You are on page 1of 19

2019

IMARISHA NDOA YAKO

Mr. Steward Dominicus Mkisi Mrs. Mkisi (Veronica B. Mkisi)

Mwandishi: STEWARD DOMINICUS MKISI


MKISI FAMILY
10/1/2019
IMARISHA NDOA YAKO

IMARISHA NDOA YAKO


UTANGULIZI
Ndoa ni nini? Ni maafikiano rasmi baina ya mwanamume na mwanamke ili waweze
kuishi pamoja kama mume na mke; Ndoa ni chuo.
Ndoa ni taasisi iliyoanzishwa na Mungu mwenyewe na hakuna taifa au jamii yo yote ile
inayoweza kusimama na kusema wao ndiyo waanzilishi wa ndoa. Kuoa au kuolewa siyo
jambo la kubahatisha, ni maamuzi halali ya mtu binafsi na makubaliano kamili ya hiari
baina mwanamume na mwanamke ya kukubaliana kuishi pamoja mume na mke.
Ndoa ni mchakato wa mwanamume kuacha wazazi wake na mwanamke kuacha wazazi
wake na kuungana pamoja na kuwa mwili mmoja yaani mke na mume. Kazi ya Mungu
ya uumbaji haikukamilika mpaka alipomuumba mwanamke.
Mungu alikuwa na uwezo wa kumuumba mwanamke kutoka mavumbini kama
alivyomuumba Adamu, lakini aliamua kufanya mwanamke kutoka ubavuni mwa Adam.
Soma Mwanzo 2:18-24 “…Adamu akasema, sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu,
na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa
katika mwanamume”.
Mungu alifanya hivyo ili kutupatia mfano sisi kwamba ndoa ya mwanamume na
mwanamke ni mfano wa kuwa mwili mmoja. Huu ni umoja wa kushangaza wa mioyo
na maisha ya wanandoa. Aidha Mungu alipanga ndoa iwe ya kudumu siyo ya muda
mfupi (Mathayo 19:6), na kwa mujibu wa Biblia Takatifu, Mungu alianzisha ndoa ili
watu wazaliane kwa kufuata utaraibu wake unaokubalika na kuwalea watoto wao
(Malaki 2:14, 15). Mungu alianzisha ndoa ili zitumike kuwaburudisha mume na mke
pamoja na kusahau taabu na shida walizopitia au uchovu waliopata wakati wa kazi
(Soma Yeremia 33:10, 11), na mapenzi ni ya muhimu sana katika ndoa (Wimbo Ulio
Bora 4:9,10). Aidha Mungu ameweka kanuni za ndoa kwa wanaotaka kuoana ambazo
zipo ndani ya upendo na siyo hisia za mapenzi kama mnyama na pia ndoa ni ishara ya
Yesu Kristo na Kanisa lake (Waefeso 5:21-32).
Kwa upande mwingine, Mungu anataka ndoa iheshimiwe na watu wote (Waebrania
13:4) kwa sababu kukosekana kwa uaminifu ndoa huvunja au msingi wa ndoa wote wa
kuanzisha kwa uhusiano wa mume na mke hubomoka (Mathayo 5:32). Ndoa inaweza
kudumu kama Mungu alivyopanga iwapo wanandoa wataishi kwa kuaminiana na
kujitoa kikamilifu kila mmoja kuwa mwaminifu (Soma Mwanzo 24:58-60).
Katika somo hili la IMARISHA NDOA YAKO tutajifunza mambo saba ambayo ni; Umoja
kupitia Kuelewa Kusudi la Mungu kuhusu ndoa, Umoja kupitia Kuelewa vizuri wajibu
wa mke kwa mumewe, Umoja kupitia Kuelewa wajibu wa mume kwa mkewe, Umoja
kupitia mawasiliano mazuri, Umoja kupitia makubaliano ya fedha, kukuza umoja wa
kujamiiana, Umoja kupitia wanandoa kuwa na falfasa ya malezi ya watoto, na kukuza
na kudumisha umoja kupitia dini ya familia.

1
IMARISHA NDOA YAKO

SURA YA KWANZA
UMOJA UNAOIMARISHWA KUPITIA KUFAHAMU MWONGOZO WA MUNGU KUHUSU
NDOA
Mwanzilishi wa ndoa ni Mungu mwenyewe na hakuna binadamu ambaye anaweza
kubadili kusudi la Mungu la kuanzisha ndoa zaidi ya Mungu mwenyewe. Kila mtu
anatakiwa kutekeleza kusudi la Mungu la kuanzisha ndoa na siyo kuharibu msingi wa
ndoa ambao Mungu ameuweka. Mungu anataka Mwanamume na mwanamke waoane
kwa kufuata utaratibu uliyowekwa.
Mungu ameuweka Mwongozo au katiba ya Ndoa kwa wanandoa hata kabla ya Adam na
Hawa kumkosea Mungu.
Mwongozo wa Ndoa uliotolewa na Mungu umeandikwa katika vitabu vinne tu katika
Biblia Takatifu, umeandikwa mara moja katika Agano la kale kabla ya Adam na Hawa
kutenda dhambi na umeandikwa mara tatu katika Agano Jipya.
Mwongozo huo una hatua tatu ambazo zinatakiwa kufuatwa ambazo ni kuacha,
kuambatana na kuwa mwili mmoja ambazo nitazifafanua vizuri katika kitabu hiki.
Lengo la somo hili ni kumsaidia mume na mke kujifunza wote pamoja kwa ajili ya
kukuza na kuboresha ndoa yao na kujua maana halisi ya kuacha wazazi, kuambatana
mume na mke na kuwa mwili mmoja.
A. Ninavyofahamu mimi katika Biblia Takatifu Mungu ametamka mara nne tu kauli
moja ya kuhusu ndoa au amesisitiza Mwongozo wa Ndoa au katiba ya Ndoa
mara nne katika Biblia Takatifu.

1. Amesema katika kitabu cha mwanzo 2:24, Mathayo 19:5, Marko 10:7, 8 na
Waefeso 5:31, ‘...na kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na
mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili
mmoja’.
2. Mungu ameirudia kauli hii mara nne katika Biblia takatifu, kama nilivyosema
awali aliitoa mara moja katika Agano la kale kabla ya la anguko la dhambi
kwa binadamu (Adamu na Hawa kutenda dhambi) na ameitoa mara tatu
baada ya anguko la dhambi katika Agano la Jipya. Kurudia kwake Mungu
kauli hiyo kuna maanisha kwamba huo ndio Mwongozo wa Mungu kuhusu
Ndoa takatifu kwa binadamu mwenye dhambi na aliyeanguka katika dhambi.
Kwa ujumbe huo au kauli hiyo, Mungu anataka ndoa bora/takatifu na siyo
bora ndoa au ndoa ya takafujo kwa wanandoa.
B. Mwongozo mzuri unaotakiwa katika ndoa nzuri ambayo Mungu anaitaka ni ule
ambao una mpango mkakati au (mradi ujenzi/building project).
1. Leo, wanandoa wengi hawana furaha, wana machungu, wana majeraha ya
ndoa, hawatimiziani au hawatoshelezani mahitaji yao ya ndoa si tu kwa
ndoa za wasio wakristo, hata ndoa za wakristo matatizo hayo yapo.

