You are on page 1of 15

TANZANIA NA UCHUMI ENDELEVU

17/02/2019

Tanzania ni moja ya mataifa yanayoendelea kimkakati na kimipango katika nyanja

mbalimbali za kimaendeleo na utekelezaji ikiwa na azma ya kukuza uchumi na kupunguza

umasikini kwa mwananchi mmoja mmoja na kwa jamii na taifa kiujumla. Kuanzia miaka ya

mwanzoni mwa karne hii ya 21, jitihada za dhati zilipangwa na kuanza kufanyika kama vile

kuimarisha ubora wa maisha na ustawi wa jamii kwa kuanzisha mpango wa maendeleo wa

elimu ya sekondari (MMES), mpango wa maendeleo wa elimu ya msingi (MMEM),

kuimarisha utawala bora na uwajibikaji hasa likihusika na mapambano dhidi ya rushwa.

Katika harakati na jitihada hizo za kimaendeleo, yapo mabadiliko ya sera za kijumla na

mipango ya kitaifa iliyojitokeza katika kipindi cha utekelezaji wa sera hizi. Kutokana na Dira

ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Muda mrefu 2011/12

hadi 2024/25, Serikali ililenga kujenga jamii iliyoelimika na yenye kupenda kujielimisha.

Pamoja na azma hiyo, Tanzania iliridhia Itifaki ya SADC (1997) kuhusu elimu na mafunzo

iliyozitaka nchi wanachama kuwa na elimu msingi ya lazima kwa kipindi kisichopungua

miaka tisa (9); Itifaki ya Dakar (2000) kuhusu Elimu kwa wote; Makubaliano ya Perth

UNESCO (2007) kuhusu Elimu ya Sayansi na Teknolojia na mafunzo ya ufundi.

Kwa mujibu wa itifaki ya makubaliano ya Dakar, mwaka 2000 (WEF 2000), yaliwekwa

malengo kadhaa kwa wanachana wake na moja ya malengo hayo ni utoaji wa elimu bure na

ya lazima kwa wote. Pia, kulingana na malengo ya millennia yaliyopangwa na nchi

wanachama wa umoja wa mataifa mwaka 2000 kule Marekani; elimu ni moja ya vipaumbele

vya malengo hayo. Na hapa ninaainisha malengo matatu tu likiwamo hili la elimu ambayo

ndio msingi wa ujumbe wangu; kuondoa umaskini na njaa, kufikia Elimu ya msingi kwa

1
wote, kuhakikisha mazingira endelevu kwa wananchi wake ili kuwajengea uwezo wa kufanya

kazi za uzalishaji na kujiongezea kipato ili kukuza uchumi.

Katika hili, nchi wanachama zilitakiwa kutoa taarifa kwa Umoja wa Mataifa, na Tanzania ni

miongoni mwa nchi wanachama walioendelea kutoa taarifa na hiyo ilianza mwaka 2001 na

kuendelea; taarifa ikieleza hatua zilizochukukuliwa au zinazochukuliwa kuhusiana na

malengo husika na kiwango kilichofikiwa cha maendeleo kuhusiana na malengo hayo.

Baada ya miaka 15, Taifa la Tanzania lilipitia nusu awamu na awamu moja ya utawala wa

maraisi wawili na kufikia mafanikio makubwa kama vile kuimarika kwa mahusiano

(kidiplomasia) na mataifa mengine hasa katika awamu ya nne. Hili lilienda sambamba na

changamoto mbali mbali katika jitihada za kukuza na kuendelea kiuchumi kwa njia ya

kumwezesha mwananchi kuinua kipato chake. Changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa

nishati ya umeme ya uhakika hasa kwa maeneo ya vijijini na pia kuzidiwa nguvu katika

mapambano dhidi ya ufisadi na usimamizi mbovu wa rasilimali za taifa.

