You are on page 1of 5

HOTUBA YA MWL.

JK NYERERE 1985 AKIZUNGUMZA NA WAZEE WA DAR ES


SALAAM.

"Mimi nimeanza siasa na wazee wa Dar es Salaam; na wazee wa Tanzania. Nimeanza


nao mapema sana; mapema kweli. Nilirudi kutoka masomoni, Uingereza Oktoba 1952
– miaka 33 nyuma. Wakati huo nikiwa kijana mdogo wa miaka thelathini na kidogo hivi.

Niliporudi nikakubaliana na wamisionari hapo Pugu (sekondari), nifundishe shuleni


kwao. Lakini nikiwa shuleni – Chuo Kikuu – nilijua. Niliishaamua kwamba maisha
yangu yatakuwa ya siasa. Niliamua hivyo: Nitafundisha kwa muda wa miaka mitatu,
nione hali inavyokwenda na kuzoeana na wenzangu kabla ya kuanza maisha ya siasa.

Niliporejea nchini hapo Oktoba, nikaenda Butiama. Januari nikarudi Dar es Salaam.
Nikaanza kazi. Nikataka kujua habari za African Association. Mzee Mwangosi
anakumbuka. Yeye ndiye aliniambia habari za African Association. Aliisha niambia
habari hizo tangu nikiwa Makerere – Chuo Kikuu – nikiwa mwanafunzi.

Pale, mimi na wanafunzi wenzangu tulikuwa tumeanzisha chama kinachoitwa


Tanganyika African Welfare Association (TAWA) cha wanafunzi wa Tanganyika; mimi
nikiwa katibu wao. Hapa tukaona mambo yanakwenda vizuri kidogo.

Tukaona kwanini TAWA iwe ya wanafunzi peke yao na siyo Tanganyika nzima. Kwa
hiyo nikawaandikia baadhi ya watu Tanganyika. Nikasema, jamani ee, tumeanzisha
chama, kwanini msianzishe huko matawi ya chama hicho?

Ndugu Mwangosi akapata barua hiyo. Alikuwa miongoni mwa waliopata barua hiyo.
Akaniandikia – nikiwa Makerere – akasema: wewe kwanini unataka kuanzisha chama
kipya? Kipo chama. Kipo chama cha TAA (Tanganyika African Association).

Kwa hiyo la maana siyo kuanzisha matawi, maana chama kipo na matawi yameenea; la
maana ni kwamba hicho chama chenu mfute, na muanzishe tawi la Tanganyika African
Association.

KUVUNJWA KWA TAWA.

Hivyo ndivyo tulivyofanya. Kwa hiyo mimi nikawa katibu wa katawi ka TAA hapo
Makerere. Niliporudi Tabora na kuanza kufundisha pale St. Marys (sasa inaitwa
Sekondari ya Milambo), nikachaguliwa katibu wa TAA wa jimbo ambalo makao yake
makuu yalikuwa Tabora. Ulipofanyika mkutano wa TAA mjini Dar es Salaam,
nilihudhuria nikiwa mjumbe kutoka Tabora.

Kwa hiyo nilikuwa naijua Tanganyika African Association. Nilipokuwa ninaondoka


kwenda Ulaya kusoma, nilikuwa nimeishaonja shughuli za TAA. Sasa niliporudi, baada
ya kukaa Pugu siku chache, nikaja mjini Dar es Salaam. Nikauliza nani wanaongoza
TAA? Nikaambiwa kuna jamaa mmoja anaitwa Abdul Sykes. Sasa ni marehemu. Abdul
ndiye alikuwa katibu wakati huo.

Nilipelekwa na Kasela Bantu - ambaye naye aliteleza-teleza na hatunaye hapa (kwenye


mkutano). Kasela Bantu alikuwa mwalimu mwenzangu. Tulifundisha pamoja Milambo.
Nilipokuja Dar es Salaam, nikakuta anafanya kazi Redio (Tanganyika Broadcasting
Corporation). Ni Kasela Bantu aliyenipeleka kwa Sykes.

Wakati huo mambo yalikuwa yanasinzia kidogo. Kwa muda mfupi mwaka ule,
tukafufua-fufua, hasa kutoka Januari. Kufika Aprili, TAA ikafufuka. Tukafanya mkutano
hapo Anautouglou. Kwenye mkutano huu wakanichagua kuwa Rais wao – wa TAA.

