You are on page 1of 4

SUMBAWANGA SI UCHAWI NA USHIRIKINA TU

By Habari Tanzania | Published 02/9/2007 | Jamii |

WENGI wetu tukisikia jina Sumbawanga ni wazi kuwa fikra zinakwenda


moja kwa moja kuwa ni uchawi, ushirikina na pengine kifo. Ukweli ni
kwamba ni jina lililotoholewa kwenye neno Sumbu wanga, likiwa na
maana ya tupa uchawi , na lilianzishwa na mtawala mmoja wa zamani
wa eneo hilo aliyeitwa Mwene Ngalu.

Sumbawanga ni makao makuu ya mkoani Rukwa, uliopo Nyanda za Juu


Kusini Magharibi mwa Tanzania. Mkoa huu unapakana na nchi za
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Zambia, Burundi na mikoa ya
Tabora na Mbeya na una jumla ya watu milioni 1.5, kwa mujibu wa
sensa ya mwaka 2002. Ulianzishwa rasmi mwaka 1972.

Mkoa huo una makabila mbalimbali ila kabila kubwa na la asili ni


Wafipa ambao ndiyo asili ya jina Sumbawanga, mji ulioanzishwa
mwaka 1803, chini ya chifu wa kwanza wa Ufipa aliyeitwa Kapufi
ambaye alitawala miaka ya 1885. Chifu Kapufi wa Kwanza alianza milki
yake ndani ya Ufipa yote na makao yake makuu yalikuwa Kijiji cha
Kisumba nje kidogo ya mji wa Sumbawanga. Mke wake aliitwa Mwene
Wakulosi ambaye walijaliwa kupata watoto watatu, wa kwanza wa
kiume na wawili waliofuata wa kike ambao ni Mwene Kiatu wa pili
aliitwa ‘Mwene Ngalu Chisichaafipa’ (jina la utawala) na wa tatu aliitwa
Mwene Mwati.

Baada ya kifo cha Chifu Kapufi wa Kwanza, milki ilitawazwa kwa


mwanae wa kwanza, Mwene Kiatu ambaye alihamia kijiji cha Lwiche
ambako kwa mila na desturi za kiutawala, ukitawazwa kuwa chifu ni
lazima uhame na kwenda kuanzisha kijiji chako kama alivyofanya
Mwene Kiatu.

Katika kipindi chake cha utawala wa eneo la ufipa, chifu Mwene Kiatu
hakujaliwa kupata watoto na alipokufa, milki ilichukuliwa na dada yake,
Mwene Ngalu ambaye ndiye mwanzilishi wa Sumbawanga.

Chifu Mwene Ngalu alikuwa mtu mwenye upendo na hakupenda uchafu


wa aina yoyote ukiwamo uchawi, hivyo kabla ya kuingia kijiji cha
Sumbawanga alichokianzisha, aliwataka wananchi waliomfuata watupe
uchafu wote kwenye mto Lwiche pamoja na uchawi kisha waingie
wakiwa safi.

Kutokana na imani hiyo watu walitupa uchawi wote na taka nyingine


kisha wakaingia kijiji cha Sumbawanga wakiwa wasafi. Aliyekiuka amri
hiyo na kuvuka mto Lwiche kutaka kuingia kijiji kipya cha Sumbawanga
alikufa katika mto huo.

Hapo ndipo ikawa asili ya Sumbawanga na kijiji kikawa na watu walio


wasafi na hakukuwa na matatizo na utawala wa Mwene Ngalu.
Alipendwa na kila ilipotokea ishara ya matatizo ndani ya ufipa ilikuwa
rahisi kutatuliwa kwa kuwa Chifu Mwene Ngalu aliomba na majibu
yalipatikana haraka, hasa kwa imani ya usafi waliokuwa nao.

Hata hivyo Chifu Mwene Ngalu alijaliwa kupata watoto saba ambao
wote aliwazalia katika nyumba yake ya utawala iliyojengwa kwa kipindi
cha miaka miwili katika mwaka 1918 hadi 1920 chini ya usimamizi wa
Mabruda wa dhehebu la Roma yaani wakatoliki ambao walikuwa
Wajerumani.

Nyumba hiyo hivi sasa imebomoka na limebaki gofu ambalo kwa nje
kuna sehemu ya makaburi yanayotumika kuzika kizazi cha utawala
huo, na jambo la ajabu kwenye gofu hilo wapo nyuki waliojenga
kwenye pango na wapo kwa muda mrefu tangu kipindi cha uhai wa
baadhi ya watawala wa kizazi hicho.

Watoto wa Mwene Ngalu ni Maria wa Ngao, Joseph Kapufi wa Ngao,


Thadeo wa Ngao, Teresia wa Ngao, Jacob wa Ngao, Victoria wa Ngao na
Antony wa Ngao, ambao baada ya kifo cha mama yao, mtoto wa
kwanza Joseph wa Ngao alitawazwa kuwa Chifu wa kizazi hicho na
kupewa jina la Joseph wa Ngao-Kapufi wa Pili.

Chifu huyo aliyejaliwa watoto wanne, ambao ni Olanda Joseph, Adolf


Joseph, Veneranda Joseph na Yovita Joseph na alipofariki dunia
nduguye ambaye ni mdogo wake wa mwisho, Antony wa Ngao
alitawazwa mwaka 1989, kuwa Chifu wa Ufipa na kupewa jina la Kapufi
wa Tatu.

Kapufi huyo wa tatu, Antony wa Ngao, alitawala ufipa tangu mwaka


1989 hadi Desemba 6 mwaka jana alipofariki dunia na kuzikwa kwenye
eneo la makaburi ya kizazi cha utawala huo, karibu na jengo la Mwene
Ngalu ambalo hivi sasa limebaki gufo tu.

