You are on page 1of 9

HOTUBA YA MGENI RASMI NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII

MHE. MHANDISI RAMO MAKANI (MB), KWENYE MAADHIMISHO YA


SIKU YA KUTUNDIKA MIZINGA KITAIFA YALIYOFANYIKA WILAYANI
ITILIMA MKOANI SIMIYU TAREHE 03 OKTOBA 2017

Mhe. Mkuu waMkoa wa Simiyu


Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Bw. Benson Salehe Kilangi
Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Dkt. Ezekiel E. Mwakalukwa
Mtendaji Mkuu Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos
Santos Silayo
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya Itilima Mhe. Mariano
E. Mwangungu
Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali mliopo mahali hapa
Ndg. Watendaji wote wa Serikali mliopo hapa
Wafugaji Nyuki na Wajasiriamali mliopo hapa
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.

Habari za mchana;

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia


afya njema na kuniwezesha kuhudhuria siku hii muhimu sana kwa Taifa
letu inayoadhimishwa hapa Itilima,

Aidha, natumia fursa hii kuwashukuru nyote mliotenga muda wenu na


kuungana nami katika tukio hili kubwa na muhimu la kuadhimisha siku
ya kitaifa ya kutundika mizinga inayofanyika kitaifa hapa Wilayani
Itilima Mkoani Simiyu.

Kama mnavyofahamu maadhimisho haya yamekuwa yakifanyika nchini


kila mwaka yapata miaka mitano sasa, ikiwa ni siku maalum ya
kuhamasisha umma juu ya ufugaji nyuki na kupima mafanikio ya
utekelezaji majukumu na malengo mbalimbali katika Sekta. Napenda
kutumia nafasi hii kuwapongeza watendaji na wataalamu wa wizara
kwa utekelezaji wa malengo mbalimbali ya sekta ndogo ya ufugaji wa
nyuki na kwa kupanga kuwa na siku hii maalum ya kila mwaka.

1
Katika hotuba yake Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki
amezungumza juu ya mafanikio yanayoendelea kupatikana katika sekta
hii ikiwa ni pamoja na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 5 katika Afrika
kuwa na asali inayokubalika katika soko la ulaya na china kutokana na
ubora wake; uendelezaji wa ufugaji wa nyuki unaoshirikisha jamii kwa
rika zote na jinsia zote, kuongezeka kwa idadi ya mizinga ya kisasa n.k.

Kwa upana wake hatua hizi ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa


Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 - 2020/21 kuhusu
uimarishaji wa mifumo bora ya uhifadhi Maliasili kwa njia ya
ushirikishaji jamii. "enhancement of comunity-based natural resource
management systems". Vilevile huu ni utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa
ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ibara ya 31 (d) iliyoahidi
kuendelea kutekeleza programu ya ufugaji nyuki ya mwaka 2007 - 2016
ili kuwajengea uwezo wadau kuzifahamu mbinu bora za uzalishaji wa
mazao ya nyuki na pia masoko ya asali na nta ya ndani na nje ya nchi.

Ndugu wananchi,

Napenda nitoe shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa Mkoa wa Simiyu


kwa kazi kubwa iliyofanywa katika kuhakikisha lengo kuu la siku hii ya
leo linafanikiwa. Pia niwashukuru sana nyie wananchi wa Isengwa na
vitongoji vya jirani kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa uongozi wa mkoa
na Wilaya wakati wote wa uratibu wa tukio hili. Kipekee niwashukuru
wafugaji wa nyuki wote, mmoja mmoja na kwa wale walioko katika
vikundi mbalimbali pamoja na wadau wengine ambao mmeweza
kufanikisha maadhimisho haya siku hii ya leo kwa kuleta bidhaa na
huduma zenu katika maonyesho haya.

Pamoja na kuwa miongoni mwa Wilaya zilizoanzishwa katika miaka ya


hivi karibuni, Wilaya ya Itilima inaendelea kufanya vizuri katika shughuli
za ufugaji nyuki kwa kiwango cha kuwa na mwelekeo wa kuleta
ushindani kwa Wilaya za Urambo (Tabora) na Manyoni (Singida)
ambazo zinaongoza. Huu ni ujumbe mahsusi kwa Wilaya zingine
kwamba INAWEZEKANA; na kwa mwitikio huu mkubwa mlioufanya
katika maadhimisho haya kuja katika uwanja huu na bidhaa na huduma
zenu, mmeweza kutoa elimu na hamasa kwa watu wengine juu ya faida
ya ufugaji nyuki hivyo kuendelea kuimarisha msingi wa kukuza ufugaji
nyuki katika Wilaya hii, Kanda ya ziwa na Taifa kwa ujumla.

