You are on page 1of 2

JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI UDANGANYIFU KATIKA MITANDAO YA SIMU ZA KIMATAIFA Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) inao mtambo maalum wa kusimamia Mawasiliano ya simu na udhibiti mapato yatokanayo na simu, zikiwemo zile zinazoingia nchini kutoka nje za nchi ili kuwezesha usimamizi wenye ufanisi zaidi kwa mitandao yote ya mawasiliano ya simu hapa nchini. Mtambo huu unajulikana kama Telecommunication Traffic Monitoring System-TTMS kwa lugha ya kiingereza. Ufungaji wa Mfumo wa kudhibiti udanganyifu (Anti-Fraud Management System) katika mtambo huu unaweza kutambua mawasiliano ya udanganyifu katika mitandao ikiwa ni pamoja na namba za ulaghai za nchini zinazotumika kuruhusu au kupitisha mawasiliano ya Kimataifa hapa nchini kinyume na matakwa ya sheria na kanuni za kudhibiti mawasiliano ya simu. Mawasiliano ya udanganyifu ni yale ambayo mtu hutumia mitambo ya simu kwa nia ya kukwepa kulipia gharama, kulipa tofauti na matumizi, kutokulipa kabisa, kumfanya mtu mwingine alipie au mbinu nyingine yeyote kwa lengo la kujipatia fedha au faida binafsi. Mamlaka ya Mawasiliano kwa kutumia mitambo hii na kwa kushirikiana na watoa huduma za simu na vyombo vya usalama inafanya uchunguzi wa kitaalamu kila wakati ili kubaini uwepo wa udanganyifu katika mitandao ya simu. Endapo mtu yeyote au kampuni itabainika kuhusika na udanganyifu huo, hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa. Zoezi hili ni endelevu na linahusisha ukaguzi na utambuzi wa mitambo inayojihusisha na udanganyifu katika mitandao ya simu. Hadi sasa tayari tumefanikiwa kuwakamata baadhi ya watuhumiwa na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria kama ilivyoshuhudiwa hivi karibuni kupitia vyombo vya habari. Ili kupata mawasiliano kutoka nje ya nchi makampuni ya hapa nchini yenye leseni yanakuwa na makubaliano ya kimkataba na makampuni ya nje kwa ajili ya kutoa huduma za mawasiliano. Hata hivyo kumekuwa na makampuni na watu binafsi wanaowezesha simu zinazopigwa kutoka nje kufika nchini bila kupitia kwenye njia rasmi na hivyo kuikosesha Serikali na Makampuni ya simu mapato halisi. Hii ni kinyume na sheria za nchi zinazosimamia Sekta ya Mawasiliano. Watu hawa hutumia internet kuweza

kuruhusu simu zinazopigwa kutoka nje ya nchi na kuzifanya zionekane kama zimetoka hapa nchini kwa kutumia kifaa kinachojulikana kama SIM BOX. Kifaa hicho kinauwezo wa kutumia laini za simu nyingi ambazo zinatumika kuidanganya mitambo ya kampuni za ndani kutokutambua kuwa simu zinazopigwa ni za kimataifa. Mwananchi anapopigiwa simu na mtu aliyeko nje ya nchi na akaona kwenye simu yake namba ya mitandao ya hapa nchini ajue kuwa simu hiyo aliyopigiwa inapita kwenye mitandao isiyo rasmi. Mara nyingi mitandao hii huwa na huduma mbovu na zisizo na viwango vinavyokubalika. Mtu anayepigiwa simu hizi hudhani kuwa mtandao wake wa mawasiliano anaotumia ndio utoao huduma zisizo na viwango kumbe ni ulaghai wa watu au kampuni zinazofanya udanganyifu. Watanzania walio wengi hivi sasa wanafaidika kwa huduma za mawasiliano, yakiwemo mawasiliano ya simu za mkononi na internet. Huduma za simu nchini zimeongezeka kwa kiwango kikubwa na kuwafikia wananchi wengi kutoka laini za simu milioni tatu tu mwaka 2000 hadi kufikia laini milioni 28. Katika kipindi hiki pia tumeshuhudia uwepo wa mikongo ya baharini ambayo imesababisha upatikanaji kirahisi wa mawasiliano ya simu kati ya nchi yetu na mataifa ya nje. Kuwepo kwa mikongo hii ya baharini pamoja na uwepo wa mkongo wa taifa kumesababisha upatikanaji wa huduma za internet kupatikana maeneo mengi nchini kwa bei nafuu na kwa ubora wa hali ya juu. Matumizi ya internet yameongezeka kwa watanzania walio wengi kutoka watumiaji laki tatu kwa miaka mitatu iliyopita mpaka watumiaji milioni 7.6 kwa takwimu za hivi karibuni. Wengi wa watumiaji wa internet, matumizi yao ni kujifunza na kujielimisha kwa kupitia kwenye mitandao ya kijamii na blog mbalimbali. Tunawaomba wananchi na watumiaji wa huduma za mitandao watupatie ushirikiano kwa kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mawasilaino ama kwa vyombo vingine vya usalama ikiwa watahisi au kuwa na taarifa za watu wanaojihusisha na udanganyifu huu katika mitandao ya simu.

Imetolewa na: Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) 3 April 2014

You might also like