You are on page 1of 36

Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Anza Kuwa Chachu Ya Mabadiliko Yenye


Tija Kupitia Wazo Lako

ADRIANO MKONDA

Adriano Mkonda +255 754 589 370 i


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

YALIYOMO

SHUKRANI .................................................................................... 1
UJUMBE KWA AJILI YAKO ......................................................... 2
DIBAJI ........................................................................................... 3
KANUNI 4 ZA WAZO ................................................................... 5
VYANZO 5 VYA KUPATA WAZO LENYE TIJA ......................... 12
WAZO HADI UHALISIA ............................................................ 17
WAZO LAKO MAISHA YAKO ................................................... 26
HITIMISHO ................................................................................. 30
BIBLIOGRAFIA ............................................................................ 31
KUHUSU ADRIANO MKONDA .................................................. 32

Adriano Mkonda +255 754 589 370 ii


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

SHUKRANI

Ninamshukuru Mungu aliyeweka ndani yangu wazo la kuwafikia


watu wengi kwa njia ya vitabu. Jina lake lihimidiwe milele.

Nimshukuru Godlisten Jacob, mtenda kazi pamoja nami katika


kusudi kubwa la kuwafikia wengi, hakika amekuwa mtu wa
Baraka sana kwangu. Mungu ayakumbuke maono yetu
makubwa.

Ninamshukuru rafiki yangu Neus Njugunya, amekuwa mshauri


wangu wa karibu sana katika mambo mengi. Na zaidi sana kwa
kuutoa muda wake kuandika dibaji ya kitabu hiki. Hakika,
amekiongezea kitabu hiki thamani kubwa.

Kwa umuhimu zaidi, ninamshukuru rafiki yangu Martin Mbago,


kwa kujitoa kufanya kazi pamoja nami. Kwa kuandaa jalada la
kitabu hiki na kufanya jitihada nyingi ili kuhakikisha kitabu hiki
kinawafikia wengi. Mungu aikumbuke kazi ya mikono yake.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 1


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

UJUMBE KWA AJILI YAKO

Mpendwa,

Ninamshukuru Mungu kwa ajili yako, na kwa ajili ya uamuzi


wako wa kujifunza “Nguvu Ya Wazo” kupitia kitabu hiki.
Hujapoteza, bali umewekeza.

Mwanzoni mwa mwaka huu (2022) Mungu aliweka “Wazo”


moyoni mwangu la kuwafikia watu zaidi ya 1000 kila mwezi kwa
njia ya vitabu (e-books). Kwa unyenyekevu niliupokea mwito
huu mkuu na kuanza kuutendea kazi.

Kitabu hiki (cha mwezi wa pili) kimeianzisha safari yangu ya


kuwafikia watu wengi, ninamshukuru Mungu kwa sababu wewe
ni mmoja wa watu hao. Nimekuombea kwamba kupitia kitabu
hiki ukapokee ufunuo mpya utakaokuwa sababu ya wewe kuwa
chachu ya mabadiliko chanya kwa ulimwengu kupitia mawazo
yako.

Ndani yako Mungu ameweka hazina kubwa ya mawazo ambayo


utakapoendelea kusoma kitabu hiki yatapata uhai na kama
utayatendea kazi yatahitimu na kuwa uhalisia. Na hayo yatakuwa
mafanikio makubwa ya uandishi wa kitabu hiki.

Mungu akubariki kwa uwekezaji wako!

Adriano Mkonda

Adriano Mkonda +255 754 589 370 2


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

DIBAJI

K aribia kila mtu Duniani anayo mawazo fulani mengi mengi


kila wakati. Inasemekana huwezi kufanya jambo lolote
kabla halikuwa wazo kichwani mwako. Ndiyo ni kweli kabisa.

Wazo si mtu, wazo ni kitu chenye sifa kama ya uhai,


kinazunguka kutafuta mtu atakayeweza kukigeuza kuwa kitu
halisi. Wazo zuri;

Likiona mtu amejaa hofu na wasiwasi linaondoka.


Likiona mtu anakwepa kulipa gharama linaendelea na
safari.
Likiona mtu amelikataa linaachana naye.
Likiwa kwa mtu mwenye pupa na papara linafeli.
Siku zote wazo zuri linatafuta mtu sahihi atakayeweza
kuligeuza kuwa kitu halisi.

Ipo Nguvu Katika Wazo

Kuna wazo hivi leo ukilitendea kazi unakuwa mchawi. Kuna


wazo tena ukiliweka kwenye matumizi unakuwa maskini. Tena,
lipo wazo ambalo kama litapewa kura yako ya “ndiyo” linaweza
kukufanya ukawa mtu wa ovyo sana. Na matokeo yake utakuwa
mtu wa majuto na mahangaiko katika maisha yako ya kila siku
hapa duniani.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 3


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Wazo Lenye Tija

Habari njema ni kwamba kuna wazo ukilipa kura yako ya


“ndiyo” na kukubali kulipa gharama kwa ajili ya hilo, utakuwa
sababu ya mabadiliko makubwa na yenye tija ulimwenguni.
Kinacholeta chachu ya mabadiliko sio ukubwa wa wazo lako,
bali malengo ya wazo na hasa ukilenga kuyaongezea thamani
maisha ya watu wengine.

Kitabu hiki hakikuja kukagua maisha yako kwamba labda unalo


wazo au la! Bali kipo ili kukusaidia kugeuza wazo lako lililokaa
kama ndoto nzuri ya maisha yako, kutoka kwenye maeneo
yanayokufanya ukwame na kukufanya uwe mshindi.

