You are on page 1of 8

TOKEO FATIMA

SWALI: Ni namna gani Mama Bikira Maria aliwatokea wale watoto watatu
Fatima?

Ndugu zangu, kwa kifupi kabisa, ni kweli kabisa kwamba Mama Bikira Maria
aliwahi kutokea kule Fatima na aliwatokea watoto watatu. Watoto hao watatu ni
Lusia, aliyekuwa na umri wa miaka 10, Fransisko, aliyekuwa na umri wa miaka 9
na Yasinta aliyekuwa na umri wa miaka 7.

Ndugu zangu, Bikira Maria aliwatokea (mara sita tangu) mnamo tarehe 13 Mei
1917, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia (vita vilivyodumu kuanzia 1914-
1918) kipindi hicho watu waliteswa na kuuawa wengi. Kila mara alipowatokea,
aliwahimiza kusali rozari kila siku, na mwezi wa kumi aliwajulisha kwamba
“Mimi ni Bikira wa Rozari”. Watoto hao watatu waliombwa kusali sana, kutoa
sadaka kwa ajili ya uongofu wa wakosefu.

Ndugu zangu, watoto hawa watatu yaani Lusia, Fransisko na Yasinta walikuwa ni
ndugu wa karibu sana. Fransisko na Yasinta walikuwa ni watoto wa baba na mama
mmoja, lakini Lusia alikuwa ni binamu yao. Lusia alizaliwa tarehe 22.3.1907
katika kijiji kilichoitwa ALJUSTREL na wazazi wake ni Antonio dos Santos na
Maria Rosa wote hawa walikuwa ni wakazi wa Aljustrel kijiji kimojawapo huko
Fatima nchini Ureno.

Ni namna gani Mama Bikira Maria aliwatokea wale watoto watatu wa


Fatima?

Basi, kuhusu namna ambavyo Mama Bikira Maria aliwatokea hawa watoto watatu
wa Fatima yaani Lucia, Fransisco na Yasinta, ninawaalika sasa muendelee
kunifuatilia kwa makini katika masimulizi yafuatayo juu ya namna ambavyo mama
yetu Bikira Maria alivyowatokea wale watoto watatu kule Fatima nchini Ureno.

Ndugu zangu, katika vijiji vingi vilivyo katika nchi ya Ureno wakati huo, watoto
walio wengi kabla hawajafikia umri wa kwenda shule walikuwa wakichunga
kondoo. Ndivyo ilivyokuwa pia kwa watoto hawa watatu wa kijiji hicho cha
Fatima yaani Lusia, Fransisko na Yasinta. Hawa nao walikuwa wakichunga
kondoo wao kama kawaida katika bonde moja lililoitwa Cova da Iria. Ndipo
wakiwa mahali hapo, mama Bikira Maria aliwatokea, hiyo ilikuwa ni tarehe
13.5.1917. Ndugu zangu, lakini kabla ya Mama yetu Bikira Maria hajawatokea,
kwanza kabisa aliwatokea malaika wa amani, malaika huyu aliwatokea ili
awaandae kwa ujio wa Mama Bikira Maria.

Katika matokeo yote, watoto hawa yaani Lusia, Fransisko na Yasinta waliweza
kumtambua Bikira Maria kwamba ni Mama wa Mungu na anatoka Mbinguni,
kwani walimwona wote watatu naye aliwatokea mara nyingi bila kificho.

Katika tokeo la kwanza la Bikira Maria kwa hawa watoto hapo tarehe 13.5.1917,
inasemekana kwamba siku hiyo walikwenda kuchungia kondoo wao kwenye
shamba la akina Lusia, lililokuwa kwenye bonde moja lililoitwa Cova da Iria.
Safari ya kufika kule ilikuwa ndefu kidogo, nayo njia ilipitia katika bonde moja
lenye mawe mawe na magugu mengi. Hata hivyo mwishowe walifika kule bondeni
salama. Watoto hawa walichagua sehemu mojawapo waliyoona kuwa inawafaa
wakakaa hapo na kuanza kucheza mchezo wa kujenga ukuta mdogo wa mawe
kama wafanyavyo watoto wa umri wao, huku wakiangalia kondoo wao
wasiwatoroke.

