You are on page 1of 20

SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.

ME/SOMAVITABUTANZANIA

UCHAMBUZI WA KITABU; Influence


(Saikolojia Ya Ushawishi - Sehemu Ya Pili)
Karibu kwenye sehemu ya pili ya uchambuzi wa kitabu kinachoitwa Influence;
The Psychology of Persuasion kilichoandikwa na mwanasaikolojia Robert B.
Cialdini, Ph.D
Kwenye sehemu ya kwanza tumepata utangulizi wa silaha sita za ushawishi na
jinsi ambavyo zimekuwa zinatumika kuwashawishi watu kukubaliana na
wengine. Pia tumejifunza silaha mbili kati ya hizo sita ambazo ni KULIPA
FADHILA na MSIMAMO. Kwenye kulipa fadhila tukaona jinsi mtu anavyotoa
kidogo na kukitumia kupata makubwa zaidi. Kwenye msimamo tukaona jinsi
mtu akishawishiwa kuanza kufanya kitu kidogo, atakubali kufanya kikubwa
baadaye.
Sehemu hii ya pili ya uchambuzi ina mbinu nyingine mbili, KUFUATA MKUMBO
na KUPENDA. Kwa kufuata mkumbo, watu hufanya vitu ambavyo peke yao
wasingefanya. Na kwenye kupenda, wale wanaotaka kushawishi, wanamfanya
mtu apende kitu na akishakipenda anakubaliana nacho.
Karibu kwenye uchambuzi wa sehemu hii ya pili, tuzijue silaha nyingine mbili za
ushawishi, jinsi zinavyotumiwa na namna ya kuepuka kulaghaiwa nazo.

SILAHA YA TATU; KUFUATA MKUMBO (SOCIAL PROOF).


Silaha ya tatu kwenye silaha sita za ushawishi ni kufuata mkumbo. Sisi
binadamu ni viumbe wa kijamii, hivyo huwa tunaathiriwa sana na kile ambacho
watu wengine wanafanya. Tunapoona kundi kubwa la watu linafanya kitu
fulani, basi tunaamini hicho ni kitu sahihi kufanya, hivyo tunashawishika
kufanya pia.
Kama tulivyoona kwenye silaha nyingine za ushawishi, silaha hizi zinagusa njia
za mkato ambazo tumekuwa tunazitumia kufikia maamuzi bila ya kufikiri sana.
Kwa sababu muda na nguvu ni chache na maamuzi ya kufanya ni mengi,
tumekuwa tunarahisisha maamuzi tunayofanya kwa kuangalia njia za mkato
tunazoweza kutumia.
Hivyo ndivyo kufuata mkumbo kulivyo, pale tunapokuwa njia panda, tusijue
nini cha kufanya, tunaangalia wengine wanafanya nini na kile kinachofanywa
na wengi tunaona ndiyo sahihi.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Kuna mpaka kauli ambazo zinaonesha jinsi tunavyoamini kwenye wingi, kauli
kama WENGI WAPE au PENYE WENGI HAPAHARIBIKI NENO zinaonesha jinsi
jamii zetu zimejengwa kufuata mkumbo.
Pamoja na manufaa makubwa ambayo kufuata mkumbo yanayo, hasa
kuturahisishia kufanya maamuzi, kuna hatari. Wale wanaojua jinsi ya kutumia
silaha hii kushawishi, wanaweza kutengeneza mazingira yanayotufanya tuone
wengi wanafanya kitu fulani hivyo ni sahihi kwetu kufanya na kumbe siyo
kweli. Hapa tunakwenda kuona jinsi silaha hii inatumika kushawishi na jinsi ya
kuepuka kushawishiwa vibaya kwa silaha hii.

Ukweli ni sisi.
Kama umewahi kuangalia vichekesho kwenye tv utagundua baadhi ya
vichekesho vina sauti za kucheka ambazo zinaambatana na vichekesho hivyo.
Sauti hizo zinaweza kuwekwa kwenye tukio ambalo hata halichekeshi, lakini
kwa kusikia sauti zikicheka, unaona hilo ndiyo jambo sahihi kufanya, unacheka
pia.
Wanaotumia njia hii kwenye vichekesho wanajua msingi mkuu wa kijamii
ambao ni kilicho sahihi kufanya ni kile kinachofanywa na wengi. Kwa kifupi,
kwenye jamii ukweli huwa unaonekana kuwa pale walipo wengi. Hivyo
unapokuwa njia panda na hujui kipi sahihi kufanya, huwa unaangalia wengi
wanafanya nini na kufanya hicho pia.
Hata unapoenda ugenini, huwa unaangalia wenyeji wanafanya nini na kisha
kufanya kwao. Iwe ni jinsi ya kusalimia, kula na mengine, huwa tunapata
mwongozo wa kilicho sahihi kwa kuangalia wengi wanafanya nini.
Kwa sehemu kubwa, msingi huu wa kufuata mkumbo una manufaa,
unatupunguzia kufikiri na kufanya maamuzi kila mara hasa kwa uhaba wa
muda na nguvu tulionao. Ukifika mahali ambapo ni mgeni na ukakuta watu
wanafanya au hawafanyi kitu fulani, kuna sababu nyuma yake, kama huna
muda wa kuchunguza sababu hiyo, utakuwa salama zaidi kama utafanya kama
wao kuliko kufanya tofauti.
Lakini hili linatuweka kwenye hatari ya kushawishiwa vibaya na wale ambao
wanatumia msingi huu kutushawishi kukubaliana na kitu, kwa sababu tu
wanatuambia wengine nao wanakubali.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Mfano wa wanaotumia silaha ya kufuata mkumbo.


Silaha ya ushawishi kwa kufuata mkumbo imekuwa inatumiwa na wengi kwa
sababu ina nguvu, pale tunapoona wengine wanafanya kitu, tunasukumwa
kufanya pia na kuamini ndiyo kitu sahihi.
Mfano wa watu wanaotumia silaha hii ni mingi, lakini michache na ambayo
unakutana nayo kila siku ni hii;
1. Omba omba huwa wanaanza kwa kuweka kiasi fulani cha fedha kwenye
chombo chao cha kuombea. Unapopita na kuona kwenye chombo kuna fedha,
unaona kwamba wengine wametoa hivyo ni sahihi na wewe kutoa pia.
Kadhalika wale wanaotaka kuwashawishi watu kutoa zawadi, huwa wanaanza
kwa kuweka kiasi fulani cha zawadi kwenye eneo la kutolea.
2. Wahubiri mbalimbali wanaotaka watu watoe shuhuda, huwa wanaandaa
watu wao wachache wanaoanza kutoa shuhuda na hapo wengine kuona ni kitu
sahihi kufanya na kutoka kutoa shuhuda.
3. Wafanyabiashara huwa wanatangaza kwamba bidhaa yao inatoka haraka na
wengi wameshaipata, yote hiyo ni kukushawishi kwamba wengi wanaitumia
hivyo na wewe unapaswa kuitumia. Matangazo kama wajanja wote wanatumia
bidhaa/huduma hii huwa yanakuvutia na wewe utumie pia.
4. Pale mfanyabiashara anapokuwa na bidhaa au huduma zaidi ya aina moja
ambazo zinaendana, huwa anaweka nembo kwenye moja na kusema hiyo
ndiyo inatoka zaidi. Kama unajikuta njia panda hujui uchague ipi, ujumbe huo
unakufanya uchague ile ambayo imeandikwa inatoka zaidi, kwa sababu
unaamini ndiyo itakuwa sahihi.
5. Watu wa mauzo huwa wanatumia shuhuda mbalimbali za wale ambao
wameshanunua bidhaa au huduma wanayouza ili kuwafanya wateja
wanaowalenga waone ni wanapaswa kununua bidhaa au huduma hiyo.
Watu hao na wengine wamekuwa wanatumia msingi wa kufuata mkumbo
kuwashawishi watu kukubaliana nao.

