You are on page 1of 3

1

STATE HOUSE ZANZIBAR


OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE
Zanzibar 15.06.2017

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed


Shein amesema kuwa utamaduni wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China wa
kuendelea kuleta Madaktari kila baada ya miaka miwili ni hatua muhimu katika
kuimarisha sekta ya afya hapa Zanzibar sambamba na kukuza uhusiano na
ushirikiano mwema kati ya nchi mbili hizo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar katika mazungumzo kati yake na
Madaktari wapya pamoja na wale wanaomaliza muda wao kutoka Jamhuri ya Watu wa
China, wakiongozwa na Balozi Mdogo wa nchi hiyo anayefanya kazi zake hapa
Zanzibar Balozi Xie Xiaowu.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alieleza kuwa utamaduni wa nchi hiyo wa kuleta
Madaktari kwa ajili ya kutoa huduma za afya hapa Zanzibar ni wa kihistoria ambao
umeanza tokea mwaka 1964 na kuendelea hadi hivi leo ambapo China ilianza kuleta
wataalamu wake mbali mbali hapa Zanzibar wakiwemo Madaktari.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wa


Zanzibar wanathamini na wanazipenda huduma zinazotolewa na Madaktari kutoka
nchini China ambao wamekuwa wakishirikiana vyema na Madaktari wazalendo kutoa
huduma hizo kwa ufanisi mkubwa hapa Zanzibar.

Pia, Dk. Shein, alitumia fursa hiyo kueleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya
China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar huku akiahidi
kuendelezwa na kudumishwa na kusisitiza kuwa China imeweza kutoa mchango
mkubwa katika mafanikio ya sekta ya afya na sekta nyengine mbali mbali hapa
Zanzibar ikiwemo sekta ya viwanda, elimu,kilimo, michezo, habari na nyengienzo.

Dk. Shein aliwakaribisha Madaktari hao wapya hapa Zanzibar na kuwaaga wale
waliomaliza muda wao huku akieleza matumaini yake makubwa kuwa madaktari hao
2

wapya kuwa watafanya kazi kwa ufanisi mkubwa zaidi kama wenzao wanao ondoka
ambao wamefanya kazi vyema katika kutoa huduma za afya.

Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Madaktari 21 wanaomaliza muda wao kwa
kusaidia kutoa huduma mbali mbali za afya ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa
madaktari na wauguzi kwa vitendo yakiwemo mafunzo ya upasuaji na matumizi ya
mashine mpya katika hospitli ya Mnazi Mmoja ikiwemo mashine mpya za kisasa
(TURP), zikiwemo upasuaji wa matatizo ya mkojo pamoja na tiba ya njia ya mfumo wa
chakula pamoja na huduma nyenginezo.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China
chini ya kiongozi wake Rais Xi Jingping kwa kuendelea kuisaidia na kuiunga mkono
Zanzibar katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo hapa Zanzibar.

Akitoa pongezi hizo, Dk. Shein alisema kuwa Rais Xi Jingping ameweza kutekeleza
makubaliano yote aliyoahidi kuisaidia Zanzibar ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali
ya Abdalla Mzee pamoja na vifaa vyake ambao tayari umekamilika, ujenzi wa uwanja
wa Maotsetung, ujenzi wa Bandari mpya ya Mpigaduri, ujenzi wa jengo jipya la abiria
katika kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume na miradi mengineyo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alimueleza Balozi mdogo huyo wa China kuwa ipo
haja kwa China kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake za kuendeleza
sekta ya afya kwa kuunga mkono uendelezaji wa kitengo cha saratani, kitengo cha
maradhi ya mkojo na vigo pamoja na uanzishwaji wa kitengo cha upasuaji wa moyo ili
huduma hizo ziweze kutolewa hapa hapa Zanzibar ambapo tayari baadhi ya huduma
hizo zimeshaanza kutolewa.

Dk. Shein alieleza kuwa miongoni mwa juhudi ilizoanza kuchukua Serikali katika
kuviimarisha vitengo hivyo ni kutoa mafunzo kwa madaktari wachache wa vitengo
hivyo pamoja na baadhi ya vifaa lakini hata hivyo alisisitiza haja ya kuungwa mkono
ili kuongeza nafasi zaidi za masomo kwa ajili ya madaktari na wataalamu wa kada
hizo, vifaa na mambo mengineyo hasa ikizingatiwa kuwa nchi hiyo imepiga hatua
kubwa katika kada hizo.

Nae Balozi Mdogo wa China anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Balozi Xie Xiaowu
alimueleza Dk. Shein kuwa timu ya 26 ya Madaktari kutoka nchini China
inayomaliza muda wake imefanya kazi vyema na kuahiadi timu ya 27 nayo itafuata
nyayo hizo hizo kwa kufanya vizuri sambamba na kuhakikisha inatoa ushirikiano
mkubwa kwa wananchi, madaktari wazalendo pamoja na viongozi wa Serikali.

Balozi Xie Xiaowu alimuhakikishia Dk. Shein kuwa China itaendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuimarisha miradi yake ya maendeleo sambamba na kuimarisha
3

uchumi wake kwa kutambua kuwa nchi mbili hizo zinaurafiki na udugu wa miaka 53
tokea Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964.

Nae kiongozi wa Madaktari hao waliomaliza muda wao, Dk. Xu Zhuoqun alitoa pongezi
kwa mashirikiano mazuri aliyoyapata kutoka kwa viongozi wa Serikali, madaktari
wazalendo pamoja na wananchi wakati wote walipofanya kazi zao hapa Zanzibar huku
wakiwasifu watu wa Zanzibar kwa ukarimu wao mkubwa.

Nao Madaktari wapya chini ya kiongozi wao Dk. Wang Hao, walitoa shukurani kwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa makaribisho na
mapokezi mazuri waliyoyapata hapa nchini na kuahidi kutoa ushirikiano wao kwa lengo
la kuwasaidia wananchi wa Unguja na Pemba katika kutoa huduma ya afya.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar


Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

You might also like