Ni matarajio yangu kwamba kitabu hiki kitakupa mwanzo mpya


wa kuuelekea uhalisia wa wazo lako, na zaidi sana kitakuongezea
shauku ya wewe kuwa sababu ya mabadiliko chanya kwa
ulimwengu kupitia wazo lako. Kumbuka;

“Ulimwengu unalihitaji wazo lako, usilipuuzie.”

Neus Njugunya
Speker, Author & Poet

Adriano Mkonda +255 754 589 370 4


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

KANUNI 4 ZA WAZO

K amusi ya Kiswahili ya karne ya 21, inalitafsiri neno “Wazo’’


kama jambo linaloangaziwa (linalofikiriwa) katika fikra ya mtu.
Kila mtu kwa asili huwa na wazo au mawazo. Katika kipengele
hiki tutajifunza kanuni 4 za wazo, ambazo ni msingi kama
tunataka kujua nguvu iliyofichika katika wazo.

Kanuni # 1: “Kila Jambo Huanza Kama Wazo”

Kila kitu unachokiona leo, haijalishi kipoje, kinaonekanaje,


kizuri au kibaya kilianza kama wazo tu na mwisho kikawa vile
unavyokiona leo. Hakuna muujiza bali ni nguvu ya wazo.

Siku moja nikiwa nafuatilia taarifa ya habari nilishangaa kusikia


kwamba kuna meli inabeba magari 3000 (pengine kwako likawa
si jambo la kushangaza). Nilijiuliza, inakuwaje? Inawezekanaje?
Kivipi? Hata wewe pengine unaweza kushangaa. Lakini hapo
hapana maajabu, meli haijalishi ni kubwa kiasi gani ilianza tu
kama wazo lililokuwa ndani ya mtu.

“Wazo ni kama mbegu, huwa na mwanzo


mdogo na mwishowe huzaa matunda
mengi.”

Adriano Mkonda +255 754 589 370 5


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Hakuna wazo hakuna maisha. Fikiri kama Mungu asingewaza


kuumba dunia. Maisha yangekuwaje? Fikiri kama asingekuwa na
wazo la kumuumba mtu. Mimi na wewe tungekuwa wapi? Kuna
uhai katika mawazo.

Fikiri kama Thomas Edison asingekuwa na wazo la kuunda taa


“Bulbu”? Inawezekana ulimwengu mzima ungekuwa giza hata
leo. Fikiri kama Mark Zuckerberg asingekuwa na wazo la
kuanzisha “Facebook”? Bila shaka ulimwengu wa karne ya 21
ungekuwa mgumu sana.

Fikiri kama wapigania uhuru kama kina Mwalimu Nyerere, kina


Nelson Mandela, n.k, wasingekuwa na mawazo ya kupigania
uhuru wa nchi zao? Si ajabu tungekuwa utumwani hata leo.

“Ulimwengu unasubiri wazo lako tu ili


uwe na mwonekano wa tofauti.”

Kila mwanadamu amepewa na Mungu zawadi ya wazo au


mawazo, utofauti unatokana na namna kila mmoja
anavyoyafanyia kazi mawazo hayo. Watu kama mwalimu
Nyerere, Thomas Edison, Steve Jobs n.k, hawana utofauti
wowote na wewe, ni uwezo wao wa kuyaishi mawazo yao
unaowapa utofauti.

Unaweza kuufanya ulimwengu uwe na mwonekano wa tofauti


kama tu utayatendea kazi kwa ufanisi mawazo yako. Kumbuka
kila kitu huanza kama wazo. Unaweza kuwa sababu ya
mabadiliko makubwa kupitia wazo lako. Amua.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 6


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

“Ulimwengu unalingoja kwa hamu wazo


lako. Amua”

Kanuni # 2: “Si Kila Wazo Huzaa Jambo”

Kila jambo huanza kama wazo, lakini si kila wazo huzaa jambo.
Aha! hii ni kusema kwamba “Si kila wazo huleta maana katika
maisha.”

Wataalamu wa Saikolojia wanasema kwa siku mtu huwaza


mawazo zaidi ya 6000. Swali ni je! Haya yote huwa uhalisia? Jibu
ni HAPANA.

Mawazo anayoyawaza mtu yamegawanyika katika makundi


mawili “Mawawo ya muda mfupi” na “Mawazo ya muda mrefu”.
Yale ya muda mfupi mara nyingi hupotea na yale ya muda
mrefu hudumu kwa kipindi kirefu, mfano siku, wiki, mwezi,
mwaka hata miaka.

“Mawazo ni kama mbegu zilizopandwa


kwenye udongo lakini si zote huota.”

Kinacholipa uhai wazo ni matendo. Kanuni ya tatu ina maelezo


zaidi kuhusu jambo hili.

Kanuni # 3: “Wazo Likifanyiwa Kazi Huwa Uhalisia”

Mambo makubwa kwa madogo unayoyaona leo ni matokeo ya


mawazo yaliyokuwa ndani ya watu yakafanyiwa kazi na kuwa
uhalisia kama unavyoona leo.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 7


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

”Wazo hutegemea matendo ili liwe


uhalisia”

Hatuhitaji maandalizi makubwa sana kuyafanya mawazo yetu


kuwa uhalisia, tunahitaji tu “kuanza” kuyafanyia kazi.

Mark Zuckerberg ambaye ni mwanzilishi wa mtandao wa


Facebook na mmiliki wa mitandao ya Instagram na Whatsapp
alisema; “Ideas don’t come out fully formed. They only become clear as
you work on them. You just have to get started.”

