You are on page 1of 26

wilsonpastory@gmail.

com

TUUNGANE KWA PAMOJA KUTEKELEZA


MALENGO 17 YA MAENDELEO
ENDELEVU

Makala hii imeandikwa na WILSON PASTORY.

1|Ukurasa
wilsonpastory@gmail.com

UTANGULIZI

Ni takribani miaka miwili sasa tukiwa tunaelekea mwaka wa tatu, tangu Umoja wa Mataifa (UN)
upitishe Malengo ya Maendeleo Endelevu maarufu kwa lugha ya kiingereza kama Sustainable
Development Goals, kwa ufupi SDGs. Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yaliletwa na
Umoja wa Mataifa (UN) kama mwendelezo wa Malengo ya Milenia (MDGs) ambayo yalianza
kutekelezwa mwaka 2000 na kufikia ukomo wake mwaka 2015.

Mnamo tarehe 25 hadi 27 Septemba 2015 huko katika jiji la New York nchini Marekani, kwenye
mkutano uliowajumuisha wakuu wa nchi nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, pamoja na
viongozi mbalimbali wa kidunia katika kuazimisha miaka 70 toka kuanzishwa kwa taasisi hiyo,
wakuu hao walitangaza Agenda ya Maendeleo Endelevu kwa kipindi cha miaka 15, kuanzia
mwaka 2015 hadi 2030.

Agenda hiyo ilikuja na malengo 17 yenye jumla ya shabaha 169 kwa pamoja kwaajili ya
utekelezaji. Pamoja na mambo mengine, malengo hayo yanalenga kwa pamoja kutokomeza
dimbwi la umaskini ambao umekisiri kwa kiasi kikubwa, ambapo ripoti mbalimbali zinasema
hadi sasa zaidi ya watu milioni 8 wanaishi kwenye umasikini wa kutupwa kote duniani.

Malengo haya yanalenga pia kutokomeza janga la njaa, kuhakikisha upatikanaji wa huduma
bora za afya, elimu bora, usawa wa kijinsia, bila kusahau suala la amani na haki duniani.

Tanzania kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), inatekeleza pia malengo haya
japo kasi yake bado sio ya kuridhisha sana. Umaskini wa kutupwa umeendelea kuongezeka
miongoni mwa watanzania walio wengi. Huduma ya afya imeendelea kuwa changamoto licha ya
maboresho kadhaa ambayo yamekuwa yakifanywa na serikali.

Suala la Usawa wa kijinsia bado halijapewa msisitizo wa kutosha maana tumeendelea


kushuhudia ukatili wa kupindukia dhidi ya watoto wa kike ambao wamekuwa wahanga wa
tamaduni mbovu ambazo zimekuwa zikiwanyima haki zao za msingi kama kupata elimu, huku
ndoa za utotoni na ukeketaji likiwa sio suala la geni tena machoni na masikioni mwa watanzania.

Hizo ni miongoni mwa sababu zilizonisukuma mimi kama mtanzania na muumini wa Malengo
17 ya Maendeleo Endelevu, kuchukua kalamu na karatasi kisha kuandika makala hii ambayo
inadhamiria kuwakumbusha watanzania wote juu ya kutekeleza malengo haya.

2|Ukurasa
wilsonpastory@gmail.com

Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ni nini?


Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ni seti ya malengo 17 ya ulimwengu ambayo
yamedhamiria kuubadilisha ulimwengu kutoka katika hali yake ya sasa ambayo imejaa umaskini
wa kutisha, bara la njaa, mabadiliko ya tabia ya nchi, uhaba na ubovu wa huduma za msingi za
jamii kama vile elimu na afya, machafuko na ghasia, uchumi husio jumuishi, na matatizo ya ajira
na kazi zisizo za staha, kwenda kwenye ulimwengu ambao utakuwa hauna aina zote za umaskini,
ulimwengu wenye chakula cha kutosha, huduma nzuri za afya, elimu, maji, nishati,
miundombinu ya usafirishaji, usawa wa kijinsia, na haki na usawa kwa jamii.

Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu


Orodha ya malengo 17 ya maendeleo endelevu ni pamoja na: 1. kutokomeza umaskini, 2.
kukomesha njaa, 3. afya njema na ustawi, 4. elimu bora, 5. usawa wa kijinsia, 6. maji salama na
usafi, 7. nishati mbadala kwa gharama nafuu, 8. kazi zenye staha na ukuzaji uchumi, 9. viwanda,
ubunifu na miundombinu, 10. kupunguza tofauti, 11. miji na jamii endelevu, 12. matumizi na
uzalishaji wenye uwajibikaji, 13. kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabia ya nchi, 14.
kuendeleza uhai katika maji, 15. kulinda uhai katika ardhi, 16. amani, haki na taasisi madhubuti,
na 17. ushirikiano ili kufanikisha malengo.

Kutokomeza Umaskini

3|Ukurasa
wilsonpastory@gmail.com

Hadi kufikia mwaka 2030 Umoja wa Mataifa umedhamiria kuwa umaskini wa aina zote katika
kila mahali unatokomezwa kabisa na kuhakikisha kuwa watu waishio kwenye umaskini
wanajiongezea kipato na kupata huduma za msingi, pamoja na kuepukana na majanga
mbalimbali.

Kwa mantiki hiyo basi, ni jukumu la serikali na wadau wote wanaohusika kuhakikisha kuwa
wanatokomeza umaskini ulioshamiri kwa watu wote hususani wale wanaoishi chini ya dola moja
ya kimarekani kwa siku ambao idadi yao inakadiriwa kuwa robo ya jumla ya watanzania wote.

Serikali na wadau wote wanaohusika wanalojukumu pia la kuhakikisha wanawatambua


wananchi wanaoishi katika hali ya umaskini, ili kuelekeza rasilimali na huduma mbalimbali za
kijamii ili kuwasaidia kuepukana na hali hiyo. Zoezi hilo likienda sanjari na kuwajengea uwezo
wa kiuchumi kwa kuwapatia huduma za kifedha na mikopo ili iwasaidie kujiinua kiuchumi.