Ndugu zangu, inalezwa kwamba wakati Fulani bado wakiwa hapo, mwanga Fulani
mkubwa kama vile mwanga wa radi ulitokea ghafla. Watoto hawa walishituka nao
wakafikiri kuwa hiyo bila shaka ni radi, na hivyo inaweza kusababisha kukawa na
mvua kubwa. Kwa hiyo Lusia aliwashauri wenzake warudi nyumbani. Nao kwa
haraka waliwakusanya kondoo wao na wakaanza kutelemka kutoka mlimani
wakirudi nyumbani. Walipofika mbele kidogo wakiwa karibu na mti mmoja
mkubwa, mara mwanga ukawamulika tena, basi hapo wakaongeza mwendo kwa
hofu ya kukutwa na mvua kubwa. Inaelezwa kuwa, baada ya kwenda hatua chache
tu hivi mara walimwona mbele yao mama mmoja amesimama akielea kiwepesi juu
ya mti mmoja mdogo!

Tena, inaelezwa kwamba mama huyo ambaye alikuwa amezungukwa na mwanga,


alikuwa mzuri mno ajabu. Alivaa mavazi meupe yanayong’aa ajabu. Wale watoto
waliduwaa wakabaki midomo wazi na macho yao yakiwa yamemkazia huyo mama
mzuri aliyekuwa karibu sana nao. Nao katika hali isiyoelezeka, walijiona wamo
ndani ya ule mwanga uliokuwa umemzunguka Mama Bikira Maria, mwanga huo
ukawa unatoka kwa Mama Bikira Maria na kuwaendea wale watoto watatu, sawa
kama ambavyo mwanga wa jua uiendeavyo milima na kuienea.
Mwishowe huyo mama alifungua mdomo wake na kusema, “Msiogope,
sitawadhuru.” Hapo Lusia akamuuliza, “Umetoka wapi?” Naye mama huyo
akajibu “Nimetoka Mbinguni.” Lusia akamuuliza tena akisema, “Unataka
tufanye nini?” Naye mama huyo akajibu akisema “Nimekuja kuwaambia kuwa,
kuanzia leo nataka muwe mkifika hapa tarehe 13 ya kila mwezi na saa hii hii
kwa muda wa miezi sita mfululizo, baadaye nitawaambia mimi ni nani na
ninataka nini kwenu.”

Ndugu zangu, hapo Lusia bila shaka kwa maongozi ya Mungu akakumbuka
kumuuliza huyo mama akisema, “Umetoka Mbinguni, je mimi nitafika
Mbinguni?” “Ndiyo utafika Mbinguni.” Huyo mama alimhakikishia. “Na
Yasinta” Naye atafika mbinguni?.” “Na Fransisko je?” Hapo mama huyo baada
ya kunyamaza kwa muda kidogo akajibu akisema, “Fransisko pia atafika mbinguni
lakini kwanza lazima asali rozari nyingi.” Kisha mama huyo akawauliza watoto
hao akisema, “Je, mko tayari kujitolea na kuvumilia mateso na magumu yote
atakayopenda Mungu kuwaletea ili yawe malipizi kwa ajili ya dhambi na ukosefu
wa shukurani kwake vinavyomchukiza sana na kwa ajili ya uongofu wa
wakosefu?” Watoto hao wakajibu, “Ndiyo tuko tayari.”