Mark alimaanisha kuwa; “Wakati wote mawazo hayaji yakiwa


yamekamilika. Yatakuwa ya kueleweka utakapoendelea
kuyafanyia kazi. Unapaswa tu kuanza.” Huu ni ukweli
unaopaswa kuuchukua na kuutendea kazi.

“Wazo ni kama mbegu, linatakiwa


kupandwa katika udongo uitwao
matendo, ili lizae matunda yatakayoupa
ulimwengu mwonekano mpya.”

Usifiche wazo ulilonalo kwa kutoliweka katika matendo huwezi


kujua kesho litazaa nini. Mwanasayansi maarufu sana Albert
Einstein, alikiri kwamba “Hakuwahi kufikiria kama watu wengine
wangezichukua kanuni zake za kisayansi kwa umuhimu mkubwa zaidi
ya vile yeye mwenyewe alivyodhani.”

Albert alifikiri kwamba mambo aliyokuwa anayawaza na


kupambana kuyaweka katika uhalisia yalikuwa ya kawaida.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 8


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Asijue kwamba yalikuwa mambo makubwa yenye kuupa


ulimwengu mwonekano bora zaidi kama tunavyoufurahia leo.

“Anza, anza sasa, hapohapo, na hilo wazo


linalouandama moyo wako.”

Ufunguo ni mmoja tu “KUANZA”, usipoteze muda anza.


Ukianza utajua nini cha kufanya ili uendelee zaidi.

Nayapenda maneno ya Zig Ziglar, anasema “If you can dream it,
then you can achieve it.” Yaani, “Kama utakuwa na uwezo wa
kuwaza jambo fulani (zaidi ya mara moja), basi ujue una uwezo
wa kulifanikisha hilo.”

Wewe ni Mark wa kesho, wewe ni Albert wa kesho, wewe ni


mpindua ulimwengu wa kesho inuka na lifanye wazo lako kuwa
mradi kwa manufaa ya ulimwengu.

Kanuni # 4: “Wazo Lina Nguvu Ya Kuishi Zaidi Ya Muwazaji”

Siku moja nilikuwa nafuatilia majadiliano ya Dk. Myles Munroe


na Benny Hinn kuhusu kitabu chake kiitwacho “God’s Big
Idea” (Wazo kubwa la Mungu). Munroe alizungumza mambo
yafuatayo yaliyonifanya nitafakari sana kuhusu wazo. Alisema;

Hakuna jambo lenye nguvu zaidi duniani kushinda wazo.


Mawazo yana nguvu kushinda kifo.
Unaweza kumuua mtu lakini huwezi kuua mawazo yake.
Ulimwengu unaongozwa na watu waliokufa.
Watu walikufa lakini waliacha mawazo yanayoishi.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 9


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Hebu fikiri kuhusu watu hawa Plato, Socrate, Aristotle n.k, hawa
ni watu wa kale sana lakini mawazo yao yanauongoza ulimwengu
hata leo. Kama umesoma elimu ya dunia hii bila shaka
umekutana na falsafa zao zinazotumika hata leo.

“Mtu anaweza kufa lakini mawazo yake


kamwe hayawezi kufa.”

Ninapenda sana kusoma vitabu lakini vingi ninavyovisoma ni vya


watu waliokufa zamani. Kwa mfano Biblia ni kitabu changu
pendwa, wanatheolojia wanasema kitabu hiki kiliandikwa na
watu wapatao 40 kwa muda wa miaka isiyopungua 1500.

Kati yao hakuna hata mmoja anayeishi leo, lakini Biblia


inaongoza kwa mauzo duniani kwa sababu ya mawazo ya watu
hawa wa kale. Kuna nguvu katika mawazo.

Kwa muda sasa nimevutiwa sana na maisha ya Steve Jobs


ambaye ndiye mwanzilishi wa kampuni ya “Apple” kampuni
inayoongoza kwa vifaa bora vya mawasiliano duniani kama simu,
kompyuta n.k. Jobs hatupo naye duniani leo lakini wazo lake
linazidi kuishi hata leo. Waooh!

“Unaweza kuishi miaka elfu zaidi kupitia


wazo lako”

Nataka kukutia moyo kuanza kuliweka wazo lako katika uhalisia.


Mimi sijui wazo lako ni lipi, lakini najua kama utaamua kuliweka
wazo lako katika uhalisia ujue utakuwa umeongeza ushawishi
wako hata baada ya kufa kwako.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 10


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Ni maombi yangu kwamba wazo utakaloamua kulitendea kazi


likaishi zaidi yako na likawaongezee thamani watu wengi katika
maisha yao.

“Ulimwengu utalitunza wazo lako baada


ya kifo chako kama tu utaliweka katika
uhalisia, kazi kwako.”

Adriano Mkonda +255 754 589 370 11


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

VYANZO 5 VYA KUPATA WAZO


LENYE TIJA

V ipo vyanzo vingi vya kupata mawazo, katika kipengele hiki


tutajikita zaidi katika vyanzo 5 ambavyo mimi nimevipa
kipaumbele zaidi. Kujua chanzo cha wazo kutatusaidia kuweka
umuhimu katika chanzo husika ili tuwe na mawazo yenye
matokeo.

Chanzo # 1: Mtu Mwenyewe

Kila mwanadamu kwa asili ana uwezo wa kuzalisha mawazo


(zaidi ya 6000 kwa siku) kupitia kiungo kiitwacho ubongo. Na
Mungu alituumba hivyo kwa makusudi maalumu.