Ninasema yote haya kwa shukrani kwa wazee. Jamaa hawa walikuwa watu wazima wa
Dar es Salaam, na mimi kijana mdogo Mzanaki, na Kiswahili changu si kizuri sana –
cha matatizo.

Nimekuja, natoka Ulaya, tena masomoni. Muda mfupi tu jamaa hawa wakaniamini
haraka sana – katika muda wa miezi mitatu. Wakanichagua Rais wa TAA. Hapo ndipo
nilianza shughuli mpya ya kuandika katiba ya TAA na kuipa madhumuni hasa ya
shabaha ya kuleta uhuru.

Baada ya miezi 13, hapo 1954, tukaanzisha TANU. Jina hili lilipendekezwa na akina
Abdul Sykes. Walikuwa wamelifikiria tangu zamani, walipokuwa askari vitani huko
Burma (Vita vya Pili).

WAZEE NA MSIMAMO

Miezi minne baada ya kuanza kazi Pugu nikawa ninakuja Dar es Salaam, kwa mguu;
kila Jumamosi. Baadaye wazee wakanipa baiskeli nikawa ninakuja mjini kukutana na
wenzangu; kufanya mikutano.

Hivyo ndivyo tulivyofanya. Wazee wakaniamini upesi sana. Tukawa na uhusiano


mkubwa sana. Wadogo wenzangu wengine walikuwa Abdul Sykes, Abass Sykes
(mdogo wake), Dosa Aziz – waliokuwa wengi ni wazee.

Katika kuhutubia mikutano yangu, nilikuwa nikisema: Wazee na Ndugu zangu! Wazee
hasa ndio walikuwa na mikutano ya awali ya TAA na TANU. Walikuwa na msimamo wa
hali ya juu kabisa! Hawakuyumba hata kidogo! Vijana walikuwa na mashaka. Wengine
walikuwa na vikazi vyao, waliogopa kuvipoteza.

Nalo jambo lenyewe ni la hatari – la kuzungumzia uhuru! Unaweza ukakosa kazi; na


wapo waliopoteza kazi; wengine wakaacha kazi. Akina Rashid (Kawawa) waliona
watoke kwenye shughuli hizo tuje tuungane katika chama.

Wazee wa Dar es Salaam, na baadaye wa nchi nzima, wakatuunga mkono, na kila


nilipokwenda, watu wa kwanza walionielewa, walikuwa wazee.

Nilikwenda Songea mwaka 1955 mara baada ya kujiuzulu. Huko wazee walinipokea na
kunielewa. Nilianza safari za kuitembelea Tanganyika nzima. Nilikwenda Mbeya.
Mkutano wangu niliufanya na wazee; kikundi kidogo cha wazee, ndani ya nyumba ya
mtu.

Kwa mkutano huu wa Mbeya, wazee wakauliza: Unatafuta nini? Nikawaambia natafuta
uhuru. Wale wazee, kwa sababu ya vita vya Maji Maji, na wanakumbuka, kabisa,
wakaona mimi ninatafuta jambo la hatari. Tulifanya mkutano wa makini kweli.
Wakauliza: Wewe unawezaje kuleta uhuru? Wewe una njia gani kudai uhuru na usitiwe
kitanzi na Waingereza?

WAINGEREZA WAONGO

Tulielezana. Nikawaambia ninyi wazee, Waingereza wanawadanganya, Waingereza


wametumwa na ule Umoja wa Mataifa uliokufa (League of Nations), waje kuishika
Tanganyika kwa muda tu; watusaidie, na wakati tutakapokuwa tayari, watuachie
tukajitawale.

Waingereza wanafanya ujanja; hawasemi. Vita vimekwisha (vya Pili) na Umoja wa


Mataifa mwingine – mpya (United Nations Organisation – UNO) umewakabidhi
Tanganyika kwa shabaha ileile. Sisi siyo koloni lao. Wamepewa dhamana tu.

Kwa hiyo nikawaambia wazee, hakuna haja ya kumwaga damu. Tuwaseme tu!
Tuwashitaki kwa waliowaleta hapa kwamba hawafanyi kazi yao; wamesahau kabisa!

Wazee wakauliza: Eh, inawezekana? Nikasema inawezekana. Kazi yetu ya kwanza


ilikuwa kuwaambia watu kwamba uwezekano wa kujitawala upo. Hilo lilikuwa la
kwanza. Wazee walijua maana ya kujitawala. Walitamani kujitawala, lakini hawakujua
waanzie wapi.

