You are on page 1of 14

1

HOTUBA YA MWISHO WA MWEZI FEBRUARI, 2015, YA


MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, ILIYOTOLEWA TAREHE
1 MACHI, 2015
Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada tunamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa
rehema kwa kutuwezesha kuzungumza kupitia utaratibu wetu huu mzuri
wa hotuba za kila mwisho wa mwezi. Kwa mwisho wa mwezi wa Februari
nina mambo matano ninayopenda kuyazungumzia.
Zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura
Ndugu Wananchi;
Jambo la kwanza ni uandikishaji wa Wapiga Kura.

Tarehe 24

Februari, 2015 Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda


alizindua rasmi uandikishaji wa wapiga kura ikiwa ni sehemu ya zoezi la
uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura nchini.

Zoezi hili

lilizinduliwa Makambako, Mkoani Njombe na litaendelea nchini kote


mpaka litakapokamilika kwa mujibu wa ratiba itakayopangwa na Tume ya
Uchaguzi. Uandikishaji unatumia teknolojia ya kisasa ya utambuzi wa
alama za vidole (BVR) na macho ya mtu anayeandikishwa. Teknolojia hii
itatusaidia kuondoa kutoaminiana, manunguniko na madai kuhusu
udanganyifu katika chaguzi zetu kwamba wamepiga kura wasiostahili.
Kuanza kutumika kwa teknolojia hii ni kielelezo cha utashi wa Serikali
kuwa nchi yetu iwe na chaguzi zilizo huru, wazi na haki.
Ndugu Wananchi;
Mtakumbuka kuwa, kabla ya uzinduzi wa zoezi hili, Tume ya Taifa
ya Uchaguzi ilifanya zoezi la majaribio ya uandikishaji wa wapiga kura
kwa kutumia mashine za teknolojia hii mpya katika kata 10 katika

Halmashauri za Kinondoni, Kilombero na Mlele kati ya tarehe 15 hadi 23


Desemba, 2014.
Habari njema ni kuwa, kwa kutumia mashine za BVR, idadi ya
waliojiandikisha ilivuka lengo la uandikishaji kwa kipindi kilichopangwa
katika Kata hizo.

Katika Halmashauri ya Kilombero walioandikishwa

walifikia asilimia 110.9 ya lengo, katika Halmashauri ya Mlele uandikishaji


ulifikia asilimia 101 ya lengo na katika Jimbo la Kawe, katika Halmashauri
ya Wilaya ya Kinondoni walioandikishwa walikuwa asilimia 105.67 ya
lengo.

Mafanikio haya ni ya kutia moyo pamoja na changamoto za

kiufundi zilizojitokeza na zile zinazotokana na upya wa mfumo wenyewe


kwa watumiaji. Changamoto hizo zimefanyiwa kazi na watengenezaji wa
vifaa vinavyotumika katika awamu hii ya uandikishaji wa wapiga kura
nchi nzima.
Ndugu Wananchi;
Nimefarijika na taarifa kuwa zoezi la uboreshaji wa Daftari na
uandikishaji wa wapiga kura limeanza vizuri Makambako.

Wananchi

wamejitokeza kwa wingi kuliko ilivyotarajiwa. Kati ya tarehe 23 hadi 25


Februari, 2015 kwa mfano, Tume ilitegemea kuandikisha wapiga kura 9,541
lakini kutokana na mwamko wa wananchi kuwa mkubwa wameweza
kuandikisha wapiga kura 13,042. Kila kituo kilikuwa kinaandikisha kati ya
wapiga kura 80 na 150 kwa siku. Lengo la Tume ni kuandikisha wapiga
kura 32,000 katika Halmashauri ya Makambako ambako kwa siku
wanatarajia kuandikisha watu 4,320. Naambiwa kuwa hesabu za juzi na
jana wameandikisha hadi wapiga kura 6,000 kwa siku. Kwa kasi hii na
kama mambo yatakwenda kama inavyotarajiwa, lengo hilo litafikiwa na
hata kuvukwa.
Ndugu Wananchi;
Hatuna budi kutoa pongeza kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa
hatua hii ya kutia moyo tuliyofikia katika mchakato huu. Inaondoa hofu
iliyoanza kuingia miongoni mwa baadhi ya watu kuwa huenda zoezi hili

lisingefanikiwa. Tunachokitaka kwa Tume ni kuona zoezi hili linaendelea


na

kukamilika

kama

ilivyopangwa.

