You are on page 1of 43

MAISHA YANAYOACHA ALAMA ISIYOFUTIKA

Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

© Oktoba 2023 by Adriano Mkonda

Simu: +255 656 189 370, +255 621 618 821


Barua pepe: mkondaadriano10@gmail.com

Haki zote zimehifadhiwa. Huruhusiwi kuiga, kunakili, kupiga


chapa, kutafsiri au kutoa sehemu yoyote ya kitabu hiki kwa
njia yoyote bila idhini ya mwandishi.

Kimeandaliwa na;

DIVINE TRANSFORMATION GLOBAL (DITRA Global)


Simu: +255 656 189 370
Barua pepe: ditraglobaltz@gmail.com
Facebook: Ditra Global Tanzania,
Instagram: ditra_global
WhatsApp link: https://wa.me/message/WSSND7DQJGVCO1

Isipokuwa imeelekezwa, maandiko yote yamenukuliwa kutoka


katika Maandiko Matakatifu ya Mungu yaitwayo Biblia yaani agano
la kale na jipya, tolea la Swahili Union Version (SUV) © Bible Society
of Tanzania 1997.
Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika

YALIYOMO

Nasaha Za Wasomaji ............................................................................1


TABARUKU ..............................................................................................3
SHUKRANI................................................................................................4
UTANGULIZI............................................................................................5
Wewe Ni Kiumbe Wa Milele .............................................................8
Kukielewa Kifo .................................................................................... 17
Funguo 5 Kuelekea Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
................................................................................................................... 25
Anza Leo Kuacha Alama Isiyofutika ............................................ 34
Maalumu Kwa Ajili Yako.................................................................. 35
MAREJEO ............................................................................................... 37
Vitabu Vingine ..................................................................................... 38

DITRA Global || +255 656 189 370 ii


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

Nasaha Za Wasomaji

Nimefanikiwa kusoma kitabu kiitwacho Kurejesha Njaa Ya


Kiroho. Kupitia kitabu hiki binafsi nimeongezeka katika usomaji
wa Neno la Mungu, maombi na kwa ujumla usomaji wa vitabu.
Zaidi ya yote nimeweza kuliambukiza kanisa la Kristo maarifa
ambayo nimeyapata. Ninashuhudia namna kanisa
linavyobadilika na kuwa na njaa ya ibada, Maombi, Neno n.k.
Hakika Mungu ambariki sana mwalimu Adriano Mkonda kwa
kuwa sababu ya wengi kufikiwa na maarifa haya.

Mchungaji David Deogratius Majula


Mchungaji kiongozi, kanisa la Beroya Christian Mission
Center Mpere-TAG- Pwani Tanzania

Nimesoma vitabu viwili hadi sasa, Nguvu Ya Kuanza na


Ulimwengu Wa Mitandao. Kiukweli kupitia vitabu hivi
nimefunguliwa kifikra na nimetolewa katika usingizi mzito wa
kimaarifa. Sijutii kuifahamu DITRA Global.

Noah Erasto
Lindi-Tanzania

Shalom, Nimebarikiwa kusoma kitabu kiitwacho Kurejesha


Njaa Ya Kiroho. Mungu akubariki sana mwalimu Adriano
Mkonda.

Mchungaji Joshua
Burundi-East Afrika

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 1


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika

Nimesoma vitabu kadhaa vya mwalimu Adriano Mkonda, lakini


Sayansi Ya Kipaji ni kitabu changu pendwa, kimenigusa na
kunibadilisha zaidi. Kwa ujumla, vitabu hivi vinatia moyo,
vinakufanya uwe jasiri, vinakupa mbinu mbadala za maisha na
zaidi vinakusogeza karibu na Mungu. Mbarikiwe sana waandaji
wa vitabu hivi.

Daniel Emmanuel
Dar es Salaam-Tanzania

Mungu akubariki sana mwalimu na mwandishi Adriano Mkonda


kwa kazi unayoifanya ya kuelimisha watu kupitia vitabu vyako.
Nimesoma kitabu chako cha Mambo Yasiyo Ya Kawaida
Kupitia Watu Wa Kawaida. Hakika kitabu hiki kimenipa
maarifa mapya, naam tangu sasa mimi si mtu wa kawaida.
Asante sana.

Philipo Phlemon
Dodoma-Tanzania

DITRA Global || +255 656 189 370 2


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

TABARUKU

Kwa kila nafsi ya mwanadamu ya mahali popote, iliyopewa


nafasi ya kuishi duniani. Kitabu hiki kiwe fursa ya kila
mmoja wetu kuyaelewa maisha katika upana wake. Maisha
yanayoacha alama isiyofutika.

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 3


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika

SHUKRANI

Shukrani kwa;

Mungu kwa kunijalia kuandika kitabu hiki. Utukufu wote


anastahili yeye.

Walezi wangu wa kimwili (kwa nyakati mbalimbali), Kwa


malezi yao.

Askofu Agnell Mguluka na Mama Askofu Agness Mguluka,


kwa malezi yao ya kiroho na kihuduma.

Wanafamilia wote wa DIVINE TRANSFORMATION GLOBAL


(DITRA Global) ambao walikubali kujifunza mafundisho
haya kupitia mitandao yetu ya kijamii. Hawa wamekuwa
sababisho kuu la uandishi wa kitabu hiki.

Rafiki yangu na mtenda kazi pamoja nami, Deogratius Evord


kwa kuandaa jalada la kitabu hiki.

Mchungaji David Deogratius Majula, Noah Erasto, Daniel


Emmanuel, Philipo Phlemon na mchungaji Joshua kutoka
Burundi kwa nasaha zao. Mungu awabariki.

Wewe msomaji, kwa kuchagua kuungana nami ili


kukamilisha makusudi ya uwepo na uandishi wa kitabu hiki.

NINAWAPENDA WOTE

DITRA Global || +255 656 189 370 4


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

UTANGULIZI

Alama Isiyofutika

H ebu nianze kwa kuuliza maswali yafuatayo ambayo ni


ya muhimu sana katika kukielewa kitabu hiki. Swali la
kwanza, Je! Katika mwili wako una kovu lolote (pasipo kujali
chanzo chake) ambalo halijawahi kufutika? (Chukua
sekunde chache kujichunguza).

Swali la pili, Je! Unamjua mtu yeyote ambaye ana kovu


mahali popote katika mwili wake (pasipo kujali chanzo cha
kovu hilo) na halijawahi kufutika?

Bila shaka utakuwa na majibu ya maswali haya. Kovu la


namna hiyo ni mfano wa alama isiyofutika. Pengine
utajiuliza alama isiyofutika ni nini? Haya hapa majibu….