Vijana hawakuwa na habari kwamba kujitawala kunawezekana. Kwa hiyo kwa wazee
sikuwa na matatizo. Wao hawakuwa na kazi; hawakumwogopa Mwingereza.
Hawakuogopa kufukuzwa kazi. Baadhi walikuwa wafanyabiashara.

Mzee John Rupia (marehemu) alikwua mfanyabiashara na kaidi kidogo. Aliwahi


kutishwa na kunyang’anywa leseni yake ya biashara. Akaambiwa akiendelea
kushirikiana na kijana mwenda wazimu (Julius Nyerere), atanyang’anywa leseni moja
kwa moja. Rupia aliwajibu: Potelea mbali!

Nasema yote haya ikiwa njia ya kutoa shukrani kwa wazee na imani yao kwa vijana
wakati huo.

Imani hujenga imani. Na mambo haya makubwa ya nchi, kama hayana baraka za
wazee hayaendi. Magumu sana. Wanasema ngoma ya watoto haikeshi! Mimi nilipata
baraka za wazee tangu zamani. Tangu awali kabisa.
mvugilije.home

TWAININGI AMEKWISHA

Siku moja, Dosa akanifuata Magomeni (Dar es Salaam). Akasema: Leo wazee
wanakutaka. Wapi? Kwa Mzee Jumbe Tambaza. Wanakutaka usiku. Nikasema haya,
nitakuja. Nikaenda. Nikakuta wazee wameshakaa; wameniita kijana wao kuniombea
dua. Mimi Mkristo, wao Waislamu watupu. Wakaniombea dua za ubani. Tukamaliza.

Tulipomaliza wakasema kuna dua pia za wazee wao. Basi wakanitoa nje. Tukatoka.
Zilipomalizika zilikuwa za Korani; sasa zikaja dua za wazee – za jadi.

Walikuwa na beberu la mbuzi. Wamechimba shimo. Wakaniambia simama.


Nikasimama. Beberu akachinjwa, huku anaambiwa, “Twining (Twainingi) umekwisha!”
(Edward Twining alikuwa Gavana wakati huo). Ndipo nikaambiwa: Tambuka! Nikavuka
lile shimo. Hapo nikaambiwa na wazee: Basi nenda zako; tangu leo Twainingi
amekwisha!

Sasa mimi Mkristo; hao Waislamu. Na mimi mkorofi-korofi katika mambo haya (ya
kutambika). Lakini tulikuwa tunaelewana na wazee wangu hao. Kwa hiyo nilitambuka
pale na kuambiwa: Nenda nyumbani salama. Twaining hawezi tena!

Wazee wangu wengine wanakumbuka tulikuwa tunakwenda Bagamoyo. Kwenye


makaburi kule! Tunapiga dua huko kwenye makaburi na wazee wangu.

Baadhi yetu mtakumbuka safari moja jamaa wa Kenya, hawa akina Tom Mboya
(marehemu) walishitakiwa. Tukasema tuwasaidie. Tuwasaidie vipi? Tukasema tufunge.
Tukaomba nchi nzima kufunga siku hiyo. Tufunge! Tukafunga. Hakuna kula. Na siku
ya kufunga tulikuwa na mkutano Bagamoyo. Tukaenda huko. Tukafanya mkutano hadi
saa 12 jioni.

Baada ya mkutano tukaenda nyumbani kwa Mzee Mohamed Ramia (marehemu). Hapa
ndipo tulikuwa tumefikia. Mimi nikamuuliza mzee: Sheikh, una Aspro? Akajibu: Kwa
nini unataka Aspro? Nikajibu kuwa kichwa kinaniuma kwelikweli. Akasema subiri.

Tulisubiri hadi saa ya kufuturu. Tukafuturu vizuri. Mzee Ramia akaniuliza: bado unataka Aspro?
Nikajibu kichwa sasa hakiumi. Kumbe ilikuwa njaa.

Nawaelezeni haya kwa sababu huko tulikotoka, tulishikamana sana. Tulishirikiana sana na wazee."’

“Ulu Mwami wa Bhantu,Ndoguheleza Izina La Bhaha,”


“Ulu Muntu Mwiza Nahoo Bhokulabha Kinige” by Ramadhani Mvugilije.

published by Kwigize@ilogiza.05may2016.
≈ ∃ ∅ All Rights Received.
@kilwa-masoko

mvugilije.home.elizeus jerad mushobozi

You might also like