You are on page 1of 80

Jinsi ya Kuishinda

Hofu ya Kuanza

Jinsi Ya Kuishinda Hofu Yako Na Namna Unavyoweza


Kujenga Kujiamini Kwako

Joel Arthur Nanauka


© Julai 2021 Joel Arthur Nanauka

Haki zote zimehifadhiwa. Huruhusiwi kunakili, kudurufu


au kutumia sehemu ya kitabu hiki bila idhini ya
mwandishi. Kufanya hivyo itakuwa ni ukiukwaji wa haki
za mwandishi, na ukiukwaji wa taratibu hii unaweza
kupelekea mashitaka toka kwa waandaaji wa kazi hii.

Joel Arthur Nanauka


Dar-Es-Salaam, Tanzania. East Africa
Simu: +255 756 094875 / 0745 252 670
Barua pepe: jnanauka@gmail.com
Tovuti: www.joelnanauka.com

Kimesanifiwa na INFINITE PRESS


Contacts +255 757 400 948
Email: praisearnold.pa@gmail.com

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 01


YALIYOMO

UTANGULIZI 04

SURA YA KWANZA: EPUKA MAJUTO KATIKA MAISHA


YAKO 06
SURA YA PILI: AMUA KUBADILI HISTORIA YA HAITI
YAKO 14

SURA YA TATU: MAKUNDI MATATU YA WATU


WASIOCHUKUA HATUA 23

SURA YA NNE: UKO TAYARI KUTOKUELEWEKA? 30

SURA YA TANO: TIBA YA DESTINY DISEASE 41


SURA YA SITA: NYAKATI TATU
ZITAKAZOKUTOFAUTISHA 52
SURA YA SABA: AINA MOJAWAPO YA WATU HATARI
ZAIDI UNAOTAKIWA KUWAEPUKA 61

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 02


HITIMISHO 67

KUHUSU MWANDISHI 68

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 03


UTANGULIZI

Kuna ndoto nyingi sana zinaozea mioyoni mwa


watu. Kuna watu ambao kinachowakwamisha sio
kukosa uwezo au kuwa na mtaji mdogo, ni hofu ya
kuanza.

Kuna ambao wana hofu ya kuanzia chini. Wanaona


watajidhalilisha, wanaona watu watawashangaa na
pengine kuwacheka. Hivyo ili kuepuka yote hayo,
wameamua bora wasianze kabisa.

Kuna watu wanaogopa kuanza kwa sababu


wanajiona hawajakamilika kabisa. Wanaona kama
kuna vitu wanatakiwa wawe navyo kwanza ndipo
waanze.

Watu hawa huwa kila siku wanajiona


wamepungukiwa kitu fulani. Wana tatizo la “Scarcity
Mentality”, Kila siku kujiona wamepungukiwa kitu.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 04


Watu wa namna hii hata wakipata kile ambacho
wanasema wanakikosa, huwa hawaanzi na
wanatafuta kingine wasichonacho ili kukitumia
kama kisingizo cha kutokuanza kwao.

Wewe mwenyewe unajua, mara ngapi ulisema


utaanza na kila siku unaghairisha na kupeleka
mbele?

Kumbuka ukitafuta visingizio vya kutokuanza, kila


siku utavitapa. Leo tafuta sababu za kuanza.

Usiogope Kuanza!!!

Je, wewe unaanza nini?

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 05


SURA YA KWANZA

EPUKA MAJUTO KATIKA MAISHA


YAKO

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 06


Dr. Anthony Campolo aliwahi kufanya stadi ya kijamii
(Sociological Study) Kwa kuzungumza na watu 50
wenye umri zaidi ya miaka tisini na tano.

Katika utafiti huu aliwauliza swali moja tu “Kama


ungepewa nafasi ya kuishi tena ungefanya nini cha
tofauti?” Katika majibu waliyotoa kuna majibu
MAWILI ambayo yalitawala zaidi kwa kutolewa na
watu wengi.

Cha kwanza kabisa wengi walisema “I would risk


more” (Ningefanya vitu bila kuogopa changamoto
ambazo zingetokea).

Wengi wao walisema pia waligundua wameshindwa


kufanya mambo makubwa kwenye maisha yao kwa
sababu ya uoga.

Wengi wao WALIKIRI kuwa waliwahi kuwa na


mawazo mazuri ya biashara ila waliogopa kuanza
kufanya. Waliwahi kutaka kubadili taaluma zao ila
walihofia kupoteza.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 07


Waliwahi kutaka kuanza upya ila waliogopa
kuchekwa. Waliwahi kutamani kufanya kitu
kitachowapa furaha ila walijawa na hofu kuwa
hawataweza n.k

Walichokuja kugundua ni kuwa, maumivu waliyopata


moyoni kwa KUTOKUFANYA kilichokuwa ni SAHIHI
yalikuwa ni MAKUBWA kuliko HATARI walizokuwa
wanaziogopa.

Na wewe unaogopa “kurisk”?

Jambo la pili ambalo wengi walilisema ni kuwa


wangefanya vitu ambavyo VINGEENDELEA kuishi
hata wao baada ya KUONDOKA DUNIANI.

Waligundua kuwa furaha ya kweli haiko kwenye


kujipatia wanachotaka tu bali kuacha ALAMA ya
kudumu duniani na kuiachia dunia kitu KIZURI
ambacho wataendelea KUKIFURAHIA baada ya wao
kuondoka.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 08


Waligundua kuwa sio lazima ufanye kitu kwa DUNIA
NZIMA, unaweza kuanza kwenye familia yako, kijiji
chako, shule yako n.k

Amua kuwa wewe hautajutia mambo haya mawili


kwa kuanza kufanya kitu leo. Umeshawahi kukutana
na watu ambao wanaonekana kama kila wakati wana
furaha tu! Na hawana huzuni kabisa?

Yaani hata wakati mwingine inakuwa ngumu sana


kujua kama wanapitia changamoto ama la!

Ukweli ni kuwa hakuna ambaye anazaliwa akiwa


namna hiyo. Unachotakiwa kujua ni kuwa “attitude”
(mtazamo) katika maisha huwa inatengenezwa.

Katika tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa njia


mojawapo ya kutengeneza mtazamo chanya
(Positive attitude) ni kufanya “Positive Visualization”
Yaani kutengeneza picha ya mambo mazuri ambayo
yanakuja mbele yako.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 09


Wachezaji wengi waliowahi kushinda mashindano ya
olimpiki huwa wanatumia njia hii. Leo, unapoanza
siku yako badala ya kuruhusu mawazo ya
kushindwa, tumia dakika 3 kufumba macho na
kufikiria jinsi siku yako itakavyoenda vizuri.

Jenga picha ya kila kitu kitakavyotokea na tukutane


jioni tupeane mrejesho. Utashangaa ukiweza
kujenga picha ya mambo mazuri yatakayotokea leo
na kuiamini bila shaka, yatatokea.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 10


IJUE KANUNI YA 70%

Juzi usiku nilitumiwa makala na rafiki yangu wa siku


nyingi sana ambaye kwa mara ya kwanza niliporipoti
kuanza kazi UN ndiye alikuwa bosi wangu.

Moja ya kitu nilijifunza kwake kwa muda niliofanya


naye kazi ni “alikuwa mtu wa vitendo” (Action
Oriented).