Asilimia 95 ni waigaji.
Mwandishi anamnukuu Cavett Robert ambaye ni mkufunzi wa mauzo ambaye
amekuwa akifundisha kwamba kwenye jamii yoyote ile, asilimia 5 tu ya watu
ndiyo waanzilishi au wabunifu, asilimia 95 iliyobaki ni waigaji. Hivyo watu
wengi huwa wanashawishika zaidi na matendo ya wengine kuliko kile

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

wanachoambiwa. Unachohitaji ili kuwashawishi watu wengi ni kuwaonesha


wachache ambao wanafanya kitu fulani na hapo wataiga.
Wachache wanapoanza kufanya kitu, kisha wengine wakaiga, hapo kanuni ya
kufuata mkumbo inaendelea kufanya kazi yenyewe. Kadiri watu wanavyozidi
kuiga, ndivyo wengi zaidi wanavyovutiwa kuiga.
Kanuni ya kufuata mkumbo inaeleza wazi kwamba kadiri idadi kubwa ya watu
inavyofanya kitu, ndivyo wengi zaidi wanavyoshawishiwa kwamba hicho ndiyo
kitu sahihi kufanya.
Wale wanaotumia silaha hii kushawishi wengine, wanahitaji kuanza na kundi
dogo la watu, ambalo litavutia wengine na baada ya hapo kundi litaendelea
kuvuta wengi zaidi na zaidi.

Nguvu ya silaha ya kufuata mkumbo.


Kila silaha ya ushawishi ina hali na mazingira ambayo ina nguvu zaidi. Silaha ya
kulipa fadhila inakuwa na nguvu kubwa pale mtu anapokuwa amepokea kitu
kutoka kwa mwingine, anakuwa ametengenezewa deni ambalo atasukumwa
kulilipa. Silaha ya msimamo huwa inakuwa na nguvu pale mtu anapoweka
msimamo wake wazi, anasukumwa kuulinda ili asionekane ni mtu asiye na
msimamo.
Silaha ya kufuata mkumbo huwa inakuwa na nguvu zaidi pale mtu anapokuwa
hana uhakika, anapokuwa njia panda na hajui nini afanye, hapo ndipo
anaangalia wengine wanafanya nini na kuwafuata.
Hivyo wale wanaotaka kuwashawishi watu kwa njia hii, huwa wanawajengea
hali ya kukosa uhakika, huwa wanawaweka njia panda na kisha kuwasukuma
kuangalia wengi wanafanya nini ili nao wafanye.
Pale mtu anapokuwa hana uhakika na kipi cha kufanya, pale hali inapokuwa
haieleweki na mtu kujikuta njia panda huwa ni rahisi kuangalia wengine
wanafanya nini na unapoona wengi wanafanya kitu fulani, unaamini ndiyo kitu
sahihi kufanya.

Ujinga wa kundi.
Tabia ya kuangalia wengine wanafanya nini ndiyo mtu ajue kilicho sahihi
kufanya, imekuwa inazalisha hali ya ujinga wa kundi. Ambapo unakuta kundi la
watu wanafanya kitu, ila hakuna hata mmoja anayejua kwa nini anafanya. Kila
mtu anakuwa anaangalia wengine wanafanya na yeye anafanya.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Kila mtu anafanya kwa kuangalia wengine wanavyofanya, akiamini wengine


wana sababu ya kufanya hivyo, kumbe hakuna anayejua, kila mtu anafanya
kwa sababu wengine wanafanya.
Hali hii imekuwa inasababisha matatizo makubwa kijamii. Mfano mzuri ni pale
mtu anapopata shida akiwa kwenye kundi la watu, labda anaibiwa au
ameumwa ghafla, watu wanaweza kumpita bila kumsaidia, kwa kuamini mtu
mwingine atafanya hivyo au kuna mtu ambaye tayari ameshaanza kumpa
msaada.
Kitu kingine kinachofanya ujinga wa kundi kuwa na madhara ni kuona siyo
tatizo. Mfano kama unapita kwenye njia ambayo watu wengi wanapita, ukaona
mtu amekaa chini, lakini watu wanampita, na wewe utampita, utaona labda
hana shida. Lakini kama ungeona watu wamemzunguka mtu aliyekaa na wewe
ungesimama kuangalia.
Hivyo mtu anaweza kukosa msaada akiwa katikati ya kundi kubwa la watu siyo
kwa sababu kundi hilo halijali, bali kwa sababu ya kufuata mkumbo ambapo
kunazalisha ujinga wa kundi. Watu wanafikiri huenda mwingine ameshasaidia
au kwa kuangalia wengine wanapita, wanaona siyo tatizo kubwa hivyo nao pia
wanapita.
Tafiti zinaonesha kwamba mtu akipata shida ya dharura akiwa amezungukwa
na watu wachache ana nafasi kubwa ya kusaidiwa kuliko akipata shida hiyo
akiwa amezungukwa na kundi kubwa la watu. Kwa kuzungukwa na watu
wachache, wanaona ni jukumu lao, lakini wanapokuwa wengi, kila mtu anaona
ni jukumu la mwingine.

Siyo kwamba watu wa mjini wana roho mbaya.


