You are on page 1of 6

NA LUQMAN MALOTO

MAMA yupo na mwanaye Hospitali ya Palestina, Sinza, Dar es Salaam.


Amempeleka kupata matibabu. Mtoto anashangazwa na wingi wa watu,
anamuuliza mama yake: Kuna nini?
Mama anamjibu mwanaye: Kuna watu walikuwa vigogo wa nchi, walitumia vibaya
madaraka yao walipokuwa viongozi wakubwa wa serikali, walihukumiwa na
mahakama kwenda jela kwa kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.
Baada ya kuhukumiwa kwenda jela, baadaye walipata punguzo la adhabu
mahakamani, walipewa kifungo cha nje pamoja na kufanya usafi kwenye maeneo
ya kijamii, hapa hospitali ni moja ya sehemu walizopangiwa.
Mtoto anatikisa kichwa kuonesha kuwa ameelewa, kisha anauliza tena: Ndiyo
wale akina babu walikuja na magari mazuri? Wanafagia kwa lazima na kupiga deki
makorido ya hospitali, kwani nyumbani kwao hakuna wadada wa kazi? Si
wangewachukua waje kufanya kazi kwa niaba yao?
Mama anamjibu mwanaye: Mwanangu hiyo ni adhabu ya mahakama, inatakiwa
kutekelezwa na mwenye kosa. Hapo hairuhusiwi kutumia fedha kuleta watu wa
kusafisha wala kuita ndugu wawasaidie, ni wao wenyewe.
Mtoto anaendelea: Kama ni hivyo basi ngoja na mimi nitapike hapa ili waje
wafute ili waitumikie adhabu vizuri.
Mama kwa hisia, anamwambia mwanaye: Usifanye mzaha mwanangu, hili jambo
siyo dogo. Hawa watu unaowaona ni matajiri, wana uwezo mkubwa lakini sheria
imechukua mkondo wake. Wanalipa gharama za walichokifanya wakiwa ofisini.
Katika kumuweka sawa mtoto wake, mama anasema: Unaziona hizi pesa? Basi
kwa taarifa yako, hao watu wawili kwa nyakati tofauti tumetumia noti zenye saini
zao, unadhani ni wadogo hao?
Mtoto sasa anashtuka, anauliza: Kumbe wenyewe ndiyo huwa wanasaini hizi
pesa tunazotumia?
Mama anajibu: Walikuwa wanasaini, siyo sasa. Walipishana wizara ya fedha
wakati Rais Benjamin Mkapa alipokuwa madarakani, kabla ja Dk. Jakaya Kikwete
na Dk. John Magufuli.
Mara mtoto anapayuka: Mama ona yule mzee anafagia anakosea. Mama
anamshika kinywa mwanaye aache kupayuka.
Mwaka 1997 mpaka 2000, Daniel Yona alikuwa waziri wa fedha na baada ya hapo
alikuwa waziri wa nishati na madini. Kati ya mwaka 2000 mpaka 2005, Basil
Mramba alikuwa waziri wa fedha. Ila sasa wapo kwenye adhabu ya usafi, nyakati
zimebadilika.
Yona anageuka anamwangalia mtoto aliyepayuka, anakuta mama kamziba
mdomo, anashindwa kusema kitu, ila inamuuma.

