kweli ni Mjamaa, na Wajamaa wenzie, yaani waamini
wenzie katika imani hii ya kisiasa na uchumi ni wote wale wanaopigania
haki za wakulima na wafanyakazi katika Afrika na popote duniani. Wajibu
wa kwanza wa mwana-TANU na hasa kiongozi wa TANU, ni kutii kanuni
hizi za ujamaa hasa katika maisha yake mwenyewe. Na hasa mwanaTANU kiongozi hataishi kwa jasho la mtu mwingine au kufanya jambo
lolote ambalo ni la kibepari au kikabaila.
Utimizaji wa shabaha hizo na nyinginezo zinazofuatana na siasa ya ujamaa
unategemea sana viongozi kwa sababu ujamaa ni imani na ni vigumu kwa
viongozi kujenga siasa ya ujamaa ikiwa hawaikubali imani hiyo.

SEHEMU YA TATU

SIASA YA KUJITEGEMEA
Tunapigana Vita
TANU ina vita vya kulitoa Taifa letu katika hali ya unyonge na kulitia
katika hali ya nguvu; vita vya kuwafanya wananchi wa Tanzania (na
26

MIONGOZO MIWILI

wananchi wa Afrika) watoke katika hali ya dhiki na kuwa katika hali ya


neema.

Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, na


tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe,
tunyonywe, na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi; mapinduzi ya kuondoa
unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na wala tusipuuzwe tena.

Mnyonge Hapigani kwa Fedha

Lakini ni dhahiri kwamba tumefanya makosa katika kuchagua silaha;


kwani silaha tuliyochagua ni fedha. Tunataka kuondoa unyonge wetu
kwa kutumia silaha ya wenye nguvu, silaha ambayo sisi wenyewe hatuna.
Katika mazungumzo yetu, mawazo yetu, na vitendo vyetu ni kama
tumekata shauri kwamba bila fedha mapinduzi yetu hayawezekani. Ni
kama tumesema, Fedha ndiyo msingi wa maendeleo. Bila fedha hakuna
maendeleo!
Hii ndiyo imani yetu ya sasa. Viongozi wa TANU mawazo yao ni kwenye
fedha. Viongozi wa Serikali, wanasiasa na watumishi, mawazo yao na
matumaini yao ni kwenye fedha. Viongozi wa wananchi na wananchi
wenyewe katika TANU, NUTA, Bunge, UWT, Vyama vya Ushirika, TAPA
na makundi mengine ya wananchi, mawazo yao na maombi yao na
matumaini yao ni FEDHA. Ni kama wote tumekubaliana na tunasema
kwa sauti moja, Tukipata fedha tutaendelea, bila fedha hatutaendelea!

Mpango wetu wa maendeleo ya miaka mitano shabaha zake kwa kifupi ni


shibe zaidi, elimu zaidi na afya zaidi. Na silaha yetu tuliyotilia mkazo sana
ni fedha. Ni kama tumesema, Katika miaka mitano ifuatayo tunakusudia
kujiongezea shibe, elimu na afya, na ili kutimiza shabaha hizo tunatumia
250,000,000. Kama tumetaja na tunapotaja vyombo vingine vya
kututimizia shabaha hizo tunavitaja kama nyongeza tu; lakini chombo
kikubwa katika akili zetu, silaha kubwa katika mawazo yetu, ni FEDHA.

Mheshimiwa Mbunge anaposema kuwa wananchi wa sehemu yake wana


shida ya maji, je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa shida hiyo? Jibu
analotaka ni kwamba: Serikali inao mpango wa kuwapa maji wananchi
wa sehemu hiyo KWA FEDHA.
MIONGOZO MIWILI

27

Mbunge mwingine anaposema kuwa sehemu yake haina barabara au


shule au hospitali au vyote, je, Serikali ina mpango gani? Naye pia jibu
ambalo angependa kupewa ni kuwa Serikali inao mpango safi kabisa
wa kutengeneza barabara au kujenga shule au hospitali au vyote kwa
wananchi wa sehemu ya Mbunge Mheshimiwa huyo kwa FEDHA.

Kiongozi wa NUTA anapoikumbusha Serikali kuwa mishahara ya chini


kwa wafanyakazi wengi bado ni midogo mno na nyumba wanazolala
si nzuri, je, Serikali inao mpango gani? Jibu apendalo kusikia ni kuwa
Serikali inao mpango maalum wa kuongeza mishahara na kujenga
majumba bora KWA FEDHA.
Kiongozi wa TAPA anaposema kuwa wanazo shule nyingi sana ambazo
hazipati msaada wa Serikali, je, Serikali ina mpango gani wa kuzisaidia
shule hizo, jibu analopenda kusikia ni kuwa Serikali iko tayari kabisa
kesho asubuhi kuzipa shule hizo msaada unaotakiwa wa FEDHA!

Kiongozi wa Chama cha Ushirika akitaja shida yoyote ya mkulima jibu


apendalo kusikia ni kuwa Serikali itaondoa shida hizo za mkulima kwa
FEDHA. Mradi kila shida inayolikabili Taifa letu wananchi tunawaza
Fedha, Fedha, Fedha!

Mwaka hata mwaka kila Wizara na kila Waziri hufanya makadirio yake ya
matumizi yaani fedha wanazohitaji mwaka huo kwa kazi za kawaida na
mipango ya maendeleo. Waziri mmoja tu na Wizara moja tu hushughulika
pia kufanya makadirio ya mapato. Ni Waziri wa Fedha. Kila Wizara ina
mipango mizuri sana ya maendeleo. Wizara zinapoleta makadirio yao ya
matumizi huwa zinaamini kwamba fedha zipo ila mkorofi ni Waziri wa
Fedha na Wizara yake. Na kila mwaka lazima Waziri wa Fedha na Wizara
yake awaambie Mawaziri wenzake na Wizara zao kwamba hakuna
fedha. Na kila mwaka Wizara zote huinungunikia Wizara ya Fedha kwa
kupunguza Makadirio yao ya matumizi.

Kadhalika Wabunge na Viongozi wengine wanapodai Serikali itimize


mipango mbalimbali huwa nao wakiamini kwamba fedha zipo ila mkorofi
ni Serikali. Lakini kukataa huku kwa Wizara, na Wabunge na Viongozi
wengine hakuwezi kuondoa ukweli; nao ni kwamba Serikali haina fedha.
28

MIONGOZO MIWILI

Na kusema kuwa Serikali haina fedha maana yake ni nini? Maana yake ni
kuwa Wananchi wa Tanzania hawana fedha. Kiasi walichonacho hutozwa
kodi, na kodi hiyo ndiyo inayoendesha shughuli za Serikali hivi sasa na
maendeleo mengine ya nchi. Tunapotaka Serikali ifanye shughuli zaidi
za maendeleo kwa fedha tunataka Serikali itumie fedha zaidi. Na kama
Serikali haina fedha zaidi tunataka izipate, yaani iongeze kodi.
Ukidai Serikali itumie fedha zaidi unataka izipate; na njia ya kuzipata
ni kodi. Kudai Serikali itumie fedha nyingi zaidi bila kukubali kodi zaidi
ni kudai Serikali ifanye miujiza; ni sawa na kudai maziwa zaidi bila
kutaka ngombe akamuliwe tena. Lakini kukataa huku kukiri kwamba
tunapodai Serikali itumie fedha zaidi nia yetu ni kutaka Serikali
iongeze kodi kunaonyesha kuwa tunatambua ugumu wa kuongeza kodi.
Tunatambua kuwa ngombe hana maziwa zaidi; kwamba hata kama
ngombe mwenyewe angependa ayanywe maziwa hayo au yanywewe na
ndama wake au yauzwe yamfae yeye na jamaa yake; utashi huo hauwezi
kuondoa ukweli kwamba hana maziwa zaidi.

Fedha kutoka Nje ya Tanzania, je?

Njia moja tunayotumia kujaribu kuepukana na lazima hii ya kukiri kodi


zaidi ikiwa twataka fedha zaidi ni kutilia sana mkazo fedha za kutoka nje
ya Tanzania. Fedha hizi za kutoka nje ni za aina tatu:(a) Zawadi: Yaani Serikali ya nje iipe Serikali yetu fedha za bure tu
kama sadaka kwa ajili ya mpango fulani wa maendeleo. Wakati
mwingine shirika lolote la nje liipe Serikali yetu au Shirika
jingine katika nchi yetu msaada fulani kwa ajili ya maendeleo.
(b) Mkopo: Sehemu kubwa ya fedha tunazotazamia kupata kutoka
nchi za kigeni si zawadi au sadaka, bali ni mkopo. Serikali ya nje au
Shirika la nje, kama vile Benki, hukopesha Serikali yetu fedha fulani
kwa ajili ya kazi zetu za maendeleo. Mkopo huu huwa una masharti
yake ya kulipa, kama vile muda wa kulipa, na kima cha faida.
(c) Raslimali ya Kibiashara: Aina ya tatu ambayo pia ni kubwa kuliko
ya kwanza, ni ile ya fedha za watu au makampuni yanayotaka
kuja katika nchi yetu kuanzisha shughuli mbalimbali za uchumi
kwa manufaa yao wenyewe. Na sharti kubwa walitakalo jamaa
MIONGOZO MIWILI

29

hawa wenye fedha zao ni kwamba shughuli yenyewe iwe ni ya


faida kwao na pia kwamba Serikali iwaruhusu kuondoa faida
hiyo Tanzania na kuipeleka kwao. Hupenda pia kwa jumla Serikali
iwe na siasa wanayokubaliana nayo au ambayo haihatarishi
uchumi wao.

Hizo ndizo njia tatu kubwa za kupata fedha kutoka nje ya nchi yetu. Kuna
mazungumzo mengi ajabu juu ya jambo hili la kupata fedha kutoka nchi za
kigeni. Serikali yetu na viongozi wetu wa makundi mbalimbali hawaachi
kufikiria njia za kupata fedha kutoka nje. Na tukizipata au japo tukipata
ahadi tu ya kuzipata mara magazeti yetu, au radio zetu na viongozi
wetu hutangaza jambo hilo ili kila mtu ajue kuwa neema imekuja au iko
njiani inakuja! Tukipata msaada hutangaza; tukipata mkopo hutangaza;
tukipata kiwanda kipya hutangaza; tukiahidiwa msaada, mkopo au
kiwanda kipya hutangaza. Japo tukianza mazungumzo tu na nchi au
shirika la kigeni juu ya msaada, mkopo au kiwanda, mara hutangaza japo
hatuna hakika ya matokeo ya mazungumzo hayo. Na kisa? Ni kuwajulisha
wananchi kwamba, tunaanza mazungumzo ya neema!

TUSITEGEMEE FEDHA KULETA MAENDELEO

Ni jambo la kijinga kuchagua fedha kuwa ndiyo chombo chetu kikubwa cha
maendeleo na hali tunajua kuwa nchi yetu ni maskini. Ni ujinga vilevile,

kwa kweli ni ujinga zaidi, tukidhani kuwa tunaweza kuondoa hali hii ya

unyonge wetu kwa kutegemea fedha za kutoka nje badala ya fedha zetu
wenyewe. Ni ujinga kwa sababu mbili.

Kwanza, hatuwezi kuzipata. Ni kweli kwamba zipo nchi ambazo zaweza


na zapenda kutusaidia. Lakini hakuna nchi moja duniani ambayo iko
tayari kutupa misaada au mikopo au kuja kujenga viwanda katika nchi

yetu kwa kiasi cha kuiwezesha nchi yetu kutimiza shabaha zake zote za

maendeleo. Nchi zenye dhiki ni nyingi sana duniani. Na hata kama nchi
zote zenye neema zingekubali kuzisaidia nchi zenye dhiki, bado ingekuwa

msaada huo hautoshi. Lakini nchi zenye neema hazitakubali. Hata katika
30

MIONGOZO MIWILI

nchi ileile, matajiri huwa hawatoi fedha zao kwa hiari ili zisaidie Serikali
kuondoa dhiki.

Njia ya kuzipata fedha za matajiri ili zisaidie umma ni kuwatoza kodi


wakipenda wasipende. Hata hivyo huwa hazitoshi. Ndiyo maana japo
tungewakamua vipi wanananchi na wakazi wa Tanzania, matajiri na
maskini, hatuwezi kupata fedha za kutosha kutimiza mipango yetu ya
maendeleo. Wala duniani hakuna Serikali ambayo yaweza kuyatoza kodi
mataifa yenye neema, yakipenda yasipende, ili kusaidia mataifa yenye

dhiki. Hata hizo zisingelitosha. Hakuna Serikali ya Dunia nzima. Fedha


ambazo nchi zenye neema hutoa huwa kwa wema wao, au hiari yao au
kwa manufaa yao wenyewe. Haiwezekani basi, tupate fedha za kutosha
kwa njia hiyo.

MISAADA NA MIKOPO VITAHATARISHA


UHURU WETU

Pili, japo kama tungeweza kuzipata; hivyo ndivyo tunavyotaka kweli?


Kujitawala ni kujitegemea. Kujitawala kwa kweli hakuwezekani ikiwa Taifa
moja linategemea misaada na mikopo ya Taifa jingine kwa maendeleo
yake. Hata kama pangetokea Taifa au mataifa ambayo yako tayari kutupa
fedha zote tunazohitaji kuendesha mipango yetu ya maendeleo isingekuwa
sawa kwa nchi yetu kuipokea misaada hiyo bila kujiuliza matokeo yake
yatakuwa nini kwa Uhuru wetu na uzima wetu.
Msaada ambao ni kama chombo cha kuongeza juhudi, au nyenzo ya juhudi,
ni msaada ambao una manufaa. Lakini msaada unaoweza ukawa sumu ya
juhudi si msaada wa kupokea bila kujiuliza maswali.

Kadhalika mikopo. Kweli mkopo ni bora kuliko misaada ya bure. Mkopo


nia yake ni kuongeza jitihada au kuifanya jitihada itoe matunda mengi
zaidi. Sharti moja la mkopo huwa ni kuonyesha jinsi utavyoweza kuulipa.
Maana yake ni kwamba sharti uonyeshe kuwa unakusudia kuufanyia kazi
itakayoleta manufaa ya kukuwezesha kuulipa.
Lakini hata mikopo ina kikomo. Sharti upime uwezo wa kulipa. Tunapokopa
MIONGOZO MIWILI

31

fedha kutoka nje mlipaji ni Mtanzania. Na kama tulivyokwishasema


Watanzania ni watu maskini. Kuwabebesha watu maskini mikopo ambayo
inawazidi kimo si kuwasaidia bali ni kuwaumiza. Na hasa inapokuwa,
mikopo hiyo ambayo wanatakiwa walipe, haikuwafaidia wao, bali ilifaidia
watu wachache tu.

Na Viwanda vya wenye raslimali zao je? Ni kweli tunavitaka. Hata tumepitisha
katika Bunge sheria ya kulinda raslimali ya wageni wanaoanzisha mipango
mbalimbali ya uchumi katika nchi yetu. Nia yetu na matumaini yetu ni
kuwafanya waone kuwa Tanzania ni nchi inayofaa kuingiza raslimali zao.
Kwani raslimali yao itakuwa salama italeta faida. Na faida hiyo wenyewe
wataweza kuiondoa bila vipingamizi. Tunayo matumaini ya kupata
fedha za maendeleo mbalimbali kwa njia hii. Lakini hatuwezi kupata za
kutosha. Lakini hata kama tungeweza kuwaridhisha kabisa Wageni hao
na Makampuni hayo mpaka yakubali kuanzisha mipango yote ya uchumi
tunayohitaji katika nchi yetu, hivyo ndivyo tunavyotaka kweli?
Kama tungeweza kushawishi wenye raslimali wa kutosha kutoka Amerika,
na Ulaya kuja kwetu na kuanzisha Viwanda vyote, na mipango mingine
yote ya uchumi tunayohitaji katika nchi hii, hivi kweli tungekubali bila
kujiuliza maswali? Tungekubali kweli kuacha uchumi wetu wote uwe
mikononi mwa wageni kwa ajili ya kupata faida na kuipeleka katika nchi
zao? Hata kama wasingedai kuhamisha faida na kupeleka makwao, bali
faida yote watakayopata wataitumia hapa hapa Tanzania kwa maendeleo
zaidi. Hivi kweli tungekubali jambo hili bila kujiuliza hasara zake kwa Taifa
letu? Huu Ujamaa tunaosema kuwa ndiyo shabaha yetu tungeujengaje?

Twawezaje kutegemea nchi za nje na Kampuni za nje kwa misaada na


mikopo na raslimali kwa maendeleo yetu bila kuhatarisha uhuru wetu?
Waingereza wana methali isemayo Amlipaye mwimbaji ndiye huchagua
wimbo. Tutawezaje kutegemea nchi za kigeni na Makampuni ya kigeni kwa
sehemu kubwa ya maendeleo yetu bila kuzipa nchi hizo na makampuni
hayo sehemu kubwa ya uhuru wetu wa kutenda tupendavyo? Ukweli
wenyewe ni kwamba hatuwezi.
Tukariri basi. Tumefanya makosa kuchagua fedha, kitu ambacho hatuna,
kiwe ndicho chombo kikubwa cha mipango yetu ya maendeleo. Tunafanya
32

MIONGOZO MIWILI

makosa kudhani kuwa tutapata fedha kutoka nchi za kigeni. Kwanza, kwa
sababu kwa kweli hatuwezi kupata fedha za kutosha kwa maendeleo yetu.
Na pili, hata kama tungeweza, huko kutegemea wengine kungehatarisha
uhuru wetu na siasa nyingine za nchi yetu.

TUMEKAZANIA MNO VIWANDA

Kwa sababu ya kutilia mkazo fedha tumefanya kosa kubwa la pili.


Tumekazania mno viwanda. Kama vile tulivyosema Bila Fedha hakuna
maendeleo, ni kama twasema pia Viwanda ndiyo maendeleo. Bila
viwanda hakuna maendeleo. Hii ni kweli siku tutakapokuwa na fedha
nyingi, tutaweza kusema kwamba tumeendelea. Tutaweza kusema,
Tulipoanza mipango yetu tulikuwa hatuna fedha za kutosha na upungufu
huu wa fedha ulitupunguzia nguvu za kuendesha maendeleo yetu haraka
zaidi. Lakini leo tumeendelea na tunazo fedha za kutosha. Na hivyo
ndivyo itakavyotupasa kusema, Tumeendelea, kwa hiyo, tunazo fedha za
kutosha. Yaani fedha zetu zitakuwa zimeletwa na maendeleo.

Kadhalika siku tutakapokuwa na viwanda tuna haki ya kusema kuwa


tumeendelea. Maendeleo yatakuwa yametuwezesha kupata viwanda.
Kosa tunalofanya ni kudhani kwamba maendeleo yetu yataanza kwa
viwanda. Ni kosa maana hatuna uwezo wa kuanzisha viwanda vingi
vya kisasa katika nchi yetu. Hatuna fedha zinazohitajiwa na hatuna
ufundi unaohitajiwa. Haitoshi kusema kuwa tutakopa fedha na kuazima
mafundi kutoka nje kuja kuanzisha viwanda hivyo. Kosa hili jibu lake ni
lilelile kwamba hatuwezi kupata fedha za kutosha na kuazima mafundi
wa kutosha kutuanzishia viwanda hivyo tunavyotaka. Na pia kwamba
hata kama tungeweza kupata msaada huo kuutegemea huko kunaweza
kukapotosha siasa yetu ya Ujamaa. Siasa ya kualika msululu wa mabepari
kuja kuhodhi viwanda katika nchi yetu ingefanikiwa kutupatia viwanda
vyote tunavyotaka, basi ingefanikiwa pia kuzuia maendeleo ya Ujamaa.
Ila labda tuwe tunaamini kwamba bila kujenga ubepari kwanza hatuwezi
kujenga Ujamaa.

MIONGOZO MIWILI

33

TUMJALI ZAIDI MKULIMA VIJIJINI


Vilevile mkazo wa fedha na wa viwanda unatufanya tukazanie zaidi
maendeleo ya mijini. Tunatambua kuwa hatuwezi kupata fedha za
kutosha kuleta maendeleo katika kila kijiji na ambayo yatamfaa kila
mwananchi. Tunajua pia kuwa hatuwezi kujenga kiwanda katika kila
kijiji ili kisaidie kuleta maendeleo ya fedha na viwanda katika kila kijiji;
jambo ambalo tunajua kuwa haliwezekani. Kwa ajili hiyo, basi, fedha zetu
huzitumia zaidi katika miji na viwanda vyetu pia hujengwa katika miji.
Na zaidi ya fedha hizi huwa ni mikopo. Japo zijenge shule, hospitali,
majumba au viwanda ni fedha za mikopo. Hatimaye lazima zilipwe.
Lakini ni dhahiri kwamba haziwezi kulipwa kwa fedha zinazotokana
na maendeleo ya mijini au maendeleo ya viwanda. Hazina budi zilipwe
kwa fedha tunazopata kutokana na vitu tunavyouza katika nchi za nje.
Kutokana na viwanda vyetu hatuuzi na kwa muda mrefu sana hatutauza
vitu vingi katika nchi za nje. Viwanda vyetu zaidi ni vya kutusaidia
kupata vitu hapa hapa ambavyo mpaka sasa tunaviagiza kutoka nchi za
nje. Itapita miaka mingi kabla ya kuweza kuuza katika nchi za nje vitu
vinavyotokana na viwanda vyetu.

Kwa hiyo ni dhahiri kwamba fedha tutakazotumia kulipa madeni haya


ya mikopo ya fedha kwa maendeleo na viwanda mijini hazitatoka mijini
na wala hazitatokana na viwanda. Zitatoka wapi, basi? Zitatoka vijijini
na zitatokana na KILIMO. Maana ya ukweli huu ni nini? Ni kwamba
wale wanaofaidi maendeleo yanayotokana na fedha tunazokopa sio kwa
kweli watakaozilipa. Fedha zitatumika zaidi katika miji lakini walipaji
watakuwa zaidi ni wakulima.
Jambo hili linafaa kukumbukwa sana, maana kuna njia nyingi za
kunyonyana. Tusisahau hata kidogo kwamba wakaaji wa mijini
wanaweza wakawa wanyonyaji wa jasho la wakulima wa vijijini.
Hospitali zetu kubwa zote ziko katika miji. Zinafaidia sehemu ndogo
sana ya wananchi wa Tanzania. Lakini kama tumezijenga kwa fedha za
mkopo walipaji wa mkopo ni wakulima, yaani wale ambao hawafaidiwi
sana na hospitali hizo. Mabarabara ya lami yako katika miji, kwa faida
ya wakaaji wa mijini na hasa wenye magari. Kama mabarabaraba hayo
34

MIONGOZO MIWILI

tumeyajenga kwa fedha za mikopo walipaji ni wakulima; na fedha


zilizonunua magari yenyewe zilitokana na mazao ya wakulima. Taa
za umeme, maji ya mabomba, mahoteli na maendeleo mengine yote
ya kisasa yako zaidi katika miji. Karibu yote yametokana na fedha
za mikopo na karibu yote hayana faida kubwa kwa mkulima, lakini
yatalipwa kwa fedha zitakazotokana na jasho la mkulima. Tusisahau
jambo hili.

Japo tunapotaja unyonyaji hufikiria mabepari, tusisahau kuwa bahari


ina samaki wengi. Nao hutafunana. Mkubwa hutafuna mdogo na
mdogo naye humtafuna mdogo zaidi. Katika nchi yetu twaweza kugawa
wananchi kwa njia mbili. Mabepari na Makabaila upande mmoja; na
wafanyakazi na wakulima upande mwingine. Pia twaweza tukawagawa
wakaaji wa mijini upande mmoja, na wakulima wa vijijini upande
mwingine. Tusipoangalia tutakuja kugundua kuwa wakaaji wa mijini nao
ni wanyonyaji wa wakulima.

WANANCHI NA KILIMO
Maendeleo ya nchi huletwa na watu, hayaletwi na fedha. Fedha ni
matokeo siyo msingi wa maendeleo. Ili tuendelee twahitaji vitu vinne: (i)
Watu; (ii) Ardhi; (iii) Siasa safi na (iv) Uongozi bora. Nchi yetu ina zaidi
ya watu milioni kumi1* na eneo la eka 362,000.

MAENDELEO YATALETWA NA KILIMO


Sehemu kubwa ya eneo hili ni yenye rutuba na mvua ya kutosha. Nchi
yetu inaweza kutoa mazao ya aina mbalimbali ambayo tunayahitaji kwa
chakula na kwa fedha. Mazao ya chakula (na fedha kama tukiyatoa kwa
wingi) ni kama vile mahindi, mchele, ngano, maharage, karanga n.k.
Mazao ya fedha ni kama vile mkonge, pamba, kahawa, tumbaku, pareto,
chai n.k.

1 *Hesabu ya watu ya mwaka 1967 ilionesha kuwa watanzania ni zaidi ya milioni


kumi na mbili.

MIONGOZO MIWILI

35

Pia nchi yetu ni nzuri sana kwa ufugaji wa ngombe, mbuzi, kondoo,
kuku n.k. Pia twaweza kuvua samaki katika maziwa, bahari
na mito.

Wakulima wetu wako katika sehemu ambazo zaweza kutoa mazao haya,
kama si yote walau mawili matatu au hata zaidi. Kila mkulima wetu
aweza akaongeza mazao haya ili ajipatie chakula kingi zaidi au fedha
nyingi zaidi. Na kwa sababu nia kubwa ya maendeleo ni kupata chakula
zaidi na fedha zaidi kwa ajili ya kujipatia mahitaji yetu mengine, ndiyo
kusema kuwa jitihada ya kuongeza mazao ni jitihada, na kwa kweli ndiyo
jitihada peke yake, ambayo italeta maendeleo, yaani chakula zaidi na
fedha zaidi kwa kila mwananchi.

MASHARTI YA MAENDELEO
(a) Juhudi
Kila mwananchi anataka maendeleo, lakini si kila mwananchi anaelewa
na kukubali masharti ya maendeleo. Sharti moja kubwa ni JUHUDI.
Twendeni vijijini tuzungumze na wananchi kuona kama inawezekana au
haiwezekani wananchi kuongeza juhudi.
Kwa mfano, katika miji, mfanyakazi wa mshahara hufanya kazi kwa saa
saba na nusu au nane kutwa kwa muda wa siku sita au sita na nusu kwa
juma. Tuseme saa 45 kwa juma, kuondoa majuma mawili au matatu ya
livu, katika mwaka mzima. Ndiyo kusema mfanyakazi wa mjini hufanya
kazi ya saa 45 kwa juma kwa majuma 48 au 50 kwa mwaka.

Katika nchi kama yetu muda huu ni mdogo kwa kweli. Nchi nyingi hata
zilizoendelea kutuzidi hufanya kazi kwa muda mrefu zaidi kuliko saa 45
kwa juma. Si jambo la kawaida nchi changa kuanza na muda mfupi kama
huo. Jambo la kawaida ni kuanza na muda mrefu zaidi na kuupunguza
kila nchi inavyozidi kuendelea. Sisi kwa kuanza na muda mfupi huu na
tunapodai muda mfupi zaidi kwa kweli tunaiga nchi zilizoendelea. Na
kuiga huku kunaweza kukaleta majuto. Lakini hata hivyo wafanyakazi wa
mishahara hufanya kazi ya saa 45 kwa juma; livu yao kwa mwaka haizidi
majuma manne.
36

MIONGOZO MIWILI

Yafaa kujiuliza wananchi wakulima hasa wanaume, hufanya kazi kwa


saa ngapi kwa juma na miezi mingapi kwa mwaka. Ni wengi mno ambao
hawatimizi hata nusu ya wastani wa mfanyakazi wa mshahara.

Ukweli wenyewe ni kwamba vijijini kina mama hufanya sana kazi.


Pengine hutimiza saa 12 au 14 kutwa. Hawana Jumapili, na hawana livu.
Kina mama wa vijijini hufanya kazi zaidi kuliko mtu mwingine yeyote
katika Tanzania. Lakini kina baba wa vijijini (na baadhi ya kina mama wa
mijini) nusu ya maisha yao ni livu. Nguvu hizi za mamilioni ya kina baba
vijijini na maelfu ya kina mama wa mijini ambazo hivi sasa hazifanyi
kazi yoyote ila kupiga soga, kucheza ngoma na kunywa pombe, ni hazina
kubwa yenye manufaa zaidi kwa maendeeo ya nchi yetu kuliko hazina za
mataifa matajiri.
Tutafanya jambo la faida kubwa kwa nchi yetu kama tukienda vijijini na
kuwaambia wananchi kwamba wanayo hazina hii na kwamba ni wajibu
wao kuitumia kwa faida yao wenyewe na faida ya Taifa letu.
(b) Maarifa

Sharti la pili la maendeleo ni MAARIFA. Juhudi bila maarifa haiwezi kutoa


matunda bora kama juhudi na maarifa. Kutumia jembe kubwa badala ya
jembe dogo, kutumia jembe la kuvutwa na ngombe badala ya jembe la
mkono, kutumia mbolea badala ya ardhi tupu, kunyunyizia dawa ili kuua
wadudu, kujua ni zao gani lifaalo kupandwa na zao gani lisilofaa, kuchagua
mbegu vizuri kabla ya kuzipanda, kujua wakati mzuri wa kupanda, wakati
wa kupalilia n.k., ni maarifa yanayowezesha juhudi kutoa mazao mengi zaidi.
Fedha na wakati tunaotumia kuwapa wakulima maarifa haya ni fedha na
wakati uletao faida kubwa zaidi kwa nchi yetu kuliko fedha na wakati
mwingi tunaotumia katika mambo mengi tunayoyaita maendeleo.

Jambo hili kwa kweli tunalifahamu. Katika mpango wetu wa miaka


mitano, mipango inayoendelea vizuri na hata kuzidi makisio ni ile
inayotegemea juhudi ya wananchi wenyewe. Pamba, kahawa, korosho,
tumbaku, pareto ni mazao yaliyoongezeka kwa haraka sana katika muda
wa miaka mitatu iliyopita. Lakini ni mazao ambayo yameongezeka kwa
sababu ya juhudi na uongozi wa wananchi, siyo kwa sababu ya fedha.
MIONGOZO MIWILI

37

Kadhalika wananchi kwa juhudi zao wenyewe na maelekezo au msaada


kidogo wametimiza mipango mingi sana ya maendeleo huko vijijini.
Wamejenga shule, dispensari, majumba ya maendeleo, wamechimba
visima, mifereji ya maji, mabwawa, mabarabara, wamejenga mabirika ya
kukoshea mifugo na kujiletea wenyewe maendeleo ya aina mbalimbali.
Kama wangengoja fedha wasingeyapata maendeleo hayo.

JUHUDI NI SHINA LA MAENDELEO


Mipango inayotegemea fedha inakwenda vizuri lakini kuna mingi ambayo
imesimama na yumkini mingine haitatimizwa kwa sababu ya upungufu
wa fedha. Lakini kelele zetu bado ni kelele za fedha. Juhudi yetu ya
kutafuta fedha inazidi kuongezeka! Sio kwamba tuipunguze, bali, badala
ya safari nyingi, ndefu na zenye gharama kubwa za kwenda katika miji
mikuu ya mataifa ya kigeni kwenda kutafuta fedha za maendeleo yetu,
itafaa kufunga safari kwenda vijijini kuwafahamisha na kuwaongoza
wananchi katika kujiletea maendeleo kwa juhudi yao wenyewe. Ndiyo
njia ya kweli ya kuleta maendeleo kwa kila mtu.
Hii maana yake si kwamba tangu sasa hatutajali fedha, wala hatutajenga
viwanda au kufanya mipango yoyote ya maendeleo inayohitaji fedha.
Wala siyo kusema kuwa tangu sasa hatutapokea wala kutafuta fedha
kutoka nchi za nje kwa ajili ya maendeleo yetu. LA, SIVYO. Tutaendelea
kutumia fedha; na mwaka hata mwaka tutatumia fedha nyingi zaidi kwa
maendeleo yetu ya aina mbalimbali kuzidi mwaka uliopita. Kwani hiyo
itakuwa ni dalili moja ya maendeleo yetu.
Lakini hii ni kusema kwamba tangu sasa tutajua nini ni shina na nini ni
tunda la maendeleo yetu. Katika vitu viwili hivyo FEDHA na WATU, ni
dhahiri kwamba watu na JUHUDI yao ndiyo shina la maendeleo, fedha ni
moja ya matunda ya juhudi hiyo.

Tangu sasa tutasimama wima na kutembea kwa miguu yetu badala ya


kupinduka na kuwa miguu juu vichwa chini. Viwanda vitakuja, na fedha
zitakuja, lakini msingi wake ni WANANCHI na JUHUDI yao na hasa katika
KILIMO. Hii ndiyo maana ya kujitegemea. Kwa hiyo basi, mkazo wetu
na uwe:
38

MIONGOZO MIWILI

(a) Ardhi na Kilimo.


(b) Wananchi.
(c) Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, na
(d) Uongozi bora.

(a) Ardhi
Kwa kuwa uchumi wa Tanzania unategemea na utaendelea kutegemea
kilimo na mifugo, Watanzania wanaweza kuyaendesha maisha yao
barabara bila ya kutegemea misaada kutoka nje kwa matumizi bora
ya ardhi hiyo. Ardhi ni ufunguo wa maisha ya binadamu kwa hiyo
Watanzania wote waitumie ardhi kama ni raslimali yao kwa maendeleo
ya baadaye. Kwa kuwa Ardhi ni mali ya Taifa, Serikali ni lazima iangalie
kuwa ardhi inatumiwa kwa faida ya Taifa zima na wala isitumiwe kwa
faida ya mtu binafsi au kwa watu wachache tu.

Ni wajibu wa TANU kuona kuwa nchi yetu inalima chakula cha kutosha
na kutoa mazao ambayo yataleta fedha nchini kwa kuuzwa katika nchi
za ngambo. Ni wajibu wa Serikali na Vyama vya Ushirika kuona kuwa
wananchi wanapatiwa vyombo, mafunzo ya uongozi unaohitajika katika
kilimo na ufugaji wa kisasa.
(b) Watu
Kuiwezesha siasa ya kujitegemea itekelezwe vizuri, wananchi ni budi
wajengwe moyo na shauku ya kujitegemea. Wajitegemee katika kuwa na
chakula cha kutosha, mavazi ya kufaa na mahali pazuri pa malazi.