Kwenye jamii yoyote ile, ukipata tatizo eneo la mjini ni vigumu kupata msaada
kuliko ukipata tatizo la aina hiyo ukiwa eneo la kijijini. Wengi wamekuwa
wanalaumu kwamba watu wa mijini wana roho mbaya, hawajali kuhusu
wengine na kila mtu anaangalia maisha yake tu.
Lakini tafiti zinaonesha kinachopelekea kupata msaada maeneo ya mjini kuwa
vigumu kuliko vijijini ni msingi huu wa kufuata mkumbo na ujinga wa kundi.
Kuna vitu vitatu vikubwa vinavyotofautisha watu wa mjini na kijijini katika
kusaidia;
1. Katika wakati wowote ule, eneo la mjini huwa linakuwa na watu wengi
kuliko kijijini. Hivyo inapotokea mtu anapata shida akiwa mjini, ni rahisi kila
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

mtu kuona kwamba wengine watasaidia. Lakini kwa kijijini, kunakuwa na watu
wachache, hivyo inapotokea shida ni rahisi kusaidiwa. Chukua mfano nyumba
imevamiwa na majambazi, kwa mjini, mtu anakuwa na majirani wengi, hivyo
hata kama wote watasikia, kila mmoja atajiambia jirani mwingine atakuwa
ameshapiga simu polisi, kinachotokea ni hakuna hata mmoja anapiga simu,
kwa sababu kila mmoja anafikiri mwenzake ameshafanya hivyo. Lakini kwa
kijijini, mtu anakuwa na jirani mmoja ambaye atabeba wajibu na hata
mwingine wa kumtegea. Hivyo wingi wa watu maeneo ya mjini unafanya
msaada kuacha kuwa jukumu la mmoja na kuwa la wengi ambapo hakuna
anayeutoa.
2. Maisha ya mjini yanawafanya watu wanakuwa wametingwa na kuzungukwa
na usumbufu, kitu kinachowafanya washindwe kujua kama kitu ni tatizo kweli
au la. Mfano kama kwa jirani kuna ugomvi, kwa mjini ni vigumu watu kuingilia
kwa sababu wanakuwa hawajui nini kinaendelea. Lakini kwa kijijini, watu
wanakuwa na utulivu wa kujua yanayoendelea na hivyo tatizo linagundulika
haraka.
3. Watu wa mjini hawajuani moja kwa moja kama ilivyo kwa watu wa vijijini.
Majirani wa kijiji kimoja wanajuana vizuri na hivyo inakuwa rahisi kusaidiana.
Watu wa mjini hawajuani kwa undani, watu wanaweza kuwa majirani lakini
wasijuane kuhusu maisha yao, hivyo inakuwa vigumu kusaidiana.
Vitu hivi vitatu vinafanya utoaji wa msaada kwa wenye uhitaji wa hali ya
dharura kuwa mgumu kwenye maeneo ya mjini kuliko maeneo ya kijijini.

Wewe mwenye shati jekundu nisaidie.


Kwa kuona madhara haya ya kufuata mkumbo na ujinga wa kundi, mwandishi
ametushauri njia bora ya kuhakikisha tunapata msaada pale tunapokuwa na
hali za dharura.
Anachukua mfano kama upo njiani ambapo kuna watu wengi wanapita na
ghafla ukaona unapata dalili za kupata shambulio la moyo na hivyo kukaa chini,
unaweza kupitwa na watu hapo mpaka ukafa.
Cha kufanya ni usisubiri mpaka mtu ajitokeze kukusaidia, badala yake chagua
mtu mmoja na muite akusaidie. Mfano kama katika watu wanaopita kuna mtu
amevaa shati jekundu basi muite kabisa, mwambie wewe uliyevaa shati
jekundu nisaidie nina dharura.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Kwa kufanya hivyo, unakuwa umeondoa ujinga wa kundi, unakuwa umempa


mtu mmoja wajibu, ambaye atakuja kukusaidia na hapo wengine nao watakuja
kukusaidia.
Kadhalika kama upo nyumbani na umepata tatizo, usifikirie kwamba majirani
wanakuja kukusaidia, badala yake chagua jirani mmoja ambaye utamuomba
akusaidie, iwe utamuita kwa sauti au kumpigia simu, hakikisha kuna mtu
mmoja umempa jukumu na hivyo hakutakuwa na kutegeana.
Unapochagua mtu wa kumuomba akusaidia, hakikisha unampa kabisa jukumu
la kufanya, iwe ni unamtaka apige simu polisi au kwingineko, hiyo inamfanya
mtu kuacha kuangalia wengine wanafanya nini na kufanya kile ulichomuomba
akusaidie.
Unapojikuta kwenye hali ya dharura na unahitaji msaada wa wengine, jukumu
lako kubwa ni kuwaondoa watu hao kwenye hali ya kutokuwa na uhakika,
kuhusu hali uliyonayo na kuhusu hatua wanazopaswa kuchukua. Hivyo katika
wengi chagua mmoja, mweleze hali uliyonayo na mwambie ni nini unataka
afanye. Usiliachie kundi kubwa kufanya maamuzi, watakupuuza na utakosa
msaada.
Katika silaha sita za ushawishi tunazojifunza kwenye kitabu hiki, hii inaweza
kuwa muhimu kuliko zote kwa sababu itakusaidia sana pale unapokuwa
kwenye hali ya uhitaji na wengine hawaelewi kutokana na wingi wao.

Ufanano na kufuata mkumbo.


Tumeona jinsi kukosa uhakika kunavyoipa nguvu silaha ya kufuata mkumbo.
Kitu kingine kinachoipa nguvu silaha hii ni ufanano, pale mtu anapoona
wengine wanaofanana naye wanafanya kitu fulani, basi nao hushawishika
kukifanya.
Mwandishi anashirikisha utafiti ambao umewahi kufanywa kwenye majanga
yanayotangazwa sana, kama ajali za ndege au watu kujiua. Tafiti zilikuwa
zinaonesha kwamba pale ajali ya aina fulani inapotokea na kutangazwa, katika
kipindi hicho ajali nyingine za aina hiyo hutokea kwa wingi.
Mfano kama ni ajali ya basi imetokea na kutangazwa sana, ajali nyingine za
mabasi hutokea pia. Kama kuna mtu amejinyonga, habari hiyo inapotangazwa
watu wengine nao hujinyonga pia.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Baada ya utafiti wa kina kufanywa kwenye hilo, matokeo yanaonesha kwamba


matukio ya aina fulani huwa yanaongezeka kwa sababu ya kuigana au kufuata
mkumbo.
Mfano kama mtu aliyejinyonga ni mwanaume mtu mzima, wengine
wanaojinyonga baada ya kusikia hivyo ni wanaume watu wazima.
Kinachosababisha ni unakuta mtu ana changamoto mbalimbali na amekata
tamaa, hajui nini cha kufanya, anaposikia mwingine aliyekuwa na changamoto
kama zake amejinyonga, anaona ni sahihi kwake pia kujinyonga.
Huwa tunasukumwa kufanya kile ambacho watu wanaofanana na sisi
wanafanya. Na hii ndiyo maana matangazo mengi ya biashara yanatumia watu
wa kawaida, ili mtu ujifananishe nao na kushawishika kununua bidhaa husika.
Wale wanaofanana na sisi kwa namna moja au nyingine, iwe ni kwa jinsia,
umri, eneo au rangi, huwa wana ushawishi mkubwa kwetu kuliko wale
wasiofanana na sisi. Hivyo huwa tunawaiga zaidi wale tunaofanana nao kuliko
tusiofanana nao.
Tafiti zinaendelea kuonesha hata vitu visivyo na mahusiano, huwa vina
ushawishi kwenye yale ambayo watu huwa wanafanya. Mfano utafiti mmoja
nchini Marekani uliwahi kuonesha kwamba kunapokuwa na pambano la ngumi
na anayeshindwa akawa mtu mweusi, siku kumi zinazofuatia vifo vya watu
weusi vinakuwa vingi zaidi. Pia inapotokea anayeshindwa anakuwa mtu
mweupe, vifo vya watu weupe vinakuwa vingi zaidi.
Ufanano una nguvu kubwa kwenye kushawishika kufuata mkumbo.