2
IMARISHA NDOA YAKO

2. Kukosekana kwa furaha huko kwa sehemu kubwa kumesababishwa na watu


kushindwa kuzingatia Mwongozo wa Mungu kuhusu Ndoa ambao aliutoa
mapema kabla ya Adamu na Hawa kutenda dhambi na hata baada ya
kutenda dhambi aliwakumbusha mwongozo wa ndoa kwa wanandoa.
3. Tujiulize, Kwa nini Mwongozo wa Mungu kuhusu Ndoa? Ndoa ya Mungu
inahusisha vitu gani?
HATUA TATU MUHIMU ZA KUZINGATIA KABLA YA KUINGIA KATIKA NDOA
Mungu ametoa Mwongozo wa ndoa ambao una hatua tatu amabazo zinatakiwa
zizingatiwe na zifuatwe kwa utaratibu huo. Hatua hizo ni; i} Kuacha, ii} Kuambatana
na iii} Kuwa mwili mmoja.
Kila hatua ina mambo mengi ambayo yanatakiwa yafanyike na yatekelezwe kwa
kufuata utaratibu pia wa jamii husika bila kuathiri Mwongo wa Mungu kuhusu ndoa ili
ndoa hiyo ikubalike mbele za Mungu. Hatua hizo naweza kuzielezea moja baada ya
nyingine kama zilivyokaa kwa mpangilio katika vitabu vyote vinne katika Biblia
Takatifu kama ifuatavyo:-
I. Kuacha Wazazi: - Mwongozo wa Mungu kuhusu ndoa unamtaka mwanamume na
mwanamke wawaache wazazi wao (baba na mama wawaache peke yao).
A. Ina maana gani kuacha wazazi wako?
1. Haina maana kwamba uwaache wazazi wako wajihangaikie
wenyewe na maisha yao wala usiwasaidie cho chote. (Linganisha
Kutoka 20:12; Marko 7:9-13 na 1Timotheo 5:8)
2. Haina maana kwamba uhame eneo au mahali ambako wazazi wako
kijiografia wanaishi uende ukaishi maisha ya ndoa mahali kwingine
au sehemu ambayo wazazi wako ni vigumu kufika. Kuishi karibu
sana na wazazi wakati wa kuanza maisha ya ndoa kunaweza
kukuwia vigumu kuwaacha wazazi wako, lakini pia unaweza
ukawaacha wazazi wako huku unaishi mlango wa pili kutoka kwa
wazazi wako. Kinyume chake, unaweza ukaishi mbali sana na
wazazi wako ambako hawawezi kufika baada ya kuoa au kuolewa
lakini ukawa bado hujawaacha wazazi wako. Ki ukweli, unaweza
usiwaache wazazi wako hata kama walikwisha fariki dunia miaka
mingi iliyopita.
B. Kuacha Wazazi wako inamaanisha kuwa uhusiano wako na wazazi
wako lazima ubadilike sana:-
1. Ina maaana kwamba unaanzisha uhusiano wa utu uzima na wao
(wazazi wako),
2. Ina maana kwamba lazima usikilize zaidi mawazo, ushauri na
matendo ya mke wako kuliko wazazi wako na wakati mwingine
unapuuzia mbali ushauri na mawazo ya wazazi wako.

3
IMARISHA NDOA YAKO

3. Ina maana kwamba ni lazima uache utegemezi kutoka kwa wazazi


wako wa kumpenda mkeo au mumeo, kuidhinisha, kusaidia na
ushauri wa namna ya kuishi katika ndoa yako.
4. Ina maana kwamba lazima uondoe na kupinga waziwazi vikwazo
vyote vinavyowekwa na wazazi wako katika ndoa yenu, mihemko
ya wazazi wako bila kujali umbali uliopo kati yako na wazazi
pamoja na kupinga mitazamo mibaya au hasi ya wazazi wako kwa
mkeo au mumeo.
5. Inamaanisha kuwa unatakiwa uzuie majaribio yote ya wazazi ya
kukutaka kukuondolea upendo wako kwa mwenzi wako kwa
sababu ya yeye alivyo, mfano mwonekano wake hauwavutii wazazi
(sura au maumbile yake hayawaridhishi wazazi).
6. Inamaanisha kuwa unafanya uhusiano wa mume na mke kuwa
kipaumbele chako cha uhusiano wa kibinadamu;-
a. Ndiyo, unatakiwa kufikiria kuhusu kuwa kijana mzuri/bora
au binti mzuri/bora au mama au baba, lakini unatakiwa
kufikiria zaidi kuwa mume bora/mzuri au mke bora/mzuri
kuliko kuwa kijana mzuri au binti mzuri au baba mzuri au
mama mzuri. Watoto hawahitaji wazazi wenye kutia moyo
ambao hawapendani wao kwa wao hawajaliani, kila mmoja
yupo kivyake. Watoto wanahitaji wazazi ambao
wataonyesha jinsi ya kukabiliana na kutatua shida. Watoto
wanahitaji wazazi ambao watawaonyesha jinsi ya kuwa
waume na wake wazuri, jinsi ya kuhusishwa au kushirikiana
na watu wengine.
b. Kama ninyi ni wazazi, malengo yenu yanapaswa kuwa ni
kuwaandalia watoto mazingira ya kuondoka na siyo kukaa
nanyi. Wazazi hamtakiwi kuwalea watoto kwa mfumo wa
kuandaa mazingira ya maishi yenu kuwategemea watoto
wenu au mnaandaa mazingira ya kuendelea kuishi na
watoto wenu, kwa sababu kufanya hivyo mnaweza
kuwasababishia watoto wenu wakawa walemavu kifikra au
kimawazo.
c. Wazazi mnatakiwa kujiandalia mazingira mazuri mapema ili
siku watoto wenu wakiondoa hakuna kitakacho punguza
upendo wenu wa awali na kutegemeana ninyi kwa ninyi.
d. Watoto wenu wakioa au wakiolewa, hamtakiwi kuingilia
mfumo wao wa maisha wala kuwawekea vikwazo maishani
mwao. Wazazi mnatakiwa muwaachie uhuru wanandoa hao
wapya waume na wake hao waanze maisha yao mapya ya
ndoa wenyewe, wafanye maamuzi, waidhinishe na kila
mmoja awajibike kwa mwenzi wake bila kuingiliwa na
wazazi. Mnatakiwa kuwafundisha na kuwahamasisha watoto

4
IMARISHA NDOA YAKO

wenu (mabinti na vijana wenu) kujitegemea wenyewe


(kutegemea wenzi wao) na siyo kujivunia malezi yenu,
msaada wenu, upendo wenu na mshikamano wenu.
Katika hatua hii ya kwanza ya kuacha wazazi, mambo mojawapo ambayo hufanyika ni
pamoja na kutambulishana kwa wazee wa kanisa, wachungaji, wazazi, kulipa mahari,
kutangaza uchumba pamoja na kuvalishana pete ya uchumba au kupeana kitu cha
kuashiri wamechumbiana, kuaga wazazi (send-off) pamoja na ununuzi wa vyombo vya
kuanzia maisha bila kusahau ujenzi wa nyumba ya kuishi au kupanga nyumba nzuri
kama muoaji hana nyumba.
Hatua hii ya kwanza, maandalizi ya mahali pa kuwapelekwa wanandoa watarajiwa
hufanyika kwa ajili ya fungate ya ndoa (honeymoon), vikao vya harusi hukaliwa au
kamati za harusi hufanyika, ununuzi wa pete za harusi na pamoja na semina za ndoa
kwa watarajiwa hao hufanyika.
II. Kuambatana: - Hatua ya pili katika Mwongozo wa Mungu kuhusu Ndoa
unawataka waume na wake kuambatana pamoja.
A. Siku hizi vijana wengi wanaoa au kuolewa wakiwa na mawazo kwamba kama
ndoa zao zitakwenda kinyume na matarajio yao watatalikiana au
wataachana na kuoa au kuolewa kwingine.
1. Wakati wanaoana, wanaapa (wanaweka nadhiri) kuwa watakuwa
waaminifu mpaka kifo kitakapo watenganisha lakini mioyoni mwao
wanasema isipokuwa wakati wa matatizo magumu au shida nzito
tutaachana.
2. Kiukweli, kuna watu wanatoa maoni kuwa vyeti vya ndoa viwe
vinahuishwa kama ilivyo kwa leseni za udereva au ATM za Bank ili kama
mtu anaona hawezi kuendelea katika ndoa asitishe ndoa yake. Na
wengine wanasema kilisahaulika cheti cha kuwazawadia waoaji kwa
kuhangaika namna ya kumpata mke wa kumuoa ili awe anaingia nacho
kwenye sherehe ya kuoa au harusini.
3. Kwa wao, ndoa ni jambo rahisi, la bahati, na linaweza kuwa la muda
mfupi tu. Yote inategemea jinsi kadi au leseni zinavyoisha muda wake
wa matumizi au kupotea.
B. Lakini Mungu anasema, “Hapana, huo si mpango wangu. Nilipanga ndoa iwe
ya kudumu (uhusiano wa kudumu) siyo ya muda mfupi. Nataka mume na
mke waambatane pamoja” (Marko 10:2-10)
1. Unajua ndoa si jambo la bahati nasibu, bali ni maumuzi ya makusudi au
ni chaguo la makusudi.
2. Ndoa si jambo la kurahisisha, ndoa inahitaji utii na kuvumiliana kwa hali
ya juu sana.
3. Ndoa siyo suala la namna gani kadi au leseni inaisha muda wake, lakini ni
kiasi gani uko tayari na umedhamiria kuifanyia kazi mapungufu
yanayojitokeza katika ndoa.