Alama isiyofutika ni kitu chochote ambacho hakiwezi


kuondoka mahali kilipo hata kama nguvu kubwa kiasi
gani itatumika kukuiondoa.
Ni alama ya kudumu (a permanent mark)

Maisha yanayoacha alama isiyofutika…

Kama kilivyo kichwa chake, kitabu hiki kinahusu maisha


yanayoacha alama isiyofutika. Kwa ujumla tunaweza
kusema maisha yanayoacha alama isiyofutika…

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 5


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
Ni maisha ya mtu yanayowapa watu wengine kitu cha
thamani ambacho kitawafanya wasimshau wakati wote.
Ni maisha ya mtu yanayowapa watu wengine kitu cha
kufuata hata kama yeye mwenyewe hatakuwepo katika
mazingira husika.
Ni maisha yanayokupa tiketi ya kuendelea kuwepo
mahali fulani hata kama katika uhalisia haupo.
Ni maisha yanayokupa tiketi ya kuendelea kuishi hata
baada ya kifo chako.
Ni kuishi zaidi ya kifo chako.

“Maisha yanayoacha alama isiyofutika ni


sawa na kovu ambalo haliwezi kuondoka
mwilini mwa mtu haijalishi umri wake.”

Ngazi Kuu Mbili

Kama utazichunguza vema maana hizi utagundua kuwa


kuna ngazi kuu mbili za kuacha alama katika maisha. Ngazi
ya kimazingira na ngazi ya kiuhai.

Ngazi ya kimazingira ni pale mtu anapoacha alama


isiyofutika katika eneo fulani alilowahi kuishi kwa kipindi
fulani na baadaye akaondoka. Ipo mifano mingi sana ya watu
ambao waliishi katika mazingira fulani na kamwe hatuwezi
kuwasahau kwa alama walizoziacha katika mazingira hayo.

Ngazi kiuhai ni pale mtu anapoacha alama isiyofutika katika


ulimwengu wake kwa ujumla baada ya kifo chake. Ni alama
inayoanza kuonekana baada ya mtu kufa. Ni maisha ya mtu
baada ya kifo chake.
DITRA Global || +255 656 189 370 6
Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

Una fursa ya kuishi zaidi…

Kitabu hiki kitajikita hasa katika ngazi ya pili ya kuacha


alama, ngazi ya kiuhai. Kupitia kitabu hiki utafahamu kuwa
kuna fursa ya wewe kuishi hata baada ya kifo chako kama tu
utaishi ipasavyo kama kitabu hiki kinavyoeleza.

Nikutie moyo kwamba haujakosea kuchagua kusoma kitabu


hiki, bali umechagua kujifunza kanuni zitakazokusaidia
kuwa mtu utakayeacha alama zisizofutika karibu kila mahali
utapokanyaga unyayo wako wakati wa uhai wako.

Na zaidi sana kanuni utakazojifunza zitakusaidia kuacha


alama zitakazokufanya usisahaurike hata baada ya kifo
chako. Utaishi zaidi ya mipaka ya uhai wako, utaishi zaidi ya
kaburi lako, utaishi zaidi ya kifo chako.

Karibu sana na endelea pamoja nami hata mwisho katika


kujifunza maisha yanayoacha alama isiyofutika.

Nimekuombea

Adriano Mkonda

Oktoba 2023

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 7


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika

Wewe Ni Kiumbe Wa Milele

“Tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi
mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu
anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.”
-Mhubiri 3:11

W ewe ni kuimbe wa milele, je! Hii ina maana gani? Ni


imani yangu kwamba swali hili muhimu tayari
limeuchukua ufahamu wako baada tu ya kukisoma kichwa
cha sura hii.

Ndiyo wewe ni kiumbe wa milele, na sura hii ina upana wa


jibu hili. Tuendelee pamoja na hadi kufikia mwisho wa sura
hii ni imani yangu kwamba kuna kitu cha tofauti utakuwa
umejifunza.

Tuanze kujifunza kwa kuyatafakari maisha ya watu


wafuatao ambao kiukweli hawapo kabisa duniani japo
walishawahi kuishi. Ni wapi kati ya hawa unawafahamu na
unafikiri ni mambo gani yanakufanya usiwasahau hata kama
walishakufa? …

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere


Nelson Mandela
Edward Moringe Sokoine
Thomas Edson

DITRA Global || +255 656 189 370 8


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

Mama Telesa
Mahtma Ghandi
Steve Jobs
Abraham Linkolin
Martin Luther Jr
Aristotle
Plato
Socrate
N.k

Wapo Japo Hawapo

Kama utafuatilia kwa ukaribu utagundua kuwa hakuna hata


mmoja kati ya watu niliowataja hapo juu aliye hai
(anayeishi). Wengi walikufa zamani sana na pengine hata
mifupa yao ilishaoza kabisa.

Lakini jambo la ajabu ni kwamba hawa ni watu maarufu sana


katika ulimwengu wetu pengine kuliko hata sisi tunaoishi. Ni
watu ambao tunaweza kusema “wapo japo hawapo”,
“wanaishi japo walishakufa”. Hawa ni viumbe wa milele.

Wanaishi japo walishakufa

Hebu tuutazame upana wa baadhi ya watu hawa. Nikianza


na mfano wangu pendwa, Mwalimu Nyerere, Rais wa
kwanza na muasisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Huyu alizaliwa mwaka 1922 na alifariki mwaka 1999. Yaani
aliishi miaka 77 tu.

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 9


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
Cha kushangaza ni kwamba mtu huyu ambaye hayupo tena
duniani ni mtu muhimu sana kwa taifa la Tanzania pengine
kuliko hata wanaoishi (usinielewe vibaya).

Jaribu kufikiria, karibu kila ofisi ya nchi hii lazima utaikuta


picha ya mwalimu Nyerere. Hii ni haimaanishi tu kwamba
taifa linatambua umuhimu wake lakini ni uthibitisho
kwamba mtu huyu anaishi hata sasa kwa kazi yake njema
aliyoifanya kwa taifa lake.

Kuna taasisi nyingi ndani na nje ya Tanzania ambazo


zinaitwa kwa jina lake, kwa mfano vyuo, shule, viwanja vya
ndege, barabara n.k. Haya nayo je! Hayatupi kitu cha
kujifunza kuwa mtu anaweza kuishi hata baada ya kifo chake
kwa kazi zake njema.

“Tunaanza kuwa viumbe wa milele kwa


kuacha alama zisizofutika baada ya kuwa
hatupo duniani.”

