You are on page 1of 14

Tanzania nyumbani sikuzaliwa bahati mbaya

‘’nimekukimbilia wewe Bwana nisiaibike milele, kwa haki yako uniponye uniopoe, unitegee sikio lako,
uniokoe. Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, nitakako kwenda siku zote. Umeamuru niokolewe,
ndiwe genge langu na ngome yangu. Ee Mungu, Wangu uniokoe mkononi mwa mkorofi katika mkono
wake mwovu mdhalimu. Maana wewe ndiwe taraja langu, Ee Bwana Mungu tumaini langu toka ujana
wangu. Nimekutegemea tangu kuzaliwa, ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, ninakusifu wewe
daima’’ (zaburi 71:1-6)
Kupitia maisha ya watu tofauti tunajifunza na kupotoka pia, hii inatokana na upeo wa mwenyekujifunza
katika kupambanua mambo yanayomzunguka, lakini uzoefu ni njia kuu ya kujifunza na kuchukua hatua.
Mwanafunzi anapofeli mtihani haimaanishi ndio mwisho wa safari kufikia malengo yake. Tunarudi katika
upeo binafsi katika kupambanua mambo. Mfano umemtumia ujumbe mfupi wa maneno mchumba
wako ambaye anaimani kuwa ipo siku utamuoa au utaoana naye.

Ujumbe huo unaosema ‘’ tarehe 28 desemba 2015 nataraji kumuoa binti nimpendae, kwa hiyo tarehe
29 ya mwezi huo nitakuwa nimeachana na ukapera” kwa haraka mchumba huyo atakasirika kwa kuwa
angetaraji umtaje yeye kwa jina kuwa tarehe hiyo nitakuoa. Lakini kumbe umeandika tarehe yake ya
kuzaliwa, ukiwa na maana ya kuwa siku yake ya kuzaliwa ndiyo itakuwa harusi yenu. Angejipa muda wa
kutafakari na kupambanua mambo ili kujua kwa nini ifanyike tarehe hiyo na si tarehe nyingine angejua
thamani yake.

Taharuki mara zote zinatufungia milango ya Baraka, zinatuondoa katika fikra sahihi za kuwaza mambo
yaliyo mema anayotuwazia Mungu. Mawazo mabaya yanatufanya kusahau asili yetu na kukumbatia asili
zisizo na maana. Mara nyingi tunadhani tunaonewa badala ya kuona fursa zilizo ndani ya uonevu na
kushinda ugumu wa maisha, kujipima uwezo wa kufikiri na kutatua matatizo magumu kwa njia rahisi
ambazo zitatuweka salama na jamii na kuwa na amani katika maisha.

‘wanafunzi nane kati ya wanafunzi 150 wa chuo kikuu walifeli somo la upigaji wa picha, kati ya hao
mwanafunzi mmoja alikaa akatafakari kwa nini nimefeli somo hili. Rafiki yake aliyefaulu somo lile
akamshauri akate rufaa kupinga matokeo. Lakini mwnafunzi Yule alimjibu rafiki yake kuwa unadhani
nalifahamu somo hili kweli kweli?. Rafiki akamwambia tatizo ni kuharibu cheti chako, mwanafunzi Yule
akaingia katika mtandao na kujifunza ili aone je nchi zingine wanasomaje lile somo!!! Akakuta nchi ya
marekani somo la kupiga picha peke yake wanajifunza kwa zaidi ya miaka miwili darasani na kwa
vitendo. mwanafunzi Yule akajipa moyo kwa kusema kama wenzetu wanasoma miaka miwili kuna ubaya
gani kama mimi nitalisoma somo hili kwa mwaka mmoja?. Akalipenda somo na kuona fursa iliyopo
katika kufeli kwake na hatimaye akajifunza kwa bidii na akafaulu somo lile kwa kulielewa zaidi ya
mwanzo.

Kweli ya leo sio ya jana!!!!!!!!.


Watu wengi wanafungwa kifikra na imani na matokeo yaliliyopita katika maisha. Haishangazi
kuona watu wakisimamia historia katika kuamua mambo yajayo au yatarajiwayo kutokea. Lakini
mtu anaweza kubadirika jinsi alivyokuwa mwanzo na kuwa mpya na mwenye tabia mpya yenye
kuvutia na kuwa na mtazamo mpya kabisa.

Kuna baadhi ya watu hutumia makosa ya jana kuwahukumu watu wa leo au kizazi cha kesho
kwa hayo. Huwezi kuita kinyesi chakula, eti kwa kuwa tu kinyesi kinatokana na chakula
anachokula kiumbe. Ata mganga wa jadi au mpiga ramli au mwizi na jambazi wa siku za nyuma
anaweza kuwa mchungaji wa leo au kesho.

Vijana wanatakiwa kuachana na mawazo potofu kuwa kuna familia ya matajiri na kizazi cha
masikini. Waliofanikiwa wengi wametoka katika familia maskini sana, lakini hawakuutukuza
umaskini wao. Waliulaani umaskini kwa kuchukua hatua kwa kufanya kazi kwa bidii na
kuutukuza utajiri hatimaye wakaukwaa ukwasi.

Tanzania imekuwa na mifano hai mingi katika kuwatoa baadhi ya watu maskini na kuwa matajiri,
viongozi bora, maarufu na wenye nyadhifa nzito duniani. Tatizo ni kwamba huwa wahusika sio
wepesi kutukuza kwao ili vijana wa leo wajifunze na wachukue hatua.