5
IMARISHA NDOA YAKO

C. Ndoa nzuri inategemea zaidi kujidhabihu au kujitolea au kumakinika kuliko


hisia au kuvutiwa kama wanyama.
1. Kwa mujibu wa kitabu cha Malaki 2:14 na Mithali 2:17, ndoa ni agano
ambalo haliwezi kuvunjwa na upande wo wote wa wanandoa.
2. Kwa hiyo, wawili hao wanapooana wanaahidiana kuaminiana bila kujali
kitu gani kitatokea maishani mwao.
a. Mke huahidi kuwa atakuwa mwaminifu kwa mume wake bila kujali
mapungufu atakayokuwa nayo, hata kama mume wake atapoteza sura
yake ya awali, atakuwa maskini, atashambuliwa na magonjwa, hata
kama atapoteza afya yake, utajiri wake, kazi yake, haiba yake; hata
ikiwa kuna mtu wa kufurahisha zaidi anakuja.
b. Mume huahidi kuwa atakuwa mwaminifu kwa mke wake hata kama
mke wake atapoteza mvuto wa awali, umbile lake litabadilika, hata
kama ni mchafu na hamtii kama alivyokuwa anataka, hata kama
hamtoshelezi kabisa kimapenzi na hata kama ana matumizi mabaya
ya fedha au matumzi ya kijinga au hajui kupika.
c. Ndoa ina maana kuwa mume na mke wanaingia katika uhusiano kwa
kukubaliana kila mmoja kutimiza wajibu wake wote kwa mwenzi
wake kwa umakini na kwa hiari yake mwenyewe bila kulazimishwa na
mtu mwingine na atajidhabihu kutunza uaminifu huo bila kujali
matatizo yatakayotokea.
D. Kwa namna nyingine kuolewa au kuoa (kuoana) ni kuwa kama Mkristo.
1. Wakati mtu anapoamua kuwa mkristo au kuokoka huacha maisha yake ya
zamani (maisha ya kale), haki zake za zamani, jitihada zake binafsi za
kujiokoa, na kumrudia Yesu Kristo ambaye alikufa kwa ajili ya wenye
dhambi.
2. Katika kitendo hicho cha mtu kumkubali Yesu Kristo kuwa Bwana na
Mwokozi wa maisha yake, anajitoa au anajiungamanisha mwenyewe kwa
Kristo. Kitendo cha kuokoka kinaambatana na kuamini moyoni na kukiri
kwa kinywa chake kwamba anampokea Yesu Kristo kuwa Bwana na
Mwokozi wa maisha yake na kuahidi kuacha matendo yote maovu
(dhambi) na kuanza kumtumikia Yesu Kristo bila kujali jaribu lolote
litakaloibuka kwa lengo la kumkatisha tamaa katika kumfuata Yesu
Kristo. (Soma Warumi 10:9-11; Matendo 16:31; Wafilipi 3:7,8 na
1Wathesolonike 1:9,10)
3. Kwa hiyo, ndoa ya iliyopangwa na Mungu inahusisha kujitoa kikamili kwa
mume na mke na kuahidiana kuendelea kupendana na kuishi pamoja bila
kujali cho chote kitakachotokea mpaka kifo kiwatenganishe.
a. Mpango wa Mungu kuhusu Ndoa unahusisha mume na mke
kuambatana pamoja katika ugonjwa na afya, umaskini na utajiri,
raha na maumivu, furaha na huzuni, nyakati njema na nyakati
mbaya, kwa makubaliano na pasipo makubaliano.

6
IMARISHA NDOA YAKO

b. Ndoa hii iliyoanzishwa na Mungu ina maana kuwa watu wanatakiwa


wajue kuwa matatizo yatawapata, na wanatakiwa wajadiliane namna
ya kuyatatua, wanatakiwa pia watafute msaada wa Mungu katika
kutatua matatizo hayo na siyo kukimbia au kuachana kwa sababu
hakuna njia nyingine ya kumaliza matatizo zaidi ya kukaa pamoja na
kujadiliana huku wakimshirikisha Mungu kutatua shida zao za ndoa.
Wanandoa wanatakiwa wajitoe wenyewe kikamilifu kushughulikia
maisha yao bila kutegemea upande wo wote wa ndugu zao. Ni lazima
wanandoa waambatane kila siku mpaka kifo kitakapo watenganisha.
Hata hivyo, katika hatua hii ya pili ya kuambatana mambo mengi hufanyika kwa pande
zote mbili mume na mke, kama vile kula kiapo cha uaminifu, kuvalishana pete za
ndoa, kupeana zawadi, sherehe za harusi, wosia kutoka kwa mchungaji pamoja na
wazazi au ndugu wa wanandoa hao, n.k
III. Kuwa Mwili Mmoja: - Hatua ya tatu katika Mwongozo wa Mungu kuhusu ndoa
inaeleza kuwa mume na mke wakiambana na wanakuwa si wawili tena bali ni
mwili mmoja. Kazi ya Mungu ya uumbaji haikukamilika mpaka alipomuumba
mwanamke. Mungu alikuwa na uwezo wa kumuumba mwanamke kutoka
mavumbini kama alivyomuumba Adamu, lakini aliamua kufanya mwanamke
kutoka ubavuni mwa Adamu. Soma Mwanzo 2:18-24 “…Adamu akasema, sasa
huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi
ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume”.
Mungu alifanya hivyo ili kutuonyesha sisi mfano halisi kwamba ndoa ya
mwanamume na mwanamke ni muunganiko wa kuwa mwili mmoja.
A. Katika kiwango chake cha msingi, hii inahusu uhusiano wa kimapenzi au
umoja wa kidunia.
1. Fikiria 1 Wakorintho 6:16
2. Ndani ya mipaka ya ndoa, uhusiano wa kimapenzi ni mtakatifu, mzuri, na
ni mwema, lakini ikiwa mume na mke wameingia katika uhusiano wa
kimapenzi bila kupitia hatua mbili nilizozisema za “kuacha wazazi na
kuambatana” wanatenda tendo mbaya, wanadidimiza hadhi ya tendo la
ndoa na wanatenda dhambi ya uasherati au uzinzi. (Soma Waebrania 13:
4)
B. Lakini kuwa mwili mmoja kunahusisha zaidi ya tendo la ndoa.
1. Kwa kweli, tendo la ndoa ni ishara au kilele cha umoja kamili zaidi wa
kujitoa kabisa kwa mtu mwingine. Kwa hiyo, ikiwa mwili mmoja hauna
uhalisia, uhusiano wa kimapenzi unapoteza maana ya ndoa.
2. Maana nyingine ya ndoa tunayoweza kuisema ni kwamba, Ndoa ni agano
kamili na ushirikiano mkamilifu wa mume na mke mpaka hadi kifo
kiwatenganishe.
a. Mpango wa Mungu katika ndoa ni kuwa watu wawili wa jinsia tofauti
waoane na washirikiane pamoja kimwili, kwa mali/miliki zao, maono