Ni ukweli husiopingika kuwa wananchi wengi bado wanaishi katika hali ya umaskini wa
kutupwa. Kwa uzoefu wangu binafsi na kwa kupitia ripoti mbalimbali, mikoa ya Simiyu,
Shinyanga, Dodoma, Lindi, Mtwara na Pwani, ni miongoni mwa mikoa ambayo wananchi wake
wanaishi kwenye hali ya umaskini unaotia huruma. Ni wakati sasa kwa mamlaka zinazohusika
kuitizama mikoa hii ili kutekeleza lengo hili na kutokomeza umaskini kwa vitendo.

Kukomesha Njaa

4|Ukurasa
wilsonpastory@gmail.com

Lengo hili linadhamiria kutokomeza na kumaliza kabisa njaa kwa kusisitiza upatikanaji wa
chakula cha uhakika, utolewaji wa lishe bora, huku likihimiza kukuza kilimo endelevu.
Linaendelea kubainisha njaa kama tatizo linalopaswa kuondolewa kwa kushughulikiwa
kikamilifu ili kuhakikisha kila kaya inakuwa na uhakika wa kupata chakula salama na cha
kutosha ambacho kina virutubisho vyote.

Lengo hili linadhamiria pia hadi kufikia mwaka 2030, kilimo kiwe kimeboreshwa kwa
kuhakikisha wakulima wanatumia zana za kisasa na bora, urutubishaji wa ardhi inayotumika
kwaajili ya kilimo, na kuongeza uwezo wa wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi
na majanga kama vile; mafuriko, ukame, na ndege waharibifu. Hii itasaidia kukuza uzalishaji wa
mazao na hivyo kutokomeza kabisa balaa la njaa.

Ili kuhakikisha lengo hili linafanikiwa kikamilifu, ni wajibu wa serikali na mamlaka zote
zinazohusika kuhakikisha wanaweka jitihada kwenye kuongeza uzalishaji katika kilimo kwa
kuhakikisha zana za kilimo ikiwa ni pamoja na pembejeo za kilimo, na viuatilifu vya wadudu
wanaoshambulia mazao zinapatika kwa urahisi zaidi kwa wakulima kote nchini.

Ni ukweli husiopingika kuwa, sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji imekuwa haipewi kipaumbele
cha dhati na watawala katika nchi hii. Kumekuwepo na sera nyingi zenye dhamira yakuhimiza
shughuli za kilimo, lakini sera hizo zote hazikuweza kufanikiwa kwa kiasi kilichotarajiwa. Sera
ya hivi karibuni ya ‘Kilimo Kwanza’ chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais wa awamu ya nne,
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ilileta matumaini kwa wakulima wengi, lakini matumaini yao
yalizimika ghafla kama mshumaa, na hivyo mpaka sasa hakuna msisitizo wala matumaini mapya
katika kilimo.

Nipende kushauri jambo katika kuboresha sekta ya kilimo ambayo ndiyo sekta pekee itakayo
tuhakikishia upatikanaji wa chakula cha kutosha; ni wakati sasa wa mawaziri wanaokabidhiwa
kusimamia wizara hii wawe ni wakulima kwa asili, nadhani hii itasaidia katika kuweka msisitizo
wa kilimo hapa nchini. Pia napendekeza yatengwe maeneo maalumu kwaajili ya kilimo na yawe
chini ya usimamizi wa serikali, vijana waliomaliza mafunzo yao kwenye masuala ya kilimo
wakabidhiwe jukumu la uzalishaji mazao ya chakula katika maeneo haya. Hii naamini itasaidia
katika kutekelza lengo hili kwa vitendo zaidi.

5|Ukurasa
wilsonpastory@gmail.com

Afya Njema na Ustawi

Lengo hili limedhamiria kuhakikisha kuwa watu wana afya njema na ustawi wa watu katika umri
na rika zote. Linatia msisitizo katika kuwawezesha watu kuishi maisha yenye afya bora ili
kuongeza umri wa kuishi kwa watu wa umri na rika zote ifikapo mwaka 2030.

Hili kuhakikisha lengo hili linafikiwa kikamilifu, Umoja wa Mataifa umetia mkazo katika
kupunguza vifo vya watoto na wakinamama wakati wa kujifungua kunakosababishwa na
kukosekana huduma na vifaa bora vya kujifungulia, na kupunguza vifo vya watoto walio chini
ya umri wa miaka mitano ambao wengi wao wamekuwa wakipoteza maisha kwa ugonjwa wa
malaria ambao umekuwa sugu barani Afrika.

Vile vile lengo hili linalenga kutokomeza maambukizi ya UKIMWI na VVU, magonjwa
mbalimbali kama kifua kikuu, kisukari, shinikizo la damu, malaria, vikope, nimonia, kichocho,
kipindupindu, homa ya matumbo, pia magonjwa mengine yanayoambukiza kama magonjwa ya
zinaa ambayo yamekuwa yakisumbua kwa kiasi kikubwa.

Lengo hili pia limedhamiria kupunguza vifo na ulemavu unaosababishwa na ajali za barabarani,
kupunguza magonjwa na vifo vinavyotokana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na
madawa yenye sumu kuchanganyikana na hewa safi, maji na udongo vitu ambavyo vinatumiwa
na binadamu kwaajili ya ustawi wa maisha yao. Bila kusahau kuhakikisha elimu na stadi za
huduma ya afya ya uzazi kwa wananchi zinapatikana kwa urahisi zaidi.