Mfano kisiwa cha Ukerewe ndiko wanatoka spika wa zamani wa bunge la jamuhuri ya
mmungano wa Tanzania Pius Msekwa na mama Getruda Mongera. Hawa wanatoka katika vijiji
ndani ya kata ya Murutunguru ambako umeme ndio umefika mwaka huu(2013). Ukitaka kupata
funzo kutoka kwao unaweza kujiuliza walitumia mbinu gani kufikia hapo walipo, mazingira ya
vijiji vyao ni umaskini lakini wameweza kutikisa nchi na wameweza kuongoza taasisi kubwa na za
heshma katika nchi.

Umaskini wa ukoo sio lazima uwe wa kila mwanaukoo kama ambavyo sio kila mwenye ukoo
anaweza kuwa raisi wa nchi eti kwa kuwa aliyewatangulia aliwahi kuwa raisi. Nakumbuka kuna
wakati nilikuwa nilitazama familia yangu hakuna aliyekuwa amefika chuo kikuu nilikata tama
sana. Nilienda mbali zaidi kwa kuangalia kota yetu pale Tandika maghorofani iliyokuwa na kaya
nne ambapo hakuna kijana aliyewahi kufaulu kidato cha nne.

Lakini nikiwa kidato cha tatu kuna dada aliitwa Sharifa alifaulu kidato cha nne kwa kupata daraja
la pili. Hapo ndipo nikapiga moyo konde kuwa sitakiwi kujihesabu kama mwanafamilia ya mzee
Rwambogo maana ndani ya kota yetu kuna mtu amefanya vizuri. Nikaanza kusoma kwa bidii
nikimtazama sharifa kama kioo katika masomo, ingawa nilikuwa nimechelewa lakini nilipata
nafasi ya kusoma kidato cha sita ingawa haikuwa nafasi ya kwenda serikalini.
Tunatakiwa kuwaiga waliofanikiwa tu, walioanguka na kupotea tunatakiwa kuwaombea tu.
Kama huoni wa rika lako aliyefanikiwa katika familia, tazama jinsia yako mahali popote.
Tusijifunge kwa kuwatazama waliokaribu yetu pekee bali tuwatazame waliofanikiwa duniani
kote wawe mfano wetu.

Tuthaminiane Leo maana kesho hakuna anayeijua.


“Mazoea yana tabu lakini yana mwisho wake” Nilipokuwa naanza kazi niliona nikithaminiwa
sana kuwa sehemu ya familia ya kampuni niliyokuwa ndo kwanza nimeanza nayo katika maisha
yangu ya ajira. Lakini kila muda ulivyozidi kwenda niliona thamani yangu ikishuka kutokana na
kauli za mabosi wangu nilizokuwa nazisikia chinichini kutoka kwa wafanyakazi wenzangu.

Hakuna jipya ni mazoea tu yanayojengeka kwa waajili wakikumbatia ule msemo wa wahenga
usemao“kipya kinyemi”. Mala nyingi waajili huwathamini sana wafanyakazi wapya na
kuwadharau wale wa zamani, ndio maana katika hili kuna misemo miingi sana baadhi ni “nabii
hakubaliki nyumbani” usiache mbachao kwa msala upitao” ukisema wewe cha nini wenzako
wanasema watakipata lini”

Misemo yote hiyo ni kumkumbusha binadamu kuwa mthamini uliyenae, maana hautakuwa nae
milele. Ndio maana ata walioko katika mahusiano wanawadharau walionao kwa wakati huo na
kuwathamini wasio wa kwao. Hivi kama unashindwa kumthamini mke wako aliekuzalia Watoto
na amaekupikia na kukufulia nguo kwa zaidi ya miaka nenda rudi unataka nini.

Tatizo ni mazoea tu!!! Mke akifa au mume akifa ndio utasikia watu wanajuta na kusaga meno.
Tunatakiwa kuwathamini wazazi, majirani, Ndugu na viongozi wetu japo kwa uchache wa mema
waliyotutendea wakiwa hai ili watuachie Baraka zao. Wengi wetu unakuta tuanamwaga sifa
kibao pindi tunapokuwa hatuna uwezo wa kukutana na kuwapa sifa zao hao watu wetu
muhimu.

Siku hizi umezuka mchezo wa kuwaita baadhi ya watu vibaraka wa pande Fulani au chama
Fulani pindi wanaposema ukweli. Ukweli hautengwi ata usipousema leo ipo siku utauhubiri bila
kukusudia.

Vijana tumeshindwa kuthamini ujana wetu kwa kuwa hatujui thamani yake leo. Lakini ata wazee
wengi walioukosea ujana wao ukikutana nao mtaani utawajua tu. Kwa nini tusijilinde na
kujithamni tungali tunanguvu za kutosha. Vijana wengi kati ya miaka 18 na 35 hawana mipango
ata ya mwaka mmoja mmoja lanini wanandoto ya kuja kuishi maisha bora siku za usoni. Kesho
hujengwa na leo, leo ilikwishajengwa na jana.
Ubaguzi wowote ni laana!!
Hulka ya binadamu hujiona ni bora kuliko binadamu yeyote, haki hiyo inaperekea ubaguzi hasa
wa kiushindani. Ni asili ya binadamu yeyote lakini pia ni laana ya binadamu yeyote kujiona
wewe ni bora kuliko mwenzao. Wengi wetu tunajiona ni bora kwa rangi zetu, imani zetu, asili
zetu, utaifa wetu na wakati mwingine kwa makabila yetu.

Kila binadamu ana mapungufu yake kama vitu vinavyotupa jeuri ya kuabaguana jinsi vilivyo na
mapungufu. Laiti kila binadamu angepewa kujua kuwa ukimbagua mwenzako kwa misingi ya
dini yake nyumba ya jilani mwanadini mwenzako anaweza kukubagua wewe kwa misingi ya
rangi yako tusinge mbagua mtu kwa dini yake.