Katika kitabu chake cha “Ideas Rule The World” (Mawazo


Huutawala Ulimwengu) mwandishi Sam Adeyemi anasema;
“Mungu hakuumaliza uumbaji, aliuanza tu. Alimpa mwanadamu fursa
ya kumsaidia kuumba kupitia mawazo yake. Angeweza kuumba kila
kitu tulichonacho leo, lakini hakufanya hivyo kwa sababu alitaka
kushirikiana na mwanadamu.”

“Wewe ni injini ya mawazo kama


ukiyachakata vizuri unaweza kuuendesha
na kuutawala ulimwengu.”

Adriano Mkonda +255 754 589 370 12


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Ben Carson aliandika kitabu kiitwacho “You Have A Brain”


(Una Ubongo) kutukumbusha kuwa tunaweza kuzalisha mambo
makubwa ulimwenguni kupitia ubongo. Amua kuutumia ubongo
wako vizuri kuanzia sasa. Uumbaji wa Mungu unategemea sana
wazo lako, una fursa ya kuumba jambo jipya ulimwenguni.

Chanzo # 2: Mungu

Licha ya kuwa yeye ndiye aliyetuumba na kutupa zawadi ya


ubongo, hayo hayamzuii yeye kuendelea kuachilia mawazo
kwetu kwa ajili ya utukufu wake. Katika Nehemia 7:5, Biblia
inasema;

“Mungu wangu akatia wazo moyoni


mwangu.”

Mungu anaweza kutia mawazo katika fahamu zetu kwa njia


mbalimbali kama maono, ndoto, mashauri, tunapolisoma neno
lake, kupitia mafundisho kutoka kwa watumishi wake,
tunapomwomba n.k. Ni sisi kukaa vizuri na yeye. Mungu ana
mawazo mema anayotuwazia (Yeremia 29:11).

Chanzo # 3: Uhitaji Au Tatizo

Nyuma ya tatizo lolote lipo wazo ambalo likigunduliwa na


kufanyiwa kazi tatizo hilo litakuwa limetatuliwa. Je! Wajua kuwa
Hospitali ni wazo lililotokana na tatizo la magonjwa? Je!
Watambua kuwa Benki, M-Pesa, Tigo-Pesa, Airtel Money, n.k
ni matokeo ya mawazo yaliyotokana na tatizo la mzunguko duni
wa pesa.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 13


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Hata ndege, meli, magari, bajaji na Bodaboda ni vitu vilivyoanza


kama mawazo ili kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji.
Karibu kila kitu duniani ni zao la tatizo.

“Tatizo ni fursa ya kuuruhusu ubongo


wako kuzalisha mawazo yenye tija.”

Dunia imejaa matatizo katika kila kona yanayohitaji mawazo


yatakayokuwa sababu ya kuondoka kwa matatizo hayo. Hata
hapo ulipo umezungukwa na matatizo. Anza kufikiri namna ya
kutatua tatizo hilo na hakika utapata wazo, baada ya kulipata
litendee kazi. Kumbuka;

“Ulimwengu unawatafuta watatua


matatizo, na upo tayari kuwalipa kwa
jitihada zao za kuyatatua.”

Chanzo # 4: Kujifunza

Kisima kingine cha kupata mawazo yenye manufaa ni kujifunza.


Kujifunza hakutupi tu mawazo bali kunatutanua pia kimawazo.
Tumia fursa ya kujifunza kupata mawazo. Jifunze katika kila kitu
unachokipitia katika maisha. Jifunze katika kila mazingira
utakayokuwepo. Kumbuka;

“Mawazo yapo tayari kujifunua kwa wote


walio tayari kujifunza.”

Kama wewe ni mwanafunzi tumia fursa hiyo kuzalisha mawazo


yenye tija. Jifunze kwa kuuliza maswali, jifunze kwa kutazama,
Adriano Mkonda +255 754 589 370 14
Nguvu Ya Wazo Februari -2022

kwa kusoma vitabu, kwa kuwasikilize watu wenye ushawishi n.k.


Kwa namna yoyote ile hakikisha unajifunza.

Mhamasishaji na mnenaji Tony Robbins kwa miaka mitatu


alisoma vitabu zaidi ya 700. Na kwa sasa ana chuo chake. Mtu
asiyekuwa na “Degree” anamiliki chuo? Hapana muujiza hapo,
ni nguvu ya kujifunza.

“Kama utawekeza katika kujifunza ni


lazima utapata mawazo mapya tena yenye
tija, ni swala la muda tu.”

Chanzo # 5: Kutembelea Maeneo Tofauti tofauti

Ukiondoa elimu ya darasani, jambo jingine linaloweza


kumuelimisha mtu ni kusafiri. Watu wanaozunguka maeneo
mbalimbali kwa namna yoyote wana utofauti mkubwa na watu
wanaokaa eneo moja siku zote.

“Kutembea kunamfanya mtu awe na


uwanja mpana wa kujua mambo mengi.”

Nikiwa nafanya tathmini yangu ya mwaka 2021, nikagundua


kwamba kwa mwaka 2021 nilisafiri maeneo tofauti tofauti 12
(wastani wa eneo moja kwa kila mwezi). Katika hayo, maeneo 9
nilisafiri na mchungaji wangu (my mentor) kihuduma.