Hii ilikuwa ni moja ya SIFA iliyomtofautisha sana na


wengine na imemfanya akue kwa haraka na
kufanikiwa kwenda NCHI mbalimbali kufanya kazi.

Katika makala hiyo maarufu iliyoandikwa katika


gazeti la ujasiriamali la India (The Entrepreneur) na
mwandishi Karshmma V Mangal ameelezea kanuni
aliyoiita 70% ambayo anasema watu wengi ambao
wanafanikiwa huwa wanaitumia.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 11


Kwenye kanuni hii anasema usisubiri hadi uwe na
uhakika wa 100% ili kuanza kufanya unachotaka,
usisubiri kuwa na uhakika wa 100% wa mtaji ili
kuanza, usisubiri kuwa na ujasiri/uhakika wa 100% ili
kuanza kuchukua hatua-

Ukiwa na 70% tu zinatosha sana kuchukua hatua


yoyote unayotaka kuanza. Ukisubiri uwe na kila kitu
ndipo ufanye utashangaa haujaaanza kufanya.

Hii ilinikumbusha maneno ambayo yaliwahi kusema


na Martin Luther King Jr aliposema “Imani ni kuanza
kuchukua hatua ya kwanza kupanda ngazi bila
kuona ngazi zinaishia wapi” (Faith is the ability to
take the first step even when you don’t see the
whole staircase).

Kumbuka huwezi kupata asilimia 70 bila kuwa na


asilimia moja-wewe kwa nini usiwe mtu wa imani
zaidi kwa kuamua kuchukua hatua ya kwanza leo.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 12


Acha maneno, weka vitendo! Kuna milango, fursa na
watu wanasubiri uanze kuchukua hatua ya kwanza
na utaanza kupata unachotafuta.

Ni hatua gani ya kwanza unaweza kuanza nayo leo?


-Ni kwenda kumuona mtu? Ni kununua bidhaa moja
ya kuanza kuuza? Ni kufanya maamuzi kwa vitendo?
Chukua hatua, usichelewe.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 13


SURA YA PILI

AMUA KUBADILI HISTORIA YA HAITI


YAKO

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 14


Umeshawahi kufanikiwa katika jambo ambalo
ulikuwa unaona kama vile haliwezekani? Ama
umeshawahi kuvuka kikwazo ambacho kilikuwa
kinaonekana kinatishia mafanikio yako ya kesho?

Umeshawahi kuwa katika hali inayoonyesha kuwa


hautaweza kuinuka tena lakini ghafla unashangaa
umefanikiwa kuvuka kikwazo kilichokuwa
kinakukabili?

Gazeti la Bussiness insider la tarehe 26, May 2016


liliripoti habari iliyokuwa inasisimua na yenye
mafunzo makubwa sana kuhusu mafanikio katika
maisha ya kila siku.

Alix Schoelcher Idrache hakuwahi kufikiria kuwa


kuna siku ambayo ndoto yake ya kumaliza mafunzo
ya kijeshi na kufanikiwa kwa kiwango cha juu
itatimia.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 15


Picha zilisambaa zikimwonyesha akitokwa na
machozi wakati wa sherehe za mahafali ya jeshi ya
kwenye kiwanja cha Michie Stadium in West Point
siku ya May 21 nchini Marekani.

Alix Idrache sio tu alifanikiwa kumaliza mafunzo


yake bali pia alifanikiwa kuwa mwanafunzi
aliyefanya vizuri zaidi kwenye somo la physics na
kupata fursa ya kuendeleza taaluma yake katika
chuo cha jeshi la anga Fort Rucker, Alabama.

Kwa nini habari ya Alix imevutia hisia za dunia?

Moja ni kwa sababu Alix anatoka HAITI, nchi


inayofahamika kwa umaskini wa hali ya juu. Kila nchi
yake inapotajwa watu hufikiri juu ya umaskini
uliokithiri na watu waliokosa matumaini katika
maisha yao ya kila siku.

Ni wazi kuwa watu wengi hupenda kutufanya


tuamini kuwa hatutaweza kufanikiwa kwa sababu ya
historia ya nchi tunazotoka, makabila ama hata ni
eneo gani la nchi unatokea.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 16


Alix hakukubali historia ya mahali anapotokea iwe ni
kikwazo cha yeye kufanikiwa kutimiza ndoto yake. Ni
mara ngapi umesikia kuwa watu wa nchi fulani ndio
wamefanikiwa zaidi?

Ama watu wa mkoa fulani huwa ndio matajiri, ama


hufanya vizuri katika masomo yao kuliko watu wa
eneo unalotokea?

Hujawahi kusikia kuwa pengine ukoo wenu watu


huwa hawamalizi shule? Ama wakiolewa lazima
waachwe, ama huwa hawafanikiwi kifedha?

Kila siku lazima utakutana na historia ya kukatisha


tamaa inayoendana na ile ya Alix, lakini ni uchaguzi
wako mwenyewe kuiamini historia unayoambiwa
ama kuchagua unachotaka kukiamini na kuiishi
ndoto yako kwa mafanikio.

Wakati Alix anahojiwa, alisema baba yake alikuwa


siku zote anamwambia kuwa elimu ndio zawadi bora
Zaidi anayoweza kumpa na kuwa kama akiamua
ataweza kufanikiwa.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 17


Ingawa walikuwepo watu wengi sana ambao
walikuwa wanamwambia kuwa hawezi, yeye
alichagua kuamini maneno ya baba yake kuwa
anaweza.

Kila siku utakutana na watu wanaokuambia maneno


mbalimbali lakini wengi wao watakuambia maneno
ya kushindwa na sio kushinda.Uamuzi ni wako,
unachagua maneno gani?

Unachagua maneno ya wanaosema haiwezekani


kujiajiri Tanzania? Unachagua maneno ya
wanaosema haiwezekani kuwa tajiri kwa sababu ya
elimu yako ndogo?

Kumbuka kuna sauti inayokuambia unaweza, na hiyo


ndio unatakiwa kuichagua na sio vinginevyo.

Kila mtu ana HAITI yake, lakini ni wajibu wako kutoka


kwenye HAITI yako na kuanza Kuiishi NDOTO
YAKO.Nakupa ushauri uwe kama Alix aliyeyashinda
mazingira ya kila aina na akaweza kuitimiza ndoto
yake bila kujali watu walikuwa wanasema nini.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 18


NI ZAMU YAKO SASA.

Natamani kukuona siku moja ukitoa machozi kama


ALIX utakapokuwa umefika kwenye KILELE CHA
NDOTO YAKO, Sio machozi ya huzuni na maumivu
bali machozi ya Furaha.

Na siku hiyo ikifika utaniruhusu nikupige picha.

DUARA MBILI ZINAZOKUKABILI

Kwa Mujibu wa mwandishi Stephen R. Covey


aliyeandika kitabu cha Tabia 7 za Watu Wenye
Ufanisi (The 7 Habits of Highly Effective People),
anasema, kila siku kuna duara mbili zinazokukabili.

Moja ni Duara la ushawishi (Circle of Influence) na


lingine ni Duara la wasiwasi (Circle of Concern).