Napenda

kurudia

ahadi

niliyokwishaitoa kwa Tume kwamba Serikali itafanya kila linalowezekana


kuiwezesha

kirasilimali

ili

iweze

kutimiza

jukumu

lake

hilo.

Nimekwishawakumbusha Hazina kuhusu umuhimu wa zoezi hili


kufanikiwa kama ilivyopangwa.

Hivyo basi, nimewataka wahakikishe

kutoa kipaumbele cha kwanza katika mgao wa fedha.

Kama haifanyiki

nawaomba Tume waniambie mimi mwenyewe.


Wito wangu kwenu, wananchi wenzangu, ni kujitokeza bila ya
kukosa kwenda kujiandikisha kwa mujibu wa ratiba ya uandikishaji katika
maeneo yenu kama itakavyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Msifanye ajizi maana hakutakuwepo na fursa nyingine ya kujiandikisha
kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu baada ya fursa hii kupita.
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyoelezwa na Tume na mimi kusisitiza mara kadhaa kuwa
watakaojiandikisha wakati huu ndio watakaopiga kura ya maoni kuhusu
Katiba Inayopendekezwa na ndio watakaopiga kura katika Uchaguzi Mkuu
wa Oktoba, mwaka huu.

Vitambulisho vya zamani vya mpiga kura

havitatumika, hivyo watu wote ambao ni Watanzania na wana umri wa


miaka 18 au zaidi lazima wajitokeze kuandikishwa upya. Watu pekee
ambao hawatapaswa kujiandikisha tena ni wale tu walioandikishwa katika
zoezi la majaribio lililofanyika katika zile kata 10 za Halmashauri za
Kinondoni, Ifakara na Mlele mwezi Desemba, 2014.

Vitambulisho

walivyopata ndivyo vyenyewe.


Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii pia kuwaomba viongozi wa vyama vya
siasa, Serikali, dini na asasi za kiraia kuungana na Serikali na Tume ya
Uchaguzi

katika

kuwakumbusha

na

kuwahamasisha

wananchi

wakajiandikishe. Naomba tusiwachanganye wananchi kwa kutoa taarifa


zisizokuwa za kweli na kuwafanya wakaacha kujiandikisha. Sisi katika

Serikali

tunafanya

kila

linalowezekana

kuhakikisha

kuwa

kila

atakayejitokeza kujiandikisha anaandikishwa. Aidha, tutahakikisha kuwa


kila panapojitokeza changamoto zinatafutiwa ufumbuzi kwa wakati
mwafaka.
Tunatambua kuwa mfumo huu ni mpya hivyo panaweza kujitokeza
changamoto zinazosababishwa na upya wake.

Nawaomba wahusika

kuendelea kuwaelimisha watendaji wanaohusika ili wapate uzoefu


unaostahili. Aidha, nawasihi wananchi kuwa wavumilivu na waelewa pale
ambapo wakati mwingine watalazimika kukaa kwenye mistari kwa muda
mrefu kusubiri kujiandikisha, au wakalazimika kuja siku ya pili.
Ndugu Wananchi;
Kupiga kura kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa au kuchagua
Rais, Wabunge na Madiwani ni haki na wajibu wa kila raia. Lakini, kuipata
haki hiyo na kuweza kutimiza wajibu huo kunategemea kuwa na
kitambulisho cha mpiga kura. Bila ya hivyo haiwezekani. Haya shime
jitokezeni, mjiandikishe, ili muweze kuitumia haki yenu na kutimiza
wajibu wenu wa kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa na kuchagua
viongozi mnaowaona wanafaa kuongoza nchi yetu, jimbo lako na kata
yako.
Kura ya Maoni
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia ni kuhusu Kura ya Maoni ya
Katiba Inayopendekezwa. Kama mjuavyo, baada ya Bunge Maalumu la
Katiba kutunga Katiba Inayopendekezwa na Rais kuchapisha Katiba hiyo
katika Gazeti la Serikali na kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni,
kinachoendelea sasa ni matayarisho ya kufanyika kwa kura hiyo. Yapo
majukumu ya Serikali, yapo majukumu ya Tume ya Uchaguzi, na yapo
majukumu ya Serikali na Tume kwa pamoja. Utekelezaji umeishaanza na
unaendelea.