Laweza kuonekana jambo la kawaida, lakini nataka nikwambie


mwaka 2021 umekuwa mwaka wa historia kwangu. Kwa sababu,
kwanza, nimeyafahamu maeneo mengi mapya kwangu. Pili,

Adriano Mkonda +255 754 589 370 15


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

nimeongeza uzoefu wangu kihuduma na kubwa zaidi nimepata


mawazo mapya kihuduma na kimaisha kwa ujumla.

“Usipuuzie safari kuna mema nyuma


yake”

Tembelea maeneo mbalimbali, kwa mfano maeneo ya


maonyesho kama vile katika siku za sabasaba, nanenane, n.k
(kwa Tanzania). Maeneo ya utalii na maeneo ambayo unadhani
unaweza kuongeza ufahamu ukiyafikia.

Jambo la muhimu ni kwamba kila unapoenda usiende bure,


hakikisha baada ya safari kuna jambo umejifunza hata kama
dogo. Kwa kufanya hivyo utajiona ukikua kimawazo kila siku.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 16


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

WAZO HADI UHALISIA

“Zijue Hatua 5 Za Wazo Linalofanikiwa”

B aada ya kuzijua kanuni za wazo na vyanzo vya wazo, ni


muhimu sasa tukajifunza mchakato wa kuyafanya mawazo
yetu kuwa uhalisia.

Katika kitabu hiki tutajifunza hatua 5 za wazo ambazo mimi


nimejifunza kutoka kwa kijana wa Biblia Yusufu. Wazo lolote
ambalo litahitimu na kuwa uhalisia lazima lifuate hatua hizi.
Kumbuka;

“Wazo hata likiwa kubwa kiasi gani kama


halitahitimu na kuwa uhalisia, litakuwa
halina maana yoyote.”

HATUA 5 ZA WAZO LENYE TIJA

Hatua # 1: Kuzaliwa Kwa Wazo

Yusufu kijana wa Mzee Yakobo akiwa na umri wa miaka 17


akapata wazo kwa njia ya ndoto. Biblia inasema “Yusufu akaota
ndoto…” (Mwanzo 37:5). Kama tulivyojifunza hapo awali, wazo
linaweza kuzaliwa katika vyanzo mbalimbali, Yusufu anapata
wazo kwa njia ya ndoto.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 17


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Mstari wa 9 unasema “Akaota tena ndoto nyingine…” Akawaza


tena (Pre-dominant thought). Ni muhimu tujifunze kwamba
wazo lenye tija haliwezi kuzaliwa tu na kupotea, litarudia na
kurudia, na kurudia… Kama kuna wazo linarudia rudia basi
kuwa makini na hilo, linaweza kuwa jambo kubwa sana baadaye.

Wazo hurudia rudia ili kutupa uhakika. Hii ni kwa sababu, wazo
linapozaliwa mara nyingi huwa halieleweki na humfanya
muwazaji awe na mashaka huku akijiuliza maswali mengi kuhusu
wazo hilo. Karibu kila mtu hupita katika hali hii.

Yusufu hakuishia tu kuwaza na kuwaza,na kuwaaaaza… wazo


hilo likageuka na kuwa picha kubwa ya baadaye yake yaani
MAONO ya Yusufu; “Kuwa mtu mkuu, mtawala.”

“Maono yote madogo kwa makubwa


huanza kama wazo.”

Hatua # 2: Kuhamasika

Katika hatua hii wazo linakuwa limeeleweka kwa muwazaji, na


linaanza kuchukua nafasi katika moyo na maisha yake. Mtu
anaanza kujiona katika lile wazo, anaanza kuona vile
atakavyokuwa kama wazo hilo litafanikiwa. Naam, wazo hukua
na kuanza kuwa maneno.

Kwenye kitabu chake cha “Be All You Can Be(Kuwa Vyote
Unavyoweza Kuwa), John Maxwell anasema “mtu anaanza
kutamka/kusema kuhusu ndoto yake (wazo lake).”

Adriano Mkonda +255 754 589 370 18


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

“Kama hutohamasika kiasi cha kulisema


wazo lako, lichunguze vizuri wazo hilo.”

Biblia inasema; “Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake


habari…akaota tena ndoto nyingine akawaambia ndugu zake,
akasema...Akawaambia baba yake na ndugu zake;” (Mwanzo 37:5, 9,
10).

Kama unafuatilia vizuri utagundua kuwa kila alipoota (alipowaza)


Yusufu alihamasika naam, hakuishia kuhamasika tu alianza
kusema kuhusu ndoto yake. Hakujali ndugu zake
wangemfikiriaje, alichojali ni kufika kwa taarifa ya wazo lake.

Je! Umehamasika kiasi cha kuweza


kulisema wazo lako hadharani?

Hatua # 3: Kukataliwa Kwa Wazo

Wazo hukataliwa kwa sababu ya hatua ya kuhamasika


inayohusisha kujulikana kwa wazo kwa watu wengi. Wazo lolote
lenye manufaa huwa ni kubwa kuliko muwazaji, haliendani na
hali ya muwazaji. Naam, kwa sababu hiyo watu huanza kulikataa
wazo kwa sababu wanaamini halitawezekana.

“Kama ukiwaambia watu wazo lako na


asiwepo wa kulikataa, jiulize mara
mbilimbili juu ya uzito wa wazo lako.”

Adriano Mkonda +255 754 589 370 19


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Akiwa amehamasika kuhusu wazo lake, Yusufu anaanza


kukutana na upinzani mkubwa kutoka kwa ndugu zake. Biblia
inasema; “…nao wakazidi kumchukia.” (Mwanzo 37:5) na “…baba
yake akamkemea.” (Mwanzo 37:10). Yote ni kwa sababu ya wazo
lake. Jaribu kutafakari.