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 19


Duara la USHAWISHI ni yale mambo ambayo yako
ndani ya uwezo wako kuyakabili. Yaani kuanzia
maamuzi yako utakayofanya leo, tafsiri yako juu ya
changamoto zinazokukabili, unachoamua kufanya
baada ya mtu kusema neno baya n.k.

Duara la WASIWASI ni yale mambo ambayo yako juu


ya uwezo wako na huwezi kuyabadilisha kama vile
hali ya hewa, asili ya familia yako, watu
wanachosema kuhusu wewe n.k.

Watu wengi ambao wanaongoza kuwa na stress na


kukosa furaha ni wale ambao kila wanapoamka
wanajikita kwenye duara la wasiwasi na matokeo
yake wanaona maisha yamewashinda.

Watu wanaotimiza malengo yao huwa wanajikita


katika duara la ushawishi kwa kushughulika na
mambo ambayo wana ushawishi nayo au kutawala
mtazamo wao katikati ya magumu wanayopitia.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 20


Badala ya kulalamikia yale ambayo yako juu ya
uwezo wako, jiulize: Ni kipi kipo ndani ya uwezo
wangu ambacho naweza kukifanya leo? Wewe leo
unachagua kujikita katika duara lipi?

Ikabili hofu yako

Kuna vitu vingi sana vya kukutia hofu utakuwa


unakutana navyo kwenye maisha yako ya kila siku.
Mara nyingine mambo haya ya kukutia hofu
yanakatisha sana tamaa hadi kukufanya uone kama
hautafika unakokwenda.

Moja ya tabia muhimu unatakiwa kujizoesha kwenye


maisha yako ni kujilazimisha kufanya katikati ya
hofu unayoisikia.

Kazi kubwa ya hofu ni kupoozesha hatua zako. Hofu


inakuwa imefanikiwa pale inapokuacha uko
“paralysed” na haujui cha kufanya.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 21


Hofu inakuwa imetimiza jukumu lake kwa 100% pale
inapokufanya ulale tu ndani, ukate tamaa, ujione
haufai tena na uishiwe nguvu kabisa.

Jambo la muhimu la kujua ni kuwa, unao uwezo wa


kuipa ushindi hofu yako au ukaifanya ishindwe. Leo
bila kujali aina ya hofu inayokukabili, amua kuishinda
hofu yako kwa kufanya kitu.

Kumbuka mara nyingi hofu zinazokukabili huwa


zinapotea unapoamua kukabiliana nazo. Badala ya
kuikimbia, amua kukabiliana na hofu yako leo.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 22


SURA YA TATU

MAKUNDI MATATU YA WATU


WASIOCHUKUA HATUA

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 23


Unaweza kuwa na mawazo makubwa sana ila kama
hauchuki hatua haitasaidia.

Mwanafalsafa maarufu Socrates aliwahi kusema “To


Move The World We Must First Move Ourselves” (Ili
kuibadilisha Dunia lazima sisi kwanza tuchukue
hatua). Ukiwa mtu ambaye unasema kila siku ila
haufanyi, basi hautaweza kufika unakotaka.

Kuna makundi makubwa matatu ya watu ambao


hawachukui hatua:

Moja wanasubiri kila mtu awasapoti wanachotaka


kufanya.

Yaani kuna watu kama nguvu wanayotumia kutaka


kila mtu awaelewe wangekuwa wameitumia kufanya
wangefika mbali sana.

Anza kufanya leo.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 24


Mbili kuna wale ambao wanasubiri kila kitu kiwe
sawa kabla hawajaanza.

Kila siku utasikia “naweka mambo sawa kwanza”.


Kuna vitu vingine vitakuja kukaa sawa ukiwa
umeshaanza tayari.

Wa tatu ni wale ambao wanasubiri HAMASA ya


kuanza.

Ni kama gari linalosubiri kupigwa “kick” ili lianze


safari. Utasikia wanasema “Yaani sina hamasa
kabisaaa, ngoja nisubirie nipewe hamasa kidogo”.

Kumbuka hamasa ya muda mfupi ya nje inatokana


na kusikia lakini hamasa endelevu ya ndani
inatokana na kuanza kufanya.

ANZA KUFANYA SASA.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 25


NAMNA BORA YA KUJIULIZA
UNAPOTAKA KUANZA JAMBO

Hivi nikifanya nikafeli itakuwaje?”Hivi nikiwekeza


nikapoteza kila kitu itakuwaje?”Vipi nikaacha hapa
na nikaenda kule na nisifanikiwe?

Umeshawahi kujiuliza maswali ya namna hii?

Kwanza unatakiwa kujua haya ni maswali ya


kawaida sana kwa kila mtu. Kila mtu huwa
anakabiliwa na hofu fulani anapotaka kufanya kitu.

Hata hivyo kuna tofauti kubwa sana ya wale


wanaofanikiwa kufanya na wale ambao hawafanyi
kabisa. Wale wanaofanikiwa kufanya wanajiuliza
maswali kama hayo ila kwa namna tofauti.

Huwa wanajiuliza, “Hivi itakuwaje nisipotumia fursa


hii na isijirudie tena?”, “Hivi nitakosa faida gani kama
sitachukua hatua leo?” n.k

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 26


Ili ufanikiwe kufanya kitu ni lazima uwe na hali ya
uharaka ndani yako (Sense of Urgency). Hii itakuwa
inakuambia kuwa ukichelewa utapoteza.

Watu wengi sana “wamerelax” sana kana kwamba


wana muda mrefu sana wa kufanya mambo.
Kumbuka leo ikipita inakuwa imepunguza kwenye
akiba za siku zako.

Utafanya nini leo ili usipoteze fursa iliyobebwa na


siku ya leo?

Usighairishe.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 27


WAZO LAKO KAMA MBEGU

Unapokuwa na wazo lolote, pale mwanzoni


linapoanza kila mtu atakuwa analiona kama ni jambo
haliwezekani.

Hii ni sawa kabisa kwani wao wanakuwa hawajaona


mwisho wa wazo bali wameona kile kilichopo kwa
wakati huo tu, hivyo usiwalaumu.

Kumbuka wazo linapokuwa linaanza ni kama mbegu


ndogo ambayo inaweza kudharauliwa na kila mtu
bila kujua mti mkubwa unaoweza kuota huko
mbeleni.

Kuna watu wengi sana ambao wamekata tamaa


baada ya wazo lao kukosolewa na kupingwa
kutokana na udogo wake pale walipolisema.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 28


Siku zote kumbuka kuna watu ambao hawatakuwa
tayari kusapoti wazo lako sio kwa sababu
hawakukubali bali kwa sababu hawaoni ukubwa
kama wewe unavyoona.

Kama umeona ukubwa na mwisho wake usikatishwe


tamaa na ambaye bado hajaona.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 29


SURA YA NNE

UKO TAYARI KUTOKUELEWEKA?

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 30


Huwezi kuwa mtu wa tofauti kama unaogopa kuwa
tofauti. Dunia imejaa watu ambao wanataka
mfanane kwa kila kitu.

Na mara utakapo onyesha kuwa una kitu au mbinu


ya tofauti, wanaanza kukugeuza kuwa adui.
Umeshawahi kusikia msemo wa kiswahili unasema
“Kifo cha wengi ni harusi?” Kuna wengi sana
wanaumini na wanauishi msemo huu.