Wakamate wachache, wengine watakamatwa na kundi.


Viongozi wanaokuwa na ushawishi mkubwa na ambao baadaye huwa na
madhara kwa wafuasi wao, huwa wanajua siri moja kubwa ya kuaminiwa na
kundi kubwa la watu.
Wanachagua watu wachache ambao wanashawishika kirahisi na kisha
kuwashawishi hao, watu hao wachache wanawaamini sana na hilo linawavuta
wengine nao kumwamini kiongozi huyo. Baada ya hapo, ushawishi wa kiongozi
unakuwa mkubwa siyo kwa sababu ya yeye kuwafikia wengi, bali kwa sababu
kundi linavyokua kubwa ndivyo linavyovutia wengi zaidi.
Viongozi hao pia huwa wanajua jinsi ya kutumia nguvu mbili za silaha ya
kufuata mkumbo. Kwanza wanawaweka wafuasi wao kwenye hali ya kutokuwa

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

na uhakika na ili wapate uhakika inabidi wamfuate kiongozi huyo. Hili


linawafanya watu wasiwe na wasiwasi na kiongozi huyo, kwa sababu anawapa
uhakika ambao wao wenyewe hawana. Njia ya pili wanayoitumia ni
kutengeneza ufanano ambapo wanachagua wafuasi wao wa mwanzo vizuri ili
kuwavutia watu wanaofanana nao.
Kwa njia hii viongozi wa makundi mbalimbali wamekuwa na ushawishi mkubwa
kwa wafuasi wao ambao unakuwa hatari kwao.

Jim Jones na Joseph Kibweteere.


Kuna viongozi wawili wa kidini ambao wamewahi kutumia nguvu hii ya
ushawishi kwa kufuata mkumbo na wakaleta maafa makubwa.
Wa kwanza alikuwa Jim Jones wa nchini Marekani ambaye alianzisha kanisa
lake na kulihamishia kwenye jangwa alipopaita Jonestown. Alijenga ushawishi
mkubwa kwa wafuasi wake na kutumia silaha ya kufuata mkumbo. Mwaka
1978 aliwashawishi wafuasi wake 918 kujiua kwa kunywa sumu na wakafanya
hivyo.
Wa pili alikuwa Joseph Kibweteere wa Uganda, ambaye alikuwa kiongozi wa
kundi la kidini aliyewaaminisha wafuasi wake kwamba mwaka 2000 ndiyo
utakuwa mwisho wa dunia. Mwaka 2000 ulipofika bila ya mwisho wa dunia
kutokea, aliwashawishi wajiue na watu 778 walikubali kujiua.
Ukisoma historia za watu hao wawili kwa undani utaona jinsi walivyotumia
silaha hizi za ushawishi na kuaminika na wengi mpaka kupelekea maafa
makubwa ya watu kupoteza uhai wao.

Jinsi ya kusema hapana.


Tumeona jinsi silaha ya kufuata mkumbo ilivyo na nguvu na hata madhara
makubwa. Tumeona pia jinsi ilivyo na manufaa kwetu na hivyo kuitegemea
kwenye maisha yetu ya kila siku. Hilo linatuweka njia panda, hatuwezi kuacha
kabisa kufuata mkumbo, lakini pia kufuata mkumbo kuna hatari yake.
Kwa bahati nzuri, kuna njia ya kuepuka kushawishiwa na wale wasio na nia
nzuri wanaotumia silaha hii ya kufuata mkumbo.
Zipo njia mbili za kutusaidia kuepuka kushawishiwa vibaya na silaha hii ya
kufuata mkumbo.
Njia ya kwanza ni kukagua uhalisia wa kundi unaloshawishiwa kulifuata. Badala
ya kujiunga tu na kundi, angalia kama kweli kundi hilo lipo na kama lipo jua
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

kama kila mtu kwenye kundi hafuati wengine kwa sababu tu ya wingi wao. Hili
litasaidia kuondoa ile hali ya kufuata mkumbo kwa sababu wengi wanafanya,
itakusaidia kujua nini kimewafanya wengi hao wafanye hivyo. Fanya hivi kabla
ya kufikia maamuzi makubwa na muhimu, usiangalie tu kundi kubwa, bali
angalia kundi hilo linajua nini.
Njia hii ya kwanza nzuri kutumia pale unapojikuta njia panda au ukiwa na hali
ya kutokuwa na uhakika. Badala ya kujiunga tu na kundi, jua kundi hilo
linasimamia nini.
Njia ya pili ni kujiepusha na ujinga wa kundi, pale unapoona kuna jambo halipo
sawa, badala ya kujiambia kuna mwingine ameshachukua hatua, wewe chukua
hatua. Jua kila mtu anafikiria mwingine ameshachukua hatua na hivyo hakuna
anayechukua hatua. Wewe vunja hilo kwa kuwa mtu anayechukua hatua na
hata kama mwingine ameshachukua, hakuna unachokuwa umepoteza.
Kwa ujumla, silaha ya kufuata mkumbo huwa inafanya kazi kwa sababu watu
wanafanya mambo yao kwa mazoea. Hivyo kuepuka kuingia kwenye ushawishi
mbaya kwa silaha hii, mara kwa mara hoji, dadisi na kagua kile ambacho
kinafuatwa na kundi kubwa la watu na jua ukweli wake uko wapi. Utaweza
kufanya hivyo kama utajiweka pembeni na kundi kwa muda na kuangalia
ukweli unaosimamiwa na kundi hilo.
Wengi wanaodhurika kwa kufuata mkumbo, kama waliojiua kwa kushawishiwa
na viongozi wa kidini ni kwa sababu wanakuwa hawapati muda wa kufikiri
wenyewe nje ya kundi wanalokuwepo. Kwa kuwa kila anayewazunguka
anafanya, wanaona ndiyo kitu sahihi kufanya. Lakini wewe ukiwa mtu wa
kukaa nje ya kundi kidogo na kufikiri kwa akili yako, utaona jinsi yale
yanayofanyika yasivyokuwa sahihi.
Na kwenye biashara mbalimbali, nunua kitu kwa sababu una uhitaji nacho na
siyo kwa sababu umeambiwa kila mtu ananunua kitu hicho. Hiyo itakuepusha
kusukumwa kununua kwa kufuata mkumbo.

