Professional Documents
Culture Documents
Ndugu,
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma,
Kaimu Mkurugenzi wa Utalii,
Mtaalamu Mwelekezi,
Wawakilishi wa Asasi mbalimbali za Sekta ya Utalii Kanda ya
Kati,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Ninayo furaha kubwa kujumuika pamoja nanyi leo katika warsha hii
muhimu ya kuendeleza mchakato wa kupitia upya Sera ya Taifa ya Utalii
ya mwaka 1999. Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wote
mnaoshiriki warsha hii iliyoandaliwa mahsusi kwa ajili ya kukusanya maoni
yatakayojumuishwa katika Sera mpya ya Taifa ya Utalii. Ni matumaini
yangu kuwa mtashiriki kikamilifu kutoa maoni yenu ili tuweze kuwa na dira
nzuri ya sekta hii yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa
taifa letu. Ninatambua kuwa, warsha hii imeshirikisha wadau wa utalii
kutoka mikoa minne ya Kanda ya Kati ambayo ni; Dodoma, Morogoro,
Singida na Tabora.
Ndugu Washiriki,
Ikumbukwe kuwa, Sera ya Taifa ya Utalii iliyopo ilifanyiwa mapitio kwa
mara ya mwisho mwaka 1999 ambapo ni takribani miaka 18 iliyopita.
Katika kutambua hilo, Wizara imeanza kupitia upya Sera hii ili kuhakikisha
Sekta ya Utalii inakidhi changamoto zinazotokana na mabadiliko
mbalimbali yanayotokea duniani yakiwamo ya teknolojia, kijamii,
kiuchumi, kisiasa na mazingira.
2
Ndugu Washiriki
Ili nchi ifaidike na biashara ya utalii ni lazima wananchi wake wengi kadiri
inavyowezekana washiriki kwenye biashara ya utalii. Hivyo, tunahitaji Sera
ya Utalii itakayowezesha ushiriki wa wananchi wetu katika biashara hii,
hususan katika ngazi ya biashara ndogo na za kati (SMEs), katika Sekta ya
utalii.
Ndugu washiriki,
Wote tunaelewa ya kuwa sekta ya Utalii ni moja wapo ya sekta zinazokua
kwa kasi na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi.
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa, sekta ya utalii inachangia 17.5% ya
Pato la Taifa (GDP) na huliingizia Taifa fedha za kigeni (asilimia 25).
3
Ukuaji wa sekta hii, umedhihirika pale ambapo katika miaka ya hivi
karibuni mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka Dola za
Kimarekani bilioni 1.7 mwaka 2012 hadi kufikia Dola za Kimarekani bilioni
2.1 mwaka 2016. Ongezeko la mapato hayo ni kutokana na kuongezeka
kwa idadi ya watalii kutoka 1,077,058 mwaka 2012 hadi kufikia watalii
1,284,279 mwaka 2016.
Ndugu washiriki,
Tuna kazi kubwa iliyoko mbele yetu, ni vyema sasa kuweka mawazo yetu
kwa pamoja katika kipindi cha masaa machache yajayo na kuibuka na
maoni mazuri yatakayojumuishwa kwenye Sera mpya ya Taifa ya Utalii.