Wakati huo (2015) Tanzania iliingia katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa Raisi, Wabunge

na Madiwani uchaguzi ambao ulifuata baada ya chaguzi za serikali za mitaa na kufanikisha

kuingia madarakani utawala mpya wa serikali ya awamu ya tano. Utawala ambao uliingia na

kauli mbiu ya “Hapa kazi tu.” Hasa ikilenga kutekeleza ilani ya chama tawala huku Raisi,

ndugu John Pombe Magufuli akiongoza jitihada za kutaka kurudisha heshima ya chama na

kuweka sawa mwelekeo wa nchi katika kujijenga kiuchumi. Hiyo ilionekana kuzaa matunda

mara baada ya muda mfupi kuonekana kuimarika nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma,

kuimarika kwa utawala bora na uwajibikaji na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika

mapambano dhidi ya rushwa na ufisaji.

Mafanikio ya mapambano na kutokomeza rushwa katika taifa yamedhihirika na kushuhudiwa

na mataifa makubwa baada ya ripoti iliyotolewa hivi karibuni katika kikao cha viongozi wa

2
nchi wanachama wa mataifa ya Afrika kilichofanyika mwezi huu wa februari 2019 huko

Addis Ababa, Ethiopia. huku Waziri mkuu, ndugu Kasim Majaliwa akimwakilisha Raisi.

Katika taarifa hiyo, Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa mataifa machache ambayo

takwimu zinaonyesha kuwa imefanikiwa zaidi katika mapambano dhidi ya rushwa.

Katika utekelezaji na uboreshaji wa huduma kwa wananchi, kulikuwa na moja ya ahadi ya

chama (kulingana na ilani yake) kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015

ambayo ni kuleta elimu bila malipo ili huduma hii ya utoaji elimu iwafikie watanzania wote

wa matabaka yote ya kiuchumi.

Utekelezaji wa ilani ya chama mwaka 2015 kuhusu sera hii ya elimu bure ulianza mapema

mwanzoni mwa mwaka 2016. Katika kufanikisha hilo, msisitizo na usimamizi makini

ulionekana katika kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza

wanaendelea na masomo hayo sambamba na uandikishaji wa watoto darasa la kwanza kwa

wale waliokuwa wameshafikisha umri wa kuanza shule. Hatua hiyo iliyoambatana na uhaba

wa vyumba vya madarasa na madawati ambao pia jitihada zimefanyika na zinaendelea ili

kuhakikisha watoto wanahudhuria shule na kupata haki yao ya msingi ya elimu bila malipo.

Kwa hatua hiyo, hapo kama taifa limefanikiwa kwa serikali kuonyesha jitihada hizo za

utekelezaji wa ahadi hiyo na kumjali mwananchi hasa wa tabaka la chini ili kumjengea

mazingira na vigezo vya kumtoa katika wimbi la ujinga na umasikini wa kipato na ikiwa na

dhamiri njema ya kulitoa hapa taifa lilipo na kulipeleka katika uchumi wa kati na wa

viwanda. Pia hii ni kwa mujibu wa makusudi ya serikali (dira ya taifa) ya kuleta mapinduzi

ya kiuchumi ili kuibadili Tazania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025.

Fursa ya elimu bila malipo (kwa usawa) imeendelea kutolewa kwa watoto wote kujiunga na

shule na kupatiwa malezi kimwili, kiakili, kimaadili na kiroho kwa shule ya msingi na mpaka

3
kidato cha nne tangu mwaka 2016 na sasa huu ni mwaka wa nne toka kuanza kutekelezwa

kwa sera ya elimu bila malipo.

Kwa upande mwingine, watahiniwa-watarajiwa hao walioanza kufaidi utekelezaji wa sera ya

elimu bure sasa wameshafika kidato cha nne mwaka huu (2019). Mazinigira na takwimu

(kwa baadhi ya maeneo) zinaonyesha kuwa kundi hili ni kubwa sana ikilinganishwa na miaka

mingine iliyopita, huku ikionyesha idadi ndogo kabisa ya walioacha masomo (drop out)

ambayo pia ni mafanikio katika kudhibiti watoto kukatisha masomo (katika awamu hii ya

tano) kutokana na sababu mbali mbali kama vile mimba, ndoa, ajira za watoto n:k. Hivyo

kuna uwezekano wa kuanza kuwa na ongezeko kubwa la ghafla la wahitimu wa kidato cha

nne mwaka huu (2019) kuliko miaka iliyopita. Hayo pia ni mafanikio kwa sababu tumeanza

kupatia ufumbuzi changamoto ya mfumo wa elimu na mafunzo ambao hapo nyuma ulikuwa

ukitawaliwa na muundo wa kitaaluma wenye dhana ya kuchuja wahitimu na kupata

wachache wenye uwezo mkubwa katika taaluma.