Miongoni mwa mambo yanayotakiwa kufanyika ni

uandikishaji wa wapiga kura ambao umekwishaanza na unaendelea.

Ipo pia kazi ya kuchapisha na kusambaza Katiba Inayopendekezwa


ili wananchi waweze kuisoma na kuielewa kabla ya kupiga kura ya maoni.
Tayari Katiba Inayopendekezwa imetangazwa katika tovuti za Wizara ya
Katiba na Sheria, Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo na
katika tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Pia

imechapichwa magazetini.
Hadi

tarehe

27

Februari,

2015

vitabu

vimechapishwa na nakala 1,341,300 kusambazwa.

1,558,805

vilikuwa

Nakala 1,141,300

zimesambazwa kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara na nakala 200,000


zimegawiwa kwa Zanzibar.

Kwa upande wa Tanzania Bara kila Kata

imepewa vitabu 300. Kwa vile Kata zina wastani wa vijiji vitano (5) hii ina
maana kwamba kila kijiji kimepata vitabu 60 kwa kila kijiji ambayo si haba.
Ndugu Wananchi;
Tume ya Uchaguzi itatoa maelekezo kuhusu utaratibu wa kutoa
elimu kwa umma. Nimeambiwa tayari asasi za kiraia 420 kwa upande wa
Bara na 75 kwa upande wa Zanzibar zimejiandikisha kwa ajili ya zoezi hilo.
Halikadhalika, Tume itatoa maelekezo husika kuhusu kampeni ya Kura ya
Maoni wakati ukiwadia. Naomba watu wawe na subira na kuzingatia
masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni na Kanuni zake. Tukifanya hivyo,
zoezi hili muhimu na la kihistoria litatekelezwa kwa usalama na utulivu.
Watu watafanya uamuzi kwa uhuru, uelewa, amani na usalama.
Hali ya Usalama Nchini
Ndugu wananchi;
Jambo la tatu ninalotaka kulizungumzia ni hali ya usalama nchini.
Kwa jumla hali ya usalama ni nzuri, hata hivyo kuna matukio ya kiusalama
ambayo ningependa kuyazungumzia. La kwanza ni mashambulizi yenye
sifa za ujambazi na mwelekeo wa kigaidi. Na, la pili ni la mauaji ya watu
wenye ulemavu wa ngozi.
Katika kipindi cha miezi 12 hivi kumekuwa na matukio ya watu
kuvamia vituo vya Polisi, wengine wanachoma moto au wengine wanapora

silaha. Pia kumekuwepo na matukio ya kuwashambulia Polisi walioko


kwenye doria na wengine kuporwa silaha. Vituo vya Polisi vilivyovamiwa
na silaha kuporwa ni vya Newala Mkoani Mtwara silaha tatu ziliporwa,
Ikwiriri katika Wilaya ya Rufiji silaha saba, Kimanzichana, Wilaya ya
Mkuranga silaha tano, mbili za polisi na tatu za raia waliokwenda
kuzihifadhi pale, na Ushirombo Wilaya ya Bukombe silaha 18.

Pugu

Machinjioni na Tanga, askari waliokuwa katika shughuli za ulinzi na doria


walishambuliwa na kuporwa silaha tatu.

Kule Songea kulikuwepo na

matukio mawili ya Polisi kushambuliwa lakini silaha hazikuporwa.


Bahati mbaya, vijana wetu saba wa Jeshi la Polisi walipoteza maisha
katika matukio hayo. Newala alikufa Polisi mmoja, Kimanzichana mmoja,
Ikwiriri wawili, na Ushirombo watatu. Wapo Polisi kadhaa waliopata
majeraha ya namna mbalimbali katika mashambulizi haya.
Ndugu Wananchi;
Silaha zote 18 zilizoporwa Ushirombo zimepatikana na watu 10
wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo wamekamatwa. Katika tukio la
Tanga silaha moja kati ya mbili zilizoporwa imepatikana. Watuhumiwa
saba wametiwa mbaroni, wanne kati yao ni wale waliokuwa wamejifisha
katika mapango ya Kiomoni katika Kitongoji cha Karasha-mikocheni,
kilichoko kijiji cha Mzizima wilayani Tanga. Tayari watu wanne
wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la Ikwiriri wamekamatwa.