7
IMARISHA NDOA YAKO

yao, mateso yao, furaha zao, mawazo yao, uwezo wao, matatizo yao,
mafanikio yao, kushindwa kwao, n.k.
b. Mume na Mke ni timu moja na cho chote atakachofanya mmoja wapo
lazima atambue kuwa anafanya kwa ajili ya mwenzake au angalau sio
lazima awe anazingatia au anajali mahitaji ya mwenzake (Waefeso
5:28; Mithali 31:12, 27).
c. Mume na mke si wawili tena bali ni mwili mmoja. Na hii dhana ya
mwili mmoja lazima ijidhihirishe kwa njia ya matendo siyo kwa
maneno ya mdomoni tu, ielewezwe kwa kuonyesha matendo. Mungu
hakukusudia hiyo iwe dhana tu au nadharia bora, lakini ni dhana
yakinifu (dhana ya ukweli). Urafiki kamili na umoja wa ndani ni
sehemu ya Mwongozo wa Mungu kuhusu ndoa.
3. Urafiki kamili na umoja wa ndani sana, hata hivyo, haumaanishi kuwa ni
wanafanana au wanakuwa sawa kimawazo na kimsimamo katika hali ya
kiroho.
a. Mfano, Mwili wangu umeumbwa na viungo mbalimbali, Mkono wangu
hauwezi ukafanya kazi ya mdomo, moyo wangu hauwezi ukafanya
kazi ya ini na wala masikio hayawezi kufanya kazi ya kichwa.
b. Kila kiungo katika mwili kina kazi yake lakini vina umoja. Viungo
vyangu vya mwili vinaonekana tofauti na vina tenda kazi tofauti,
lakini uhalisi ni kwamba kila kiungo kina fanya kazi kwa manufaa au
kwa faida ya viungo vingine na kiungo kimoja hakiwezi kamwe
kikajaribu kukiumiza kiungo kingine.
c. Kazi za viungo vya mwili ni sawa na kazi za mume na mke ambazo
zinafanyika ndani ya ndoa na wanaweza wakawa wanaoneka tofauti
kwa sura, kimo, kimaongezi, kielimu, kiheshima na hata kiimani
lakini hawatakiwi kuruhusu tofauti zao kuzuia au kuharibu umoja wao
katika ndoa kwa sababu kusudi la Mungu kuhusu ndoa ni kuwa mwili
mmoja, kuwa na umoja kamili.
C. Lakini tambua kwamba kuwa mwili mmoja (umoja kamili-total oneness)
ambako Mungu anataka wanandoa tufikie siyo rahisi sana kufanikiwa kama
hatutazingatia Mwongozo wa Mungu kuhusu Ndoa na kutambua vikwazo
vyake ambayo ni dhambi kupitia milango mbalimbali kama ifuatavyo:-
1. Mojawapo ya kikwazo kikubwa cha kuzuia wanandoa wasiwe mwili
mmoja au kuwa na umoja kamili na wanaendelea kubaki kuwa wawili
badala ya mwili mmoja ni dhambi zetu.
a. Katika kitabu cha Mwanzo 2:25, mara tu baada ya Mungu kuwaambia
Adamu na Hawa kuwa Mume na Mke wawe mwili mmoja na si wawili
tena, Maandiko yanasema, “Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu
na mkewe, wala hawakuona haya”.
b. Kuwa uchi Adamu na Hawa siyo pendekezo la jamii kuwa uchi. Hilo
lilitokea kabla ya watu kuwa wengi au kuongezeka. Adamu alikuwa
binadamu pekee ambaye alimwona Hawa akiwa uchi wa mnyama, na

8
IMARISHA NDOA YAKO

Hawa pia alikuwa mwanamke pekee aliyemwona Adamu akiwa uchi


wa mnyama.
2. Na zaidi ya yote, mambo hayo yalitokea kabla hawajatenda dhambi.
Baada ya Hawa na Adamu kutenda dhambi, maandiko yanasema, Mwanzo
3:7 “wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi,
wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo”. Mara tu dhambi
ilipoingia kwenye picha au kwenye akili zao, walianza kujificha.
a. Jaribio hilo la kujificha hakika ilikuwa ni ishara ya kutambua kwao
juu ya dhambi yao mbele za Mungu. Kwa haraka na kwa upumbavu,
walijaribu kuficha dhambi yao kwa Mungu.
b. Lakini bado kitendo cha kujifunika ni ishara ya kujaribu kufichamana
wao kwa wao. Wakati dhambi ilipoingia kwenye mioyo yao, uwazi,
uwajibikaji na kuwa mwili mmoja (umoja kamili) uliharibiwa.
3. Kwa hiyo, dhambi ilipoingia iliharibu umoja kamili wa Adam na Hawa,
kwa maana hiyo, dhambi zetu bado ndiyo kikwazo kikubwa katika umoja
kamili wa ndoa zetu (kuwa mwili mmoja) kwa siku hizi.
a. Wakati mwingine mwili mmoja ( umoja kamili katika ndoa zetu)
unaharibiwa na dhambi ya ubinafsi wa wanandoa (mume au mke).
b. Wakati mwingine mwili mmoja unaharibiwa na dhambi ya majivuno.
c. Wakati mwingine mwili mmoja unavunjwa na dhambi ya machungu au
ugumu wa maisha au kauli isiyofa (kauli mbaya kwa mume au mke) au
ukatili au ukali au kukosa shukrani au kukosa kuvumiliana au kukosa
falsafa moja ya malezi ya watoto au kukosa mawasiliano ndani ya
ndoa, kukosa watoto, kuruhusu wazazi au wana ukoo kuingilia
mipango ya maisha ya wanandoa.
d. Mwili mmoja kati ya Adam na Hawa ulivunjwa na dhambi, hivyo na
sisi leo dhambi inaharibu au inavunja mwili mmoja wa mume na mke.
e. Hivi uliwahi jiuliza kwa nini mtoto mdogo anaweza kutembea uchi
kutoka chumba kimoja hadi kingine mbele ya wageni bila kuona haya?
Mtoto haoni haya kwa sababu hajitambui kuwa yu uchi, kama
ilivyokuwa kwa Adamu na Hawa kabla ya kutenda dhambi. Baada ya
Adamu na Hawa kutenda dhambi, wajiona aibu na haya ikawafuata na
ikawatenganisha wao na Mungu. Ndivyo ilivyo kwetu tuna vikwazo vya
ndoa vinavyolingana. Dhambi isitutenganishe na Mungu na
kusababisha kumficha Mungu mawazo yetu ya siri ambayo inazuia
mawasiliano kati yetu na Mungu na kutukosesha haki zetu.
4. Sasa baada ya kutambua vikwazo au vitu vinavyotenganisha au kuvunja
mwili mmoja wa mume na mke, tunatakiwa tufanye nini kuzuia uharibifu
huo? Jibu ni kwamba, tunamhitaji Yesu Krito kuwa Bwana na Mwokozi wa
maisha yetu na ndoa zetu.
a. Jambo la kwanza kabisa, tunamhitaji Yesu Kristo atupatanishe na
Mungu tuwe na uhusiano mzuri naye. (Soma Warumi 3:10-23;

9
IMARISHA NDOA YAKO

Isaya 59:2; Wakolosai 1:21-23; Waefeso 1:7; 2:13-21;