6|Ukurasa
wilsonpastory@gmail.com

Mengi yamefanywa na serikali katika kutekeleza lengo hili, lakini bado changamoto ni nyingi
hasa maeneo ya vijijini ambako huduma za afya bado zinapatikana kwa kusua sua. Baadhi ya
vijiji havina kabisa zahanati, huku baadhi ya mikoa ikikosa hospitali za rufaa. Upatikanaji wa
madawa bado ni mtihani mkubwa sana, huduma kwa mama mjamzito na mtoto zinatolewa lakini
si kwa kiasi kinachotakiwa. Baadhi ya maeneo wazee wamekuwa bado wakitozwa pesa ili
kupata huduma ya afya ambayo inapaswa waipate bure pasipo malipo yoyote.

Baadhi ya maeneo wamama wamekuwa wakijifungulia nyumbani, na wengine vichakani wakiwa


njiani kuelekea hospitalini kutokana na umbali wa sehemu huduma za afya zinakopatikana. Vifo
vya wakinamama na watoto wakati wa kujifungua vimepungua ila havijaisha kabisa, idadi ya
watoto chini ya umri wa miaka mitano wanaokufa kwa malaria imepungua japo nayo haijaisha
kabisa.

Utekelezaji wa lengo hili unahitaji mikakati endelevu ambayo inapaswa kuwashirikisha


watanzania wote. Lazima kuwepo usimamizi makini kuanzia ngazi ya taifa hadi serikali za
mitaa. Wadau mbalimbali pia wajitokeze kusaidia sekta ya afya nchini kwa kujitolea kujenga
vituo vya afya kwenye vijiji ambavyo havina huduma hii, pia wasaidie upatikanaji wa madawa
katika hospitali na zahanati zote nchini.

Serikali pia ihakikishe inazalisha wataalamu wa kutosha wa kuhudumu katika sekta hii maana
kumekuwa kukiripotiwa upungufu wa wataalamu (specialists) katika nyanja mbalimbali za afya.
Pia ihakikishe inadhibiti madaktari feki ambao wamekuwa wakijipenyeza katika baadhi ya
mahospitali kwani suala hili linahatarisha usalama na uhai wa mgonjwa endapo atahudumiwa na
daktari feki asiyekuwa na ujuzi wa kitabibu.

7|Ukurasa
wilsonpastory@gmail.com

Elimu Bora

Lengo hili linalenga kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora na jumuishi, inayozingatia usawa na
kutoa fursa kwa wote kujiendeleza. Linasisitiza kuwezesha kila mtu kusoma, kujifunza na
kuhakikisha kwamba binadamu wote wanafikia vipawa vyao kikamilifu.

Lengo hili linalenga kupunguza idadi ya watu ambao hawajui kusoma na kuandika duniani huku
likisisitiza kuboreshwa kwa mazingira ya kutolea elimu, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa
walimu wa kutosha, vitabu vya kutosha vinavyokidhi vigezo, miundombinu bora kama
madarasa, meza na madawati.

Vile vile linasisitiza juu ya utoaji fursa ya elimu kwa watu wote isiyokuwa na ubaguzi kwa watu
wenye ulemavu, huku likidhamiria kuongeza idadi ya vijana na watu wazima wenye ujuzi
pamoja na ufundi stadi kwa ajili ya ajira, kazi zenye heshima na ujasiriamali.

Nchini Tanzania lengo hili linaendelea kutekelezwa kwa kasi ambayo tunaweza kusema ni ya
kulizisha. Jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na serikali iliyopo madarakani kuhakikisha
elimu bora inatolewa kwa wananchi wake ili kuwajengea uwezo wa kupambana na umaskini
ambao umekuwa tatizo kwa taifa.

Katika kuhakikisha lengo hili linatekelezwa kwa vitendo, serikali imekuja na sera ya elimu bure
ambayo inatoa fursa sawa kwa watoto wa maskini na matajiri kupata elimu sawa, tofauti na hapo
zamani ambapo watoto wengi wa maskini walishindwa kupata fursa hii kwa kukosa mahitaji

8|Ukurasa
wilsonpastory@gmail.com

muhimu ya kishule ikiwa ni pamoja na ada, michango ya madawati na taaluma, michango ya


walinzi, na hata michango kwaajili ya ujenzi wa maabara.

Tumeshuhudia pia serikali ikiendesha kampeni mbalimbali kwaajili ya upatikanaji madawati,


meza na viti, ambavyo vimekuwa vikipelekwa mashuleni kwaajili ya kurahisisha zoezi la
ufundishwaji kwa kuwawezesha wanafunzi kujifunza wakiwa wamekaa na kustarehe kabisa.
Suala la upatikanaji wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia pia limefanyiwa kazi licha ya kuwa
bado kuna kasoro mbalimbali katika baadhi ya masomo.

Mkoa wa Dar es Salaam unaweza kuwa mkoa wa mfano kwa Tanzania kwa kuonesha jitihada
zake kwa vitendo katika kutekeleza lengo hili. Tumeshuhudia uongozi wa mkoa kwa
kushirikiana na wadau wa elimu wakifanikisha upatikanaji wa meza, viti, na madawati kwa
wanafunzi wa mkoa huo, huku miundombinu kama ofisi na nyumba za walimu zikijengwa tena
kwa hadhi juu.

Licha ya mafanikio hayo machache, changamoto katika sekta ya elimu bado ni nyingi na
zinahitaji ufumbuzi wa haraka ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 lengo hili liwe limefikiwa
kwa asilimia mia moja. Walimu wameendelea kulalamikia mishahara midogo, jambo
linaloshusha morali ya ufundishaji kwa walimu hao. Walimu wa masomo ya sayansi kwa shule
za sekondari bado hawatoshi, huku wale wa masomo ya sanaa (arts) wakisubiri ajira kwa
takribani miaka miwili sasa bila kuajiriwa.

Usawa wa Jinsia

9|Ukurasa
wilsonpastory@gmail.com

Lengo hili linalenga kufanikisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake na wasichana wote.
Linakusudia kutokomeza ukatili wa aina zote dhidi ya wanawake na wasichana kwa kuhakikisha
wanapata fursa sawa katika umiliki wa rasilimali za kiuchumi kama vile ardhi, nyumba, na hata
magari.