Polisi

wanaendelea na upelelezi kuwapata watu wengine na kuzipata silaha saba


zilizoporwa kituoni hapo.

Kwa tukio la Newala silaha zote tatu

zimepatikana pamoja na bastola moja ya mtuhumiwa aliyehusikaa

na

watu wawili wametiwa nguvuni. Hali kadhalika, upelelezi unaendelea wa


kuzipata silaha zilizoporwa ambazo hazijapatikana mpaka sasa: yaani
Kimanzichana moja, Pugu Machinjioni moja na Tanga iliyosalia moja.
Ndugu Wananchi;
Matukio haya yana sura mbili. Yana sura ya ujambazi, lakini pia
baadhi yake yana dalili za ugaidi. Vyombo vyetu vya usalama vinaendelea

kufanya kazi yake ya uchambuzi wa kila tukio na kulipa nafasi yake


stahiki. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa Jeshi la
Polisi wakishirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na
vyombo vingine vya usalama kwa kazi kubwa na nzuri waifanyayo
kupambana na uhalifu nchini. Mafanikio tunayaona, kama nilivyoeleza na
kama tulivyosikia kule Tanga hivi karibuni ni matunda ya ushirikiano huo.
Hata hivyo, nimewataka waendelee kuwasaka watu hawa waovu po pote
walipo ili wafikishwe mahakamani na kuzirejesha mikononi mwa Polisi
silaha zote zilizoporwa.
Nawaomba wananchi wenzangu wote kushirikiana kwa karibu na
vyombo vya usalama hususan Jeshi la Polisi ili tuweze kupata mafanikio
zaidi dhidi ya uhalifu huu na uhalifu mwingineo. Nawaomba mfanye
mambo mawili:

Kwanza, toeni taarifa Polisi mnapozipata habari za

vitendo viovu au nyendo za watu waovu wanavyokusudia kufanya


wahalifu au taarifa za wale waliokwishafanya uhalifu.
Pili, naomba watu waache kuwashabikia watu hawa waovu wala
kueneza taarifa zao potofu kwenye mitandao ya kijamii.

Badala yake

tutumie mitandao ya kijamii kuponda fikra zao potofu, fikra zao hasi na
vitendo vyao viovu pamoja na kuwafichua wao na mambo yao mabaya
wayafanyo. Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza
wananchi wote walioweza kutoa taarifa zilizowezesha kuzuia uhalifu
usifanyike au zilizowezesha kutiwa mbaroni kwa wahutumiwa wa vitendo
vya ujambazi na ugaidi.

Hatuwezi kushinda uhalifu bila ushirikiano

baina ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama.


Mauaji ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi
Ndugu wananchi;
Nimesikitishwa sana na taarifa kuwa mauaji ya ndugu zetu wenye
ulemavu wa ngozi (Albino) yameibuka upya baada ya hali kuwa tulivu
mwaka 2011. Mwaka jana (2014) yalitokea matukio matatu katika mikoa ya

Mwanza, Tabora na Simiyu na mwaka huu limetokea tukio moja mkoani


Geita.
Lazima tulaani vikali mauaji ya ndugu zetu albino. Ni vitendo vya
kinyama ambavyo havitegemewi kufanywa au kutokea katika jamii yeyote
ya watu waliostaarabika, ya watu wanaomuabudu Mungu. Watu wenye
ulemavu wa ngozi ni wanadamu wenzetu, wenye haki sawa ya kuishi na
kupata hifadhi ya maisha yao kama walivyo wanadamu wengine.
Hawastahili kufanyiwa wanayofanyiwa.

Hawapaswi kuishi kwa hofu

katika kijiji chao, mtaa wao au katika nchi yao. Jamii nzima na sisi sote
mmoja mmoja na katika umoja wetu, tunao wajibu wa kuhakikisha
usalama wa maisha yao na mali zao kama ilivyo kwa watu wengine wote.
Kwa kweli, mauaji ya albino ni jambo linalofedhehesha na
kulidhalilisha taifa letu. Ni vitendo visivyovumilika.

Hatuna budi sote

kushikamana na kuhakikisha kuwa tunapambana nao kisawasawa na


kuwashinda. Tusikubali kamwe wakaturudisha kule kubaya tulikokuwa
zamani.