Basi, baada ya watoto hao kukubali hivyo, Mama Bikira Maria akawaambia,
“Tazama mtapata mateso mengi, lakini neema ya Mungu itawasaidia na kuwapa
nguvu na faraja”. Ndugu yangu, Watoto hao baadae walisema kuwa mama huyo
wakati alipotamka maneno alifungua viganja vya mikono yake kwa mara ya
kwanza na kutoka humo ulichomoka mwanga ukaenda kama vile mwanga wa taa
kubwa ya kuangazia usiku, mwanga huo ukapenya ndani ya mioyo yao nao
wakajiona ama wakajikuta wamo ndani ya Mungu ambaye huo mwanga ndiye
yeye. Ndani ya mwanga huo waliweza kujiona wazi na vizuri zaidi kuliko
wawezavyo kujiona ndani ya kioo safi. Halafu kwa nguvu hiyo waliyoipata ya huo
mwanga, mara walishitukia wamepiga magoti chini nao wakawa kama vile ndotoni
wakirudia rudia kimoyomoyo wakisema: “Ee utatu Mtakatifu, nakuabudu, Ee
Mungu wangu ninakupenda katika sakramenti kuu.” Baadaye kidogo mama
huyo aliagiza akasema, “Salini rozari kila siku ili kupata amani duniani na ili
vita iishe”.

Tukumbuke kwamba wakati huo ulikuwa ni wakati wa vita ya kwanza ya dunia.


Naye baada ya kusema maneno hayo akaanza kuinuka na kupaa juu polepole
akielekea upande wa mashariki huku ule mwanga uliomzunguka ukionekana kama
ambao ndiyo unampasulia njia angani na ukizifanya mbingu ziwe kama
zinafunguka na mwishowe mama huyo mzuri akatoweka katika ubuluu wa anga la
mbali.

Kwa hiyo, mama huyo mzuri aliendelea kuwatokea watoto hao tarehe ileile kila
mwezi kuanzia mwezi huo wa tano hadi mwezi wa kumi. Habari za matokeo hayo
ya mama mzuri zilizidi kuenea na hata mwishowe viongozi wa serikali nao
wakapata taarifa kuwa eti kule kijijini Fatima, kuna watoto wanaoleta uzushi wa
ajabu ajabu na kusababisha vurugu. Hivyo mkuu wa mji bila ya kuchelewa alituma
askari, nao watoto hao wakaenda kukamatwa na kupelekwa mahabusu ili
huko wakapate kuhojiwa vizuri. Basi, pamaja na kupewa vitisho vya kila aina
hawakusema kitu. Basi mbinu zote ziliposhindikana waliwatoa mahabusu na
kuwarudisha nyumbani.

Ndugu zangu, kwa vile watoto hao walikuwa mahabusu, kumbe wali chelewa ile
ahadi ya Yule mama mzuri ya kukutana nao hapo tarehe 13.8.1917. Hivyo badala
yake aliwatokea tarehe 19.8.1917, Na siku hiyo mama huyo aliahidi kufanya
muujiza kusudi watu wote wapate kusadiki. Mama huyo aliwasisitiza tena kusali
rozari kila siku.

Katika tokeo la mwisho la mwezi wa kumi yaani tarehe 13.10.1917, siku hiyo
watoto hao watatu walisindikizwa safari yao na wazazi wao, walianza safari
mapema ili waweze kuwahi ingawa mvua ilikuwa inanyesha, pia ulikuwepo
msongamano mkubwa sana wa watu kuliko siku zingine zote, watu hao
inasemekana walikuwa zaidi ya elfu sabini. Walipofika mahali penyewe yaani
kwenye bonde la Cova da Iria, Lusia aliwaomba watu wote waliofika hapo
wakunje miamvuli yao ili waanze kusali pamoja rozari, maana ilikuwa inanyesha
mvua kubwa sana. Watu walifanya hivyo, na baadaye kidogo watoto hao
wakauona ule mwanga ambao huwa ndiyo unatangulia ujio wa huyo mama kutoka
mbinguni, nao wakajua tayari anakuja.

Mara baada ya mwanga huo kutokea mvua ilikatika ghafla na ajabu zaidi watu
wakaanza kuona zile nguo walizovaa zilizokuwa zimelowa kwa sababu ya mvua
zote zikakauka ghafla kwa namna isiyojulikana wala kuelezeka. Na baada ya muda
mfupi mama alionekana katika mti mdogo uleule. Ndipo Lusia akamuuliza,
“Unataka tufanye nini?” Ndipo safari hii huyo mama kama ambavyo alikuwa
amewaahidi, akajibu na kusema, “Nataka pajengwe kanisa hapa kwa heshima
yangu. Mimi ni Bikira Maria wa rozari. Endeleeni kusali rozari kila siku.”