Tumeona wachezaji mpira weusi huko ulaya, wakifunga gori wanashangalia kwa ishara ya
msaraba wakiashiria wao ni dini moja na robo tatu ya waliokuja kutazama mpira huo. Lakini
jukwaa la pili wanamrushia ndizi kwa weusi wa rangi yake, wanapiga mbiu ya sokwe mtu kwa
asili ya anakotoka.

Baadhi ya watu huchinja kama kuku watu wa rangi nyeupe kwa imani za kishirikina. Kubwa zaidi
wanakijiji wanauziana ardhi kwa bei ya kutupa kwa kuangalia rangi zao, anapokuja mtu mweupe
ata kama kazaliwa kimbangulile kama mwekezaji. Ukabila nao umesahau dini, rangi au asili wa
kwetu kwanza mengine baadaye.

Jiulize wewe ni nani utakayekubalika kuanzia ndani kwako mpaka kwa nyumba jilani. Na wote
tunapaswa kujua ardhi haibagui na bingu haibagui pia. Kwa imani zetu wote tunaonja mauti kwa
hiyo razima tuhifadhiwe ardhini bila kujali umri, rangi, dini, utaifa wala kabila unalotoka. Lakini
pia mbingu itatutenga katika makundimawili, wenye dhambi na wasio dhambi haijalishi
ulikuwaje huku duniani

Cha kujiuliza imani inatuzaa sisi au sisi tunaizaa imani. Huwa najiuliza ingekuwaje kama wazazi
wangu wangekuwa waislamu!! Na ingekuwaje kama ningezaliwa Mchaga au Mmatumbi?, au
ingekuwaje wazazi wangu wangekuwa wahindi? Jibu ni kwamba sina uchaguzi binafsi wa kuwa
dini Fulani au kabila Fulani au rangi Fulani. Na ndivyo ilivyo kwa binadamu weengi, ni neema tu
tunajikuta tayari tuna dini, rangi, kabila na wakati mwinine majina yakiwa yamekwishaandikwa
katika vyeti vya kuzaliwa.

Wakati mwingine tumekataa ushauri mzuri na wakufaa kwa kuogopa au kudharau baadhi ya
mawazo na maonyo ya watu makini kwa ajili ya imani zao, makabila yao na wakati mwingine
majina ya watu yamekuwa kikwazo kwetu kufikia malengo yetu. Inafikia wakati tunaogopa ata
kula chakula chao ata kama tuna njaa, tumewakataza wototo wetu wasichangamane na baadhi
ya watoto wengine na ata wsisome shule Fulani kwa minajili ya aina za sare zinazovaliwa na
shule husika.

Baadhi ya maeneo watu wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kutafuta kufuata matibabu
kukwepa huduma za karibu kwa imani za kidini, ukabila, rangi na majina ya hospitali husika.
Wengine wamediriki kufungua mitandao na vyombo vya habari kwa ajili ya kukashifu na
kudhihaki imani za watu wengine, makabila ya watu wengine, lugha na uvaaji wa watu wengine.

Tukumbuke tulikotoka WOTE hatujaoteshwa kuwa imani Fulani, bali tumefuata imani za wazazi
wetu. Tumekuwa wakabila na rangi zetu hizi kwa kuwa hatukukuulizwa tuweje hapa duniani.
Pengine wewe ungeulizwa ungechagua dini Fulani au rangi Fulani kabla ya kuja duniani.

Makosa wa bwisya.
Kama ilivyo sehemu kubwa ya nchi maadili kwa vyombo vyetu vya dola yamepolomoka kama sio
kufa kabisa. Ukisikia kibaha askari kakamatwa na pembe ze ndovu basi kwingineko haishangazi
mwanajeshi mstaafu anamiliki kokolo(nyavu halamu ya uvuvi). Lakini vyombo vya dola
kujihusisha na matukio ya ujambazi na kisha kuwabambikia wananchi kesi ni jambo la kawaida
sana. Wakuu wa wilaya wanayajua haya, wakurugenzi, wakuu wa polisi na pengine ata baadhi ya
maraisi wa kiafrika wanajua na wanashiriki kwa namna moja au nyingine.

Tunakutana na kisa kimoja kinachosikitisha sana.. usiku mmoja palitokea tukio la ujambazi
ukara kisiwa jidogo katika wilaya ya ukerewe. Usiku wa kuamkia siku ya tukio palikuwa na
mabishano makubwa kati ya mlinzi wa nyumba ya kulala wageni na askari aliyekuwa amelala
akitaka kutoka usiku wa manane.

Mlinzi alimuuliza askari Yule unakwenda wapi usiku wote huu?. Askari akajibu nifungulie
mrango kuna kazi nataka nikafanye, mlinzi Yule alikataa akamwambia hakuna utaratibu huo
apa kwetu, kama ni kazi utaifanya kesho asubuhi. Baada ya mabishano marefu askari Yule
akajibu wanabahati hao wachibasi wanajifanya wanajua sana.

Baada ya dakika kumi kulisikika mshindo wa mtu akiruka ukuta na kuangukia upande wa pili wa
nyumba. Mlinzi Yule alipoenda kutazama akakuta kuna dariri za mtu kutoka nje, akaenda moja
kwa moja kwenye chumba alichokuwa amelala askari Yule, na kukuta mrango umefungwa kwa
nje na ndani hakuna mtu.

Usiku huo palitokea tukio la ujambazi, ambapo muhusika wa hilo duka alikwenda kuchukuliwa
nyumbani kwake ili akatoe fedha dukani kwake na kuwakabidhi watu hao. Wakafanikiwa kopola
zaidi ya milioni kumi na mbili usiku huo. Majambazi hao Wakiwa wanatoka kupola wakakutana
na mvuvi mmoja akiwa ametoka kuvua usiku, mvuvi alipowaona kuwa ni maaskari akajificha
bila wao kumuona na kumtambua.