Karibu kila siku katika madarasa ya shule za misingi, za


sekondari na hata vyuo vya ndani na nje ya nchi mamilioni
kwa mamilioni ya wanafunzi wanaendelea kumfahamu zaidi
mwalimu Nyerere kwa kazi zake.

Hii inatoa tafsiri kuwa Nyerere ataendelea kuishi katika


vizazi na vizazi na vizazi. Huyu ni mtu aliyeacha alama
ambayo hakuna kifutio ulimwenguni kinaweza kuifuta.
Huyu ni kiumbe wa milele.

DITRA Global || +255 656 189 370 10


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

Je! Tutawezaje Kumsahau? ….

Edward Moringe Sokoine aliyewahi kuwa waziri mkuu wa


Tanzania. Mtu aliyeishi kwa miaka 46 tu (1938-1984).
Aliishi kwa muda mfupi tu lakini wajua kuwa…. Mkoani
Morogoro-Dakawa, mahali tu alipofia (alipopatia ajali) pana
kijiji kilichopewa jina lake (Wami Sokoine).

Hapo hapo pana shule ya sekondari (High school)


ijulikanayo kama Sokoine Memorial High School na
wanafunzi wasio na hesabu wanatarajia kusoma hapo.
Hapohapo pana Hospitali iitwayo kwa jina lake (Hospitali Ya
Sokoine). Je! Huyu naye haishi hata sasa….

“Ubora wa maisha haupimwi kwa wingi


wa miaka anayoishi mtu bali kwa alama
anazoziacha hata kama ataishi miaka
michache.”

Mwaka 1984 (mwaka aliofariki waziri Edward Sokoine) kwa


heshima yake Mkoani Morogoro kilianzishwa chuo cha
kilimo cha Sokoine (SUA) miongoni mwa vyuo bora vya
kilimo katika Afrika.

Chuo ambacho mpaka sasa kimetoa wataalamu wasio na


hesabu katika nyanya mbalimbali, mimi nikiwa mmoja wao.
Kipekee najivunia kuwa tunda la chuo hiki, na hii ndiyo
sababu nimewekeza muda kujifunza maisha ya waziri
Edward Sokoine.

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 11


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
Hii ikupe tafsiri kwamba Sokoine anaishi hata leo na
ataendelea kuishi kwa alama hizi zizofutika ambazo ni
matunda ya kazi zake njema kwa muda mfupi wa uhai wake.

Hawa nao je! Si viumbe wa milele? …

Leo hatunaye Thomas Edson, lakini anaishi kupitia


balbu na vifaa vingi alivyoviasisi.
Hatunaye James Naismith, lakini anaishi kupitia mchezo
pendwa wa kikapu (Basketball) aliouanzisha. (Rejea
kitabu changu cha Nguvu Ya Kuanza).
Leo hatunaye Mama Telesa lakini anaishi kwa matendo
yake ya upendo na huruma ambayo ulimwengu kamwe
hauwezi kuyasahau.
Hatunaye Steve Jobs lakini anaishi kwa kupitia kampuni
aliyoianzisha (Apple Campany) inayojihusisha na
utengenezaji wa vifaa bora vya kimawasiliano kama
simu (iphones), Apple Kompyuta, n.k.
Na mifano mingine mingi.

Umilele ndani ya watu

Hawa ni watu ambao ulimwengu kamwe hauwezi


kuwasahau kwa sababu ya alama walizoziacha baada ya
uhai wao. Mimi nawaita watu hawa “viumbe wa milele
(eternal beings). Swali ni je! Ina maanisha nini kuwa kiumbe
wa milele? Twende pamoja.

Watu wengi (hasa wa dini) wanaamini juu ya umilele, lakini


sidhani kama wanaielewa dhana hii katika uhalisia wake. Kwa
umuhimu wa mada ya kitabu hiki ninaomba kwa pamoja

DITRA Global || +255 656 189 370 12


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

tuuchunguze kwa ukaribu ukweli kuhusu umilele. Na mahali


sahihi tunaweza kuupata ukweli huu ni katika neno la Mungu;

Maandiko yanasema;

Mhubiri 3:11: “Kila kitu amekifanya[Mungu] kizuri


kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya
mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza
kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo
hata mwisho.”

“…tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao…”

Kwa Kiswahili cha kawaida sawa na Kamusi ya Kiswahili ya


karne ya 21, neno milele lina maana ya “bila kikomo, bila
mwisho, daima.”

Biblia inasema Mungu ameiweka milele ndani ya


wanadamu. Hii yaweza kutupa tafsiri kadhaa;

1. Mungu alikusudia mwanadamu awe kiumbe wa


milele (asiye na ukomo) kama yeye mwenyewe
alivyo wa milele.
2. Umilele (kutokuwa na mwisho) ni jambo ambalo lipo
ndani ya kila mwanadamu, tumeumbiwa nalo.
3. Kutokuwa na mwisho (umilele) linapaswa kuwa
lengo mama la kila mwanadamu.

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 13


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
Huu ni ukweli ambao watu wengi hawaufahamu. Wengi
wanaamini umilele ni baada ya kifo. Hapana umilele upo
ndani yako unatembea nao. Wewe ni kiumbe wa milele.

Kazi ya Mungu isiyovumbuliwa …

Suleimani anaendelea kusema … “ila kwa jinsi mwanadamu


asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu
mwanzo hata mwisho.” Hii inatoa tafsiri kwamba kuna
namna Mungu anafanya mambo kwa namna ambayo akili ya
kibinadamu haiwezi kuvumbua.

Na eneo mojawapo ambalo mwanadamu hushindwa


kuvumbua utendaji wa Mungu ni namna umilele uliondani
ya watu unavyofanya kazi. Haya ni mambo ya ajabu tena
sana.

Umilele kwa njia ya kazi njema, alama zisizofutika

Kuna namna nyingi za kuuelewa ukweli huu, njia moja wapo


ambayo tutajikita nayo ni kupitia kazi njema. Kila
mwanadamu ana fursa ya kuishi milele katika ulimwengu
wake (kabla hata ya ule umilele unaojulikana na wengi) kwa
kazi njema. Kazi za thamani atakazozifanya wakati wa uhai
wake.

Rejea mifano hapo juu, hatuna uhakika sana wa maisha ya


watu hawa baada ya vifo vyao wapo wapi na wanaishi wapi
lakini tuna uhakika wa umilele wao katika ulimwengu huu
kupitia kazi zao (alama zisizofutika) walizozifanya wakati
wa uhai wao.