Upinzani ni wa muhimu sana kwa sababu unatoa uhakika wa


wazo unaloliwaza. Unakusaidia kujua kuwa wazo hilo lina
manufaa kwa wengi, ni mti wenye matunda huo. Na kumbuka
siku zote;

“Mti wenye matunda ndio hupigwa


mawe.”

Kila mtu mwenye wazo lenye tija hupitia hatua ya wazo lake
kukataliwa. Watu kama kina Mwalimu Nyerere, Mama Teresa,
Mahatma Ghandi, Abraham Linkolin, Martin Ruther King Jr,
Nelson Mandela, Bill Gates na wengine wengi, wanaijua vizuri
radha ya hatua hii.

Lakini hawakukata tamaa walipiga hatua na kuielekea hatua ya


nne ili kuuhakikishia ulimwengu uhalisia wa mawazo yao. Hata
Yusufu alifanya hivyo, wewe pia unaweza.

“Vinginevyo umechagua kusonga mbele,


uwe na uhakika kwamba wazo lako litafia
hapo.”

Adriano Mkonda +255 754 589 370 20


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Hatua # 4: Kulipa Gharama

John Maxwell katika kitabu chake kiitwacho “Put Your Dream


ToThe Test” (Iweke Ndoto Yako Kwenye Kipimo), ameelezea
maswali 10 ambayo mtu anapaswa kujiuliza kama anataka ndoto
yake iwe uhalisia. Na swali la 7 (sura ya 7) ni swali la gharama, je!
Upo tayari kulipa gharama kuielekea ndoto yako?

Ni sawa na kusema je! Upo tayari kulipa gharama kwa ajili ya


wazo lako? Katika kitabu cha “Be All You Can Be” (Kuwa
Vyote Unavyoweza Kuwa), Maxwell anaielezea hatua hii kama
hatua ya kulinunua wazo (I bought it stage). Lazima ulipe
gharama ili kuhakikisha kwamba wazo lako linakuwa uhalisia.

“Hakuna hata mtu mmoja ulimwenguni


aliyeweza kukamilisha ndoto yake (wazo
lake) pasipo kulipa gharama.”
John Maxwell

Watu karibu wote hupitia hatua ya 1 hadi ya 3 ya wazo. Ni


wachache hufika katika hatua ya kulipa gharama, naam, hao
ndio hufanikiwa kuyafanya mawazo yao uhalisia.

Katika hatua nyingine Yusufu sasa anapaswa kulipa gharama ili


kuhakikisha wazo lake linatimia. Dunia itakupitisha katika
majaribu ya kila aina ili kukufanya uachane na wazo lako.
Unapaswa kushinda kila jaribu ili ufikie lengo, naam huko ndiko
kulipa gharama.

“Unapaswa kulipa gharama.”

Adriano Mkonda +255 754 589 370 21


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Yusufu alipitia majaribu makubwa manne na alipaswa


kuyashinda (kulipa gharama) katika safari yake ya kuwa “mtu
mkuu, mtawala”. Majaribu hayo ni;

1. Jaribu la kifo – Kutoka kwa ndugu zake


2. Kuuzwa na kuwa mtumwa ugenini
3. Kutamaniwa na mke wa bosi wake Potifa
4. Kufungwa gerezani kwa miaka mingi.

Hayo ni magumu ambayo Yusufu aliyapitia, japo yalikuwa na


uchungu ndani yake na aliyapitia kwa miaka mingi, yalimpa
hatua kuuelekea uhalisia wa wazo lake. Kwa nini? Kwa sababu
Yusufu hakuchagua kukata tamaa, bali kulipa gharama.

“Kukata tamaa sio chagua, kulipa


gharama ndiyo busara.”

Pengine wazo lako halitakuwa na gharama kama za Yusufu,


lakini unalopaswa kujua ni kwamba kwa namna yoyote utapaswa
kulipa gharama.

Yawezeka ikawa gharama ya kuondokana na hofu binafsi,


kufanya kazi kwa bidii, kutoa pesa yako, kutengana na baadhi ya
marafiki, kuishi eneo usilolipenda, upweke, kushinda vikwazo
n.k. Jiandae kama kweli unataka wazo lako liwe uhalisia, lazima
tu ulipe gharama.

“Wewe si mtu maalumu sana kiasi


kwamba usitarajie kulipa gharama kwa
ajili ya wazo lako, jiandae.”

Adriano Mkonda +255 754 589 370 22


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Wasomaji wa Biblia tumfahamu vizuri Ibrahimu (Baba wa


imani). Mungu aliahidi kumbariki yeye pamoja na uzao wake
lakini haikuwa rahisi, alipaswa kulipa gharama nyingi tena zenye
kumuumiza.

Kwa mfano, alipaswa kuondoka katika nchi yake na kwenda


asikokujua. Alipaswa kutengana na ndugu yake Lutu. Alipaswa
kusubiri mtoto wa ahadi kwa miaka mingi. Alipaswa kumtoa
mwanae Isaka sadaka ya kuteketezwa n.k. Na mwisho wa yote
alizifikia Baraka alizoahidiwa. Nataka nikutie moyo kwamba;

“Jiandae kulipa gharama, mema yapo


mbele.”