Lengo hili linasisitiza hadi kufikia mwaka 2030 kusiwe na vitendo vya kikatili kwa wanawake na
wasichana ambavyo vimekuwa vikisababishwa na baadhi ya tamaduni ovu ambazo zimekuwa
zikikumbatiwa na baadhi ya jamii hapa duniani, ikiwemo Tanzania. Vitendo kama ukeketaji na
ndoa za utotoni kwa watoto wa kike ni miongoni mwa vitendo vinavyopigwa vita na Umoja wa
Mataifa kupitia lengo hili.

Lengo hili pia linakusudia kutoa fursa za elimu, uongozi, na ajira kwa wasichana na wanawake
kama ilivyo kwa wavulana na wanaume. Kwa kipindi kirefu sasa, kundi la wasichana na
wanawake limekuwa likibaguliwa katika masuala ya elimu, uongozi, na ajira, ambapo fursa
nyingi zimekuwa zikitolewa kwa wanaume na wavulana zaidi. Lengo hili limekuja kama
mwarobaini wa kutibu suala hili ambalo tunaweza kuliita ni kansa sasa.

Kwa upande wake nchi ya Tanzania imejitahidi kwa kiwango chake katika kutekelza lengo hili.
Idadi ya wasichana kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu ni kubwa ukilinganisha na
ilivyokuwa hapo awali. Idara nyingi za serikali na binafsi pia zimeajiri wanawake wa kutosha.
Bila kusahau baraza la mawaziri nalo limejumuisha wanawake, achilia mbali wakuu wa mikoa
na wilaya ambao nao pia kuna wanawake ndani yake.

Mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kama Children’s Dignity Forum (CDF), UNICEF
Tanzania, Save the Children, WHO, na mengine mengi yamekuwa yakipinga vikali vitendo vya
kikatili dhidi ya watoto wa kike ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni na ukeketaji. Wizara ya Afya
pia imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu juu ya athari ya ndoa
(mimba) za utotoni pamoja na ukeketaji.

Licha ya jitihada hizo zote, msisitizo na mkazo zaidi unatakiwa kuendelea kutolewa katika
kukemea vitendo vya kikatili dhidi ya mtoto wa kike ambavyo vimeendelea kuripotiwa katika
baadhi ya mikoa hapa nchini.

10 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

Maji Salama na Usafi

Watu husema Maji ni Uhai, na Usafi ni Maisha. Maji salama na usafi ni lengo la sita ambalo
linaweka msisitizo katika upatikanaji na usimamizi endelevu wa maji na usafi kwa wote.
Limelenga kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa watu wote ifikapo mwaka 2030.
Hivyo linasisitiza jamii zote duniani kuhakikisha zinaongeza kasi katika kuongeza upatikanaji
wa maji safi ya kunywa na kutumia kwa gharama nafuu, kupunguza uchafuzi wa mazingira
ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kemikali zenye sumu hazitiririki na kuathiri vyanzo vya maji,
bila kusahau kuboresha maji taka kwaajili ya matumizi ya baadae.

Nchini Tanzania suala la upatikanaji maji salama na usafi limekuwa likifanyiwa kazi kwa
kiwango chake, licha ya kutoonesha matokeo chanya mpaka sasa. Huduma ya upatikanaji maji
safi na salama imekuwa ikiboreshwa kwenye maeneo mengi ya nchi lakini bado kumekuwa na
kero ya ukosefu wa maji safi na salama. Kampeni ya kumtua mwanamke au mtoto wa kike ndoo,
ilianzishwa kwenye maeneo mengi hapa nchini ikilenga kuhakikisha maji yanapatikana kwa
karibu zaidi ili kumpunguzia kero mtoto wa kike kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji.

Kwenya baadhi ya mikoa kama Dar es Salaam wameweka mfumo wa kuwawezesha wananchi
kuunganishiwa maji kwa mkopo ili kuhakikisha wananchi wake wanaendelea kupata huduma ya
maji huku wakifanya malipo polepole, jambo ambalo limesaidia wananchi wengi wasiokuwa na

11 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

uwezo nao kupata fursa ya kunufaika na huduma ya maji. Kwa hili, mkoa wa Dar es Salaam
umeendelea kuwa mkoa wa mfano katika kutekelza Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Kuhusu suala la usafi, kumekuwa na kampeni za kuhamasisha usafi katika maeneo yote ya nchi,
kampeni ambazo ziliasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli katika miezi ya awali kabisa ya uongozi wake. Katika kuunga mkono kampeni
hii, mkoa wa Dar es Salaam uliandaa kampeni maalumu ya kusafisha jiji hilo ambalo awali
lilikuwa likiongoza kwa uchafu hapa nchini, kampeni hiyo imeonesha mafanikio kwa kiasi chake
ambapo kwasasa maeneo mengi ya jiji hilo la kibiashara ni masafi tofauti na hapo awali.

Licha ya mafanikio hayo kiduchu katika utekelezaji wa lengo hili, kero za ukosefu wa maji
zimeendelea kuripotiwa kutoka kila kona ya nchi. Huku hali ikisemekana kuwa mbaya zaidi
katika mikoa ya Kigoma, Singida, na Shinyanga. Hivyo jitihada zaidi zinahitajika katika
kuhakikisha maji salama yanapatikana kwa wananchi wote wa Tanzania.

Nishati Mbadala kwa Gharama Nafuu

Lengo hili limelenga kuhakikisha nishati mbadala kwa gharama nafuu inapatikana ili
kumwezesha kila mmoja kumudu gharama zake. Nishati hiyo pia inategemewa kuwa endelevu

12 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

na ya kisasa kwa watu wote. Serikali na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapaswa
kuhakikisha zinapunguza matumizi ya nishati inayotokana na misitu.