Katika nchi yetu kazi iwe ni kitu cha kujivunia. Bali uvivu, ulevi na
uzururaji uwe ni jambo la aibu kwa kila mwananchi. Katika upande
wa ulinzi wa Taifa, wananchi wawe macho na vibaraka waliomo nchini
ambao wanaweza kutumiwa na maadui wa nje wenye nia mbaya ya
kuliangamiza Taifa hili na wawe tayari kulilinda Taifa inapolazimika
kufanya hivyo.
(c) Siasa Safi
Msingi wa siasa ya kujitegemea lazima uambatane na siasa ya Ujamaa
ya TANU. Ili kuzuia unyonyaji ni lazima kila mtu afanye kazi na aishi kwa
MIONGOZO MIWILI

39

jasho lake yeye mwenyewe. Na ili kuleta usawa wa kugawana mapato ya


nchi ni lazima kila mtu atimize wajibu wake kwa kufanya kazi kwa bidii
zake zote. Asiweko mtu wa kwenda kwa ndugu yake na kukaa kwa muda
mrefu bila kufanya kazi kwa sababu atakuwa anamnyonya yule ndugu
yake. Vilevile mtu yeyote asiruhusiwe kuzurura zurura hovyo mijini au
vijijini bila kufanya kazi ya kumwezesha kujitegemea mwenyewe bila
kuwanyonya ndugu zake.

TANU inaamini kuwa kila anayelipenda Taifa lake ni budi aweze


kulitumikia kwa kujitolea nafsi yake na kushirikiana na wananchi
wenzake kwa kuijenga nchi kwa manufaa ya watu wote. Ili kudumisha
Uhuru wa nchi yetu na raia zake barabara ni budi kujitegemea kwa kila
hali bila kwenda kuomba misaada nchi zingine.
Kujitegemea kwa mtu mmoja ni kujitegemea kwa nyumba kumi.
Kujitegemea kwa nyumba zote kumi za balozi ni kujitegemea kwa tawi
zima. Kujitegemea kwa matawi ni kujitegemea kwa Wilaya ambayo ni
kujitegemea kwa Mkoa. Kujitegemea kwa Mikoa yote ni kujitegemea kwa
Taifa lote ambalo ndilo lengo letu.
(d) Uongozi Bora
TANU inatambua umuhimu wa kuwa na Uongozi Bora. Tatizo lililopo
ni ukosefu wa mipango maalum ya kuwafundisha Viongozi na kwa
hiyo Ofisi Kuu ya TANU ni budi itengeneze utaratibu maalum kuhusu
mafundisho ya Viongozi tangu wa Taifa zima hadi Mabalozi ili waielewe
siasa yetu na mipango ya uchumi. Viongozi ni lazima wawe mfano mzuri
kwa wananchi kwa maisha yao na vitendo vyao pia.

SEHEMU YA NNE
UANACHAMA

Tangu Chama kilipoanzishwa, tumethamini sana kuwa na wanachama


wengi iwezekanavyo. Hii ilifaa wakati wa kupigania vita vya kumngoa
mkoloni. Hivyo ndivyo ilivyobidi TANU kufanya kwa wakati huo. Lakini
sasa Halmashauri Kuu inaona kuwa wakati umefika wa kutilia mkazo
kwenye imani ya Chama chetu na siasa yake ya Ujamaa.
40

MIONGOZO MIWILI

Kifungu cha Katiba ya TANU kinachohusu uingizaji wa mtu kwenye


Chama kifuatwe na ikiwa inaonekana kuwa mtu haelekei kuwa anakubali
imani, madhumuni na sheria na amri za Chama, basi asikubaliwe kuingia.

Na hasa isisahauliwe kuwa TANU ni Chama cha wakulima na wafanyakazi.

SEHEMU YA TANO

AZIMIO LA ARUSHA
Kwa hiyo basi, Halmashauri Kuu ya Taifa iliyokutana katika Community
Centre ya Arusha kuanzia tarehe 26/1/67 mpaka 29/1/67, inaazimia
ifuatavyo:
A. Viongozi
1. Kiongozi wa TANU au wa Serikali sharti awe mkulima au
mfanyakazi na asishiriki katika jambo lolote la kibepari au
kikabaila.
2. Asiwe na hisa katika makampuni yoyote.

3. Asiwe mkurugenzi katika kampuni ya kikabaila au kibepari.


4. Asiwe na mishahara miwili au zaidi
5. Asiwe na nyumba ya kupangisha.

6. Viongozi tunaofikiria hapa ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya


Taifa, Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa Vyama vilivyoshirikishwa
na TANU, Wakuu wa Mashirika ya Kiserikali, Viongozi kutokana
na kifungu chochote cha Katiba ya TANU, Madiwani, na
Watumishi wa Serikali wenye vyeo vya kati na vya juu. (Kwa
mujibu wa kifungu hiki kiongozi ni mtu au mtu na mkewe au
mke na mumewe).

B. Serikali na Vyombo Vingine


1. Inaipongeza Serikali kwa hatua zote ilizokwishachukua mpaka
hivi sasa katika kutimiza siasa ya Ujamaa.

2. Inaihimiza Serikali, bila kungojea Tume ya Ujamaa, ichukue

MIONGOZO MIWILI

41

hatua zaidi za kutimiza siasa yetu ya Ujamaa kama ilivyoelezwa


katika Tamko la TANU juu ya Ujamaa.

3. Inahimiza Serikali kutengeneza mipango yake kwa kutegemea


uwezo wa nchi hii kuiendesha mipango hiyo na wala isitegemee
mno mikopo na misaada ya nchi za ngambo kama ilivyofanya
katika mpango wa maendeleo ya miaka mitano. Halmashauri
Kuu ya Taifa inaazimia mpango huo urekebishwe ili ulingane na
siasa ya kujitegemea.
4. Serikali ione kuwa mapato ya wafanyakazi nje ya Serikali
hayapitani mno na yale ya wafanyakazi Serikalini.
5. Serikali itilie mkazo sana njia za kuinua maisha ya wakulima.

6. Inahimiza NUTA, Vyama vya Ushirika, TAPA, UWT, TYL, mashirika


yote ya Serikali, kuchukua hatua ili kutekeleza siasa ya Ujamaa
na Kujitegemea.

C. Uanachama
Wanachama wafundishwe kwa ukamilifu imani ya TANU ili waielewe, na
wakumbushwe wakati wote umuhimu wa kuishika imani hiyo.

42

MIONGOZO MIWILI

SURA YA PILI
MWONGOZO WA TANU WA 1971
TUMECHOKA KUCHEZEWA
1.




Mabeberu wathubutu
Kujifanya mbwa-mwitu,
Au kujifanya mwewe,
Kwa kuachia wenyewe
Tudhaniwe tu makoo
Ya kuku au kondoo.

2. Lakini watu ni watu,


Watu si mangondi katu:
Beberu angajigamba,
Angaruka, angatamba,
Ni mtu, hana mabawa:
Naye hufa, hana dawa.
3. Sasa linalia tena
La mgambo, linanena:
Beberu, leo ni leo!
Tulipozima koleo,
Mlidhani ndiyo mwisho,
Mkazidisha vitisho!
4.




Linalia la mgambo,
Lisikike hadi ngambo:
Tumechoka kuonewa!
Tumechoka kuchezewa!
Tunasema: sasa basi
Ubeberu na uasi!

5. Kwani sasa kimefika,


Kizazi cha Afrika;
Kizazi kipya thabiti,
Sumu yao wasaliti;
Mabeberu watajuta
Hapo kitapowakuta.
MIONGOZO MIWILI

6. Si kizazi cha vivuli,


Na wala sio cha nduli
Si kizazi cha watwana:
Ni kizazi cha vijana
Madhubuti, Wajamaa,
Waso ila, waso waa.
7.




Kimefika pasi shaka


Kiyashike madaraka;
Wanaojidai ubwana
Watalia kama wana;
Watatetema kwa homa,
Na kutubu: Tumekoma!

8. Vijana wa Afrika,
Siku yenu imefika!
Siku yenu ndiyo leo,
Siku ya kufunga teo:
Tumechoka kuonewa!
Tumechoka kuchezewa!
9. Shime, Onyesheni njia,
Vijana wa Tanzania:
Wapigeni wanyonyao,
Pamwe na vijibwa vyao;
Mabeberu makaburu,
Wapigeni kwa uhuru.

10.

Wamezidi kutughasi
Kwa kudhani ndiyo basi:
Semeni: leo ni leo,
Twali tukisuka teo!
Kimbieni, tumefika:
Iacheni Afrika!
43

MWONGOZO WA CHAMA JUU YA KULINDA,


KUIMARISHA NA KUENDELEZA MAPINDUZI YA
TANZANIA NA YA AFRIKA
Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi
cha kutosha, tumepuuzwa kiasa cha kutosha. Unyonge
wetu ndio uliotufanya tuonewe tunyonywe na kupuuzwa.
Sasa tunataka kufanya mapinduzi . . .

(Azimio la Arusha)

UTANGULIZI
1. Bara letu la Afrika leo ni kiwanja cha mapambano makali ya
ukombozi. Mapambano hayo ni kati ya wale ambao kwa karne
nyingi wamekuwa wakinyonya utajiri wa Afrika, na kuwatumia
wananchi wa bara hili kama vyombo vyao, kama watumwa wao, na
wananchi wa Afrika ambao, baada ya kutambua hali ya unyonge na
kunyonywa, wameamua kuingia katika mapambano ya kujikomboa.
Mapambano haya ni magumu na ya muda mrefu. Wakati mwingine
huwa ya kimya kimya, mara yalipuke kama baruti; wakati mwingine
mafanikio huenda kwa wananchi, halafu punde si punde mafanikio
yakawaponyoka wananchi. Hiyo ndiyo historia ya Afrika mpaka
mwaka 1960, ambapo nchi nyingi za Afrika zilipata uhuru wao wa
bendera. Tangu mwaka huo mpaka leo Serikali nyingi za Afrika
zimeangushwa kwa nguvu, na Serikali mpya kuundwa. Hivi juzi
mabadiliko ya ghafla na ya mabavu yametokea Uganda, ambako
Kibaraka Amini na kikundi cha wanajeshi wenzake waasi wameiasi
Serikali ya Kimapinduzi ya U.P.C inayoongozwa na Raisi Obote.
Wanajeshi walio wengi hawakubaliani na maasi hayo, na wengi
wao, hasa maafisa wakubwa wameuawa na vibaraka hao. Ni dhahiri
kuwa wanaofurahia maasi ya vibaraka hawa ni wale waliokuwa
wakipinga siasa ya U.P.C ya kuleta Umoja na Ujamaa, na kuondoa
ukabila na Unyonyaji. Ndiyo maana Chama chetu kina wajibu
wa kuifafanua shabaha kuu ya mapinduzi yetu na ya Afrika, na
kuwatambua maadui wa mapinduzi haya, ili kutayarisha mipango
44

MIONGOZO MIWILI

na mbinu zitakazotuwezesha kulinda, kuimarisha na kuendeleza


mapinduzi yetu.

2. Mapinduzi ni mabadiliko ya haraka katika jamii, mabadiliko


ambayo yanawanyanganya wachache madaraka ambayo walikuwa
wakiyatumia kwa manufaa yao (na ya wanyonyaji wa nje), na
kuyaweka madaraka hayo mikononi mwa wengi ili kuendeleza
maslahi yao. Kinyume cha mapinduzi ni kupinga mapinduzi, yaani
mabadiliko ya haraka yanayo wanyanganya madaraka wananchi
walio wengi, na kuwapa wachache, kwa madhumuni ya kuzuia
maendeleo ya Umma.
3. Shabaha kuu ya mapinduzi ya Afrika ni kumkomboa Mwafrika.
Ukombozi huu haudondoki kama mvua, bali hupatikana kwa
kupambana na unyonyaji, ukoloni, na ubeberu. Wala ukombozi
huu hauletwi na wataalam maalum. Wataalam wa ukombozi huu
ni sisi wenyewe tunaonyanyaswa, tunaonyonywa, na tunaoonewa.
Hakuna taifa lolote ulimwenguni lenye utaalam wa kufundisha
Waafrika jinsi ya kujikomboa. Wajibu wa kujikomboa ni wetu, na
utaalam wa mbinu za mapambano ya kujikomboa tutaupata katika
mapambano yenyewe.

4. Kadhalika, hali ilivyo hivi sasa katika Afrika ni kwanba hakujawa


na wananchi wa nchi yoyote ya Afrika ambao wamekwisha fikia
kiwango cha ukombozi halisi. Afrika bado ni Bara la watu waliomo
katika unyonge wa kuonewa na kunyanyaswa, ndiyo kusema
kwamba Vyama vya Siasa vya kimapinduzi katika nchi nyingi za
Afrika zinazojitawala, kama vile TANU, bado vingali ni Vyama vya
Ukombozi.
5. Mapinduzi ya Afrika ambayo lengo lake ni ukombozi kamili wa
Mwafrika yanapingana na siasa za unyonyaji za Ukoloni-Mamboleo
na Ubeberu na kuhakikisha kwamba utajiri wa Afrika unatumika
kwa maslahi ya nchi za kibepari za Ulaya na Marekani, badala
ya kuwanufaisha Waafrika wenyewe. Kwa hiyo kushiriki katika
mapinduzi ya Afrika ni kushiriki katika mapambano ya kupinga
Ukoloni na Ubeberu.
MIONGOZO MIWILI

45

6. Nchi za kibeberu ambazo zimekuwa zikinyonya na kukandamiza


Afrika kwa karne nyingi ni nchi za Ulaya Magharibi, hasa Uingereza,
Ufaransa, Ureno, Ubelgiji na Hispania. Nichi za kibeberu ndiyo hasa
zinazokabiliana na wananchi wa Afrika katika suala la ukombozi
wa Mwafrika. Majaribio mbali mbali yanayofanywa kuvuruga
maendeleo ya mapinduzi ya Afrika hasa kutokana na hila za
mabeberu wa Ulaya kutaka kuhifadhi na kuendeleza mirija yao ya
zamani.
7. Kwa Tanzania lazima ieleweke kwamba maadui tunaokabiliana
nao ana kwa ana ni ubeberu wa Kiingereza, ukoloni wa Kireno, na
ubaguzi wa rangi wa makaburu wa Afrika ya Kusini na Rhodesia.
Kwa sababu za historia, za jiografia na za siasa, mabeberu hawa
watakuwa tayari kutushambulia pindi wapatapo nafasi.

8. Mashambulio yaliyofanywa na mabeberu wa Kireno kuivamia


Jamhuri ya Guinea ni funzo kubwa sana kwetu. Sababu ya kwanza
ya Guinea kuvamiwa na mabeberu wa Kireno ni siasa yake ya usawa
na kupinga unyonyaji; na sababu ya pili ni msimamo wake thabiti
wa kuunga mkono wapigania ukombozi wa Guinea Bissau na wa
Afrika. Kwa sababu hizo hizo mabeberu hawa wanaweza siku moja
wakathubutu kuishambulia Tanzania. Lakini Guinea inatufundisha
vile vile kuwa wananchi na majeshi yao wakisimama imara pamoja,
hakuna mtu atakayeweza kuwanayanganya uhuru wao.

9. Funzo tulilojifunza Uganda ni la usaliti na la kupinga mapinduzi.


Yaani, badala ya kuivamia nchi ili kuiangusha Serikali ya
kimapinduzi, mabeberu hupendelea sana kuwatumia vibaraka
wananchi kuiangusha Serikali halali, ili kuunda Serikali ya
wanyapara, itakayowaruhusu mabeberu hao, wakishirikiana
na vibwanyenye vienyeji, kunyonya mali ya Taifa. Wananchi
inawapasa kuelewa, kutokana na tukio la Uganda na hata la
Guinea kwamba ingawa ubeberu bado una nguvu, uwezo wake wa
kuangusha Serikali ya Kimapinduzi unategemea sana uwezekano
wa kuwapata wapinga mapinduzi wa ndani wa kuwasaidia
kuyasaliti mapinduzi.
46

MIONGOZO MIWILI

10. Watanzania tunathamini sana uhuru wa Taifa letu, maana hapo


ndipo unapoanzia ukombozi wetu, na mategemeo ya mapambano
ya ukombozi wa wananchi wengi wa Afrika. Kwa sabau hii
tunawajibu wa kuchukua hatua zote muhimu zitakazotuwezesha
kuulinda uhuru wetu, ili tuweze kuendeleza mapinduzi yetu, na
kuifanya nchi yetu kuwa mfano imara wa mapinduzi ya Afrika.

SIASA
Chama
11. Wajibu wa kuongoza Umma na vyombo vyake mbali mbali katika
juhudi ya kulinda uhuru, ili mapinduzi ya ukombozi wa Mwafrika
yaendelee, ni wa Chama. Wajibu wa Chama cha Kijamaa ni kuongoza
shughuli zote za Umma. Serikali, Mashirika, Vyama vya Umma, n.k,
ni vyombo vya kutekelezea siasa ya Chama. Historia yetu fupi ya
uhuru inaonyesha matatizo yanayoweza kutokea wakati Chama
hakiongozi vyombo vyake. Sasa wakati umefika wa chama kushika
barabara hatamu na kuongoza shughuli zote za Umma.

12. Kuongoza kwanza maana yake ni kutoa lengo la Taifa. Hili


linaeleweka, na Chama kimekwisha timiza wajibu huo. Lengo letu
ni kujenga Ujamaa Tanzania. Chama kimekwisha toa miongozo juu
ya Ujamaa vijijini, Elimu ya Kujitegemean.k. Lakini, ili lengo la Taifa
liweze kufikiwa, lazima chama kitoe siasa na miongozo kuhusu
mipango mbali mbali ya shughuli za umma. Uko umuhimu wa
kufafanua siasa ya Chama juu ya nyumba, afya, kazi, siasa ya fedha,
mikopo n.k.

13. Lakini kutoa lengo la siasa hakutoshi kudhihirisha uongozi


madhubuti wa Chama. Maana nyingine ya kuongoza ni kuwaandaa
watu. Ndiyo kusema Chama ndicho kinachoamua umbile la
Serikali, mashirika mbali mbali, majeshi, n.k. Pamoja na umbile
la Serikali, Chama kitoe mwongozo juu ya utaratibu wa kutenda
kazi, na namna ya kufikia uamuzi. Ukweli ni kwamba siyo tu kuwa
tumerithi muundo wa Serikali ya kikoloni, bali hata tabia za kikoloni
MIONGOZO MIWILI

47

za utaratibu wa uongozi tumezifanya zetu. Kwa mfano, Serikalini,


viwandani, na katika Mashirika ya Umma, tumerithi tabia ya utawala
wa mtu mmoja, na wengine ni watu wa kupokea amri. Matokeo ya
watu kutokushirikishwa katika mipango ya kazi ni kuwafanya watu
wakione chombo cha Umma kana kwamba si chombo chao, na
wafanya kazi kuwa na tabia ya wakodiwa. Chama kina wajibu wa
kuchukua hatua za kudhihirisha uongozi wake katika jambo hili.

14. Pamoja na kuwaandaa watu, kuongoza ni kusimamia utekelezaji


wa siasa ya chama. Lazima zitafutwe njia za kuhakikisha kwamba
Chama kinasimamia, kwa vitendo shughuli na mwendo wa vyombo
vyake vya utekelezaji. Kadhalika, kuongoza ni kuweza kupima
matokeo ya utekelezaji. Ni wajibu wa Chama kuhakikisha kwamba
kinapima matokeo ya utekelizaji wa siasa unaofanywa na vyombo
vyake. Hii ndiyo njia ya pekee ya kuweza kuwa na hakika kwamba
maofisini, viwandani, katika majeshi, vijijini, n.k. wananchi wenyewe
wanashiriki katika kutafuta njia za kutatua matatizo yao.

15. Pamoja na suala la watu kushiriki katika kutatua matatizo yao


kuna swala la tabia ya viongozi kazini na katika maisha yao ya kila
siku. Lazima iwepo jitihada ya kujenga usawa kati ya viongozi na
waongozwa. Iwe ni mwiko kwa kiongozi wa Tanzania kuwa mwenye
majivuno, ubadhirifu, dharau au uonevu. Kiongozi wa Tanzania awe
mtu anayeheshimu watu, asiwe mpenda makuu; siyo mnyapara,
mkaripiaji na mwamrishaji watu. Kiongozi awe mfano wa ushujaa,
upiganiaji haki na usawa. Kadhalika Chama kina wajibu wa kukomesha
maonevu yanayofanywa na baadhi ya vyombo vyake kwa wananchi,
maana vitendo hivi haviendelezi Siasa ya Ujamaa. Hivyo ni vitendo
vinavyokifanya Chama na Serikali vifarakane na watu.
16. Kuna tabia hivi sasa ya baadhi ya viongozi kutotimiza masharti hayo,
na kupuuza na kukwepa kiujanja masharti na nia ya masharti ya
Uongozi. Wakati umefika wa Chama kuwa na utaratibu wa kusimamia
mwenendo na tabia za viongozi.

48

MIONGOZO MIWILI

Siasa ya Nchi za Nje


17. Siasa yetu ya nchi za nje ni siasa ya kutofungamana na upande wo
wote. Tuko tayari kushirikiana kirafiki na nchi yoyote yenye nia
njema kwetu bila kujali kama hiyo ni ya mashariki au ya magharibi.
Jambo la pili muhimu katika siasa yetu ya nje ni kuimarisha uhusiano,
ushirikiano na kuunga mkono vyama halisi vya Ukombozi wa Afrika.
Tumesema hapo mwanzoni kwamba sisi wenyewe bado tuko kwenye
hatua za Chama cha Ukombozi. Hivi sasa katika Afrika Vyama vya
Ukombozi ndivyo vilivyo katika mstari wa mbele wa mapambano
ya kupinga Ukoloni na Ubeberu, Tukiimarisha kushirikiana kwetu,
tukielewa kuwa vita vyao ni vita vyetu, tutaongeza sana nguvu zetu
za kuleta ukombozi wa Afrika nzima. Chama kichukue hatua zinazofaa
za kujenga uhusiano huo wa kimapinduzi na Vyama vya Ukombozi
vya Afrika, vya Asia na vya Marekani Kusini. Vile vile ni wajibu wetu
kujenga uhusiano wa kidugu na wa kimapinduzi na raia wa Amerika
wanaopigania haki na usawa wa binadamu.

18. Aidha, tunao wajibu wa kuimarisha kushirikiana na kuungana mkono


na nchi za kimapinduzi za Afrika, maana sote tumo katika jahazi
moja, na safari yetu ni moja. Tukiungana na kushirikiana, maadui
zetu hawataweza kutumaliza mmoja mmoja kama ilivyo tabia yao.

19. Kwenye Umoja wa Mataifa katika Mashirika mengine ya kimataifa


kuna haja ya kutilia mkazo kushirikiana na nchi zote za kirafiki, za
Kijamaa na za Kimapinduzi za Afrika, Asia na Marekani ya Kusini.

Uganda na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki

20. Tunatambua umuhimu na manufaa yaliyopo, kisiasa na kiuchumi,


katika umoja na ushirikiano uliopo kati ya nchi za Afrika ya
Mashariki. Hivyo, hali ya hivi sasa iliyoletwa na vibaraka wa
Uganda kwa kuvamia serikali halali ya Chama cha U.P.C. inatuletea
wasiwasi mkubwa katika ushirikiano na katika kuendesha shughuli
za Jumuiya. Hali hii ikiendelea inaweza kufanya maendeleo na
mafanikio ya Jumuiya hii kuwa magumu sana, na pia ushirikiano
MIONGOZO MIWILI

49

wa nchi za Afrika Mashariki huenda ukawa wa shida sana na dhaifu.


Chama kinaunga mkono msimamo wa Serikali ya Tanzania juu ya
Uganda na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ingawa swala la ukombozi
wa Uganda ni la wananchi wa Uganda, ni wajibu wa wananchi wa
Tanzania kuunga mkono ndugu zetu wa Uganda katika juhudi zao
za kujikomboa.

ULINZI NA USALAMA
Katika upande wa ulinzi wa Taifa, wananchi wawe macho
na vibaraka waliomo nchini ambao wanaweza kutumiwa
na maadui wa nje wenye nia mbaya ya kuliangamiza Taifa
inapolazimika kufanya hivyo.

(Azimio la Arusha)

21. Msingi wa Maendeleo yote ya Watanzania ni Watanzania wenyewe:


kila Mtanzania; na hasa kila mzalendo, na kila mjamaa. Msingi
wa Maendeleo ya Ulinzi na Usalama wa Tanzania ni Watanzania
wenyewe: kila Mtanzania; na hasa kila mzalendo, na kila mjamaa.

22. Kama Chama chetu kingalilazimika kupigana Vita vya Ukombozi,


kila mwana-TANU angalilazimika kuwa askari, ama ndani ya
jeshi, au popote alipo: Mwana-TANU angalikuwa ni Mwanajeshi,
na Mwanajeshi angalikuwa ni Mwana-TANU. Siyo Chama chetu tu
ambacho kingalikuwa ni Chama cha Ukombozi; bali Jeshi letu pia
lingalikuwa ni jeshi la Ukombozi-ngumi na ngao ya Chama cha
Ukombozi.

23. Chama chetu hakikulazimika kupigana Vita ya Ukombozi. Kilikuwa


Chama cha Ukombozi bila Jeshi la Ukombozi. Likini tangu mwaka
1964 tumekuwa tukiunda Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Kama vile
Chama cha TANU kilivyo bado ni Chama cha Ukombozi; basi Jeshi
la Wananchi wa Tanzania pia ni Jeshi la Ukombozi wa Wananchi wa
Tanzania. Uhusiano wa TANU na Jeshi la Wananchi ni lazima uwe
50

MIONGOZO MIWILI

ni uhusiano baina ya Chama cha Wananchi na Jeshi la Wananchi.


Ni juu ya TANU kuhakikisha kuwa Jeshi la Wananchi ni Jeshi la
Ukombozi na Ulinzi wa Wananchi. Ni kazi ya TANU pia kuona kuwa
kazi kubwa ya Jeshi wakati wa amani ni kuwawezesha wananchi
kulinda uhuru wao na siasa yao ya Ujamaa na Kujitegemea.

24. Halmashauri Kuu ya Taifa inatilia mkazo juu ya utekelezaji wa


Azimio la Arusha, na hasa kuzidisha mwamko wa Siasa, ili kila
Mwananchi aweze kufahamu mazingira ya Taifa letu, na umuhimu
wa kulinda usalama na maisha ya wananchi: Siasa yetu, Uhuru
wetu, Uchumi wetu na Utamaduni wetu.

25. Kutokana na mwamko wa Siasa, wananchi wafahamishwe maadui


wa Taifa letu, na hila wanazotumia kupiga vita siasa yetu, Uhuru
wetu, Uchumi wetu na Utamaduni wetu. Papo hapo, ili wananchi
waweze kumkabili adui huyo, lazima wafahamishwe nguvu za adui
huyo katika fani zote, kama vile majeshi yao, biashara zao, maisha
yao na tabia zao, na jinsi zinavyogongana na hali zetu.

26. Ili waweze kuwakabili maadui hao, wananchi hawana budi


kufahamu kwamba wao wenyewe ndio ngao ya Taifa. Hii maana
yake ni kwamba shughuli za Ulinzi na Usalama ziwekwe mikononi
mwa watu wenyewe. Hatuna uwezo wa kuunda majeshi makubwa
makubwa ya kudumu kulinda nchi yetu yote. Majeshi yetu lazima
yawe majeshi ya Umma, na yatumike kwa kuwafunza wananchi
wenyewe jinsi ya kujilinda katika sehemu wanazoishi, na kuwa na
uwezo wa kutoa habari zinazohusu usalama wa Taifa letu. Kwa hiyo
ni lazima kuanzisha mafunzo ya malisha kwa nchi nzima. Hawa
malisha, kwa sababu wataenea nchini, ndio watakaokuwa na wajibu
wa kulinda mipaka ya nchi kavu na pwani, hali kadhalika anga, na
kuwafichua majasusi na maadui kwa kushirikiana na majeshi yetu
ya kawaida.

Chama Kuongoza Majeshi

27. Uandikishaji wa malisha na wa majeshi yote lazima uwe wa uangalifu


sana, na usimamiwe na Chama. Ushirikiano wa majeshi na malisha, na
MIONGOZO MIWILI

51

mafunzo ya Elimu ya Siasa kwa wote, iwe ni kazi muhimu ya Chama.


Chama basi kiunde Kamati ndogo ya Kamati kuu, ishughulikie Ulinzi
na Usalama.

UCHUMI NA MAENDELEO
Maendeleo ya nchi huletwa na watu
(Azimio la Arusha)
Maendeleo ya Watu
28. Kwa watu ambao walikuwa watumwa, au ambao walikuwa
wakionewa, wakinyonywa, na kunyanyaswa kwa sababu ya Ukoloni,
Ukabaila au Ubepari, maendeleo maana yake ni ukombozi.
Kitendo chochote kinachowapa uwezo zaidi wa kuamua mambo yao
wenyewe, ni kitendo cha maendeleo, japo kama hakiwaongezei afya
wala shibe. Kitendo chochote kanachowapunguzia uwezo wao wa
kuamua mambo yao wenyewe na kutawala maisha yao wenyewe,
si kitendo cha maendeleo, ni kitendo cha kuwarudisha nyuma,
japo kama kitendo chenyewe kinawaongezea afya na shibe kidogo.
Kwetu sisi maendeleo ya maana ni yale yanayotuondolea kuonewa,
kunyonywa, kunyanyaswa na mawazo ya kufungwa, na kutuongezea
uhuru na utu wetu. Kwa hiyo katika kufikiria maendeleo ya Taifa
letu, na katika kupanga mipango ya maendeleo, wakati wote mkazo
mkubwa utiliwe kwenye maendeleo ya WATU na siyo ya vitu. Ili
maendeleo hayo yawe ya watu, watu wenyewe lazima washiriki
katika kufikiria, kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo yao.
Chama chetu kazi yake si kuhimiza wananchi kutekeleza mipango
iliyoamuliwa na wataalam na viongozi wachache. Chama chetu kazi
yake ni kuona kuwa viongozi na wataalam wanatekeleza mipango ya
maendeleo kama ilivyoamuliwa na wananchi wenyewe. Uamuzi huu
wa wananchi unapokuwa unahitaji ujuzi ambao walio nao ni viongozi
na wataalam, ni wajibu wa viongozi na wataalamu hao kufikisha
ujuzi huo kwa wananchi ili waweze kujifanyia uamuzi wao; lakini
52

MIONGOZO MIWILI

si haki kwa viongozi na wataalam kujinyakulia wajibu wa kuamua


kila jambo badala ya wananchi wenyewe, ati kwa sababu wao ndio
wenye ujuzi.

29. Ili wananchi wawe na ari ya kulinda nchi yao, lazima Serikali ya
TANU kwanza itilie nguvu sana hali ya Uchumi wa wananchi.
Mtindo wa Uchumi tuliorithi kwa wakoloni, ambao umewatupa
wananchi wengi nje ya uchumi, lazima ubadilishwe bila kukawia,
na kuanzisha mipango ya kuongeza matumizi na kutumbukiza
rasilimali katika Wilaya zote. Kwa mfano, Mpango wa Fedha za
Maendeleo Mikoani umeonyesha kusaidia kuamsha shughuli za
kiuchumi na kuleta manufaa ya wazi wazi kwa wananchi, na itafaa
mpango huo utiliwe mkazo kwa kuongeza fedha hizo na kufanya
matumizi hayo yawe ya mwanzo katika makisio ya fedha za Serikali.
Chama kitilie mkazo kushirikisha watu katika kazi mbali mbali za
kujenga Taifa.

Akiba

30. Pia ni wajibu wa Chama kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa


kujiwekea Akiba katika vyombo vya Umma, kama vile Benki ya
Akiba na Benki ya Biashara badala ya kuweka ovyo ovyo tu.

Uchumi wa Kitaifa

31. Katika kuimarisha Maendeleo ya watu, hivi sasa ipo haja kubwa ya
kujenga na kustawisha uchumi wa ndani ya Taifa letu. Ingawa jambo
hili limegusiwa katika Mpango wa Pili wa Miaka Mitano, halikutiliwa
mkazo katika utekelezaji, na matokeo yake hayajaonekana. Kadhalika,
vitu ambavyo vinatengenezwa nchini mwetu lazima vilindwe na
mashindano yasiyo ya lazima kutoka nchi za nje.

Biashara ya Nje

32. Juu ya Biashara yetu na nchi za nje ni lazima kuepuka utumiaji


wa akiba yetu ya fedha za Kigeni kwa kununua vitu visivyosaidia
Uchumi wetu. Serikali na Mashirika yake vionyeshe mfano katika
MIONGOZO MIWILI

53

jambo hilo. Vikao vinavyoagiza vitu toka nje lazima vipewe


mwongozo unaolingana na Siasa yetu ya Ujamaa na Kujitegemea,
na ihakikishwe kwamba vinafuata. Ni wajibu wa kila Mwanachi, na
hasa Kiongozi kukumbuka kwamba upungufu wa fedha za Kigeni
unadhoofisha uchumi wetu na kuhatarisha uhuru wetu.

Mashirika ya Umma

33. Hali, tabia na shughuli za mashirika ya Umma lazima kutupiwa


macho na kuhakikisha kuwa zinasaidia kupeleka mbele Siasa yetu
ya Ujamaa na Kujitegemea. Shughuli za mashirika hayo lazima ziwe
za kuridhisha na sio za kuleta manunguniko. Chama kihakikishe
kwamba mashirika hayo hayatumii fedha kwa fujo na katika mambo
yasiyonufaisha Uchumi wa Nchi kwa jumla.

Ziada

34. Serikali isimamie na kuongoza matumizi ya fedha zote za ziada


zinazopatikana kutokana na shughuli za Uchumi za Mashirika ya
Umma

35. Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha


kutosha, na tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu
ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa
tunataka mapinduzi; mapinduzi ya kuondoa unyonge
ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na wala tusipuuzwe tena.

