Professional Documents
Culture Documents
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa
siku hii ya leo. Aidha, ninakushukuru kwa kukubali mwaliko wa kuja kuzindua Mradi
Kuimarisha usimamizi wa Maliasili na Kuendeleza Utalii Ukanda wa Kusini ujulikanao
kama Resilient Natural Resource for Tourism and Growth (REGROW).
Napenda pia kutoa shukrani za pekee kwa Benki ya Dunia kwa kukubali kutoa Mkopo
wa masharti nafuu kwa ajili ya mradi huu. Namshukuru sana mama Bella Bird,
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia
ambaye leo ameambatana na mama Julia Bucknall, Mkurugenzi wa Mazingira na
Maliasili wa Benki ya Dunia, kwa kutenga muda wao kuja kuungana nasi katika tukio hili
muhimu. Ninawashukuru Waheshimiwa Mawaziri wenzangu, Wakuu wa Mikoa na
Wabunge kwa kukubali kuja kutuunga mkono. Aidha, napenda niwashukuru watalaam
na watendaji wa Wizara na Taasisi zote walioshiriki katika maandalizi na hatimaye
kukamilisha kuanza kwa mradi huu. Napenda niwashukuru sana wadau wa uhifadhi na
utalii na wananchi wa mikoa ya Iringa na Mbeya, kwa ushirikiano wa hali na mali katika
kufanikisha maandalizi ya mradi huu, ambao hatimaye leo utazinduliwa rasmi.
Mradi huu utagharimu jumla ya Dola za Marekani Milioni 150 ambazo ni sawa Shilingi
bilioni 340. Aidha, Mradi utatekelezwa kwa muda wa miaka sita kuanzia mwaka huu wa
fedha 2017/2018. Kwa heshima na taadhima naomba sasa nikukaribishe uweze
kuongea na wananchi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, mama yetu Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, KARIBU SANA.