Mama anapomwachia mdomo mtoto, anapayuka tena: Kwa hiyo na wale ni


mafisadi? Si wamechezea fedha za serikali na kuitia hasara?
Mtoto aliongea harakaharaka, mama alipotaka kumuwahi mdomo, alikuta
ameshamaliza. Mama anaogopa, anaona hatari hiyo maana Mramba na Yona ni
watu wakubwa! Nyakati tu zimebadilika!
Mramba anafagia, kuna mkazi wa Manzese mtukutu, yupo Hospitali ya Palestina
anasubiri huduma. Alikuwa amekaa, mara anainua miguu kisha anamwita: Mzee
huoni uchafu huu, pitisha hapa ufagio sisi raia wema tukae kwenye maeneo
masafi.
Wakati anafagia, mtukutu wa Manzese anazungumza kwa ukauzu: Si ulisema
bora tule nyasi ndege ya rais inunuliwe? Lipia gharama za maneno yako. Mramba
anakumbuka maneno hayo aliyoyatamka bungeni katika Bunge la 8. Roho inauma,
siku haziwezi kurudi nyuma! Na nyakati zimebadilika!
Yona akiwa anaendelea kufanya usafi, teja wa Kinondoni Manyanya ambaye yupo
kliniki (rehab) akitumia dawa mbadala ya methadone, anampita Yona kisha
anamwambia kwa sauti ya kebehi: Mwana hii ndiyo laifu, ona sasa hivi umekuja
kudeki matapishi ya wagonjwa hapa Palestina.
Ni maneno ambayo yanamuuma Yona, anawatazama polisi kisha anatamani
kuwaamrisha wamuweke ndani yule teja, ghafla anakumbuka, jeuri hiyo hana tena,
na pale yeye ni mfungwa. Wale askari wapo kwa ajili kumsimamia anavyotekeleza
adhabu. Anatikisa kichwa kwa uchungu! Nyakati zimebadilika!
Nyakati hizo alikuwa akitamka kuwaambia polisi kamata, ilikuwa hakuna kuhoji
kwa kosa gani, maafande wanakubeba msobemsobe mpaka kituoni, hutoki wala
hupelekwi mahakamani mpaka aamue! Ndiyo, si vigogo wengi walikuwa
wakitumia nguvu hiyo kandamizi?
Kuna mama mmoja mzuri, msafi, anaonekana wa heshima. Anatembea
kumwelekea Mramba. Anamfikia na kumsalimia vizuri kisha anatoa noti mbili za
shilingi 10,000 na 5,000, zile pana, kabla ya hizi vipotabo za sasa.
Anamwambia Mramba: Samahani, hii saini kwenye hizi pesa ni kama yako hivi,
au?
Mramba kwa unyenyekevu anajibu: Ni kweli hiyo ni saini yangu.
Mama anajibu kisharishari tena kichokozi: Utajibeba baba, toka kusaini pesa
mpaka kusafisha vyoo vya hospitali, mbona unalo!
Mramba anamuangalia kwa kumshangaa, alimuona ni mtu mwenye heshima zake,
kumbe hovyo kabisa, mama mgomvi! La kumjibu anakosa, anatikisa kichwa.
Anakumbuka enzi zake mwanamke yule hata asingepata nafasi ya kumkaribia.
Ndiyo hivyo tena, nyakati zilishabadilika!
Yona anamtazama Mramba, anamuona kama mtu aliyetahayari. Anabaini atakuwa

amekwazwa na yule mwanamke. Anamnyooshea ishara kuwa awe mvumilivu


wasije kuharibu adhabu. Maana mahakama haishindwi kuagiza warudi gerezani
kwa sababu nje ya gereza wanagombana na raia.
Wanaendelea na usafi, mara kuna mgonjwa anamuona Yona, anamwambia: Baba
nimekukumbuka, wewe si ndiye yule mwenye lile jengo la kifahari pale Bahari
Beach? Mzee upo vizuri, mjengo wote ule wako peke yako. Hii nchi watu mnafaidi
jamani.
Yona anashindwa kujibu, anaamua kumpuuza na kuendelea na usafi, yule
mgonjwa anaendelea: Ila usijali mtu mzima, hii inaitwa mchana na usiku, giza na
nuru. Nyumbani kwako una wafanyakazi kibao kwenye ule mjengo wako lakini
hapa umekuja kutusafishia wodi zetu. Wajibika kiongozi, ndiyo maisha hayo na
pande zake mbili za shilingi.
Mzee anatumia hekima zake za kuzaliwa kuendelea kumpuuza. Yona anaendelea
na kazi yake ya usafi.
Mwingine kafika na kupanga foleni ya kuingia kwa daktari. Mara anapaza sauti:
Mzee Mramba eeeh!
Mramba anageuka kumtazama, yule mtu anapayuka: Nilikuwa nadhani utani,
kumbe mpo hapa mnafyekeshwa nyasi. Mimi siumwi wala nini, nilikuja tu hapa
mara moja kuwashuhudia kwa macho yangu na kuwaambia kuwa haya ndiyo
maisha. Wazee wa Ngwasuma waliimba Dunia Kigeugeu, yaani dunia imewageukia
kiukweliukweli.
Hili pia Mramba linamsikitisha, linamuondolea ujasiri wake. Anajiona mnyonge.
Anajilaumu kwa nini aliomba kifungo cha nje, maana kule gerezani angekuwa
hakutani na raia. Kifua kinajaa kwa hasira na uchungu. Anaangalia hadhi yake na
kazi anazotumikishwa. Ila hana jinsi, nyakati zilishabadilika!
Najaribu tu kuvuta picha! Mramba na Yona kufanyishwa usafi siyo jambo dogo. Ni
mambo ambayo kwa Tanzania na Bara la Afrika hatujapata kuyazoea.
Kwa wenzetu wenye kuheshimu utawala bora, mtu kuwa kigogo wa serikali leo
kisha baadaye kutupwa jela kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka ni kitu
cha kawaida kabisa.
Rod Blagojevich, alikuwa Gavana wa Illinois, Marekani. Mwaka 2009 aliondolewa
kazini baada ya kupoteza sifa kutokana na kashfa za rushwa. Hivi sasa yupo jela!
Jesse Jackson ni mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu, na mtetezi wa
Wamarekani weusi. Alifanya kazi kubwa mwaka 2008, alipomfanyia kampeni za
nguvu Rais Baraka Obama na kumuwezesha kushinda urais, hivyo kuwa rais wa
kwanza mweusi kuliongoza Taifa la Marekani.
Pamoja na mchango mkubwa wa Jesse, lakini mtoto wake, Jesse Jackson, Jr, hivi
sasa yupo jela, kwa makosa ya rushwa akitumikia kifungo cha miaka miwili na