Naungana na Chama cha Albino Tanzania kulaani ukatili huu na

kutaka watu wote wanaojihusisha na ukatili huu wasakwe, wakamatwe,


wafikishwe

Mahakamani

na

kupewa

adhabu

kali

inayowastahili

wanapopatikana na hatia.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa wakati wote Serikali imelipa uzito
mkubwa suala la kudhibiti na kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu
wa ngozi au kukatwa baadhi ya viungo vyao wenyewe wakiwa hai.
Tumefanya hivyo bila ya kuchoka tangu tukio la kwanza baada ya mimi
kuingia madarakani Aprili 17, 2006 na miezi mitatu tu kule Nyahunge,
Geita alipouawa Alfa Amon ambapo watuhumiwa wawili waliuawa na
raia. Mwaka 2007 kulikuwa na matukio saba. Mwaka 2008 ndio ulikuwa
mwaka mbaya sana walipouawa watu 18.
Kutokana

na

jitihada

kubwa

zilizofanywa

na

Serikali

kwa

kushirikiana na wananchi mauaji yalipungua na kuwa tisa mwaka 2009.

Mwaka 2010 kukawa na tukio moja na mwaka 2011 hapakuwepo na tukio


lolote.

Mwaka 2012 kukawa na tukio moja, mwaka 2013 aliuawa mtu

mmoja na wawili kujeruhiwa. Mwaka 2014 waliuawa watu watatu na


wawili kujeruhiwa, na Januari, 2015 kumetokea tukio moja kule Geita.
Ndugu Wananchi;
Tangu mwaka 2006 mpaka 2015, watuhumiwa 139 wametiwa
nguvuni, miongoni mwao wako watuhumiwa 16 wa matukio ya Desemba
na Januari mwaka huu. Mashauri 35 yamefunguliwa mahakamani na kati
ya hayo 10 bado yanaendelea na yapo katika hatua mbalimbali.
Watuhumiwa 73 wameachiliwa na 15 wamepatikana na hatia. Kati ya hao
waliopatikana na hatia 13 wamehukumiwa kifo na wawili wamepata
kifungo cha miezi 6. Watuhumiwa kwa matukio sita bado wanasakwa.
Matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yametokea
katika mikoa kumi kati ya mikoa 30 hapa nchini.

Mikoa hiyo ni hii

ifuatayo: Mwanza matukio 13, Kagera sita, Tabora matano, Geita manne,
Mara manne, Kigoma manne, Simiyu matatu, Shinyanga mawili, Arusha
moja na Mbeya moja. Utaona matukio 41 kati ya 43 yametokea katika
ukanda wa ziwa ambapo pia wanaongoza kwa mauaji ya vikongwe na
wanawake kwa sababu za ushirikina.
Ndugu Wananchi;
Inawezekana kuwa matukio ya hivi karibuni yanaashiria kuwa
uhalifu huu unataka kuibuka upya. Napenda kuwahakikishia ndugu zetu
wenye ulemavu wa ngozi na Watanzania kwa jumla, kuwa hatutaacha hali
iwe mbaya kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Tutatumia mbinu na

maarifa tuliyoyatumia kukabili wimbi kubwa la mauaji lililokuwepo


mwaka 2007 na 2008 na kwa sababu hiyo tukaweza kupunguza hadi
kufikia kutokuwa na tukio lolote la mauaji mwaka 2011.
Tunachokiomba kutoka kwa wananchi ni ushirikiano na msaada wa
kuwafichua watu wanaofanya vitendo vya mauaji na kukata viungo vya
watu wenye ulemavu wa ngozi.

Pia wasaidie kutoa taarifa kuhusu

10

wanunuzi wa viungo hivyo na waganga wanaochochea mahitaji ya viungo


vya albino.

Ushirikiano wa wananchi wa wakati ule uliwezesha

kupatikana kwa mafanikio niliyaeleza. Naamini safari hii tukifanya hivyo


tutafanikiwa pia.
Ndugu Wananchi;
Kutokomeza kabisa matukio ya mauaji na ukataji wa viungo vya
watu wenye ulemavu wa ngozi ni jambo linalowezekana.