SILAHA YA NNE; KUPENDA (LIKING).


Silaha ya nne kwenye silaha sita za ushawishi ni ya kupenda. Kisaikolojia huwa
tunakubaliana zaidi na wale watu ambao tunawapenda kuliko ambao
hatuwapendi. Na hilo limewafanya wale wanaotaka kutushawishi kujua njia
rahisi ya sisi kukubaliana nao.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Njia hiyo ni wao kujiweka kwenye mazingira ambayo yatatufanya tuwapende.


Wanavaa mavazi mazuri na kujiweka kwenye hali za kupendeza,
wanatabasamu na kufanya mengine, yote kwa lengo la kutufanya tuwapende
na hapo tukubaliane na kile wanachotaka kutushawishi.
Hapa tunakwenda kuona jinsi silaha hii inavyotumika kushawishi na jinsi ya
kuepuka kushawishiwa vibaya kwa kutumia silaha hii.

Rafiki mwizi.
Huwa tunakubaliana kwa urahisi na watu tunaowajua na kuwapenda kuliko
watu tusiowajua au kutokuwapenda. Huu ni msingi wa mahusiano wa kijamii
ambao unatupa njia ya kufanya maamuzi haraka bila ya kufikiri sana.
Kama tulivyoona kwenye silaha nyingine za ushawishi, zote ni njia za mkato
kwetu kufanya maamuzi na zimekuwa na msaada mkubwa kwetu.
Chukua mfano kama ingekubidi ukague nia ya kila mtu unayejihusisha naye
kwenye maisha yako, uchunguze kila mtu kabla hujakubaliana naye,
usingeweza kufanya lolote. Itakuchukua muda mpaka uweze kumchunguza
mtu na kumjua kiundani.
Kuondokana na hilo, tumekuwa na njia ya mkato ambao inatusaidia. Kwa wale
tunaowajua, tunakuwa na uhakika kwama lolote wanalofanya ni kwa wema na
wana nia njema na sisi, hivyo tunakubaliana nao bila kuwachunguza sana.
Kwa marafiki, ndugu na jamaa wa karibu, huwa tunakubaliana nao bila hata ya
kuwachunguza kwa sababu tunajua wana nia njema kwetu, hawawezi kufanya
jambo la kutuumiza.
Na hapo ndipo mwanya wa wale wenye nia ya kutushawishi unapotokea,
wanakuja kwetu wakijifanya ni marafiki zetu, tunawaamini na kukubaliana nao
bila kuwachunguza kwa undani.

Biashara ya mtandao.
Biashara zinazoendeshwa kwa mfumo wa mtandao (network/multilevel
marketing) huwa zinatumia nguvu ya urafiki kuwashawishi watu kununua
bidhaa zao.
Mfumo wa biashara hii unamtaka mtu ajiunge na kuwa mteja, kisha
awashawishi marafiki na watu wake wa karibu nao kujiunga na kuwa wateja.
Biashara hizi huwa zinatoa faida kubwa kwa anayejiunga na kulipa kamisheni
pale anapoweza kuwashawishi wengine nao kujiunga.
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Inakuwa rahisi kwa kampuni husika kuuza kwa sababu watu wanatumia
mahusiano yao na watu wao wa karibu kuwashawishi.
Kama umewahi kualikwa uhudhurie mikutano ya biashara hizi, utagundua
ulialikwa na mtu wako wa karibu. Na alipokualika hata kama ulikuwa hutaki
kuenda, hukuwa tayari kukataa, badala yake ulikubali kuhudhuria na huenda
hata kujiunga.
Silaha hii ya kupenda ina nguvu kubwa, ni vigumu sana kumkatalia mtu
unayemjua na unayempenda.
Silaha hii kama ilivyo kwa silaha nyingine inatumia udhaifu wetu wenyewe
kutuangusha. Kwa kutumia mfano wa biashara ya mtandao, unaweza kuwa
huna uhitaji na kitu, lakini ukaishia kukinunua, ndani yako utajishawishi
kwamba umemuungisha rafiki yako, lakini hiyo ndiyo mbinu ya kampuni
husika, kutumia uhusiano wa watu kuuza zaidi.

Wauzaji wana mwonekano mzuri.


Biashara zote zinazotumia watu wa mauzo kishawishi watu kununua, huwa
zinawaweka wauzaji wake kwenye mwonekano mzuri. Wanakuwa wamevalia
nguo nadhifu na wanapendeza kweli kweli. Pia muda wote wanakuwa na
tabasamu na hujitahidi kujua jina lako. Wakati wa mauzo wanakuita kwa jina
na kufanya kila namna kuonekana ni marafiki zako na wako upande wako.
Hata pale unapotoa sababu kwa nini huwezi kununua, hukaa upande wako, na
kuonekana kama wanakusaidia ili ukipate kitu hicho. Yote hayo yanaongeza
ushawishi wako na kujikuta unakubali kununua. Muuzaji anaweza kukuambia
kabisa kwamba anaenda kukuombea kwa meneja upate kwa bei unayoweza,
yote hiyo ni kukufanya umpende, uone yuko upande wako.
Pia biashara nyingi huwa zinachagua wauzaji wenye mwonekano mzuri kuliko
wasio na mwonekano mzuri, kwa sababu wanajua mwonekano wa mtu ni kitu
cha kwanza kwenye ushawishi.

Jina la rafiki linatosha.