54

MIONGOZO MIWILI

SURA YA TATU
MWONGOZO WA CCM WA 1981
YALIYOMO
DIBAJI
SEHEMU YA KWANZA
UTANGULIZI


SEHEMU YA PILI

UCHAMBUZI WA KUJIKOSOA KAMA CHAMA


SEHEMU YA TATU

KUJENGA MSINGI WA UCHUMI WA KIJAMAA WA TAIFA


LINALOJITEGEMEA

SEHEMU YA NNE

CHAMA NA MAPINDUZI YETU


MIONGOZO MIWILI

55

DIBAJI
Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama, katika Mkutano wake uliofanyika
mjini Dar es Salaam kuanzia tarehe 23 Novemba, 1981 hadi tarehe 7
Desemba, 1981 ilipitisha MWONGOZO WA CHAMA CHA MAPINDUZI
wa 1981. Halmashauri Kuu ya Taifa ilifikia uamuzi huu baada ya
kuzingatia na kuchambua hali halisi ilivyo hivi sasa nchini katika
masuala ya siasa, uchumi na maendeleo ya jamii, na kuona kuwa
kuna haja sasa ya kutoa msukumo mpya wa ujenzi wa Ujamaa, pamoja
na utekelezaji sahihi wa maamuzi mengine mbalimbali yaliyokwisha
kutolewa. Shabaha ya Mwongozo wa 1981 ni kufafanua kwa upana zaidi
nadharia ya Chama juu ya masuala muhimu na ya msingi ya Siasa yetu
katika fani mbalimbali, pamoja na kutoa maelekezo yaliyo wazi zaidi
kuhusu mbinu sahihi za utekelezaji wa siasa hiyo.
Katika kipindi kilichofuatia kutangazwa kwa Azimio la Arusha, Chama
kilitoa maandishi muhimu kadhaa yanayochambua na kufafanua fani
mbalimbali za Siasa yetu ya Ujamaa na Kujitegemea, pamoja na kuelekeza
njia sahihi za utekelezaji wa siasa hiyo. MWONGOZO WA TANU wa mwaka
1971 ni miongoni mwa matamko hayo muhimu ya kipindi hicho.

Mwongozo huo wa TANU unabaki na nafasi yake maalum katika historia


ya mapambano ya Chama katika kusukuma mapinduzi ya Tanzania na
Afrika kwa jumla katika kipindi hicho.

56

MIONGOZO MIWILI

SEHEMU YA KWANZA
Utangulizi
1. Historia ya Watanzania kwa vile ni sehemu tu ya historia kubwa
zaidi ya Waafrika kwa jumla lazima wakati wote ichambuliwe na
kueleweka katika mazingira ya umoja wa Afrika na watu wake.
Waafrika wamepitia vipindi na karne za fanaka na maendeleo ya
jamii na pia vipindi na karne za misukosuko mikubwa na hata
unyonge kitaifa.

2.

3.

Historia ya Waafrika ina mifano ya dola zilizofikia hatua kubwa


ya maendeleo, ustaarabu na fanaka katika sehemu mbalimbali za
bara hili na kwa nyakati mbalimbali. Maandishi, magofu, zana na
mabaki ya vifaa vya aina mbalimbali vinavyogunduliwa sasa na
wataalamu katika sehemu mbalimbali za Afrika vinathibitisha
ustaarabu wa wakati huo katika fani za kilimo, ujenzi, vita,
biashara na siasa.

Historia ya bara hili pia ina kumbukumbu za vipindi vya misukosuko


ya kuingia kwa mataifa ya kigeni. Kuna kipindi Waasia walipoingia
Afrika kwa madhumuni ya kujinufaisha na biashara walizoendesha
humu Afrika. Mojawapo ya biashara haramu walizoanzisha ni
biashara ya watumwa ambayo ilienea hata hapa Tanzania. Biashara
ya Watumwa katika Afrika iliendeshwa pia na mataifa ya Ulaya.
Inakisiwa kuwa Waafrika wapatao milioni mia moja walihusika
na biashara hii ya utumwa. Kumbukumbu za kipindi hiki ambacho
watu walisakwa, walikamatwa na kuuzwa bado zingali hai miongoni
mwa Watanzania.

4. Kipindi kilichofuatia ni cha wakoloni wa mataifa ya Ulaya


waliowanyanganya Waafrika ardhi yao, kuigawa na halafu
wakawatawala. Wakati huu Watanzania walitumikishwa na
wakoloni. Mazao na matunda ya jasho lao yalichukuliwa kupelekwa
nchi za wakoloni kujenga uchumi wao.

5. Watanzania, kama ilivyokuwa kwa Waafrika wengine kote


barani Afrika, hawakukiri uvamizi, utumwa wala kutawaliwa bali
MIONGOZO MIWILI

57

walisimama imara kupambana na maadui kwa vita na mbinu


nyingine.

6. Ni vigumu hapa kueleza kwa undani mifano yote ya mapambano


ya Watanzania dhidi ya uvamizi wa kikoloni. Hata hivyo ni muhimu
kutaja mifano michache ambayo ni vielelezo vya ushujaa, moyo
wa uzalendo na jeuri ya kukataa kutawaliwa: vita vya Wasambaa
chini ya Kimweri, vita vya Wahehe vikiongozwa na Mkwawa,
vita vya Maji Maji vikiongozwa na Kinjeketile, Mputa na Kibasila.
Wakati huo huo Waafrika wa Zanzibar walipambana kuupinga
uvamizi uliofanywa na Waarabu ambao baadaye walishirikiana na
ukoloni wa Waingereza. Watanzania wakati huo hawakufanikiwa
kuwangoa wakoloni.

7. Kushindwa kwa Waafrika katika mapambano hayo kunaelezeka.


Kwanza ni kwa sababu Waafrika hawakuwa na umoja, walikuwa
wamegawanyika katika makabila ambayo yaliishi kwa kutiliana
mashaka, kushambuliana na kudharauliana. Wavamizi waliuelewa
mfarakano huu na walitumia laghai za aina mbalimbali ili kuwagawa
zaidi na kuwashinda mmoja mmoja. Pili zana za vita za Waafrika
wakati huo zilikuwa hafifu ukilinganisha na silaha bora zaidi za
wavamizi. Na Tatu ni kuwa sababu ya kwanza na ya pili zilifanya
upeo wao wa kuandaa malengo na mbinu za vita uwe mfinyu sana
na ambao ulitegemea zaidi ushupavu na ushujaa kuliko kuchambua
uhusiano wa nguvu kati yao na adui na kutambua nguvu na udhaifu
wao na nguvu na udhaifu wa adui ili kuvitumia vipengele hivyo kwa
maslahi yao.
8. Miaka iliyofuatia Vita vya Maji Maji ilikuwa ya misukosuko na
matatizo makubwa kwa wananchi. Pamoja na unyonge wa watu
waliopoteza maelfu ya ndugu zao, miaka hiyo ilikuwa na janga la
njaa na magonjwa ya kuambukiza, hasa ndui.

9. Wakati huo huo maelefu ya watu walilazimishwa kuutumikia


ukoloni kwenye ujenzi wa Reli ya Kati na ya Tanga na kazi nyingine
za harubu ambako walikumbana na ukatili wa Wajerumani
usioelezeka. Katika Vita Vikuu Vya Kwanza Vya Dunia wananchi
58

MIONGOZO MIWILI

walilazimishwa kushirikiana na wakoloni wa Kijerumani au wa


Kiingereza kutetea ukoloni na kwa mara nyingine tena wengi
walipoteza maisha yao katika vita visivyokuwa vyao.

10. Lakini, pamoja na hayo vuguvugu la kisiasa liliongezeka. Haikupita


miaka mingi baada ya Vita Vikuu vya Kwanza ishara za kwanza
zilijitokeza Bara na Visiwani. Mwaka 1929 Waafrika walianzisha
African Association kwa Bara ambayo mwaka 1948 ikajiita
Tanganyika African Association na 1934 walianzisha African
Association Visiwani, vyote vikiwa vyama vilivyojishughulisha
na ustawi wa jamii pamoja na utetezi wa maslahi fulani fulani ya
Waafrika.
11. Mwisho wa Vita Vikuu vya Pili ulifuatiwa na vuguvugu la mwamko
wa kisiasa ulioongezeka kutokana na hali ya ukoloni nchini
kuwakera na kuwabana mno wananchi pamoja na vuguvugu la
askari waliorudi toka mpakani.
12. Wakati huo huo, kuongezeka kwa idadi ya wafanyakazi bandarini
na Serikalini na siasa ya ubaguzi wa rangi na ya mishahara
iliyoendeshwa na watawala wa Kiingereza kuliwatia wafanyakazi
dukuduku la kutaka kuungana na kupigania haki zao. Mgomo
mkubwa wa kwanza wa makuli wa Dar es Salaam na pia Zanzibar
uliowatikisa wakoloni ulitokea kunako mwaka 1948. Hali ilikuwa
inajiandaa kwa uwezekano wa kuanzishwa vyama halisi vya kisiasa
nchini.

A. KUZALIWA KWA TANU NA ASP

13. Historia ya sasa ya mapambano ya ukombozi katika Tanzania


ni historia ya vyama vya kisiasa vya TANU na ASP. Tanganyika
African Association na African Association na Shirazi Association
kwa Zanzibar vilianzisha vuguvugu la siasa na kuandaa mazingira
ya kuviwezesha vyama kamili vya kisiasa kujitokeza. Vuguvugu la
vyama vya wafanyakazi nalo liliongezea joto joto la kisiasa nchini.
Wakati huo huo nchi nyingine kama Ghana ya Kwame Nkrumah
MIONGOZO MIWILI

59

na Kenya ya Jomo Kenyatta, zilikwisha anza kuunda vyama vya


kuongoza mapambano ya uhuru, na vuguvugu lake liliongezea
mwamko wa uhuru wa Watanzania.

14. Hivyo, TANU (7.7.54) na ASP (5.2.57) viliundwa na kujipa majukumu


ya mashujaa wa Maji Maji na wengineo walioshindwa huko nyuma na
kujibunia malengo, mbinu na zana mpya kwa madhumuni yale yale
ya kuungoa ukoloni wa Kiingereza nchini Tanzania Bara na usultani
na uwakala wa Kiingereza Visiwani Zanzibar. Mapambano yalikuwa
makali na magumu Tanzania Bara na Visiwani.

15. TANU, chini ya uongozi wa Mwalimu Julius K. Nyerere, ilifaulu


kuwaunganisha Watanganyika kwa jumla katika hali ngumu ya ukabila,
hila, vitisho na mbinu za Serikali ya Kiingereza. TANU iliyafikisha
mapambano ya uhuru hadi kwenye uwanja wa kimataifa na Umoja
wa Mataifa ambako hila za ukoloni wa Kiingereza zilifichuliwa na
kushindwa. Vyama kadhaa vilivyozushwa ili kuwagawa Waafrika na
kuchelewesha uhuru vyote vilishindwa. Uingereza ilibidi ikiri nguvu
na sauti ya TANU na tarehe 9 Desemba, 1961 Tanganyika ilijinyakulia
uhuru wake, miaka saba tu baada ya kuundwa kwa Chama hicho.
16. Afro-Shirazi Party, chini ya uongozi wa Sheikh Abeid Amaan Karume,
kilikua mwaka hadi mwaka na kuvishinda vyama vingine vyote
vya upinzani. Lakini dola ya Sultani kwa kushirikiana na ukoloni
wa Uingereza walikinyanganya Chama cha Afro-Shirazi ushindi
wake wa halali katika Uchaguzi Mkuu mara nne mfululizo. Ndipo
tarehe 12.1.1964 Chama Cha Afro-Shirazi kikafanya mapinduzi
halali ya silaha yaliyoitokomeza Serikali haramu ya Sultani mwezi
mmoja baada ya Sultani na vibaraka wake wa Nationalist Party
kukabidhiwa uhuru wa bandia na Waingereza.

17. Vyama vya TANU na ASP vilijenga historia ya kushirikiana na


kuungana mkono tangu kuundwa kwao. Kwa hiyo, mara baada ya
mapinduzi ya Zanzibar, Serikali ya TANU iliyatambua mapinduzi
hayo na kuyaunga mkono kwa vitendo. Miezi mitatu baada ya
mapinduzi ya Zanzibar ushirikiano na udugu wa jadi wa wananchi
wa Tanganyika na wa Zanzibar uliimarishwa kwa kitendo cha
60

MIONGOZO MIWILI

kimapinduzi cha kuunganisha nchi mbili hizi katika Muungano wa


Tanganyika na Zanzibar ambao sasa unaitwa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.

B. MAPAMBANO YA KULINDA UHURU NA


KUJENGA JAMII MPYA

18. Serikali ya Mapinduzi ya ASP haikuchelewa kuchukua hatua za


kuimarisha ushindi iliyoupata dhidi ya usultani. Hatua muhimu
katika fani za siasa, uchumi na ustawi wa jamii zilichukuliwa kama
msingi wa kwanza katika kazi ngumu ya kuijenga jamii mpya ya
haki na usawa. Ardhi ilitaifishwa na hodhi kubwa za makabaila
wa kiarabu waligawiwa umma wa wananchi wasiokuwa na ardhi.
Wakati huo huo mabenki na biashara ya nje zilitaifishwa na vyombo
vya umma kuundwa.

19. Serikali ya TANU haikuchelewa kuchukua hatua za dhati za


kujiimarisha ili kuikabili kazi kubwa ya kulinda uhuru na kuanza
ujenzi wa uchumi na wa jamii mpya inayojitawala katika hali ya
matazamio makubwa ya wananchi kwamba uhuru utawaletea
mabadiliko ya haraka katika hali ya maisha yao. Miaka mitano ya
kwanza iliyofuatia uhuru ilikuwa kipindi kigumu kwa TANU na
Serikali yake changa. TANU yenyewe ilibidi iondokane na hali ya
kuwa Chama cha kupigania uhuru na kuwa Chama cha kulinda
uhuru na kujenga Taifa linalojitawala. Wakati huo huo Chama
kiliwajibika kuiongoza Serikali na wananchi kwa jumla katika
jitihada ya kutafuta falsafa ya jamii itakayolingana na matazamio ya
wananchi na inayoweza kuwaletea maendeleo halisi nchini.
20. Ilidhihirika katika miaka hiyo ya mwanzo ya uhuru wa Tanganyika
kuwa mgongano ulianza kujengeka kati ya matazamio ya wananchi
kwa jumla kwamba uhuru ungaliwaletea mabadiliko katika
hali ya maisha yao na kwa haraka, na uwezo mdogo wa Serikali
wa kukidhi haja za wananchi kulingana na matazamio yao.
Mabadiliko makubwa ya mapato na hali ya maisha yaliyoonekana
kwa wachache, viongozi na maafisa wa Chama na serikali
MIONGOZO MIWILI

61

waliokabidhiwa madaraka yaliyokuwa yanashikwa na wakoloni


zamani, pamoja na vitendo vya baadhi ya viongozi na maafisa hawa
vya kuanza kutumia nafasi zao kujitajirisha, viliimarisha mgongano
huo. Tafsiri ya hali hii ilijitokeza wazi wazi wakati umma ulianza
kuwaita wale walioonekana wanafaidika kwa vyeo vya uhuru
Naizesheni wakati wananchi waliobaki kuitwa Baba kabwela.

21. Pamoja na misuguano hii ya kijamii, uongozi wa Chama ulianza


kuwa na wasi wasi na maendeleo ya kiuchumi yaliyopatikana
tangu uhuru. Maongozi ya uchumi wakati huo yalikuwa kwamba
msingi wa maendeleo ya nchi ni rasilimali toka ngambo. Ilianza
kudhihirika kuwa utekelezaji wa msimamo huo kiuchumi haukuwa
na matokeo yaliyotarajiwa.

22. Katika hali hiyo ambapo Chama kilianza kuona kuwa Serikali
yake inashindwa kutosheleza matazamio ya wananchi kwa jumla
na badala yake kukabiliwa na ongezeko la misuguano ya kijamii
mijini na vijijini, na ambapo kilianza kuingiwa na mashaka na
kutoridhika na matokeo ya utekelezaji wa mipango ya uchumi wa
taifa uliotegemea rasilimali toka ngambo kuwa ndiyo msingi wa
maendeleo, Chama kiliwajibika kujiuliza maswali juu ya usahihi wa
siasa ambayo kimeifuata na kuitekeleza tangu nchi ijipatie uhuru.
Siasa ya uchumi ya kipindi hiki ilikuwa na sura mbili: kujenga nchi
kwa msingi wa ubebari na kwa kutegemea rasilimali toka ngambo.
Funzo tulilopata kama Chama ni kuwa siasa hiyo ya uchumi ilikuwa
imeshidwa kwa maana mbili: Kwanza ni kuwa badala ya kusaidia
kuimarisha umoja wa Taifa ulioanza kujengwa wakati wa kupigania
uhuru ilizalisha migongano ya kijamii na kuanza kukifarakanisha
Chama na umma. Pili, Siasa hiyo ya uchumi wa kibepari
unaotegemea rasilimali toka ngambo kama msingi wa maendeleo
hayo pia ilishindwa maana utekelezaji wake hakuleta vuguvugu
la maendeleo ya kiuchumi yaliyotegemewa na wala hakukuwa na
mtiririko wa rasilimali za kutosha toka ngambo kuingia nchini.

62

MIONGOZO MIWILI

C. AZIMIO LA ARUSHA
23. Tangu nyakati za kupigania uhuru Chama kiliweza wakati wote
kuelewa na kutambua mwenendo wa hali ya mapambano nchini
na duniani kwa jumla na kuchukua hatua sahihi kwa wakati
unaofaa ili kuimarisha na kuendeleza mapambano ya wananchi.
Kuna maamuzi kadhaa katika historia ya Chama chetu, ambayo ni
pamoja na uamuzi wa kuunganisha nchi za Tanganyika na Zanzibar
yanayoonyesha kinaganaga uwezo huo wa Chama kukua na nyakati.

24. Kielelezo kimoja kikubwa cha uwezo wa Chama kukua na nyakati


na kuelewa mahitaji halisi ya maendeleo ya mapinduzi ya umma ni
Azimio la Arusha juu ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Kwa uamuzi
huo, misingi mipya na ya kimapinduzi ya kulijenga na kulilinda Taifa
iliwekwa hadharani. Kutaifishwa kwa mabenki, biashara ya nje na
mashamba makubwa ya mabepari, kuundwa kwa mashirika ya
umma na kuanzishwa kwa viwanda vya umma ni baadhi tu ya mambo
yaliyodhihirisha nia ya Chama ya kuunda mfumo mpya wa uchumi
utakaofanana na jamii ya kijamaa inayodhamiriwa kujengwa.

25. Hatua za kujenga Ujamaa zilizochukuliwa hadi sasa zimejenga


msingi unaotia moyo na ni mafanikio ya kujivunia. Njia muhimu za
uchumi kama benki, viwanda, biashara ya nje na ya ndani, mashamba
makubwa, reli na posta zinamilikiwa na umma, tofauti ya mishahra
kati ya iliyokuwa chini kabisa na iliyokuwa juu kabisa serikalini wakati
wa kupata uhuru ilikuwa ya uwiano wa 1:7 na sasa ni ya uwiano
wa 1:4. Pamoja na hali ya uchumi wetu kitaifa kuwa ya matatizo,
tumefaulu kutoa elimu bure toka msingi hadi Chuo Kikuu na elimu
kwa watoto wote wa kiwango cha msingi; wakati huo huo tunatoa
matibabu bure toka vijijini hadi mijini; wananchi wana nafasi ya
kushiriki katika mambo yanayowahusu, wafanyakazi wana mabaraza
yao, wakulima vijijini wana Serikali zao zinazoendesha shughuli zao
wakati mpango wa demokrasia ya Chama kimoja unawapa nafasi
wananchi kuchagua wabunge wao. Yote haya na mengine ni vielelezo
vya mafanikio ya Siasa ya Ujamaa. Aidha, uwezo tuliouonyesha kwa
kukabiliana na shida kubwa ya njaa mwaka 1974/75 bila Watanzania
MIONGOZO MIWILI

63

kupoteza maisha yao na pia ushindi wetu dhidi ya majeshi ya uvamizi


ya Iddi Amin ambao umepatikana kutokana na mshikamano sahihi
wa Chama, Serikali, wananchi na wapiganaji, yote haya ni mafanikio
ya ujamaa.

26.
Tungeweza kuendelea kukariri mafanikio yaliyopatikana
nchini kutokana na utekelezaji wa siaisa ya Chama ya Ujamaa
na Kujitegemea. Lakini jambo la kuzingatia ni kuwa hatua
tulizozichukua katika kutekeleza Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea
ni za awali tu na kwamba kubwa zaidi tulilofanikiwa ni kujichorea
barabara tunayodhamiria kufuata katika kulijenga Taifa letu la
watu sawa na huru ambalo lengo lake ni maendeleo kwa wote.

SEHEMU YA PILI

UCHAMBUZI WA KUJIKOSOA KAMA CHAMA


(1) Upungufu katika kusimamia uchumi
27. Halmashari Kuu ya Chama ya Taifa katika kikao chake cha tarehe 15
hadi 17 Mei, 1981 ilizingatia hali ya uchumi na jamii inayolikabili
Taifa na kufanya uchambuzi ili kubainisha kiini cha matatizo haya.
Uchambuzi uliofanywa ulidhihirisha mambo makubwa matatu.
Kwanza, ni kwamba matatizo ya kiuchumi yanayoikabili nchi yetu
si ya kipekee kwa Tanzania bali ni matatizo yaliyozikumba nchi
zote, zisizoendelea na hata zile zilizoendelea, zilizoamua kujenga
ujamaa na zile zilizoamua kujenga ubebari.

28. Jambo la pili lililodhihirika ni kuwa baadhi ya sababu za matatizo


yetu ya kiuchumi ziko nje ya uwezo wetu. Mfumo wa biashara ya
kimataifa ulivyo unazikandamiza na kuzinyonya nchi changa kama
Tanzania. Kwa mujibu wa mfumo huu wa biashara ya kimataifa nchi
za viwanda zinajipangia bei za bidhaa za viwanda vyao na kutuuzia
sisi na wakati huo huo nchi hizo hupanga wao bei za mazao ya
kilimo tunayozalisha sisi na kuwauzia. Vile vile Tanzania haina
kauli na bei za mafuta tunayoyaagiza toka ngambo.
64

MIONGOZO MIWILI

29. Sasa, bei za mafuta na bei za bidhaa za viwanda vya nchi zilizoendelea
zimepanda sana katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Tanzania
sasa inawajibika kutumia asilimia sitini ya mapato yake yote ya
fedha za kigeni kununulia mafuta ambapo mwaka 1972 ilitumia
asilimia kumi ya fedha za kigeni kununua kiasi hicho hicho cha
mafuta. Wakati huo huo, kwa kutumia mbinu za kupandisha
bei za bidhaa zao za viwanda na kushusha bei za mazao ya nchi
changa, nchi zilizoendelea zimefaulu kuupunguza kabisa uwezo
wetu wa kununua bidhaa za viwanda vyao zinazohitajika sana na
nchi changa. Kwa mfano, miaka kumi iliyopita Tanzania iliweza
kununua trekta moja toka ngambo kwa thamani ya tani tano za
chai iliyouzwa ngambo. Leo Tanzania inahitaji tani kumi na saba za
chai ili kununua trekta la aina ile ile. Hali hii lazima iwe na matokeo
mabaya kwa uchumi wa Taifa letu.
30. Nchi yetu pia imepatwa na matatizo ya ndani ambayo pia
tusingekuwa na uwezo wa kuyazuia na yote yameathiri hali
yetu ya uchumi. Matatizo hayo ni pamoja na vita vya kujihami
tulivyolazimika kupigana dhidi ya majeshi ya uvamizi wa Iddi Amin,
mafuriko makubwa ya 1978/79 na hali ya ukame katika baadhi ya
mikoa.

31. Jambo la tatu lililodhihirika vile vile ni kwamba sisi wenyewe


kama taifa hatukutumia kwa kiasi cha kutosha nguvu za Chama,
Serikali na za wananchi katika kutatua matatizo ya uchumi ambayo
ufumbuzi wake tuna uwezo nao.
32. Jambo la kwanza linahusu kilimo kwa jumla. Pamoja na kuwa bei za
mazao yetu tuyauzayo ngambo imekuwa ikishuka, mapato ya fedha
za kigeni kwa Taifa kutokana na mazao yanategemea pia kiasi taifa
linachozalisha na kuuza. Taifa linalozalisha kidogo litauza kidogo
na kupata fedha chache za kigeni. Likizalisha mazao kwa wingi na
kuuza litapata fedha za kigeni zaidi. Lakini, utoaji wa karibu mazao
yetu yote ya biashara umepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Ni dhahiri kuwa hata kama tumekuwa na matatizo ya mafuriko
na ya ukame hapa na pale, kushindwa kwetu kuongeza utoaji
MIONGOZO MIWILI

65

wa mazao ya biashara na chakula kunatokana pia na kushindwa


kwetu kuwaongoza wananchi kwa maandalizi thabiti, mipango na
msukumo katika kilimo.

33. Pili kuna suala la utengenezaji mali wa kijamaa. Laiti kama Chama
kingeongoza, kusimamia, kuhimiza na kusaidia utekelezaji wa
Ujamaa Vijijini vizuri tangu Azimio la Arusha hadi sasa, tungeweza
kuwa na sekta kubwa ya ujamaa katika kilimo vijijini ambavyo
ingetuwezesha kutoa ziada ya mazao ya chakula na biashara kuliko
ilivyo sasa. Kama wastani wa ekari za ujamaa wa kila kijiji nchini
ungekuwa angalau ekari mia kwa kila kijiji wakati huu basi sekta
ya Ujamaa vijijini katika kilimo ingekuwa na ekari zipatazo laki
sita. Ekari laki sita za ujamaa zingeweza kuongeza ziada ya mazao
yanayotolewa na Taifa kwa kiasi kikubwa.

34. Na tatu ni kuwa jitihada zetu za kuunda na kupanua sekta ya umma


haikuambatana na jitihada ya kutosha ya kuelimisha, kuwaandaa
na kuwajenga wafanyakazi na viongozi wa kazi katika misingi
ya kufanya kazi kwa nidhamu na ari, misingi ya uzalendo na ya
uaminifu kwa umma. Hali hii imeathiri utengenezaji mali na utoaji
huduma wa sekta hii. Viwanda vingi nchini havitoi mali kwa kadri
ya uwezo vilio nao na pia mali nyingi ya umma hupotea kutokana
na vitendo vya wizi, uzembe na ubadhirifu. Upungufu wetu katika
kujenga maadili ya kijamaa miongoni mwa wafanyakazi na wakuu
wa kazi ni moja ya sababu zilizofanya viwanda na mashirika yaliyo
mengi nchini yasitoe mchango wa kutosha katika kuujenga uchumi
wa taifa.

35. Lakini maadui wa ujamaa wa nje na wa ndani wanaeneza kuwa


matatizo yetu yanatokana na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Maadui hawa wa ujamaa wanajua kuwa wayasemayo si kweli,
lakini kwao wao kukashifu ujamaa ni sehemu muhimu ya mbinu
zao za vita vya ghiliba dhidi ya Ujamaa. Kwani ukweli unaojitokeza
wazi wazi ni kuwa baadhi ya matatizo yetu ya uchumi yanatokana
na kutotekeleza kwa dhati Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea
vijijini na katika sekta ya umma tuliyoianzisha. Zaidi ya hivyo,
66

MIONGOZO MIWILI

wakati mwingine katika miaka kumi na minne tangu Azimio la


Arusha, Chama, Serikali na vyombo vyake vimetumika kukuza
sekta ya kibepari nchini katika viwanda, biashara, usafirishaji,
ujenzi na kadhalika na ubepari huo uliopanuka katika kipindi hiki
umeimarisha vitendo vya kuivuruga na kuidhoofisha sekta yetu ya
Umma.

36. Aidha, kuna matatizo ya kijamii kama vile kuongezeka kwa rushwa,
hujuma za kiuchumi, wizi, ujambazi na uharibifu wa mali ya
umma, mambo ambayo yanatupunguzia nguvu zetu za kiuchumi
na kudhoofisha dhamira ya umma ya kujenga ujamaa. Haya yote
yamo katika uwezo wa Chama, Serikali na wananchi kuyapiga vita
na kuyashinda.

37. Hivyo, katika kufanya uchambuzi wa kujikosoa, Halmashauri Kuu


ya Chama ya Taifa ya Mei, 1981 ilikiri kuwa pamoja na kwamba
Chama chetu, tangu TANU na ASP hadi sasa Chama Cha Mapinduzi,
kimepata mafanikio na ushindi wa kihistoria katika nyanja
mbalimbali za mapambano, ni muhimu kukubali pia kwamba
kimeonyesha upungufu usiokatalika, kama chombo kikuu cha
uongozi wa Taifa na hasa chombo cha uongozi wa harakati za kujenga
Ujamaa na Kujitegemea nchini. Kukiri upungufu huu si kitendo cha
kujidhoofisha bali ni kitendo cha kujiamini na kujiimarisha.

(2) Wana CCM ndiyo askari wa mstari wa mbele wa


mapambano ya kujenga Ujamaa

38. Uchambuzi wa kujikosoa umedhihirisha kuwa kwa miaka mingi


Chama hakikuthamini ipasavyo uanachama na kuitambua nafasi ya
wanachama katika harakati za ujenzi wa ujamaa na wa Taifa kwa
jumla. Chama cha kijamaa kama CCM ni chombo cha kuongoza
mapambano ya ujamaa nchini. Ni kweli kuwa ujamaa kimsingi
ni siasa ya Wakulima na Wafanyakazi na kwamba utajengwa na
wafanyakazi katika umoja wao wa kitabaka. Lakini ni kweli pia
kwamba bila ya wapiganiaji ujamaa wa mstari wa mbele, bila ya
kikosi cha askari wa mstari wa mbele wa harakati za ujamaa, lengo
MIONGOZO MIWILI

67

la kujenga ujamaa haliwezi kufikiwa. Kikosi hicho cha wapiganiaji


ujamaa wa mstari wa mbele ni wanachama wa Chama Cha
Mapinduzi.

39. Vyama vyetu asilia, ASP na TANU, vilifaulu kuwawezesha


wanachama wake kuwa kikosi thabiti cha mstari wa mbele cha
kupigania uhuru. Wanachama hao kwa jumla walijitolea mhanga
kwa ajili ya mapambano ya uhuru wa nchi yao, mapambano yao
waliyaweka kabla ya maslahi yao binafsi na mengine yoyote.
Tutakuwa tunajidanganya tukisema kuwa wanachama wote wa
Chama cha Mapinduzi na pia wanachama wote wa TANU na ASP
katika miaka kadhaa kabla ya kuundwa kwa CCM, walikuwa kikosi
kinachotimiza sifa hizo kwa upande wa lengo la kujenga Ujamaa.
Mapambano ya uhuru yalikuwa ya wenyewe, wanaTANU na wana
ASP wa enzi hizo, na kuwa wananchi waliobaki walielimishwa,
walihamasishwa na walishirikishwa katika mapambano ambayo
chimbuko la vuguvugu lake lilikuwa msimamo na vitendo vya
wanachama. Katika maana hiyo, mapambano ya kujenga Ujamaa
Tanzania lazima yawe na wenyewe.

40. Hali hii haikuzuka siku moja bali ni matokeo ya msimamo na


vitendo vya miaka mingi. Ilianza tangu baada ya uhuru, wakati
viongozi wa ngazi ya taifa, Mkoa na Wilaya hawakuipa uzito kwa
vitendo nafasi ya mwanachama katika mapambano yetu. Karibu
viongozi wote tulishughulika na mikutano ya hadhara, mikutano
ya wananchi kwa jumla bila ya kujali kukutana na wanachama.
Viongozi wengine wa Chama tulilemazwa na umangi meza na
wengine hata kufikiri wangeimarisha utekelezaji wa shughuli
za Chama kwa njia ya vyombo vya habari tu. Ingewezekana kwa
viongozi kuhakikisha kuwa kila baada ya mikutano ya hadhara ya
wananchi wote, ambayo pia ina umuhimu wake, wanakutana na
wanachama wenzi wao ili kuulizia juu ya hali ya Chama mahali
hapo na pia kuonyesha kuwa uanachama ulikuwa na maana na
uzito maalum ambao viongozi wanautambua. Lakini hatukufanya
hivyo na matokeo yake ni kwamba fikra zilijengeka kuwa uananchi
ulikuwa unatosha kabisa.
68

MIONGOZO MIWILI

41. Kwa wanachama walio wengi wa CCM kutokuwa kikosi cha


mstari wa mbele cha kupigania ujamaa na kutojiona kuwa ndiyo
wenye mapambano ya kujenga ujamaa kumetokana pia na ukweli
kuwa Chama hakikuwa na mpango wa kuwajenga na kuwaandaa
wanachama kwa madhumuni hayo. Mwamko wa kitaifa na wa
kizalendo ulikuwa rahisi kumpata Mwafrika wa Tanzania wakati
wa ukoloni maana adui, ambaye ni mtawala wa kigeni, alikuwa
anaonekana wazi wazi na hivyo suala la fedheha ya kutawaliwa
ilikuwa rahisi kulieleza na rahisi pia kueleweka na kumkera mtu.
Uadui wa mfumo wa kibepari ni mgumu zaidi kuuelezea mpaka
ueleweke na kumtia mtu mori ya kuuchukia na kuukataa. Ubepari au
unyonyaji si suala la rangi ya mtu na hivi sasa baadhi ya wanyonyaji
nchini ni Waafrika wenzetu. Kwa hiyo, wanachama wa Chama cha
kujenga ujamaa wanahitaji zaidi maandalizi ili waelewe uzito wa
mapambano na kupata mbinu za kuongoza mapambano ya umma
kwa vitendo. Viongozi wanahitaji maandalizi ya hali ya juu zaidi.

42. Hali hii ambapo wanachama na viongozi kwa jumla waliachiwa


wajitetee wenyewe (na wengine wametimiza wajibu wao kwa sifa)
iliimarisha hali iliyozungumziwa hapo awali kwamba uanachama
na uananchi ulikuwa sawa tu na hivyo suala la nani amwongoze
nani lilijitokeza: maana kama kuongoza ni kuonyesha njia basi
haikuweza kuwa dhahiri wakati wote kuhusu nani aijuaye njia, ni
mwanachama wa CCM au wananchi kwa ujumla, ni viongozi wa
CCM au wanachama.

43. Vyuo vya chama ambavyo ndivyo ingebidi viwe mahala pa kuandaa
wanachama hasa viongozi wa Chama vimeendelea kuwa vyuo
vya Elimu ya Siasa kwa jumla. Ni kweli kuwa Chama chochote cha
kijamaa halisi lazima kiwe na mipango thabiti ya kutoa elimu ya
siasa ili kuwahamasisha wananchi kwa jumla na hasa makundi ya
taasisi mbalimbali kama vyuo, shule, majeshi, vijana, wafanyakazi,
wakuu wa kazi na kadhalika. Lengo la elimu ya siasa kwa taasisi hizi
ni kuinua mwamko wao wa siasa na kuwapa wahusika mwelekeo
wa kisiasa kwa kulingana na shughuli zao katika nchi. Lakini
wanachama wanahitaji mafunzo ya siasa ya Chama ili kuongeza
MIONGOZO MIWILI

69

upeo wao wa kuielewa siasa ya ujamaa, mafunzo ya mbinu za


kushiriki na kuongoza umma mahali walipo katika harakati za
kujenga ujamaa na mafunzo ya kuwapa uwezo wa kueneza na
kutetea siasa ya Chama. Mafunzo haya hutolewa na vyuo vya Chama
kwa utaratibu na malengo yaliyo wazi.