Kwa sababu hiyo huwa wanatamani kama wao


wanapata shida basi kila mtu apate shida. Kama wao
hawana furaha basi kila mtu asifurahi...Kama wao
wameshindwa kitu basi kila mtu ashindwe.

Haujawahi kumuona mtu anakuchukia Kwa sababu


ya ulivyo tofauti? Haujawahi kukutana na mtu
anakusema vibaya kwa sababu unaonekana una
furaha kila siku?

Au haujaona watu wanakutungia uzushi kwa chuki


tu kwa sababu umeamua kuwa mtu wa tofauti?

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 31


Hii ni gharama ambayo lazima uilipe katika safari
yako ya kuelekea kwenye kilele cha ndoto yako.

Kama unaogopa kuwa tofauti huwezi kufanya


mambo ya tofauti. Kuna wakati inabidi ukubali
kutokueleweka leo ili uelekeweke kesho.

Kuna watu wanaweza wasikuelewe leo ila


wakakuelewa kesho. Mtu mmoja aliwahi kusema
“Kama unataka kupendwa na kila mtu basi usiwe
kiongozi, nenda kauze ice-cream”.

Kwenye chochote unachotaka kuwa mbele na juu:


biashara, kipaji, siasa n.k, lazima ukubali
kutokueleweka na baadhi ya watu.

Sio kwa sababu wanakuchukia, bali ndio utaratibu


wa maisha ulivyo. Uko tayari kutokueleweka
unapofukuzia malengo yako?

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 32


Sio Lazima Kila Mtu Akuelewe

Kuna wakati unapoamua kufanya kitu


unachokipenda (Passion), watu wengine
hawatakuwelewa kwa sababu unakuwa unaona
hatima ambayo wao hawaioni. Unaona kesho
ambayo wao hawaioni, hata kama ukiwalazimisha
kuiona hawataiona.

Hii ndio maana kuna watu wanaweza kuona


unajitesa kwa kung’ang’ania kufanya kitu ambacho
wao wanahisi akina umuhimu.

Kuna maamuzi utayafanya na hawatakuelewa kwa


sababu mko kwenye ulimwengu wa aina mbili
tofauti kabisa. Kumbuka muziki ni wewe ndiye
unausikia na wao hawausikii.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 33


Hii ndio maana Friedrich Nietzsche akasema “Na
wale ambao walionekana wanacheza muziki,
walifikiriwa kuwa wamechanganyikiwa na wale
ambao walikuwa hawasikii sauti ya muziki” (And
those who were seen dancing were thought to be
insane by those who could not hear the music).

Kuna matukio kwenye maisha yako hautayaweza


kuyaelewa kwa haraka kama unavyotaka. Kuna
mambo ambayo huwa ni mafumbo kwa muda huo
na utayaelewa baada ya muda fulani kupita.

Hii ndio maana Steve Jobs aliwahi kusema “you


can't connect the dots looking forward; you can
only connect them looking backwards” (huwezi
kuunganisha matukio na kuyaelewa kwa kuangalia
mbele, unaweza kufanya hivyo kwa kuangalia
nyuma tu).

Kuna mambo ni magumu kuyaelewa kwa nini


yalitokea kwako, kuna watu ni ngumu kuwaelewa
kwa nini walifanya walichofanya, kuna vitu ni
ngumu kuelewa kwa nini ulipoteza.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 34


Ingekuwa ni uwezo wako ungetamani ubadilishe
majira ambapo mambo hayo yangetokea-
ungetamani pengine uyasogeze mbele zaidi ama
yangetokea wakati wa nyuma zaidi.

Kuna mambo hauwezi kuyabadilisha ila unaweza


kubadilisha mtazamo wako kuhusiana na mambo
hayo.

Badala ya kila siku kujilaumu kwa ulivyokosea


unaweza kuamua kujisamehe, badala ya kila siku
kuendelea kuchunguza na kutaka kuelewa kwa
undani fanya maamuzi ya kusogea hatua mbele,
badala ya kila siku kulia machozi kila unapokumbuka
dhamiria kupiga hatua zaidi.

Katika hali zote hizi kumbuka kuwa Mungu anaweza


kutumia matukio ambayo kwa macho ya kibinadamu
ni mabaya na yanaumiza akayafanya kuwa daraja la
kukupeleka unapopatamani. Usitafute sana kuelewa
bali tafuta sana kusogea.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 35


Lazima uilipe gharama ya kutokueleweka na
wengine unapoamua kuishi kwenye kile
unachokipenda.

Je, umeshawahi kutokueleweka na ndugu, rafiki,


mwezi, kazini n.k baada ya kuamua kuanza kuishi
passion yako?

JENGA KUJIAMINI KWAKO

Kuna watu wengi sana ambao kama wangeongeza


kiwango kidogo tu cha kujiamini, basi dunia
ingewashangaa sana. Yamkini wewe ni miongoni
mwao!

Hivi unajua kuna watu wana uwezo mdogo sana


kuliko wewe, ila wanafanya mambo makubwa kuliko
wewe? Na sababu ni kwamba wanajiamini kuliko
wewe!

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 36


Moja ya eneo unalotakiwa kujenga uwezo wako kwa
bidii ni kujiamini. Yamkini kwa kukosa kujiamini
unaogopa kumpigia mtu simu ambaye angekupeleka
hatua inayofuata. Una mawazo mazuri ila huyafanyii
kazi kwa sababu unogopa utafeli n.k

Njia ya kwanza kabisa unayoweza kuitumia kujenga


kujiamini, Ni kuamua kila siku kufanya jambo moja
unaloliogopa ila ni la muhimu.

Hii ndio maana mwandishi nguli Mark Twain aliwahi


kusema “Fanya lile unalolihofia, na hapo utaiua
hofu”. Kwamba (Do what you fear and the Death of
Fear Is Certain).

Kuna hatua leo ambayo unatakiwa kuichukua. Kila


siku umekuwa unaghairisha. Leo amua kumalizana
nayo kabisa.

Hofu haiondoki kwa kuikimbia ila inaondoka kwa


kuikabili. Face Your Fears Today. Nini huwa
unafanya unapogundua kuwa unakosa kujiamini na
ujasiri.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 37


Kama kuna eneo fulani la maisha yako unakosa
kujiamini na ujasiri, basi kuna kitu kingine cha ziada
unaweza kukifanya. Unachotakiwa kukifanya ni
kuamua kujenga uwezo kwenye eneo fulani ambalo
utajulikana kuwa uko bora zaidi.

Siku zote kumbuka kuwa kujiamini kwenye eneo


moja hujenga ujasiri kwenye eneo lingine. Hebu
rudia kusoma hii Sentesi hapo juu uelewe
nilichomaanisha, Hapo natumai umenielewa.

Ukipata eneo moja la maisha yako ambalo unaweza


kujenga uwezo wa hali ya juu sana na ikakupa hali
ya kujiamini itakusaidia kujiamini katika maeneo
mengine ya maisha yako pia.

Hii ndio maana unakuta mtu akifanikiwa kwenye


jambo moja au biashara moja huwa anapata ujasiri
wa kufanya na kingine pia.