Tumeona kwenye mfumo wa biashara ya mtandao, rafiki anapokuja
kukushawishi ununue kitu, unakubaliana naye haraka. Tafiti zinaonesha hata
kama rafiki huyo hayupo, kitendo cha jina lake kutajwa tu, unashawishika
kukubali kuliko asipotajwa.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Kwa kujua nguvu ya hili, wale wanaofanya mauzo ya nyumba kwa nyumba,
wakikushawishi ununue, iwe utanunua au la, mwisho huwa wanakuomba
uwape jina la rafiki yako ambaye unaona anaweza kunufaika na ofa nzuri
waliyonayo. Wewe utafutahi kutoa jina la rafiki na wao wanaandika na kisha
kumtafuta.
Wanapofika kwa rafiki yako, wanamwambia tulimtembelea rafiki yako fulani
na amekuchagua wewe pia upate ofa nzuri tunayoitoa. Kwa kutaja jina lako na
kueleza kwamba wewe ndiyo umewaelekeza, rafiki yako anashawishika zaidi
kununua.
Mtu akija kwako na kukuambia rafiki yako fulani amekuchagua wewe unaweza
kunufaika na ofa yetu, unajikuta njia panda, ukisema hapana, hujasema
hapana kwa wauzaji tu, bali umesema hapana kwa rafiki yako, na hilo ndiyo
linaipa silaha hii nguvu.
Kwa kutumia njia hii, makampuni ya mauzo yamekuwa yanatengeneza orodha
kubwa ya wateja na marafiki zao na kuitumia vizuri kushawishi watu wanunue
wanachouza.
Njia nyingine ambayo makampuni hayo yamekuwa yanatumia ni kukupa ofa
kwa kutumia jina la rafiki yako. Watakuambia tuko kwenye mpango wa kutoa
ofa na rafiki yako fulani amekuchagua wewe upate ofa hii. Utaona ni jambo la
heshima, katika watu wote rafiki huyo kukuchagua wewe na hapo
utashawishika zaidi. Wakishakushawishi na ukanunua, wanakuomba uchague
rafiki yako ambaye ungependa pia apate ofa. Hapo wanazidi kupata wateja
zaidi na ambao ni rahisi kuwashawishi.

Muuzaji aliyevunja rekodi ya dunia kwa kutumia silaha ya kupenda.


Mwandishi anatushirikisha mfano wa mtu ambaye amewahi kuwa muuzaji
namba moja wa magari duniani na aliyevunja rekodi ya dunia kwa kuwa mtu
mmoja aliyeweza kuuza magari mengi zaidi kuliko watu wengine wote duniani.
Mtu huyo ni Joe Girard ambaye alikuwa muuza magari wa nchini Marekani.
Girard aliweza kuuza idadi ya magari 13,001 ya aina ya Chevrolet kati ya
mwaka 1963 na 1978, kitu kilichopelekea aweke rekodi ya dunia ya Guinness
kama mtu aliyeweza kuuza magari mengi zaidi ndani ya mwaka.
Alipoulizwa kuhusu siri ya mafanikio yake, Girad alitaja vitu viwili; URAFIKI na
BEI NZURI. Alisema; pale mteja anapokutana na muuzaji anayempenda na
muuzaji huyo akampa bei nzuri, lazima atanunua.
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Pale watu walipoanza kufuatilia ili kujua kwa nini wateja wanampenda sana
Girard kuliko wauzaji wengine, ndipo walipogundua siri, alijenga mahusiano ya
urafiki na ukaribu na kila mteja wake. Girard alikuwa na orodha ya wateja wote
ambao wamewahi kununua kwake na wale ambao analenga kuwauzia. Kisha
kila mwezi alituma kadi moja kwa kila mteja wake, aliyoiandika kwa mwandiko
wake na kuweka sahihi yake.
Kila mwezi alitafuta sababu ya kutuma kadi kwa kila mteja, iwe ni siku yake ya
kuzaliwa, iwe ni sikukuu za kitaifa, za kidini au yoyote ile, alihakikisha mwezi
hauishi bila kila mteja wake kupata kadi kutoka kwake. Alikuwa na malaki ya
wateja, lakini wote waliwatumia kadi hizo.
Hilo liliwafanya wateja kumjua na kumchukulia kama mtu wa karibu na pale
walipohitaji kununua gari hawakufikia mtu mwingine bali Girard.
Mfano wa Girard na ambao umekuwa unatumiwa na wengi, unaonesha jinsi
silaha hii ilivyo na nguvu ikifanyiwa kazi vizuri.

Vigezo vinavyotuvutia kupenda.


Tafiti mbalimbali za kisaikolojia na kijamii zinaonesha kuna vigezo ambavyo
vikiwepo kwa mtu anapendwa zaidi na wengine. Wale wanaotumia silaha ya
kupenda kushawishi, wamekuwa wanavijua vigezo hivi na kuhakikisha
wanavitumia.
Vifuatavyo ni vigezo vyenye nguvu kwenye kupenda.
1. Mwonekano mzuri.
Wale wenye mwonekano mzuri, warembo au watanashati huwa wanapendwa
zaidi kuliko wasio na mwonekano mzuri. Huwa inatokea hivyo bila hata ya
anayevutiwa kujua kwamba mwonekano ndiyo umemfanya avutiwe.
Watu wenye mwonekano mzuri huwa wanaonekana wana tabia na sifa nzuri
hata kama siyo kweli. Huonekana ni wema zaidi, waaminifu na wenye akili.
Akili zetu zimekuwa zinatumia njia hiyo ya mkato, kwamba mtu mwenye
mwonekano mzuri basi pia ni mtu mzuri.
Tafiti zimekuwa zinaonesha kwamba watu wenye mwonekano mzuri
wamekuwa wanapata fursa nzuri kwenye jamii kuliko wasio na mwonekano
mzuri. Mfano kwenye biashara, wanakubalika zaidi, kwenye kesi hata
wakishindwa wanapewa adhabu kidogo na hata kwenye mashindano au

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

uchaguzi, mwenye mwonekano mzuri anakuwa na nafasi kubwa ya kushinda


kuliko asiye na mwonekano mzuri.
2. Kufanana.
Watu huwa wanawapenda watu wanaofanana nao kuliko watu wasiofanana
nao. Na haijalishi ufanano huo uko kwenye kitu gani, inapokuwa tu kuna kitu
ambacho watu wanakubaliana pamoja basi ushawishi unakuwa mkubwa zaidi.
Mfano watu wanapojikuta wana maoni sawa, wanashangilia timu au chama
kimoja, wametoka eneo moja au walisoma shule moja hata kama ni kwa
vipindi tofauti, wanapendana zaidi kuliko kutokuwepo kwa ufanano huo.
Hivyo wale wanaotaka kutushawishi, huwa wanatafuta kitu ambacho
tunakubaliana nao na kukazania hicho. Wale ambao biashara yao kuu ni
kutumia nguvu ya kupenda kushawishi, huwa wanahakikisha wanajua
unapenda nini na kisha kujifanya na wao wanapenda pia, hata kama
hawapendi. Lengo ni muwe upande mmoja ili ushawishike zaidi.
Mfano kama umeenda kununua kitu ukiwa umevaa fulana ya timu ya mpira
unayoshabikia, moja kwa moja anayetaka kukushawishi atakuambia na yeye ni
shabiki wa timu hiyo, ataanzisha mazungumzo yanayohusu timu, hapo utaona
uko na mwenzako na hivyo kumpenda na kushawishika zaidi.
Ufanano una nguvu kubwa na hata kwenye vitu vidogo kama mavazi, umri,
jinsia, dini, siasa, starehe na kadhalika.
3. Pongezi.
Pale mtu anapotusifia, huwa tunakubaliana naye kwa urahisi zaidi. Hivyo
pongezi imekuwa ni njia inayotumika kuibua kupenda na kushawishika zaidi.
Haijalishi kama pongezi ni ya kweli au la, ambacho mtu anaangalia ni kama
imetoka ndani ya mtu kweli.
Mfano mzuri ni Girard ambaye kwa kila kadi ambayo alikuwa anatuma kwa
mteja wake, alimpongeza kwa kitu fulani na kumalizia kwa ujumbe Nakupenda.
Hiyo iliwafanya watu wampende na kumkubali zaidi.
Pongezi huwa zina nguvu kubwa, hata kama siyo za kweli, hivyo wale
wanaotumia njia hii kushawishi huwa wanatafuta chochote cha kupongeza kwa
mtu, iwe ni mavazi, mwonekano, watoto au chochote. Wengi huhakikisha
wanapata kitu cha kupongeza kwa mtu kabla hawajaanza ushawishi wao.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