2
Ndugu wananchi,

Ufugaji nyuki hapa nchini una fursa nyingi katika kusaidia jamii yetu.
Fursa hizo ni pamoja na kuwezesha wananchi kujikimu kimaisha kwa
kujipatia riziki; kuhifadhi mazingira kutokana na tabia ya nyuki
kuchavusha maua mbalimbali; kutumika kwa mazao ya nyuki kama
chakula na malighafi viwandani na Kuwepo kwa viambato vya dawa
katika asali kama inavyoaminika katika baadhi ya jamii.

Ndugu wananchi,

Katika fursa ya viwanda, pamoja na mazao ya asali na nta yaliyozoeleka


miongoni mwa jamii, tunayo pia mazao mengine ambayo ni gundi ya
nyuki (Propolis) na maziwa ya nyuki (Royal jelly), ambayo yote yanafaa
kutumika kama malighafi ya viwandani.

Ndugu wananchi,

Sote tunafahamu kwamba nchi yetu katika awamu hii ya tano ya uongozi
wa Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli, inalenga kuwa nchi ya
Viwanda na yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Ili kufikia hatua
hiyo, hatuna budi kufanya kazi kwa bidii na kutumia raslimali
mbalimbali tulizonazo katika kujiendeleza wenyewe ikiwemo raslimali
za Ufugaji nyuki. Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Kutundika
Mizinga Kitaifa kwa Mwaka 2017 ni: Ufugaji nyuki kibiashara
unachangia katika ukuaji wa Viwanda. Kufuga nyuki kibiashara
maana yake ni kuendesha ufugaji nyuki wenye tija kwa kuzalisha mazao
mengi yenye ubora na kuyaongezea thamani (Value addition).

Ndugu wananchi,

Tunapozungumzia viwanda, baadhi yetu wanafikiria kuwa na maeneo


makubwa sana ya ardhi, majengo makubwa na mitambo/mashine
kubwa, tekinolojia kubwa n.k. Ukweli ni kwamba katika viwanda vidogo
na vya kati ikiwa ni pamoja na vinavyotokana na ufugaji nyuki, hayo yote
sio mahitaji ya lazima na badala yake mahitaji ya wastani tu yanatosha
kuanzisha na kuendeleza viwanda endelevu vidogo, vya kati na hatimaye
vikubwa. Ikumbukwe kuwa aina ya viwanda mbalimbali hutegemeana au
hutegemea viwanda vingine.

3
Kwa mfano, Kiwanda cha magari kinahitaji kuwa na kiwanda kingine cha
vipuri, kiwanda cha nguo kinahitaji viwanda vingine vya kuchambua
pamba (ginneries) na kusokota nyuzi n.k.

Vilevile, katika ufugaji nyuki, unaweza kuwa na kiwanda cha


kutengeneza zana za ufugaji nyuki kama mizinga na mavazi ya kinga
dhidi ya nyuki na mwingine akawa na kiwanda cha kuchakata na
kufungasha na kuyaongezea thamani mazao ya nyuki kama asali, nta,
gundi ya nyuki na mengineyo. Haya yote yanawezekana kwani hayahitaji
fedha nyingi sana katika kuanzisha. Mojawapo ya faida za ufugaji nyuki
ni kwamba hauhitaji mtaji mkubwa sana; pia rasilimali muhimu ambazo
ni nyuki wenyewe na mimea vyote vipo asilia. Kinachohitajika hapa ni
elimu zaidi ya ufugaji nyuki na mahitaji ya wastani ambayo ni rahisi
kumudu (affordable).

