You are on page 1of 7

HOTUBA YA UTEKELEZAJI WA MAFANIKIO YA BARAZA LA

MADIWANI KWA KIPINDI CHA MIAKA MITANO (2010-2015)


ILIYOTOLEWA WAKATI WA KUVUNJA BARAZA TAREHE 06-07-2015
KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA ARNATOGLOU
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilianzishwa rasmi Mwezi wa Februari 2000, hivyo kufikia
mwaka 2015 sasa imetimiza miaka kumi na tano (15). Katika kipindi chote hicho zimekuwepo
awamu tatu za Uongozi wa Waheshimiwa Madiwani, ambao ni kuanzia mwaka 2000-2005,
2005-2010 na 2010-2015. Nachukua fursa hii kuwapongeza Madiwani na Watendeaji wote
ambao kwa pamoja walikaa na kuweka mipango mbalimbali ya kimaendeleo ya Halmashauri ya
Manispaa ya Ilala.
Baraza la Madiwani linalomaliza muda wake wa Uongozi leo tarehe 6/07/2015 ni awamu ya tatu
ya Uongozi ulioanza kazi mwaka 2010. Naamini kuwa kila mmoja atakubaliana na mimi kuwa
yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki cha miaka mitano (5). Kupitia
miongozo iliyopo ya kuandalia Mipango na Bajeti ikiwemo-Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2010, MKUKUTA, MKURABITA, Malengo ya malenia na Maelekezo ya Viongozi wa
Kitaifa na Baraza la Madiwani, Halmashauri imetekeleza vyema azma ya kupeleka maendeleo
kwa wananchi wake na kwa mujibu wa Dira ya Halmashauri isemayo;
Kuwa na Jamii yenye maisha bora ifikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Manispaa ya Ilala kupitia Idara mbalimbali na Vitengo vyake imeweza kutekeleza Dira yake kwa
ufanisi. Mafanikio haya yanaonekana katika maeneo yafuatayo;
UKUSANYAJI WA MAPATO
Ili kuweza kutekeleza majukumu yake, Halmashauri inapaswa kuhahikikisha inakusanya mapato
ya kutosha, hususani ya ndani kuwezesha utoaji wa huduma kwa wananchi wake kupitia
utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwa kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano (5)

Halmashauri ya Manispaa imekuwa ikiongeza juhudi za kukusanya mapato yake ya ndani. Katika
mwaka wa fedha wa 2010/2011 Halmashauri ilikisia kukusanya jumla ya Sh. 16,110,130,000,
mapato halisi yaliyokusanywa mwisho wa mwaka yalifikia Sh. 13,059,508,452 sawa na Asilimia
81% ya lengo lake. Kiwango hicho kimekuwa kinaongezeka na kufikia mwaka huu wa fedha
2014/2015, makisio yalikuwa ni Sh. 30,450,000,000 hadi kufikia Juni, 2015 makusanyo halisi
yamefikia Sh. 30,862,178,729.90 sawa na Asilimia 103 ya lengo la mwaka. Aidha kwa mwaka
unaofuata wa 2015/2016 Halmashauri imepanga kukusanya Sh. 54,258,100,000 kutoka mapato ya
ndani.

Jambo kubwa linalochangia mafanikio haya ni kuboreshwa kwa zoezi la kukusanya

Takwimu za walipa kodi, mpango unaolenga kubaini idadi ya walipa kodi wa Halmashauri na
hivyo kuwa na makadirio halisi ya mapato. Aidha kutokana na kukua kwa Tekinolojia ya
mawasiliano Manispaa imeanza kuwasiliana na Walipa kodi wake kwa njia ya simu zao za
mkononi kwa ajili ya kuwahimiza na kuwakumbusha ulipaji wa Kodi/Tozo na Ushuru mbalimbali.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Usimamizi mzuri ambao umekuwa ukifanywa na Waheshimiwa Madiwani katika kuhakikisha
kuwa kanuni za matumizi ya fedha zinazingatiwa, umeiwezesha Halmashauri kuendelea kupata
Hati safi za Ukaguzi wa Mahesabu. Uthibitisho wa karibu ni taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali ya mwaka wa fedha wa 2014/15 ambapo Manispaa ya Ilala ni miongoni mwa
Halmashauri zilizopata hati safi ya Mahesabu.
MASOKO
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Manispaa ya Ilala ina jumla ya masoko 18, masoko makubwa ni Matano (5), masoko
madogomadogo ni 8 na maeneo matano (5) yasiyotumika kikamilifu. Kati ya masoko matano
makubwa, masoko matatu (3) ya Kisutu, Ilala na Buguruni ni masoko yaliyojengwa miaka ya
1960 hivyo kwa sasa hayakidhi mahitaji makubwa ya Wafanyabishara walioko katika masoko
hayo. Katika kipindi hiki cha miaka mitano Halmashauri ya Manispaa imeweka mazingira
mazuri kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Sekta za Biashara na Masoko kwa lengo la kuzalisha
ajira, hususani kwa wafanyabiashara wadogo. Halmashauri imeweza kuanisha maeneo 17 ya
kuendelezwa ikijumuisha shughuli za wafanyabiashara wadogo. Lengo kuu likiwa kuwafanya
wafanyabiashara wadogo kuondokana na uchuuzi mdogo mdogo na kuwa wajasiriamali. Aidha
2