4. Ukaribu na ushirikiano.
Ukaribu na ushirikiano umekuwa unapelekea watu kupendana. Hata pale watu
wanapokuwa wanatofautiana au hawajuani, wakikaa karibu kwa muda na
kushirikiana kwenye jambo lolote mwisho hujikuta wakipendana na
kukubaliana.
Wale wanaotaka kutushawishi huwa wanatengeneza mazingira ya kuleta
ushirikiano, kujiona tuko upande mmoja na hapo tunakubaliana nao zaidi.
5. Hali na Uhusianisho.
Huwa tuna tabia ya kuwahusianisha watu na hali wanazokuwa nazo. Ule usemi
kwamba mjumbe hauawi siyo kweli, mjumbe anapotuletea taarifa ambazo ni
mbaya, huwa tunamuona na yeye ni mbaya, hata kama yeye ameleta tu taarifa
na hahusiani nazo.
Huwa tuna tabia ya kusianisha watu na vitu au hali fulani wanazoendana nazo.
Mfano mzuri ni wasomaji wa utabiri wa hali ya hewa, pale wanaposoma taarifa
kwamba hali ya hewa itakuwa mbaya, watu huwa wanawachukia wao kama
vile ndiyo wameleta hali hiyo mbaya.
Kwa kujua hili, wale wanaotaka kutushawishi huwa wanahakikisha
wanajihusisha na vitu vizuri tu ili tuwapende na kukubaliana nao.
Hii imekuwa inatumika sana kwenye matangazo, bidhaa au huduma
inahusianishwa na kitu ambacho tayari mtu anakipenda.
Mfano mzuri ni wasanii na watu maarufu wanapochaguliwa kuwa mabalozi wa
taasisi au biashara fulani, au wanatumika kwenye matangazo. Kinachofanyika
hapo ni kuwafanya wale wanaowapenda wasanii na watu hao maarufu,
kupenda pia bidhaa ambayo wanaonekana kuitumia. Kwa kuwa unampenda
msanii fulani na kwa kuwa umemuona kwenye tangazo la kitu fulani, moja kwa
moja unakipenda kitu hicho pia.
Hili huwa linafanya kazi hata kama kinachotangazwa hakina uhusiano na
umaarufu wa mtu. Mfano msanii maarufu wa muziki anaweza kuwa kwenye
tangazo la vinywaji, sabuni au chochote na bado tukavipenda vitu hivyo kama
tunavyompenda msanii huyo.
Wanasiasa na washawishi wengine wamekuwa wanatumia nguvu hii ya
uhusianisho kuhakikisha wanaweza kuwashawishi watu. Wanachofanya ni
kutafuta kitu ambacho watu wanakipenda na kisha kutengeneza uhusiano
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

utakaowafanya watu wawapende na kukubaliana nao. Kitu ambacho


kimekuwa kinatumika sana ni chakula. Mtu anapotaka kuwashawishi watu,
anaandaa tafrija na kuweka vyakula vizuri, kisha wakati watu wanakula au
baada ya kula, analeta mapendekezo yake. Kwa kuwa umeshakifurahia na
kukipenda chakula, utampenda aliyekuandalia na kukubaliana naye.
Hata wale wanaofanya harambee au kuomba michango kwa wengine,
watapata ahadi kubwa kama watawaandalia watu chakula kuliko wasipofanya
hivyo. Kinachofanya watu wakubaliane nao siyo kuona chakula kama zawadi,
bali kukipenda chakula na kisha kumpenda aliyewaandalia.
Hili la chakula limethibitishwa kisayansi, ambapo mwanabaiolojia Palvol
aliweza kuonesha kupitia mbwa hali ya kutengeneza uhusiano baina ya chakula
na kinachokuja na chakula hicho. Alikuwa akigonga kengele kisha kuwapa
mbwa chakula. Baada ya muda alipogonga kengele, mbwa walianza kutokwa
mate hata kama hakukuwa na chakula. Mbwa hao walijifunza kuhusianisha
kengele na chakula.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwetu binadamu, huwa tunahusianisha chakula na kile
ambacho kimeambatana na chakula hicho na hilo linatoa mwanya wa
kushawishika kirahisi pale tunapopewa chakula.

Ushabiki wa timu.
Ushabiki wa michezo mbalimbali umekuwa na nguvu kubwa kwa watu. Mtu
anayeshabikia timu huwa anajihusisha na timu hiyo kabisa, hata pale timu
inaposhinda mtu anasema tumeshinda, kama vile alikuwa uwanjani.
Hii yote inatokana na nguvu ya silaha ya kupenda, pale mtu anapokipenda kitu
kutoka ndani ya moyo wake, anakiona kama ni kitu chake au anashiriki moja
kwa moja hata kama siyo kweli.
Kadiri mtu anavyoipenda timu yake, ndivyo nafsi yake inavyojiona kupitia timu
hiyo. Ndiyo maana baadhi ya mashabiki wanaweza kufanya hata mambo
ambayo ni hatari, kwa sababu wanajiona kama vile wao ndiyo timu zao. Wapo
wanaofikia hatua hata ya kujiua, kwa sababu wanakuwa wamemezwa nafsi zao
na timu zao.
Kinachopelekea watu kupenda sana timu au kitu wanachoshabikia ni kwa
sababu ya kutaka kuhusianishwa na mafanikio ya kitu hicho. Iko hivi, washabiki
kindanindaki wa kitu chochote kile, ni watu ambao hawana mafanikio
makubwa kwenye maisha yao. Hivyo mafanikio ya kile wanachoshabikia huwa
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