Matumizi ya umeme wa uhakika unaotokana na nishati mbadala kama jua, upepo, na gesi
yanasisitizwa. Hii itasaidia pia kuepusha hatari ya kutokea kwa jangwa kutokan na ukataji miti
hovyo kwaajili ya kupata kuni za kupikia na kuchoma mkaa.

Nchini Tanzania jitihada mbalimbali zimefanywa na zinaendelea kufanywa katika kuhakikisha


lengo hili linafanikiwa kwa kiasi kikubwa. Wizara ya Nishati imeendelea kuhakikisha huduma
ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi kupitia miradi yake mbali mbali, ukiwemo mradi wa
REA ambao umekuwa ukisambaza umeme vijijini kwa gharama nafuu zaidi.

Licha ya upatikanaji wa nishati ya gesi hapa nchini, nishati hii haijaweza kuwasaidia wananchi
kwani matumizi yake ni ya kiwango cha chini, pia upatikanaji wake umeendelea kuwa ghari
licha ya nishati hiyo kupatikana hapa nchini. Inasikitisha zaidi kuona hata maeneo ya Mtwara
ambako gesi inazalishwa wameendelea kutumia kuni huku gesi hiyo ikitumiwa na wakazi wa
miji mingine hapa nchini.

Licha ya serikali pia kujitahidi kuhakikisha nishati ya umeme inawafikia watanzania wengi zaidi,
maeneo mengi ya nchi yameendelea kubaki gizani bila huduma hiyo, huku baadhi ya maeneo
ambayo tayari yana huduma hiyo yakiendelea kupata umeme husiokuwa na uhakika kufuatia
katika katika umeme ya mara kwa mara ambayo imekuwa ikiyakumba maeneo hayo.

Ni wakati sasa wa serikali kuhakikisha inaongeza nguvu katika wizara ya nishati kwa kuitengea
bajeti ya kutosha itakayoiwezesha kusimamia zoezi la usambazaji umeme katika maeneo mengi
zaidi ya nchi. Ikimbukwe kuwa upatikanaji nishati mbadala ni suala lenye matokeo mtambuka
kwani licha ya kutumika majumbani, umeme hutumika pia viwandani katika kuzalisha bidhaa
mbalimbali na hivyo kuongeza pato la taifa.

13 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

Kazi zenye Staha na Ukuzaji Uchumi

Lengo hili linahimiza ukuaji endelevu wa kiuchumi wenye kujumuisha watu wote, huku kukiwa
na uzalishaji wa ajira na kazi za staha kwa wote. Linahamasisha pia sera za maendeleo
zinazosaidia shughuli za uzalishaji, ujasiriamali, ubunifu na uvumbuzi, huku likihimiza
urasimishaji na ukuzaji makampuni na taasisi ndogo ndogo na za kati, ikiwa pamoja na
kuhakikisha zinapatiwa huduma za kifedha.

Limedhamiria ifikapo mwaka 2030 kuwepo na ajira kamili na za uhakika kwa wanawake na
wanaume wote, bila kusahau vijana na watu wenye ulemavu ikiwa sanjari na ujira sawa kwa kazi
zenye thamani sawa. Linasisitiza pia suala la kupunguza kiasi cha vijana wasio na ajira, elimu au
mafunzo ifikapo mwaka 2020.

Linahimiza pia nchi zote duniani kuchukua hatua za haraka na za ufanisi kuondoa kazi za
kulazimisha, kukomesha utumwa wa kisasa na biashara ya binadamu. Suala la kukomesha aina
zote za utumikiswaji watoto na matumizi ya wanajeshi watoto ifikapo mwaka 2025,
limezungumziwa pia.

Lengo hili pia linazitaka nchi zote duniani kuhakikisha zinalinda haki za wafanyakazi na kuweka
mazingira salama ya kazi kwa wafanyakazi wote, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wahamiaji,
hasa wahamiaji wanawake, na wale walio katika kazi ngumu na hatarishi.

14 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

Nchini Tanzania utekelezaji wa lengo hili bado unasua sua. Tatizo la ajira kwa vijana
limeongezeka mara dufu, huku vyuo vikiendelea kuzalisha wasomi na watalaamu ambao baada
ya kuhitimu masomo yao wanasota mtaani bila kupata ajira toka serikalini. Utumikiswaji wa
watoto katika shughuli mbalimbali ikiwemo kazi za nyumbani (ndani) umeendelea kuwepo licha
ya hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na serikali kukomesha utumikiswaji wa
watoto.

Haki za wafanyakazi bado hazifuatwi. Wafanyakazi wawekuwa wakisimamishwa na kufukuzwa


kazi bila kufuatwa kwa utaratibu. Wengine wamekuwa wakikosa stahiki zao wanazostahili mara
baada ya kuwa wamefutwa au kusimamishwa kazi. Ni wakati sasa kwa serikali ya Tanzania
kutazama suala la haki za wafanyakazi hapa nchini, ikiwa pamoja na kuwaandalia mazingira
mazuri ya kufanyia kazi.

Viwanda, Ubunifu na Miundombinu

Lengo hili linalenga kuhimiza nchi zote duniani kujenga miundombinu imara, kukuza viwanda
jumuishi na endelevu, na kuchochea ubunifu (uvumbuzi). Limedhamiria kukuza miundombinu
yenye ubora na kuaminika inayozingatia jiografia ya maeneo husika hasa vijijini ili kusaidia
ustawi wa maendeleo ya kiuchumi kwa wote.

15 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

Linalenga pia kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha, ikiwa pamoja na mikopo yenye
masharti nafuu kwa viwanda vidogo vidogo, na kwa wazalishaji wengine. Jambo hili sharti
liende sambamba na kuhakikisha masoko yanapatikana kwa ajili ya bidhaa zinazozalisha na
viwanda hivi vidogo vidogo.

Lengo hili pia linazitaka nchi zote mwanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kunakuwa
na ongezeko la upatikanaji wa habari na teknolojia ya mawasiliano, pamoja na huduma nafuu ya
mtandao (internet) kwa nchi zinazoendelea ifikapo mwaka 2020.