Katika kipindi cha utawala wake, Chifu Kapufi wa Tatu, alijaliwa kupata
watoto watatu ambako mkewe wa kwanza alijaliwa kupata mtoto
mmoja wa kike aliyeitwa Ntalu na mke mdogo alijaliwa kupata watoto
wawili wa kiume ambao ni Oscar na Apolinary. Hata hivyo baada ya
kifo cha Kapufi wa Tatu, hivi sasa ukoo huo wa kichifu uko kwenye
mchakato wa kutafiti mrithi wa kiti hicho.

Msemaji wa familia ya akina Kapufi Adolf Joseph (61), ambaye ni mtoto


wa Chifu Joseph wa Ngao wa Pili, anasema jinsi ya kumpata mrithi huyo
ni kwa njia ya kuwashirikisha wazee wa mji huo (wa zamani) walio hai
hivi sasa pamoja na wale wa vijiji vya karibu kisha kuteua majina
kadhaa na kuyachambua kupata anayestahili.

Anasema jina la mrithi likipatikana sherehe za kumsimika kuwa Chifu


wa kabila hilo huanza kufanyiwa maandalizi, na kwa kawaida hufanywa
nje ya mji kwa kutengeneza sehemu maalumu ya kumpitishia ambayo
huiita mzingo. Pia huvuka mto Lwiche kwa imani kuwa ni moja ya
hatua za kudhihirisha kiwango cha usafi wake kabla ya chifu mtarajiwa
kutawazwa.

Baada ya sehemu hiyo kukamilika kutengenezwa chifu mtarajiwa


hupitishwa kwa nyuma kuingia kwenye mzingo huo huku akipuliza
filimbi tatu, ya kwanza ikikataa kulia hupewa ya pili nayo ikigoma
hupewa ya tatu ambayo nayo ikigoma ni dalili kuwa hafai kuwa chifu,
hivyo huenguliwa na kutafutwa mwingine.

Adolf anasema ikiwa filimbi moja au mbili zikilia na moja kugoma


watampa utawala wa muda huku wakijiandaa kumtafuta chifu
mwingine, kwa imani kuwa filimbi zote lazima zilie kwa sababu ni
ishara ya sifa njema za utawala za kiongozi anazopaswa kuwa nazo
ndipo apewe mamlaka.

Wakati mchakato huo ukiendelea, wa kumpata mrithi wa kiti hicho,


mavazi ya Chifu Kapufi wa Tatu, Antony wa Ngao amepewa Vicent
Kafumu ambaye ni mjukuu wa Chifu Mwene Ngalu kwa mzaliwa wake
wa kwanza aliyeitwa Maria wa Ngao.

Pamoja na hayo yote pia enzi za utawala wa viongozi hao walitumia


silaha mbalimbali ambazo hadi leo baadhi yake zimehifadhiwa ili
mtawala ajaye akabidhiwe kwa ajili ya kudumisha mila. Zana hizo ni
upinde (ulapwa), mishale (ncheto), fimbo (wasi), mkuki (ilawa) na
chombo cha kubebea mishale (untontowaancheto). Silaha nyingine ni
shanga (inkasi) zinazovaliwa mikononi na shingoni kwa chifu, kiti cha
miguu mitatu (kisumbi) na vazi la kujifunga kiunoni na mabegani
(seketa) ambayo husukwa kwa pamba.

Anasema mabadiliko ya dunia na teknolijia na mapinduzi ya kilimo kwa


kiasi kikubwa zilibadilisha mtazamo na fikra za wakazi wa
Sumbawanga ambako muingiliano wa watu ulipoanza imani ya uchawi
na ushirikina zilipungua na watu wakaingia katika shughuli za uzalishaji
mali ingawa baadhi yao wanaendelea na ushirikina kama zilivyo
sehemu nyingine nchini.

Mabadiliko hayo pia yalipunguza nguvu ya kuabudu mizimu


iliyokuwapo hapo awali kwa kuwa misitu mingi ilifyekwa kwa ajili ya
shughuli za kilimo na ufugaji hivyo, imani ya kuwapo mizimu iliondoka
kwa asilimia kubwa na watu wakabakia kuabudu katika nyumba za
ibada kufuatana na imani ya dini zao, anasema Adolf.

Hata hivyo bado kuna sehemu au vijiji vyenye kuendelea kuamini


mizimu na ushirikina kama vile kijiji cha Chipu kilicho kilomita kama 30
kutoka Sumbawanga mjini na vijiji vya Milanzi na Kalambo ambavyo
bado imani ya uchawi na vitendo vya kishirikina vinaendelea kwa
baadhi ya wakazi wake.

Kwa kijiji cha Milanzi baadhi ya wakazi wake hutumia mapango yaliyo
kwenye mlima uitwao Itwelele kwa kufanya matambiko na mambo
mengine ya kishirikina kwa imani kuwa mizimu iliyopo huko huwasaidia
kutekeleza mahitaji yao na kumdhuru mtu au watu waliotenda makosa
na kuyakana.

Adolf anasema hilo siyo tatizo kubwa kwa sababu hakuna


anayemdhuru mgeni anayeingia mkoani hapo kwa kufanya shughuli
zake kama vile biashara au kilimo. Ila kwa wale ambao hawajafika
Sumbawanga hudhani kuwa huo ni uchawi na ushirikina tu, dhana
ambayo si ya kweli kwa kuwa maendeleo yanayopatikana katika karibu
makabila yote nchini hivi sasa yapo pia Sumbawanga

You might also like