(3) Umuhimu wa nadharia sahihi ya Ujamaa

44. Pamoja na upungufu wetu kama Chama kuhusu nafasi ya uanachama


na wanachama katika mapambano yetu ya kujenga ujamaa kuna
suala linalohusu umuhimu wa nadharia sahihi ya Chama. Chama
ni muungano wa watu wanaokubaliana juu ya lengo katika jamii na
namna ya kulifikia. Kinachowaunganisha ni fikra zao, itikadi yao,
inayohusu jinsi gani shughuli za jamii nchini ziendeshwe na kwa
maslahi ya nani. Ni muhimu kusisitiza kuwa kinachowaunganisha
wanachama ni itikadi, fikra na falsafa yao ya siasa.

45. Lakini masuala ya falsafa, itikadi na fikra ni masuala ya nadharia.


Hivyo suala la nadharia ya Chama ni suala la msingi kabisa kwa uhai
wa Chama, kwa maendeleo ya mapambano ya Chama, kwa malengo
na mbinu za mapambano hayo na kwa umoja, nguvu na usahihi wa
vitendo vya Chama na vya wanachama.

46. Chama chetu ni miongoni mwa vyama vichache katika Afrika


ambavyo vimefaulu kubuni nadharia ya ujamaa iliyo sahihi, wazi
na ya kiwango cha juu. Nadharia hiyo ya Chama inajidhihirisha
yenyewe katika Katiba, Azimio la Arusha, Mwongozo na maandishi
mengine muhimu ya Chama. Nadharia hii ya siasa yetu ya Ujamaa
na Kujitegemea imetujengea msingi wa uelewano, umoja na
ushirikiano wa aina mpya katika ujenzi wa taifa na kutufanya
tueleweke na wengi kimataifa, jambo ambalo limetupa sifa na
heshima duniani kote.
47. Tumetamka hapo awali katika kujikosoa kuwa siku za nyuma
tumeonyesha upungufu kwa kutokuwa na mipango thabiti ya
kuwaandaa wanachama na hasa viongozi. Upungufu huu umekuwa
na matokeo kwa upande wa nadharia. Pamoja na nadharia fasaha
70

MIONGOZO MIWILI

iliyomo katika maandishi makuu ya Chama, pamoja na jitihada na


uwezo wa Mwenyekiti wa Chama Mwalimu J. K. Nyerere, wa kufafanua
na kuendeleza nadharia ya Chama, viongozi wengi tumetosheka na
kiwango kisichoridhisha cha nadharia. Wengine tumediriki hata
kuipiga vita nadharia na kupuuza umuhimu wa kujifunza siasa na
nadharia ya Chama, kuinua uwezo wetu wa uchambuzi wa masuala
mbalimbali ili kuweza kutetea na kueneza siasa ya Chama kwa hoja,
uchambuzi na ufafanuzi ulio wazi na sahihi.

48. Ni muhimu kusisitiza kuwa pamoja na maandishi ya Chama yaliyo


sahihi na ya kimapinduzi, pamoja na upeo na uwezo mkubwa alionao
Mwenyekiti, Mwalimu J. K. Nyerere, wa kutafakari na kuchambua
masuala mbalimbali kwa kina na ufasaha au wa kiongozi mwingine
yeyote, lakini kwa kuwa Chama ni wanachama na viongozi wote
kwa pamoja katika mshikamano wao wa nadharia na vitendo, basi
ni hatari kwa maendeleo ya Chama na ya siasa yake ya ujamaa
kuiachia hali ambapo kiwango cha kuielewa nadharia ya Chama
kinahitilafiana mno kati ya wana CCM na hata kati ya viongozi wa
ngazi moja ya uongozi.

49. Chama chetu kinaongoza mapambano ya Watanzania katika


mazingira ya kimataifa yaliyo magumu na yenye sura nyingi katika
siasa, uchumi na jamii. Kuweza kuliongoza Taifa katika mazingira
haya magumu, Chama kinahitaji kuwa na uwezo wa juu wa kuyaelewa
mazingira hayo ambayo hayawezi kueleweka bila ya uchambuzi wa
kina na nyenzo za kufanyia uchambuzi huo. Uchambuzi huu lazima
ukiwezesha Chama kufichua mvutano wa maslahi uliopo baina
ya mataifa kufichua uhusiano halisi wa nguvu kati ya ubeberu na
ubepari wa dunia kwa upande mmoja na nguvu za ujamaa kwa
vuguvugu la ukombozi wa taifa kwa upande mwingine, na kufichua
uhusiano halisi uliopo kati ya mataifa ya viwanda na mataifa yasiyo
ya viwanda. Uchambuzi wa aina hiyo ndio utakaokiwezesha Chama
kuliongoza Taifa kwa usalama kimataifa na kwa maslahi yetu.
50. Wakati huo huo hali ya ndani ya Tanzania imebadilika sana. Uchumi
wa taifa, huduma na jamii yenyewe yote imekuwa na kupanuka.
MIONGOZO MIWILI

71

Kuielewa vema jamii ya Tanzania ya leo kunataka uchambuzi wa hali


ya juu pia. Uchambuzi huu ukiwezeshe Chama kuielewa migongano
ya maslahi ya tabaka ambayo imejitokeza nchini. M i g o n g a n o
hii ina mizizi yake katika mgongano wa msingi kati ya ujamaa na
ubepari, kati ya maslahi ya wakulima na wafanyakazi kwa upande
mmoja, na ya ubinafsi ubwanyenye na ubepari ambao umekuwa
ukijengeka tangu Azimio la Arusha kwa upande mwingine. Kwa
hiyo, ili Chama kiweze kuendelea kuongoza mapambano ya kujenga
ujamaa ni muhimu kuwa na uwezo wa kufanya uchambuzi sahihi
wa hali ya jamii yetu.

51. Jambo linalosisitizwa hapa ni kuwa kwa Chama Cha Mapinduzi


kuongoza ipasavyo siasa ya ndani na ya nje ya nchi yetu ni muhimu
kwa viongozi wa ngazi zote na pia wanachama kuwa na uwezo
wa hali inayoridhisha ya nadharia kama silaha katika kutekeleza
jukumu hilo. Hivyo, ni jambo la umuhimu wa kwanza kwa viongozi
na wanachama kujiendeleza katika nadharia ya siasa ya Chama.
Kwa kiongozi au mwanachama wa CCM kupuuza, kudharau au
kukataa kujiendeleza katika nadharia kwa visingizio vyovyote ni
msimamo wa uhasama dhidi ya maendeleo ya Chama.

52. Ujenzi wa ujamaa si lelemama bali ni mapambano, mapambano ya


kudumu dhidi ya ubepari na unyonyaji, dhidi ya wapinga maendeleo
na wababaishaji wa kisiasa, dhidi ya wahujumu uchumi, majambazi,
wezi, wazururaji na wazembe. Msimamo sahihi wa mapambano
unaotokana na nadharia sahihi ya ujamaa ungelituepusha na maamuzi
na vitendo ambavyo vimerahisisha kuoteshwa kwa mizizi ya ubepari,
kinyume cha msimao wa mapambano dhidi ya ubepari. Leo ubepari
una vishawishi vingi zaidi nchini kuliko ulivyokuwa kabla ya Azimio
la Arusha kwa sababu pamoja na kwamba sasa tuna sekta kubwa
ya umma lakini kutokana na udhaifu wa kutopambana nao, ubepari
umefaulu kujipanua na kujipenyeza hata ndani ya sekta yenyewe
ya Umma. Na ndiyo maana ubepari sasa unathubutu kujitokeza
hadharani kuukashifu ujamaa, kubabaisha baadhi ya viongozi na
kututaka tubadilishe siasa yetu.
72

MIONGOZO MIWILI

53. Upungufu wa nadharia ya ujamaa unaweza kuathiri maslahi ya Chama


kwa namna nyingine. Chama cha kijamaa kama CCM ni chombo cha
uongozi, si chombo cha amri na utawala wa mabavu. Kinaongoza
kwa kuelimisha, kuelewesha, kushauri, kushawishi, kushirikisha na
kuelekeza na nguvu yake kubwa inatokana na kukubalika kwake na
umma, mshikamano wa wanachama wake na fikra sahihi za siasa
yake inayolingana na maslahi ya Umma, mshikamano wa wanachama
wake na fikra sahihi za siasa yake inayolingana na maslahi ya Umma.
Ili kutimiza jukumu lake la uongozi kinahitaji nguvu ya hoja siyo
hoja ya nguvu. Hivyo, kiwango cha juu cha nadharia kinahitajika
kwa viongozi wa ngazi zote na hata wanachama ili kuwaelimisha na
kuwashawishi wasio wanachama, kuitetea siasa dhidi ya hujuma za
maadui, kufafanua masuala mbalimbali na kujibu hoja za wanachama
au wananchi kwa jumla. Kufanya ufafanuzi usioridhisha, kujibu hoja
halali kwa juu juu au kuwaita waulizao maswali wapinzani wa Chama
kama ifanyikavyo wakati mwingine hakujengi bali hudhoofisha
Chama.

(4) Mshikamano wa nadharia na vitendo

54. Katika kufanya uchambuzi wa kujikosoa katika Chama ni muhimu


kuzingatia suala la uhusiano uliopo, mshikamano uliopo, kati ya
nadharia na vitendo. Nadharia ina kazi ya kuangaza na kuongoza
vitendo. Lakini kwa kuwa lengo la ujamaa ni kuibadili dunia, kujenga
misingi mipya ya uchumi, kuleta mfumo mpya wa jamii basi vitendo
vya kijamaa ndicho kipimo cha ujamaa kwa Chama na ujamaa kwa
Wanachama.

55. Suala hili la mshikamano wa nadharia na vitendo, la kutenda


mapinduzi, linatusaidia kuelewa kwa undani mwenendo wa
ujenzi wa ujamaa kama linavyohusu uamuzi wa kutaifisha na kazi
ya kukibadili kilichotaifishwa kiwe chombo cha ujamaa. Kazi ya
kuunda vyombo vya umma kama mabenki, viwanda, mashirika
ya biashara, mashamba ya Taifa ni kazi ya kujenga ujamaa. Lakini
kazi nyingine muhimu ya kijamaa ni kuhakikisha kuwa ujamaa
unajengwa ndani ya vyombo hivyo. Tatizo letu katika siku za
MIONGOZO MIWILI

73

nyuma ni kuwa hatukutilia mkazo umuhimu wa kujenga ujamaa


ndani ya vyombo vya umma na hii imerahisisha fikra na tamaa za
kibepari kuzagaa katika vyombo hivi na mwisho kutekwa nyara ili
vihudumie ubepari na ubinafsi.

56. Upungufu wa kuuelewa vilivyo uhusiano wa nadharia na vitendo katika


harakati za ujamaa unaweza kusababisha pia msimamo usio sahihi wa
kutenganisha jukumu la uongozi na utendaji au kazi. Uongozi si kazi
ingawa zipo kazi za uongozi. Hivyo, wajumbe wa vikao vya Chama ni
lazima wawe au na kazi zao za kawaida kama za ajira au kilimo ama
wawe na kazi za uongozi katika Chama, Serikali au Mashirika ya Umma.
Vinginevyo kutakuwa na watu katika Chama ambao si wakulima wala
si wafanyakazi na huu ndio mwanzo wa kujenga kundi la wababaishaji
wa kisiasa, jambo ambalo ni hatari sana kwa harakati za ujamaa. Tabia
ya kutenganisha uongozi na utendaji imeathiri maendeleo ya Chama
kwa msukumo, usimamizi na utekelezaji maana kati ya uamuzi na
utendaji kumekuwa hakuna kiungo.

57. Tatizo hili la kutenganisha uongozi na utendaji linaweza pia


kukizorotesha Chama kwa kukifanya kisahau kuwa chenyewe
vile vile ni mtendaji na kwamba kitapimwa kwa vitendo vyake
kama Chama. Katika maana hiyo Halmashauri Kuu ya CCM ya Tawi
ipimwe na vikao vya juu kwa utekelezaji wake wa Siasa ya Chama;
kama wanachama wake wako mstari wa mbele kwa ujamaa, kama
wanashiriki katika shughuli za kujitolea, kama ni wafanyakazi hodari,
kama kijiji chao kina maendeleo ya kijamaa na kadhalika. Vivyo hivyo
kwa kamati ya utendaji ya Wilaya, Mkoa na Taifa. Kwa hiyo, pamoja
na kushughulikia uongozi wa serikali, Jumuiya na vyombo vingine,
Chama kina kazi ya kujijenga chenyewe ili kujipa uwezo wa kutosha
wa kuongoza Umma na vyombo vyake, ili kutekeleza majukumu yake
ambayo ndiyo sababu ya kuwepo kwake.

(5) Kujikosoa na kukosoana ni silaha ya Mapinduzi

58. Kuna mambo mawili tuliyojifunza ambayo ni muhimu pia


kuyazingatia. La kwanza linahusu suala la kukosoa, kujikosoa
74

MIONGOZO MIWILI

na kukosoana kama njia ya kukijenga na kukiimarisha Chama


na wanachama. Ni kweli kuwa katika TUJISAHIHISHE Mwalimu
anasisitiza jambo hili na kwamba Katiba ya CCM inatamka waziwazi
juu ya umuhimu wake. Lakini ni kweli pia kuwa hatujaijenga tabia
hii ipasavyo. Mara nyingi tumependelea kuteteana, kufichiana
makosa na hata kutafuta visingizio visivyo na msingi. Neno kuleana,
kwetu sisi (ingawa kuna malezi mema na mabaya) limechukua
nafasi ya kukosoana. Wanachama wenye upungufu husaidiwa
kama wanakosolewa ili wajirekebishe. Lakini hatua za nidhamu
wakati mwingine zimechukuliwa bila ya mhusika kuelezwa wazi
wazi upungufu wake ili ajirekebishe na pia wananchi wameachiwa
wabuni wenyewe sababu.

59. Suala la kukosoa, kujikosoa na kukosoana lina sura kadhaa.


Kwanza linataka wanachama na viongozi kuwa tayari kusema
kweli katika vitendo vyao na kukubali kuambizana ukweli. Pili,
linataka wanachama na hasa viongozi wawe tayari kukosolewa
bila kuhamaki na inapobidi kukubali kujirekebisha. Tatu ni kuwa
Chama chenyewe katika vikao vyake vya ngazi mbalimbali kuwa na
utaratibu wa kujikosoa.
60. Sura hii ya tatu ni muhimu sana kwa mafanikio ya utekelezaji
wa siasa ya Chama. Kuongoza ni kutoa maamuzi yanayohusu
utekelezaji wa siasa. Kujikosoa kama Chama ni kuwa na utaratibu
wa kuyarudia maamuzi ya nyuma, kuona jinsi yalivyotekelezwa na
kupima matokeo ya utekelezaji huo kwa kuzingatia nia ya Chama
katika kutoa uamuzi huo. Kama makosa yamefanyika katika
utekelezaji basi ni muhimu kutafuta sababu za makosa hayo na
kuchukua hatua za haraka za kuyarekebisha. Makosa pia yanaweza
kutokana na uamuzi wenyewe kutokuwa sahihi. Katika hali hiyo,
itabidi uchambuzi ufanywe ili kubainisha kiini cha upungufu wa
uamuzi huo na kuchukua hatua za kurekebisha mambo. Kama kuna
mafanikio basi ni nafasi kwa Chama kuzingatia mbinu zilizotumika
kwa manufaa ya utekelezaji wa baadaye. Hivyo utaratibu wa
kujikosoa kwa Chama ukitekelezwa kwa dhati ni shule kubwa ya
ujenzi wa Ujamaa.
MIONGOZO MIWILI

75

61. Ni dhahiri kuwa mapinduzi yetu yangekuwa yamepiga hatua


kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa kama tungezingatia utaratibu huu
wa harakati za kujenga Ujamaa. Mfano mmoja unatosha kuelezea
ukweli wa mambo. Msimamo wa Chama juu ya UJAMAA VIJIJINI
uliopitishwa na Mkutano Mkuu wa Chama, Mwanza, mwezi Oktoba,
1967. Tangu wakati huo wananchi wameitikia mwito huo kwa njia
na mafanikio mbalimbali. Lakini hadi sasa, miaka kumi na minne
baadaye, hakuna kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichokaa
na kupima maendeleo ya Ujamaa vijijini, kubainisha kilichofanya
kuwa mpaka sasa sekta ya ujamaa vijijini ikawa bado finyu na
kutafuta malengo na mbinu mpya za kuleta msukumo wa ujenzi
wa ujamaa vijijni. Ni dhahiri kuwa Chama kingalifanya hivyo kila
mwaka na baada ya kila miaka mitano, kiwango cha ujamaa vijijini
na nchini kingelikuwa cha juu kuliko kilivyo sasa na kwamba Chama
kingalikuwa na hazina kubwa zaidi ya mbinu za kuongoza harakati za
ujamaa. Na kwa kuwa ujamaa vijijini kwanza kabisa ni utengenezaji
mali, basi maendeleo ya vijijini hii leo yangekuwa yamepiga hatua
kubwa na kwamba huenda matatizo ya sasa ya upungufu wa ziada ya
mazao nchini yangelikuwa yamepatiwa ufumbuzi wake.
62. Msimamo wa kujikosoa ni msimamo wa kimapinduzi. Unazingatia
upungufu wa binadamu na papo hapo kutambua uwezo wa
binadamu wa kufanya vizuri na zaidi mradi tu anajipa nafasi ya
kujifunza, kujirekebisha na kujaribu tena na tena. Kwa Chama
cha kijamaa kama Chama cha Mapinduzi hakuna kinachoweza
kuchukua nafasi ya kujikosoa.

(6) Umuhimu wa kuzungumzia jinsi ya kutekeleza

63. Jambo la pili tulilojifunza katika kujikosoa na ambalo linahitaji


kuzingatiwa linahusu methodolojia ya kuunganisha uamuzi wetu
na utekelezaji. Tumekuwa na tabia ya kuzungumzia suala na
kufanya uamuzi. Baada ya hapo tunaachia utekelezaji ufanyike kwa
kutegemea hisia, uwezo na msimamo wa wanaohusika. Kwa kawaida,
suala la kuzungumzia namna ya kutekeleza, kuzungumzia mipango
76

MIONGOZO MIWILI

na mbinu za utekelezaji, hatukuwa na tabia ya kulishughulikia hasa


kitaifa. Huu ni upungufu katika Chama maana namna ya kutekeleza
uamuzi, mipango na mbinu za utekelezaji ni sehemu muhimu ya
harakati za kutafsiri fikra (uamuzi) katika vitendo na ndiyo njia
iliyo wazi ya kuhakikisha mafanikio ya utekelezaji.

64. Tabia ya kutozungumzia namna ya kutekeleza mipango na mbinu


za utekelezaji husababisha matatizo katika Chama. Tatizo lililo
dhahiri ni kuwa viongozi mmoja mmoja au vikao vya mikoa, wilaya
na vijiji vinaachiwa vibuni njia za utekelezaji kwa kutegemea
aonavyo kiongozi mhusika au kikao kihusika. Pale ambapo kiongozi
mhusika ana msimamo thabiti wa chama au wajumbe wa kikao
ni watu makini na wenye uwezo na busara, utekelezaji unaweza
kufanyika vizuri. Lakini kuna pia sehemu nyingine katika nchi
yetu na kwa vipindi mbalimbali ambako viongozi wamelazimisha
utekelezaji kinyume cha matazamio ya Chama na wananchi na
mara nyingine hata kusababisha usumbufu usio wa lazima kwa
wananchi. Ufafanuzi wa namna ya kutenda na mbinu za utekelezaji
unajenga nidhamu katika utekelezaji, unarahisisha usimamizi wa
shughuli za Chama katika ngazi zote na unajenga na unawezesha
kutumika kwa utaratibu wa kujikosoa na kukosoana. Zaidi ya hayo,
unaimarisha umoja na nguvu za Chama kama chombo cha kutenda,
yaani kuongoza mapinduzi ya kujenga Ujamaa Tanzania.
65. Mwongozo mpaka hapa umegusia historia ya mapambano ya taifa
letu katika vipindi mbalimbali, umechambua mafanikio makubwa
tuliyoyapata katika kutekeleza siasa ya Chama ya Ujamaa na
Kujitegemea na kumalizia kwa kufanya uchambuzi wa kujikosoa
katika Chama ili kwa kuzielewa nguvu na upungufu wa Chama
chetu tuweze kujizatiti kwa kuikabili kazi kubwa iliyo mbele yetu.
66. Historia ya nchi yetu tangu kuzaliwa kwa TANU na ASP ni historia ya
mapambano makali dhidi ya ukoloni na ubeberu na tumefanikiwa
kupata ushindi mwaka hadi mwaka. Hali yetu ya uchumi na ya jamii
ni ngumu kuliko ambavyo imewahi kuwa tangu tupate uhuru. Huko
nyuma tulishinda katika mapambano yetu kutokana na umoja wetu
MIONGOZO MIWILI

77

wa kitaifa, usahihi wa siasa yetu na uongozi bora wa Chama. Leo


na katika siku za usoni tutahitaji umoja imara zaidi, siasa sahihi na
uongozi bora wa chama. Lakini katika kipindi hiki ambapo ubepari
na ubeberu wa dunia umejitokeza hadharani kwa kampeni na njama
za kuhujumu ujamaa na kutaka kulibana Taifa, wakati ambapo
vibepari na vibwanyenye vya humu nchini vimeonyesha dhahiri
uhasama wao dhidi ya maslahi ya wakulima na wafanyakazi, umoja
wa sasa lazima usimame juu ya misingi iliyo wazi na sahihi, misingi
ya ujamaa; kwa hiyo ni umoja wa wakulima na wafanyakazi na wale
wote wanaounga mkono kwa vitendao ujenzi wa ujamaa nchini.

SEHEMU YA TATU

KUJENGA MSINGI WA UCHUMI WA UJAMAA


WA TAIFA LINALOJITEGEMEA
67. Lengo kuu la mapinduzi ya Tanzania ni kujenga nchi ya ujamaa
ambamo unyonyaji wa mtu na mtu utakuwa umetokomezwa,
ambamo uchumi wa taifa utakuwa unamilikiwa na kudhibitiwa na
umma wa wakulima na wafanyakazi washirika na ambamo uhusiano
wa watu katika jamii utakuwa ni wa udugu na kushirikiana kwa
maendeleo ya wote na ambamo kazi imepewa hadhi ya kuwa wajibu
wa kila mtu.

68. Uamuzi wa kujenga ujamaa Tanzania ni uamuzi wa kimsingi na


kihistoria na haubadiliki. Chama kilijua tangu mwanzo kuwa kujenga
ujamaa hakungekuwa mteremko bali ni mapambano magumu dhidi
ya ubepari na unyonge wa humu humu ndani na dhidi ya njama za
ubeberu wa dunia. Na isitoshe, Chama kilijua tangu mwanzo kuwa
kujenga ujamaa ni pia mapambano dhidi yetu wenyewe katika
ubinafsi na upungufu wetu wa aina mbalimbali. Harakati za miaka
kumi na minne tangu Azimio la Arusha zimetuthibitishia ukweli huu.
69. Mapambano ya kutekeleza siasa ya Ujamaa ya Chama katika miaka
kumi na minne tangu Azimio la Arusha yametuwezesha kufanya
mabadiliko ya kimsingi katika uchumi wa nchi yetu. Kabla ya Azimio
78

MIONGOZO MIWILI

la Arusha uchumi wetu ulikuwa na mfumo wa kikoloni mamboleo


kwani benki, bima, biashara ya nje yote yalikuwa matawi tu ya
makampuni ya kibepari ya ulaya na marekani wakati mazao ya
kilimo cha biashara yaliwekewa lengo la kutumikia viwanda vya
kibepari vya nchi za ngambo.

70. Kutaifishwa kwa benki, bima na kampuni za biashara za nje za


kibepari na kuanzishwa kwa mashirika ya biashara ya ndani na ya
nje katika kutekeleza Azimio la Arusha kumeleta marekebisho ya
kimapinduzi ya mfumo wa uchumi. Hatua thabiti zimechukuliwa pia
za kuanzisha na kupanua viwanda vinavyotumia bidhaa asili za kilimo
chetu kama ngozi, pamba, katani, korosho, tumbaku, pareto, miwa na
kadhalika. Kwa upande wa kilimo hatua za mwanzo zimechukuliwa
kukielekeza kwenye mfumo wa kijamaa: sehemu kubwa ya
mashamba ya kibepari, hasa ya mkonge ilitaifishwa, mashamba
makubwa kadhaa ya Taifa ya kilimo na ya ufugaji yameanzishwa
wakati sekta ya ujamaa katika baadhi ya vijiji imeanza kushamiri.
Tanzania Visiwani, Serikali ya Mapinduzi ilitaifisha ardhi, benki,
nyumba na kuanzisha mashirika ya biashara ya nje na ya ndani na
kuanzisha viwanda vinavyotumia miwa na mbata. Hatua zote hizi
zilizochukuliwa zimetujengea msingi wa uchumi wenye mwelekeo
wa nchi ya ujamaa. Mafanikio haya yamewezekana kutokana na
kazi, ujasiri na kujitolea mhanga kwa wakulima na wafanyakazi
chini ya uongozi wa Chama.
71. Lakini, pamoja na mafanikio haya, nchi yetu hivi sasa imekumbwa
na hali mbaya ya uchumi kama vile hali hiyo ilivyozikumba nchi
zote duniani, zilizoendelea na zisizoendelea, nchi kubwa na ndogo,
za kibepari na za kijamaa. Hali hii lazima tuikabili kwa kujipa kazi
mbili ambazo zitakwenda sambamba. Kazi moja ni kutekeleza
malengo ya muda mrefu ya kujenga msingi wa uchumi wa kijamaa
wa Taifa linalojitegemea. Na kazi ya pili ni kuchukua hatua thabiti
kuanzia sasa za kujihami kiuchumi ili kuhakikisha kuwa hali
ya uchumi wetu haiendelei kudidimia na kuathiri hata msingi
tuliokwisha ujenga.
MIONGOZO MIWILI

79

72. Ni muhimu kutamka hapa kuwa siasa ya uchumi ya Chama cha


Mapinduzi ina lengo la kutosheleza mahitaji ya wananchi ya
chakula na kulipa Taifa uwezo wa kujitegemea katika mahitaji ya
maendeleo ya sasa na ya baadaye.

MWELEKEO WA MAENDELEO YA UCHUMI NA


JAMII YA MUDA MREFU

73. Chama Cha Mapinduzi kiimekwishatoa mwelekeo wa maendeleo ya


uchumi na jamii kwa miaka ishirini ijayo. MWONGOZO wa Chama
unayazingatia na kuyafanya maelekezo hayo ndiyo msingi wa
mwelekeo wake wa uchumi na wa jamii kwa kipindi hicho.

74. Kwa hiyo, Mwongozo wa Chama hautayakariri yaliyomo katika


mwelekeo wa miaka ishirini isipokuwa kusisitiza juu ya masuala
yanayohitaji mkazo maalum pia ni kutoa mwelekeo mpya pale
ambapo pana umuhimu wa kutazamwa upya na hapakushughulikiwa
na mwelekeo wa maendeleo ya miaka ishirini.

75. Mambo makubwa mawili yanastahili kutajwa katika kiwango


hiki. La kwanza linahusu kilimo. Kwa kuwa kilimo ndio msingi wa
maendeleo yetu ya sasa na ya miaka mingi ijayo, ni muhimu kwa
Chama kulitilia mkazo suala hili kwa kufanya ufafanuzi wa nafasi ya
kilimo katika maendeleo ya uchumi wa taifa na njia inayohitajika
kuhudumia maendeleo hayo. Hivyo, suala la kilimo na hasa kilimo
cha kijamaa linapewa nafasi kubwa katika mwongozo huu.

76. Jambo la pili linahusu mfumo wa upangaji wetu wa maendeleo.


Kwa kuzingatia kwamba maendeleo ya kijamaa ni maendeleo
yaliyopangwa, Chama katika kipindi kinachoanza sasa kitalitazama
kwa undani zaidi suala la upangaji wetu wa mipango ya maendeleo
kwa madhumuni ya kuimarisha na kukaza usimamizi wa utekelezaji.
Chama kitaona kama Tume ya Mipango katika sura yake ya sasa
kinatimiza makusudio ya Chama. Wakati huo huo Tume ya Bei
itafanyiwa uchambuzi ili ipatiwe nafasi yake ya kuwa chombo cha
upangaji wa uchumi badala ya kuwa chombo cha biashara kama
80

MIONGOZO MIWILI

ilivyo sasa. Sifa moja kubwa ya uchumi wa kijamaa ni kuwa ni


uchumi wa mpango tofauti na uchumi wa kibepari ambao ni uchumi
wa soko. Uchumi wetu kwa sasa ni mchanganyiko: kwa sehemu
fulani unapangwa na kwa sehemu kubwa unategemea mvutano wa
soko. Chama kitalitazama suala hili kwa undani zaidi ili kuelekeza
zaidi uchumi wetu kwenye mfumo wa uchumi wa mpango kuliko
ilivyo sasa. Nafasi ya Tume ya Mipango na Bunge katika kupanga
na kusimamia utekelezaji wa mipango itatazamwa upya. Aidha,
matumizi ya fedha za kigeni yataingizwa katika mfumo wa upangaji
mipango.

77. Kwa kuwa uchumi wa kijamaa ni uchumi wa mipango, basi


tutahitaji watu wenye taaluma ya kupanga katika taifa. Mikoa,
Wilaya na Vijiji na kwa viwango mbalimbali vya utaalamu. Hivyo
Serikali itawajibika kuwaandaa mapema iwezekanavyo wataalam
wa mipango kwa wingi. Wakati huo huo ihakikishwe kuwa upangaji
wa kinchi unapewa uzito sawa na upangaji wa kimradi ambao ndio
unaoeleweka zaidi na wataalam wetu.

A. MAPINDUZI KATIKA KILIMO NDIYO KAZI YA


UMUHIMU WA KWANZA

78. Msingi wa uchumi wa nchi yetu ni kilimo. Asilimia themanini na


tano ya Watanzania wanaishi kwa kilimo; biashara yetu na nchi za
kigeni inategemea zaidi mazao tunayoyatoa katika kilimo; viwanda
vichache tulivyonavyo nchini vinategemea mazao ya kilimo;
uwezekano wa kutoa ziada itakayowezesha nchi kugharimia
mapinduzi ya viwanda (kugharimia viwanda vya madawa) upo
katika sekta ya Kilimo.

79. Katika hali hii, uongozi na usimamizi thabiti na makini wa Chama


cha Mapinduzi uelekezwe zaidi katika sekta hii ya uchumi wa Taifa.
Kazi iliyo mbele yetu ni kuleta mapinduzi katika kilimo. Kwa kuwa
asilimia themanini na tano ya Watanzania ni wakulima wa vijijini,
basi mkazo wa mapinduzi katika kilimo lazima uwe kilimo cha
vijijini wakati mashamba ya Taifa pia yanashughulikiwa.
MIONGOZO MIWILI

81

80. Mapinduzi ya kilimo vijijini katika nchi yetu ni kilimo cha kijamaa
na cha kisasa ambacho kina sifa zifuatazo: Kwanza ni kilimo cha
mashamba makubwa ya kijamaa ya vijiji, pili ni kilimo kinachotumia
pembejeo, zana za utaalamu na tatu ni kilimo kinachotekelezwa
kwa utaratibu bora wa kazi unaoleta ufanisi.

81. Sifa moja ya kilimo cha kisasa duniani kote ni kuwa ni kilimo cha
mashamba makubwa. Tofauti iliyopo ya mashamba hayo ni katika
umilikaji. Katika nchi za kibepari mashamba hayo makubwa ni
mali ya mabepari, wakati katika nchi za kijamaa mashamba hayo
makubwa ni mali ya Taifa au ni mali ya ushirika wa wanavijiji.
Hali hiyo imeanza kujitokeza pia katika kilimo cha kisasa nchini
Tanzania.

82. Mantiki iliyokisukuma kilimo cha kibepari cha kisasa kiwe cha
mashamba makubwa ni ile ile iliyokisukuma kilimo cha kijamaa cha
kisasa kiwe cha mashamba makubwa. Kilimo cha kisasa ni kilimo
cha zana, na ukishavuka kilimo cha plau za maksai na kuingia
katika matrekta na mashine nyingine za kupandia na kuvunia,
basi ni hasara kubwa kuzitumia zana hizo katika vishamba vidogo
vidogo vya ekari kadhaa tu. Ufanisi wa hali ya juu unapatikana
wakati zana hizo zinatumika katika maeneo makubwa. Wakati huo
huo ni kuwa zana hizi za kisasa ni aghali na haiwezekani kwa kila
mkulima mwenye ekari chache kupata uwezo wa kuzinunua hata
katika nchi za kibepari. Hivyo, katika nchi za kibepari ni wakulima
wakubwa tu ndio wenye uwezo wa kumiliki zana hizi na katika
mashindano hayo, wakulima wadogo wamelazimika kutoa nafasi
kwa wakulima wakubwa. Katika nchi za kijamaa uwezekano wa
kumiliki zana hizi ni kwa kupitia Serikali (Mashamba ya Taifa) na
ushirika wa wakulima vijijini.
83. Uwezekano wa kuanzishwa kwa mashamba makubwa ya ujamaa
vijijini ni mkubwa katika Tanzania maana mafanikio yaliyopatikana
mpaka sasa katika vijiji vilivyotekeleza ujamaa vijijini yameufungua
macho umma wa Wakulima vijijini. Wakati huo huo maeneo ya
kuanzisha na kupanua mashamba ya ujamaa hayana matatizo katika
82

MIONGOZO MIWILI

sehemu kubwa ya vijiji vyetu nchini mradi tu kuna nia, mipango na


uongozi thabiti.