Suala la uanzishwaji wa viwanda nchini Tanzania limefanikiwa kwa kiasi chake chini ya
uongozi wa awamu ya tano ambao umeweka mkazo katika uchumi wa viwanda. Viwanda
mbalimbali vimeanzishwa katika maeneo tofauti ya nchi ikiwemo mkoani Simiyu ambako
wameanzisha kiwanda cha chaki kinachohudumia mkoa huo pamoja na maeneo mengine ya
jirani.

Licha ya mafanikio hayo katika uanzishwaji viwanda nchini, dhana ya viwanda kwa wananchi
wa Tanzania bado haijaeleweka vizuri, huku wananchi wakitaka ufafanuzi zaidi kuhusu dhana ya
‘kiwanda kwa vyerehani vinne’ kama ilivyoelezwa na mamlaka yenye kusimamia sekta ya
viwanda nchini.

Kupunguza Tofauti

16 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

Lengo hili linalenga kupunguza hali ya kutokuwepo kwa usawa ndani na miongoni mwa nchi
mbalimbali hapa duniani. Linasisitiza juu ya uwezeshaji na ushirikishwaji jumuishi wa shughuli
za kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa watu wote bila kujali umri, jinsia, ulemavu, ukabila, asili ya
mtu, dini, hali ya kiuchumi, au hali yoyote ile.

Linalenga pia kuhakikisha kunakuwepo na usawa wa fursa na kupunguza tofauti ya kimatokeo,


ikiwa ni pamoja na kuondoa sheria, sera na taratibu za kibaguzi, na kuhamasisha sera na hatua
zenye kuhimiza usawa kwa wote. Linasisitiza juu ya kuimarisha sheria na taratibu juu ya
usimamizi wa masoko ya kifedha zitakazokuwa na sura ya usawa kwa mataifa yote.

Linadhamiria pia kuhakikisha kunakuwepo na uwakilishwaji sawa katika kufikia maamuzi ya


masuala mbalimbali ya kimataifa ikiwemo uchumi na fedha ili kujenga mazingira ya uwazi na
uwajibikaji kwa mataifa yote. Vilevile linasisitiza juu ya kutekelezwa kwa sera zenye kutoa
upendeleo maalumu wa huduma kwa nchi zinazoendelea kwa kuzingatia makubaliano na shirika
la biashara duniani.

Nchini Tanzania bado kumeendelea kuwepo na tofauti kubwa ya kimaendeleo kati ya maeneo ya
mjini na vijijini, hali inayoonesha kutofanikiwa kwa lengo hili hapa nchini. Huduma za kijamii
na kiuchumi kama barabara zimebaki kuwa changamoto kubwa katika maeneo mengi ya vijijini
ukilinganisha na maeneo ya mjini.

Wakati wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakifurahia usafiri safi na wa haraka wa mwendo kasi,
hali ni tofauti kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma ambao hawategemei kabisa kupata huduma hiyo
katika kipindi hiki. Huduma za kifedha kama benki bado hazijafika kwenye baadhi ya maeneo ya
vijijini na hivyo kuwalazimu wakazi wa maeneo husika kutembea umbali mrefu kwenda kupata
huduma za kifedha.

Miji na Jamii Endelevu

17 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

Lengo hili linalenga kuweka miji, majiji, na makazi ya watu kuwa jumuishi, salama, imara na
endelevu. Linasisitiza serikali na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha zinazuia
ujenzi holela kwa kuweka mipango miji na kuhakikisha zinatenga maeneo maalumu kwaajili ya
ujenzi wa maeneo ya kijamii kama viwanja vya mipira, masoko, na nyumba za serikali.

Vile vile linalenga kuzuia ujenzi wa makazi kwenye maeneo hatarishi, na kwa yale ambayo
tayari watu washajenga basi wapewe mahali salama kwa ajili ya makazi. Linasisitiza pia ujenzi
wa miundombinu ya usafiri kwa umma kuzingatia watu wenye mahitaji maalumu kama
walemavu, wazee na watoto.

Linahimiza pia kuweka mipango mikakati ya kuendeleza huduma za msingi vijijini ili kuwepo
uwiano kati ya Miji na Vijiji. Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Serikali Kuu zina wajibu
wakutambua urithi wa asili na utamaduni na kuhifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo mfano;
mapango, wanyama, majengo ya kale, nakadhalika.

Nchini Tanzania lengo hili bado halijapewa kipaumbele kwani maeneo mengi ya nchi
yamejengwa pasipo kufuata utaratibu wa mipango miji, nyumba zimebanana kiasi cha
kutoruhusu hata barabara za mitaa kupita na kufanya utoaji huduma muhimu kama zima moto
kushindwa kuwafikia wananchi kwa ufanisi pindi majanga ya moto yanapotokea. Kwa uzoefu
wangu na kwa maono yangu binafsi, ni mji wa Dodoma pekee ambao umejitahidi kupangiliwa
vizuri ukilinganisha na miji mingine.

Lakini pia suala la uwiano wa huduma za kijamii kati ya sehemu ya mijini na vijijini bado
limeendelea kuwa changamoto kwani hakuna uwiano sawa wa upatikanaji wa huduma hizo.

Matumizi na Uzalishaji wenye Uwajibikaji

18 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

Lengo hili linalenga kuhakikisha kunakuwepo na mifumo endelevu ya utumiaji na uzalishaji wa


rasilimali. Linasisitiza pia juu ya kupunguza kiasi kikubwa cha taka kupitia mifumo endelevu ya
kuzuia, kupunguza, na kuzichakata tena kwa matumizi mengine. Suala la kupunguza upotevu wa
chakula unaosababishwa na njia mbaya za uzalishaji na usambazaji, ikiwa ni pamoja na hasara
baada ya mavuno pia limepewa msisitizo wa kutosha.