Gharama Za Msingi Kuelekea Uhalisia Wa Wazo Lako

Yafuatayo ni mambo ambayo unapaswa kuyafanya baada tu ya


kupata wazo. Kila jambo ni la muhimu, litakupelekea katika
hatua ya kulifanya wazo lako kuwa uhalisia. Mambo haya mimi
nayaita “gharama za msingi kuelekea uhalisia wa wazo”;

Andika wazo lako – Wazo lazima liandikwe (Hab. 2:2-3)


Ligeuze wazo lako kuwa lengo – Zingatia kanuni za lengo
(S-M-A-R-T” principle)
Andaa mpango kazi wa kufikia wazo lako.
Fanya jambo kila siku – Wajibika kuuelekea uhalisia wa
wazo lako.
Tathmini maendeleo ya wazo lako mara kwa mara
Liombee wazo lako mara kwa mara.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 23


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Hatua # 5: Kukamilika Kwa Wazo (Uhalisia)

Uhalisia ni hatua ambayo kila mtu huitamani, kila mtu hutamani


baada tu ya kuzaliwa kwa wazo aone uhalisia, jambo ambalo
haliwezekani. Kukamilika kwa wazo ni matokeo ya hatua nne za
awali, na zaidi sana hatua ya nne, yaani kulipa gharama.

Ni kama tunapoenda dukani kununua bidhaa baada ya kulipia


tu tunapewa bidhaa, hivyo ndivyo ilivyo katika wazo pia. Uhalisia
unakuja baada ya kulipa gharama. Na wakati mwingine
unatukuta tukiwa tumekata tamaa kabisa, hatuna tumaini la
ukamilifu wa wazo husika.

“Vile unavyoendelea kulipa gharama


ndivyo unavyoukaribia uhalisia wa wazo
lako.”

Katika magumu aliyokuwa anayapitia naamini Yusufu kuna


wakati alichoka hata kama Mungu alikuwa pamoja naye. Lakini
ukweli ni kwamba katika kuchoka kwake ushindi wake ulikuwa
karibu sana.

Kwa mfano, katika Mwanzo 40, Yusufu akiwa gerezani kwa


miaka mingi, anawatafsiria ndoto watumishi wawilli wa Farao na
anamwomba mmoja wao amkumbuke (amsaidie kutoka
gerezani). Lakini Biblia inasema huyo hakumkumbuka Yusufu
(Mwanzo 40:23).

Wakati mwingine tunaweza kutumia njia ya mkato (shortcut)


kuutafuta uhalisia, lakini ukweli ni kwamba, ukamilifu wa wazo
hautafutwi, unakuja wenyewe kwa wakati sahihi.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 24


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

“Huhitaji kupita njia ya mkato, unahitaji


tu kuendelea kulipa gharama na uhalisia
utakuwa matokeo ya gharama uliyoilipa
kwa muda.”

Katika sura ya 41, kwa namna asiyoitarajia Yusufu akapata


mwaliko maalumu ikulu kwa Farao kufanya jambo ambalo
hakuna mganga wala mchawi wa Misri aliweza kulifanya. Kufasiri
ndoto ya Farao, gharama ya mwisho aliyopaswa kuilipa
kuuelekea ukamilifu wa wazo lake.

Baada ya kukamilisha hilo ndipo Farao anasema; “...Tupate wapi


mtu kama huyu, mwenye Roho ya Mungu ndani yake.” (Mwanzo
41:38). Na katika mstari wa 40-wazo lililozaliwa kwake akiwa na
umri wa miaka 17 linahitimu na kuwa uhalisia. Ooh! Haleluya.
Na Farao anamwambia;

Mwanzo 41:40 “Basi wewe utakuwa msimamizi wa


nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu
watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu
kuliko wewe.”

Bila shaka utakuwa umejifunza kitu hapa. Huhitaji kuhangaika


na uhalisia wa wazo. Unahitaji kuwa na wazo, kuhamasika,
kujiandaa kwa sababu upinzani utakuja na kulipa gharama.
Kukamilika kwa wazo kutakuwa ni matokeo ya hizo hatua nne.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 25


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

WAZO LAKO MAISHA YAKO

“Ijue nguvu ya wazo katika maisha yako”

S iku moja nilikuwa namfuatilia mwalimu James Kalekwa


(ambaye kwa sasa ni mchungaji wa New Vine Church
Dodoma-Tanzania), akiwa anafundisha somo la “Ujenzi Wa
Tabia” kwa njia ya CD. Somo hili lilibadilisha maisha yangu
sana.

Katika somo hilo Kalekwa alieleza kwamba maisha ya


mwanadamu ni mchakato ambao huanza na;

1. Wazo
2. Wazo hukomaa na kuwa Neno (Maneno)
3. Neno likikomaa hujitafsiri na kuwa Tendo.
4. Tendo likiwa endelevu hugeuka na kuwa Tabia.
5. Tabia mbalimbali zikiungana huzaa Mfumo wa Maisha.
6. Na Mfumo wa Maisha ndiyo huamua Hatma ya mtu.

Tazama kielelezo hapa chini kwa ufahamu zaidi.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 26


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

WAZO

MAISHA NENO

TABIA TENDO

Katika kujifunza kwangu ndipo nilitoka na hitimisho kwamba


“Wazo langu ndiyo maisha yangu.” Na toka hapo mfumo wangu
wa maisha umebadilika mno kuanzia namna ninavyowaza.
Kumbuka, kila kitu huanza na wazo hata maisha yanaanza na
wazo.

“Maisha yako ni matokeo ya namna


unavyowaza, huwezi kuishi zaidi ya
mawazo yako.”