Ndugu wananchi,

Mazao ya nyuki ni malighafi katika viwanda vya aina mbalimbali


vikiwemo viwanda vya vyakula vinavyotumia asali, viwanda vya dawa za
tiba na vipodozi vinavyotumia asali na nta hadi viwanda vya
utengenezaji (manufacturing) vinavyotumia Nta katika kuzalisha
maturubai, dawa za kungarisha viatu na kadhalika. Wafugaji nyuki
mnayo fursa kubwa sana ya kuanza kujikita katika viwanda
vidogovidogo vya kuchakata, kufungasha na kuongeza thamani mazao ya
nyuki na hata kutengeneza vipodozi vya kawaida kabisa kutokana na
mazao ya nyuki. Wajibu wetu hapa ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya
nyuki na ujuzi wa kuyaweka katika ubora na kuyaongezea thamani.

Ndugu wananchi,

Kumbukumbu zilizopo zinadhihirisha wazi kwamba mazao ya nyuki


yanahitajika sana katika soko, liwe la ndani na hata lile la nje ya nchi.
Suala ni kwamba hatujaweza kutosheleza mahitaji ya soko kutokana na
uzalishaji mdogo uliopo kwa sasa pamoja na kwamba nyuki wapo karibu
kila mahali katika nchi yetu na misitu bora kuwawezesha nyuki
kuzalisha asali bora tunayo. Shughuli hii ya ufugaji nyuki inaweza
kufanywa na kila mtu mwenye uhitaji kwa kupata mafunzo kidogo sana,
na pale inapowezekana, kupata mitaji. Ni wito wangu kwa wananchi
wote wenye nia ya kushiriki katika sekta hii, kuwasiliana na Wizara ya
Maliasili na Utalii Idara ya Misitu na Ufugaji Nyuki ili kupata taarifa za
kina na elimu zaidi juu ya ufugaji nyuki.
4
Ndugu wananchi,

Pamoja na mafanikio makubwa yanayoweza kupatikana kupitia sekta hii


ya ufugaji nyuki, zipo pia changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na
uzalishaji duni, upungufu wa wataalamu wa ufugaji nyuki kwenye
Halmashauri zetu na mabadiliko ya tabia nchi. Katika kila moja ya
changamoto hizi, serikali, watu binafsi, sekta binafsi na Taasisi
mbalimbali tunao wajibu wa kushiriki kwa namna na viwango
mbalimbali katika kuzitatua na ni jambo linalowezekana.
Hivyo, tuunganishe nguvu katika kukamilisha lengo hili kwa mustakabali
mwema wa Taifa letu.

Ndugu wananchi

Kuhusu uzalishaji mdogo wa mazao ya nyuki nchini ni wito wa serikali


kwa wafugaji nyuki kuachana na matumizi ya mizinga ya kiasili ambayo
ni duni na inachukua nafasi kubwa lakini uzalishaji wake ni kidogo.
Wananchi wafugaji nyuki waanze kutumia mizinga ya kisasa. Serikali
inaendelea kutoa elimu na kuwahamasisha juu ya matumizi ya mizinga
ya kisasa. Nawaagiza, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki Nchini na Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, kwa pamoja, mbuni
njia rafiki ya kuweka msisitizo katika utoaji wa elimu, uhamasishaji na
hatimaye kupima mafanikio kila mwaka; taarifa ya utekelezaji wa
maagizo haya itolewe mara kwa mara na muhimu zaidi taarifa ya
utekelezaji ya mwaka itolewe katika siku ya maadhimisho kama hii
mwaka 2018.

Ndugu wananchi,

Serikali inafahamu kwamba upatikanaji wa masoko ya uhakika


umekuwa ni mojawapo ya changamoto kubwa katika biashara ya mazao
ya nyuki, hali ambayo inasababisha wafugaji wetu wa nyuki kuuza
mazao yao kwa bei ndogo. Natoa rai kwa wazalishaji kuongeza viwango
vya ubora na uwingi wa asali inayozalishwa nchini ili kuvutia soko la nje
ambalo linahitaji asali bora na kwa wingi. Njia mojawapo ya kulifikia
soko hili ni kwa wafugaji kuungana katika vikundi vyenye usajili, ili
kuweza kuzalisha asali kwa uwingi unaotakiwa na yenye kufanana
(uniformity).