2Wakorintho 5:21na 1Petro 3:18).
b. Lakini si kwamba tunamhitaji Yesu Kristo atupatanishe na Mungu
tuwe na uhusiano mzuri naye, pia tunamhitaji Yesu Kristo
atusaidie kuwa na uhusiano mzuri wa sisi kwa sisi (ili mume na
mke waweze kutekeleza Mwongo wa Mungu kuhusu ndoa wa
kuacha, kuambatana na kuwa mwili mmoja). Yesu Kristo alikuja
ulimwenguni kuvunja vikwazo au vifungo vilivyokuwepo kati ya
wanadamu na Mungu, kati ya mtu na mtu, hali kadhalika vikwazo
kati ya mtu na nafsi yake mwenyewe. Aidha Yesu Kristo alikuja
kuvunja uhasama au kuondoa uhasama au uadui uliokuwepo kwa
binadamu na kumfanya mtu kuwa sehemu ya mwili wake (Soma
Waefeso 2:14-16 na “Wagalatia 3:28; Hapana Myahudi wala
Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala
mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Yesu Kristo”).
Yesu Kristo pekee ndiye anayeweza kuchukua dhambi zetu na
kuondoa ubinafsi wa mwanamume na mwanamke na kuwawezesha
kuacha wazazi wao, kuambatana pamoja na kuwa mwili mmoja.
c. Ikiwa ninyi wanandoa mnahitaji kuishi katika maisha ya ndoa kwa
kufuata Mwongozo wa Mungu kuhusu ndoa ambao ni muhimu kwa
ndoa nzuri, mnatakiwa kumfuta Yesu Kristo. Yesu Kristo anavunja
vikwazo vyote. Yesu Kristo anavunja ukuta unaokutenganisha
naye, anavunja utawala wa dhambi, anasafisha dhambi zote kwa
damu yake, anawaweka huru walifungwa na minyororo ya shetani
(dhambi). Yesu Kristo huwapa watu wake Roho Mtakatifu ambaye
huzaa tunda la roho, upendo, furaha, Amani, uvumilivu, wema,
utauwa, Imani, utu wema, na kiasi. Yesu Kristo huwajaza Roho
Mtakatifu wanaume kwa wanawake ambaye huwasaidia wenye
dhambi kuacha wazazi wao, kuambatana na kuwa mwili mmoja.
Namshukuru Mungu kwa leo tumehitimisha sehemu ya kwanza ya somo hili la Imarisha
Ndoa Yako kwa kuangalia misingi mitatu ambayo ipo katika Mwongozo wa Mungu
kuhusu Ndoa na ni matumaini yangu umefurahia somo hili na nikuahidi Mungu
akipenda kipindi kijacho tutajifunza sehemu ya pili ya somo hili yenye kichwa cha
Umoja Kupitia Kuelewa Vizuri Majukumu Ya Mke Kwa Mume.
Jina langu naitwa Steward Dominicus Mkisi, a.k.a Baba Jebediah S. Mkisi na kama
una maswali, maoni au ushauri usisite kunitafuta kwa njia ya baruapepe
stewardmkisi2011@gmail.com au nipigie kupitia simu ya mkononi +255764539949
au +255692485203
Mungu wa Mbinguni akubariki na tukutane Mungu akipenda kipindi kijacho, kwa herini
na uwe na siku njema.

10
IMARISHA NDOA YAKO

UMOJA KUPITIA KUELEWA VIZURI MAJUKUMU YA MKE KWA MUME


Katika sura hii ya pili sehemu ya pili ya somo la Imarisha Ndoa Yako, tutajifunza zaidi
jinsi ya kukuza mwili mmoja kupitia kuelewa vizuri majukumu ya mke katika ndoa.
Mke ana majukumu yake ambayo anatakiwa ayafanye ambayo hayawezi kufanywa na
mume wake au amsaidie mume wake kukamilisha umoja wa ndoa. Aidha dhana ya utii
wa lazima wa mke kwa mumewe itajadiliwa kwa kina kwa lengo la kuelewa nini
maana ya kutii na Mungu anapomwambia mke na amtii mumewe anamaanisha nini ili
tafsiri mbaya iliyokaa mioyoni mwa wanaume ifutike na kila mmoja ampe nafasi
mwenzake ya kufanya au kutimiza majukumu yake katika ndoa ili ndoa ziendelee
kudumu kama Mungu anavyotaka.
A. Wachumba wengi huoana wakiwa na matarajio makubwa katika ndoa zao.
1. Wanajua kuwa ndoa nyingi zipo kwenye misukosuko na zimekosa furaha ya
kweli. Lakini wao wanafikiri kuwa wakioana ndoa zao zitakuwa tofauti na
ndoa nyingine ambazo zimekuwa na migogoro ya ndoa mara kwa mara kwa
sababu wao wanaona wanapendana kwa dhati na hakuna kitakacho
watenganisha au kitu kitakachovunja upendo wao.
2. Kwa maana hiyo, wanaanza maisha ya ndoa wakiwa na matarajio makubwa,
mara muda si mrefu, matarajio yao yanapotezwa kwa kuingia katika
mpasuko wa ndoa. Ndoa ambayo walikuwa na uhakika kuwa imefanyika
mbinguni inakuja kuanguka kirahisi duniani; nyota zinabadilika kuwa
mchanga; raha ya ndoa inabadilika na kuwa uchungu/shubiri (matumaini
yanapotea kwa kukataa tamaa kabisa na kuanza kulaani siku ya kuoa au
kuolewa).
B. Ni kimetokea?
1. Ndiyo, wawili hao hawakusomana au hawakujifunza mapema maisha yao
binafsi kuwa kila mmoja anataka baada ya kuolewa waishije au hawakujua
Mwongozo wa Mungu kuhusu Ndoa kuwa baada ya kuoana na kuwa mwili
mmoja kila mmoja anatakiwa kufanya nini kwa ajili ya mwenzake ili
kudhihirisha kwa vitendo dhana ya mwili mmoja na si wawili tena.
2. Wakati Mungu anamuumba mwanamume na mwanamke na kuanzisha taasisi
ya ndoa, hakuwa kama mvumbuzi ambaye anagundua mashine lakini
anamtaka mnunuzi wa mashine atafute namna gani mashine inaweza
kutumika na kuendeshwa na pia abainishe kila kifaa kilichopo kwenye
mashine kina kazi gani na uhusiano wake na kifaa kingine katika mashine
hiyo upoje.
3. Hapana, Mungu ametoa taarifa maalumu na maelekezo muhimu kuhusiana
na kusudi la kuanzisha ndoa na majukumu tofauti ya kila mmoja (mume na
mke) kwa lengo la kukamilisha umoja kamili wa ndoa (kuwa mwili mmoja).
Majukumu yanayofanywa na wawili hao kila mmoja na majukumu yake kwa
wakati mwafaka ndiyo yanayotengeneza ndoa. Mungu amempa majukumu
fulani mke na majuku fulani mume. Wakati wawili hao (mume na mke)
wakijua, wakikubali, na kutimiza majukumu yao tofauti lakini