Usipokuwa hata na kitu kimoja unachojiamini nacho,


kiukweli itakuwa ngumu kujiamini katika maeneo
mengine.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 38


Jaribu kujichunguza kama hakuna eneo hata moja
ambalo unajiamini kwa 100% kuwa uko vizuri sana.
Inabidi uweke mkakati wa kufanya hivyo leo.

Je, wewe binafsi ni eneo gani ambalo unataka


kujenga kujiamini kwako kwanza ili likusaidie
kujiamini kwenye maeneo mengine?

Jinsi Ya Kujenga Kujiamini Kwako

Simba huwa anaitwa mfalme wa nyika. Hata hivyo,


ukweli ni kuwa simba siye mnyama mzito zaidi,
kwani hata tembo anamzidi. Simba siye mrefu zaidi
kwani hata twiga anamzidi urefu.

Simba siye mnyama mwenye kasi zaidi, kwani


wakati cheetah anaweza kufikia kasi ya 113 Km kwa
saa Simba hapo atafikia 81 Km kwa saa.

Nini kinamfanya Simba aitwe na awe mfalme wa


pori? Kitu kitakachokusaidia kujenga kujiamini na
kuwa na ujasiri ni kubadilisha unavyojiona.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 39


Usisubiri uwe mrefu kama Twiga ila ujithamini,
usisubiri uwe mzito kama Tembo ili uamini kwenye
uwezo wako n.k Badilisha mtazamo wako leo.

Usisubiri uwe na “connection” kubwa kama


wengine, usiishi kwa kutamani uwe na elimu kubwa
kama wengine, usiendelee kuzungumzia kama
ungekuwa na kipaji kama wengine n.k Wewe una
nini?

Jifunze kwa Simba na utumie ulichonacho kwa


kujiamini, utashangaa unakuwa mfalme wa Nyika
kwenye eneo lako.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 40


SURA YA TANO

TIBA YA DESTINY DISEASE

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 41


Umeshawahi kuusikia ugonjwa unaitwa “Destination
Disease”? Dalili kubwa ya ugonjwa huu ni pale mtu
anapoanza kusema mambo kama; nikipata cheo
fulani nitaanza kufurahia maisha, siku nikiwa na
kipato cha kiwango fulani nitaanza kuenjoy sanaa,
siku nikimpata mtu fulani ndio furaha yangu itakuwa
kamili n.k

Kwa ufupi ni kuwa watu wenye “Destination


Disease” huwa wanaamini kuwa furaha yao ya kweli
itakamilika pale ambapo watapa vitu au mtu ambaye
kwa sasa bado hawajapata.

Matokeo ya fikra hii ni kuwa kila siku wanaendea


kukimbizana na furaha ambayo wanaweza wasiipate
maisha yao yote.

Hata leo kuna mtu ameamka na ameanza kulalamika


na kunung’unika kwa sababu hana kitu
anachotamani na hicho kinamkosesha furaha
kabisa.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 42


Kuna tiba za aina mbili kuhusiana na jambo hili:

Moja ni kujizoeza kuwa na moyo wa SHUKRANI


(grateful heart). Hii inaanza pale ambapo kwa
makusudi kabisa kila siku unapoamka unatafuta kitu
cha kumshukuru Mungu.

Inaweza kuwa uhai wako, afya yako au kitu chema


ambacho umewahi kupata kwenye maisha yako.
Hakuna mtu ambaye hana kitu cha kumshukuru
mungu-badala ya kulalamika kwa usichonacho kwa
nini leo usianze siku kwa kutafuta kitu kimoja cha
kumshukuru mungu?

Tiba ya pili ni kuwa usiache furaha yako ishikiliwe


na kitu au mtu-fanya maamuzi ya kuimiliki 100%.
Watu wenye furaha duniani sio kwa sababu wana
kila kitu ila ni kwa sababu furaha yao haishikiliwi nje
yao.

Kwa mujibu wa Jack Carnfield, 90% ya furaha


maishani inatokana na mtazamo wako na 10% ndio
inatokana na watu na matukio.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 43


Mtu yoyote anayeweza kutawala furaha yako ina
maana ameweza kutawala maisha yako. Furaha
yako ijengwe katika uhakika wa ndani kuwa kesho
yako inang’aa kuliko jana yako.

Je, leo utaruhusu kutokuwa na kitu fulani au mtu


aibe furaha yako?

JINSI YA KUISHINDA HOFU YAKO

Jia Jiang ni mjasiriamali na mfanyabiashara ambaye


akiwa na umri mdogo alikutana na changamoto
nyingi za maisha. Akiwa na Miaka 6 alipitia hali ya
kukataliwa darasani kwake.

Hata alipokuwa mkubwa aligundua kuwa hofu ile


imekuwa ni chanzo cha yeye kutofanya mambo
makubwa kwenye maisha.

Kwani kila anapofikiria kufanya kitu huwa anakuwa


na hofu ya watu kumkataa (fear of rejection) na
kumwambia hapana.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 44


Yamkini na wewe unayo hii hofu, pole. Ili kuiondoa
hofu hii Jia Jiang aliamua kuanza safari ya siku 100
kufanya vitu atakavyoambiwa hapana (100 Days of
Rejection).

Yaani alikusudia moyoni mwake kwa dhati yote


kwamba kwenye kila siku atafute kufanya au
kuomba kitu ambacho ataambiwa hapana.

Nia yake ilikuwa ni kwamba, kama ataweza


kuambiwa hapana kwa siku 100 mfululizo basi
mwisho wa siku atazoea na hofu ya kukataliwa
itaisha. Unahisi nini kilitokea?

Jia Jiang anasema haikuwa rahisi hata kidogo


kuzipata HAPANA 100.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 45


Kwa nini?

Kwa sababu hata yale mambo ambayo alikuwa


anafikiri watu watasema Hapana kwa haraka,
alishangaa WANAMKUBALIA.Kiukweli Jia Jiang
alistaajabu sana.

Somo kubwa alilolipata anasema “Niligundua kuwa


kuna mambo ambayo tunahitimisha kuwa watu
watasema hapana na nilipojaribu walisema ndio,
kumbe mara nyingi tunajizibia mafanikio wenyewe”

Na wewe leo kabla haujajiambia mwenyewe hapana.


Jaribu kwanza kufanya. Leo utajaribu nini?

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 46


UNAIFAHAMU “THE EDSON METHOD”?

Moja ya kitu cha ajabu sana ambacho mvumbuzi


mkubwa wa kisayansi Thomas Edson alikuwa
anakifanya mara kwa mara ni kuwa, pale alipokuwa
anapata wazo basi alikuwa anaitisha waandishi wa
habari kisha anatangaza wazo lake na ana ahidi lini
atalitekeleza.

Akimaliza alikuwa anaenda kujifungia maabara ili


aanze kulitekeleza hadi litakapofanikiwa.

Alipokuwa anaulizwa kwa nini anafanya hivyo


alisema “watu wengi wanashindwa kufanya kwa
sababu hakuna kitu kinachowasukuma kutimiza
walichoahidi, kwangu mimi kutangaza kunanipa
nguvu ya kufanya juhudi ili nitimize nilichoahidi na
sitaki kuaibika”.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 47


Nguvu ya kufanikisha lengo ulilonalo iko kwenye
commitment yako ya kufanya ulichosema. Hii ndio
maana mwandishi maarufu Mark Twain aliwahi
kusema “The secret of getting ahead is getting
started” (Siri ya kusonga mbele ni kuanza).