DITRA Global || +255 656 189 370 14


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

Unaweza kusema ni bora kuhangaikia maisha ya umilele


ujao (mbingu) ni sawa lakini lazima ujue pia kuwa Mungu
anatarajia pia uendelee kuwa baraka kwa vizazi vya baada
yako kupitia kazi zako njema.

“Unaweza kuwa baraka kwa vizazi na


vizazi baada ya kifo chako kama tu
utauachia ulimwengu wako kazi za
thamani, kazi njema.”

Baada ya kuujua ukweli huu lengo langu mama ni “kuishi


zaidi ya kifo changu, kuishi zaidi ya kaburi langu” na ndiyo
maana najitaabisha kuandika vitabu, kufundisha na kwa
ujumla kuwa baraka kwa wengi kadiri niwezavyo. Kwangu
huko ndiko kuishi ipasavyo.

Usiuache ulimwengu wako katika hali ya uyatima

Wewe ni kiumbe wa milele. Umilele ni urithi ulioupata


kutoka kwa Mungu. Ni kosa la jinai kuuacha ulimwengu
wako katika hali ya ukiwa.

Dk. Myles Munroe anasema …

“Kama ili tukukumbuke kwamba uliwahi kuishi


duniani tutahitaji kutafuta kaburi lako lilipo
ndipo tujue kuwa uliwahi kuishi basi wewe
utakuwa mtu uliyeishi kihasara sana.” (baadhi ya
maneno yameongezwa)

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 15


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
Maisha yako yanaweza kuacha alama isiyofutika, alama
kama kovu la kidonda lisilofutika hadi mtu anakuwa mzee.
Alama ambayo hakuna mamlaka duniani inaweza kuifuta.
Inawezekana…

Wewe unaweza kuishi miaka mingi zaidi, unaweza kuishi


baada ya kifo chako, unaweza kuishi zaidi ya mipaka ya
kaburi lako. Inawezekana…

Mafanikio ya kitabu hiki ni wewe kutambua kuwa wewe ni


kiumbe wa milele. Kutambua kuwa unaweza kuuachia
ulimwengu wako alama zisizofutika na zaidi kutambua
kuwa unaweza kuishi zaidi ya kifo chako. Mungu akusaidie
kuyaelewa haya. Naam, ukawe sababu ya mafanikio ya
kitabu hiki.

NIMEKUOMBEA

DITRA Global || +255 656 189 370 16


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

Kukielewa Kifo

“Sote tunakufa. Lengo siyo kuishi milele [duniani]. Lengo


linapaswa kuwa kufanya vitu vitakavyoishi milele.”
- Chuck Palahniuk

L engo mama la kitabu hiki ni kutaka kumsaidia kila


msomaji kujua kuwa inawezekana kuishi zaidi ya kifo.
Na bila shaka sura iliyopita imetupa ufahamu mkubwa
ambao naamini umekupa kujua kuwa lengo hili
linawezekana na bila shaka pengine hili limekuwa lengo
mama kwako pia kama ilivyo kwangu.

Kama kuna kuishi zaidi ya kifo basi kuna kifo. Hivyo ni


muhimu tukakielewa kifo katika upana wake. Ni imani
yangu kwamba kama utakielewa kifo katika uhalisia wake
maisha yako yatabadilika sana na zaidi mtazamo wako
kuhusu kifo.

“Haiwezekani kuishi zaidi ya kifo pasipo


kuwa na ufahamu sahihi kuhusu kifo.”

Niombe radhi kwa watu ambao hawapendi kusikia au


kusoma habari za vifo (pengine kwa sababu yoyote).
Sambamba na kuomba radhi, ninawaomba pia wajaribu japo
kupitia kitabu hiki kusoma ukweli kuhusu kifo uliofunuliwa

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 17


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
katika kurasa chache za sura hii kwani ninaamini
utawaweka huru.

Kifo …

Ni moja ya maajabu ya ulimwengu. Ni kitu kisichoeleweka


na wengi. Ni kitu kinachoupa ulimwengu maswali yasiyo na
majibu kila iitwapo leo. Ni uzoefu usio na mwenyeji. Kifo…

Vizazi kwa vizazi vimeendelea kukishuhudia kifo kwa


nyakati zote. Watu wa kila mahali, kila kabila, kila rangi, kila
hadhi wote hukutana na kifo. Tafiti kwa tafiti zimefanywa
karibu kila katika kizazi kujaribu kukichunguza kifo lakini
hakuna utafiti wenye hatima inayoweza kueleweka kwa
uzuri kuhusu kifo kwa ulimwengu mzima.

Wengi wamefikia hatua ya kukiita kifo “tajiri” kwani kila


siku kifo hakikosi wateja. Karibu kila sekunde watu
wanakufa kila pahali ulimwenguni. Naam, hayo ndiyo
maajabu ya kifo.

Ukweli Kuhusu Kifo

Kama utajaribu kukichunguza sana kifo ni dhahiri kuwa ni


rahisi zaidi kuishia kuwa na majuto zaidi kuliko kuwa na
tumaini. Lakini kitabu hiki kinakuja na ukweli wenye
matumaini zaidi ya majuto.

Ungana nami kujifunza zaidi. Nimemwomba Mungu


kwamba hadi mwisho wa sura hii na zaidi sana hadi mwisho
wa kitabu hiki kila msomaji (wewe ukiwa wa kwanza)

DITRA Global || +255 656 189 370 18


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

apokee ufunuo mpya kuhusu kifo utakaokuwa sababu ya


yeye kutokukiogopa kifo bali kukiona kitu cha kawaida
kama vitu vingine. Kama unayaamini haya basi pokea
maombi yangu.

Kweli 5 Kuhusu Kifo

Haijalishi unakitafsirije kifo. Kifo tunaweza kukielewa katika


uhalisia wake kwa kweli zifuatazo;

Kweli #1: Kifo ni halisi

Unaweza kuwa na mashaka na vitu vingi lakini hupaswi


kuwa na mashaka na kifo. Kifo ni halisi na historia ya
ulimwengu tayari imelithibitisha hili.

Tangu mwanzo Mungu hakukusudia watu wafe. Kifo ni zao


la anguko la mwanadamu (dhambi). Biblia inasema;

Mwanzo 2:16-17: “Bwana Mungu akamwagiza huyo


mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza
kula, 17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na
mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda
ya mti huo utakufa hakika.”

1Wakorintho 15:21-22: “Maana kwa kuwa mauti


ililetwa na mtu… 22 Kwa kuwa kama katika Adamu
wote wanakufa, ….”

Maandiko haya (na mengine mengi) yanaufunua ukweli


kuhusu kifo. Kifo ni halisi. Na tunaweza kuuthibitisha ukweli

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 19


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
huu kwa sababu tangu mwanadamu wa kwanza alipoanza
kufa wanadamu wote wameendelea kufa.

