You are on page 1of 3

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

Itakumbukwa kwamba, mnamo tarehe 13 June 2016, Wizara ya Afya, Maendeleo


ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea taarifa kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma inayotambua uwepo wa ugonjwa usiofahamika katika
Wilaya ya Chemba. Ugonjwa huu ulianza kuwakumba wanafamilia moja ambapo
watu 9 wameugua wakitokea kijiji cha Mwaikisabe, kata ya Kimaha, Wilayani
Chemba. Na baadae wagonjwa wengine kuanza kupatikana katika vijiji vya karibu
vikiwemo, Soya(3), Itolwa(4), Kelema balai(1), Gubali(1), Chemka(1), Kintima (1),
Ilesi(1) na Ubembeni Wilaya ya Kondoa (1).
Wagojwa hawa walikuwa na dalili za kutapika, kuharisha, kupata rangi ya manjano
machoni na sehemu nyingine za mwili. Sambamba na dalili hizo pia, walionekana
kuwa na maumivu ya tumbo na hatimaye kuvimba tumbo kwa kujaa maji ndani ya
muda mfupi. Wagonjwa hawa hawakuwa na joto kali, wala harara katika ngozi.
Ugonjwa huu umeonekana kuwapata makundi ya watu wote wakiwemo, watu
wazima na watoto. Inaaminika kwamba, wagonjwa wa mwanzo walipatwa na
ugonjwa huu baada ya kutumia nyama ya ngombe ambaye alichinjwa kwa
kuvunjika mguu hapo kijijini. Hata hivyo, wanakijiji wengine hawakuugua licha ya
kutumia nyama hiyo hiyo. Vile vile ugonjwa huu umeathiri wanyama ambao ni
mbwa wakubwa 3, mbwa wadogo wa 3 na paka 1 katika familia hii ambao pia
walikufa.
Mpaka kufikia tarehe 18 Juni 2016, Wagonjwa wameendelea kuongezeka siku
hadi siku na kupelekea ongezeko la wagonjwa kufikia watu 21, ambapo kati yao 7
wamefariki. Wagonjwa hawa wanatibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na
Hospitali ya Wilaya Kondoa. Hali ya wagonjwa wengineo ni nzuri isipokuwa wawili
ambao ni watoto hali zao bado si nzuri. Wagonjwa hawa bado wako wodini kwa
kuogopa ugonjwa kuendelea kusambaa.
1

Hatua zilizochukuliwa
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana
na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, wamefanya yafuatayo katika
kudhibiti na kuzuia athari za ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na;
a) Kuhudumia wagonjwa hawa katika Hospitali tajwa hapo juu kwa kutenga
wodi maalum
b) Kuunda kamati mbali mbali zikiwemo za
a. Madawa
b. Matibabu
c. Uhamasishaji na utoaji Elimu
d. Maabara
c) Kupeleka timu ya mwanzo ya Wataalamu wa Afya, Wilayani Chemba na
Kondoa kwa uchunguzi wa awali. Aidha maandalizi ya timu nyingine kutoka
ngazi ya Taifa inayoundwa na Daktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa
Muhimbili, Epidemiolojisti, Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa
Serikali, TAMISEMI na Taasisi ya Chakula na Dawa (TFDA) inawasili leo
tarehe 19/6/2016 ili kuongeza nguvu za uchunguzi zaidi. Vile vile, wataalam
wa Sekta ya Kilimo na Mifugo wanaungana na timu inayoendelea na
uchunguzi.
d) Kuchukua vipimo vya sampuli za maabara kwa ajili ya utambuzi wa ugonjwa
ambapo; Damu, mkojo, kinyesi, matapishi, Vinyama vitokanavyo na ini
vimechukuliwa. Sampuli hizi zote zimepelekwa katika Maabara ya Taifa,
Mkemia Mkuu wa Serikali na Maabara ya Kilimanjaro Christian Research
Institute (KCRI), iliyopo Kilimanjaro kwa uchunguzi zaidi.
e) Sampuli za vyakula aina ya nafaka vimechukuliwa kwa ajili upimaji.
Aidha, vipimo vya awali ambavyo vilifanywa na Maabara Kuu ya Taifa vinaonesha
kutokuwepo kwa homa ya manjano, wakati huo huo wanaendelea kufanya vipimo
vingine ikiwemo Homa ya Rift Valley (RVF). Pia tunatazamia kuanza kupata
majibu mengine kutoka kwa Mkemia Mkuu siku ya Jumanne, tarehe 21 Juni 2016.
2

Linganifu na taarifa za awali, tunatazamia kuwa ugonjwa huu unaweza


kuhusishwa na ulaji wa vyakula vyenye sumu kuvu (Aflatoxins) ambapo
hupatikana kutokana na matumizi ya vyakula vya namna mbalimbali na
visivyohifadhiwa vizuri. Hii ni kinyume na mtazamo wa wale wanaosema kuwa
ugonjwa huu ni kimeta, kwani kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, ugonjwa
haunekani kuwa ni wa kuambukizwa ila unaweza kutokana na matumizi ya kitu
ambacho ni maarufu kwa kundi hili la watu. Sampuli za nafaka kutoka katika
familia zilizoathirika zimechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi ngazi ya Taifa na
TFDA na Mkemia Mkuu toka jana. Tunategemea kupata ya majibu kutoka TFDA
kesho siku ya Jumatatu mchana.
Lengo ni Kuutambua Ugonjwa Huu Haraka
Wizara inashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Shirika la Afya Duniani
(WHO) na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (Centre for Disease Control (CDC), Ofisi
ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika kuhakikisha kuwa ugonjwa huu unatambuliwa
kwa haraka na hivyo kupunguza wingu la wasiwasi lilojaa miongoni mwetu, na
hasa kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma.
Wizara itaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wananchi ili waweze
kuelewa kuhusu ugonjwa huu. Aidha, ninatoa rai kwa jamii, kuacha kutiliana
wasiwasi na kushutumiana kwa kupigana, badala yake wahimizane kwa yeyote
yule atakayeumwa na dalili kama zilizotajwa hapo juu, awasili au kumpeleka kituo
cha Afya ili aweze kusaidiwa kwa haraka.
Natoa shukurani kwa makundi ya jamii, watu na Mashirika ya Kimataifa kwa
mchango wao mkubwa katika jitihada zetu za kuutambua ugonjwa huu.

Imetolewa na:
Ummy Mwalimu (Mb)
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto,
DODOMA.
19/6/2016

You might also like