84. Wakulima vijijini wamepiga hatua za mwanzo katika kutekeleza


maagizo ya Siasa ni Kilimo kwa upande wa masharti ya kilimo bora
cha mazao ya chakula na mazao ya biashara. Pembejeo za viwanda
na samadi zimeanza kutumika pia. Katika siku za usoni Chama
kitawajibika kufanya mambo mawili kuendelea kuwaelimisha
wakulima juu ya umuhimu wa kutimiza masharti ya kilimo bora
na kuhakikisha kuwa serikali inakuwa na mipango thabiti ya
upatikanaji wa pembejeo na kwa bei nafuu kwa wakulima. Matumizi
ya samadi lazima yahimizwe kwa mkazo zaidi.
85. Suala la zana za kisasa ni gumu zaidi. Hivi sasa sehemu kubwa ya
kilimo vijijini inalimwa kwa jembe la mkono. Kuna maeneo yenye
mifugo mingi ambako kazi ya kilimo inaendeshwa pia na plau za
kuvutwa na maksai. Yapo pia matrekta katika baadhi ya vijiji. Lengo
la Chama katika miaka ijayo ni kumtoa mkulima kutoka kwenye hali
yake ya sasa ya kutegemea jembe la mkono na kumfikisha kwenye
kutumia zana za kisasa. Kazi hiyo, pamoja na ya kuhakikisha kuwa
matumizi ya mikokoteni yanaenea vijijini kote lazima itekelezwe
kwa nguvu zote.

86. Wakati huo huo Chama kihakikishe kuwa serikali inaagiza matrekta
toka ngambo kwa kuzingatia uwezo na uzito unaolingana na umuhimu
wa kilimo kwa maendeleo ya Taifa letu. Kupanga ni kuchagua. Hivyo,
kama kwa mfano, ni kuchagua kati ya magari madogo na matrekta,
basi uzito uwe kwenye matrekta. Lakini, kwa kuzingatia hali halisi
ya uchumi wetu (upungufu wa fedha za kigeni na kwamba hatuna
viwanda vyetu vya chuma na vya matrekta), itachukua muda wa
miaka mingi kabla ya kilimo cha trekta kuwa ndicho kilimo cha vijiji
vyetu. Kwa sasa mbinu ya kutufikisha huko siyo kungoja matrekta
bali ni kutumia majembe ya mkono na plau za maksai katika kilimo
cha kijamaa na cha binafsi vijijini ili kuongeza ziada ya mazao kitaifa
ambayo ndiyo ufunguo wa kulipatia Taifa uwezo wa matrekta zaidi
na kukuza uwezo wetu wa kuanzisha viwanda mama na vinginevyo.
MIONGOZO MIWILI

83

87. Sifa ya tatu ya mapinduzi ya kijamaa katika kilimo vijijini ni utaratibu


wa kazi wenye ufanisi. Shughuli za kijamaa vijijini huko nyuma
zimezoroteshwa pia kutokana na vijiji kutokuwa na utaratibu
mzuri wa kazi. Mara nyingi kazi za ujamaa zimefanywa holela, bila
kujali ufanisi wa kuridhisha. Chama kitawajibika kuhakikisha kuwa
unabuniwa utaratibu wa kupanga na kugawa kazi kwa mfumo
ambao utajenga nidhamu, kurahisisha utekelezaji wa majukumu,
kubainisha mchango wa kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi
kuendeleza hisia za ushirikiano na kuongeza ufanisi.
88. Lakini mapinduzi katika kilimo nchini lazima pia yaambatane
na mapinduzi ya msimamo wa serikali na vyombo vyake kuhusu
nafasi ya kilimo katika mapambano ya ujenzi wa taifa. Katika siku
za usoni, Chama kitahakikisha kuwa serikali na vyombo vyake, kwa
vitendo, vinautekeleza wajibu wake wa kuhudumia na kusukuma
maendeleo ya kilimo, kilimo cha kijamaa kikipewa nafasi ya kwanza.

89. Mapinduzi katika msimamo ni pamoja na kuupiga vita umangi meza


na mila na tabia zinazopingana na mahitaji ya kilimo cha kisasa na
pia kubuni njia bora zaidi za kuandaa wataalamu watakaohitajika
sana vijijini kama zile zilizotuwezesha kutekeleza Azimio la
Musoma kuhusu Elimu ya msingi kwa wote. Kwa kuwa kilimo
cha kijamaa ni kilimo cha mashamba makubwa, basi ihakikishwe
kuwa mafunzo ya kilimo yanazingatia pia suala la menejimenti ya
mashamba makubwa.

B. HATUA NYINGINE ZA UMUHIMU WA KWANZA


KATIKA UCHUMI
90.

Pamoja na maelekezo ya maendeleo ya miaka ishirini


yaliyokwishapitishwa na Chama, masuala yafuatayo yanahitaji
kusisitizwa:

(1) Kilimo cha umwagiliaji maji


Kilimo hiki kimepewa umuhimu wake katika mwelekeo wa muda
mrefu. Kwa kuelewa kuwa pamoja na miradi mikubwa ya kitaifa ya
84

MIONGOZO MIWILI

umwagiliaji, miradi midogo midogo ya vijijini ndiyo ambayo inaweza


kutoa matunda ya haraka, hatua za dhati zichukuliwe za kuandaa
wataalam wa fani hiyo kwa wingi nchini na ngambo na pia kutafuta
uwezekano wa kuanzisha kiwanda cha zana za umwagiliaji maji. Wakati
huo huo Chama kijizatiti barabara ili kuimudu kazi ya kuwashirikisha
wananchi, maana utekelezji wa miradi ya umwagiliaji vijijini utategemea
zaidi jasho la wananchi wenyewe kuliko matumizi ya zana za kisasa.

(2) Kilimo cha matunda na mboga


Kilimo hiki hadi sasa hakijatiliwa mkazo nchini. Licha ya mahitaji ya
chakula bora yanavyozidi kuongezeka, matunda na mboga yanaweza
kuwa mazao muhimu ya biashara ya nje kwa nchi yetu. Nchi nyingi
za Afrika ambazo hazina mazingira bora zaidi ya haya ya nchi yetu
hujipatia fedha nyingi za kigeni kutokana na matunda na mboga. Chama
kihakikishe kuwa m i r a d i ya Taifa na ya vijiji ya kilimo cha matunda na
mboga inaanzishwa kwa madhumuni ya kuwapatia wananchi matunda
na mboga za kutosha nchini kote na ziada ya kuuza ngambo. Katika
lengo maalum la kuwapatia wafanyakazi wa mijini matunda na mboga
kwa wingi, vijiji vilivyo karibu na miji mikubwa visaidiwe kuanzisha
miradi mikubwa ya vijiji ya mazao haya.

(3) Uendelezaji wa mifugo na ufugaji


Tanzania ina utajiri mkubwa wa mifugo hasa ngombe, mbuzi na kondoo.
Inakisiwa kuwa idadi ya ngombe peke yake waliomo nchini ni zaidi ya
milioni kumi. Lakini hali ya mifugo yenyewe ni duni maana wa f u ga j i
walio wengi bado wanathamini zaidi wingi wa mifugo badala ya
ubora wa mifugo. Misingi ya ufugaji wa kisasa haijafikishwa ipasavyo
kwa wananchi na aina bora za mifugo kwa ajili ya maziwa na nyama
hazijaenezwa nchini.
Katika hali hii kazi kubwa ya Chama katika fani ya mifugo itakuwa
kuhakikisha kuwa Serikali inaandaa sera ya kuendeleza mifugo nchini
na kuhakikisha kuwa wafugaji wanaelimishwa na wanatekeleza misingi
ya ufugaji wa kisasa na kuchukua hatua za dhati za kueneza mbegu
bora za ngombe wa maziwa na wa nyama.
MIONGOZO MIWILI

85

Chama kitaongoza jitihada za kuanzisha na kupanua ufugaji wa


kijamaa vijijini kwa njia ya ranchi za ngombe bora wa maziwa na ranchi
za vijijini za kunenepesha mifugo. Katika hali hiyo, suala la mipango ya
matumizi bora ya ardhi vijijini linakuwa la umuhimu wa kwanza.
Jingine la kulikabili ni suala la uhaba wa nyama, maziwa na mayai na
bei za juu mno za mazao hayo nchini. Ili kulipatia ufumbuzi tatizo hili,
Chama kitawajibika kuhakikisha kuwa serikali inaingiza katika mipango
yake miradi mikubwa ya ufugaji wa kuku, nguruwe na ngombe karibu na
miji mikubwa. Aidha, Chama na Serikali visaidie vijiji vinavyozunguka
miji kuanzisha miradi ya ufugaji hasa wa kuku, nguruwe, sungura na
ngombe wa maziwa.
Wakati huo huo, jitihada za kueneza mifugo katika maeneo yasiyo nayo
ya kutosha itabidi isimamiwe na Taifa. Pamoja na kwamba wafugaji
wengi wa Tanzania wana mifugo mingi, bado wengi wao hawaitumii
wala kuiona mifugo kama chombo cha kuwaletea maendeleo na
maisha bora zaidi. Hivyo, suala la kutumia mifugo ili kuinua hali halisi
ya maisha ya wafugaji na ya vijiji vyao lazima liwe mkabala maalum wa
Chama kuanzia sasa.

(4) Viwanda
Jambo la kusisitiza linahusu hali ya utengenezaji mali katika viwanda
vilivyopo nchini hivi sasa ambapo vilivyo vingi havitengenezi mali kwa
kadiri ya uwezo vilivyo nao. Chama itabidi kijihusishe na matatizo
ya viwanda hivi na kuhakikisha kuwa vinapata misaada yote ili viweze
kutengneza mali kwa kadiri ya uwezo wake. Licha ya matatizo ya vipuri
na utaalam, viwanda hivi vinakabiliwa pia na matatizo ya kisiasa kama
vile upungufu wa mwamko wa siasa na utovu wa nidhamu.
Viwanda vingi tulivyonavyo nchini hutoa makapi ambayo yangeweza
kutumika kwa utengenezaji wa bidhaa nyingine, lakini jitihada hiyo
haijafanywa. Viwanda kama vya sukari, mafuta, mbolea, nyama na vya nguo
ni miongoni mwa viwanda vya aina hiyo. Kuanzia sasa Serikali itawajibika
kuandaa mipango ya kuyatumia makapi yatokanayo na viwanda vya aina
hiyo ili kutengeneza bidhaa zinazoweza kutengenezwa.
86

MIONGOZO MIWILI

Chama pia kitatilia mkazo utekelezaji wa Agizo la Viwanda Vidogo


Vidogo mijini na vijijini. Chama kitahakikisha kuwa kila Mkoa unaandaa
mpango wa muda mrefu wa utekelezaji wa Agizo hili la viwanda vidogo.
(5) Mwamko wa Siasa wa wafanyakazi
Mwamko wa siasa una uwezo mkubwa wa kuongeza ufanisi wa kazi
kwa kuwatia wafanyakazi ari na makini zaidi katika kazi. Hali ya sasa
viwandani na ofisini inaonyesha upungufu wa mwamko wa siasa.
Hisia za kimapinduzi za kuthamini kazi na wajibu, moyo wa uaminifu
na wa kujitolea muhanga, tabia ya kuthamini mali ya umma, yote haya
yamepoteza nguvu zake.
Ni jukumu la Chama kutia pumzi mpya wakati wote katika viwanda,
Serikalini na katika Mashirika ya Umma itakayoleta vuguvugu la
kimapinduzi miongoni mwa wafanyakazi kwa kuuinua mwamko wao wa
siasa, mwamko wa uvumbuzi, ili waongeze juhudi ya kazi wakitambua
kuwa sehemu zao za kazi ndio uwanja wao wa mapambano ya kujenga
ujamaa na hivyo washiriki kwa dhati katika harakati hizo.

(6) Wizi wa mali ya umma, hujuma katika uchumi, magendo na ujambazi


Kumekuwa na ongezeko kubwa la uhalifu wa aina mbalimbali nchini
tangu tupate uhuru. Uhalifu wenye kutia wasiwasi maalum ni uhalifu
katika uchumi. Wizi wa mali ya umma umeanza kuwa jambo la kawaida.
Kumekuwa na matukio ya baadhi ya maafisa kuhusika na kuidhinisha
mikataba na kampuni za nchi za nje bila kujali maslahi ya Taifa. Wakati
huo huo vipusa, dhahabu na mali mbalimbali za taifa zinatoroshwa nje
ya nchi kwa magendo na kusabisha hasara kubwa kwa Taifa. Ujambazi
wa kutumia silaha nao umetumika ili kunyanganya mali na kutisha
wananchi.
Chama kitahakikisha kuwa serikali inachukua hatua kali za kupambana
na vitendo hivi vinavyodhoofisha uchumi wa Taifa. Iko haja pia kwa
sasa ya kubuni sheria maalum zitakazoelekezwa kwenye vita dhidi
ya uhalifu katika uchumi unaozidi kuongezeka.
MIONGOZO MIWILI

87

(7) Uharibifu wa vyombo vya kazi na wa mali ya umma


Imezuka tabia ya aibu nchini ambayo imekuwa ikiongezeka ya vitendo
vya kuharibu na kuvitumia vibaya vyombo muhimu vya kazi na mali ya
umma kwa jumla. Magari, matrekta zana nyingine muhimu za Chama,
Serikali na Mashirika ya Umma mara nyingi hayadumu muda mrefu
kama ambavyo ingetazamiwa kutokana na matumizi mabaya. Nchi
inapatishwa hasara kubwa ya fedha za kigeni itokanayo na ajali za
malori, mabasi, magari madogo n.k. zinazosababishwa na uzembe na
ulevi. Kuna tabia ya baadhi ya abiria kuharibu mabehewa ya treni
ambayo kesho watahitaji kuyatumia mabehewa hayo hayo tena. Tunalo
tatizo vile vile la tabia ya kuchafua na kuharibu nyumba za serikali na
za mashirika za kuishi inayofanywa na baadhi ya wapangaji wenyewe.
Wakati mwingine majengo ya ofisi za Chama, Serikali na Mashirika ya
Umma hayahifadhiwi na kuhudumiwa ipasavyo.
Tabia ambayo baadhi ya mifano yake imetolewa hapo juu ni ishara
kuwa kuna mushkeli wa msimamo katika jamii. Chama kuanzia
sasa kitalifanyia uchunguzi suala hili ili kukielewa chanzo chake na
kulipatia ufumbuzi wa kudumu.

C . MAENDELEO YA JAMII
91. Katika kipindi kinachoanzia sasa Chama kitatilia mkazo suala la
ujenzi wa tabia na maadili ya kijamaa nchini. Pamoja na jitihada
iliyofanywa ya kutoa elimu na kuunda vyombo vya umma, jamii
yetu bado inazo mila, tabia na maadili yaliyo kinyume na maadili
ambayo yanafanana na misingi ya siasa ya ujamaa tunayosukudia
kuijenga.

92. Watu wameanza kuthamini zaidi vitu kuliko utu na tamaa ya


kujipatia mali bila ya kuitokea jasho inaenea, matukio ya wizi
wa mali ya umma yameongezeka. Lakini lililo baya zaidi ni kuwa
mwizi wa aina hiyo anapogunduliwa, baadhi ya wananchi badala
ya kumfichua au kulaani kitendo chake, humsifu na kumhusudu.
Wakati mwingine mvivu na mtegaji kazini hutetewa hata na vyombo
88

MIONGOZO MIWILI

vya Chama vyenyewe. Wakati huo huo, bado kuna mabaki ya tabia
ya kupuuza elimu ya shule kwa watoto na badala yake kuna wazazi
wanaopendelea watoto wao wachunge mifugo au hata kuolewa
badala ya kuendelea na shule.

93. Jitihada ya Chama za kujenga tabia na maadili ya kijamaa


itaelekezwa kwenye taasisi muhimu za nchi kama shule na vyuo,
majeshi na sehemu za kazi. Lakini Chama kitahakikisha pia kuwa
maisha ya hadhara ya jamii yetu yanasaidia kujenga misingi ya
tabia na maadili ya Taifa linalojenga ujamaa na la kimaendeleo kwa
ujumla. Hivyo, Chama kitapiga vita tabia ya baadhi ya wananchi
na hasa wakiwa viongozi inayokwaza na kupotosha umma. Jamii
lazima iwe shule ya kwanza ya maadili ya kijamaa.
(1) Maendeleo ya jamii
(a) Uchumi wa fedha ni mpya katika nchi yetu na ndiyo maana tabia
ya kutumia fedha kwa mipango haijaenea. Chama kitaendelea
kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutumia fedha kwa
mipango, kuweka akiba benki na kupiga vita tabia ya ufujaji mali na
matumizi ya fahari.

(b) Uzururaji wa aina mbalimbali umeongezeka nchini. Kwa kuzingatia


kushindwa kwa hatua za pupa zilizotumika katika siku za nyuma,
Chama kitalitafakari kwa undani zaidi suala la mipango na mbinu
za kupambana na uzururaji kwa kutia maanani kuwa ufumbuzi wa
kudumu utategemea maendeleo ya ujenzi wa ujamaa vijijini pamoja
na mipango thabiti ya kuwashirikisha wakazi wa mijini katika
ushirika wa viwanda vidogo. Vijiji ambavyo vimepiga hatua za
ujamaa vimekwishaanza kulitatua tatizo la uzururaji na vimeanza
kuwa na mipango ya kuwatunza vikongwe na walemavu.
(c) Utaratibu wa bima na pensheni hauwezi kuwa wa wafanyakazi
pekee. Katika siku za usoni Chama kitahakikisha kuwa unaanzishwa
utaratibu wa bima na pensheni kwa wakulima washirika kwa
kutegemea maendeleo yao.
MIONGOZO MIWILI

89

(d) Hali ya vijiji vingi ingali duni kwa ustawi wa jamii na utamaduni.
Chama kitalishughulikia suala la kuleta mapinduzi ya mazingira
vijijini katika fani hiyo.
(e) Kuhusu walemavu, Chama kitahimiza serikali kuchukua hatua
za kuimarisha na kuvipanua vifaa muhimu kwa walemavu kama
baiskeli, viatu, magongo, na kadhalika.

(2) Elimu
Chama kuanzia sasa kitajihusisha zaidi na shughuli za elimu nchini
hasa kwa upande wa maandalizi ya waalimu na maendeleo yao na ya
shule na vyuo maana waalimu wana mchango mkubwa wa kutoa katika
kumjenga Mtanzania mpya. Katika lengo hilo, Chama kitafanya tathmini
ya mafanikio tuliyoyapata katika kuielewa na kuitekeleza falsafa ya
Chama ya Elimu ya Kujitegemea.
Aidha, Chama kitalitazama upya Agizo la Musoma katika vipengele vyake
vyote. Kwa sasa imedhihirika kuwa utekelezaji wa Azimio hilo kuhusu
utaratibu wa kuingia Chuo Kikuu unahitaji mabadiliko ya msingi.
Pamoja na mafanikio tuliyoyapata katika Elimu ya Watu Wazima
Chama kitaendelea kuhimiza wananchi na hasa wanaCCM na viongozi
kujiendeleza kwa elimu kwa kadiri ya uwezo wao na kujenga tabia ya
kusoma kama sehemu ya maisha yao.
(3) Afya
Kazi moja muhimu ambayo ni ya Chama katika miaka ijayo ni kuhimiza
kuenezwa kwa elimu ya kinga ya maradhi pamoja na kuongoza
mapambano dhidi ya tabia na mila zisizo nadhifu. Hali ya afya ya
wananchi wengi vijijini inaathiriwa na tabia na mila ambazo zinapingana
na maendeleo ya jamii kama vile tabia ya kutotumia vitanda, tabia ya
kuishi katika nyumba moja na mifugo, tabia ya kutotumia vyoo, tabia ya
kunywa maji yasiyochemshwa, miiko mbalimbali, na kadhalika. Wakati
huo huo Chama kitatilia mkazo suala la usafi wa mazingira mijini na
vijijini pamoja na umuhimu wa kuwepo kwa vyoo vya umma mijini.
90

MIONGOZO MIWILI

(4) Ujenzi wa nyumba


Mahitaji ya ujenzi wa nyumba za kuishi mijini na wa majengo ya ofisi
na viwanda nchini yanazidi kuwa makubwa. Kazi moja ya Chama ni
kuona kama kuna umuhimu wa kuingiza teknolojia mpya ya ujenzi
nchini itakayosaidia kutoa msukumo wa shughuli za ujenzi wa nyumba
za kuishi na za kazi. Kuna ukweli kuwa upungufu wa vifaa vya ujenzi
umechelewesha maendeleo ya ujenzi nchini. Lakini huenda ikadhirika pia
kuwa mashirika ya Msajili wa Majumba na Shirika la Nyumba yatahitaji
pia teknolojia bora zaidi ili kuweza kutatua matatizo ya nyumba za
wafanyakazi mijini. Sera ya nyumba itashughulikiwa pia katika kipindi
kinachoanza sasa.

(5) Nishati
Suala la nishati ni la msingi kwa maendeleo ya Taifa letu. Pamoja na
kuendelea kutafuta mafuta, Chama kitahakikisha kuwa serikali inazidisha
mipango thabiti itakayoliwezesha Taifa kuanza kutumia nguvu za maji,
makaa, upepo na jua. Pamoja na miradi mikubwa ya nguvu za maji
kuna haja ya kutia maanani miradi midogo midogo ya nguvu za maji.
Suala la kuni itabidi lipewe umuhimu mkubwa kwa kuwa na mipango
kamambe ya kupanda miti vijijini na miradi ya Mikoa na Taifa. Chama
kiihimize Serikali kuendelea na kutafuta mbinu za kutumia makaa ya
mawe tuliyonayo kusukuma uchumi wetu. Umuhimu wa suala la nishati
utahitaji sera maalum.
(6) Msimamo juu ya kuendeleza sayansi na teknolojia
Mpango wa miaka Ishirini unatoa mwelekeo wa maendeleo ya sayansi na
teknolojia, kwani sayansi na teknolojia ni msingi muhimu kwa maendeleo
ya kisasa. Chama kijihusishe zaidi na mipango ya kuwapata wanasayansi
na wanateknolojia wenye uwezo wa viwango mbalimbali vya utaalamu na
msimamo sahihi wa siasa. Wakati huo huo, Chama kishughulikie ustawi
wa wataalamu na mabingwa tulionao hivi sasa nchini ili kuhakikisha
kuwa wanaishi katika mazingira yanayowawezesha kutoa mchango wao
kwa ukamilifu katika ujenzi wa Taifa letu. Kutokana na kukosa msimamo
sahihi wa kuwashughulikia wataalamu wetu kumewafanya baadhi ya
MIONGOZO MIWILI

91

wataalam kubabaika na Serikali kupoteza mabingwa katika fani za


uganga, uhandisi, urubani wa ndege na kadhalika.

Maendeleo ya uchumi wetu hasa kwa upande wa viwanda na nishati


utahitaji mafundi wa viwango mbalimbali kwa wingi sana. Chama
kihakikishe kuwa serikali inakuwa na mipango thabiti ya namna ya
kuwapata mafundi hawa na kwamba inatumia nafasi zinazoweza
kupatikana kuwaandaa hapa nchini na ngambo.
94. Chama kitakuwa na utaratibu wa kuandaa mikutano na wataalamu
wa fani mbalimbali ili kubadilishana mawazo juu ya mbinu za
kusukuma mbele mapinduzi katika sayansi na teknolojia nchini.

D. ULINZI NA USALAMA

Msingi wa maendeleo ya Ulinzi na Usalama wa


Tanzania ni Watanzania wenyewe, kila Mtanzania,
na hasa kila mzalendo na kila mjamaa.
(Mwongozo wa TANU, 1971)
95. Kazi kubwa ya Chama ni kuhakikisha kuwa uhuru wa taifa, mipaka ya
nchi na matunda ya uhuru na ya ujamaa ya wakulima na wafanyakazi
yanalindwa na kuhifadhiwa. Majeshi yetu yote kwa pamoja ndicho
chombo kikuu cha kutekeleza siasa ya Chama ya ulinzi na usalama.
Lakini chimbuko la majeshi ni Umma wa wakulima na wafanyakazi
ambao pia wanashiriki katika ulinzi na usalama wa nchi yao kwa
kupitia ulinzi wa mgambo na kwa kuwa macho katika sehemu zao
za kazi na za kuishi viwandani na maofisini, vijijini na mijini.

96. Chama kitaendelea kuimarisha kazi ya kuyaelimisha majeshi na


wananchi kwa jumla juu ya maumbile ya mapambano yetu na
kufanya uchambuzi wa kutambulisha maadui wa taifa na wa siasa
ya Ujamaa na Kujitegemea ambao ni ubepari na ubeberu wa dunia
na vibaraka wao wa humu nchini.
97. Kazi ya Chama ni kuhakikisha kuwa majeshi yetu yanakuwa
tayari kwa mapigano wakati wote. Ili kufikia lengo hilo, Chama
92

MIONGOZO MIWILI

kitahakikisha kuwa wanajeshi wanakuwa na mwamko wa hali ya


juu wa kizalendo na wa kijamaa na wanajengeka katika misingi ya
nidhamu ya kujituma ya jeshi la kijamaa. Chama kitahakikisha pia
kuwa maendeleo ya teknolojia na uimarishaji wa michepuo jeshini
yanapewa umuhimu wa kwanza. Ni muhimu kwa Chama kuyasaidia
majeshi yetu katika jitihada zao za kupambana na tabia iliyoanza
kujitokeza hapa na pale majeshini ya kutothamini mali ya jeshi,
ubadhirifu na tabia ya kutojali kwa jumla. Vitendo hivi ni kinyume
cha mila za kijeshi na maadili ya jeshi lolote na hasa jeshi la kijamaa
amayo majeshi yetu, chini ya uongozi wa Chama, yatatilia mkazo
wakati wote.

98. Ushindi wetu wa vita dhidi ya majeshi ya uvamizi ya fashist Idd


Amin umetudhihirishia usahihi wa siasa ya Chama ya Ulinzi na
Usalama, kutuonyesha ushujaa na uzalendo wa wanajeshi wetu
na uwezo mkubwa walionao makamanda wetu wa kuongoza
mapigano. Kazi ya Chama sasa ni kufanya majumuisho ya ujuzi
mkubwa tulioupata kwa manufaa ya harakati za ulinzi na usalama
wa Taifa kwa siku za usoni. Miongoni mwa mambo yanayohitaji
uchambuzi na ufafanuzi wa Chama ni uhusiano wa majeshi, nafasi
ya ulinzi wa mgambo katika mfumo wa ulinzi na usalama wa
Taifa wakati wa amani na vita, muundo wa ulinzi na usalama kwa
uongozi na utendaji yaani uhusiano wa wizara na majeshi, nafasi ya
wanawake katika majeshi yetu na kazi za Chama katika majeshi.
99. Chama kitahakikisha kuwa jeshi la Polisi linapata misaada yote
toka Serikalini ili kuliimarisha. Jeshi la Polisi linahitaji kupewa
uwezo zaidi wa mafunzo ya hali ya juu ya mbinu za kupambana na
majambazi na wahalifu wenye ujuzi mkubwa pamoja na kupewa
uwezo wa zana muhimu za kazi.

100. Chama pia kina kazi ya kuchambua tena na kwa makini nafasi ya
Jeshi la Kujenga Taifa katika kusukuma mapinduzi ya ulinzi na ya
uchumi wa Taifa. Pamoja na kwamba madhumuni ya awali ya J.K.T.
bado hayajakiukwa na wakati, Chama kitazame namna ya kulipa
J.K.T. na J.K.U. uwezo wa kuwa chombo cha kukabili kazi za ujenzi
MIONGOZO MIWILI

93

wa barabara, majengo, mabwawa n.k. kwa hali ya juu zaidi, kuukuza


uwezo wao wa kutoa chakula na mifugo kwa ajili ya Taifa na pia
kuwezesha J.K.T. na J.K.U. kuwa mahali pa kutoa mafunzo ya muda
mfupi ya wataalamu wengi wa kada ya chini ya ufugaji, kilimo na
ufundi toka Vijijini.

101. Jambo moja tulilojifunza kutokana na vita dhidi ya uvamizi ni


umuhimu wa viwanda vinavyohudumia majeshi. Chama kitahimiza
Serikali kulipa uzito maalum suala la kukuza na kupanua viwanda
vya majeshi kwa madhumuni ya kuyapatia majeshi na ulinzi wa
mgambo vifaa muhimu wanavyohitaji.

E. MSUKUMO WA UJENZI WA UJAMAA

102. Imedhihirika katika kipindi cha miaka kumi na minne tangu


Azimio la Arusha kuwa serikali na vyombo vyake na hata baadhi
ya viongozi wamehusika katika kuupa nguvu na kuukuza ubepari
nchini. Katika kipindi kinachoanzia sasa, Chama kitakuwa macho
na kitahakikisha kuwa uwezo wa Serikali na vyombo vyake, uwezo
wa Chama, unatumika kuimarisha na kuendeleza Ujamaa.
103. Katika lengo hili, dhamira ya Chama ya kujenga ujamaa ijidhihirishe
kwa kuhakikisha kuwa:
(a) Benki zinaelekeza nguvu za fedha za Taifa kwenye kujenga
ujamaa kwa kuvipa umuhimu wa kwanza vijiji, vyama halisi
vya ushirika na mashirika ya umma.

(b) Kampuni za umma za ujenzi zilizopo zinapewa uwezo wa kumudu


kazi zaidi na kwamba kampuni mpya za umma za ujenzi zinaundwa
ili kuikabili kazi ya ujenzi nchini inayoongezeka mwaka hadi
mwaka. Ihakikishwe pia kuwa Serikali na mashirika ya umma
hayawapi kazi za ujenzi makontrakta wa kibepari isipokuwa
wakati hakuna uwezekano mwingine. Fedha za Serikali na
mashirika ya umma zimesaidia sana kuupa nguvu ubepari katika
sekta hii.
(c) Utaratibu wa sasa wa serikali na vyombo vyake kutumia

94

MIONGOZO MIWILI

mawakala wa biashara za nje na biashara za ndani ya nchi


ukomeshwe. Utaratibu huu pia umesaidia kujenga ubepari
nchini.

(d) Kamati za kugawa matrekta na magari nchini zinatoa umuhimu


wa kwanza kwa mashirika na makampuni ya umma, vijiji na
vikundi vya ushirika halisi.

(e) Mipango thabiti inafanywa na serikali ya kuhakikisha


kuwa mtindo wa sasa wa watu binafsi kupewa zabuni za
kulisha makundi ya umma kama majeshi, shule na vyuo
unakomeshwa hatua kwa hatua. Kwa hatua ya kwanza, vyakula
vinavyoshughulikiwa na mashirika ya umma kama sembe,
mchele, maharage na sukari vipatikane moja kwa moja toka
huko.

(f) Usafirishaji unaofanywa na vyombo vya umma uimarishwe na


kupanuliwa na kwamba ugawaji wa malori na mabasi ufanywe
kwa lengo la kukuza ujamaa katika sekta hii.
(g) Kila Mkoa unaandaa mpango wa muda mrefu unaoonyesha
malengo ya ukuaji wa sekta ya ujamaa katika kilimo, ufugaji,
viwanda na viwanda vidogo, biashara na usafirishaji. Mpango
huo uhakikishe kuwa kila kijiji kinakuwa na malengo
yanayoonyesha ukuaji wa shughuli za kijamaa, mkazo ukiwa
katika kukuza uzalishaji mali. Kutokana na mipango yake,
Serikali iandae mpango unaoonyesha mwelekeo wa ukuaji wa
sekta ya ujamaa nchini.
(h) Utekelezaji wa Siasa ya ujamaa unatilia mkazo suala la
Kujitegemea maana Ujamaa unaojengwa kwa misingi ya
kutegemea ni ujamaa batili. Chama kitaichambua falsafa
inayoongoza upangaji wetu wa mipango ili kuhakikisha kuwa
mipango ijayo ya maendeleo inaonyesha waziwazi mwelekeo
wa kujitegemea katika mpango. Serikali ihakikishe pia kuwa
uwezo wetu wa kujitegemea katika vipuri mbalimbali unakuzwa
kwa kutumia uwezo uliopo nchini.
MIONGOZO MIWILI

95

SEHEMU YA NNE
CHAMA NA MAPINDUZI YETU
Chama tunachokiunda tunataka kiwe chombo madhubuti
katika muundo wake na hasa katika fikra zake na vitendo
vyake vya kimapinduzi vya kufutilia mbali aina zote
za unyonyaji nchini, na kupambana na jaribio lolote lile
la mtu kumwonea mtu, au shirika au chombo cha nchi
kuonea au kudhalilisha wananchi, kudhoofisha uchumi au
kuzorotesha maendeleo ya Taifa.
(Katiba ya CCM)
104. Chama chetu, Chama cha Mapinduzi, ni Chama chenye historia
ya kipekee katika Afrika. Historia yake ni ya mafanikio na ushindi
katika fani mbalimbali za utekelezaji wa malengo ya siasa yake.
Wanazuoni watakapokuja andika historia ya Chama chetu wataweza
kuyachambua kwa kina na mapana mafanikio hayo yasiyo na kifani.

105. Chama cha Mapinduzi ni Chama cha kijamaa. Kazi kubwa ya CCM
ya sasa ni kuziunganisha nguvu zote za kijamaa na za kimaendeleo
nchini na kuziongoza katika mapambano ya kujenga ujamaa
Tanzania na kujenga ushirikiano wa kimapinduzi wa wajamaa
na wapenda maendeleo wote katika Afrika na Dunia katika
mapambano dhidi ya ukoloni, ukoloni mambo leo, ubepari na
ubeberu.

106. Chama cha Mapinduzi ni chombo kikuu na cha pekee cha uongozi
wa taifa letu. Kuongoza ni kuonyesha njia. Kwa hiyo, Chama chetu
ni mwanga unaotumulikia njia katika hali ngumu ya mapambano
ya wakulima na wafanyakazi kuelekea kwenye ujamaa. Uhalali wa
uongozi wa Chama chetu una misingi ya kihistoria ingawa historia
peke yake haitoshi kuelezea uhalali wa Chama cha Mapinduzi kwa
sasa kuongoza Taifa. TANU na ASP vilijijengea uhalali machoni
mwa wananchi kwa kuwadhihirishia kuwa vinastahili kuongoza
kutokana na usahihi wa siasa na mbinu zao katika mapambano
96

MIONGOZO MIWILI

dhidi ya ukoloni, kwa vitendo vya kujitoa mhanga vya wanachama


na viongozi wa vyama hivyo na kwa kudhihirisha kwa vitendo kuwa
ndio watetezi halisi wa maslahi ya wananchi. Hatua za kimapinduzi
zilizochukuliwa Zanzibar baada ya Mapinduzi Januari 12, 1964,
na hatua za kimapinduzi zilizofuatia kutangazwa kwa Azimio la
Arusha Februari 5, 1967 zilijenga uhalali mpya wa ASP na TANU
katika misingi ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

107. Pamoja na uhalali wa kihistoria, ambao ni uhalali wa kurithi, Chama


cha Mapinduzi chenyewe lazima kijijengee uhalali wake katika hali
ya mapambano ya sasa kwa kudhihirisha kwa vitendo kuwa ndicho
mtetezi wa kuaminika wa maslahi ya wakulima na wafanyakazi
nchini. Kwa kuwa kukubalika na kuaminika kwa ASP na TANU
kulijengwa kwa vitendo vya kimapinduzi vya uamininifu na ukweli
kwa umma na kwa kujitolea mhanga kwa wanachama na viongozi
wa TANU na ASP wakati huo, vivyo hivyo, uhalali wa uongozi wa
CCM na kukubalika na kuaminiwa kwake na umma kutategemea
vitendo vya kimapinduzi vya uaminifu na ukweli kwa umma vya
wanachama na hasa viongozi wa CCM katika harakati za kila siku za
kujenga ujamaa viwandani, ofisini, vijijini na mijini. Hii ndiyo njia ya
pekee ya kukifanya Chama kiwe ndani ya umma na kiwe mwakilishi
wa kweli na halali wa matumaini yao ya haki.