nusu.
Jesse, Jr, kwa mwavuli wa baba yake alifanikiwa kuwa mwanasiasa anayechanua
na akawa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, akiwakilisha Chama cha Democrats,
Jimbo la Illinois 2nd District. Obama hajamkinga na jela!
William Jefferson alikuwa kigogo wa kisiasa nchini Marekani. Hivi sasa yupo jela,
akitumia kifungo cha miaka 13 jela, baada ya kukutwa na hatia ya kujihusisha na
vitendo vya rushwa.
Mwaka 2005 akiwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Jimbo la Louisiana 2nd
District, alikutwa nyumbani kwake na dola 90,000, shilingi milioni 117 kwa chenji
ya wakati huo. Fedha hizo Jefferson, maarufu kama Bill Jefferson alikuwa
amezificha kwenye friji.
Unaweza kujiuliza ni wangapi leo hii wanakaa nyumbani kwao na fedha nyingi
kiasi hicho hapa nchini. Kuna wanaoishi nyumbani kwao na mabilioni ya shilingi
bila wasiwasi wowote. Hii ndiyo Tanzania!
Marekani, mwanasiasa mkubwa alipokutwa na shilingi milioni 117 moto
ulimuwakia. Umaarufu wake ulipungua, na tangu mwaka 2012 yupo anatumikia
kifungo jela.
Hapa kwetu, yupo ambaye alibainika kuhifadhi shilingi bilioni moja Jersey,
Uingereza, alipoulizwa, alijibu: Hivyo vijisenti tu! Hajawahi kufanywa chochote
tangu mwaka 2008 alipobainika na alipojibu hivyo.
Yupo ambaye amekuwa akizungumzwa kuwa alifanya hamisho kubwa la fedha
kwenye akaunti za nje, tangu mwaka jana kabla ya Uchaguzi Mkuu, mpaka leo
hajawahi kuitwa hata mara moja kuulizwa, uhalali wa miamala aliyofanya.
Taarifa ya Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pamoja na ile
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kisha kuthibitishwa na
Bunge la 10, Novemba 2014, iliezwa kuwa ipo miamala ilihamishwa kwa magunia,
masandarusi, lumbesa na viroba Benki ya Stanbic.
Magunia ya fedha, wapi yalipelekwa? Kama siyo kwenye nyumba za watu?
Inaelezwa mgao ulikuwa shilingi bilioni 70. Je, hakuna waliokwenda kuficha
kwenye uvungu wa vitanda vyao noti za mabilioni?
Nakumbusha, Jefferson aliponzwa na shilingi milioni 117 tu, hapa kwetu, watu na
mabilioni yasiyo na maelezo wala hawachukuliwi hatua.
Andrew Theophanous alikuwa kigogo katika Baraza la Wawakilishi nchini
Australia. Makosa ya rushwa yalimpeleka jela miaka sita, na maisha ya kisiasa
yalikoma mwaka 2002 baada ya hukumu. Wenzetu wamezoea, sisi bado sana.
Inapozungumzwa hoja kuhusu Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter
Muhongo ni kwa sababu suala lake lake la kashfa ya Tegeta Escrow halijafungwa.
Wapo watu wanajaribu kusema kuwa Muhongo alipojiuzulu ilitosha, kweli? Mtu