Halmashauri imesaini Mkataba na Benki ya Rasilimali (Tanzania Investment Bank-TIB) kujenga


soko la kisasa la Kisutu, baadaye masoko ya Buguruni na Ilala yataendelezwa.

ELIMU YA MSINGI NA SEKONDARI

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,


Manispaa ya Ilala imefanikiwa katika utoaji wa Elimu ya Msingi na Elimu ya Sekondari kwa
wananchi wake. Katika kipindi hiki cha miaka mitano jitihada mbalimbali zimefanyika za
kukabiliana na changamoto zinazoikabili Sekta ya Elimu. Pamoja na juhudi za Serikali Kuu na
Halmashauri, wadau mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kuboresha Sekta hii. Mashirika ya simu
ya Vodacom Foundation, Tigo, Benki Kuu na KCB ni miongoni mwa waliochangia samani katika
shule mbalimbali za Msingi. Aidha Ofisi yangu kupitia Mayors Ball na Mpango uliobuniwa na
Mhe Diwani wa Kipawa umezipatia baadhi ya shule madawati. Mpango wa Mnazi Mkinda wa
kuibua vipaji mbalimbali kwa wanafunzi wa shule ya Msingi nao umechangia kuboresha sekta hii.
Kwa takwimu zilizopo katika kipindi husika madawati 32,021 yamenunuliwa katika jitihada za
kukabiliana na upungufu wa madawati. Vyumba vya madarasa 111 na Matundu ya vyoo 2109
yamejengwa katika shule za msingi. Watoto 4,876 wa elimu ya awali na 21,798 wa elimu ya
msingi waliandikishwa kuanza masomo mwaka 2015, Hali hiyo imechangia ufaulu wa shule ya
msingi kupanda kutoka chini ya Asilimia 58 mwaka 2010 kufikia Asilimia 70.5 mwaka 2014.
Aidha ujenzi wa vyumba 76 vya madarasa na maabara 154 katika shule za Sekondari umekamilika
kwa asilimia 98. Nachukua nafasi hii kuwapongeza Madiwani wajumbe wa Kamati iliyosimamia
masuala ya Elimu, Mkurugenzi wa Manispaa na Wataalam wake kwa kuhakikisha mipango ya
elimu inatekelezwa kwa ufanisi.
HUDUMA ZA AFYA
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Katika eneo la Afya yapo mafanikio makubwa yaliyofikiwa. Kwa mujibu wa Takwimu
zilizokuwepo mwaka 2010 kulikuwa na jumla ya zahanati, vituo vya Afya na Hospital 19
3