A. CHAMA NA SERIKALI

108. Serikali ndicho chombo kikuu cha utekelezaji wa siasa ya Chama.


Chama kinaiongoza Serikali na vyombo vyake kwanza kabisa
kwa kutoa shabaha na malengo, siasa (sera), maelekezo na
maagizo ya mara kwa mara ambayo Serikali huyatafsiri katika
mipango ya utekelezaji na sheria. Hii ina maana kuwa Chama
ndicho kinachowajibika kuzungumzia na kuamua juu ya masuala
mazito na makubwa ya nchi kabla hayajaelekezwa Serikalini kwa
uchambuzi na utekelezaji.

109. Serikali kwa maumbile yake ni chombo cha madaraka ya mabavu.


Serikali ni sheria, ni majeshi, ni mahakama na ni jela. Kwa hiyo,
MIONGOZO MIWILI

97

hata katika hali yetu ya demokrasia na ujamaa, wakati wote ni


muhimu kwa Chama na umma kuwa na hakika na anayekabidhiwa
madaraka haya ya Serikali maana yakiangukia mikononi mwa
mpinga mapinduzi madaraka hayo yanaweza kutumiwa dhidi
ya maslahi ya umma wenyewe. Hivyo, Chama kuongoza maana
yake ni kuhakikisha pia kuwa madaraka muhimu ya Serikali na
ya mashirika ya umma wanakabidhiwa watu ambao pamoja
na uwezo wao wa kitaalamu ni wenye msimamo wa kizalendo
na waaminifu kwa Chama na kwa wakulima na wafanyakazi wa
Tanzania.

110. Kuhusu suala hili, Chama cha Mapinduzi kina kazi mbele yake ya
kujumlisha tuliyojifunza tangu tupate uhuru na hasa baada ya
Azimio la Arusha juu ya hatari zinazoweza kutokea kwa siasa ya
Chama na kwa taifa wakati madaraka muhimu ya Chama, Serikali
au Mashirika ya Umma wanakabidhiwa watu ambao kisiasa ni
chui katika ngozi ya kondoo.

111. Serikali na Mashirika ya Umma vile vile ni vyombo vya kutoa


huduma kwa wananchi. Katika nafasi yake ya uongozi, Chama
kina wajibu wa kuhakikisha kuwa utoaji wa huduma kwa umma
hausababishi manunguniko. Kuongoza katika hali hii maana yake
ni kuwaelimisha na kuwasaidia watendaji katika siasa ili kuinua
na kuimarisha ari na uwezo wao wa kutoa huduma. Wakati
huo huo kuongoza ni kuwaelimisha na kuwaelekeza wananchi
juu ya maamuzi halali ya serikali na umuhimu wa kuyatekeleza
kwa maendeleo yao na ya taifa na pia wakati wote kuhakikisha
kuwa wananchi hawafichwi au kudanganywa juu ya hali halisi na
matatizo ya kweli ya nchi yao.

112. Aidha katika nafasi yake ya kiongozi wa serikali na vyombo vyake,


Chama kina wajibu wa kuhakikisha kuwa muundo, taratibu na
utendaji kazi wa serikali na wa mashirika ni wenye kutekeleza
siasa ya Chama kama ilivyokusudiwa na kuleta ufanisi. Hapa ni
muhimu kusisitiza kuwa Chama kiongoze mapambano dhidi ya
umangi meza na tabia zozote zionazozorotesha kazi na utoaji wa
98

MIONGOZO MIWILI

huduma bora kwa umma. Chama kione pia kuwa mifumo iliyopo
Serikalini na katika Mashirika ya Umma inamwezesha mfanyakazi
kushiriki katika uongozi wa kazi mahali alipo na kwamba kwa
kushirikiana na wenzake anapata nafasi anayostahili ya kulijenga
na kulitumikia Taifa lake.

Chama na mfumo wa siasa na jamii

113. Chama cha Mapinduzi ni muungano wa Wakulima na Wafanyakazi


wa mstari wa mbele kaika mapambano ya kujenga Ujamaa
Tanzania. Mfumo wetu wa kisiasa na kijamii unajengwa kwa
mujibu wa msingi na mahitaji ya nchi inayojenga ujamaa. Lengo
ni kujenga mfumo wa demokrasia ya kijamaa ambamo wakulima,
wafanyakazi, washirika na watu wote wanaoishi kwa jasho lao sio
tu kuwa watashirikiana na kuwa na kauli ya mwisho katika mambo
ya siasa na ya jamii ya nchi yao bali wakati huo huo watamiliki
na kudhibiti uchumi wa Taifa kwa kupitia Serikali, Mashirika ya
umma, Vijiji vya ujamaa na vyama vya ushirika. Demokrasi ya
Chama kimoja ya sasa ni hatua inayotuelekeza kwenye lengo hilo.

114. Hivyo ni muhimu kwa Chama katika kipindi kinachoanza sasa


kuonyesha njia itakayolielekeza Taifa kwenye kiwango cha juu
zaidi cha demokrasi ya wakulima na wafanyakazi washiriki kila
hali inapohitaji ifanyike hivyo. Katika maana hiyo, ni muhimu
kwa Chama kuutazama tena mfumo wa demokrasi yetu ya Chama
kimoja kwa lengo la kuuimarisha.

115. Kwanza kuna suala la mgawanyo wa madaraka ya nchi kati ya Chama,


Rais wa Jamhuri ya Muungano na Bunge na kati ya Chama, Rais wa
Zanzibar na Baraza la Wawakilishi. Sasa ni miaka ishirini tangu
Tanzania bara ipate uhuru na miaka 18 tangu Mapinduzi ya Zanzibar.
Huu ni wakati unaofaa kutazama upya mfumo wa madaraka wa nchi
yetu ili kuchukua hatua za kuimarisha uongozi wa pamoja kwa kutoa
madaraka zaidi kwa Bunge ambalo pamoja na Rais ndio wawakilishi
wa taifa. Kulipa Bunge madaraka zaidi ya kusimamia utekelezaji wa
Serikali ni kuimarisha madaraka ya Umma.
MIONGOZO MIWILI

99

116. Jambo la pili ni kuwa Bunge lenyewe linahitaji kufanyiwa uchambuzi


kwa madhumuni ya kuimarisha uwakilishaji wa maslahi ya
wakulima na wafanyakazi. Chama kitatumia kipindi kinachoanza
sasa kutafakari juu ya njia bora zaidi zitakazohakikisha kuwa
wakulima, wafanyakazi, washirika, vijana na wanawake wote
wanawakilishwa kulingana na nia ya Chama ya kuendeleza
mapinduzi yetu ambayo yanahitaji Bunge linalowakilisha maslahi
halisi ya Wakulima na Wafanyakazi na kwa kutia maanani nafasi
ya wanawake na vijana katika Taifa letu.

117. Jambo la tatu linahusu wabunge wa kuchaguliwa na wa kuteuliwa.


Bunge letu katika sura yake ya sasa lina asilimia kubwa ya
wateuliwa. Chama kitalitafakari suala hili ili kuona kuwa ubunge
wa kuchaguliwa unapata nafasi kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa
ikieleweka kuwa uchaguzi wa wawakilishi ni sehemu muhimu ya
demokrasi ya kijamaa.

118. Wakati huo huo, Chama kitafanya uchambuzi ili kupata njia za
kuimarisha madaraka ya umma tangu vijijini hadi Taifa kwa
jumla. Chama kitayarudia maamuzi yake ya nyuma kuhusu suala
hili tangu tupate uhuru hadi sasa ili kujipa msingi wa kubuni
utaratibu wa kujenga madaraka ya umma yatakayotuelekeza
kwenye demokrasia ya kijamaa, katika jitihada hii, Chama
kitaepuka jaribio la kurudisha mifumo ya tawala za kizamani,
badala yake Chama kitajifunza toka mifumo ya zamani na hata ya
nchi nyingine ili kubuni mfumo mpya utakaolingana na mahitaji
ya maendeleo ya kidemokrasi na ya ujamaa ya Tanzania ya leo na
ya kesho. Hivyo, Chama kitayashughulikia masuala ya madaraka
ya miji, wilaya na vijiji pamoja na suala la vyama vya ushirika
katika msimamo huo.

119. Kwa hiyo, Chama pia kina wajibu wa kuhakikisha kuwa wananchi
katika fani zote za maisha wanashiriki kwa ukamilifu katika ujenzi
wa taifa lao. Katika nchi yetu wakulima na wafanyakazi ndio
msingi wa mfumo wa jamii yetu na siasa ya ujamaa ya Chama ni
siasa ya tabaka hili. Hivyo harakati za kujenga ujamaa ni harakati
100

MIONGOZO MIWILI

za kuwaendeleza wakulima na wafanyakazi. Pamoja na hayo,


Chama kinatambua nafasi maalum ya wanawake na vijana katika
mapambano yetu. Lengo hili linaweza kufikiwa kwa kupitia Jumuia
ya wafanyakazi, Jumuia ya vijana, Jumuia ya wanawake na Jumuia
ya Washirika. Suala la Jumuiya ni suala ambalo Chama kinahitaji
kulifanyia uchambuzi zaidi ili kufafanua waziwazi uhusiano wake
na Chama na nafasi yao halisi katika harakati za ujenzi wa Taifa.

120. Pamoja na suala la Jumuia za Wananchi kuna umuhimu kwa Chama


kuunda mazingira nchini yatakayowawezesha wakulima na
wafanyakazi kushiriki kwa ukamilifu zaidi katika mapambano ya
kisiasa na ya kiitikadi. Miaka iliyofuata Azimio la Arusha na baadaye
mwongozo wa TANU ilikuwa kipindi cha vuguvugu la kimapinduzi
lililowawezesha vijana, wakulima na wafanyakazi nchini kushiriki
katika kuijadili siasa ya Chama na kujiendeleza kinadharia na
kiitikadi. Utekelezaji wa Mwongozo wa Chama cha mapinduzi
unahitaji vuguvugu la namna yake. Hakuna msukumo wa kweli wa
ujenzi wa ujamaa unaowezekana bila ya msukumo unaolingana
na mijadala juu ya nadharia na itikadi ya ujamaa. Chama kitaunda
mazingira nchini yatakayouwezesha umma kushiriki kwa nadharia
na kwa vitendo katika utekelezaji wa maelekezo ya mwongozo
wa Chama.

121. Tabia moja ya mapinduzi iliyoanza kujengeka wakati wa vuguvugu


la Azimio la Arusha na Mwongozo wa TANU na imefifia sasa ni ile
ya wafanyakazi na vijana wa vyuoni na shule za Sekondari kujenga
uhusiano wa kidugu na ushirikiano na vijiji vilivyo karibu nao.
Maelfu ya wafanyakazi na vijana walifanya kazi za kujitolea wakati
wa mwisho wa juma kudhihirisha mshikamano wa wakulima na
wafanyakazi, na vijana katika kujenga ujamaa.

122. Utaratibu wa kazi za kujitolea kwa wanachama wa Chama Cha


Kijamaa, kwa wafanyakazi na vijana wana mapinduzi, ni jambo
muhimu kwa maendeleo yao ya kisiasa na kiitikadi na kwa
maendeleo ya Ujamaa. Katika jitihada zake za kushirikisha umma
katika ujenzi wa Taifa, Chama cha mapinduzi kitawajibika kufufua
MIONGOZO MIWILI

101

na kuendeleza tabia itakayowawezesha wana CCM, wafanyakazi


na vijana kujitokeza kwa wingi katika kazi za kujitolea na kujenga
ushirikiano kwa vitendo kwa vijana, wanajeshi, wakulima na
wafanyakazi vijijini.

Chama na siasa ya nchi za nje

123. Siasa ya nchi za nje ya Chama cha Mapinduzi inaongozwa na misingi


ya Uhuru wa Taifa wa kujiamulia mambo yake bila kuingiliwa na
yeyote; kushirikiana na vyama na nchi za kimaendeleo na za kijamaa
katika kuimarisha mapambano dhidi ya nguvu za ukoloni, ukoloni
mamboleo, ubepari, ubeberu na ubaguzi wa rangi katika Afrika na
kote duniani; kuunga mkono ukombozi wa Afrika na Umoja wa
Afrika; na kushirikiana na mataifa mengine katika umoja wa nchi
huru za Afrika, katika nchi zisizofungamana na upande wowote na
katika Umoja wa Mataifa katika jitihada za kulinda na kudumisha
amani na usalama duniani.

124. Kwa kuwa chimbuko la siasa yetu ya nje ni ya ndani ya ujamaa


na kujitegemea tunayoijenga, basi kazi moja kubwa ya Chama na
Serikali katika suala hili ni kuielezea siasa yetu na kutetea misingi
ya haki, usawa na uhuru katika mikutano ya kimataifa na kulijengea
Taifa uhusiano wa kidugu na ushirikiano na mataifa ya kimaendeleo
na ya kimapinduzi na yale yote ambayo yanataka ushirikiano nasi
katika misingi ya kuheshimiana, kutoingiliana katika mambo ya
ndani na ya kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.

125. Chama chetu, tangu wakati wa ASP na TANU kiliwajenga wanachama


wake na wananchi kwa jumla katika hisia za kimapinduzi za
kujishirikisha na mapambano ya ukombozi wa nchi nyingine za
Afrika na za dunia. Lakini pamoja na historia hiyo ya Chama na
wananchi kushiriki kwa vitendo katika kuongoza siasa yetu ya nchi
za nje, kumekuwa na vipindi ambapo shughuli za nchi za nje Chama
kiliachia Serikali pekee.
126. Kuanzia sasa Chama kitahakikisha kuwa uhusiano wetu
na nchi za kigeni unakuwa sehemu muhimu ya shughuli zake.
102

MIONGOZO MIWILI

Katika lengo hilo Chama kitaendeleza na kujenga uhusiano


maalum na vyama halisi vya ukombozi, vya kijamaa na vya
kimaendeleo vya Afrika na kote duniani ili kubadilishana
uzoefu na kuimarisha mapambano dhidi ya ubeberu
wa dunia.

B. CHAMA KUJIZATITI ILI KUONGOZA MAPINDUZI

Lakini Ujamaa hauwezi kujijenga wenyewe. Kwani


Ujamaa ni Imani. Hauna budi kujengwa na watu
wanaoamini na kufuata kanuni zake. MwanaTANU wa kweli ni mjamaa, na wajamaa wenziwe
yaani waamini wenziwe katika imani hii ya kisiasa
na kiuchumi ni wote wale wanaopigania haki za
wakulima na wafanyakazi katika Afrika na popote
duniani.
Azimio la Arusha
127. Kazi kubwa ya Chama Cha Mapinduzi kwa mujibu wa Mwongozo
huu ni kuchukua hatua za kujizatiti, kujijenga na kujiimarisha ili
kujipa uwezo unaolingana na uzito wa mapambano yaliyo mbele
yetu ya kujenga ujamaa katika kipindi ambapo ubepari na ubeberu
wa dunia na vibwanyenye na wapinga Ujamaa wa humuhumu
nchini wanazidisha kujenga vitimbi vya uhasama dhidi ya siasa
yetu ya Ujamaa na Kujitegemea.

128. Kujizatiti kwa mapambano ya kujenga ujamaa kwanza kabisa ni


kuwa na hakika na wapiganaji wa mstari wa mbele wa mapambano
hayo ambao ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi. Kwa
hiyo, hatua ya kwanza ya Chama kujizatiti kwa mapambano ni
kuwawezesha wanachama wa CCM kifikra na vitendo, mmoja
mmoja na katika umoja wao, kutimiza wajibu wao wa kimapinduzi.

(1) Kazi ya kuwajengea na kuwaimarisha wanachama:

(a) Maandalizi: Vuguvugu la mijadala ya kichama katika Mashina,


Matawi na Nchini kote.
MIONGOZO MIWILI

103

129. Chuo Kikuu cha Wanamapinduzi duniani kote ni kushiriki kwa


vitendo katika harakati za kimapinduzi pale walipo. Chuo cha
kuwajenga Wana CCM katika msimamo wa kimapinduzi ni kwa
Wana CCM kushiriki kwa vitendo katika harakati za kusukuma
mbele ujenzi wa ujamaa pale walipo, kama ni kijijini, kiwandani,
ofisini, jeshini, chuoni au katika kata ya mjini wanakoishi.
Kushiriki kwa vitendo katika mapinduzi ni pamoja na vitendo vya
kujiendeleza au kujinoa katika nadharia ya mapinduzi.

130. Kwa hiyo, hatua ya kwanza kuelekea kwenye lengo


litakalomwezesha mwana CCM kushiriki katika harakati za
mapinduzi pale alipo ni kwa Chama kuanzisha mashina na
matawi nchini kote. Mikutano hii ya wana CCM tu iitishwe
kujadili maendeleo ya Chama katika sehemu zao; wanachama
wakosoane na kujikosoa kuhusu vitendo vyao kama wanachama
ili kuona kama vinafanana na mahitaji ya mapinduzi. Mikutano
hii pia izungumzie hali ya uchumi ilivyo nchini na kuchambua
hatua za kujihami zinazotarajiwa kuchukuliwa na Taifa na katika
sehemu zao.

131. Viongozi na maafisa wa Chama wa ngazi zote wawajibike kushiriki


katika mijadala hii kama wanachama wengine. Mijadala hii iwe na
lengo la kumwezesha kila mwanachama na kila Tawi kudhihirisha
walivyojitahidi kutekeleza majukumu yake katika Chama, wapi
mwanachama (tawi) alipoonyesha udhaifu na kutafuta njia za
kutimiza majukumu vizuri zaidi.

132. Vuguvugu hili la mikutano ya wanachama liende sambamba na


mijadala ya hadhara ya wananchi wote vijijini, katika sehemu za
kazi na mijini. Mikoa ipange mipango itakayowawezesha viongozi
wa Chama wa ngazi zote kwenda vijijini, viwandani, majeshini,
vyuoni na mijini kuelezea kwa kinaganaga hali ya uchumi wetu na
hatua za kujihami kiuchumi ambazo lazima zichukuliwe. Kushiriki
huku kutawapa nafasi ya kujifunza na kuielewa zaidi hali ya nchi.
Wakati huo huo magazeti na redio vitumike na Chama kuendeleza
na kuelekeza mijadala hii.
104

MIONGOZO MIWILI

133. Mijadala hii ya wanachama na ya wananchi kwa jumla itasaidia


kuinua mwamko wa kisiasa wa wananchi, kuwaelimisha zaidi juu ya
matatizo ya nchi yetu na kuwaongezea ari ya kudhamiria kushiriki
kwa ukamilifu zaidi katika harakati za kujihami kiuchumi na
kisiasa. Mijadala hii katika Matawi, ikiendeshwa kwa makini na kwa
utaratibu mzuri, itawezesha wanachama wa kweli kufahamiana
na wanachama wa bandia kufichuliwa. Hii itahusu pia viongozi
kueleweka katika msimamo.

134. Katika hali hii, hatua inayofuata ni kwa kila Tawi la Chama
kuchukua hatua ya kuwajadili wanachama wake mmoja mmoja ili
kuamua kama bado wanastahili kuendelea na uanachama au la.
Kwa kuwa wazembe, wazururaji, wezi na majambazi watakuwa
wamefichuliwa katika vikao hivi, kwa kuwa wapinga ujamaa
kiitikadi na kwa vitendo watakuwa pia wamefichuliwa, basi hii
ndiyo nafasi ya kukitakasa Chama. Matawi yapendekeze kwenye
vikao vya juu hatua za kuwachukulia wanachama watakaodhihirika
kuwa hawatimizi masharti na wajibu wa wanachama. Azimio la
Arusha linasisitiza juu ya ubora wa wanachama badala ya wingi wa
wanachama. Vuvuvugu hili la mijadala ya wanachama wenyewe tu
litasaidia kuunda hali itakayowezesha kupiga hatua za mwanzo za
kuelekea kwenye lengo hilo la Azimio la Arusha.

135. Kazi hii ya Chama ya kuongoza mijadala ya kujikosoa na kukosoana


iendelee hadi itakapofikia kipindi cha mikutano mikuu ya mwaka
wa tano tangu CCM kuzaliwa. Kipindi hiki ni kirefu cha kutosha
kwa mashina na matawi ya Chama kufanya vikao kadhaa vya
wanachama wote ili kuwezesha kuelewana na kupimana kwa
makini. Kipindi hiki ni kizuri pia kupimana kwa sababu ni kipindi
ambapo Chama kitaongoza mapambano ya utekelezaji wa hatua za
kujihami kiuchumi nchini kote. Na wakati huo huo hiki ni kipindi
cha kuanzisha msukumo mpya wa ujenzi wa ujamaa nchini.

136. Ni dhahiri kuwa katika hali hii ya vuguvugu la mapinduzi la


utekelezji wa siasa ya Chama, wanachama matawini watapata
nafasi nzuri ya kufahamiana na kuelewana kwa vitendo. Wana
MIONGOZO MIWILI

105

CCM halisi watajitokeza kwa vitendo katika utendaji wao wa kila


siku kazini na wanakoishi. Wana CCM wa vijijini watadhihirisha
uanachama wao kwa kuwa katika mstari wa mbele katika
kutekeleza majukumu ya Ujamaa ya kijiji na katika kushiriki kwa
dhati katika kazi za kujitolea kwa jumla kama ujenzi wa shule,
zahanati, barabara za kijiji, shamba la kijiji, kushiriki katika elimu
ya watu wazima, ulinzi wa kijiji na kadhalika.

137. Wana CCM wafanyakazi, watadhihirisha uanachama wao kwa


vitendo kwa kufanya kazi kwa makini na kwa nidhamu, kwa
kushirikiana na wafanyakazi wenzao kuhakikisha kuwa malengo
ya kazi yaliyowekwa yanatimizwa, kwa kupambana bila woga na
vitendo vyo vyote vile vya uvivu na uzembe kazini, vya kuzorotesha
kazi au vya kuhujumu uchumi.

(b) Mafunzo ya Siasa ya Chama


138. Chama kinapanga na kuendesha mafunzo ya siasa yake ikiwa
na malengo makubwa matatu: Mafunzo ya Siasa ya Chama
yanatolewa kwa wananchi kwa jumla kwa lengo la kuieneza
siasa hiyo ili ieleweke na kukubalika na wakati huo ili kupiga
vita upotoshaji na uzushi juu ya siasa ya ujamaa unaoenezwa na
maadui wa ujamaa kwa nia ya kukifanya Chama kifarakane na
Umma. Nia wakati wote ni kuelimisha umma na kuufanya uwe
karibu zaidi na Chama ili ushiriki katika kutekeleza maelekezo
na mwito wake kwa ari na hiari.

139. Lengo la pili la mafunzo ya siasa ya Chama ni kuhakikisha


kuwa wananchi katika taasisi maalum za wananchi: wanafunzi,
wanajeshi, wafanyakazi, vijana, wanawake, wanautamaduni,
viongozi wa kazi, waandishi wa habari n.k. wanahamasishwa ili
kuinua mwamko wao wa kisiasa, na kuwapa wahusika mwelekeo
wa siasa kulingana na jinsi Chama kinavyoiona nafasi yao katika
ujenzi wa taifa kwa sasa na kwa baadaye.

140. Lengo la tatu la mafunzo ya siasa ya Chama ni kuhakikisha kuwa


wanachama na viongozi wanaimarika katika itikadi ya ujamaa na
106

MIONGOZO MIWILI

kujitegemea; kuwapanua wanachama na viongozi upeo wao wa


kuyaelewa masuala mbalimbali; kuwapa methodolojia na mantiki
ya kutafakari na kufanya uchambuzi wa msuala; kuwazatiti kwa
hoja na mbinu zitakazowasaidia katika harakati za kuongoza
utekelezaji wa siasa ya ujamaa pia kueneza na kutetea siasa
ya Chama.

141. Mafunzo ya aina zote tatu ni muhimu kwa maendeleo ya mapinduzi


yetu. Mafunzo ya aina ya tatu, yaani mafunzo ya wanachama na
viongozi, ndiyo yatakayowezesha kufanikiwa kwa mafunzo ya aina
ya kwanza na ya pili. Katika miaka ya usoni, Chama kitaendelea
kuendesha mafunzo ya siasa ya Chama kwa mipango na msukumo
mkubwa zaidi kwa kuzingatia kuwa mapambano ya kisiasa na
kiitikadi ni sehemu muhimu ya mapambano ya kujenga ujamaa na
kuzifichua na kuzishinda mbinu za adui.

142. Hivyo, Chama kitachukua hatua za kuimarisha na kupanua


mipango ya mafunzo ya wanachama na viongozi. Wanachama
walio wengi itabidi wapate mafunzo yao ya nadharia matawini
kwao. Mafunzo hayo yatakayoendeshwa kwa msingi wa semina
yatasimamiwa na mikoa na wilaya zenyewe. Wanachama
watakaojitokeza, kwa msimamo na uwezo, yaani wanachama
wenye sifa za kada, pamoja na viongozi wa matawi, wilaya, mikoa
na Taifa wataingia katika mpango maalum wa kupata mafunzo
katika vyuo vya Chama vya ngazi zinazolingana na mahitji yao.
Utaratibu katika vyuo vya Chama wa mafunzo ya kada na viongozi
wa Chama utahitaji maandalizi ya makini na ya hali ya juu.

143. Chuo cha Chama ni mahala anapopelekwa mwanachama


aliyejitokeza katika Chama, yaani kada wa Chama au kiongozi wa
Chama, kwa madhumuni ya kumwandaa kwa kazi kubwa zaidi za
Chama. Chama ndicho kinachomwandaa mwanachama mwenye
msimamo wa sifa za kada wa Chama au kinaamua kumpeleka
chuoni apate upeo mkubwa zaidi wa kukitumikia Chama.
Mwanachama huyu anaweza akawa afisa wa serikali, mfanyakazi
wa chama au mkulima. La msingi ni kuwa anateuliwa na Chama
MIONGOZO MIWILI

107

kutokana na sifa zake katika Chama na kwa madhumuni ya Chama


ya kuendeleza kazi zake za kuongoza Taifa kama Chama.

144. Wakati huo huo Chama kitaimarisha mafunzo ya siasa ya Chama


ya aina ya pili kwa ajili ya taasisi kama majeshi, shule na vyuo,
wafanyakazi, vijana pamoja na wataalamu na Wakuu wa kazi wa
viwango na taasisi mbalimbali. Kwa utaratibu, mafunzo ya aina hii
huendeshwa kwenye taasisi zenyewe na kusimamiwa na Chama.

145. Mafunzo haya ya siasa ya Chama yatatumika pia kuwatambua wale


wenye sifa za kada wa Chama. Wale watakaobainika kuwa wana
mwelekeo huo basi wataingizwa katika utaratibu wa kupatiwa
mafunzo zaidi katika vyuo vya Chama. Hii ina maana kuwa maafisa
wa serikali na mashirika yake hata wafanyakazi katika sekta ya
kibepari walio wana CCM wakijitokeza katika mafunzo ya Chama
ya taasisi zao kwa kuwa wana sifa za kada wa Chama watafanyiwa
mpango ili inapotokea nafasi wajiunge na vyuo vya Chama.

(2) Kuimarisha muundo, demokrasi na utendaji wa Chama

146. Vyama hujipa muundo unaowesesha shughuli zake kutekelezwa


kwa nidhamu na ufanisi. Kwa madhumuni hayo vyama hujipa
vikao vya aina tatu hivi katika kila kiwango: Kikao cha aina ya
Mkutano Mkuu ambacho ni cha wajumbe wengi na ndicho kikao
kinachotoa mwelekeo na kupanga siasa na mambo makubwa ya
kutekelezwa katika kipindi kirefu kifuatacho. Vikao vya aina hii
hukutana baada ya kipindi kirefu kupita. Kikao cha aina ya pili
ni kipana na kina wajumbe wengi na ndicho kinachoongoza na
kusimamia utekelezaji na maamuzi ya mkutano mkuu. Mwisho
huwa kuna chombo kidogo cha wajumbe wachache ambao huunda
Kamati ya Utendaji ya kikao kikubwa cha aina ya pili.

147. Sasa, utaratibu wa zamani wa TANU na wa ASP ulikuwa na


mfumo wa aina hii. Na uzoefu tulioupata hadi sasa unadhihirisha
ubora wa mfumo wa aina hii maana unaunganisha mahitaji ya
demokrasi pana ya vikao vya aina ya kwanza na ya pili na wakati
huo huo unarahisisha utendaji kwa kuwa na kamati ya utendaji
108

MIONGOZO MIWILI

ya Wajumbe wachache watakaokabidhiwa majukumu ya utendaji


siasa wa kila siku. Chama kitachukua hatua za kurekebisha
muundo wake wa sasa ili kulifikia lengo hili katika ngazi zote za
Chama.

148. Imedhihirika pia kuwa kuna umuhimu kwa sasa wa kuimarisha


demokrasi ya Chama katika kiwango cha Taifa na baadaye katika
viwango vya chini yake. Hali ilivyo kikatiba hivi sasa ni kuwa
wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ni mchanganyiko wa
wanaochaguliwa na wanaoteuliwa. Wakati umefika wa kuimarisha
demokrasi ya Chama kwa kurekebisha Katiba ili wajumbe wote
wa Halmashauri Kuu ya Taifa watokane na uchaguzi wa Chama.

149. Hatua nyingine inayohitaji kuchukuliwa ili kuimarisha Chama


inahusu kuunganisha uongozi wa Chama yaani wa Halmashauri
Kuu ya Taifa na utendaji kazi wa Ofisi yake yaani Makao Makuu ya
Chama. Mfumo wa hivi sasa una hitilafu inayoathiri kazi za Chama.
Kwa mujibu wa mfumo huu viongozi kazi yao ni kuamua katika vikao
na halafu kuna watendaji ambao ni maafisa waajiriwa wa Chama
wa kutekeleza maamuzi hayo. Chama kitaurekebisha utaratibu huu
(pamoja na mfumo wa sasa wa Kamati za Kamati Kuu) kwa kuweka
utendaji kazi za Halmashauri Kuu ya Taifa chini ya makatibu wa
Halmashauri Kuu ya Taifa yenyewe. Kazi muhimu za Halmashauri
Kuu ya Taifa ni pamoja na Elimu, Uenezi na Itikadi ya Siasa, Uchumi
na Mipango, Organaizesheni, Ulinzi na Usalama, Uhusiano na Nchi za
Nje na Nidhamu na Udhibiti. Utaratibu huu utahusu Mikoa, Wilaya na
Matawi kwa hatua zitakazoamuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa.

(3) Kuimarisha uongozi wa Chama katika sehemu za kazi

150. Kuanzia sasa Chama kitahakikisha kuwa serikali inachukua hatua


za kuuwezesha utaratibu wa malengo ya utoaji mali kutumika
katika viwanda na mashirika yake na kuinua uwezo wa utoaji
huduma wa vyombo vyake. Wakati huo huo Chama kitahakikisha
kuwa wakuu wa kazi wanasaidia kisiasa ili wawe na msimamo wa
kizalendo utakaoimarisha uwezo wao wa kitaalamu.
MIONGOZO MIWILI

109

151. Hata hivyo, kazi kubwa ya Chama katika sehemu ya kazi itafanywa
na tawi la Chama la mahali pa kazi panapohusika. Kazi ya Chama
katika Taifa, Mkoa na Wilaya ni kuunda hali itakayoliwezesha Tawi
la Chama kutekeleza wajibu wake wa uongozi. Ili kuhakikisha
kuwa Chama katika sehemu ya kazi kinashika nafasi yake ya
uongozi kuna masuala kadhaa ya kutia maanani.

152. La kwanza ni kuwa suala la umuhimu wa kwanza kwa Chama katika


mahali pa kazi katika mazingira ya nchi inayojenga ujamaa ni kuleta
mafanikio ya utekelezaji wa kazi. Hivyo, jitihada ya Chama katika
sehemu ya kazi ni kuhakikisha kuwa wanachama na viongozi wa
chama wanakuwa katika msitari wa mbele katika kutimiza wajibu
wao wa kazi na kuona kuwa malengo yaliyowekwa yanafikiwa. Ni
mwiko kwa mwanachama wa CCM au kiongozi kuwa miongoni
mwa wategaji, wavivu na wazoroteshaji kazi.

153. Jambo la pili ni kuwa vyama vya kijamaa halisi haviongozi kwa
mabavu bali kwa kuelimisha, kushawishi, kuelekeza na kwa
chama chenyewe kuonyesha njia kwa vitendo. Kwa hiyo, kazi ya
Chama katika sehemu za kazi itakuwa kuwajenga wana CCM kujua
namna ya kuwashirikisha wafanyakazi wenzao katika kutekeleza
malengo na wajibu wa kazi kutokana na mfano wao wenyewe
wa kutekeleza wajibu kwa makini na kwa ari na uwezo wao wa
kushawishi, kushauri na kuwashirikisha wafanyakazi.

154. Jambo la tatu la kuzingatia kuhusu suala la uongozi wa Chama


katika sehemu za kazi ni kuwa ujuzi ni madaraka. Watu wana
tabia ya kumsikiliza anayejua zaidi kuliko wao juu ya suala fulani.
Sasa, mahali pa kazi ni mahali penye ujuzi wa aina mbalimbali.
Atakayejitokeza kuwa anajua zaidi katika fani fulani wenzake
humheshimu, humtegemea na kumsikiliza. Chama kitahakikisha
kuwa katika siku za usoni wanachama wa CCM wanajiendeleza
katika fani zao za kazi ili kuwa miongoni mwa wanaotegemewa na
kusikilizwa na wafanyakazi wenzao katika fani zao za kazi.