Baadaye mama huyo alifungua viganja vya mikono yake na mara humo ikatoka ile
mishale ya mwanga naye akaielekeza nuru hiyo ya mwanga juu kwenye jua. Hapo
Lusia alisema kwa sauti ya juu ya kuita akiwaambia watu, “Tazameni jua,” hapo
kila mtu alinyanyua macho yake na kutazama jua. Hapo uso wa nchi mara ghafla
uliingiwa na hali fulani isiyo ya kawaida na ambayo haikuweza kuelezeka ikoje
ama imekuwa vipi ama kutolewa mfano wake. Halafu mwanga wa jua mara
ulipungua nguvu zake, mtu akaweza kulitazama hilo jua bila mwanga wake
kuweza kuumiza macho, ingawaje hakuna mawingu yoyote yanayolifunika. Ndipo
watu wakazidi kulikazia macho jua kila mmoja akishangaa nini kinatokea. Lakini
mshangao wao huo ulizidi kuongezeka pale walipoona jua hilo limeanza kutikisika
na kufanya miondoko ya kushitua shitua. Baadaye kidogo lilianza kuzunguka
likawa kama vile gurudumu linaloendeshwa na mtambo wa mashine, nalo wakati
linafanya hivyo likawa linatoa mishale ya mwanga wenye rangi mbalimbali tofauti
pande zote kwa kasi sana. Lilifanya kitendo hicho mara tatu.

Hatimaye jua hilo liliondoka pale mahali lilipokuwa kwa kuchomoka na likaanza
kutelemka likishuka chini kwa watu, hali likigeukageuka na joto lake likawa
linazidi kuongezeka kila linaposogea. Hapo watu walilia kwa hofu kuu, kila
mmoja akiamini kwamba huo ndiyo mwisho wa dunia, kila mmoja alilia na
kutamka sala aliyoijua mwenyewe.

Ndugu zangu, mwisho jua hilo lilipofika sehemu fulani, lilisimama na kutulia.
Watu walibana mioyo yao na kushikilia pumzi kufa na kupona vifuani pao
maana hawakujua jambo ambalo lingefuata. Halafu baadaye kidogo jua hilo
lilianza kupanda juu kwa namna na mwendo uleule lililojia na lilipofika pale
mahali pake, lilitulia na kuanza kuangaza tena kama kawaida. Wakati huo huo pale
penye hilo jua wale watoto watatu walikuwa wameyaona yafuatayo: Kwanza,
alionekana mtoto Yesu na mama yetu Bikira Maria akiwa amevaa mavazi
meupe na amejitanda shela yenye rangi ya samawati. Pia Mtakatifu Yosefu na
mtoto Yesu walionekana wanaubariki ulimwengu kwa sababu walifanya
ishara ya msalaba kwa mikono yao kama ambavyo hufanya padre anapotoa
Baraka.
Basi ndugu zangu, kama mmenifuata vizuri katika masimulizi haya mafupi ya
matokeo ya mama Bikira Maria kwa watoto watatu yaani Lusia, Fransisko na
Yasinta kule Cova da Iria katika kijiji cha Fatima nchini Ureno mtaweza
kufahamu sasa kwamba, Bikira Maria alipowatokea hao watoto, ingawa walikuwa
ni watoto waliweza kumwona, na baada ya yeye mwenyewe kujitambulisha
kwamba yeye ni Bikira Maria wa rozari na kwamba ametoka mbinguni. Watoto,
waliweza kumtambua, na hapo ndipo aliwapa maagizo mbalimbali likiwamo kusali
rozari ili kuleta amani duniani.

Tena, katika tokeo la mwisho yaani tokeo la tarehe 13.10.1917, si Bikira Maria tu
alionekana, bali watoto hao waliweza kuwaona pia Mtakatifu Yosefu na mtoto
Yesu wakibariki ulimwengu. Kwa sasa watoto hao wa Fatima wote wamekwisha
fariki. Fransisko ndiye aliyekuwa wa kwanza kufariki, alifariki tarehe 4.4.1919
akiwa na umri wa miaka 11, akifuatiwa na Yasinta aliyefariki tarehe 20.2.1920
akiwa na umri wa miaka 10, na wa mwisho alikuwa ni Lusia aliyefariki mwezi wa
pili mwaka 2005 akiwa na umri wa miaka 98.