Linasisitiza pia juu ya kuhakikisha manunuzi ya umma yanakuwa endelevu kulingana na sera na
vipaumbele vya kitaifa. Suala la uanzishwaji wa zana za kusimamia matokeo chanya ya
maendeleo endelevu kwaajili ya utalii ambao unazalisha ajira na kuhamasisha utamaduni na
bidhaa za ndani pia limepewa uzito wake.

Katika kutekeleza lengo hili, nchi ya Tanzania imefaulu kwa kiasi chake hasa katika kusimamia
rasilimali zake kama madini. Kumetungwa sheria zinazosimamia uzalishaji wa madinni ambao
una manufaa kwa taifa. Suala la uzuiaji taka pia halijaachwa nyuma, jitihada mbalimbali
zimekuwa zikioneshwa na serikali katika kupambana na uzalishaji taka nchini.

Kuchukua Hatua dhidi ya Mabadiliko ya Tabia Nchi

Lengo hili linalenga kuhakikisha nchi zote duniani zinachukua hatua za haraka kupambana na
mabadiliko ya hali ya nchi pamoja na athari zake. Limekusudia kuimarisha uwezo wa
kupambana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na majanga yote katika nchi zote za
ulimwengu.

19 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

Linalenga pia kuboresha elimu na kuhamasisha watu pamoja na taasisi mbalimbali kupunguza
kasi ya mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na njia za kukabiliana na mabadiliko hayo
kwa kutoa tahadhari kabla ya kutokea.

Linadhamiria pia kukuza utaratibu wa kuongeza uwezo wa mipango na usimamizi wa hali ya


hewa inayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi ambazo zinaendelea kukua na nchi
ndogo za visiwa vinavyoendelea, huku msisitizo ukiwa kwa kundi la wanawake, vijana na jamii
zilizotengwa.

Suala la kuingiza kwenye sera za nchi na mipango mbalimbali hatua zote zinazotakiwa
kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi pia linapewa msisitizo katika lengo hili.

Nchini Tanzania hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kudhibiti mabadiliko ya tabia ya


nchi ikiwa ni pamoja na kuhimiza zoezi la upandaji miti katika maeneo mbalimbali ya nchi kama
moja ya hatua katika kutekeleza lengo hili.

Licha ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kupambana na mabadiliko ya tabia


ya nchi, nguvu zaidi bado zinahitajika ikiwa pamoja na kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi
dhidi ya athari ya ukataji miti ovyo ambayo ni moja ya sababu zinazopelekea mabadiliko ya
tabia ya nchi kama ukame kutokea.

Kuendeleza Uhai katika Maji

20 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

Lengo hili linahimiza juu ya kuhifadhi na kutumia kwa njia endelevu malighafi za baharini kwa
ajili ya maendeleo endelevu. Limedhamiria kufikia mwaka 2025, kunakuwa na matokeo chanya
katika kuzuia na kupunguza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa kila aina unaofanywa baharini ikiwa
ni matokeo ya shughuli mbalimbali za binadamu zinazoendelea kwenye fukwe za bahari.

Lina lenga pia kufikia mwaka 2020, kuwe na matokeo chanya katika kuhifadhi angalau asilimia
10 ya maeneo ya pwani na bahari, kulingana na sheria za kitaifa na kimataifa juu ya usimamizi
wa bahari. Usimamizi wa shughuli za uvuvi na kuzuia uvuvi haramu pia ni miongoni mwa
mambo yanayopewa uzito katika lengo hili la 14.

Nchini Tanzania kumekuwa na jihada za kulizisha katika kutekeleza lengo hili. Kumetungwa
sheria mbalimbali za kulinda, kuifadhi, na kuendeleza viumbe vya baharini na ziwani. Uvuvi
haramu umekuwa ukipigwa vita, huku hatua stahiki zikichukuliwa ikiwa ni pamoja na uchomaji
nyavu zisizostahili.

Licha ya matokeo chanya katika kutekeleza lengo hili, changamoto mbalimbali zimeendelea
kuwepo ikiwa ni pamoja na shughuli zenye kuhatarisha uhai wa viumbe vya baharini kwenye
maeneo ya ufukwe, uvuvi wa kutumia sumu, na kadhalika.

Kulinda Uhai katika Ardhi

Lengo hili linalenga kulinda uhai katika ardhi na baionuwai. Linasisitiza juu ya kulinda na
kurejesha katika hali ya awali mifumo ya mazingira ya nchi kavu, huku kukiwa na udhibiti wa
uharibifu wa misitu kwa njia endelevu, bila kusahau kupambana na hali ya nchi kugeuka jangwa.

21 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

Linatia mkazo pia katika kukomesha uharibifu wa ardhi na kupiga vita vitendo vyote
vinavyosababisha upotevu wa wanayama na mimea anuwai.

Serikali na wadau wote wanalojukumu la kuhamasisha jamii juu ya ushiriki wao katika kulinda,
kusimamia maliasili za nchi hii kwa kuhakikisha unakuwepo ulinzi shirikishi wa kuwalinda
wanyama wetu dhidi ya majangiri.

Serikali imepiga hatua kubwa katika kulinda maliasili zote ikiwemo wanyamapori hapa nchini.
Licha ya hatua kubwa hizo kumeendelea kuripotiwa vitendo vya ujangiri katika baadhi ya
maeneo, huku watu mbalimbali wakiendelea kukamatwa wakiwa na nyara za serikali kama
pembe za ndovu na meno ya tembo. Baadhi ya wanyamapori wameendelea kupoteza maisha kwa
kugongwa na magari hasa nyakati za usiku kwenye hifadhi ambazo zimepitiwa na barabara.

Ni jukumu letu sote kuhakikisha tunalinda maliasili zetu kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na
cha baadae.