Mvuvi yule aliwasikia maaskari wale wakisemezana ‘’wachibasi wajinga kweli fedha zote hizi
badala ya kuweka benki anakaa nazo ndani’’. Asubuhi ilipofika, mvuvi aliposikia kuna duka
limeibiwa alichokifanya akajitokeza na kuwataja maaskaari aliokutana nao usiku na
mazungumzo yao yalivyokuwa. Waananchi walikwenda kujazana katika nyumba ya wageni
kutaka kuwapiga kwa hasira.

Baada ya muda wakaja maaskari kutoka wilayani na kuwachukua maaskari wenzao. Askari
wale walikwenda moja kwa moja kufungua kesi mahakamani. Mtuhumiwa namba moja kwa
kesi ya uchochezi alikwa ni mvuvi na baadhi ya wananchi waliokuwepo siku ya tukio. Cha
kushangaza Pamoja na mwenye duka kutamka mbele ya wananchi kuwa ana uhakika
waliofanya tukio lile ni maaskari. Hakuonekana mahakamani na wala hakufungua kesi ya wizi
iliyokuwa ikiwakabili maaskari wale.
Kituko mahakamani, sijui ni sheria za wapi watuhumiwa hawaruhusiwi kuzungumzia kiini cha
wao kuwekwa kizuizini kwa kesi ya uchochezi. Kesi ilifanywa nyembamba kiasi cha watuhumiwa
kushindwa kujitetea na kubaki hawana maswali. Maana kiini ilikuwa ujambazi uliofanywa usiku
ule ndio ulizaa kesi ya uchochezi, hakimu wa wilaya kwa kejeri na masimango alikuwa akiwaita
watuhumia vimbelembele, wanaodakia mambo yasiyowahusu wakati kesi inaendelea.

Hakimu alidiriki kuwaambia ‘’kama mwenye duka hajafungua kesi kwa hawa nyie
kinachowawasha nini?. Kwenda kuhatarishaa maisha ya watu wakati aliyeibiwa ametulia tuli!!
Tunataka kuwakomesha ili tabia hii ikome na muache kudakia mambo yasiyowahusu..
alihitimisha hakimu na kusoma siku ya hukumu’’.

Vyombo vya dola vitaficha vielelezo lakini ukweli jamii inaujua, na itaendelea kuuishi ukweli huo
bila kikomo. Jamii mpaka kesho itaendelea kulaani vitendo vinavyofanywa na baadhi ya polisi
kukandamiza wanyonge na kuwatupa ndani kwa kigezo cha wao kushika makali. Watanzania
muishio bwisya na mahali popote yanapotokea mambo kama haya. Kazeni moyo yana mwisho
wake, watanzania wengi hawahukumiwi kwa haki na hawapewi fulsa sawa ya kujieleza mbele
ya vyombo vya dora.

Biblia katika kitabu cha isaya 40:3-4 inasema sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, itengenezeni
nyikani njia ya Bwana. Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wenu. Kila bonde litainuliwa
na kila mlima na kilima kitashushwa, palipopotoka patakuwa pamenyoka, na palipoparuza
patasawazishwa. Maandiko haya yanamanisha utawala dhalimu unakikomo chake, siku moja
utakuja kuangushwa na kuingia utawala wa wananchi.
Suruhisho sio wake wengi
Siku moja nilipokuwa natoka Ukara naenda nansio nilipanda meli na kijana mmoja mwenye umri
wa kati ya miaka 30 na 40. Kijana huyu ana wake wawili na ana Watoto sita mke mkubwa
Watoto wanne mke mdogo amezaa nae Watoto wawili. Anasimulia kisa cha kuoa mke wa pili na
sasa anataka kuwakimbia wake zake hao wawili akaoe mke mwiningine Magu mwanza ili wake
hawa aachnane nao kabisa.

Anasema ‘’wanawake watazame kwa nje tu, lakini ukikaa nao wanamapungufu
yasiyosameheka”. Anaongeza kwa kusema mke kilicho chake ni chake chako ni chenu wote,
unaweza kuuguliwa na mama mzazi asiende ata kumatazama hospital. Lakini kaka yake
akiumwa anataka wewe ndiye uwe mtumishi wa kumlea kaka yake huyo.

Kaka yangu huyo anadiriki kusema ata kaka yake ata baba yake mke mmoja alimshinda hivyo
akaoa wake nane na kaka ameoa wake wanne kazi anawazalisha na kuwaachia mzigo wanawake
hao walee Watoto. Kosa moja ambalo jamii haijawahi kulijua wala kulisikia ni kuwa mke ni jicho
la familia.

Jicho ni taa ya ya mwili, ukisema unalipa adhabu jicho, harafu ukalipa adhabu ya kutazama
hakuna adhabu hapo bali umelipa majukumu yake sahihi. Jinsia ya kike kulea Watoto ni jukumu
lake, mtazame simba, twiga, nyati, sungura na ata kuku jinsi asivyohtaji msaada wa malezi
kutoka kwa dume, ingawa wanaposaidiwa malezi hujiskia rahaaa sana.

Mwanamke kama jicho la familia anachohitaji kutoka kwa mume ni mwanga tu ili aweze kuona
vizuri. Lakini haimaanishi kiumbe yeyote mwenye jicho anaweza kufa kwa kukosa mwanga,
kamwe haiwezi kutokea na haijawahi kutokea. Petro 3:7 ‘’kadhalika ninyi waume, kaeni na
wake zenu kwa akili na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu, na kama
warithi Pamoja wa neema ya uzima kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe” .

