You are on page 1of 8

WARSHA YA KUKUSANYA MAONI TOKA KWA WAKAZI WA

KANDA YA KATI KWA AJILI YA KUBORESHA RASIMU YA


SERA MPYA YA MISITU YA MWAKA 2016

HOTUBA YA KUFUNGUA WARSHA ILIYOTOLEWA NA NAIBU


KATIBU MKUU WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII MHE.
DKT. ALOYCE K. NZUKI, DODOMA TAREHE 11 JULAI, 2017

Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dkt. Ezekiel E.


Mwakalukwa
Wakurugenzi, toka Wizara ya Maliasili na Utalii,
Mwakilishi wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa
Mataifa (FAO), Bw. Geofrey Bakanga
Wajumbe wa Kikosi Kazi
Wadau wa Misitu
Waandishi wa habari
Mabibi na Mabwana

Ninashukuru kwa kunialika na kwa heshima ya kufungua


warsha hii. Nikushukuru wewe Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki
kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa
Mataifa (FAO) kwa kuandaa warsha hii muhimu. Warsha hii
inayokutanisha wadau wa sekta ya misitu na wajumbe wa
Kikosi Kazi cha kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Misitu ni ya
kwanza kati ya warsha zaidi ya tano zinazotarajiwa kufanyika
katika kanda mbalimbali nchini.

Aidha, nawashukuru kwa dhati wadau wote wa misitu mliopo


hapa kwa kukubali kuja kushiriki kwenye Warsha hii. Natambua
kuwa mna majukumu mengine katika kujenga taifa letu lakini
kwa kutambua umuhimu wa sekta ya misitu mmekukabli
kushiriki ili kutoa maoni yenu kuhusu mapitio na maboresho ya
1
Sera mpya ya Misitu. Nina imani kuwa umahiri wenu utasaidia
sana kuboresha Sera hii mpya ya Taifa ya Misitu inayotarajiwa
kutoa mwelekeo mpya wa uhifadhi wa rasilimalizetu za misitu
hapa nchini.

Ndugu Washiriki,
Tanzania imebahatika kuwa na rasilimali ya misitu ambayo ni
muhimu kimazingira, kiuchumi na kijamii na hatuna budi
kuhakikisha zinalindwa na kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi
cha sasa na kijacho. Kulingana na taarifa ya Tathimini na
Ufuatiliaji wa Rasilimali za Misitu (National Forest Resources
Monitoring and Assessment NAFORMA) ya mwaka 2015,
rasilimali za misitu nchini zinakadiriwa kuwa takribani hekta
milioni 48 sawa na asilimia 55 za eneo la Tanzania Bara. Kati ya
hekta hizo, asilimia 93 ni misitu ya matajiwazi (woodlands) na
asilimia saba ni misitu iliyofunga (closed forests). Rasimali hii
ya misitu ina madhumuni ya kuzalisha mazao ya misitu na
kulinda mazingira. Kuna jumla ya hekta milioni 20 ya misitu
iliyotengwa kwa kuzalisha mazao ya misitu na hekta milioni 28
kwa ajili ya misitu ya kulinda mazingira inayojumuisha Hifadhi
za Taifa, Misitu ya Hifadhi Asilia, Misitu ya Lindimaji, na Mapori
ya Akiba kwa ajili ya uhifadhi wa Wanyamapori.

Ndugu Washiriki,
Umiliki na usimamizi wa misitu nchini umegawanyika katika
mamlaka zifuatavyo: Serikali Kuu hekta milioni 19.24 ambayo
ni asilimia 34.5; Serikali za Mitaa kupitia Halmashauri za Wilaya
hekta million 3.1 ambayo ni asilimia 6.5; misitu iliyo katika
ardhi za vijiji ni hekta 21.9 ambayo ni asilimia 45.7; na watu
binafsi na vikundi wanasimamia hekta milioni 3.5 ambayo ni
asilimia 7.3. Eneo lililobaki lenye ukubwa wa hekta 2.87 sawa
na asilimia 6.0 ni ardhi huria. Kutokana na takwimu hizo,
mtaona kuwa rasilimali ya misitu ya nchi yetu ina wadau wengi
2
na hivyo kuwa na mchango mkubwa kwenye maendeleo ya
taifa.