Kama kifo ni halisi hatuna haja ya kuwa na maswali kuhusu


hicho bali tunapaswa kuishi tukijua kifo ni sehemu ya
maisha ya mwanadamu. Zaidi ya kujua kuwa kifo ni halisi ni
muhimu pia kufahamu mpango wa Mungu nyuma ya kifo.
Kama inavyofafanua kweli ifuatayo.

Kweli #2: Kifo siyo mwisho

Kifo kinasababisha hofu nyingi kwa sababu kwa wengi kifo


hutafsirika kama mwisho. Lakini huu siyo ukweli. Ukweli ni
kwamba kifo siyo mwisho. Maandiko yanaufunua ukweli
huu;

1Wakorintho 15:22: “Kwa kuwa kama katika Adamu


wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote
watahuishwa.”

Warumi 6:5 “Kwa maana kama mlivyounganika naye


[Yesu Kristo] katika mfano wa mauti yake, kadhalika
mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake;”

Tatizo la dhambi lilimfanya mwanadamu awe katika hatari


ya kifo wakati wote. Mungu kwa huruma zake alimtoa Yesu
Kristo ambaye alikufa kwa ajili ya dhambi ya mwanadamu
na zaidi sana alimwondoa mwanadamu katika hatari ya kifo.

Kupitia Yesu kuna tumaini la kuishi baada ya kifo. Kama vile


ambavyo yeye alikufa akafufuka, sisi nasi hata kama

DITRA Global || +255 656 189 370 20


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

tutakufa basi tujue kuna tumaini la kuishi tena katika Kristo.


Jambo la msingi ni sisi kumwamini (kwa kuokoka).

Kweli #3: Hatupaswi Kukiogopa kifo

Kama kifo ni halisi, tena kifo si mwisho ya nini kukiogopa


kifo? Kuogopa kifo ni sawa na kusema hatujatambua kazi ya
msalaba iliyofanywa na Yesu Kristo. Kama tunatambua basi
hatupaswi kabisa kuwa na hofu ya kifo, lakini tunapaswa
kutafuta zaidi kuishi maisha yenye tija.

Nayapenda maneno ya Marcus Aurelius, Yeye anasema;

“Si kifo anachopaswa kugopa mtu, bali


anapaswa kuogopa kutokuanza kuishi.”

-Marcus Aurelius

Usikae kuwaza itakuwaje kuhusu kifo, nitakufaje kufaje,


itakuwaje baada ya kifo, n.k. Mawazo ya namna hii
yatakupotezea muda na kukuingiza tu katika majuto.

Acha kuwa na hofu ya kifo na tafuta kuishi maisha yenye


maana, maisha yanayowaongezea thamani watu wengi
wanaokuzunguka. Maisha yanayompa Mungu utukufu,
maisha yatakayokufanya uwe na alama zisisizofutika hata
baada ya kifo chako.

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 21


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
Kweli #4: Kifo ni tangazo la mwanzo mpya

Kwenye kitabu chake kiitwacho “Who will cry when you


die?” Robin Sharma anaandika maneno aliyoambiwa na
baba yake akiwa mdogo. Baba yake alimwambia;

“Kijana, ulipozaliwa ulilia wakati


ulimwengu ulifurahi. Ishi maisha yako
kwa namna ambayo utakapokufa
ulimwengu utalia na wewe utafurahi.”

-Robin Sharma

Mwanzoni sikuyaelewa kabisa maneno haya lakini nikiwa


katika mchakato wa kuandika kitabu hiki ndipo
nilipoyaelewa. Maneno haya yanatoa tafsiri kwamba kifo ni
tangazo la mwanzo mpya.

Ulimwengu utakuwa ukilia kwa maana ya kukupoteza lakini


kama uliishi maisha yenye tija utaondoka ukiwa na kicheko
kwani utakuwa unajua kuwa sasa unaanza kuishi kupitia
alama ulizoziacha. Raha ilioje.

Kifo ni sawa na uotaji wa mbegu. Tunapoifukia mbegu ni


kama tunaipoteza lakini inapopotea ndipo inatudhihirishia
kuwa ndani yake kulikuwa na mmea (kumbuka mada ya
umilele sasa).

Mbegu itaoza yote lakini itauacha ulimwengu ukiyashangilia


matunda yake kwa muda mrefu na wakati mwingine mengi
sana. Hivi ndivyo kifo kinavyopaswa kuwa.

DITRA Global || +255 656 189 370 22


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

Unpokufa unakuwa unautangazia ulimwengu kwamba


nimeacha hazina (alama) ambazo ulimwengu wangu
utazifaidi hata kama mimi sitakuwepo. Unakuwa kama
mbegu inayoacha mti mkubwa wa matunda baada ya
yenyewe kuoza. Naam, haya ndiyo maisha sasa, maisha
yanayoacha alama isiyofutika.

“Kama uliishi maisha yenye tija kifo chako


kitakuwa tiketi yako ya kuishi zaidi,
kitakupa mwanzo mpya katika
ulimwengu wako.”

Nimejifunza pia kwamba kifo huuongeza utambulisho wa


mtu. Kwa mfano, mtafakari Yesu wa kabla ya kifo na baada
ya kifo. Utagundua wa baada ya kifo alikuwa na utukufu zaidi
ya yule wa kabla ya kifo (Tafakari).

Watu wanaoishi maisha yenye tija utambulisho wao


huongezeka zaidi wanapokufa (wanakuwa na utambulisho
mkubwa zaidi) na mambo yao yenye tija hujulikana zaidi.

Kwa mfano nilikuwa namfahamu kwa sehemu Rais


Benjamini Mkapa (Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania)
lakini baada ya kifo chake niliyajua mambo mengi
yaliyofanywa na mtu huyu kuliko nilivyoyajua wakati wa
uhai wake.

Nimekuwa nikijifunza mambo mengi kwa watu wengi kama


Ruge Mutahaba, Steve Jobs, Dk. Myles Munroe, n.k. Lakini

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 23


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
kwa sehemu kubwa taarifa nyngi na hazina nyingi za watu
hawa zimekuwa wazi zaidi baada ya wao kufa. Hicho ndiyo
kifo.

Kweli #5: Kifo kinapaswa kuwa chachu ya mtu kuishi


maishi yenye tija zaidi

Kifo kinapaswa kuwa kihamasisho. Kinapaswa


kutuhamasisha kuishi maisha yetu ya siku kwa siku kwa
umakini zaidi huku tukiukomboa wakati kwa kufanya
mambo ya maana ambayo yatabakia hata kama sisi
wenyewe tutakuwa hatupo duniani (baada ya kufa).