ambapo hadi kufikia mwaka 2015 vimeongezeka na kufikia 29. Aidha katika kipindi hiki baadhi
ya Hospitali na Zahanati zimeingizwa kwenye mchakato wa kupandishwa hadhi. Hospitali ya
Amana imepanda hadhi na sasa ni Hospital ya Mkoa ambapo Kituo cha Afya Mnazi Mmoja
kimepandishwa hadhi kuwa Hospital. Zahanati ya Pugu Kajiungeni inaendelea na mchakato wa
kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya. Kumekuwa na kuimarika kwa ushirikiano kati ya Idara
ya Afya na Wadau wa Afya hususan Taasisi zinazojihusika na utoaji wa Tiba. Utoaji wa Chanjo
kwa Watoto na Kina Mama Wajawazito umevuka lengo la Kitaifa la asilimia 90 na kufikia
asilimia 100 kwa chanjo karibu zote. Mafanikio haya yote yanaonesha ni jinsi gani Waheshimiwa
Madiwani pamoja na Watendaji wameweza kuelekeza jitihada zao katika eneo hili muhimu la
huduma linalogusa moja kwa moja maisha ya Wananchi, kwani inaaminika kuwa Mtu mwenye
Afya bora anao mchango mkubwa katika familia yake na Taifa lake.
USAFI NA HIFADHI YA MAZINGIRA
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Katika eneo hili, Halmashauri inaendelea na juhudi za kuliweka Jiji katika hali ya usafi. Takwimu
zinaonesha wakazi wa Manispaa ya Ilala wanazalisha tani 1,100 za taka ngumu kila siku wakati
uwezo wa kuzoa na kusafirisha hadi dampo la Kigogo Fresh katika Kata ya Pugu ni Tani 676
kufikia Juni, 2015 kiwango hicho ni sawa na Asilimia 61% ya uzalishaji. Mwaka 2010
Halmashauri pamoja na Wakandarasi wengine wa kuzoa taka waliweza kuzoa wastani wa Asilimia
50% za taka ngumu kwa siku. Aidha Halmashauri ina uwezo wa kufagia Km. 136 za barabara
kwa siku dhidi ya Km. 126 za mwaka 2010. Uwezo huu mdogo wa uzoaji wa taka umechangiwa
kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa vitendea kazi hususani, malori yenye uwezo mkubwa wa kuzoa
taka. Baraza hili la Madiwani linavunjwa likiwa tayari limetoa idhini ya kukopa Sh. 2.55 Bilioni
kwa ajili ya kununua malori 17 ya kusafirisha taka ili kuboresha zaidi hali ya usafi Jijini.
Kwa kushirikiana na Sekta binafsi Halmashauri inaendelea kutunza jumla ya Ha. 137.4 za misitu
katika bonde la Zingiziwa, Kinyerezi, Kivule dhidi ya majanga ya moto na uvunaji usio endelevu
wa mazao ya misitu. Vikundi 7 vinaendelea na ufugaji nyuki kutumia mizinga ya 157
iliyotundikwa katika misitu ya asili, na ya kupandwa katika maeneo mbalimbali ya Manispaa.
Kupitia Kamati za mazingira za Kata, Wananchi wamekuwa wakielimishwa juu ya umuhimu wa

kutunza Vyanzo vya maji na Uoto wa asili hususani kwenye maeneo ya miinuko.

MIPANGOMIJI
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Kama inavyofahamika Manispaa ya Ilala ndiyo yenye kubeba taswira ya Jiji la Dar es Salaam,
hivyo katika kipindi hiki cha miaka mitano (5) jitihada zimefanyika za kuhakikisha kuwa ujenzi
wa nyumba na majengo unazingatia Sheria na kupunguza makazi holela. Kumekuwa na mipango
ya kubadilisha taswira ya eneo la Manispaa ambapo mipango ya uendelezaji upya wa maeneo
mbalimbali imeidhinishwa. Jumla ya viwanja 29,243 vimemilikishwa kwa wananchi na viwanja
9,123 vimepimwa katika maeneo ya umma, leseni mpya za makazi 1,568 zimesajiliwa. Aidha
wananchi 62,000 wamepata elimu ya sheria za ardhi, Mipango miji na matumizi bora ya ardhi.
UJENZI WA MIUNDOMBINU
Kupitia Idara ya Ujenzi, Halmashauri ya Manispaa imeweza kuboresha zaidi miundombinu yake
ya Barabara, ambapo imeweza kuongeza urefu wa Km. 71.31 za barabara za lami kutoka jumla ya
Km. 190.32 zilizokuwepo mwaka 2010 kufikia Km. 261.63 mwaka 2015. Urefu wa barabara za
Changarawe umeongezeka kwa Km. 56.77 kutoka Km. 76.6 za mwaka 2010 kufikia Km. 133.37
mwaka 2015 na barabara za udongo zenye urefu wa Km. 638.95. zimetengenezwa. Aidha,
makalavati 37 nayo yameweza kujengwa. Katika kipindi hiki Manispaa imeweza kununua Greda
mbili (2) kwa njia ya mkopo ikilenga kuhakikisha kuwa barabara zake zote zinapitika katika
vipindi vyote vya mwaka.
HUDUMA ZA MAJI
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Sote tunatambua kuwa maji ni rasilimali muhimu. Katika kipindi hiki cha miaka mitano (5)
jitihada za kusambaza maji safi na salama katika Manispaa zimefanyika ambapo Halmashauri
imechimba visima virefu 42 na kufanya jumla ya visima vyote vilivyopo kufikia 247. Visima
vifupi nane (8) vilichimbwa na kufikia jumla ya visima 69. Vituo vya kuchotea maji 1,239