Hata hivyo,

litategemea watu kuacha imani za ushirikina. Imani potofu, ati kuwa mtu
akiwa na kiungo cha mtu mwenye ulemavu wa ngozi atafanikiwa katika
shughuli zake za biashara, uvuvi na uchimbaji wa madini ndicho
kichocheo cha uovu wote huu unaoendelea. Ni ujinga ulioje kwa mtu
kuamini kuwa mafanikio yake hayatategemea juhudi zake na maarifa yake
bali kuwa na kiungo cha mwanadamu mwenzake mwenye ulemavu wa
ngozi.
Nilisema katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi Machi, 2008
kwamba, kama kuwa na kiungo cha albino ndiko kutakakomfanya mtu
kufanikiwa katika shughuli zake za kibiashara na kiuchumi basi ndugu
zetu wenye ulemavu wa ngozi wangekuwa ndiyo matajiri wakubwa nchini
na duniani. Maana wao sio tu wana viungo bali wana mwili mzima.

Kwa

sababu ya kuwepo imani hizi za hovyo, juhudi za kuelimisha jamii


kuachana na imani hizi potofu ziongezwe. Naomba hili ndilo liwe jambo la
msingi katika mapambano haya. Tukifanikiwa katika hili, matatizo yote
haya yatakoma. Serikali na jamii haitalazimika kushughulikia mambo haya
ambayo siyo tu ni fedheha hata kumsimulia mtu bali yanatisha na
kusikitisha.
Ndugu Wananchi;
Wiki ijayo nitakutana na baadhi ya viongozi na wanachama wa
Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi. Nimekubali maombi yao ya
kukutana nao ili niweze kusikiliza maoni yao na tubadilishane mawazo juu
ya namna bora ya kumaliza tatizo hili. Mimi naamini kuwa ushirikiano wa

11

karibu kati ya Serikali na jamii utatuwezesha kutokomeza mauaji ya ndugu


zetu wenye ulemavu wa ngozi na kuliondolea taifa letu aibu hii.
Ziara ya Zambia
Ndugu Wananchi;
Tarehe 25 na 26 Februari, 2015 nilifanya ziara ya siku mbili ya
kiserikali nchini Zambia kwa mwaliko wa Rais mpya wa nchi hiyo,
Mheshimiwa Edgar Lungu. Ziara ilikuwa na mafanikio makubwa. Mimi
na ujumbe wangu tulifarijika sana kuona kuwa mawazo ya nchi zetu mbili
yanashabihiana sana kuhusu namna ya kuimarisha na kuboresha uhusiano
wetu na ushirikiano na uhusiano wa nchi zetu mbili.

Kimsingi

tumekubaliana katika masuala yote muhimu tuliyoyazungumza.


Kuhusu TAZARA tumekubaliana kuchukua hatua thabiti kutatua
matatizo ya kiungozi, kifedha na kiufundi yanayolikabili shirika letu hilo
hivi sasa.

Tumeelewana kuwa hatuna budi kufanya marekebisho ya

kimfumo na kiutendaji ili kutatua matatizo ya kimuundo na kimenejimenti


yanayochangia kuzorota kwa ufanisi wa Shirika.

Tumekubaliana pia

kuwa, Serikali zetu mbili zitekeleze ipasavyo wajibu wake kwa TAZARA
ikiwa ni pamoja na kutoa mchango wake wa fedha kwa ajili ya kulifufua
Shirika hili muhimu kwa uchumi wa nchi zetu mbili.
Ndugu Wananchi;
Tumekubaliana pia, kwamba, tuangalie uwezekano wa kuruhusu
makampuni au mashirika mengine ya reli kutumia reli ya TAZARA
kusafirishia mizigo yao kwa kulipa ushuru kwa TAZARA kwa huduma
hiyo. Tumeagiza Baraza la Mawaziri kulifanyia kazi wazo hili jema ili
litekelezwe mapema iwezekanavyo.
Kwa upande wa sekta ya nishati, tumekubaliana kuwa, nchi zetu
mbili ziendelee kushirikiana kuimarisha bomba la mafuta la TAZAMA.
Ndugu zetu wa Zambia walitueleza dhamira yao ya kutaka kujenga bomba
la kusafirisha gesi kutoka Dar es Salaam hadi Zambia.

Wameomba

12

tukubali kuwauzia gesi asilia.

Niliwaeleza ni jambo linaowezekana,

tumekubaliana nchi zetu zilifanyie kazi ombi hilo.