Kanuni ya Thomas Edson ina pande mbili muhimu:


Moja ni kujiwekea mfumo wa uwajibikaji
unaokusaidia.

Hapa swali la muhimu ni-hivi nani anakuwajibisha


usipotekeleza ulichosema? Utajisikia vibaya au
utaona ni kawaida tu?

Jambo la pili linakutaka kuingia maabara ili


ulichokisema kiwe halisi. Hii inamaanisha kutumia
muda wako mwingi na kuwekeza fedha zako katika
kile ulichoamua kukifanya na kuachana na mambo
mengine yote.

Je, wewe ungeita waandishi wa habari mwaka huu


unatuahidi kufanya nini?

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 48


JIVIKE UJASIRI WA KUKABILIANA NA
HATARI: USIZIZIKIMBIE

William Get aliwahi kusema “A ship in harbor is safe


but that is not what ships are built for” (Meli ikiwa
ufukweni iko salama, lakini meli haijatengenezwa
kwa ajili ya kukaa ufukweni).

Kwenye maisha ukiishi kwa kuepuka hatari badala


ya kutafuta kufanya unachotakiwa utabakia kuwa
mtu wa kawaida.

Watu wanaofanya mambo makubwa duniani ni wale


ambao wakikutana na changamoto kubwa sana
kwenye maisha yao badala ya kuzikimbia
wanazitumia kama na hivyo thamani yako
haitakuwepo.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 49


Wewe mwenyewe unajua hatua ambazo unatakiwa
kuchuka ila unaogopa mawimbi na unaendelea
kukaa ufukweni, unajua kabisa maamuzi
unayotakiwa kuchukua na unachelewa kwa sababu
unaogopa ngazi ya kufika wanakotaka kwenda.

Moja ya sababu inayoua uwezo wa wengi na ndoto


zao kufeli ni pale wanapoamua kukaa “ufukweni” ili
kuepuka mawimbi na hatari ya kuzama.

Tatizo ni kuwa ukibakia hapo hakuna mtu


atakayeona umuhimu wako mawimbi, unajua watu
unaotakiwa kuachana nao haraka kabla mambo
hayajaharibika ila unaogopa mawimbi n.k

Kumbuka hauwezi kufanya mambo makubwa zaidi


ya uliyofanya sasa kama utaendelea kubakia
ufukweni na kuogopa kuingia baharini. Ifanye leo ni
siku yako ya kutoka ufukweni kwa kuchukua hatua
inayostahili.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 50


Kumbuka kuwa mambo mengi unayoogopa kufanya
kwa kuhofia matokeo yatakuwa mabaya ndio
yanabeba mafanikio yako.

Uko tayari kutoka ufukweni na kukabiliana na


mawimbi kwa ajili ya ndoto yako kubwa? Nakutakia
mafanikio makubwa.

Kumbuka wewe ni meli na thamani yako inaonekana


unapoanza kufanya safari na sio unapoegeshwa
bandarini.

Tuanze safari leo.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 51


SURA YA SITA

NYAKATI TATU
ZITAKAZOKUTOFAUTISHA

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 52


Kuna nyakati kubwa tatu ambazo zinatofautisha
maisha ya mtu mmoja na mwingine katika kwenye
mafanikio yao. Uwezo wako wa kukabiliana na
nyakati hizi na kupita salama ndio itajulisha utafika
mbali kiasi gani:

1) Wakati wa ukimya (Moment of silence)

Huu ni wakati ambao nguvu zako zitakuwa


hazilingani na matokeo unayoyapata. Wakati huu
hutokea kwa sababu ni wakati wa mbegu kukusanya
nguvu ya kuchipua.

Ni kama vile ukianza kufanya mazoezi kwa ajili ya


kujenga misuli, inaweza kupita wiki kadhaa bila
kuona matokeo ila haimaanishi hakuna
kinachotokea.

Kama wewe ni mkulima mbegu ikiwa haijaota


haimaanishi imekufa, unatakiwa uendelee
kuimwagilia maji hata kama hakuna unachokiona
kwa juu.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 53


Kuna wakati utapitia wakati huu wa ndoto yako:
usiache kufanya kwa sababu hakuna unachokiona.

2) Wakati wa watu kutoamini ndoto yako (Moment


of public unbelief)

Kuna wakati kila mtu ataonekana kuwa na shaka na


ndoto yako. Ingawa wewe mwenyewe utakuwa na
uhakika kuwa unachofanya ni kitu
kitakachofanikiwa na unaona mbele mambo
yatakuwa mazuri; utashangaa kuona kila
anayekuzunguka haamini katika unachofanya.

Cha ajabu ni kuwa wewe utakuwa unaona wazi


kabisa inawezekana, na itakupa shida kwa nini
wengine hawaoni na kuamini kama wewe. Usiache
kwa sababu wengine hawaamini: kumbuka sio ndoto
yao ni ndoto yako.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 54


3) Wakati wa kuchoka (Moment of exhaustion).

Kuna wakati utafika nguvu ambazo ulikuwa nazo za


kupambania ndoto yako hautakuwa nazo tena,
itakuwa kama vile umepoteza kabisa munkari wa
kupambana.

Itafika sehemu utakuwa kama uko tayari kila


ulichoanza kipotee na uanze kitu kipya kwa sababu
hauna nguvu za kuendelea.

Kumbuka haufanikiwi kwa sababu unajisikia una


nguvu za kufanya, utafanikiwa kwa kujilazimisha
kuendelea hata kama haujisikii. Leo jilazimishe.

Je, kuna hatua yoyote kati ya hizi unaipitia leo katika


safari ya kuelekea kutimiza ndoto yako? Songa
mbele.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 55


UWE TAYARI KUSUBIRI WAKATI WAKO

Ujumbe wa kwanza ulitoka kwa Mc “sasa tumeona


muda umeenda sana, badala ya dakika 60
tutaomba uongee kwa nusu saa” nikamwambia
sawa.

Baada ya dakika chache nikapewa kikaratasi


“Samahani, tunaomba ufupishe uzungumze kwa
dakika 10 manake wakuu wengine bado
hawajaongea” Nikajibu sawa, nitafanya hivyo.

Kama dakika 10 zimepita nikaona muandaaji anakuja


akaniambia “Samahani sana Joel, tumeona
tucancel presentation yako kwani muda hautoshi
kabisa”-Nikavuta pumzi, nikamwambia sawa.

Nilijiandaa kwelikweli kwa ajili ya hii siku. Nilitumia


masaa mengi na isitoshe hawakuwa wananilipa
chochote. Nilijigharamia nauli na kila kitu.
ILINIUMIZA ila HAIKUNIKATISHA tamaa.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 56


Hii ilikuwa mwaka 2009. Baada ya miaka mitatu
kupita, watu walewale walinitafuta na kunilipa pesa
tena kwenye ratiba nikawekwa wa kwanza kuongea.

Kuna wakati watu hawataona thamani yako. Sio kwa


sababu hawakupendi au wanakinyongo na wewe
bali muda wako haujafika.

Wengi wakipitia hatua hii wanaamua kususa na


kuacha kunoa uwezo wao. Usipokata tamaa, wale
wasiokuthamini leo, kesho watakutafuta

-Stay Strong.
Umeshawahi kupitia hali inayofanana na hii?