5
Ndugu wananchi,

Lengo la Siku ya Kutundika Mizinga Kitaifa ni kukumbushana na


kuhimizana kuhusu mbinu na njia sahihi za kutunza makundi ya nyuki ili
kupata mazao yenye ubora na mengi. Ufugaji nyuki sio kumiliki nyuki
kwenye mizinga peke yake bali ni pamoja na kuchagua eneo la kufugia,
kulitunza eneo hilo kwa kutokukata miti hovyo, na kuongeza au kupanda
mimea ifaayo kwa nyuki. Nyuki wanahitaji mbochi (nectar) na chavua
(pollen) ili waweze kutengeneza masega na kuweka asali ambayo ni
chakula chao. Eneo likiwa na mimea duni uzalishaji wa asali nao utakuwa
hafifu na hivyo umuhimu wa dhana nzima ya uhifadhi unajitokeza wazi.

Ufugaji nyuki hapa nchini hutegemea mimea ambayo kwa sehemu


kubwa ni ya uoto wa asili ingawa hata mimea ya mashambani na miti ya
kupanda, ina mchango katika kuboresha ufugaji nyuki na uzalishaji
wake. Kwa ufupi, ufugaji nyuki unategemea mazingira yaliyo bora na
utunzaji wa makundi ya nyuki. Mazingira bora hutoa matokeo bora.
Mfano katika nchi za ulaya wastani wa uzalishaji kwa mzinga mmoja ni
kilo 25 za asali; wakati hapa Tanzania wastani wa uzalishaji ni kilo 7 kwa
mzinga wa asili na kilo 15 kwa mzinga wa kisasa. Hii ni dhahiri kwamba
sehemu nyingi katika nchi yetu hatujaweza kutunza makundi yetu ya
nyuki kwa utaalamu unaotakiwa. Hata hivyo, yapo baadhi ya maeneo
ambako wafugaji nyuki huvuna hadi kilo 25 kwa kila mzinga.; na hapa
natumia fursa hii kuwapongeza.

Naamini tukizingatia utalaamu na tukiwa na malengo ya uzalishaji na


kwa kila mdau kuhakikisha mizinga yote inakuwa na makundi imara ya
nyuki, tunaweza kuzalisha na kuongeza wastani wa uzalishaji kwa
mzinga. Katika suala la kuboresha mazingira yakiwemo ya kufugia nyuki,
napenda kupongeza jitihada zinazofanywa na Mradi wa LVEMP II za
kuhifadhi raslimali za asili za bonde la Ziwa Victoria kwani, zaidi ya
kusaidia kutunza vyanzo vya maji, mazingira hayo yaliyoboreshwa
yanafanywa kuwa maeneo bora kwa ufugaji nyuki. Tumeona matunda ya
jitihada hizo kwa kuwepo vikundi kadhaa vya ufugaji nyuki katika eneo
hili. Nimeambiwa kuwa jumla ya vikundi 22 vyenye mizinga 2080
vimeanzishwa hapa Itilima kwa msaada wa LVEMP II. Tunawapongeza
sana na tunawashauri muendeleze mafanikio yaliyokwisha patikana. Hii
iwe ni sehemu ambayo watu wengine watakuja kujifunza kinachofanyika
hapa na kukipeleka maeneo mengine.

6
Ndugu wananchi,

Ni ukweli uliodhahiri kwamba ufugaji nyuki unawapa wananchi shughuli


mbadala na hivyo kupunguza utegemezi mkubwa wa moja kwa moja
kwenye misitu kama kuchoma mkaa ili kujipatia kipato. Sehemu
nyingine nchini ambako uchomaji mkaa umekithiri, tumekuwa
tukiwaambia Acha shoka, kamata mzinga ; najiuliza, hapa kwenu
tusemeje?

Ndugu wananchi,

Serikali yenu itahakikisha inawaunganisha wafugaji na walaji wa ndani


na nje. Kwa miaka takribani 11 tumekuwa na ushirikiano na soko la
Ulaya. Kila mwaka sampuli za asali kutoka maeneo mbalimbali
zinapelekwa Ulaya ambapo taarifa za maabara zinathibitisha kuwa asali
yetu ni salama kwa afya ya mlaji. Hata hivyo bado hatujaweza kulifikia
soko hilo kwa kuwa kiwango kinachosafirishwa ni kidogo. Natoa wito
kwenu wafugaji wa nyuki, wafanyabiashara na taasisi zinazojikita katika
kuongeza thamani ya mazao ya nyuki kuweza kuchangamkia fursa za
masoko ya nje. Hali hii itaongeza mwamko wa uzalishaji na wananchi
wetu kunufaika zaidi na ufugaji nyuki.