Ndugu Washiriki,
Umuhimu wa misitu kwenye maendeleo ya taifa unatokana na
mchango wake kwenye Pato la Taifa. Rasilimali za misitu
inakadiriwa kuchangia asilimia 3.5 kwenye Pato la Taifa (GDP)
na asilimia 10 ya biashara ya nje. Sekta ya misitu inachangia
kwa takribani asilimia tatu ya ajira rasmi nchini; na ajira isiyo
rasmi inafikia watu milioni tatu. Aidha, misitu inachangia kwa
kiasi kikubwa katika uchumi wa Taifa kwa kutoa zaidi ya
asilimia 75 ya vifaa vya kujengea na huchangia zaidi ya asilimia
90 ya nishati inayotumika nchini. Misitu hii inatupatia mbao,
kuni, mkaa, chakula, malisho ya mifugo, dawa, kivuli na makazi
ya wanyama. Hivyo utaona kuwa mchango halisi wa misitu ni
mkubwa kuliko ule unaowasilishwa katika mfumo rasmi wa
takwimu za uchumi. Vilevile, misitu ni muhimu katika kuhifadhi
bioanuai, udongo na vyanzo vya maji ambavyo ni chanzo
kikubwa cha kufanikiwa kwa miradi mingine mikubwa ya
maendeleo kwa nchi yetu.

Ndugu Washiriki,
Sera ya Taifa ya Misitu ina wajibu wa kusaidia jamii au wadau
kunufaika na rasilimali ya misitu ili kufikia malengo ya
maendeleo kitaifa na kimataifa, kukabiliana na changamoto za
kimazingira kama vile mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza
uhifadhi, na kujipatia mazao ya misitu kwa matumizi mbalimbali
ya kimaendeleo. Kutokana na wajibu huu, kazi ya kuandaa Sera
ya Taifa ya Misitu ina jukumu la msingi la kuhakikisha kuwa
wadau wote wa misitu na serikali wanakubaliana kwa pamoja
kuhusu Dira, Malengo na Mikakati ya kusimamia rasimali
hizi za misitu. Aidha, Sera ni mkataba kati ya serikali na
wadau wengine unaotokana na mashauriano na
makubaliano katika kuhakikisha misitu hii inaendelea kulinda
3
mazingira na kukidhi mahitaji mbalimbali ya kijamii na malengo
ya maendeleo kwa njia endelevu.

Ndugu Washiriki,
Mwaka 1998, Serikali ilipitisha Sera ya Taifa ya Misitu
inayofanyiwa maboresho. Kwa kipindi cha nyuma Sera
iliyokuwa ikitumika ilikuwa ile ya mwaka 1953 tuliyoirithi kutoka
kwa Wakoloni na baadae kuuhishwa mwaka 1963. Sera ya
Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 iliandaliwa kufutia maboresho
ya kiuchumi, kisera na kitaasisi ambayo yalianza kufanyika
kwenye miaka ya 1980. Kutokana na maboresho hayo, Sera ya
Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 imekuwa na lengo la
kuhakikisha kuwa sekta hii ya misitu inachangia katika kuleta
maendeleo endelevu ya nchi, na kuhifadhi na kusimamia
maliasili zake kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo. Ili
kufikia lengo hilo Sera ilikuwa na madhumuni yaliyogawanyika
katika maeneo manne makuu ambayo ni:-
a) Kuhakikisha upatikanaji endelevu wa mazao na huduma za
misitu kwa kuwa na maeneo ya kutosha ya misitu
iliyohifadhiwa chini ya usimamizi madhubuti.
b) Kupanua ajira na kuongeza pato la fedha za kigeni kutokana
na maendeleo endelevu katika viwanda vilivyojikita kwenye
misitu na biashara.
c) Kuimarisha mifumoikolojia kwa kuhifadhi bionuwai ya misitu,
maeneo ya lindimaji na rutuba ya udongo, na
d) Kukuza uwezo wa taifa katika kusimamia na kuendeleza
sekta ya misitu kwa kushirikiana na wadau wengine.