155. Jambo la nne linahusu matatizo ya kila siku ya wafanyakazi.


Kiongozi, pamoja na sifa nyingine, ni mtu mwenye kuyaelewa
110

MIONGOZO MIWILI

matatizo ya watu na anayejua vile vile kuyaelezea na kuyajengea


hoja. Chama kitahakikisha kuwa wanachama wa CCM wanaaminiwa
na wafanyakazi wenzao kwa kuwa wanayaelewa matatizo yao
na wana uwezo wa kuyaelezea kwa ufasaha na kushirikiana nao
katika kutafuta jawabu. Ili kufikia hapo Wana CCM watawajibika
kujiendeleza katika nadharia ya Chama na elimu kwa jumla.

156. Suala linarudia pale pale tulipoanzia. Kwa Chama cha Mapinduzi
kuongoza mapinduzi katika sehemu za kazi, kazi ya msingi ni
kuwaandaa wanachama na viongozi wa matawini kwa mafunzo
thabiti ya siasa ya Chama; ni kwa Chama kuhakikisha kuwa katika
kila sehemu ya kazi viongozi wa Chama waliopo na wanachama
kwa jumla wanapata miongoni mwao kada wa Chama wenye
uwezo wa juu wa uchambuzi na mbinu watakaosaidiana nao
katika mawimbi ya harakati. Hii ndiyo kazi kubwa ya Chama
katika siku zijazo.

K.m. katika jitihada za kuimarisha uongozi wa chama katika


majeshi, miradi muhimu ya Taifa na taasisi, Chama kinaweza
kuteua kamisaa wa siasa na kumpeleka katika sehemu hiyo. Kazi
yake ni kusaidiana na uongozi uliopo kuimarisha utekelezaji wa
majukumu, kuendeleza nidhamu na kwa kusaidiana na Chama
katika sehemu hizi, kuuinua mwamko wa siasa na wa uzalendo wa
wapiganaji, wafanyakazi au wanafunzi na kuwaongezea ari katika
utekelezaji wao.

Matawi na Mashina ya kazini na mijini


kuimarishwa

157. Ili Chama kitimize wajibu wake wa kuongoza katika sehemu za


kazi tegemeo lake kubwa ni wanachama. Lakini wanachama pia
wanategemea muundo wa mashina na matawi uliopo. Hivi sasa
kuna matawi ambayo wanachama wao ni wengi mno kwamba
uwezekano wao wa kufahamiana na kushirikiana ni mfinyu mno.
Katika siku zijazo Chama kitahakikisha kuwa katika sehemu za
kazi suala la kuwaunganisha wanachama katika mashina linatiliwa
MIONGOZO MIWILI

111

mkazo zaidi. Wakati huo huo utatazamwa uwezekano wa kuunda


matawi zaidi ya moja katika sehemu za kazi zenye wanachama wa
CCM wengi mno.

158. Aidha, Chama kitalishughulikia suala la matawi ya Chama ya Kata


za Mijini. Katika hali ya sasa matawi mengi ya kata za mjini ni
makubwa kiasi kwamba wanachama hawawezi kujihusisha kwa
ukamilifu katika matawi yao.

(4) Kuimarisha Chama kwa kuimarisha uongozi

159. Kiongozi wa Chama cha Mapinduzi kwanza kabisa lazima awe na


msimamo wa kijamaa. Itikadi yake ya ujamaa, vitendo na tabia yake
vijidhihirishe kwa wanaowaongoza, wanachama na wananchi,
kuwa ni vya kijamaa. Imani ya kiongozi inaambukiza na kuimarisha
imani ya anaowaongoza. Lakini kiongozi anayegunduliwa na
anaowaongoza kuwa ni mnafiki kwa msimamo ni adui mkubwa
kwa Chama maana anawavunja moyo wanachama, anawavuruga
wananchi na kuunda hali itakayowafanya wananchi wasiwe na
imani na viongozi wengine na Chama. Hivyo suala la viongozi wa
Chama kuwa na msimamo sahihi kwa itikadi na katika maisha
ya kila siku ni jambo lenye umuhimu wa kwanza kwa Chama cha
Mapinduzi.

160. Lakini pia msimamo thabiti wa ujamaa wa kiongozi uambatane


na uwezo wa kuongoza. Tumetamka hapo juu katika Mwongozo
huu kuwa Chama cha Mapinduzi hakiongozi kwa mabavu bali kwa
kuelimisha, kuelekeza, kushauri, kushawishi na kushirikiasha.
Hii ina maana kuwa kiongozi wa Chama hana budi awe na uwezo
wa kushauri na kuelimisha, kushawishi na kushirikisha, kwa
jumla awe na uwezo wa kuieneza na kuitetea siasa ya Chama
na kuwaunganisha wanachama na wananchi katika harakati za
kujenga ujamaa nchini na kwa kiwango cha uongozi wake.

161. Kutokana na hayo, Chama kuanzia sasa kitalipa uzito suala la


msimamo na uwezo wa viongozi wake. Ndiyo kusema kwamba
112

MIONGOZO MIWILI

katika siku za usoni uchambuzi wa viongozi waliopo na waombao


nafasi za uongozi utasisitiza juu ya msimamo wao kwa itikadi na
kwa vitendo pamoja na uwezo wao wa kumudu uongozi huo.

162. Chama kitatumia njia mbali mbali za mafunzo ili kuwasaidia


viongozi wenye nia njema kuimarisha msimamo wao kiitikadi.
Chama pia kitakuwa na utaratibu wa kuwasaidia viongozi wenye
msimamo sahihi lakini uwezo mdogo wa kuongoza kupata nafasi ya
kuendeleza uwezo wao. Lakini Chama kitahakikisha kuwa viongozi
ambao msimamo wao kwa itikadi na kwa vitendo ni kinyume cha
misingi ya ujamaa hawapewi nafasi ya kukihujumu Chama kutoka
ndani ya Chama. Wakati huohuo Chama kitahakikisha pia kuwa
suala la uwezo linakuwa sehemu muhimu ya uchaguzi au uteuzi
wa viongozi wa Chama cha Mapinduzi.

(5) Maandalizi ya waombaji unachama

163. Chama kitaendelea kupokea wanachama wapya isipokuwa


kwamba kuanzia sasa suala la wanachama litekeleze kwa vitendo
agizo la Azimio la Arusha kuhusu ubora wa wanachama badala
ya wingi wao. Wakati huo huo, jitihada zitafanywa ili kuhakikisha
kuwa idadi ya wanachama wanawake, wakulima, wafanyakazi na
vijana inafanana na nafasi yao halisi katika jamii yetu.

Mafunzo kwa waombaji uanachama

164. Mwelekeo na mkazo wa mafunzo ya wanachama wapya


yatafanyiwa mabadiliko ya kimsingi. Mwanachama wa CCM kwa
mujibu wa Mwongozo huu atapimwa kwa vitendo vyake vya
kutekeleza siasa ya Chama katika maisha yake ya kila siku. Vivyo
hivyo, mtu anayeomba kuwa mwanachama wa CCM itabidi apewe
kipindi cha majaribio ambapo atapimwa kuhusu kufaa kwake
kuingia katka Chama kwanza kabisa kwa vitendo vyake vya
kutekeleza siasa ya Chama. Aidha, atawajibika kuhusika na shina
na tawi ambalo ndilo litakalompangia majukumu ya kichama ya
kuyatekeleza na ndiko atakakokuwa akijadiliwa hatua kwa hatua
MIONGOZO MIWILI

113

na uamuzi kufanywa kuhusu kuingizwa au kutoingizwa katika


Chama wakati utakapofika.

(6) Kuimarisha Chama kifedha

165. Pamoja na kuimarisha usimamizi wa Fedha za Chama, Chama


kitachukua hatua thabiti za kujiimarisha kwa kujiongezea mapato.
Mambo matatu yanakusudiwa kufanywa: -

Jambo la kwanza ni kuwa Chama kitaimarisha udhibiti wa fedha


zake. Jambo la pili ni kuwa kitawataka wanachama na viongozi wa
CCM kutoa mchango wa hiari wa kuimarisha Chama kwa kiwango
cha asilimia itakayoamuliwa ya mshahara wa kila mwezi kwa kila
kiongozi na mwanachama. Utaratibu wa aina hiyo utabuniwa kwa
ajili ya wanachama wakulima na wanaojiajiri wenyewe. Hatua ya
tatu ni Chama kutafuta njia nyingine za kudumu za kukiwezesha
kuongeza mapato yake.

(7) Kuimarisha Jumuia za Wananchi

166. Jumuia za wananchi zina umuhimu mkubwa sana kwa Chama


katika malengo na mbinu zake za mapambano. Pamoja na kuwa
vyombo vinavyowaunganisha wananchi wenye hali inayofanana
katika shughuli zao za kazi za kila siku au wananchi wanaofanana
kwa maumbile ili kuendeleza maslahi yao, Jumuia za wananchi pia
ni mikondo inayokiwezesha Chama kuufikia umma wa wananchi
kwa fikra, msimamo, maelekezo na miito mbalimbali.

167. Katika hali hii Jumuia za wananchi zinaweza kuwa vyombo muhimu
vya mapambano ya Chama na kuwa nguvu zake za akiba. Katika
kipindi kinachoanzia sasa, Chama kitajitahidi kuzijenga jumuia
kwa kushirikiana nazo ili ziweze kuwa nguvu thabiti za mapinduzi
ya kujenga ujamaa. Papo hapo, Chama kitahakikisha kuwa Jumuia
za wananchi zinapata msaada utakaoziwezesha kushirikiana na
Chama bila ya kupoteza uwezo wao wa kuziendesha shughuli zao
wenyewe bila ya kuingiliwa.
114

MIONGOZO MIWILI

168. Kwa sasa, wakati Chama kinaanzisha vuguvugu la mapinduzi la


mijadala ya kujikosoa na kukosoana kwenye Chama katika matawi
yake, Jumuiya zichukue nafasi hii kushiriki kwa ukamilifu katika
harakati hizi. Chama kitawataka wana CCM wote kuwa katika
mstari wa mbele katika vuguvugu la kuleta mwamko wa siasa
katika Jumuia zao. Ni wajibu wa kila mwanachama wa jumuiya
hizo kujiunga na Jumuiya zinazomhusu kueneza siasa ya Chama
miongoni mwa wanachama wa Jumuiya hizo na kuwashawishi
wananchi wengine kujiunga na Jumuiya.

MWISHO

MIONGOZO MIWILI

115

SURA YA NNE
MAAMUZI YA ZANZIBAR, 1991
(Hotuba ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Ali Hassan Mwinyi wakati
akizungumza na wazee wa chama, viongozi wa taifa, mashirika ya umma
na watu binafsi juu ya ufafanuzi wa maamuzi ya Halmashauri Kuu ya
Taifa katika kikao chake cha Zanzibar: Diamond Jubilee Dar es Salaam,
tarehe 25/2/1991)

Ndugu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Mkoa wa Dar es Salaam,


Ndugu Katibu Mkuu,
Ndugu Mwenyekiti wa Wazee wa Dar es Salaam,
Ndugu Viongozi wa Chama na Serikali na
Ndugu zetu waalikwa,

Kabla ya yote, labda niseme kwamba kwa kuwa tumo katika mwezi wa
pili tokea kuanza kwa mwaka mpya, nami sijapata nafasi ya kukutana
nanyi wazee, ni vyema nitumie nafasi hii kwanza kukutakieni heri ya
mwaka mpya, na baraka zote za mwaka 1991. (Makofi). Ninakuombeeni
uzima, nguvu, baraka na mafanikio.
Pili, tuna kawaida katika nchi yetu, kwamba kila linapotokea jambo
muhimu katika Taifa, tunatafuta nafasi ya kukutana nanyi na kukuelezeni.
Hivyo, leo napenda kuzungumza nanyi wazee wa Dar es Salaam na, kupitia
kwenu, iwe ninazungumza na Wazee wenzenu wa Tanzania nzima. Kwa
hiyo, hayo nitakayokuambieni nyinyi, ninawaambia pia Wazee wa Taifa
letu wote kwa jumla.
Hivi karibuni Halmashauri Kuu ya Taifa ilifanya kikao chake cha
kawaida Zanzibar, ambacho kilijadili mambo mbalimbali. Kikao hicho
kilimalizika kwa kutoa maamuzi maalum. Maamuzi hayo yana uzito
mkubwa. Inaelekea baadhi yetu, pamoja na Vyombo vyetu vya Habari,
hatukuyaelewa vizuri maamuzi hayo. Kwanza, nataka nivivue lawama
Vyombo vyetu vya Habari. Maana hatukuwa nao huko. Kwa hivyo
walitangaza vile walivyoelewa. Kwa sababu hiyo nimeona ni vyema
116

MIONGOZO MIWILI

kuzungumza nanyi ili kusahihisha matangazo ya vyombo vyetu. Nimeona


ni vyema kutumia nafasi hii kutoa ufafanuzi.

LAZIMA TWENDE NA WAKATI

Inaelekea kuna hofu kwamba Azimio la Arusha linageuzwa. Kwa hiyo,


tokea mwanzo, kabla ya kusema lolote, nataka tuelewane kwamba siasa
yetu bado ni ile ile ya Ujamaa na Kujitegemea. (Makofi). Haikugeuka wala
hatutazamii kuigeuza. Kwa hali yoyote sisi Wanachama wa Chama Cha
Mapinduzi hatutaigeuza Siasa hii. (Makofi). Kule Zanzibar tulizungumza
mambo mengi, miongoni mwao, ni kutoa tafsiri ya baadhi ya vipengele
vya Azimio ili vifanane na wakati tulionao.

Azimio la Arusha, kama tunavyojua, limetangazwa mwaka 1967. Hii


leo tuko katika mwaka 1991. Imepita miaka mingi, zaidi ya 20 tokea
kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Na katika kipindi cha miaka 20
yametokea mabadiliko mengi duniani na pia katika hali ya maisha
yetu. Hali yetu ya sasa, hasa ya kiuchumi, siyo ile ile ya mwaka 1967.
Ndio maana mishahara ya wafanyakazi ingawa imeongezeka sana
lakini bado haikidhi mahitaji yao - haiwatoshi hata wale wanaopokea
mishahara mikubwa miongoni mwetu. Isitoshe, wakati wa Azimio idadi
ya Watanzania ilikuwa ndogo. Sasa hivi idadi yetu imeongezeka zaidi ya
mara mbili. Kwa sababu ya wingi wetu mahitaji yetu nayo yemeongezeka
sana, wakati mapato yetu yamekuwa yakipungua wakati wote.
Kwa hivyo ni dhahiri kwamba jamii ya Tanzania lazima itie maanani
mabadiliko haya na ijiandae kwenda na wakati. Kama hatukwenda na
wakati, kazi yetu itakuwa ni kufukuzia wakati - jambo ambalo hatulimudu.
Tabia ya wakati ni kama ile ya bahari. Bahari inakupwa na kujaa mpaka
ukingoni mwa maji. Baadaye maji huopwa polepole, mpaka kufika
wakati ikawa maji yote yamekwishaondoka ufukoni. Samaki werevu
huondoka nayo hayo maji, yaani yakijaa huja nayo, yakitoka hutoka nayo,
vinginevyo hupwelewa. Samaki watakaozembea kufuata maji watajikuta
wamechelewa wanatapatapa juu ya mchanga wakati maji hayo hayapo.
Hiyo ndiyo maana ya kupwelewa (Makofi).
Hapa Afrika, kwa mfano, imeanzishwa mipango mbalimbali ya
MIONGOZO MIWILI

117

ushirikiano wa uchumi. Mipango hiyo ni pamoja na Ushirikiano wa


Nchi za Kusini mwa Afrika (SADCC) na Eneo la Soko Nafuu (PTA). Afrika
pia imeazimia kuunda Jumuiya ya Uchumi. Nchi zinazoendelea nazo
zimedhamiria kuzidisha ushirikiano miongoni mwao. Nchi yetu lazima
ifanye mabadiliko ili iweze kushiriki kwa ukamilifu katika shughuli zote
hizo zinazosaidia maendeleo yetu.

KILA ZAMA NA MWONGOZO WAKE

Ndugu Wazee, Msahafu wa Waislam unasema LIKULLI AJALIN KITABU


Mwingereza mmoja kaitafsiri aya hiyo hivi: TO EVERY AGE ITS BOOK
yaani Kila zama ina Kitabu (Mwongozo) chake. Na sisi Wana-CCM
tunakubali kuwa kila Zama zinahitaji kuwa na Mwongozo wake. Azimio
la Arusha ni Mwongozo wetu wa msingi. Ni dira inayoongoza mwelekeo
wa jamii yetu. Lakini tafsiri zake zinabidi zirekebishwe kila inapohitajika
ili zisipitwe na wakati. Miongozo ina tabia moja: inakuja ili kufafanua,
kuelekeza au kukemea hali mbaya inayojitokeza.
Mojawapo ya malengo ya maamuzi ya Zanzibar ni kutoa tafsiri sahihi
ili kupunguza kebehi inayofanywa dhidi ya siasa yetu ya Ujamaa na
Kujitegemea na pia kwenda na wakati.

Mwaka 1967 lilitangazwa Azimio la Arusha. Mwaka 1971 ulifuatiwa


na tamko la Iringa la Siasa ni Kilimo. Tamko hili lilikuwa ni mbinu na
msisitizo wa Siasa yetu ya Kujitegemea. Lilipanua tafsiri ya Azimio la
Arusha. Katika mwaka 1981 ilionekana kuna haja ya kutolewa mwongozo
mwingine kulingana na wakati ule ambao nao ni upanuzi wa tafsiri ya
Azimio. Ulitangazwa ili kukidhi haja ya wakati ule.
Aidha, kabla ya hapo, katika mwaka 1974, Chama kilipitisha Agizo
la Musoma kuhusu Elimu ya Kujitegemea ambalo madhumuni yake
yalikuwa kutazama upya suala la uingizaji wanafunzi Chuo Kikuu na
kupanua Elimu ya Msingi ili kutoa fursa kwa watoto wote wenye umri
wa kwenda shule kufanya hivyo.
Maandiko yote hayo hayakupingana na Azimio la Arusha ila yakiongeza
mwangaza kwa mambo ambayo yalihitaji yafanane na wakati wake. Na
lazima iwe hivyo, kwani bila ya kwenda na wakati tungechekesha.
118

MIONGOZO MIWILI

Kwa mfano wakati wa Azimio la Arusha, mtakumbuka kuwa tafsiri


ya neno Kiongozi ni pamoja na yule mwenye mshahra uliofikia
shilingi 1,066/= kwa mwezi. Tungengangania tafsiri hii tu, basi leo
pasingekuwapo wafuasi. Wafanyakazi wote wangetafsirika kuwa ni
viongozi wa CCM. Kwani ukiacha wakulima, wafanyakazi wote sasa kwa
tafasiri ya 1967 ni viongozi tena maradufu. Maana kima cha chini sasa ni
Sh.2,500/=, ambazo ni zaidi ya mara mbili ya Sh.1,066/=. Ndiyo maana
tukasema jamii yetu italazimika kufanya marekebisho kila inapokuwa
lazima kufuatana na wakati. Tutafanya hivyo bila ya kuachana na misingi
ya siasa yetu.
Kwa hivyo, tulichokifanya kule Zanzibar ni kupanua tafsiri za Azimio
ili ilingane na wakati tulionao. Kufanya hivyo si kuua Azimio bali ni
kuliimarisha.

CHIMBUKO LA AZIMIO LA ARUSHA

Historia ya Azimio la Arusha tunaijua sote. TANU ilipigania kwa


maneno mpaka nchi ikapata UHURU wake. Tanganyika ilipopata Uhuru
na tukaanza kujitawala ishara potofu zilianza kuchomoza. Baadhi ya
viongozi walianza kuutumia uongozi wao kama mradi wa kujineemesha.
Kwa kutumia nyadhifa zao, wakikopa fedha benki na kuanza kujijengea
mashamba - si ya miti - bali ya majumba; si nyumba za kuishi tu bali
majumba mengi ya kupangisha.

Tabia hiyo ilizusha manunguniko ya watu. Jamii ilianza kugawanyika


makundi mawili; manaizi na makabwela. Kitendo hicho ndio chimbuko
la kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Azimio lilikuja kutoa mwongozo wa
maadili ya wanachama na viongozi wa TANU. Kwa hivyo nia ya Azimio la
Arusha, miongoni mwa mambo mengine, ilikuwa ni kuwazuia viongozi
kutumia uongozi wao kujitajirisha. Hilo ndilo lililokuwa tatizo la hatari
miongoni mwa matatizo wakati ule. Azimio lilikuja kuokoa jahazi kukemea tabia potofu.

MIONGOZO MIWILI

119

TATIZO LA SASA NI UCHUMI TEGEMEZI


Mtu anaweza kuuliza je sasa kuna tatizo gani? Tatizo letu katika miaka ya
tisini na kuendelea ni lile la uchumi tegemezi. Tatizo letu sasa ni kwamba
uchumi wetu ni duni mno. Wakati idadi yetu inaongezeka, mapato ya
Taifa, hasa ya fedha za kigeni, hayaongezeki. Wakati wa Uhuru idadi
yetu ilikuwa ni watu milioni tisa. Lakini leo, tuko milioni tisa na tisa tena
na nusu ya tisa. Lakini mapato yetu ya pesa za kigeni yapo pale pale, $
milioni 400. Wakati Azimio la Arusha lilitutaka tujitegemee, hali halisi ni
kuwa tumekuwa wategemezi wakubwa. Maana Taifa letu hivi sasa, kwa
pato lake lenyewe la fedha za ndani, linaweza kujitegemea kwa kipindi
cha miezi saba tu katika mwaka. Tunategemea watu wengine, kwa njia ya
ruzuku na mikopo, kumalizia miezi mitano inayosalia katika mwaka. Hii
ni hatari. Lazima tuendelee kubuni mbinu za kuondokana na hali hiyo.

MBINU ZA KUJITEGEMEA

Ilani ya Uchaguzi inasema hivi:

Makusudi ya Chama katika kipindi cha miaka


mitano ijayo ni kwa Taifa kukusanya nguvu zote za
wananchi kwa kusaidiana na Serikali zao (Mbili), na
kuzitumia katika kila eneo la maendeleo ili kutoa
msukumo mpya wa utekelezaji wa siasa ya Ujamaa
na Kujitegmea.

Hivyo, Chama na Serikali zake zinawajibika kuwarahisishia wananchi


wao kujitegemea kwa chakula, kujitegemea kwa mavazi na kujitegemea
kwa malazi. Ili kutimiza lengo hilo Taifa lazima liwawezeshe wananchi
wake kuzalisha mazao ya biashara na chakula kwa wingi. Pia ni wajibu
wa Chama na Serikali kuandaa mbinu za kuwasaidia wananchi kujijengea
nyumba zao za kuishi ili ziwasitiri wanapostaafu au kuwa wazee.
Je wananchi wakituuliza: hivi ni mbinu gani mlizofanya kumshirikisha
kila mmoja wetu kutumia nguvu zake zote katika kuzalisha kama Ilani
inavyosema? Tungejibu nini? Lakini sasa kila mwananchi, pamoja na
mwana CCM, hataweza kutoa kisingizio kwa kusema:120

MIONGOZO MIWILI

Mimi sikuweza kutumia nguvu zangu zote katika


kufanya kazi ya kuzalisha kwa sababu nimezuiwa na
Azimio la Arusha.

MWANACHAMA KUCHANGIA UCHUMI KIKAMILIFU


Azimio la Arusha lipo. Narudia tena kusema kuwa wanaohusika
na tafsiri hii ni wanachama. Sisemi Viongozi, bali wanachama wa
CCM. Tunataka kumpa Mwanchama wa CCM, kama mwanachama
mwingine yeyote, uhuru zaidi wa kuzalisha ili kuchangia kadiri
ya uwezo wake katika pato lake yeye mwenyewe na pato la Taifa
kwa jumla.

Ili tujitoe, kitaifa, kwenye shimo la utegemezi tulimo hivi sasa, mbinu
bora ni kutoa uhuru kwa kila mwananchi wa kila Kaya, wa kila Kata, wa
kila Tarafa, wa kila Wilaya na wa kila Mkoa kutumia nguvu zake zote
katika kuzalisha. Matokeo ya hatua hii ni kumwezesha kila mtu katika
Kaya, Kata, Tarafa, Wilaya na Mkoa kujitegemea. Tukifika hapo ndipo
Taifa litapokuwa limeondokana na hali ya sasa ya uchumi tegemezi.

KUPANGISHA NYUMBA

Jambo la kupangisha nyumba nalitaja tu, kwani si lazima kwa sababu si


jipya; hata hivyo ni vyema nalo litajwe. Mwenyekiti Mstaafu alilisemea
jambo hili mahali pengi sana, tena alianza zamani kulisemea, sijui. Kwa
mfano, hivi karibuni alilitaja tena katika hotuba yake ya kuadhimisha
miaka ishirini ya Azimio aliposema hivi:
Masharti hayo yanamkataza kiongozi wetu kuishi
kikabaila kwa mbinu za kupangisha majumba.

Lakini sharti hili halimkatazi mtu mwenye


vyumba vya ziada katika nyumba yake anamoishi
kuvipangisha kwa watu wengine kwa kodi nafuu,
Hili ni jambo la kawaida kabisa katika nyumba
zetu za Waswahili na upangishaji huu mimi
MIONGOZO MIWILI

121

nimekuwa nikiutetea tangu zamani. Utaratibu


huu unawasaidia sana watu wenye mapato madogo,
wanafunzi, au wafanyakazi ambao bado hawajaoa
au kuolewa kupata vyumba vya kupanga kwa kodi
nafuu.

Ni kweli kwamba huko nyuma tumekuwa wakali


mno katika kutafsiri msharti haya.

Azimio la Arusha linachokataa ni unyonyaji. Hivyo maskini ya Mungu


mwenye kijumba chake cha mbavu za mbwa akimwona maskini
mwenziwe anapata taabu, hana pakukaa, asimpangishe? Je akimpangisha
atakuwa anamnyonya? Au anamstiri? Kwa hiyo tangu zamani kustiriana
ni ruhusa (Makofi).
Hatukuishia hapo kule Zanzibar, tulikwenda zaidi, tulisema pia kwamba
wapo viongozi miongoni mwetu ambao baadhi yao wamefanya kazi za
Chama au za Serikali kwa miaka 30 au zaidi. Lakini hawana nyumba;
ukifika wakati wao wa kustaafu viongozi hao huwa wanababaika kwa
kutojua wataishi wapi. Ndipo wanapoanza kutafuta mbinu - ndiyo maana
siku hizi utakuta misururu mirefu katika Ofisi ya Vyeti vya kuzaliwa.
Watu wanakwenda kubadilisha tarehe zao za kuzaliwa, kujifanya bado
wangali vijana ili wachelewe kustaafu. (Makofi).

Sisi tunaamini kwamba baada ya kipindi kirefu cha utumishi, mtu aweze
kuwa na nyumba ili, hata akiwa kipofu angalau aweze kupapasa kuta
zake na kusema: Hii ni nyumba yangu niliyoipata kwa jasho langu la kazi
ya miaka 30. Tunataka awe na kitu. Lakini, Ndugu Wazee, bahati nzuri
wanachama wa CCM, kama wananchi wengine, wanaruhusiwa kukopa.
Wanaweza kukopa kwenye benki zetu wakajenga nyumba za kukaa. Sasa
jamani tukisema kwamba hata mtu aliyekopa asiipangishe nyumba hiyo
atalipia nini huo mkopo?
Vinginevyo tutakuwa tunamfanyia mzaha mtu huyo. Maana
atachukua mkopo, ajenge nyumba, kisha ashindwe kulipa huo mkopo.
Waliomkopesha wataikamata hiyo nyumba na kuiuza ili kurudisha
fedha yao. Katika hali hiyo mwana-CCM gani atakayekuwa na nyumba
122

MIONGOZO MIWILI

iwapo mwisho wake ni kuchukuliwa na kile chombo kilichomkopesha?


Kwa hivyo nasema mtu kama huyu ana dharura; ana dharura ya deni.
Amejenga nyumba kwa nia ya kukaa mwenyewe lakini ana deni la
mkopo. Kama anaweza kukaa nyumbani mwake, akae. Lakini pia awe na
ruhusa ya kupangisha nyumba yake, akitaka, ili imsaidie kulipa mkopo.
Anapostaafu awe anayo nyumba ya kumstiri uzeeni. Kitendo hicho
kisimpotezee uanachama wake wa CCM.

Kwa hivyo Ndugu Wanachama, huko ndiko kwenda na wakati, vinginevyo


tutapwelewa. Mtu kama huyu aruhusiwe kupangisha nyumba yake, iwe
nusu ya nyumba, ama robo ya nyumba au yote (makofi).

BIASHARA YA KUPANGISHA MAJUMBA BADO


NI MWIKO

Lakini kikao cha Zanzibar hakikutengua miiko ya kiongozi wala ya


mwanachama wa CCM. Bado ni mwiko kwao kuwa na biashara ya
kupangisha majumba. Kwa mfano, kama kuna mwanachama anayeomba
mkopo, akipata anajenga nyumba, halafu anaikodisha, akipata fedha za
kodi anajenga nyingine mpya, ambayo nayo anaikodisha na kuendelea
kujenga nyingine. Huyo ni mfanyabiashara. Kazi yake ni kujenga na
kupangisha majumba. Kikao cha Zanzibar hakikusudii mwanachama wa
aina hii. Huyu siye (Makofi).

Vile vile, Mwanachama wa CCM, hata akiwa kiongozi katika mazingira


maalum, aruhusiwe kukodisha nyumba yake, ikiwa haihitaji kuikaa
wakati ule. Inawezekana haihitaji kuishi katika nyumba yake kwa kuwa
kapata uhamisho. Mfano, mtu kahamishiwa Iringa kwa kazi wakati
nyumba yake iko Dar es Salaam. Je ikae bure watu waitumie bure tu
kweli? (Makofi).
Ni mwanachama wa aina hii ndiyo tulisema huko Zanzibar kuwa
aruhusiwe kupangisha nusu ya nyumba ama robo ya nyumba au yote,
maadam mtu huyo anapo pengine pa kukaa. Lakini tunasisitiza kuwa
bado si ruhusa kwa mwana CCM wala kiongozi wa CCM kuendesha
biashara ya kupangisha majumba.
MIONGOZO MIWILI

123

HISA KATIKA MAKAMPUNI YA UMMA,


KUPUNGUZA UKWASI!
La pili lililoamuliwa huko Zanzibar ni kuwaruhusu wanachama wa CCM,
kwa kufuatana na hali ya wakati ulivyo, sasa aruhusiwe kuwa na hisa
katika kampuni ya Umma. Hii leo tunayo Mashirika ya Umma zaidi ya
400, lakini mengine yao hayana fedha za kuendeshea kazi zao.

Mfano kuna mwananchi mmoja alikwenda kwenye kiwanda cha


Umma kutaka huduma ya kusafishiwa ngozi zake. Alipofika hapo
alikuta pamelala paka; yaani palikuwa kimya, hapakuwa na kazi
yoyote inayofanyika. Kumbe kile kiwanda kilikuwa kimefungwa kwa
kukosekana fedha za kukiendeshea ... umeme ulikatwa na wafanyakazi
walipewa likizo.
Meneja alimfahamisha huyo mteja kuwa kiwanda kimefungwa kwa
sababu ya deni la maji na umeme pamoja na pesa za mishahara ya
wafanyakazi. Huyo mteja alikubali kulipa arubuni (advance) ya milioni
saba ili kukikwamua kiwanda. Wiki ya pili yake kiwanda kilianza kufanya
kazi zake za kuzalisha kama kawaida.
Kisa cha kiwanda hicho kusimama kazi ni kukosa fedha za kuendeshea.
Kiswahili cha siku hizi huitwa ukwasi. Kwa hiyo kazi ilisimama.

Katika hali kama hii, tumeona ni vyema kuwaruhusu wananchi wote


pamoja na wakulima, na wafanyakazi wa shirika lenyewe wakiwemo
wanachama wa CCM kununua hisa chache kwa kila atakaetaka.

UBIA WA UMMA NA DOLA KATIKA SHIRIKA


Narudia, watakaoruhusiwa kununua hisa ni wananchi wowote
watakaopenda pamoja na wakulima wa pamba, korosho, kahawa,
tumbaku na wafanyakazi wa hilo shirika lenyewe. Kwa njia hiyo,
Shirika hilo sasa litapata sura mpya, litakuwa ni la ubia kati ya Serikali,
wafanyakazi na wananchi. Fedha tunazozizungumzia hivi sasa, za kulipia
taa na mahitaji mengine zingetokana na ununuzi wa hisa ili uzalishaji
uendelee. Katika hali kama hiyo kiwanda kitakuwa ni mali ya umma
kweli. Maana kuna tofauti ya Shirika la Dola na Shirika la Umma kwa
maana ya wananchi wenyewe.
124

MIONGOZO MIWILI

Endapo shirika la umma litataka kuwashirikisha wananchi na


wafanyakazi wake kwa kulichangia ili kuondoa tatizo la Ukwasi, jambo
hilo liwe ni halali, na Mwana CCM naye aruhusiwe kuwa miongoni mwao.
(Makofi)..Kilichofanywa na maamuzi ya Zanzibar ni kumruhusu
mwanachama wa CCM naye kushiriki kikamilifu katika sera ya Taifa
ya uwekezaji wa rasilimali nchini.
Katika sera ya uwekezaji rasilimali tunaruhusu ubia katika uchumi wetu.
Ubia huo unaweza kuwa baina ya watu wa ndani ya nchi peke yao, au
kati ya wawekezaji wa nje na wa ndani. Baada ya kuikubali misingi hiyo
hatuoni kwa nini tusianzie kwa kuwaruhusu wananchi, wakulima na
wafanyakazi kuwa na hisa katika Mashirika wanayofanyia kazi (Makofi).

WAFANYAKAZI KUSIMAMIA UWAJIBIKAJI

Nia nyingine ya kufanya hivyo inatokana na kutambua kuwa wafanyakazi


wenye hisa katika kiwanda watakuwa wasimamizi wakereketwa wa
uwajibikaji katika viwanda hivyo. Watakereketwa zaidi pakiwa na
ubadhirifu au kutowajibika.
Hivi leo baadhi ya mashirika ya Umma ni mashirika ya umma kwa jina
tu. Watu wanayaibia wakidai wanachukua chao. Pengine wanashindana
kufanya hivyo ili wasipunjwe. Baadhi ya mashirika ya Umma
yanahujumiwa kana kwamba hayana wenyewe. Baada ya maamuzi ya
Zanzibar kuanza kutekelezwa, Mashirika hayo yatakuwa na wenyewe.