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 57


USIKUBALI KUWA DNF (Did Not Finish)
KAMA DEREK

Kwenye mashindano ya Olimpiki ya Mwaka 1992


yaliyofanyika Barcelona mmoja wa washiriki alikuwa
ni Derek Redmond.

Baada ya kushindwa kuwakilisha taifa lake la


Marekani miaka 4 nyuma kwenye Olimpiki
Iiliyofanyika Korea, Seoul, wakati huu alikusudia
kushinda medali ya dhahabu iliyokuwa ndoto yake
ya siku zote.

Katika round mbili za kwanza alikuwa ameongoza na


sasa alikuwa hatua ya nusu fainali. Mita chache
baada ya kukimbia na akiwa amebakiza mita 100
alipata maumimivu ya kukatika kwa msuli nyuma ya
paja (Hamstring injury). Anasema yalikuwa makali
kama vile amechomwa kisu kikali.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 58


Ingawa alikuwa na sababu ya kutoendelea lakini
anasema alipokumbuka mashindano yaliyopita ya
korea alijiandaa vizuri lakini alishindwa kukimbia kwa
sababu ya maumivu na kwenye jina lake liliandikwa
DNS (Did Not Start),

Hakuanza kukimbia. Na safari hii alijua kuwa


asipomaliza jina lake litaandikwa (DNF-Did Not
Finish), kwamba Hakumaliza, na yeye hakutaka hilo.

Alijilazimisha kuendelea huku analia kwa maumivu


na alikataa hata ushauri wa wasimamizi wa
mashindano kuwa aache kwani alikuwa hataki kuwa
“DNF” wa mwaka 1992.

Baba yake alipoona mwanawe anateseka alienda


kumuomba aache ili apewe matibabu lakini Derik
akakataa ndipo Baba yake alipoamua kumsaidia kwa
kumshika na kutembea naye hadi mwisho wa
mstari.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 59


Alimaliza mbele ya mashabiki 65,000 na
alishangiliwa na anakumbukwa kuliko Steven Lewis
aliyeshinda siku ile.

Kuna mambo unatamani kuyafanya mwaka huu?


Kuna kitu unatakiwa kukikamilisha leo? Ni kweli
unasikia maumivu, ni kweli kuna watu hadi
wanakuonea huruma wanaona kama unajitesa na
una kila sababu ya kuachia njiani.

Wewe ndiye unayejua unachokitaka katikati ya


maumivu unayosikia. Kitu muhimu zaidi usikubali
kuwa katika orodha ya “DNF-Do Not Finish; ya
mwaka 2020

Je, uko tayari kuwa Derik unapoanza siku yako leo?

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 60


SURA YA SABA

AINA MOJAWAPO YA WATU


HATARI ZAIDI UNAOTAKIWA
KUWAEPUKA

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 61


Wakati nafundishwa somo la uongozi, Mwalimu
wangu alituchambulia aina kumi za watu ambao
huwa ni kikwazo katika kumfanya kiongozi/mtu
mwenye maono kufikia malengo yake.

Katika aina hizo moja ya aina yenye matatizo zaidi ni


ile inayoitwa “Problem perceivers”. Aina hii ya watu
ni wale wanao ona tatizo katika suluhisho. Sifa yao
kubwa ni kukuonyesha matatizo bila kukupa
suluhisho lolote.

Ukizungukwa na watu wa namna hii; kila siku


utajiona wewe una udhaifu mkubwa sana na
wazo/ndoto yako haitafanikiwa kabisa.

Watu hawa huwa wana nguvu kubwa sana ya


kuchambua na kuyaelezea matatizo na hatari
zinazoweza kukutokea ila hawana nguvu kabisa ya
kukushauri njia mbadala.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 62


John Henry Newman aliwahi kusema kuwa “hakuna
kitu kingefanyika duniani kama kila mtu angesubiri
hadi awe na uwezo wa kufanya kitu hicho katika
namna nzuri sana ambayo asingepata mkosoaji.
(Nothing would get done at all if a man waited until
he could do something so well than no one could
find fault with it).

Changamoto kubwa ya “Problem perceivers”


watakuogopesha kuanza kufanya au kuendelea
unachofanya kwani kila wakati watataka
kukuonyesha upungufu, madhaifu na
kutokuwezekana.

Kumbuka kitu muhimu sio kutokukosea katika


unachofanya bali ni kujifunza kwa haraka makosa
yako unapokosolewa na pale unapoona unahitaji
kujirekebisha unafanya hivyo kwa haraka.

Ila usiache kufanya kwa kuwaogopa “Problem


perceivers” hawataisha!

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 63


Umeshawahi kukutana nao? Akiongea tena leo
mwambie “Nimekushtukia”

USIOGOPE KUKATALIWA

Hofu ya kukataliwa (Fear of rejection) imeua uwezo


wa watu wengi sana duniani. Kuna watu wana vipaji
vikubwa sana ila kitu pekee kinachowafanya wawe
wa kawaida ni hofu ya kukataliwa.

Kuna watu wana mawazo ambayo kama


wangechukua hatua yangebadilisha maisha yao,
kinachowakwamisha ni hofu ya kukataliwa, kuna
wengine kila siku wanaghairisha kufanya ila
ukichunguza kwa ndani kinachosababisha ni hofu ya
kukataliwa n.k

Wapo ambao hofu hii imejengwa ndani yao kwa


sababu ya yale ambayo walipitia hapo kabla, kuna
ambao wakikataliwa na Baba yao.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 64


Kuna wengine walikataliwa na watu waliowapenda
sana, kuna wengine walitengwa na marafiki kwa
sababu ya udhaifu wao fulani n.k

Wapo pia ambao hofu hii imejengwa kutokana na


yale wanayoyashuhudia yakiwatokea wengine.
Wamewahi kuona wengine wakikataliwa walipojaribu
kufanya kama wao, na wanaogopa maumivu ya
kukataliwa.

Usiruhusu hofu ya kukataliwa iue ndoto yako: hata


kama unasikia maumivu makali, kumbuka kila
unapokataliwa unazidi kusogea hatua kwenye
maisha yako:

1) Mungu huwa anaitumia njia hii kukuepusha na


mabaya ya mbeleni ambayo huwezi kuyaona sasa
hivi ila baadaye utakuja kumshukuru.

2) Inakufundisha unyenyekevu ili utakapokuja


kufanikiwa usiwe na kiburi na majivuno na usidharau
wengine.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 65


3) Maumivu unayoyasikia yanakusaidia kuwa makini
(sensitive) unaposhughulika na wengine ili
usiwaumize kwani unajua madhara yake.

4) Inakupa njia bora ya kufanya. unalazimika


kupandisha viwango. kama usingetaliwa
ungebweteka na ungebakia wa kawaida.

5) Inakufanya ubadilishe mwelekeo kwa lazima


ambao katika hali ya kawaida usingekuwa tayari.
Mwishoni unakuja kugundua mwelekeo wako mpya
ndio sahihi zaidi.

Leo unapoanza siku yako usiache kufanya


unachotakiwa kufanya kwa hofu ya kukataliwa.
kwenye kila kukataliwa kuna faida imejificha.