Ndugu Washiriki,
Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998, pamoja na mambo
mengine, imesisitiza ushiriki wa wananchi katika upandaji na
usimamizi wa misitu ili kuongeza upatikanaji wa mazao ya
misitu. Mathalani, Wizara kwa kushirikiana na mamlaka za

4
serikali za mitaa imeendelea na shughuli za uratibu wa
utekelezaji wa dhana ya usimamizi shirikishi wa rasilimali za
misitu na nyuki katika wilaya 67 za Tanzania Bara. Hadi sasa
zaidi ya hekta milioni nane za misitu zimehifadhiwa na
kusimamiwa kisheria na serikali za vijiji kwa utaratibu huo.
Aidha, kumekuwa na juhudi za kuhifadhi maeneo ya misitu
zaidi ikiwa ni pamoja na kuanzisha misitu mipya ya hifadhi.
Uhifadhi na usimamizi wa misitu umeendelezwa kwa kuongeza
jumla ya misitu ya hifadhi 59 yenye jumla ya hekta 359,063.
Misitu 12 imepandishwa hadhi kuwa Hifadhi za mazingira Asilia
(Nature Reserves). Pia, katika kipindi hiki tumeshuhudia
kuanzishwa kwa Mfuko wa Misitu Tanzania (Tanzania Forest
Funds) ambao ulianzishwa mwaka 2012 kwa lengo la
kuhakikisha upatikanaji endelevu wa fedha ili kuwezesha
uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali hizi za misitu
hapa nchini.

Ndugu Washiriki,
Sera inayotumika hivi sasa ina takribani miaka 19 tangu
kupitishwa mwaka 1998 na kumekuwepo na mabadiliko
mbalimbali ya kiuchumi, kijamii na kimazingira yanayoendelea
kutokea ndani na nje ya nchi yetu. Mabadiliko haya hayana
budi kuzingatiwa ili kuhakikisha kila mdau wa misitu anafaidika
na uwepo wa rasilimali hii. Hivyo hitaji hili nimesababisha kuwa
na ulazima wa kuiangalia upya sera hii ili kujiridhisha kama
bado inakidhi mahitaji haya na malengo yaliyotarajiwa. Aidha,
misitu yetu bado inakabiliwa na changamoto za uharibifu
zinazochangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa shughuli
za kibinadamu ndani ya misitu hiyo na ongezeko la mahitaji ya
mazao ya misitu. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwapo na
uvamizi mkubwa wa maeneo ya misitu kwa ajili ya shughuli za
kilimo, malisho ya mifugo, uchimbaji wa madini, makazi, ukataji
haramu wa miti kwa ajili ya nishati, mbao na nguzo za ujenzi.
Mathalani, misitu imeendelea kuwa chanzo kikuu cha nishati,
5
ambapo uvunaji mkubwa wa mkaa unaathiri sana ubora wa
misitu hii. Aidha, majanga ya moto na uvunaji usio endelevu
kwa ajili ya ujenzi hasa kwenye misitu ya asili unachochea
kutoweka kwa eneo la misitu linalokadiriwa kufikia hekta
372,000 kwa mwaka. Changamoto hizi zinaashiria umuhimu wa
wadau wote kuongeza jitihada za kusimamia, kuhifadhi na
kupanda miti ikiwa ni pamoja na kuboresha utawala bora na
usimamizi wa sheria katika sekta hii ya misitu na sekta zingine
mtambuka ambazo kwa namna moja ama nyingine zinachangia
katika uharibifu wa misitu hii.

Ndugu Washiriki,
Kutokana na mabadiliko hayo mbalimbali na changamoto
kwenye sekta ya misitu, ni dhahiri Sera ya Taifa ya Misitu ya
mwaka 1998 inapaswa kufanyiwa mapitio ili kuhakikisha
usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za misitu unakidhi matakwa
ndani ya nchi na kimataifa katika viwango vyenye ubora
unaostahili. Aidha, Wizara kupitia mikutano yake na wadau
mbalimbali wa misitu walishauri kufanyika mapitio ya Sera ya
Misitu ya Taifa, Sheria na Kanuni zake ili kutatua changamoto
zinazokabili sekta hii ya misitu. Kutokana na sababu hizi Wizara
imeona umuhimu wa kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya
Misitu ambayo yatafuatiwa na kufanyika mapitio ya Sheria ya
Misitu Namba 14 ya mwaka 2002 na Kanuni za Misitu za
mwaka 2004 ili kuboresha zaidi usimamazi na matumizi
endelevu ya rasilimali za misitu nchini. Sera itakapokamilika na
kuidhinishwa na Serikali, itasaidia kubuni na kuandaa mikakati
na mbinu za kutafuta fedha za kutekeleza mikakati ikiwa ni
pamoja na kujenga uwezo na kuboresha mawasiliano na wadau
mbalimbali wa misitu. Pia utekelezaji wa Sera unatarajiwa
kuendeleza ushiriki wa wadau kupitia Programu ya Taifa ya
Misitu ili kuwezesha kubuni, kufafanua, kuratibu na kuoanisha
utekelezaji wa mikakati yake na sera za sekta nyingine. Kazi hii
ya kufanya mapitio ya Sera inapaswa kukamilika Mwezi Septemba
6
mwaka huu wa 2017 ili kuwezesha hatua nyingine za kufanya
mapitio ya Sheria ya Misitu na Kanuni zake ziweze kufanyika. Nina
imani kuwa shughuli ya kukusanya maoni ya wadau itakamilika
kabla ya kwisha kwa mwezi wa Agosti 2017 ili kazi ya kutayarisha
rasimu ya Sera ikamilike kwa wakati uliopangwa.