Leo Buscaglia ana usemi usemao;

“Kifo ni changamoto. Kinatukumbusha


kutopoteza muda.”

- Leo Buscaglia

Huu ndiyo mtazamo unaopaswa kuwa nao kuhusu kifo. Kifo


siyo jaribu kifo ni chachu ya kuendelea kwa ubora zaidi.

Kila siku unapaswa kukumbuka kuwa wewe si wa milele


katika dunia hii bali una fursa ya kuacha alama
zitakazodumu milele.

Huu ndiyo mtazamo walioishi nao wau wengi ambao


waliacha alama ambazo kamwe haziwezi kufutika. Wewe
pia unaweza kuwa miongoni mwa waacha alama kama
utayaelewa haya. Mungu akujalie uelewa zaidi.

DITRA Global || +255 656 189 370 24


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako
3

Funguo 5 Kuelekea Maisha


Yanayoacha Alama Isiyofutika

“Maisha yanayoacha alama isiyofutika hayaji kama ajali,


yanaanza na maamuzi binafsi. Amua sasa”
- Adriano Mkonda

K atika sura ya kwanza nimejaribu kuyaelezea maisha ya


baadhi ya watu ambao hata leo hatuwezi kuwasahau
kwa sababu ya alama zisizofutika walizoziacha baada ya vifo
vyao.

Jambo la msingi ninalotaka ulielewe ni kwamba hawa


hawakuwa watu maalumu sana. Walikuwa watu wa kawaida
kama wewe.

Hii ikusaidie kutambua kuwa hata wewe unaweza kuwa


kama wao tena zaidi. Unaweza kuishi zaidi ya kifo chako.
Unaweza kuacha alama isiyofutika katika ulimwengu wako.
Naam, sura hii ipo kwa lengo la kukusaidia zaidi katika hili.

Katika sura hii tutajifunza funguo 5 ambazo kama


utazielewa na kuzitendea kazi kikamilifu wewe utakuwa
miongoni mwa waacha alama wakuu kuanzia sasa ukiwa hai
na zaidi sana hata baada ya kifo chako. Twende pamoja;

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 25


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
Funguo 5 …

Funguo #1: Tambua kuwa wewe ni kiumbe wa milele


uliyekusudiwa kuacha alama itakayodumu vizazi hata
vizazi baada yako

Kama tulivyojifunza katika sura ya kwanza ni muhimu


ulielewe jambo hili tena katika upana wake. Mungu
ameweka umilele ndani yako, yaani wewe si kiumbe wa kuja
na kupotea, hapana.

“Ni mpango wa Mungu wewe uendelee


kuwa baraka kwa ulimwengu wako hata
baada ya kifo chako.”

Ulikusudiwa uishi maisha yatakayoacha alama ambayo


hakuna kifutio ulimwenguni kinaweza kuifuta. Ni mpango
wa Mungu wewe uendelee kuwa baraka kwa ulimwengu
wako hata baada ya kifo chako.

Rafiki, kama maisha yako hayataacha kitu kitakachowafanya


watu wakukumbuke baada ya kuondoka kwako basi tambua
kuwa utakuwa umeishi maisha ya hasara sana na hakika
Mungu hatapendezwa na wewe. JITAMBUE.

Huu ni wakati wako wa kulifanya jambo hili kuwa moja ya


malengo yako muhimu. Kuishi maisha yatakayoacha alama
ambayo haitafutika kirahisi. Mungu akujalie.

DITRA Global || +255 656 189 370 26


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

Ufunguo #2: Tambua kusudi la kuumbwa kwako na


amua kuliishi kikamilifu

Kusudi ni sababu ya uwepo wa kitu fulani. Kila kitu


kiliumbwa kwa kusudi maalumu, hapa ni pamoja na wewe.
Haukuja duniani kama bahati nasibu au kama ajali ulikuja
duniani kwa kusudi maalumu.

Watu wengi hawana ufahamu wa sababu zilizomfanya


Mungu awaumbe (kusudi) na matokeo yake wanaishia
kuishi maisha yasiyo na maana na wakifa wanapotea kabisa
pasipo kuwa na alama yoyote inayothibitisha kwamba
waliwahi kuishi. Haya si maisha!

Wewe hupaswi kuwa miongoni mwa watu kama hawa


pambana kujua kusudi la Mungu katika maisha yako na jitoe
kikamilifu kuliishi hilo. Ni muhimu kufanya hivyo kwa
sababu ndani ya kusudi lako ndimo ulimofungwa umilele
wako.

“Kusudi lako ndilo litakaloamua kiwango


cha alama utakayoiacha katika
ulimwengu wako wakati wa uhai wako na
zaidi sana baada ya kifo chako.”

Watu wote waliofanikiwa kuacha alama ambazo hatuwezi


kuzisahau walianza kwa kujua wao ni akina nani, kwa kujua
sababu za uwepo wao hapa duniani. Vivyo wewe, kwa

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 27


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
kulijua tu kusudi lako unakuwa katika mstari wa watu
ambao ulimwengu hauwezi kamwe kuwasahau. Zingatia hili.

Kwa msaada zaidi wa namna unavyoweza kulitambua


kusudi la kuumbwa kwako tafadhali pata kitabu changu
kiitwacho “Kusudi 101” Kitakusaidia.

Ufunguo #3: Ishi kwa ajili ya kesho na si leo (uwe na


maono)

Maono ni picha ya baadaye ya jambo fulani. Ni kesho ya


jambo fulani. Ni taswira ya mambo yatarajiwayo. Kuwa na
maono ni kuwa na uwezo wa kuiishi kesho kuanzia leo.

Ni watu wenye maono tu wanaoweza kuacha alama


zisizoweza kufutika. Fikiri watu kama kina mwalimu
Nyerere, kina Nelson mandela, n.k, je! Tungeweza
kuwakumbuka hata leo kama wasingekuwa na maono
makubwa kwa ajili ya nchi zao? HAPANA.

“Maono yana tabia ya kuishi zaidi ya


mbeba maono. Maono ndiyo yanayowapa
watu fursa ya kuishi zaidi ya vifo vyao.”

Watu wenye maono mara zote huijali zaidi kesho kuliko leo,
huishi kwa ajili ya kesho na si kwa ajili ya leo. Hawa
huvifikiri zaidi vizazi vya mbele yao kuliko hata
wanavyojifikiria wao wenyewe. Matokeo yake watu hawa
huishia kuacha alama ambazo kamwe haziwezi kufutwa
haijalishi kifutio gani kitatumika.