Dariri ya zinazoonyesha mwanaume hana akili ni kama zifuatazo.


1) Kutoka nje ya ndoa aliyoiasisi yeye mwenyewe. Kuna mtu aliwahi kumwambia mtot
wake kuwa “ukitoka nje ya ndoa, bila shaka utaenda kutafuta ujuzi na jambo jipya
lililoboleshwa na mwanaume mwenzako mpaka kufikia wewe kutamani, kwa kutumia
akili ni rahisi kuboresha ulicho na uwakika nacho yaani mke wako kila siku ukawa
unamuona mpya kwa juhudi zako mwenyewe.
2) Kuongeza idadi ya wake Kwa kukimbia majukumu. Wengi wanaoa mke mwingne kwa
gharama ambazo angeweza kumboresha mke wake wa asili ili aburudike maisha yake
yote. Mwanaume mwenye akili anamtunza mke tangu ujana mpaka uzee anafaidi kile
alichokitunza kwa akili yake sio ya kujrazimishwa na umri.
3) Kukimbia familia. Kuna mzee mmoja alikuwa akiishi kisiwa kidogo cha Ukara, mzee huyu
alimfumania mke wake akizini na mwanamme mwingine chumbani kwake. Alipoamua
kumuacha mahakama ikaamulu wagawane mali, na kwa kuwa mke alikuwa na Watoto
wawili wadogo waliokuwa hawajafikisha miaka mitano ikabidi mke apewe duka na
nyumba waliyokuwa wakiishi. Mwanaume akaambiwa amalizie nyumba waliyokuwa
wameanza kuijenga huko lyamungo kati ndiyo iwe yake. Mzee huyu akauza nyumba na
kukimbilia Ukara. Huku akanunua mkokoteni na kiwanja kisha akajenga, kadili siku
zilivyozidi kwenda maisha yalizidi kuwa magumu kwake. Miaka mitano kila gurudumu la
mkomkoteni likipata pancha anakaa chini ya mti na kuanza kulia akimlaumu Mankia
wake kuwa yote haya umesababisha wewe nilikuwa na duka na nyumba. Anahitimisha
kwa kusema lakini sirudi ng’o huko nimekuachia kumbukumbu ya Watoto hao
inatosha!!.
Ndo sio kolomeo kila mtu analo kwa ajili ya kumezea matonge. Ndoa ni zawadi ya wanaume na
wanawake jasiri. Wenye uwezo wa kupambanua mambo na mbingu zikajibu, wenye uwezo wa
kumwambia shetani toka ndani ya nyumba yangu bila kupepesa macho na shetani akatii mala
moja. Wengi wanoa kwa kugopa umri usiwatupe mkono matokeo yake anakuja kufanya
majaribio na mwisho kushindwa mapema.

La kujiuliza ni pale mtu anashindwa kumwongoza mke mmoja anataka kuongeza mwingine.
Unashindwakumwambia Mungu huyu ni wangu kwa nini unaruhusu waasherati wamguse
huyu unakimbia nji na natokeo yake mika nenda rudi unalia usiku na mchana bila majibu na
kuipa nafasi dunia iseme

Mtazamo
Unapomtazama binadamu yeyote kwa jicho la huruma na kwa umakini wa hali ya juu kutokana
na matendo yake lazima utaambulia mambo mawili kati ya haya, Kutenda dhambi au kupata
thawabu. Kuna mzee mmoja aliwahi kuniambia nikikutazama kijana awangu naona kabisa
utafikia umri wangu (miaka 70). Nikamuuliza kwa nini umesema hivyo? Akanijibu we ni kati ya
vijana wanaotunza afya zao niliwahi kuwaona katika maisha yangu.

“Akaongeza kwa kusema wewe sio mzurulaji, hauna mambo ya wanawake lakini pia unafanya
sana kazi za mikono hivyo unafanaya mazoezi ya kutosha”. Nilipoachana nae nilikaa sehemu
nikatamani kulia!!!, kwa kuwa wiki moja nyuma nilikuwa nimezini. Moyo wa mtu ni kichaka
ukimtazama nje unaweza toa mtazamo wako kadri unavyojua na kadili unavyojisikia. Mzee huyu
alinijua kiukweli lakini jambo moja hakunijua vizuri.
Tendo moja linaweza punguza zaidi ya miaka 60 aliyoisema mzee wangu huyu. Lakini pia kuna
rafiki yangu mmoja aliniambia “unaweza fanya jambo lolote kadili unavyojiskia na ukafikia
maamuzi yoyote. Lakini kumbuka kuzingitia ushauri wa watu kwa kuwa wanaokusahauri hawana
la kupoteza kutoka kwako. Wengi wao wanakutakia mema kwa kuwa ata ukifeli sanasana wewe
utakuwa mzigo wao”.

Mtazamo wa jamii kwa vijana sio mzuri. Wazee wengi wanaamini vijana wa siku hizi
wamepotoka na hawana maadili. Kinyume chake vijana hawana muda wa kuzungumzia mazuri
yaliyofanywa na wazee wao ata kama yako wazi. Lakini hiyo inatokana na ata wazee wenyewe
kutokuwa tayari kukubaliana na hali halisi ya maisha na nini vijana wanafanya.

Kuna kijana mmoja anaheshima na anaheshimika na kila rika mtaani, lakini tabia zake sio nzuri
kwa kuwa ni msiri sana. Kijana mzinzi, mchonganishi na muongo wa kupindukia, lakini machoni
kwa watu wazima ni mfano wa kuigwa. Ata kuna waume wana mali na kila kitu ndani wakitoka
majumbani mwao wanaheshimika na niwachangiaji wazuri katika kazi za kijamii. Lakini ni mwiba
kwa wake zao na sio mfano mzuri wa kuigwa na jamii.