Serikali ya Zambia, imeahidi kuimarisha njia ya umeme kutoka
Kasama

hadi

Mbala

Zambia

inakoanzia

njia

inayoleta

umeme

Sumbawanga. Kufanya hivyo kutaondoa matatizo ya sasa ambapo umeme


unaofika Sumbawanga kutoka Mbala huwa mdogo kiasi kwamba hauna
nguvu ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani, maofisini na viwandani.
Kwa sababu hiyo, hata mpango wa kuupeleka umeme huo Namanyere,
Nkasi na Mpanda haukuweza kutekelezwa kama ilivyokuwa imekusudiwa
awali.
Ndugu Wananchi;
Kuhusu kuboresha huduma kwa abiria na mizigo katika mpaka wa
Tanzania na Zambia pale Tunduma, tumekubaliana kuwa, Serikali ya
Tanzania ikamilishe ujenzi wa jengo

litakalowezesha huduma zote

muhimu za mpakani kutolewa katika jengo hilo (One Stop Border Post).
Wakati tunasubiri kukamilisha ujenzi huo, tumekubaliana tuwe na jengo la
muda la kurahisisha taratibu za usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo
katika mpaka wetu na Zambia.
Vilevile, tulizungumzia njia za kuimarisha na kuboresha taratibu za
forodha kwa mizigo itokayo bandari ya Dar es Salaam kwenda Zambia na
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia Zambia. Tumekubaliana kuwa,
Mamlaka ya Kodi ya Mapato ya Zambia iangalie uwezekano wa kuwaweka
maafisa wake katika Bandari ya Dar es Salaam kama inavyofanyika kwa
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hii itarahisisha taratibu
za forodha kwa bidhaa za Zambia katika bandari yetu.

Jamhuri ya

Kidemokrasia ya Kongo imeshaanza mchakato wa kupata fursa hiyo. Kwa


jumla, ziara ilikuwa ni yenye mafanikio makubwa.
Rambirambi
Ndugu Wananchi;

13

Wakati tulipokuwa tunajiandaa kurekodi hotuba hii tukapata habari


ya huzuni na majonzi makubwa ya kifo cha Mbunge wa Mbinga
Magharibi, Mheshimiwa Capt. John Damian Komba.

Kifo chake

kimeliondolea taifa letu mmoja wa viongozi wake wazuri, msanii mahiri,


raia mwema na mzalendo wa kweli. Marehemu alitumia muda mwingi wa
maisha yake kuelimisha jamii kuhusu mambo mema, amefanya hivyo
akiwa mwalimu na baadaye Kiongozi wa Kikundi cha Sanaa cha JWTZ na
hapa mwishoni kiongozi wa kikundi cha Tanzania One Theatre cha Chama
Cha Mapinduzi. Kwa kutumia kipaji alichojaaliwa na Mola wake ametoa
mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu na ustawi wa Chama
Tawala.

Daima tutamkumbuka kwa mambo mengi mema aliyoifanyia

jamii ya nchi yetu na taifa kwa jumla.


Ndugu Wananchi;
Katika salamu zangu za rambirambi kwa Spika wa Bunge na Katibu
Mkuu wa CCM niliwaomba kupitia kwao salamu ziwafikie Wabunge wote
na viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi. Hali kadhalika,
niliomba kupitia kwao salamu ziwafikie familia ya marehemu Capt. John
Komba. Kwa familia ya ndugu yetu mpendwa, napenda kuwahakikishia
kuwa tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na
maombolezo.

Tunawaombea kwa Mola awape moyo wa subira na

uvumilivu. Wananchi wa Wilaya ya Nyasa tunawapa pole nyingi kwa


msiba mkubwa uliowakuta na pengo kubwa mlilolipata.

Nawaomba

watambue kuwa namna bora zaidi ya kumlilia Mbunge wao aliyewapenda


ni kudumisha mema yote aliyofanya na kukamilisha zile kazi ambazo
alikusudia kuzifanya lakini hakuweza kufanya hivyo kwa sababu ya
kukutwa na umauti.
Mwisho nawaomba, Watanzania wote tuungane na familia yake
kumwombea marehemu Capt. John Damian Komba mapumziko mema.
Amin.

14

Mungu Ibariki Afrika!


Mungu Ibari ki Tanzania!
Asanteni kwa kunisikiliza.

You might also like