Badala ya kuogopa maumivu utakayopata, ogopa


fursa utakazokosa kama hautafanya.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 66


HITIMISHO

Mafanikio ni safari ya kila siku, ambayo mtu anaiishi


mpaka siku ya kufa kwake. Yako mengi
yanayotusonga ndio maana sio kila mtu
anafanikiwa. Lakini ni wajibu wa kila mtu kufanikiwa.

Asante kwa kukisoma kitabu hiki mpaka mwisho.


Hakuna maana ya kuandika kama hakuna msomaji.
Naamini kitabu hiki kimefanyika daraja kukuvusha
kimtazamo na kimatendo.

Usiogope kuthubutu. Ishinde hofu yako, chukua


hatua ya kiujasiri. Ushuhuda wako ni wa muhimu
sana kwangu. Usisite kuniandikia.

See you at the Top!!

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 67


KUHUSU MWANDISHI

Joel Arthur Nanauka ni mwalimu anayefundisha


sayansi ya maisha, kijana mwenye ushawishi
mkubwa juu ya maendeleo kibinafsi, mkufunzi wa
mashirika na mwandishi wa vitabu Zaidi ya 20 vya
Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 68


Amepata elimu yake rasmi kwenye chuo kikuu cha
Dar es Salaam katika masomo ya Biashara na
Uongozi,Commerce and Management) na pia katika
Diplomasia yaUchumi (Economic Diplomacy) Kutoka
katika chuo cha Diplomasia (Centre for Foreign
Relations - CFR)

Joel amejikita kuwasaidia watu kuwa na matokeo


makubwa katika wanachokifanya (peak
performance trainings) na kushinda vikwazo
ambavyo vimeaathiri watu wengi.

Anatoa mafunzo kwa makampuni mbalimbali na


watu binafsi wanaotaka kutimiza malengo yao ya
kibiashara na kitaaluma kupitia program maalumu
ya malezi (Mentoring and Coaching).

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 69


Amewahi kuwa mshauri wa kibiashara kwa
wajasiriamali wanawake kupitia program ya Graca
Machel Trust (GMT), Mshauri na mlezi wa Africa
Entrepreneurship Award (Tuzo za wajasiriamali
vijana Africa), Mshauri na mkufunzi wa kibiashara na
kiuongozi kwa vyombo vya habari Tanzania bara na
visiwani kupitia Tanzania Media Foundation.

Pia amewahi kufanya kazi kama mwajiriwa wa


Umoja wa Mataifa kupitia shirika la UNESCO
linalojishughulisha na elimu, sayansi, teknolojia na
utamaduni.

Alitambuliwa na kampuni ya Avance Media yenye


makao yake makuu nchini Ghana kama kijana
mwenye ushawishi zaidi nchini Tanzania katika eneo
la kutoa Elimu ya Maisha na Uandishi (Personal
Development and Academia) kwa mwaka
2019/2020.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 70


Amewahi pia kutambuliwa kama kiongozi bora kijana
wa dunia katika kongamano la kimataifa nchini
Taiwani - China mwaka 2012 .

Pia amewahi kuwa mwanafunzi bora wa kitaifa


kidato cha nne na mwanafunzi bora katika masomo
ya Diplomasia ya Uchumi.

Mwaka 2020 pia Joel Nanauka ametambuliwa na


kampuni ya Avance Media yenye makao yake makuu
nchini Ghana kuwa miongoni mwa vijana 100 wenye
ushawishi mkubwa barani Afrika katika eneo la
kutoa elimu ya maisha na uwandishi yaani (Personal
Development and Academia)

Ameandika zaidi ya vitabu 22 vilivyoweza


kubadilisha maisha ya watu katika nchi mbalimbali
Duniani.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 71


Joel, ni mkurugenzi wa taasisi ya Africa Success
Academy inayojishughulisha na kutoa mafunzo kwa
taasisi mbalimbali, wajasiriamali, wanawake na
vijana walioko vyuoni na mashuleni ili kuwajengea
uwezo.

Joel amemuoa Rachel na wamebarikiwa watoto


wawili, Joyous na Joyceline.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 72


VITABU VINGINE VILIVYOANDIKWA NA JOEL
ARTHUR NANAUKA.

HARDCOPY (Nakala ngumu)

1. Timiza Malengo Yako (Mbinu 60 walizotumia


watu maarufu kufanikiwa)
2. Ishi Ndoto Yako (Siku 30 za kuishi maisha
unayotamani)
3. Tabia 12 Zinazoleta Mafanikio.
4. Ishinde Tabia Ya Kughairisha Mambo.
5. Ongeza Kipato Chako (Maarifa juu ya fedha,
Biashara na uwekezaji)
6. Nguvu Ya Mwanamke.
7. Mbinu Za Kufanikisha Ndoto Katikati Ya
Changamoto.
8. How To Pass Your Exams With Ease.
9. Uzalendo Na Ujenzi Wa Taifa.
10. Ufanisi Kazini
11. Boresha Mahusiano Yako.
12. Money Formula Core Genius

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 73


eBooks / SOFTCOPY (Nakala laini).

1. Money Formula (Elimu ya fedha isiyofundishwa


shuleni)
2. Hatua Sita Za Kujiajri
3. Muongozo Wa Mafanikio
4. Core Genius (Jinsi ya kugundua uwezo wako wa
kipekee)
5. Jinsi Ya Kufanikiwa Katikati Ya Nyakati
Ngumu.
6. Saikolojia Ya Mteja
7. Mbinu Za Kujenga Ujasiri Na Kujiamini.
8. Surviving The Crisis.
9. Namna Ya Kuondokana Na Madeni
10. Uzalendo Na Ujenzi Wa Nchi.
11. Mbinu Za Kuongeza Kipato.
12. Strategy 2021, Siri Za Kupata Matokeo
Makubwa Ndani Ya Mwaka Mmoja.
13. Nifanye Biashara Gani?
14. Marafiki.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 74


Kozi Alizoziandaa, Unaweza Kuzisoma Online.

1. Mbinu Za Kuuza Zaidi.


2. Jinsi Ya Kujenga Kipato Cha Uhakika Kwa
Kujiajiri.
3. Jinsi Ya Kuondokana Na Madeni.

Kupata kozi hizi wasiliana nasi


Whatsapp: 0762 312 117

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 75


TEMBELEA MITANDAO YA KIJAMII YA JOEL
NANAUKA.

YOUTUBE: Joel Nanauka (Utapata VIDEO nyingi za


kukufundisha mambo mbalimbali)

Instagram: joelnanauka_ (Utapata mafunzo kila


siku yatakayokusaidia kupiga hatua katika maisha)

Facebook: Joel Nanauka page (Utapata mafunzo


kila siku na pia shuhuda mbalimbali za watu
walionufaika na mafunzo)

Twitter: jnanauka.

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 76


Unaweza kupata vitabu vingine vilivyoandikwa na
JOEL NANAUKA kutoka TIMIZA MALENGO
BOOKSHOP tunapatikana Njia Panda Chuo Kikuu
Ubungo, wasiliana nasi kwa namba zifuatazo.

Instagram: timizamalengo_bookshop

Simu: 0745 252 670


0756 094 875 au 0683 052 686

Jinsi ya Kuishinda Hofu ya Kuanza | Joel Arthur Nanauka | 77

You might also like