Niwakumbushe kuwa asali na mazao mengine ya nyuki yanapata bei


nzuri kutokana na takwimu au habari sahihi zinazoambatana na bidhaa.
Kwa mfano asali inauzika vizuri zaidi pale ambapo imezalishwa kwenye
uoto wa asili na mimea yake kujulikana. Hata hivyo, baadhi ya
wajasiliamali huandika kwenye Nembo za bidhaa zao za asali maneno
"asali hii haina kemikali". Ukweli ni kwamba, asali ni zao ambalo,
lenyewe linakemikali mathalani fruktose ambayo ni jumuiko la
haidrojeni, oksjeni na kaboni, zote hizi ni kemikali. Kinachopimwa
kwenye maabara ni zile tindikali nzito ambazo zimevuka kiwango cha
ustahimilivu. Ni vizuri kuweka taarifa sahihi za mahali ambapo asali
imezalishwa. Mfano, kuna walaji katika nchi zilizoendelea hupenda
kununua asali iliyozalishwa katika maeneo ya uhifadhi na ambayo
miongoni mwa jamii zinazozunguka maeneo hayo ni wafugaji.

7
Ndugu wananchi,

Ili kuboresha sekta hii ya ufugaji nyuki, hatua ya kwanza itakuwa


kuongeza uzalishaji wa asali ikiambatana na kutafuta masoko na kujenga
uhusiano wa kudumu na walaji. Hatua ya pili ni kuzalisha nta kutokana
na masega yaliyochujwa asali.

Hatua ya tatu ni kuanza kuzalisha gundi ya nyuki (propolis) na maziwa


ya nyuki (royal jelly). Mazao haya yanauzwa kwa bei kubwa na soko lipo
ndani na nje ya nchi. Naziagiza Taasisi za Utafiti za Wizara zishirikiane
na wafugaji nyuki katika kufanya utafiti ili kupata teknolojia sahihi
kuweza kuzalisha mazao haya kwa ufanisi.

Natumia nafasi hii kuwataka wataalamu wa Ufugaji Nyuki kote nchini


kutoa ushauri kwa wafugaji nyuki unaozingatia usimamizi wa makundi
ya nyuki, uchakataji wa mazao ya nyuki na kuweka kumbukumbu sahihi
za ufugaji nyuki.

Mambo haya yakizingatiwa yataongeza uzalishaji, ubora na kukubalika


kwa mazao yetu sokoni. Niwaombe Wafugaji Nyuki; mjenge mazoea ya
kutoa taarifa sahihi na kwa wakati, kuhusu changamoto mnazokumbana
nazo katika shughu;i zenu za ufugaji nyuki ili kuiwezesha serikali
kuandaa mipango ya utekelezaji kwa ajili ya kuboresha sekta. Hivi punde
tutaanza kukusanya maoni kuhusiana na maboresho ya Sera yetu ya
Ufugaji Nyuki. Kwa hiyo taarifa sahihi zitasaidia katika kuandaa mipango
thabiti ya kukuza sekta hii ya ufugaji nyuki.

Mwisho

Ndugu wadau wa ufugaji nyuki na wananchi kwa ujumla, naomba nitoe


wito kwenu, kuwa tutumie vema fursa zilizopo katika maeneo yetu
kujiendeleza kiuchumi ikiwa ni pamoja na shughuli za ufugaji nyuki.

Bila shaka fursa nilizozizungumzia leo katika ufugaji nyuki na umuhimu


wa ufugaji nyuki katika kuhifadhi mazingira itakuwa kichocheo kwenu
kushiriki katika kutengeneza Tanzania ya Viwanda na yenye uchumi wa
kati.

8
Mwisho kabisa, ninawashukuru wote mlioshirikiana nami siku hii ya leo
katika kutundika mizinga ya nyuki hapa kijijini Isengwa. Nina imani,
eneo hili litakuwa pia shamba darasa kwa wananchi kuja kujifunza na
kuweza kuchukua hatua bora za ufugaji nyuki. Nawashukuru wadau
mlioonyesha bidhaa za ufugaji nyuki na huduma mnazotoa. Aidha,
nikushukuruni viongozi wa mkoa wa Simiyu kwa ushiriki wenu.

Asanteni kwa kunisikiliza

You might also like