Usinilize tena mpenzi!!


Alisikika msichana akimwambia mpenzi wake kando ya dirisha baada ya kutuhumiwa
anatembea nje ya ndoa, “unanijua vizuri mpenzi kwa kuwa kabla ya kuoana tulikuwa marafiki
kwa zaidi ya miaka mitatu”. Tuhuma ya kusingiziwa huwa inauma sana, hasa wasichana
wanaumia sana wanaposingiziwa kutenda jambo wasilolitenda.

Kwa zaidi ya miaka mitatu Joe na Mankia walikuwa marafiki wa karibu. Mankia hakuwa na
mpenzi, zaidi alikuwa na marafiki wa kiume ambao Joe aliwajua na baadhi walikuwa ni marafiki
zake pia. Joe hakuwahi kumfahamu mpenzi wa mankia na hakuwahi kusikia tuhuma kwa
marafiki zake mankia kuwa aliwahi kuwa na mahusiano na mvulana Fulani.

Sasa ndoa yao ina miaka mitano, Joe anapandisha hasira kwa kumtuhumu Mankia anatembea
na mfanya biashara wa vitunguu hapo mjini iringa. Imetokana na simu iliyopigwa kwa Joe na
kuulizwa kama anajua mke wake amechukua fedha bila kurejesha na simu imekata harafu mtu
huyo hajapatikana tena.

Joe anaoorodhesha makosa, Kosa la kwanza ni kwa nini amekopa fedha bila kumtaarifu, na kwa
nini simu ipigwe kwa Joe tena kwa ukali?. Kinachomuuma mankia kutuhumiwa anatembea na
huyo mfanyabiashara wakati yeye anajua sio kweli na hajawahi kuisaliti ndoa yake. Mankia
anamwambia Joe usinilize mpenzi, ulinikuta nikiwa na usichana wangu nikiwa na miaka 26,
kama niliweza kujitunza kipindi chote hicho sembuse hii miaka mitano?.
Kulia sio suruhisho na sababu zote hizo zinaonyesha kugonga ukuta kwa kuwa Joe hampati
hewani mfanya biashara huyo ili kuthibitisha ukweli wa mambo. Hatmaye baada ya nyumba
kuwa katika taharuki na magomvi ya takribani masaa matatu, mfanyabiashara anapiga simu kwa
Joe na kumwambia “samahani shemeji, nilikuwa na hasira kwa kuwa mke wangu kanitibua,
lakini kuna mzigo mke wako alinikopa ili aendeleze duka lake kiasi cha shilingi laki moja
tulipokutana duka la jumla alikuwa amepungukiwa, kumbe alikuwa keshamlipa mke wangu nae
ameitumia bila kuniambi, samahani sana”
Mankia kwa hasira, hataki tena kusikia kinachoendelea kwa kuwa ametuhumiwa kutembea na
huyo mfanya biashara. Anakumbuka katika maisha yake amewahi kutuhumiwa anatembea na
bosi Fulani huko Ngorongoro hali iliyompelekea kushindwa kumaliza masomo yake kwa vitendo
kwa kuwa shangazi yake alimfukuza kwa kumfokea sana. Katika kichwa cha mankia tuhuma ina
madhara sana kuliko faida. Kwa kuwa tuhuma ya ngorongoro imemtenganisha na shangazi yake
ambae mpaka leo hawana mahusiano mazuri, na aliyewagombanisha ni Ruth rafiki wa karibu wa
mankia ambaye mpaka leo nae urafiki ulikwisha tangu siku hiyo.

Kauli ya mwisho ya mankia “usinilize tena mpenzi” nilijitunza ili niwe na ndoa itakayoniheshimu
na kuwa mfano wa kuigwa, sina ninachokosa kwako. Vijana wengi hukurupuka katika kutatua
matatizo ya ndoa zao, Ndio maana Biblia ikamwambia mwanaume aishi kwa akili na mke wake,
kauli ya kijinga isiyotoka katika akili huchachusha ndoa moja kwa moja.

Nafuu ya mwanaume akisingiziwa na mke wake hutumia mikono, mateke, vichwa na wakati
mwingine meno kupunguza hasira zake. Lakini mwanamke hodari hutumia machozi kujifariji na
sio kutumia ulimi kujitetea. Kimya ni fimbo, hekima ni ngao, atakayemzidi hekima mwenzake
katika ndoa huyo ndo kichwa cha familia.

Namkumbuka mzee Mchafu Mungu amlaze mahari pema poponi “Amina” aliniambia…
wanaojitambua peke yao ndio wanatakiwa kuwa na wake wanaowastahili. Kujitambua ni neno
pana sana kama hujitambui unaweza kuvaa nguo isiyokutosha ukajifariji inakutosha, unaweza
kuvaa suruali bila kuzingatia mipaka ya kiuno na ukaacha makata mavi nje ukafikili unaenda na
wakati. Vijana wengi akili zao zimekuwa zimekuwa upana wa tawi na zinawabana kama nguo
zao. Ndio maana haishangazi kuona kijana akiwatukana wazazi wake au watu wazima
waliomzidi akili na jamii isichukue hatua yoyote.
Wangapi ndoa zao haziwapwayi?. Na ni watu wangapi sahihi wanaweza kutatua migogoro ya
ndoa?. Tatizo lipo pande zote mbili, jamii imekosa watu wenye busara na wanandoa wenye
busara pia hawapo. Ndio maana hakuna mahali pa wanandoa kukimbilia ili kupata mafunzo na
kushusha pumzi zao. Kanisa linajukumu kubwa kujenga watumishi wenye uwezo na kuaminika
na jamii katika kutatua matatizo ya ndoa.
Unataka kusikia ata usichostahili?
Katika maisha binadamu angependa kusikia mambo mazuri tu yanayomuhusu ata kama
hayamjengi. Mfano siku moja nilikuwa napita nyumba ya mchungaji wangu nikakutana na
Watoto wa mchungaji wawili wa kike. Kabla ya kusalimiana mkubwa akaniambia “kaka leo
nimekuota” . kabla hajasema ameniota nini mdogo akadakia “ amekuota eti umeiba fedha za
watu” nikajiskia vibaya sana.