Ukiurudisha ufahamu wako tangu mwanzo wa kitabu hiki


mpaka hapa tulipofikia unaweza kugundua kwa upana zaidi
nguvu ya wazo. Kwa umuhimu huo, katika kipengele hiki nataka
tujifunze kwa kina zaidi nguvu ya wazo.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 27


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Nguvu Ya Wazo Katika Maisha

Biblia inasema;

Mithali 23:7 “Maana aonavyo nafsini


mwake ndivyo alivyo.”

“Maana awazavyo mtu katika ufahamu wake ndivyo


atakavyoishi.” (Tafsiri yangu). Wazo lina nguvu katika maisha
kwa sababu zifuatazo;

1. Wazo ndiyo chanzo cha kusudi la maisha ya mwanadamu.


Kulikuwa na wazo moyoni mwa Mungu lililomsukuma
Mungu akuumbe wewe. Hilo ndilo lililoamua maisha
yako hapa duniani.
2. Wazo ni chanzo cha maono.
Haijalishi una maono makubwa kiasi gani katika maisha
yako. Tambua kuwa yalianza kama mawazo tu.
3. Wazo ni chanzo cha malengo
Yawe ya muda mrefu au mfupi. Malengo ni mazao ya
mawazo.
4. Wazo ni chanzo cha mipango
Tunaweza kupanga mipango kwa sababu tuna mawazo.
Hakuna mawazo hakuna mipango.
5. Wazo huleta msukumo wa utendaji
Tunawajibika kwa sababu ndani yetu kuna mawazo
ambayo tunatamani kuyaweka katika uhalisia.
6. Wazo ni mtaji (chanzo cha utajiri)
Huhitaji pesa ili uwe tajiri, unahitaji wazo ambalo
litakupa utajiri.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 28


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

7. Wazo ni chanzo cha mabadiliko


Palipo na mawazo mara zote huwa pana mabadiliko na
kinyume chake ni sahihi.
8. Wazo ni chanzo cha mafanikio
Mafanikio yote yamefichwa nyuma ya mawazo.
Wawezao kuyafichua ndiyo hufanikiwa.
9. Wazo ndiyo maisha, hakuna wazo hakuna maisha.

Kumbuka!

Kuna nguvu nyuma ya kila wazo. Usiyaone mawazo yako ya


kawaida, hayo ndiyo yamebeba hatma yako. Kwa hayo unaweza
kufanikiwa au kutofanikiwa. Wekeza katika mawazo yako hasa
yale ambayo ni chanya, baadaye utakula matunda yake.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 29


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

HITIMISHO

N ikushukuru sana kwa kuutoa muda wako, kusoma kitabu


hiki mpaka nukta hii. Uwekezaji wako si bure, utayaona
matunda yake sawasawa na shauku yako.

Tunapomalizia nataka nikuulize swali lifuatalo “Unawaza nini?”


Ni imani yangu kwamba tangu tulipoanza kuna mawazo
yamekuwa yakitiririka katika kichwa chako. Au kama sivyo
ninaamini una wazo lililouandama moyo wako kwa muda sasa.

Kumbuka, mpango wa Mungu ni hilo wazo lako likomae na


kuwa uhalisia. Wewe pekee ndiye unayeweza kuamua kama
wazo hilo litakuwa uhalisia au la.

Kwa kufuata kanuni na mashauri yaliyositirika katika kitabu hiki


unaweza kulifanya wazo lako uhalisia. Chukua hatua.
Kumbuka, ulimwengu unasubiri kwa hamu matunda ya
ukamilifu wa wazo lako.

Zaidi sana, mimi nitafurahi kusikia mafanikio ya wazo lako,


maana mafanikio yako ni kipimo kikubwa cha mafanikio ya
maono makubwa aliyoyaweka Mungu ndani yangu.Nikutakie
safari njema ya kuyatafsiri mawazo yako katika uhalisia.

“Shiriki nami ushuhuda wako kupitia mawasiliano


yanayopatikana katika kitabu hiki. Nitafurahi kusikia
kutoka kwako.”

Adriano Mkonda +255 754 589 370 30


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

BIBLIOGRAFIA

Longhorn. (2011). Kamusi ya karne ya 21. Dar es salaam,


Tanzania: Longhorn publishers (T) Ltd.

Maxwell, J. (2001). Be all you can be. India: WorldAlive


Publishers.

Maxwell, J. (2009). Put your dream to the test. USA: Thomas


Nelson in association with Yates & Yates.

Munroe, M. (2012). Gods big idea. USA: Destiny image


publishers.

The Holy Bible in Kiswahili. (2013). Dodoma, Tanzania: The


Bible society of Tanzania.

Adriano Mkonda +255 754 589 370 31


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

KUHUSU ADRIANO MKONDA

Adriano Mkonda ni mwalimu kitaaluma, mwalimu wa Neno la


Mungu na mwandishi wa vitabu.

Yeye ni muasisi wa Mkonda’s Teaching And Learning Program,


aliyoiasisi kwa malengo makuu mawili. Kwanza, kuwafikia watu
kwa njia ya vitabu vya kimtandao (e-books) na vya kawaida. Na
pili, kuwafikia “Vijana Chipukizi” (miaka 10-20), ili kuinua kizazi
bora cha kesho.

Unaweza kuwasilana naye kwa mawasiliano yafuatayo;

Adriano Mkonda
Barua Pepe: mkondaadriano10@gmail.com
Simu: +255 754 589 370/+255 621 618 821
Whatsapp: +255 754 589 370

Adriano Mkonda +255 754 589 370 32


Nguvu Ya Wazo Februari -2022

Adriano Mkonda +255 754 589 370 33

You might also like