11
IMARISHA NDOA YAKO

yanayokamilishana au yanayosaidiana au yanayotegemeana, umoja kamili


katika ndoa utadumu (kuwa mwili mmoja kutakuzwa). Kinyume chake,
wakati mume na mke aidha kwa kutokuelewa ama kwa kukaidi kutekeleza
majukumu ambayo Mungu amewapangia, mkanganyiko mkubwa na mpasuko
ndani ya ndoa utatokea.
C. Kwa wakati huu tujikite zaidi kujadili kwa mujibu wa Neno la Mungu
majukumu ya msingi ya mke katika ndoa. Katika sehemu inayofuata ya somo au
sura ya tatu tutajadili Majukumu ya msingi ya mume katika ndoa. (Kuna vifungu
vingi vya Neno la Mungu vinavyozungumzia majukumu ya msingi ya mke katika
ndoa. Baadhi ya vifungu hivyo ni; Mwanzo 2:18-25; Mithali 31:10-31; Waefeso
5:22-24, 33; Tito 2:4, 5; 1Petro 3:1-6.)
I. Katika Agano Jipya, mke huamriwa mara nyingi kumtii mume wake (Waefeso
5:22-24, 33; Wakolosai 3:18; 1Timotheo 2:9-12; Tito 2:4, 5; 1Petro 3:1-6.).
A. Wazo la Kutii kwa mke siyo maaurufu sana siku hizi. Wakati mwingine
mgongano wa mke kutii unatokana na uasi wa dhambi dhidi ya mapenzi ya
Mungu. Wakati mwingine, hata hivyo, inaweza kutokea kwa picha ya uwongo
ambayo tafsiri yake ya mke kumtii mume wake kwa jamii inamdunisha au
inamfanya kiumbe dhaifu mbele ya mume. Ili kurekebisha picha hii ya uwongo,
nataka kusema mambo kadhaa ambayo yapo katika Bibilia lakini tafsiri ambayo
jamii nyingi inaitumia siyo dhana sahihi kwa mke kumtii mume wake.
1. Kutii siyo dhana tu kwa wanawake, ni dhana inayowahusu waumini wote.
(Soma Waefeso 5:21; Wafilipi 2:3, 4; 1Petro 5:5; Warumi 13:1;
Waebrania 13:17). Kwa suala la kutii ni la kila mtu; mke kwa mume,
mwanamke kwa mwanamume, kijana kwa mzee. Mungu ameagiza utii kwa
watu wote na wakati mwingine tafsiri ya kutii ndiyo inayowachanganya
wengi, wengine wanadhani kutii ni kumsujudia mtu au kumpigia magoti
mume au mtu mwenye hadhi ya juu, hapana, kutii ni kitendo cha kutekeleza
agizo la Mungu kwa hiari bila kulazimishwa na anayetakiwa kupigiwa magoti
ni Yesu Kristo tu kwa mujibu wa maandiko Wafilipi 2:8-10.
2. Kutii hakumaanishi kuwa mke anatakiwa kuwa mtumwa wa mume wake.
Kwa kweli, mke huwa huru kabisa kuliko wakati wo wote pale anapotii kwa
mume wake, kwa kuwa yuko huru kutii kwa yote ambayo Mungu alimkusudia
mke kutii na si vinginevyo. (Tujifunze maelekezo ya mawazo ya Mungu kwa
mke katika Mithali 31:10-31.)
3. Kutii haina maana kwamba mke hatakiwi kufungua kinywa chake mbele
ya mumewe, hatakiwi kumshauri mume, hatakiwi kutoa maoni mbele ya
mume wake. (Angalia Mithali 31:26; Matendo 18:26; Waamuzi 13:21-23.)
4. Kutii haina maana kwamba mke anakuwa maua ya ukutani ambayo
hujinyoosha na kuficha uwezo wake kwa kukaa kimya mithili ya kinyago
au mdoli. Mungu amempatia uwezo na vipaji mbalimbali mke ambavyo
anatakiwa avitumie kwa ajili ya manufaa au faida ya mwili mmoja (ndoa
yake). Soma kitabu cha Mithali 31.

12
IMARISHA NDOA YAKO

5. Kutii hakuna maana kuwa mke ni mnyonge (kiumbe duni au dhaifu) kwa
mume wake. Yesu Kristo hakuwa mnyonge kwa Maria na Yusufu (wazazi
wake), na bado Maandiko yanaeleza kuwa kama mtoto, “Yesu aliendelea
kuwatii” (Luka 2:51). Yesu kwa namna yo yote hakuwa mnyonge kwa Mungu.
Yesu alikuwa na ni Mungu kamili, kwa kila sifa. Bado Maandishi yanaeleza
kuwa kuna utaratibu na Muundo wa Utata mtakatifu (Mungu baba, Mungu
Mwana na Roho Mtakatifu). Yesu anasema, “Mimi siwezi kufanya jambo lo
lote kwa mamlaka yangu mwenyewe. Mimi nahukumu kufuatana na jinsi
Mungu anavyoniambia. Na hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti
kufanya nipendavyo, bali nafanya mapenzi yake yeye aliyenipeleka.”
(Yohana 5:30) naye Paulo anasisitiza, “Lakini napenda muelewe kwamba
Kristo ni kichwa cha kila mwanamume, kama vile mume alivyo kichwa
cha mkewe, na Mungu ni kichwa cha Kristo” (1 Wakorintho 11:3). Kwa
kweli, haimaanishi kuwa Yesu alikuwa mnyonge kwa Mungu baba. Badala
yake Yesu anatufundisha kwamba kuna mgawanyiko wa kazi na majukumu
katika Utatu mtakatifu. Kwa mtindo kama huo, utii wa mke kwa mumewe
kwa njia yoyote haimaanishi ni udhalilishaji au unyonge. Badala yake,
inafundisha umuhimu wa kufuata utaratibu na muundo wa mgawanyiko wa
majukumu ndani ya nyumba (ndoa). Ukisoma Mwanzo 1:26,27; 2:23 na
Wagalatia 3:28 vyote hivyo vinaeleza hali ya usawa na haki ya mwanamke
na mwanamume.
B. Baada ya kujifunza mtazamo hasi au picha mbaya ya maana ya utii wa mke kwa
mumewe kwa mujibu wa Biblia Takatifu, sasa tuangalie maana halisi ya utii wa
mke katika ndoa yake kwa mtazamo chanya kwa mujibu wa Biblia takatifu;-
1. Maandishi yanaonyesha kuwa ni wajibu wa mke mwenyewe kuwa mtiifu
(kutii): - Hakuna mahali po pote kwenye Biblia ambapo panaeleza kuwa
Mungu amemuagiza mume kumlazimisha mke amtii. Badala yake maandiko
yanaeleza kuwa Mungu amemamuru mke mwenyewe kuwa mtiifu au amtii
mume wake bila kulazimishwa na mtu ye yote kwa kuwa ni agizo la Mungu
ambalo mke anatakiwa kulitekeleza. (Soma Waefeso 5:22 na 1Petro 3:1.)
2. Maandishi yanaonyesha kuwa utiifu wa mke ni lazima uwe endelevu au
usiwe na mwisho ni wa kila siku: - Katika mstari huo unaoelezea kutii kwa
mke katika vifungu vya Biblia kitenzi kipo katika wakati uliopo wa sasa
kikiwa na maana ya kwamba mke kutii ni suala la wakati uliopo wa sasa ni
suala endelevu lisilo na mwisho mpaka kifo kiwatenganishe wanandoa hao.
(Soma Waefeso 5:22 na 1Petro 3:1.)
3. Mke Kutii au kuwa mtiifu kwa mume wake ni lazima, siyo hiari: - Ukisoma
kitenzi cha Kiswahili kinachoelezea mke kutii kipo katika hali ya lazima.
(Soma Waefeso 5:21, 22 na 1Petro 3:1.) Mke kuwa mtiifu au kumtii mume
wake hakupaswi kutegemea namna gani mume anaishi na mke wake au
mume anavyomtendea mkewe. Utiifu wa mke kwa mumewe hakutegemei
kipaji cha mume, uwezo wa mume, hekima ya mume, elimu ya mume, au
hali ya kiroho ya mume. (Soma 1Petro 3:1 na Luka 2:51.)