Ndugu Washiriki,
Napenda kuwaomba kwamba mtumie muda huu mliopo hapa
mpate kuchambua na kuainisha kwa undani masuala yanayoikabili
sekta ya misitu ili tuweze kuwa na Sera bora yenye dira na malengo
yatakayotuwezesha kuwa na mikakati na sheria zitakazo tuwezesha
kukabiliana ipasavyo na changamoto nilizozianisha hapo awali.
Aidha, niwaombe wadau wote kutoa mawazo yenu kwa uwazi na
bila woga ili kuhakikisha rasilimali hii muhimu kwa nchi yetu inapata
msukumo wa uhifadhi unaostahili. Ili kuongeza uwazi na ufanisi
katika kuchangia maoni haya, itakuwa vema kama wadau hawa
watapatiwa ile rasimu ya sera ya mwisho kabisa ya mwaka jana ya
Mwezi Octoba 2016, ili iwe rahisi kwao kuweka maoni yao mapya
na kuepuka kurudia mambo ambayo tayari yalishazingatiwa huko
nyuma. Hivyo nikuagize Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki,
hakikisha unawapatia wadau hawa rasimu hiyo ili kazi yao iwe
rahisi. Itakuwa vizuri pia ukizingatia kuwa wadau ulionao si waliopo
hapa nchini peke yao, natambua wapo pia wadau wengine walioko
nje ya nchi, ambao wamekuwa msitari wa mbele katika kusadia
uhifadhi wa misitu yetu hapa nchini. Nao pia ni vema ukiwatumia ili
waweze kuweka maoni yao.
Aidha, wekeni utaratibu kwenye Tovuti za taasisi mbalimbali ziweze
kupokea maoni.

Ndugu Washiriki,
Nichukue fursa hii tena, kwa niaba ya Wizara kulishukuru Shirika la
Kilimo la Chakula la Umoja wa Mataifa kwa mchango wake katika
kufanya mapitio ya Sera yetu ya Taifa ya Misitu. Serikali inathamini
na itaendelea kushirikiana na Shirika hili katika kuendeleza misitu
7
kwa manufaa ya nchi na dunia kwa ujumla. Aidha, ninatambua kazi
hii bado ni kubwa. Nimesikia mnayo malengo ya kuwafikia wadau
wengi iwezekanavyo walioko katika kanda saba zilizopo nchini,
ikiwemo kanda ya kati ambayo leo mmeanzia kazi hii. Kwenda kote
huko kutahitaji rasilimali fedha. Hivyo natoa wito kwa wadau
wengine kuiga mfano wa FAO, kushirikiana na Idara ya Misitu na
Nyuki ili kuhakikisha malengo haya ya kuwafikia wadau wote
yanafanikiwa. Tayari nimeshatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa
Idara ya Misitu na Nyuki kuhakikisha anawasiliana na wadau wote
ikiwemo taasisi zetu zilizo chini ya wizara ili kuhakikisha fedha
zinazohitajika kukamilisha kazi hii zinapatikana, na kwamba kazi hii
inakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.

Ndugu Washiriki,
Baada ya kusema maneno haya ya utangulizi, Napenda sasa
kutamka kuwa Warsha ya Wadau ya kukusanya maoni ya kufanya
mapitio na maboresho ya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998
imefunguliwa rasmi.

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

You might also like