ambaye ndiye kitovu cha wizi mkubwa kufanyika, zaidi ya shilingi bilioni 300,
zikachotwa kihuni, eti siyo jambo zito hilo.
Inavyoonekana ni kwamba Jefferson angepata kashfa hiyo akiwa Tanzania, leo hii
asingekuwa jela. Hata kuziona fedha hizo, nani angethubutu kwenda kumkagua?
Blagojevich kwa Tanzania asingefungwa, tena angekuwa anaendelea kuula
serikalini.
Wakati James Rugemalira anaendelea kudunda, ugawaji wake wa fedha, ni zaidi
ya ule wa mtu wa kati (lobbyist), Jack Abramoff, aliyetikisa Serikali ya Marekani
katika kashfa ya Jack Abramoff CNMI.
Bob Ney, akiwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Jimbo la Ohio, kwa Chama cha
Republican, alibainika kupewa fedha na Abramoff, papo hapo ukaibuliwa
uchunguzi wenye maswali mengi, wamepeana fedha za nini?
Hakukuwa na kitu zaidi ya rushwa! Abramoff na Ney, wote walihukumiwa kwenda
jela, miezi 30. Yaani miaka miwili na nusu.
Sisi huku Rugemalira aligawa fedha kama njugu, watu hawahoji. Wengine
wakasema ni za mboga.
Hivi karibuni, kuna maofisa wa serikali walishinda kesi mahakamani baada ya
kuonekana mashtaka dhidi yao hayana kichwa wala miguu.
Yaani unampeleka mtu mahakamani kwa tuhuma za rushwa. Mashtaka yako
yanasema alipewa rushwa na Lugemalira. Jaji, anauliza sasa mbona huyo mtoa
rushwa hamjamleta hapa?
Rushwa hujumuisha mtoaji na mpokeaji. Kama ambavyo Abramoff na Ney
walivyofungwa. Utani wa namna hii ni rahisi kupatikana Tanzania peke yake.
Hivyo, hapa kwetu bado hakujawa na mazoea ya kuwajibishana, ndiyo maana
adhabu hii ya Mramba na Yona naona ina maana kubwa, pengine kuliko
walivyokuwa wanaitumikia gerezani. Nitaeleza!
Lipo kundi kubwa linalalamika kuwa adhabu ni ndogo kuliko kosa. Wanahoji iweje
mfungwa wa kuku afungwe miaka 10, aliyeisababishia serikali hasara ya mabilioni
apewe kifungo cha nje? Ni haki yao kutoa maoni. Nchi huru hii!
Hata hivyo, wote wenye kutoa maoni hayo hawajui maana ya adhabu
wanayoitumikia Mramba na Yona kwa sasa.
Watu hawaadhibiwi kwa lengo la kukomoana tu, bali pia kupitisha mafunzo kwa
jamii ili itambue kuwa kuna malipo ya gharama baada ya kutenda makosa.
Mtoto aliyewaona Mramba na Yona, anapata picha kuwa kumbe nchi inaongozwa
kwa sheria. Ukifanya makosa baadaye lazima utalipia gharama kwa mujibu wa
sheria za nchi. Hii inafundisha zaidi.
Watu ambao wanalingana na babu yake, wanabebeshwa mafagio, chepe na ndoo
za kupigia deki kwa ajili ya kufanikisha usafi, kisha anatambua wanasota kwa

sababu walifanya makosa walipokuwa na nyadhifa zao serikalini.


Huwezi kuiona adhabu ya kufagia ya Yona na Mramba ni kali kama hufikirii nje ya
sanduku. Hadhi zao, mamlaka waliyokuwa nayo! Maisha yao ya jela ni wangapi
wangeyaona zaidi ya wafungwa wenzao?
Wanaposhiriki usafi kwenye maeneo ya jumuiya, wanafunzi wanaona, wanaingiza
kitu kichwani kwamba siku wakipewa dhamana za kuongoza nchi, wanatakiwa
kuwa waadilifu, kinyume chake ni kudhalilika kama taadhira wanayokutana nayo
Mramba na Yona!
Inawezekana ikawa ni adhabu ndogo kwa macho, ila utaiona ni ngumu kama
utavaa uhusika wa Mramba na Yona! Binadamu tumeumbwa na aibu. Mtu wa
kawaida tu kutumikishwa kazi hawezi kuona sawa, itakuwa Yona na Mramba?
Fikiria japo kidogo tu, umekuwa kiongozi, ukilindwa, ukipanga bajeti za nchi,
ukisaini mikataba mikubwa kati ya serikali na wawekezaji, kila waziri anakutazama
wewe apate fungu, ni wewe ndiye unamiliki hazina, benki kuu ipo chini yao. Leo
unakuwa msafisha vyoo hospitali!
Wakiwa jela wanakuwa tu simulizi. Fulani na fulani wamefungwa, lakini vifungo
vyao havitoi fundisho kama kuwaona kwa macho.
Hata mwanamuziki Nguza Viking Babu Seya na mwanaye, Johnson Nguza Papii
Kocha, adhabu yao haifundishi chochote. Watu wanasimuliana tu, yupo jela,
picha hutoa elimu kubwa kuliko simulizi.
Binafsi naona adhabu hii ya Mramba na Yona ina faida kubwa kwa jamii kuliko
walipokuwa jela. Watu wengi watakuwa wakiwaona na kuelimika kuhusu umuhimu
wa uadilifu. Kesi ya Babu Seya na Papii, ni ya kihistoria lakini haifundishi jamii.
Watu hawawaoni, hawanyooshewi vidole. Mramba na Yona kwa sasa
wananyooshewa vidole.
Ndimi Luqman Maloto

You might also like