13
IMARISHA NDOA YAKO

4. Mke Kutii au kuwa mtiifu kwa mume wake ni suala la kiroho:- Suala la
mke kumtii mume wake linafanyika kama kwa Bwana (Waefeso 5:22).
Bwana anamuamuru mke kutii kwa hiyo mke kutokuwa mtiifu au kushindwa
kutii ni kumuasi Mungu mwenyewe. Mungu ndiye aliyetoa amri kwa mke
kumtii mume wake na siyo mume ametoa amri kwa mke wake amtii. Suala
la mke kumtii mume wake ni jaribio la kuona namna gani mke anampenda
Mungu pamoja na mume wake. Kwa hiyo mke anatakiwa aangalie kuwa
mtiifu kwa mume wake kama tendo la kudhihirisha utii wake kwa Yesu
Kristo na siyo kwa mume wake. Yesu alisema, “Mkinipenda, mtazishika amri
zangu” (Yohana 14:15), na moja ya amri zake kwa wake ni, “Wake, watiini
waume zenu kama mnavyomtii Bwana” (Waefeso 5:22). Bado nasisitiza
kuwa suala la mke kumtii mume wake ni sauala la kiroho ambalo mke
ambaye ametakaswa na Yesu Kristo na kujaa nguvu za Roho Mtakatifu
hataona uzito kutekeleza amri hiyo ya kutii (Waefeso 1:1-5:21; 1Petro 1:1-
3, 6.)
5. Utiifu katika dhana nzuri (mtazamo mzuri), na siyo dhana mbaya (siyo
mtazamo mbaya):- Biblia inasisitiza zaidi jambo la mke kutii kuliko jambo
ambalo hatakiwi kutii. Kuna mtumishi wa Mungu Bill Gothard amefafanua
Kutii kuwa ni haki iliyokusudiwa. Anaendelea kufafanua kuwa utiifu ni uhuru
wa kuwa mbunifu katika kutekeleza maagizo ya Mungu. Utiifu wa mke kwa
mume ni kitendo cha mke kuwekeza nguvu zote za vipaja, uwezo,
rasilimali, nguvu yote kwa ajili ya mume wake. Utii wa mke kwa mume
wake ni uwezo wa mke kutekeleza mipango mkakati waliyopanga na mume
wake kwa ajili ya faida ya familia yao pamoja na kumshauri mume mambo
mazuri na kumkataza kufanya mambo mabaya yayoweza kuiingizia hasara
familia au ndoa yake pamoja na kumkosanisha na Mungu. Mke anajua wajibu
wake kama mjumbe mmojawapo katika maamuzi ya mipango ya familia na
mtekelezaji wa maamuzi yanayofanyika katika ndoa na humshauri mume
kwa hekima.
6. Kutii kunajumuisha mtazamo pamoja na matendo ya mke:- Yesu alikuwa
mtiifu kikamilifu kwa baba. Lakini Yesu akawajibu, “Chakula changu ni
kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma, na kuikamilisha kazi yake”
(Yohana 4:34). Alifanya kazi ya Mungu kwa moyo wa furaha na si kwa
kulazimisha. Yesu Kristo alitimiza mapenzi ya Mungu (Zaburi 40:7, 8).
Ndivyo ilivyo hata kwa mke anatakiwa kumtii mume wake kwa moyo wa
furaha pasipo na chuki wala kulazimishwa na mtu ye yote. Kwa mujibu wa
maandiko, Mungu anamtaka mke kufanya kazi kwa mikono yake mwenyewe
kwa ajili ya kuinua kipato cha familia yake (Mithali 31:13), anatakiwa
atafute mahitaji kwa ajili ya kutosheleza mahitaji ya familia yake na
kutimiza mahitaji ya mume wake. Waefeso 5:33 inaelezea mtazamo kwa
baadhi ya mambo ambayo mke anatakiwa atii kwa mume wake.
7. Utiifu wa mke ni jambo linalotakiwa liangaliwe kwa upana zaidi: - Mke
anatakiwa amtii mume wake pamoja na kanisa la Kristo (Waefeso 5:24).

14
IMARISHA NDOA YAKO

Kristo ni kichwa cha kanisa (Waefeso 1:22) na mambo yote yanafanyika kwa
utukufu wa Mungu mwenyewe (Wakolosai 3:17; Mithali 3:5, 6 na
1Wakorintho 10:31).
Kwa maana nyingine, kutii hakuna maana kwamba mke amtii mume wake
hata kama anamuamuru amkatae au amtukane Mungu, anatakiwa atii amri
za Mungu zote na atekeleze maagizo mume wake kama sehemu ya
mgawanyiko wa mamlaka kutoka katika taasisi ya ndoa ambayo ipo chini ya
Mungu. Mke anatakiwa kukataa maagizo au maelekezo yo yote
yanayotolewa na mume wake ambayo kusudi lake ni kumkosanisha mke na
Mungu, mfano mume anamuagiza mke aiende akaibe au akajiuze kwa
wanaume huko wapate fedha, hayo hatakiwi kufanya kabisa na ikiwezekana
amshughulikie kikamilifu ili amuokoe mume wake katika mikono ya shetani
(Soma Wakolosai 3:18). Mume hana mamlaka ya kumuzuia mke asifanye kile
ambacho Mungu ameagiza afanye na kushindwa kutekeleza amri au maagizo
ya Mungu ni uasi (Matendo 5:28-29).

Utii wa mke kwa mume wake ni tendo lisilo na kikomo, linatakiwa kufanyika
kila wakati, muda wo wote (asubuhi, mchana, jioni na usiku). Mke
anatakiwa kumtii mume wake kwa kila kitu ilimradi hakipingani na Neno la
Mungu. Mke anatakiwa kuwa msaidizi wa mume wake na siyo mpinzani wa
mume wake (Soma Mwanzo 2:18).

II. Kwa hiyo kutokana na maandiko tunachoweza kusema ni kwamba jukumu


la awali la mke ni kumsaidia mume wake (kuwa waziri Mkuu wa mume wake
au mtendaji mkuu katika ndoa). Wakati Mungu alipomuumba Hawa kwa ajili
ya Adamu alisema, si vema Adamu akaye pekee yake, nitamfanyia msaidizi
wakufanana naye (Soma Mwanzo 2:18-22)
A. Kutokana na maandiko haya tunapata mambo matatu muhimu kuhusu
uhusiano wa mke kwa mume wake:-
1. Mungu alimuumba mwanamke awe msaidizi wa mwanamume. Pasipo
mwanamke, mwanamume hata hali ya ukamifu wake haijakamilika.
2. Mungu alimuumba mwanamke awe msaidizi mzuri wa mume: Hakuna
mnyama ye yote kama mwanamke ambaye angeweza kusaidia
kutosheleza msaada au mahitaji ambayo mwanamume alikuwa
anahitaji. Mwanamke pekee ndiye aliyeweza kutoa msaada aliyokuwa
anauhitaji mwanamume. (Soma Mithali 18:22 na Mithali 31:10, 11).
3. Mungu alimuumba mwanamke ili kukamilisha kwa mwanamume:
Mwanamke anafanana na mwanamume lakini wanatofautiana
kimajukumu na hawapo sawa. Mwanamke anakamilisha mambo
ambayo mwanamume peke yake hawezi kukamilisha, mwanamke ni
sawa na mkanda katika kamera, kamera bila mkanda huwezi kupiga
picha au kurekodi video (1Wakorintho 11:11).