Basi, baada ya kueleza namna ambavyo Mama Bikira Maria aliwatokea


watoto wa Fatima kama ndugu yetu alivyohoji, sasa naomba nimalizie majibu
yangu na maagizo ya mama yetu Bikira Maria kwa wale watoto wa Fatima na
kwa ulimwengu wote.

Kama tulivyoona hivi punde katika masimulizi mafupi ya matokeo ya Mama


Bikira Maria kwa watoto watatu wa Fatima kwamba moja kati ya maagizo
aliyowaachia ilikuwa ni kusali rozari. Rozari ni litania ya Salamu Maria. Sala ya
salamu Maria ilitokana na Malaika Gabrieli alipomsalimu Bikira Maria, unaweza
ukarejea Injili ya Luka 1:28, na pia ilitokana na Elizabeti, unaweza pia ukarejea
Injili ya Luka 1:42.

Kumbe basi maamkio haya mawili yaani maamkio ya malaika yaani “Salamu
Maria umejaa neema Bwana yu nawe” na maamkio ya Elizabeti mara baada ya
kujazwa na Roho Mtakatifu yaani, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote naye
(Yesu) mzao wa tumbo lako amebarikiwa,” hutengeneza sehemu ya kwanza ya
Sala ya Salamu Maria, sehemu ya pili yaani, “Maria Mtakatifu mama wa
Mungu utuombee sisi wakosefu sasa na saa ya kufa kwetu,” iliongezwa na
Kanisa ambalo limeruhusu kusali kwa nia njema.

Kumbe mama Bikira alipowaambia watoto hao na watu wote wa ulimwengu huu
wasali sana rozari takatifu, ni wazi kabisa alipenda na anapenda tumwombe yeye
atuombee kwa mwanae Yesu Kristu Mungu na Mkombozi wetu, kama
alivyowaombea watu waliotindikiwa divai katika harusi ya Kana, rejea Injili ya
Yohane 2. Nasi pia tumwombe atuombee kwa Mungu, Mama Bikira Maria ni
mwombezi wetu. Ndugu zangu, mama yetu Bikira Maria, alieleza kwamba kwa
kusali rozari tutawaombea wakosefu, tutawaombea marehemu toharani, na
tutatuliza moyo wake wenye huzuni kutokana na dhambi zetu.

Ndugu zangu, pamoja na kuwaambia watoto hao wasali sana rozari mama Bikira
Maria alitoa maagizo mengine ikiwa ni pamoja na: Wanadamu tuache dhambi
na tufanye malipizi ambayo kwa kifupi ni tujitahidi kila mmoja kutimiza
vema kiaminifu wajibu wake halali wa kila siku, kujitolea kwa moyo safi wa
Bikira Maria na kuzitolea na kuziombea nchi zote zenye kueneza mafundisho
ya uongo na yenye kudanganya ulimwengu na kupotosha wengi.

Ndugu zangu kwa kumalizia tu naomba niseme kwamba, matokeo ya mama Bikira
Maria kule Fatima ni moja kati ya matokeo mengi sana ya Bikira Maria hapa
duniani, anachosisitiza Mama yetu ni kusali rozari ili kupata amani duniani na kwa
ajili ya uongofu wa wakosefu. Ndugu zangu tukisali rozari na kufuata maagizo
aliyotuachia tutaweza kuipatia dunia yetu amani na kupata uongofu. Basi
nawaalika tuzidi kusali Rozari Takatifu mara kwa mara na ikiwezekana kila siku,
ili kupitia rozari hiyo Takatifu tumwombe mama Bikira Maria atuombee kama
alivyofanya katika harusi ya Kana (rejea Injili ya Yohane sura ya 2), ili tuweze
kuwa na amani na kupata uongofu.

Asanteni Sana.

TUMSIFU YESU KRISTU.

You might also like