Mifumo 9 ya kuvuna maji ya mvua imejengwa. Vikundi vya watumia maji 15 na kamati za maji
50 zimeundwa. Hadi kufikia Juni, 2015 idadi ya wakazi wanaopata maji safi na salama
wanaohudumiwa na visima vya Halmashauri wamefikia Asilimia 52% ya wakazi wote wa
Manispaa wanaokadiriwa kuwa 1,220,611 (Sensa ya 2012).
MAENDELEO NA USTAWI WA JAMI
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Katika kipindi cha kuanzia 2010 hadi 2015 Manispaa ya Ilala imeendelea kutekeleza mipango
mbalimbali ya Ustawi wa Jamii ambapo upo mfumo mzuri wa kuendeleza vikundi vya Wanawake
na Vijana. Makundi haya yamekuwa yakinufaika kwa kupatiwa mikopo kutoka Benki yetu ya
DCB ambapo Halmashauri ina hisa, pia Mfuko wa Wanawake na Vijana umeendelezwa kwa
Halmashauri kutenga fedha kukopesha makundi hayo. Hadi kufikia Juni 2015 vikundi 37 vilifikia
hatua za mwisho za kukopeshwa mitaji ya biashara. Aidha Manispaa ya Ilala imeweka mfumo
mzuri wa kuhudumia Watoto waishio katika mazingira hatarishi kupitia Timu ya Ulinzi na
Usalama wa Mtoto. Dawati la kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu
lililofunguliwa Hospital ya Amana limewezesha kuokoa idadi kubwa ya Watoto waliokuwa
wakifanyiwa ukatili wa kijinsia.
MAHUSIANO NA WADAU
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Tunapopima mafanikio ya Manispaa ya Ilala hatuwezi kuacha kuzungumzia eneo la mahusiano.
Dhana ya maendeleo kwa njia ya kushirikisha Wadau wakijumuisha Wafadhili imeendelea
kutekelezwa ndani ya Manispaa ya Ilala. Ofisi ya Mstahiki Meya imeweza kushawishi Shirika la
KOICA kujenga Hospitali eneo la Chanika. Mkataba wa Makubaliano ya kuanza ujenzi
umeshasainiwa. Ujenzi wa Hospital hii utasaidia kusogeza huduma karibu na Wananchi na
kupunguza msongamano wa Wagonjwa katika Hospitali ya Amana. Katika kipindi hiki mipango
ya Maendeleo inayoibuliwa imekuwa Shirikishi. Kata zote 26 zimeunda Kamati ya wananchi
zenye jukumu kuu la kuibua vipaumbele vya ngazi ngazi ya Kata ambavyo baada ya kuidhinishwa
na Kamati za Maendeleo za Kata inajumuishwa katika Mipango na Bajeti ya Halmashauri ambako
inatengewa fedha. Aidha Halmashauri imesimamia na kuendeleza mahusiano yaliyopo kati ya
6

Manispaa ya Ilala na Mji wa Kokkola ulioko Finland.

KUTANGAZA SHUGHULI MBALIMBALI ZA HALMASHAURI


Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeweza kuweka mahusiano mazuri na vyombo vya Habari
ambavyo vimekuwa vikiuhabarisha umma masuala mbalimbali yanayotokea na yanayoihusu
Manispaa ya Ilala. Katika kujitangaza huko Halmashauri inalo Jarida lake ambalo limekuwa
likitangaza kazi mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa. Aidha kupitia mitandao ya kijamii
Manispaa imeanzisha Blog - Habari ilala.Blogspot.Com ambayo hadi kufikia Juni 2015 jumla ya
wanaoingia katika mtandao huo imefikia 30,000 kutoka pande zote za dunia.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Napenda kumalizia hotuba yangu kwa kusema kwamba, Baraza hili la Madiwani la Awamu ya
tatu ya Uhai wa Halmashauri linavunjwa likiwa lina mambo ya kujivunia hususani katika kuandaa
mazingira endelevu ya Uwekezaji, Kuongezeka kwa mapato ya ndani, Uboreshaji wa huduma za
Kiuchumi, elimu na Afya. Nampongeza Mkurugenzi na timu yake ya wataalam, Waheshimiwa
Madiwani wote, Uongozi wa Wilaya, Uongozi wa Mkoa na wataalam wake. Ushirikiano wa
karibu wa timu hii umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio tunayoyaona kwa sasa. Naamini
Awamu ya nne ya Uongozi unaokuja utaanzia mahali pazuri.
Ahsante sana kwa kunisikiliza.
Jerry Silaa
MEYA WA MANISPAA
HALMASHAURI YA MANISPAA YA ILALA

You might also like