MWONGOZO WA 1981 KUHUSU UWAJIBIKAJI

Maamuzi ya Zanzibar si mapya. Mwongozo wa chama wa 1981 umetoa


ilani juu ya kupungua kwa uwajibikaji katika Mashirika ya Umma, jambo
ambalo hivi sasa tunalitafutia ufumbuzi. Mwongozo wa 1981 unasema
hivi:
Imezuka tabia ya aibu nchini ambayo imekuwa
ikiongezeka ya vitendo vya kuharibu na kuvitumia
vibaya vyombo muhimu vya kazi na mali ya umma
kwa jumla. Magari, matrekta, zana nyingine
muhimu za chama, serikali, mashirika ya umma

MIONGOZO MIWILI

125

mara nyingi hayadumu muda mrefu kama ambavyo


ingetazamiwa kutokana na matumzi mabaya.

Lakini ikiwa watu pale pale wenyewe wana hisa katika kampuni au
shirika - mfano TANESCO [au] kuwa Mkurugenzi katika kampuni ya
Kibepari. Napenda suala hili lieleweke vizuri ili kujibu fikra zilizojengeka
kuwa uamuzi huo umevunja Azimio la Arusha.

Kwanza inafaa tufafanue maana ya Mkurugenzi. Tafsiri ya Mkurugenzi


inayojulikana sana ni ile ya mjumbe wa bodi ya wenye hisa katika
Kampuni fulani. Kwa hiyo wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi katika
Kampuni ya Kibepari huwa ni miongoni mwa wale wenye hisa zao
katika kampuni inayohusika. Watu hao huchaguliwa na wenzao wenye
hisa kama wa kuongoza shughuli za Kampuni yao kwa faida ya pamoja.
Mkurugenzi wa aina hii hawezi kuwa mwanachama wa CCM.

Lakini kuna Mkurugenzi wa aina nyingine ambaye ni tofauti kabisa na


Mkurugenzi mwenye mali. Mkurugenzi huyu ni yule ambaye ameajiriwa
tu na wenye mali yao, kutokana na sifa zake za utaalam, kuendesha
kampuni. Mtu huyu huwa ni mwajiri tu, anayefanya kazi. Huyu ni mtumishi
tu kama watumishi wengine, hana chake katika kampuni inayohusika.
Anachotegemea ni mshahara wake na marupurupu mengine kama yapo.
Huyu ndiye Mkurugenzi anayeruhusiwa kuwa mwanachama wa CCM.
Azimio la Arusha bado liko pale pale kwa wale wakurugenzi wa aina ya
kwanza. Wao Azimio linawabana, hawawezi kuwa wanachama wa CCM.
Lakini huyu wa aina ya pili aliyeajiriwa tu, akija kuomba uwanachama
tunamkubali. Azimio la Arusha kamwe halijamkataa mfanyakazi
mwenziwao kwa koa la kutumikia Kampuni ya Kibepari, hivyo
ndivyo tulivyoamua Zanzibar.

MWANA-CCM KUWA NA HISA KATIKA


KAMPUNI YA KIBEPARI

Jambo jingine ambalo halikueleweka vizuri na linahitaji ufafanuzi ni lile


la kumruhusu mwanachama wa CCM kuwa na hisa katika kampuni ya
Kibepari. Hili nalo tumeliruhusu huko Zanzibar, lakini sharti iwe katika
mazingira maalum.
126

MIONGOZO MIWILI

Ni vyema kukumbushana kuwa yapo makampuni ya kibepari ambayo


tumekuwa nayo hata kabla ya Azimio la Arusha. Kampuni hizo zimekuwa
zikikidhi kiasi fulani cha ajira ya Watanzania, pamoja na Wanachama
wa CCM.

Ili jambo hili lieleweke vizuri, nitatoa mfano tu wa Kampuni ya mtu


binafsi. Mwenye Kampuni ya binafsi anaweza kabisa akaamua kwa hiari
yake kuuza baadhi ya hisa kwa wafanyakazi wake ili kuwapa motisha ya
kazi. Tajiri yeyote akiamua kufanya hivyo, Chama na Serikali vitamwona
kuwa amechukua hatua ya kimaendeleo. Kitendo chake hicho ni halali.
Kwa sababu itakuwa ameuzimua ubepari kwa kuifanya kampuni yake
ni ya ubia kati yake na wananchi aliowaajiri. Kwa kweli kampuni hiyo
itakuwa kama chama cha ushirika.
Katika hali hiyo, hata Mwanachama wa CCM anaruhusiwa kupokea/
kununua hisa alingane na wafanyakazi wenzie. Ni mazingira maalum
ya namna hii tu ndiyo yanayoruhusu Mwanachama wa CCM, kama
mfanyakazi mwingine, kuchukua hisa katika Kampuni anayofanyia kazi.
Atakapostaafu ataweza kuendelea kupokea faida ya hisa yake au kuiuza.

MISHAHARA MIWILI KWA MWANA-CCM


Kuhusu mishahara miwili, Azimio la Arusha linasema hivi:

Kwamba kila mtu anayo haki ya kupata malipo ya


haki kutokana na kazi yake.

Kufuatana na ukweli huo, anayefanya kazi mbili za halali anastahiki


kupata malipo ya kazi ya pili. Tuchukue mfano wa Profesa ambaye
mchana kutwa anasomesha Chuo Kikuu. Baada ya saa za kazi anaweza
kuamua kufanya kazi ya akili, kwa mfano kutoa ushauri au kuandika
mradi kwa aliyemwomba huduma hiyo.

Mwanachama huyo atastahiki kupata malipo ya kazi hiyo. Hili si geni,


katika sherehe za kuadhimisha miaka 20 ya Azimio la Arusha, baba wa
taifa alisema hivi:
MIONGOZO MIWILI

127

Lile sharti la kutopokea mishahara miwili kwa kweli


ni sharti la tahadhari tu. Ni vigumu sana kufanya kazi
mbili za kuajiriwa na zote mbili ukazifanya vizuri.
Huwezi kuwatumikia mabwana wawili! Lakini sharti
hili halimkatazi kiongozi wetu kujiongezea pato kwa
kutumia muda wake wa kupumzika kwa kufanya
shughuli nyingine: kama kulima au kufuga, ikiwa
yeye si mkulima au mfugaji, kuandika, kufanya kazi
ya useremala, au kufanya shughuli nyingine yoyote
kwa mikono yake au kwa ajili zake.

Jambo la msingi ni kwamba lazima twende na wakati. Mwaka 1967


lilipotungwa Azimio la Arusha ilikuwa hakuna haja ya kuwa na mishahra
au malipo ya kazi zaidi ya moja kwa sababu wakati ule mshahara mmoja
ulikuwa unatosha kukidhi mahitaji yote muhimu. Kwa mfano, mimi,
mwenyewe, mshahara wangu wakati ule ulikuwa shilingi 2,200/= kwa
mwezi. Mshahara huo, hasa kwa Zanzibar, ulikuwa ukinitosha kukidhi
mahitaji yangu yote ya lazima.
Wazee wangu watakumbuka kwamba wakati ule kule kitunguu, pilipili na
bizari - vyote hivyo kwa senti tano tu. Ilikuwa inawezekana pia kununua
samaki mkubwa kiasi kwa senti ishirini mpaka 50 tu; au kununua kuni
za kuweza kupikia mlo mzima kwa senti kumi tu. Siku hizo iliwezekana
mnunuzi kujaziwa mafuta ya kupikia au samli kikombe kizima kwa
senti ishirini au sitini tu. Halikadhalika kwa senti ishirini tu mtu aliweza
kununua matunda, kama vile fungu la ndizi mbivu au machungwa au
papai. Kwa ufupi, kwa mahitaji ya siku nzima, tangu asubuhi hadi jioni,
iliwezekana mtu kutumia pesa kidogo sana.

Katika hali hiyo, kulikuwa hakuna ulazima wa kufanya kazi ya pili. Afanyae
kazi zaidi ya moja huonekana ni mlafi au ana tamaa. Kwa mshahara huo
huo niliweza kudunduliza pesa na mwishowe kununua gari mpya kabisa.
Gari hilo lilinigharimu pesa nyingi kwa wakati huo - shilingi 13,000/=!!
Wakati huo bei ya mafuta nayo ilikuwa shilingi tatu tu kwa galoni zima.
Katika mazingira ya aina hii mshahara mmoja ulimudu kukidhi mahitaji
ya wafanyakazi wengi ukiacha walevi.
128

MIONGOZO MIWILI

HALI IMEBADILIKA
Lakini leo mambo yamebadilika. Gharama ya maisha imepanda sana.
Serikali yenyewe imeungama waziwazi kuwa haina uwezo wa kumlipa
mfanyakazi wake mshahara unaomwezesha kumudu gharama za
maisha. Kutokana na hali hiyo, wafanyakazi wengi, wanashindwa kukidhi
mahitaji yao muhimu. Ndio maana Chama na Serikali yake vimekuwa
vikiwahimiza wafanyakazi kufanya shughuli nyingine za halali, baada
ya saa za kazi, ili kujiongezea mapato. Mfano wa kazi hizo ni kama vile:
kutibu, kuandika vitabu, kuandika mradi, kutoa ushauri wa kitaalamu,
kufundisha, overtime, useremala, ufundi bomba, ufundi umeme, ufundi
cherahani, kilimo, ufugaji, kuziba mipira ya magari, kuteka maji ya kuuza,
kupiga matofali, kutengeneza baiskeli na kadhalika.

KOFIA MBILI MSHAHARA MMOJA

Lakini lazima tuelewane kuwa hii mishahara miwili tunayozungumzia


haimhusu kiongozi mwenye kofia mbili. Kwa mfano, Mkuu wa Mkoa
na Mkuu wa Wilaya, ambao vile vile ni Katibu wa Chama wa Mkoa au
Wilaya, hawaruhusiwi kupokea mishahara miwili. Hawa watalipwa
mshahara mmoja tu, maana hii kazi ya pili ni sehemu tu ya ile ya kwanza.
Lakini wanaruhusiwa kufanya kazi za ziada kama vile kilimo, ufugaji
na kadhalika, baada ya saa za kazi, kama walivyoruhusiwa wafanyakazi
wengine. Hapa nitapenda kusisitiza kuwa wale watu wanaoeneza maneno
ya kejeli kuwa ati Maamuzi ya Zanzibar ni mbinu tu za wakubwa
kujinufaisha wenyewe, ijulikane kuwa si kweli. Kazi zilizoorodheshwa
hapa si za wakubwa bali ni kazi zinazoweza kufanywa na kila mtu
kufuatana na ujuzi alionao na mazingira ya mahali anapofanyika kazi.

MWANA-CCM MKULIMA NA MFUGAJI

Watanzania wengi ni wakulima, wakulima ndio wengi zaidi. Mkulima


kwa maana pana ni pamoja na mfugaji. Katika siku za nyuma, baadhi
ya wanachama waliwahi kutiwa msukosuko kwa kuwa na mashamba
makubwa au kufuga kuku 500. Lakini baadaye Chama kilijisahihisha
kama inavyosema Programu ya Chama:
MIONGOZO MIWILI

129

Chama Cha Mapinduzi ni Chama kinachokua


(haikudumaa). Kinakaa katika nadharia na falsafa
yake, (ili kwenda na wakati).

Hii ndio ilivyokifanya Chama kijisahihishe kila kinapokosea.

Kwa hiyo kama siku moja tulimtia mwenzetu msukosuko kwa kuwa
na shamba kubwa, mbuzi 18 au kuku 500, sasa Chama kimekua katika
falsafa yake. Falsafa ya sasa inatia maanani hali halisi ya wakati wa sasa.
Ndio maana kule Zanzibar tukaruhusu kiongozi awe na shamba lisilozidi
hekta 20, hasa kama shamba hilo limo katika eneo la kijiji.

Kuhusu ufugaji, kuna baadhi ya wenzetu katika makabila ya Tanzania


ambao kwao ni utamaduni wao kuwa na ngombe wengi. Mfano mzuri
ni wenzetu wa makabila ya Wamasai, Wasukuma na Wagogo. Je, mwenye
utamaduni wa kumiliki ngombe wengi akataliwe katika Chama kwa
sababu ya kumiliki ngombe wengi? Tunasema hapana. Akiomba
uanachama wa CCM akubaliwe. Chama Cha Mapinduzi hakimkatai tajiri
aliyepata utajiri wake kwa njia ya halali na kulipa kodi ya Serikali analipa.
Anayekataliwa na CCM ni yule aliyepata utajiri kwa wizi, kwa rushwa,
dhuluma na kwa njia nyingine za haramu.
Huko Zanzibar tulifikiria labda tuweke kiwango maalum cha mifugo,
kama vile iwe mwisho ngombe 200 peke yake. Lakini tulijiuliza kama
ngombe mmoja akizaa na jumla kufikai 201, je huyo ndama amnyonge
shingo?
Hiyo ndio hali halisi iliyotufanya tukubaliane kuwa mfugaji yeyote
anaetaka kuwa mwanachama bila ya kujali idadi ya mifugo yake. Mwenye
mshahara mkubwa, vile vile hata wa malaki, maadam ni mshahara wa
kazi halali, naye pia aruhusiwe kuwa mwanachama wa CCM.

MAFUNZO YA MIEZI MITATU

Ili kukiimarisha zaidi Chama, tumewaruhusu wananchi kuwa wanachama


wa CCM bila ya kuhudhuria yale mafunzo ya miezi mitatu.
130

MIONGOZO MIWILI

BIASHARA NDOGO NDOGO


Huko Unguja hatukuishia hapo. Tuliamua kuwa Mwanachama wa CCM
wa kawaida naye pia aruhusiwe kuwa na biashara ndogo ndogo ili
kumwongezea kipato. Biashara hizo, ambazo sharti zifanywe baada ya saa
za kazi, ni pamoja na uvuvi, kuwa na gari ndogo au pick-up ya kukodisha
kwa kuchukulia abiria au mizigo, kushona, kusindika matunda, mafuta
na mashine ya kukoboa au kusaga unga.
Mwanachama mwenye mashine ya kusaga unga hanyonyi bali anatoa
huduma kwa jirani zake kijijini. Chama na Serikali vimo mbioni kuhimiza
na kutafuta teknolojia ya kumrahisishia kazi Mtanzania, hasa wanawake.
Ni vyema kukaribisha teknolojia ya kuwasaidia wanawake waondokane
na kufanya kazi ngumu ngumu zinazoweza kuwapotezea wakati na
kuathiri afya zao, kama vile kutwanga au kusaga nafaka, kubeba mizigo
ya kuni, maji na mtoto mgongoni. Si vyema kwa jamii yetu kuingia katika
karne ya ishirini na moja katika hali hiyo. Ndio maana kule Zanzibar
tuliamua kuruhusu biashara ndogo ndogo kuendeshwa na mwanachama
wa CCM kwa manufaa yao na ya jamii.

Ndugu Wazee, haya kwa muhtasari ndio yaliyoamuliwa Zanzibar. Haya


kamwe hayabomoi Azimio la Arusha, badala yake yanaliimarisha. Azimio
la Arusha ni msingi wa siasa yatu ya Ujamaa na Kujitegemea. Ili tuweze
kujitegemea lazima tuandae mbinu na mikakati ya kuzalisha mali,
huduma na chakula. Hili ndio lengo la maamuzi ya Zanzibar.
Mshairi mmoja amesema:Kutaraji uongofu bila kupitia njia zake ni kama kulitaka
jahazi kutembea nchi kavu.
Ndugu Wazee Ahsanteni sana. (Makofi)

MIONGOZO MIWILI

131

SURA YA TANO
Miongozo Miwili ya Chama na
Tabaka Lililopindua Ujamaa*
Issa Shivji

Mwongozo wa TANU, 1971

Chama cha TANU kilichopigania uhuru wa Tanganyika chini ya uongozi


wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndicho kilichoasisi Azimio la
Arusha mwaka wa 1967. Azimio liliweka mtazamo na sera za Ujamaa na
Kujitegemea. Wakati ule nyaraka mbalimbali ziliandaliwa na kuandikwa
ili kutoa miongozo katika kutekeleza Azimio la Arusha. Waraka muhimu
mmojawapo ni Mwongozo wa TANU wa 1971. Mwongozo huo una
umuhimu wa kipekee katika historia ya siasa za Tanzania. Mambo
muhimu matatu yamezungumziwa katika Mwongozo huo. Mosi ni
kutambua kwamba ubeberu unaendelea kunyanyasa na kunyonya
Waafrika hata baada ya ukoloni kupitia sura yake mpya ya ukolonimamboleo. Kutokana na ukweli huo, Vyama vya Siasa vya kimapinduzi
katika nchi nyingi za Afrika zinazojitawala, kama vile TANU, bado vingali
ni Vyama vya Ukombozi.
Pili ni umuhimu na ulazima wa kuunda jeshi la mgambo ambalo litalinda
uhuru wa nchi dhidi ya maadui. Chimbuko la uamuzi huo linajulikana.
Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kusaidia ukombozi wa nchi za
Afrika ambazo bado zilikuwa chini ya ukoloni. Wapigania uhuru ambao
walikuwa wanasaidiwa na Tanzania moja kwa moja walikuwa wale wa
Afrika ya Kusini, Namibia, wakati ule ikiitwa South West Afrika, na
Msumbiji ambayo ilikuwa chini ya ukoloni katili wa Wareno.
Huko Afrika ya Magharibi, nchi mojawapo ambayo ilifanana sana na
Tanzania katika sera zake na hasa katika kusaidia wapigania uhuru
ilikuwa Guinea-Conakry chini ya uongozi wa Sekou Toure. Wapigania
* Makala hii yalichapishwa mara ya kwanza katika jarida la Chemchemi, toleo na. 2, Oktoba,
2009. Imesahishishwa kwa ajili ya kitabu hiki.

132

MIONGOZO MIWILI

uhuru wa Guinea-Bissau na Cape Verde, ambazo zilikuwa nchi moja


wakati huo, chini ya uongozi shupavu wa Amilcar Cabral, walisaidiwa
na Sekou Toure. Kutokana na nafasi ya Guinea-Conakry katika vita vya
ukombozi, majeshi ya Wareno yalivamia Guinea-Conakry. Hata hivyo
hawakufanikiwa kwa sababu Guinea-Conakry iliweza kuwashinda, hasa
kutokana na jinsi wanamgambo walivyopigana kwa ujasiri na ushupavu.
Isitoshe, karibu na nyumbani, Rais Obote wa Uganda alipinduliwa na jeshi
lake chini ya Idi Amin Dada akisaidiwa na Uingereza na Israeli. Hii ilitokea
baada ya Obote kutangaza kasiasa ka kijamaa na pia kuunga mkono nchi
zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika
ambazo bado zilikuwa zinatawaliwa na wakoloni na makaburu.

Mambo haya yote mawili ni wazi yalikuwa tishio kwa Tanzania. Tanzania
pia ilikuwa na wasiwasi wa kuvamiwa na jeshi la Wareno. Ndio maana
chama na serikali waliamua kuwa na jeshi la wanamgambo. Jambo hili
ni la kwanza linalozungumziwa katika Mwongozo wa Tanu wa 1971.
Pia, Tanzania ilikuwa haipendwi na mabeberu kutokana na siasa zake
za kijamaa.
Pamoja na mambo haya, sifa moja ya Mwongozo ni uchambuzi wake wa
radikali wa hali halisi ambao unaufanya Mwongozo kuwa nyaraka ya
kimapinduzi zaidi kuliko zote zingine zilizoandikwa wakati wa enzi za
Azimio la Arusha. Mfano mmoja tu unatosha kudhihirisha hili.
Mapinduzi ni mabadiliko ya haraka katika jamii,
mabadiliko ambayo yanawanyanganya wachache
madaraka ambayo walikuwa wakiyatumia kwa manufaa
yao (na ya wanyonyaji wa nje), na kuyaweka madaraka
hayo mikononi mwa wengi ili kuendeleza maslahi yao.

Katika hili, Chama chini ya uongozi wa Mwalimu, kwa mara ya kwanza,


umeweka wazi maadui wa Mapinduzi ya kijamaa, wakiwa vibaraka wa
ndani wakiungwa mkono na wanyonyaji wa nje kwa maana ya mabepari
wa kimataifa kutoka nchi za kibeberu.
***

MIONGOZO MIWILI

133

Lakini zaidi ya yote jambo ambalo lilifanya Mwongozo uwe na historia ya


kipekee ni ibara ya 15 ya Mwongozo. Ibara hii inasema:
Lazima iwepo jitihada ya kujenga hali ya usawa
kati ya viongozi na wanaowaongoza. Iwe ni mwiko
kwa kiongozi wa Tanzania kuwa mwenye majivuno,
ubadhirifu, dharau na uonevu. Kiongozi wa Tanzania
awe ni mtu anayeheshimu watu, asiwe ni mpenda
makuu, sio mnyapara, mkaripiaji na muamrishaji
watu.

Ibara hii ikawa kauli mbiu na itikadi ya tabaka la wafanyakazi dhidi ya


menejimenti yao viwandani. Takribani miaka minne kufuatia kutangazwa
kwa Mwongozo, kuliibuka vuguvugu la wafanyakazi ambalo lilikuwa
halijawahi kutokea katika historia ya nchi. Katika kipindi kifupi cha
miaka mitatu tu (1971-1974), kulikuwa na migomo zaidi ya 30, ambayo
ilihusisha wafanyakazi takriban 23,000 na siku za kazi zilizopotea ni
takriban 64,000. Kwa kasi kubwa sana wafanyakazi walijifunza mikakati
na mbinu za mapambano ya kitabaka. Walianza na migomo ya kawaida
kwa maana ya kuweka chini zana za kazi. Kutokana na kulaumiwa
kwamba wafanyakazi walikuwa hawajali maslahi ya taifa, wafanyakazi
wakabadili mbinu zao katika awamu ya pili. Badala ya kugoma, wakaanza
kuwafungia nje wanyapara na wamiliki wa viwanda wakati wakiendelea
na uzalishaji.
Lakini kama unaweza kuzalisha bila menejimenti, kwa nini ukubali
menejimenti? Kwa hivyo, mapambano yakakoma na wafanyakazi
wakaanza kutwaa viwanda. Hapo ndipo, watawala wa kisiasa na kiuchumi
wakashtuka. Viongozi wa chama na serikali wakaanza kuwashutumu
wafanyakazi wazi wazi kwa kusema kwamba ingawa chama kilikuwa na
sera ya kutaifisha viwanda hii haikuwa na maana kwamba wafanyakazi
wenyewe waanze mtindo huo. Utaifishaji lazima ufuate taratibu na
ustaarabu!

Katika hotuba ya Mei Mosi (ya mwaka wa 1974) yenye kichwa cha habari
Ukigoma unamgomea nani? Mwalimu aliwashutumu wafanyakazi, jambo
134

MIONGOZO MIWILI

ambalo mara moja lilivunja nguvu za wafanyakazi. Hotuba ya Mei Mosi


ikawa mwongozo wa menejimenti au warasimu, nao walifurahia sana.

Kwa kweli, vuguvugu la wafanyakazi lilikuwa mapambano ya kitabaka


dhidi ya tabaka la warasimu. Katika makala yangu (The Silent Class
Struggle au Mapambano Baridi ya Kitabaka) iliyochapishwa na jarida
la kimapinduzi la wanafunzi wanamapinduzi wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Cheche, nilifanya uchambuzi na nikaliita tabaka hili jipya
mabepari wa kirasimu (bureaucratic bourgeoisie). Baada ya mwaka
mmoja nikaandika makala ya pili ambayo hatimaye ilichapishwa kama
kitabu, kwa jina la Class Struggles in Tanzania (Mapambano ya Kitabaka
Nchini Tanzania). Wakati ule watu wachache sana waliweza kukubaliana
na uchambuzi wangu na viongozi walibeza kwamba Tanzania ni nchi
ya wakulima na wafanyakazi na hakuna matabaka. Kwa kiasi fulani,
kulikuwa na ukweli humu kwa sababu matabaka bado yalikuwa katika
uchanga wake, yalikuwa hayajakomaa hasa kutokana na sera mbalimbali
za Mwalimu za kuzuia viongozi na warasimu wasijilimbikizie mali (kwa
mfano kwa kupitia katika Miiko ya Uongozi).
Kwa hivyo, nguvu ya tabaka la wafanyakazi ikavunjika na hatimaye kwa
sheria ya 1975, wafanyakazi wakawekwa chini ya chama cha NUTA
(National Union of Tanganyika Workers) ambacho kwa vyovyote vile
kilikuwa chini ya himaya ya chama tawala.

Kwa upande mwingine, sera ya Chama juu ya vijiji vya ujamaa pia
ikatekwa na wenye jazba na wapiga debe katika Chama. Mtazamo
wa Ujamaa Vijijini ambao ulisisitiza kwamba vijiji vya ujamaa viwe
chaguo la hiari la wakulima wenyewe ukageuzwa. Sera ukawa vijiji vya
maendeleo na wanakijiji wakalazimshwa, mara nyingine chini ya ulinzi
na mabavu ya FFU (Field Force Unit) kuhamia katika vijiji vya maendeleo.
Jambo hili lilifanya wakulima waanze kupoteza imani na Chama. Kwa
ufupi basi, matabaka ya wafanyakazi na wakulima wakafarakanishwa na
kutenganishwa na Chama, na kwa kiasi fulani Mwalimu mwenyewe. Kwa
upande mwinigine, kuvunjika kwa nguvu za wavujajasho, kukasafisha
njia kwa warasimu na wamangimeza wa Chama na Serikali, kuendelea
kujilimbikizia madaraka (na hata mali angalau kwa kificho) na kujijenga
MIONGOZO MIWILI

135

kama tabaka jipya la vibepari chini ya himaya ya ubeberu. Hawa ndio


hatimaye wakaja kuainishwa kwa ufasaha kama wapingamapinduzi
katika Mwongozo wa 1981.
Mwongozo wa CCM, 1981

Kipindi cha mwisho cha Mwalimu Nyerere (1980-85) kilikuwa kigumu


kuliko vyote katika utawala wake. Hali ya uchumi ilidorora kutokana na
sababu mbalimbali za ndani na nje, pamoja na vita vya Uganda, ambavyo
viliigharimu nchi sana; kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kupanda kwa bei za petroli. Mnamo 1981, Chama tawala, wakati huo CCM,
kilifanya tathmini ya miaka 14 ya Azimio la Arusha na kiliainisha hali halisi
ya siasa, jamii na uchumi. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Chama kufanya
uchambuzi wa kina bila ya kujali maslahi yake ya muda mfupi.
Kwa maoni yangu, hoja ambayo ni nzito katika uchambuzi huo ni kwamba
chini ya mwavuli wa Azimio la Arusha na sekta ya umma, hususan
mashirika ya umma, lilijengeka tabaka jipya la mabepari. Mwongozo
unasema:
Kwani ukweli unaojitokeza wazi wazi ni kuwa baadhi
ya matatizo yetu ya uchumi yanatokana na kutotekeleza
kwa dhati siasa ya Ujamaa na Kujitegemea vijijini na
katika sekta ya umma tuliyoianzisha. Zaidi ya hivyo,
wakati mwingine katika miaka kumi na minne tangu
Azimio la Arusha, Chama, Serikali, na vyombo vyake
vilitumika kukuza sekta ya kibepari nchini katika
viwanda, biashara, usafirishaji, ujenzi na kadhalika na
ubepari huo uliopanuka katika kipindi hiki umeimarisha
vitendo vya kuivuruga na kuidhoofisha sekta yetu ya
Umaa (ib. 35).

Sehemu nyingine, Mwongozo unaendelea kueleza kwa ufasaha mkubwa


kwamba:

136

MIONGOZO MIWILI

Leo ubepari una vishawishi vingi zaidi nchini kuliko


ulivyokuwa kabla ya Azimio la Arusha kwa sababu
pamoja na kwamba sasa tuna sekta kubwa ya umma
lakini kutokana na udhaifu wa kutopambana nao,
ubepari umefaulu kujipanua na kujipenyeza hata ndani
ya sekta yenyewe ya umma. Na ndio maana ubepari sasa
unathubutu kujitokeza hadharani kuukashifu Ujamaa,
kubabaisha baadhi ya viongozi na kututaka tubadilishe
siasa yetu (ib. 52).

Kwa hakika matamko haya yalikuwa ni kukiri wazi wazi kwamba sera
za Ujamaa zilikuwa zimehujumiwa na viongozi wenyewe waliopewa
jukumu la kuongoza ujenzi wa Ujamaa kutokana na maslahi yao ya
kitabaka ya kibepari.
Hapa tunashuhudia kwa mara ya kwanza, Chama kikikiri kwamba kuna
mapambano au harakati za kitabaka dhana ambayo kila mara Chama, na
hasa Mwalimu mwenyewe, alikuwa anaikanusha. Kinadharia na kiitikadi
Mwalimu hakukubaliana kabisa na dhana ya mapambano ya kitabaka.
Hata hivyo ibara ya 50 ya Mwongozo inaenda mbali zaidi kwa kueleza
kwamba:
Kuielewa vema jamii ya Tanzania ya leo kunataka
uchambuzi wa hali ya juu pia. Uchambuzi huu
ukiwezeshe Chama kuielewa migongano ya maslahi ya
tabaka ambayo imejitokeza nchini. Migongano hii ina
mizizi katika mgongano wa msingi kati ya Ujamaa na
ubepari, kati ya maslahi ya wakulima na wafanyakazi
kwa upande mmoja, na ya ubinafsi, ubwanyenye na
ubepari ambao umekuwa ukijengeka tangu Azimio la
Arusha kwa upande mwingine.

Uchambuzi huo ni wazi na umefanywa kwa ufasaha na kisayansi. Swali


muhimu kwa wasomi, wanazuoni na wakereketwa wa Usoshalisti ni:
Je, Chama kilifanikiwa katika mapambano haya na kurudisha nchi
kwenye Ujamaa? Au tabaka hili liliojengeka lilishinda mapambano na
MIONGOZO MIWILI

137

ndilo injini inayosukuma gurudumu la mageuzi ya kisiasa na kiuchumi


kuelekea kwenye uliberali mamboleo, ambao ni mfumo wa kibepari?
Je, tabaka hilo la mabepari warasimu ndilo hasa chimbuko la mfumo
huo wa ubepari uchwara, ukiungwa mkono na ubeberu, na ambao ndio
unatutawala leo? Je, si kweli kwamba, katika awamu hasa ya tatu tabaka
hili la mabepari warasimu ndilo lililokuwa mstari wa mbele kutetea
ubepari wakimnukuu kwa furaha Deng Tsio-Ping, kiongozi wa China,
aliyepindua ujamaa nchini China?
Katika mahojiano yake na mwandishi wa habari Jonathan Power wa
jarida la Prospect (na. 112, Julai 2005), Rais mstaafu Benjamin Mkapa
alikiri kwamba yeye alikuwa anamheshimu Deng Tsio-Ping. Alipoulizwa
na Jonathan Power kwamba je, Nyerere akifufuka angesemaje, Mkapa
akamjibu: Angesema kwamba mimi nimegawia mengi yaliyokuwa
katika sekta ya umma. Na angefadhaishwa na ukweli kwamba mimi
nimefanikiwa kujenga tabaka la mabepari matajiri.
Sina hakika kama Rais Mkapa alifanikiwa kujenga tabaka la mabepari
matajiri au alijenga tabaka la vibepari uchwara tu. Ni suala la kutafiti.
Haikuwa nia yangu kuangalia suala hili kwa undani bali ni kudokeza tu
kwamba kama tunataka kuelewa vema na kisayansi hali halisi ya nchi
na jamii yetu ya leo hatuna budi kufanya uchambuzi wa kitabaka katika
mfumo wa ubepari uchwara chini ya utawala wa kibeberu, hususan,
tabaka lililoongoza mageuzi. Na hoja yangu ni kwamba Mwongozo wa
CCM wa 1981 unatuweka mahali pazuri pa kuanzia. Kazi kwetu!
Ni jukumu la wasomi na wanazuoni kuchambua jamii yao, kuonyesha
jamii sura yake halisi na kuainisha mielekeo ya maendeleo na mielekeo
ya wapingamendeleo. Kama Mwongozo wa 1981 unasema:mapinduzi
sio lelemama. Mapinduzi yanahitaji wakereketwa wa kijamii ambao
msimamo wao kwa upande wa wavujajasho hautetereki:
Ujenzi wa ujamaa si lelemama bali ni mapambano,
mapambano ya kudumu dhidi ya ubepari na unyonyaji,
dhidi ya wapinga maendeleo na wababaishaji wa
kisiasa, dhidi ya wahujumu uchumi, majambazi,

138

MIONGOZO MIWILI

wezi, wazururaji na wazembe. Msimamo sahihi wa


mapambano unaotokana na nadharia sahihi ya ujamaa
ungelituepusha na maamuzi na vitendo ambavyo
vimerahisisha kuoteshwa kwa mizizi ya ubepari,
kinyume cha msimamo wa mapambano dhidi ya
ubepari. Leo ubepari, una vishawishi vingi zaidi nchini
kuliko ulivyokuwa kabla ya Azimio la Arusha kwa
sababu pamoja na kwamba sasa tuna sekta kubwa ya
umma lakini kutokana na udhaifu wa kutopambana nao,
ubepari umefaulu kujipanua na kujipenyeza hata ndani
ya sekta yenyewe ya Umma. Na ndiyo maana ubepari sasa
unathubutu kujitokeza hadharani kuukashifu ujamaa,
kubabaisha baadhi ya viongozi na kututaka tubadilishe
siasa yetu. (ibara ya 52)

Ukweli uliojitokeza tangu uchambuzi huo wa Mwongozo wa 1981, ni


kwamba ubepari ukisimamiwa na vibepari uchwara wa ndani na nchi
za kibeberu (ambao siku hizi wanaitwa eti wabia wetu wa maedeleo)
ukashinda katika mapambano. Chini ya visingizio mbalimbali, pamoja
na fikra hafifu ya kwenda na wakati, Azimio likapinduliwa na uliberali
mambo-leo ukashinda.

MIONGOZO MIWILI

139

Marejeo
Mapolu, Henry. (mh.), (1976), Workers and Management, Dar es Salaam,
Tanzania Publishing House.

Mapolu, Henry na Issa Shivji. (1984), Vuguvugu la Wafanyakazi Nchini


Tanzania, Kampala, Urban Rural Mission.

Mihyo, P. (1975), The Struggle for Workers Control in Tanzania, Review


of African Political Economy, No.4.

Shivji, Issa G. (1976), Class Struggles in Tanzania, Dar es Salaam, London


& New York, Tanzania Publishing House, Heinemaan and
Monthly Review.

Shivji, Issa G., (1970), Tanzania: The Silent Class Struggle (Cheche 1970)
na kuchapishwa tena katika Issa G. Shivji (mh.) na wengine: The
Silent Class Struggle, (1972), Tanzania Publishing House.

140

MIONGOZO MIWILI

You might also like