Amani, Haki na Taasisi Madhubuti

Lengo hili limedhamiria kuendeleza jamii jumuishi na yenye amani kwa ajili ya maendeleo
endelevu, huku ikitoa haki kwa wote na kujenga taasisi imara zenye kuwajibika katika nyanja
zote. Linahimiza kudumisha usalama wa wananchi (raia) ambao unategemea sana uwepo wa
taasisi zenye ufanisi, zenye kuwajibika, na zenye kuhusisha watu wote katika viwango vyote.

22 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

Serikali inalojukumu lakuhakikisha kunakuwa na utawala bora, utawala wa kufuata sheria,


demokrasia, na haki inatolewa kwa wote bila upendeleo wowote ule. Inaowajibu pia wa
wakuonesha ufanisi na uwajibikaji kwa wananchi wake kwa kuhakikisha inapambana na rushwa,
na kuongeza uhuru wa wananchi kupata taarifa.

Licha ya kufanya vizuri katika kusimamia utawala bora na demokrasia nchini, bado
kumekuwepo na malalamiko ya baadhi ya watumishi na watendaji wa serikali kutokufuata
utawala wa sheria, ni wakati sasa wahusika wajitathimini na kufikiria upya namna nzuri ya
kuweza kufanikisha lengo hili kwa kuhakikisha wanafuata utawala wa sheria na kuheshimu haki
za binadamu.

Katika kupambana na rushwa serikali imefanya vizuri sana. Tumeshuhudia mafisadi


wakifikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua stahiki. Licha ya kufanya vizuri
katika kupambana na rushwa, vitendo vya rushwa vimeendelea kuripotiwa sehemu nyingi za
nchi, hivyo naiomba serikali kuendeleza vita hii maana haki haiwezi kupatikana endapo kuna
utitiri wa rushwa, na rushwa siku zote ni adui wa haki.

Baadhi ya kesi mahakamani zimeendelea kuchukua muda mrefu bila kusikilizwa huku
watuhumiwa wakiendelea kusota rumande na mahabusu bila sababu za msingi. Watuhumiwa pia
wameendelea kunyimwa dhamana hata kwa makosa ambayo yanastahili dhamana. Mabambiko
ya kesi yameendelea kuwepo licha ya kupungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na siku za
nyuma.

Matukio ya watu kutekwa, kupotea katika mazingira ya kutatanisha, na baadhi ya miili ya watu
kuokotwa wakiwa wamekufa, ni miongoni mwa mambo yanayoenda kinyume na lengo hili. Ni
wajibu wa seriklia na raia wote kuhakikisha wanakomesha jambo hili. Serikali ifuatilie matukio
haya, na wananchi watoe ushirikiano kwa serikali kwa kutoa taarifa za matukio haya polisi kabla
na baada ya kutokea.

23 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

Ushirikiano ili Kufanikisha Malengo

Kama ilivyo usemi usemao ‘umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu’, lengo hili linazitaka nchi zote
na wadau wote kuendeleza ubia katika ngazi zote ili kuweza kufanikisha Malengo ya Maendeleo
Endelevu. Linasisitiza juu ya kuimarisha njia za utekelezaji kwa kuunganisha nguvu na
ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu.

Linahimiza juu ya ushirikiano katika masuala ya kifedha, teknolojia, biashara, masuala ya kisera,
na masuala ya kuzijengea uwezo nchi maskini kuweza kutekeleza mipango yake. Linalenga
kuimarisha uwezo wa nchi katika kusimamia na kukusanya mapato ya ndani, huku ikizitaka nchi
zilizoendelea kutoa misaada kwa nchi zinazoendelea (maskini) katika kufanikisha malengo yake.

Tumeona serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali wa kimataifa na kitaifa katika kutekeleza


malengo haya. Licha ya jitihada hizi kufanyika, mimi binafsi naona haitoshi hivyo naendelea
kuomba ushirikiano zaidi toka pande nne za dunia katika kufanikisha malengo haya. Lazima
tuhakikishe dunia inakuwa sehemu salama kwa binadamu kuishi huku akifurahia utu wake.

Serikali kuanzia ngazi ya serikali za mitaa hadi serikali kuu zinaowajibu wa kuhakikisha
upatikanaji wa rasilimali, teknolojia pamoja na maarifa ya kutekeleza malengo yote endelevu.
Hii ikiwa ni pamoja na serikali kuhakikisha inatenga fedha za kutosha kwa kila wizara
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi maana tunaamini wizara zote zinatekeleza malengo
haya.

24 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

HITIMISHO

Ni matumaini yangu kuwa baada ya kusoma makala hii fupi, kila mmoja wetu atafanya jitihada
za kuhakikisha malengo haya 17 yanatekelezwa kwa ufanisi mkubwa. Serikali kwa upande
wake, asasi za kiserikali na zisizo za kiserikali pia zitahakikisha zinachukua hatua katika
kutekeleza malengo haya.

United Nations Tanzania, Youth of United Nations Tanzania (YUNA), na machampioni wote
ambao wanajukumu la kutoa elimu kuhusu malengo haya, naamini wataongeza msisistizo
kwenye malengo ambayo yanaonekana kusahaulika.

Malengo yote yanatekelezeka, tuungane kwa pamoja kuyatekeleza.

25 | U k u r a s a
wilsonpastory@gmail.com

Marejeo

Global View (2016). The United Nations 2030 Agenda: 17 Sustainable Development Goals to
Transform Our World. New York: United Nations.
http://www.globalview.at

Policy Forum (2016). Malengo ya Maendeleo Endelevu na Wajibu wa Serikali za Mitaa.

Dar es Salaam: Policy Forum.

The Sustainable Development Goals Center for Africa, From 26th – 27th Januari 2017: How
Africa can achieve the SDGs by 2030.
https://www.youtube.com/watch?v=fng8cGGYg3w&t=158s

Hotuba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim M.


Majaliwa (Mb), Kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Fedha Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2017/2018.
http://www.parliament.go.tz/budget-list

26 | U k u r a s a

You might also like