DITRA Global || +255 656 189 370 28


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

Je! Una maono katika maisha yako? Unafikiri utakuwa mtu


wa namna gani baada ya miaka 5, 10, 30 au hata 50 ijayo?
Kama huna maono usitarajie kabisa kuwa miongoni mwa
watu watakaocha alama. AMKA.

Kwa msaada zaidi kuhusu namna unavyoweza kuwa na


maono ya maisha yako tafadhali pata kitabu changu
kiitwacho “Maono 101” kitakusaidia.

Ufunguo #4: Wekeza zaidi kwa watu na siyo kwenye vitu


(watumikie watu)

Kwenye kitabu changu kiitwacho “Uwekezaji Wenye


Matokeo” (ukikipata kitakusaidia zaidi), nimeeleza aina 5
za uwekezaji wa maana, na aina mojawapo ni kuwekeza kwa
watu. Huu ndiyo uwekezaji mkubwa na wa maana zaidi
anaoweza kuufanya mtu.

“Biashara pekee yenye faida ya milele ni


biashara ya kuwekeza kwa watu. Watu
watakufanya uishi zaidi ya kifo chako”

Watu wengi wanahangaika kuwekeza kwenye vitu kama


ardhi, biashara, mali, elimu, n.k (mambo ambayo si mabaya).
Lakini watu wenye busara huwekeza zaidi kwa watu. Hii
kwa sababu watu hawa wanajua kuwa watu wana uwezo wa
kuishi zaidi ya vitu.

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 29


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
Ni rahisi sana vitu kupotea, kuteketea, kuharibika lakini ni
ngumu sana kupoteza hazina zilizowekezwa ndani ya watu.
Mfano mzuri ni uwekezaji alioufanya Yesu Kristo akiwa
duniani.

Hakuna mahali tunasoma kwamba Yesu alijenga kanisa,


wala nyumba, wala kwamba alikuwa na mashamba, wala
gari, wala biashara, n.k. Lakini wakati wote wa kuishi hapa
duniani aliwekeza kwa watu. Alikaa na wanafunzi wake,
alikaa na wenye dhambi, aliwatembelea watu, kwa ujumla
aliwatumikia watu.

Si ajabu leo huduma aliyoiasisi Yesu (kanisa) inadumu hata


sasa na itaendelea kudumu mpaka atakaporejea. Ni kwa
sababu Yesu aliwekeza zaidi kwa watu na si katika vitu. Ni
muhimu utambue kuwa;

“Kiwango cha uwekezaji unaoufanya kwa


kuwatumikia watu ukiwa hai, ndicho
kitakachoamua kiwango cha alama
(legacy) utakayoiacha baada ya kifo
chako.”

Je! Umejitoa kiasi gani kuwekeza kwa watu? Je! Ni mara


ngapi umeona watu ni wa muhimu kuliko shughuli zako au
mali zako? Je! Ni muda kiasi gani unautoa kwa ajili ya watu?

Kama kweli unataka kuacha alama isiyofutika mahali popote


utakapokuwa na zaidi sana hata baada ya kifo chako
tafadhali wekeza zaidi kwa watu. Watu watakufanya uishi
zaidi ya kifo chako.
DITRA Global || +255 656 189 370 30
Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

Watumikie….

Utajiuliza nawekezaje kwa watu? Ni rahisi tena sana. Njia


rahisi zaidi ya kuwekeza kwa watu ni kwa kuwatumikia.
Kuwatumia watu ni …

Uwezo wa kutumia vipawa, ujuzi, elimu na kila kitu


ulichopewa na Mungu kufikia mahitaji ya wengine.
Ni uwezo uwezo wa kuona mahitaji ya wengine na
kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha unayafikia
mahitaji husika.
Ni uwezo wa kuyaongezea thamani maisha ya wengine.
Ni kuwa baraka kwa wengine.
Yesu ni mfano bora zaidi (Soma Mathayo 20:28).

“Kadiri unavyoongeza idadi ya watu


unaowatumikia wakati wa uhai wako
ndivyo unavyotanua zaidi kiwango cha
alama (legacy) na ushawishi wako wa
baada ya kifo chako.”

Kama utachagua kuwatumikia watu, basi utakuwa na nafasi


katika mioyo yao na kama utakuwa na nafasi katika mioyo
yao basi wewe hutasahaulika kamwe. Mungu akupe neema
ya kuyaelewa haya zaidi na kuyatendea kazi.

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 31


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika

Ufunguo #5: Andaa watu baada yako (Succession)

Wakati fulani nilikuwa nachunguza ukuaji na uzaaji wa


migomba, nikagundua kuwa hakuna mgomba unaoweza
kuzaa kama hakuna mgoja mwingine (mchanga)
utakaochukua nafasi badala yake.

Hii ni kusema kwamba mgomba utaanza tu kubeba ndizi


pale tu kutakapokuwa na mgomba mwingine utakaokuwa
unachipuka nyuma yake. Na matokeo yake kwa kanuni hii
rahisi migomba ni kati ya zao ambalo hufanikiwa sana.

“Wewe si wa milele katika dunia hii, ni


wajibu wako kuwaandaa watu
watakaoyaendeleza yale mema
uliyoyanzisha.”

Jambo la ajabu ni kwamba watu wengi tunashindwa


kujifunza hata kwa viumbe wa kawaida (migomba). Ni nadra
sana kuona watu wawe wazazi, viongozi wa serikali,
viongozi wa dini, wafanyabiashara, n.k wakiwaandaa watu
watakaoendeleza yale waliyoyaanzisha.

Matokeo yake kwa kosa hili wao wanapokufa na yale


waliyoyaanzisha hufa na wao huhesabika kama watu
walioshindwa kama Dk. Myles munroe anavyoeleza katika
kitabu chake kiitwacho “Passing it on”.

DITRA Global || +255 656 189 370 32


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

Kumbuka wewe si wa milele (hapa duniani). Unapaswa


kuwaandaa wengine ambao watasimama baada yako yako
na kwa kufanya hivyo utakuwa umeacha alama isiyofutika
ulimwenguni kupitia wale uliowaandaa.

Yesu kabla ya kuondoka duniani aliwaanda wanafunzi 12 na


kupitia hao leo ulimwengu umefurikwa na mamilioni kwa
mamilioni ya wafuasi wake.

Musa akijua kuwa yeye si wa milele alimwandaa Yoshua.


Eliya alimwandaa Elisha, Paulo aliwaandaa kina Timotheo,
na akina Tito. Wewe unamwandaa nani?...