15
IMARISHA NDOA YAKO

B. Kulingana na maandiko mke aliumbwa ili kukamilisha mahitaji,


mapungufu, uhaba kwa mume wake. Aliumbwa awe msaidizi wa tofauti
kwa mume wake. Amtendee mambo mazuri siyo mabaya siku zote za
maisha yake (Mithali 31:12). Awe kama tunda zuri la nyumba ya mume
wake (Zaburi 128:3). Ni mwili mmoja na mume wake, na hili linaweza
kutimilika kwa yeye kukubali kutii na kutekeleza wajibu wa mke katika
ndoa kwa mujibu wa Mwongozo wa Mungu kuhusu ndoa.
1. Hii haina maanishi kuwa kila jambo analofanya linatakiwa liwe na
muunganiko wa moja kwa moja na mume wake. Hapana, haina
maana hiyo ila hatakiwi kufanya jambo au kazi kwa ajili ya faida yake
mwenyewe au kwa ajili ya faida ya wengine au hatakiwi
kujishughulisha na shughuli yo yote au taasisi yo yote ambayo haina
manufaa katika ndoa yake (Mithali 31:10-31).
2. Ina maana kwamba mke hatakiwi kufanya jambo lo lote ambalo
linaweza kumdhalilisha au kumuumiza mume wake kwa sababu
atakuwa amekwepa majukumu yake ya awali ya kuwa msaidizi wa
mume wake (Mithali 31:10-31).
C. Sasa kwa kuhitimisha sehemu hii ya Umoja unaopatikana kwa kuelewa
vizuri wajibu wa mke kwa mume wake, naweza kupendekeza mambo
ambayo mke anaweza kufanya kwa ajili ya kumsaidia mume wake.
Anaweza kumsaidia mume wake kwa kufanya yafuatayo:-
1. Kufanya nyumbani kuwa mahali salama kwa mume wake: mke
anatakiwa kumfariji, kumtia moyo, kumuelewa na kumfanya mume
aone nyumbani ndiyo mahali pa kukimbilia (Mithali 31:11, 20).
Usitumie utani au mambo ya kuumiuza kama sehemu ya utambulisho
kwake. Usiendelee kumkumbusha mapungufu yake, makosa yake au
kushindwa kwake. Msahihishe au mshauri kwa maneno ya
hekima/busara pale inapobidi. Epuka kuruhusu hatari ya kufanya
nyumba iwe mahali pa matembezi (shamble) na mahali palipojaa
migogoro na matukano. Vile vile, epuka hatari ya kufanya nyumba ya
maonyesho ambako kila kitu wakati wote kinakaa safi na katika hali
ya mpangilio usiobadilika, yaani mume akiweka au akihamisha kiti tu
unampigia kelele na kumtukana kama mtoto mdogo. Mume anataka
nyumba ya kuishi siyo nyumba ya maonyesho au mahali pa wageni
kufanyia utalii.
2. Uwe mwaminifu na tegemeo (Mithali 31:11, 12).
3. Tunza hekima au busara (Jibu kwa hekima na hoji kwa busara)
(Mithali 31, 26, 28-29; Yakobo 3:13-18 na Wafilipi 4:4).
4. Jadili mambo kwa upendo, uwazi na hekima (Waefeso 4:25).
5. Ridhika na cheo chake, mali zake, na majukumu yake pia (Wafilipi
4:6-13, Waebrania 13:5, 16).
6. Uwe mvumilivu, samehe na kuachilia (Waefeso 4:2, 31-32;
Waakolosai 3:12-14).

16
IMARISHA NDOA YAKO

7. Onyesha uhusika katika tatizo lake na saidiana naye kutatua tatizo


alilolipata (Wafilipi 2:3-4).
8. Jishughulishe na kazi, uwe mpenda maendeleo (frugal), mwenye
shauku na mbunifu wa miradi ya familia (Zaburi 128:3; Mithali
31:10-31).
9. Toa maoni, ushauri, na marekebisho wakati yatakapohitajika
kwa upendo (Mithali 31:26).
10. Tunza uzuri wake, hasa mambo binafsi ya ndani (1Petro 3:3-5)
11. Tunza maisha mema ya kiroho (tunza maisha ya utakatifu)
(1Petro 3; 1, 2, 7).
12. Shirikiana naye kulea watoto (Waefeso 6:20; Mithali 31:26-28 na
1Thimotheon 5:13-14).
13. Mjengee heshima na uaminifu mumeo kwa watoto: Mtazamo wa
mke kwa mume wake unaweza kuchukuliwa na watoto. Mke
akimdharau mume na watoto watamdharauli baba yao. Kukosekana
heshima, kukosa ujasiri mume katika uongozi wake, lawana kulingana
na anavyofanya huhamasisha watoto kumdharau baba yao. Mke
hatakiwi aungane na watoto wake kumdhihaki na kumtenga mume
wake. Mke ashirikiane na mume wake kuwalea watoto katika malezi
mazuri (Mithali 22:6).
14. Uwe na shukurani. Unatakiwa kutambua mchango wake kwa
kumshukuru (Warumi 13:7).
15. Onyesha ujasiri katika maamuzi yake. Kejeli, kukosa ujasiri, tamaa
au upinzani mkali wa mke juu ya maamuzi ya mume wake kunaweza
kusababisha mume atumie nguvu kutetea maamuzi yake. Kama mke
haridhiki na maamuzi ya mume wake au ana wasiwasi na maamuzi
yaliyofanyika anatakiwa atumie njia ya kuuliza swali au maswali
ambayo hayataleta ugomvi na pia maswali hayo yawe na mwelekeo
wa kuonyesha mwelekeo mzuri unaotakiwa kufuata kwa kuonyesha
matokeo hasi ya uamuzi huo na matokeo chanya yakivunjwa maamuzi
hayo kwa pande zote mbili (1 Wakorintho 13:4-8).
D. Wake wameumbwa na Mungu ili wawatii waume zao, kuwa wasaidizi
kamili wa waume zao.
1. Kwa namna nyingine naweza kusema tumejifunza namna gani umoja
unaimarishwa kupitia kuelewa vizuri wajibu au majukumu ya mke
katika ndoa.
2. Lakini kujua tu haitoshi kama hatutayaishi kwa vitendo katika ndoa
zetu. Wanandoa wanatakiwa kuyafanya haya kwa matendo katika
uhusiano wao wa ndoa na kwa kufanya hivyo tutaudhihirisha umoja
kamili wa wanandoa wa kuwa mwili mmoja.
3. Niwaombe wake chunguzeni uhusiano wenu na waume zenu kutokana
na ukweli wa neno la Mungu tulilojifunza kama unaendana. Ni kweli

17
IMARISHA NDOA YAKO

unamtii mume wako? Je, wewe ni msaidizi kweli wa mume wako?


Nikushauri pale unapoona haujatimiza fanya yafuatayo:
a. Omba toba kwa Mungu na umwombe msamaha mume wako.
b. Jitakase na dhambi hiyo na dhambi nyingine pia kwa damu ya
Yesu Kristo (Waefeso 2:12-13 na Yakobo 1:19-24).
c. Omba Nguvu za Roho Mtakatifu ili uwe mke wa tofauti na wake
wengine wanaoishi na waume zao kwa mazoea (Wagalatia 5:16,
22-23).
d. Endelea kuwa na bidii katika kusoma na kuelewa Neno la Mungu,
na fanya mabadiliko kila inapotakiwa kufanyika hivyo kwa lengo la
kumpendeza Mungu na mume wako (Wafilipi 2:12,13 na Yakobo
1:19-24).
Namshukuru Mungu kwa leo tumehitimisha sehemu ya pili ya somo hili la Imarisha
Ndoa Yako kwa kuangalia umoja unaopatikana kupitia Kuelewa Vizuri Majukumu ya
Mke katika ndoa ambayo yapo katika Mwongozo wa Mungu kuhusu Ndoa na ni
matumaini yangu umefurahia somo hili na nikuahidi Mungu akipenda kipindi kijacho
tutajifunza sehemu ya tatu ya somo hili yenye kichwa cha Umoja Kupitia Kuelewa
Vizuri Majukumu Ya Mume Kwa Mke.
Jina langu naitwa Steward Dominicus Mkisi, a.k.a Baba Jebediah S. Mkisi na kama
una maswali, maoni au ushauri usisite kunitafuta kwa njia ya baruapepe
stewardmkisi2011@gmail.com au nipigie kupitia simu ya mkononi +255764539949
au +255692485203
Mungu wa Mbinguni akubariki na tukutane Mungu akipenda kipindi kijacho, kwa herini
na uwe na siku njema.

18

You might also like