Mkubwa akasema “hamna anakudanganya, nimeota utakuwa tajiri sana katika maisha yako,
nikashusha pumzi na kujisikia furaha sana na kumpenda yule mkubwa kuliko mdogo. Binadamu
hatupendi kusikia habari mbaya kutuhusu, hii inatokana na uoga wa maisha na kukwepa
chanagamoto za maisha, hali inayotupelekea kukumbwa na Changamoto tukiwa hatujajiandaa
nazo.

Ata rafiki zangu niliowahi kuishi nao mala nyingi walipenda kuambiwa mema tu, mfano atataka
kuambiwa umependeza ata kama sio kweli. Ni bora ukae kimya kwa lile unaloliona haliendi
sawa kuliko kumkosoa. Nadhani katika hili ndio jambo gumu sana kuishi na binadamu kuliko
jambo lolote katika maisha yangu nililokutana nalo.

Binadamu na kusifiwa ni kama samaki na maji, kukosolewa ni kama petrol na moto. Ukitaka
kupendwa na kila mtu uwe na jicho la kuona mema tu. Lakini mtu hajengwi kwa kuonyeshwa
alichopatia pekee, katika mazingira tunayoyaishi tunawatu na viumbe tunaoishi nao mfano ni
wanyama na ndege wanaotuzunguka. Ni rahisi kumfundisha ngombe asikupige mateke wakati
wa kumkamua kuliko kumfundisha binadamu kulala na chandarua ili asing’atwe na mbu.

binadamu ukimwambia jifunike chandarua anahisi ndio umemwambia chandarua hakina maana
na umuhimu wowote. Hiyo yote inatokana na binadamu hapendi kuonekana hatimizi wajibu
wake. Lakini pia ni rahisi kumfundisha kuku asitawanye chakula anapokula kuliko kumfundisha
binadamu asizurule kama hana jambo la msingi katika kuzurula kwake, Binadamu ana kasumba
ya kutoitikia kile anachofundishwa.

Kuna mzee mmoja alimwambia kijana wake “katika maisha ogopa mambo makuu matatu, wake
za watu, udokozi na tamaa. Udokozi na tamaa alivishinda lakini wake za watu hakufanikiwa
kushinda usia wa baba. Alipoulizwa kwa nini hufuati usia wa baba yako? Alijibu nadhani ata
baba aliweza kushinda tama na udokozi lakini wake za watu alishindwa pia.Jibu rahisi watu
wangependa kufundishwa na kuambiwa jambo na mtu ambaye anamaanisha kuwa mfano wa
kile anachoambiwa na muhusika. Watu wengi tumekuwa wakosoaji lakini sisi wenyewe
hatupendi kokosolewa, hatupendi ukweli, hatutendi tunayoyasema, hatuishi kile
tunachokizungumza na kukihubiri.
Mfano kama mchungaji sio mwaminifui wa ndoa yake anawezaje kuimbia jamii uzinzi ni dhambi
na jamii ikamwelewa?. Mwalimu anawezaje kumwambia mwanafunzi history ni nyepesi wakati
vyeti vyake vinaonyesha alifeli?, mzazi anawezaje kumwambia mtoto wake kumpiga mke ni kosa
wakati kila siku anampiga mama wa Watoto wake. Serikali inawezaje kuiambia jamii rushwa ni
hatari kwa maendeleo ya jamii wakati tasisi zake ndio zinaongoza kwa takwimu katika kupokea
na kutoa rushwa?.
Lakini wote hao wangependa kuambiwa wanachokipenda kukisikia, baba angependa kuambiwa
unampenda sana mkeo na majirani zake ata kama sio kweli. Mwalimu angependa kuambiwa
unajua kufundisha na haimaanishi kufeli ndio kushindwa kufundisha somo husika, lkini pia
serikali ingependa kusoma katika vyombo vya habari ikisifiwa kuwa inapambana na rushwa kwa
asilimia 100%. Na mchungaji angeapenda kuambiwa bila nyie wachungaji ndoa za watu
zingekuwa hatarini, lakini sasa zipo salama kwa kuwa mpo katikati ya jamii.

Tunapenda kuambiwa tusichostahili, ndio maana ata maendeleo yetu hayaji kwa muda muafaka
kwa kuwa tunakosa watu wa kutushauri katika kweli. Sehemu nyingi watu hujisifu kwa
kutokuwa na marafiki, kuogopwa na wakati mwingine kusikilizwa wao tu bila kupokea ushauri
wa watu wengine. Hali hiyo inatufanya kudumaa kifikra na kimtazamo, nchi nyingi za kiafrika
hazina maendeleo ya kweli kwa kuwa viongozi wanadhani wanajua kila kitu kinachohaitajika na
jamii.
Tumeona miradi mingi inayozinduliwa na serikali haidumu kwa kuwa jamii haikuhitaji, makanisa
nayo miradi inakufa kwa kuwa hawaamini katika kushirikisha waumini wao wakati waumini ndio
wanatoa michango kufanikisha shughuri za kanisa. Mijadara imekuwa ikitekwa na watu
wachache wanaotaka kusifiwa kuwa wao ndio waasisi na waanzirishi wa hayo mambo.

