You are on page 1of 2

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI



TAARIFA KWA UMMA

UFAFANUZI KUHUSU ZAWADI KWA WANAFUNZI WALIOFANYA VIZURI
KATIKA MTIHANI WA KUMALIZA ELIMU YA MSINGI NA SEKONDARI
MWAKA 2013

Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Elimu kilifanyika tarehe 10 Mei, 2014 katika
uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma ambapo tuzo mbalimbali zilitolewa zikiwemo za
fedha na zile zisizo za fedha kwa makundi tofauti tofauti.

Tuzo ya fedha taslimu ilitolewa kwa wanafunzi 30 waliofanya vizuri katika mtihani
wa mwaka 2013 ambapo wanafunzi watano bora wasichana na watano bora wavulana
waliofanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya kumaliza Elimu ya Msingi walipata
shilingi 125,000/=, Wanafunzi watano bora wasichana na watano bora wavulana
waliofanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya kumaliza Elimu ya Sekondari Kidato
cha Nne walipata shilingi 250,000/= na Wanafunzi watano bora wasichana na watano
bora wavulana waliofanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya kumaliza Elimu ya
Sekondari Kidato cha Sita walipata shilingi 500,000/=.

Fedha hizi zilitolewa na serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
pamoja na Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China na zilitolewa kama fedha taslimu.

Aidha, fedha nyingine taslimu iliyotolewa ilikuwa ni Hundi ya Shilingi 3,000,000/=
kwa walimu wa shule 60 zilizoongeza ufaulu katika mtihani wa mwaka 2013.

Pamoja na fedha taslimu za shilingi 250,000/= wanafunzi 10 wa Kidato cha Nne
walipewa vocha za thamani ya shilingi 500,000/= kwa ajili ya kununulia vitabu vya
kiada na ziada.

Aidha, Wizara imeamua kuwakabidhi wanafunzi 10 wa Kidato cha Nne fedha taslimu
Sh. 500,000/= badala ya vocha ili wanunue vitabu wao wenyewe. Hii ni kwasababu
wanafunzi hawa wanaweza kujiunga na Kidato cha Tano katika tahasusi
(combination) mbalimbali na ni vyema wakanunua vitabu kulingana na tahasusi zao.

Katika kutoa zawadi hizo yamejitokeza mapungufu kadhaa ambayo yalisababisha
usumbufu kwa baadhi ya wanafunzi na wazazi wao waliofika Dodoma kupokea
zawadi hizo.

Wizara inaomba radhi kwa wanafunzi na wazazi hao kutokana na usumbufu
uliojitokeza. Aidha, matatizo yaliyojitokeza yameshatatuliwa.

Prof. Sifuni E. Mchome
KATIBU MKUU
26/5/2014

You might also like