wanayahesabu kuwa mafanikio yao. Ndiyo maana huwa wanataka sana kile
wanachoshabikia kifanikiwe, maana wanakitumia kupima mafanikio yao.
Kila mtu huwa anapenda kuwa sehemu ya ushindi, hivyo pale ambapo mtu
hana ushindi kwenye maisha yake, anachagua kitu cha nje ambacho anaweza
kujihusisha na ushindi wake na hapo ndipo ushabiki mkubwa unapozaliwa.
Tafiti zinaonesha pale timu inaposhinda, watu wengi zaidi huvaa jezi za timu
hiyo kuliko timu iliyoshindwa. Yote hiyo inaonesha jinsi gani tunapenda
kujihusisha na mafanikio ya wengine.
Hata lugha inayotumika huwa ni tofauti kwenye ushindi na kwenye kushindwa.
Timu inaposhinda mashabiki wake hutumia lugha ya umiliki, husema
‘tumeshinda’ lakini timu inaposhindwa hawatumii lugha ya umiliki, badala yake
wanajitenga na timu kwa kusema ‘timu imeshindwa’ na siyo tumeshindwa.
Tafiti zinaonesha kadiri mtu anavyokosa ushindi ndani yake, ndivyo
anavyotafuta ushindi wa nje wa kujihusianisha nao. Mfano wapo wanaoenda
hatua ya ziada na kununua tiketi za mchezo ambao hawakuhudhuria ili tu kuja
kuwaonesha wengine kwamba walihudhuria mchezo huo. Kitu kama hicho
kinawafanya waonekane nao kuna kitu wamefanikisha, hata kama siyo kweli.

Waliofanikiwa wana marafiki wengi.


Hili la kujihusianisha na mafanikio huwa linatumika hata nje ya michezo, watu
waliofanikiwa huwa wana ndugu wengi, marafiki wengi na hata wanaowajua
wengi kuliko wale walioshindwa.
Kwa kila aliyefanikiwa utasikia utitiri wa watu wengi wanaosema wanamjua,
walimsaidia na mahusiano gani wanayo na mtu huyo. Lakini walioshindwa
hawana watu wengi wanaojihusisha nao.
Yote hiyo ni mtu kutaka ahusianishwe na mafanikio ya mtu mwingine, hasa
pale anapokuwa hana mafanikio yake binafsi.
Hata wale ambao wamekuwa wanatumia majina ya watu wengine, wanatumia
hali hiyo ya uhusianisho. Mfano mtu anajitambulisha kama shangazi wa
mbunge au mchumba wa msanii maarufu na mengineyo. Yote ni kutaka
kuhusianishwa na mafanikio ya mtu huyo anayejitambulisha kupitia yeye.

Wazazi wanaotaka kulipiza kupitia watoto wao.


Hili la kujihusianisha na mafanikio limekwenda mbali zaidi na kufikia hatua ya
mtu kutumia wengine kufikia kile ambacho yeye ameshindwa kufikia.
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Mfano mzuri ni wazazi ambao wamekuwa wanawatumia watoto wao kufikia


kile ambacho wao hawakuweza kufikia.
Labda mzazi alipenda sana kuwa daktari, lakini mazingira au uwezo
haukuruhusu hilo. Basi anaanza kumuandaa mtoto wake mapema ili aje awe
daktari.
Japo mzazi anaweza kutimiza hilo, anakuwa hajamsaidia mtoto huyo, kwa
sababu anakuwa hajamjengea maisha yake, bali amelipa alichokosa kupitia
mtoto huyo.

Jinsi ya kusema hapana.


Katika silaha zote za ushawishi, silaha ya kupenda ndiyo ina vigezo vingi.
Tumeona njia tano zinazochochea upendo kwa watu, hivyo kukabiliana na
silaha hii inahitaji mtu uwe na njia ambayo itakabili vigezo hivyo mbalimbali.
Na kwa kuwa silaha hii huwa inafanya kazi bila sisi kujua, mfano unajikuta
tayari unampenda mtu mwenye mwonekano mzuri bila hata ya wewe
mwenyewe kujua, kuipinga inaweza kuwa vigumu.
Hivyo cha kufanya ni kuacha mchakato uendelee, lakini inapofika kwenye
kufanya maamuzi ndiyo unajiuliza swali moja muhimu. Swali hilo ni je
nampenda mtu huyu kuliko kile anachonishawishi kuwa nacho? Kama jibu ni
ndiyo basi hapo jua silaha ya kupenda imetumika.
Swali hilo linakusaidia kutenganisha mtu na kile kitu anachotaka kukushawishi
nacho. Mtu huyo anakuteka umpende na hapo utapenda anachokushawishi
nacho moja kwa moja. Hivyo wewe unavunja huo uhusiano na kukiangalia kitu
kama chenyewe na siyo kupitia yule anayekushawishi.
Unapojikuta unataka kununua kinywaji fulani kwa sababu umeona msanii
maarufu kwenye tangazo anakunywa, jiulize je unapenda kinywaji hicho kweli
na ndiyo bora kwako, au unampenda zaidi msanii anayekitangaza. Kama
mapenzi kwa mtu ni makubwa kuliko kwa kitu ulichoshawishika, hapo jua
umenasa kwenye silaha hii na jinasue haraka kwa kutokufanya maamuzi ya
ushawishi huo.
Kabla hujafanya maamuzi yoyote hakikisha umekagua umependa nini zaidi,
kitu au mtu anayekushawishi. Tambua kwamba wewe ndiye utakayebaki na
kitu hicho na yule unayempanda hatakuwepo ukishafanya maamuzi. Kwa njia
hiyo utafanya maamuzi ambayo ni sahihi zaidi.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Kwenye makubaliano yoyote yale, angalia unachokwenda kupata na siyo


unayekubaliana naye. Wengi wanaweka mazingira ya kukufanya uwapende ili
ukubaliane nao, upendo wako kwao utakupa upofu usiangalie kile
unachokwenda kupata na mwisho unaumia.
Na kwa wale wanaotumia mahusiano yenu kukushawishi, mfano kwenye
biashara za mtandao, usikubali tu ili kumridhisha mtu, bali kubali pale kitu
kinapokuwa na manufaa kwako.
Huu ni mwisho wa sehemu ya pili ya uchambuzi wa kitabu cha INFLUENCE,
kwenye sehemu hii tumejifunza silaha mbili ambazo ni KUFUATA MKUMBO na
KUPENDA. Usikose sehemu ya tatu ya uchambuzi ambapo tutamalizia silaha
mbili za mwisho ambazo ni MAMLAKA na UHABA. Pia kwenye sehemu hiyo
tutapata hitimisho kuhusu ushawishi na matumizi bora ya silaha hizi.
Umejifunza mambo muhimu sana kupitia uchambuzi huu wa kitabu. Sasa kazi
ni kwako kwenda kuyaweka kwenye matendo ili uweze kupiga hatua na
kufanikiwa kwenye maisha yako.
Kuendelea kupata chambuzi za kina za vitabu na vitabu vilivyochambuliwa,
jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kwa kufungua
www.t.me/somavitabutanzania
Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na
mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na
upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua;
https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007

You might also like