Kama unajua una maono na maono hayo ni makubwa


tafadhali anza mapema kuwandaa watu watakaoyaendeleza
maono hayo badala yako. Kwa kufanya hivyo utakuwa na
uhakika wa kuacha alama isiyofutika katika ulimwengu
wako.

Ni Maombi Yangu

Mungu wa mbingu akujalie kuyaelewa haya naam, akupe


neema ya kuyaishi yote ili uwe miongoni mwa watu ambao
watakuwa baraka kwa ulimwengu tangu sasa ukiwa hai na
hata baada ya kifo chako.

Na iwe hivyo

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 33


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika

Anza Leo Kuacha Alama


Isiyofutika

“Maisha yako ya leo ndiyo alama yako ya kesho.”


- Adriano Mkonda

N ihitimishe kwa jambo hili la muhimu. Ni hivi…


tunaposema maisha yanayoacha alama isiyofutika ni
rahisi kudhani kwamba maisha hayo unaweza kuanza
kuyaishi kipindi fulani hivi au pengine ukadhani maisha
hayo yatakuja tu. HAPANA.

Tunaanza kuishi maisha yanayoacha alama isiyofutika leo na


siyo kesho. Maisha yako ya leo ndiyo alama yako ya kesho.
Hivyo huhitaji kuanza kesho kuishi maisha yanayoacha
alama, unahitaji kuanza leo.

Leo iwe ndiyo siku pekee ya wewe kuandika historia


ambayo itakumbukwa kesho. Leo iwe ndiyo siku utakayoishi
maisha yenye tija ili kesho ulimwengu ukukumbuke.

Leo ishi vizuri na watu, leo uwe baraka kwa wengine, leo
watumikie wengine. Leo na siyo kesho.

“Kumbuka, leo yako ndiyo kesho yako.”

UBARIKIWE

DITRA Global || +255 656 189 370 34


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

Maalumu Kwa Ajili Yako

“Mungu Anakupenda”

Je!Ulipozisikia
Umewahi kusikia habari za upendo wa Mungu? Na je!
ulijisikiaje? Inawezekana ulihisi ni za kawaida
tu au pengine ulisema hizi ni habari ninazozisikia kila siku,
hivyo hukuzipa uzito kabisa.

Leo una nafasi tena ya kuzisikia na hupaswi kuzichukua kwa


ukawaida tena kwa sababu zitakupa mwanzo mpya wa
maisha kama hutazipuuza.

Mungu aliwaumba wanadamu wote ili waishi maisha


ambayo yeye aliwakusudia. Lakini dhambi iliharibu mfumo
wa maisha ambao Mungu aliwakusudia watu wake.

Kwa ushawishi wa dhambi Mwanadamu akaanza kuishi


mbali na Mungu tena akaanza kuishi maisha yasiyofaa hadi
pale Mungu alipomtuma Yesu mwanae kuja kumwokoa.

Maisha halisi yanaanza pale tunapochagua kutubu dhambi


zetu na kumgeukia Mungu kwa njia ya kumpokea Yesu kama
Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Na hizi ndizo habari
njema.

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 35


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika
Kama moyo wako unakushuhudia kwamba unahitaji sasa
kutubu dhambi zako na kuanza maisha mapya na Mungu
wako, tafadhali usipuuze jambo hili. Amua leo kumfuata
Mungu wako, amua leo kuokoka na maisha yako yatakuwa
salama.

Kama upo tayari kuokoka tafadhali sali sala hii toka ndani ya
moyo wako;

Ee! Mungu wangu ninakuja kwako,


nimetambua kuwa nimekuwa mbali nawe kwa
sababu ya dhambi yangu. Leo ninarudi kwako
kwa kutubu, ninaomba unisamehe, unipokee
na unifanye kuwa mwanao. Katika jina la Yesu.
AMINA

Kama umesali sala hii Sasa Umeokoka, wewe ni mwana wa


Mungu.

Kwa maelekezo zaidi ya namna unavyoweza kuukulia


wokovu, tafadhali wasiliana nami kwa mawasiliano
yanayopatikana katika kitabu hiki. Nitafurahi kuwasiliana
nawe na nitakusaidia. Karibu sana.

MUNGU AKUBARIKI

DITRA Global || +255 656 189 370 36


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

MAREJEO

Longhorn. (2011). Kamusi ya karne ya 21. Dar es salaam,


Tanzania: Longhorn publishers (T) Ltd.

Munroe, M. (2011). Passing it on. New York: FaithWords


Hachette Book Group.

The Holy Bible in Kiswahili. (2013). Dodoma, Tanzania: The


Bible society of Tanzania.

Who will cry when you die? by Robin Sharma.

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 37


Maisha Yanayoacha Alama Isiyofutika

Vitabu Vingine

Vitabu vingine vilivyoandikwa na Adriano Mkonda ni


pamoja na;

1. Nguvu Ya Wazo
2. Kuwa Baraka Kwa Wengine
3. Kusudi 101
4. Maono 101
5. Malengo 101
6. Mafanikio Halisi
7. Sayansi Ya Muda
8. Mambo Yasiyo Ya Kawaida Kupitia Watu Wa
Kawaida
9. Kijana Na Ujana
10. Sayansi Ya Kipaji
11. Nidhamu Binafsi
12. Nguvu Ya Kuanza
13. Uwekezaji Wenye Matokeo
14. Ulimwengu Wa Mitandao
15. Utoaji Unaomgusa Mungu
16. Kurejesha Njaa Ya Kiroho
17. Baraka Za Kutumika Chini Ya Maono Ya Wengine
18. Unamhitaji Baba
19. Na vinginevyo

DITRA Global || +255 656 189 370 38


Ishi Zaidi Ya Kifo Chako

Kwa Mawasiliano Na Kujifunza Zaidi

Ikiwa umeguswa na ujumbe wa kitabu hiki, una swali, una


maoni, ushauri, ushuhuda au unahitaji vitabu vingine,
unaweza kuwasiliana moja kwa moja na mwandishi;

Adriano Mkonda

Simu/meseji/WhatsApp: +255 656 189 370, +255 621 618 821


Barua pepe: mkondaadriano10@gmail.com

Pia unaweza kupata mafundisho zaidi kutoka kwa Adriano


Mkonda kupitia;

DIVINE TRANSFORMATION GLOBAL (DITRA Global)

Barua pepe: ditraglobaltz@gmail.com


Facebook: Ditra Global Tanzania
Instagram: ditra_global
WhatsApp: +255 656 189 370
WhatsApp link:
https://wa.me/message/WSSND7DQJGVCO1

Adriano Mkonda || +255 656 189 370 39

You might also like