Lakini wanaokwamisha mambo mengi katika jamii ndio wameshika bendera kupokea sifa kuwa
bila wao jamii isingefika hapo ilipo, sifa za kijinga zinaliingiza taifa na kanisa shimoni. Hakuna wa
kusema ukweli akawa salama, hakuna wakujitoa akahesabiwa ana nia njema na kanisa. Baadhi
ya mambo yanafanywa kwa gharama kubwa wakati yangefanywa na waumini kwa gharama
ndogo sana.
Tunasubiri kuambiwa nakupenda mpenzi, bila wewe sipati usingizi, serikali inasubiri kuambiwa
wanaokufa mahospitalini wamepungua sana wakati watu wanafia majumbani mwao kwa
kutokuwa na imani na vituo vya afya. Kanisa linasubiri kuambiwa waumini wako ni wasafi kuliko
dini Fulani, huku dhambi zote zinafanywa ndani ya kanisa kuanzia muunini mpaka askofu
anashiriki kulinajisi kanisa. Nani ashiriki na kujitoa muhanga kutuambia tunayostahili,
yasiyotuhusu ayaweke kando waambiwe wanaostahili kuambiwa ukweli unaompendeza
Mungu?.
Barua ya kuagana na ukapera!!
Najua tumeshirikiana mambo mengi sana tangu tufahamiane, sijakuficha jambo ata moja
lililokuwa na manufaa katika mahusiano yetu mungu shahidi katika hilo. Kibaya ninachokihofia
mbele yangu ni wewe kukumbuka mabaya yangu pekee na kusahau wema ata mmoja
niliokutendea. Kama binadamu nilikosea na pia nilipatia pale nilipojiweza kukuridhisha, lakini
muda haurudi nyuma na matukio yanazidi kuongezeka ili kumkamilisha binadamu katika dunia.

Maana yangu ni kuwa punguza lawama mpenzi, ili upate japo sekunde moja ya kukumbuka
wema wangu ili unibariki Kupitia tabasamu lako ili walau nichote tone la Baraka zako katikati ya
bahari ya lawama juu yangu. Kuna kitu kinaitwa kupokezana vijiti, kila awamu huja na kuondoka
na awamu inapoondoka lazima itaacha maswali na majibu yasiyo na kikomo. Kupitia hayo ndio
maana vitabu vinawataja manabii kuanzia Mwanzo wa dunia mpaka leo lakini hakuna
aliyedumu mpaka leo.

Najua uhuru wa kupitiliza nakuzika leo lakini haimaanishi kuingia katika ndoa nakwenda kuwa
mfungwa wa maisha, bali nakuwa wakuhesabu hatua na kuzitafakali kwa kuwa muda si mrefu
nitakuwa baba. Nani angependa kuwa baba wa hovyo asiye na dira, mke asijisifu kuwa nina
mume bora na mwenye busara? Kama wapo mimi sio mmoja wao napenda familia yangu
ijivunie baba, mke wangu ajitambe kuwa nimepata mume.

Kazi iliyopo mbele yangu kubwa na inayohitaji ujasiri wa hali ya juu, ni kutafuta makazi ya
kudumu na kujipatia kipato cha kudumu ili nitulie sehemu moja. Ningetamani niwe zaidi ya hapa
lakini najua mungu ana makusudi na mimi kunifanya hivi nilivyo, kwa kuwa ata ninae ondoka
nae hapa siku ya leo ni mpango wa Mungu kwa kuwa kabla ya hapa nilikuwa na macho meengi
yaliyonifanya kila siku niingie katika migogoro.

Majukumu ni sehemu ya maisha, lakini nitayamudu kama mke wangu hatakuwa na lawama
kutokana na yale nitakayokuwa nayatenda wakati huo. Mshauri wangu namba moja nitapenda
awe Mungu wangu niliyemwamini tangu nikiwa tumboni mwa mama yangu. Washauri wengine
wafuate, biblia kiwe ndio katiba ya familia yangu, na hii itawezekana kwa kuwa mke ninayemuoa
leo ni mcha Mungu na analijua neno.

Sihitaji kuonewa huruma ili nifikie malengo yangu yaliyopo mbele yangu, jambo la msingi
napaswa kujulikana kuwa mimi ni binadamu wa kawaida, niliyekuwa kapera wa jana na baba wa
leo na kesho. Kama nilivyosamehe Kwa moyo wa dhati wale walionitendea uovu nami natangaza
kuomba msamaha kwa niliowadanganya na pengine kupita katika maisha yao bila kuwaambia
nini malengo halisi juu yao.
Wakati nakua, nakumbuka rafiki yangu kapera alikuwa akinipa ushauri wakujiamini kuwa kuoa
kunahitaji umaki, Upande wa pili kauli hii imnamaanisha ukiwa kapera ata usipokuwa makini
unaweza kuishi bila shaka na maisha yakaenda sawa sawia. Tena wakati mwingine alinishauri
kuwa mke mmoja anaeweza kuwa nae ni njia tu binadamu hawezi, ukiitafakari vizuri hii kauli
utagundua rafiki yangu kapera anaamini njiwa ana akili kuliko yeye.

Nampenda sana rafiki yangu kapera ingawa sioni haja ya kuendelea kumkumbuka baada ya
hapa kwa kuwa mala zote yeye si rafiki wa kudumu. Harafu hakui, na ukimwendekeza utakuja
kujuta kwa kuwa yeye anaweza kukupa ushauri wakati huo anashikilia moyo wako juu ya
walimbwende wanaopita mbele yako. Furaha yake ni mimi na wewe tuendelee kuwa na maisha
ya kujificha ficha kama magaidi.

You might also like