Kwa mujibu wa matokeo ya mitihani mwaka 2017/2018 na 2018/2019 ni rahisi matokeo

hayo kuakisi aina ya matokeo yajayo ya 2019/2020 na kutupa picha ya jinsi ambavyo

tunapaswa kujiandaa kupokea idadi kubwa ya (wananchi watakaoingia mitaani) walioshinda

au kushindwa kabisa. Na hapo ndipo panahitaji uvumilivu, umakini na usikivu wa hali ya juu

katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya kijamii na kitaifa katika sekta nyeti kama hii ya

elimu. Kwa sababu swala hili halitakiwi kuwekwa katika mkondo wa kisiasa wala ushawishi

wa amri inayoelekezwa kwa watendaji na watumishi wa chini ili wafanikishe kuboresha

matokeo hayo yajayo. Bali ni swala linalogusa gharama kwa pande zote mbili; serikali na

nguvu kazi iliyopo. Endapo jukumu litaachiwa upande mmoja tu litafutie ufumbuzi,

hakutakuwa na matokeo chanya. Na itakuwa ni jambo la kushangaza hapo mwakani endapo

tutaanza kuunda tume ili kuchunguza chanzo na sababu baada ya matokeo hayo yajayo ya

kidato cha nne 2019/2020.

4
Kwa upande mwingine, watanzania tuna utamaduni wa kusubiri tukio litokee ndio

tunachukua hatua kulitatua, ingawa mazingira na hali ilianza kuonekana hapo kabla. Kwa

mfano idadi ya madarasa kwa kidato cha tano na sita na madawati inaweza kutokidhi hitaji

kwa sababu ya wingi wa wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga kidato cha tano. Sasa upo

uwezekano kwamba tukaanza kuamshana na kukimbizana ili kuwashughulikia watoto hao

(wenye sifa) wasikose masomo ya kidato cha tano kuanzia mwezi wa saba, 2020. Lakini hilo

ni angalizo tu kutokana na mtazamo wangu ambao pia unaweza kukosolewa.

Sasa, ninarudi tena kwenye hoja yangu, kulingana na aina ya wanafunzi wanaopokelewa

(miaka hii) wa kidato cha kwanza kwa shule nyingi za kawaida za sekondari serikalini

unaotokana na mfumo (ule unaojulikana) wa kujibu maswali ya mitihani ya darasa la saba

kutoka shule ya msingi; Ni matarajio kwamba idadi ya wasiojiweza na wasio na sifa mitaani

itaongezeka ghafla kwa mwaka ujao 2019/2020, maana hao tunawajua na pia tunao huko

madarasani na tunawafundisha. Lakini je, hii ndio idadi kubwa ya watanzania

tunaowasafirisha katika chombo hiki cha elimu ili wafikie hatua ya kuwa nguvu kazi ya taifa

lililoelimika ili lipate maendeleo? … (hiyo ni changamoto pia).

Ijapokuwa haya (yawezekana) ni matokeo ya swala la vipaumbele. Kuamua kutilia mkazo wa

kujenga upande Fulani na kuacha upande mwingine au kufumbia macho changamoto zilizopo

eneo fulani au kuzitatua polepole pasipo kujali madhara na matokeo yake.

Lakini, tatizo kama hilo si la mtu fulani pekee, wala kiongozi fulani pekee, wala taasisi fulani

ya elimu pekee. Ni ugonjwa wa kitaifa unaomhusa kila mtanzania wa kiwango cha chini, kati

na juu kiuchumi. Lakini kwa kuwa sio katika kila changamoto ya taifa itahitaji wananchi

wote wahusike moja kwa moja katika kutatua changamoto hizo ila tunao wawakilishi (wenye

sifa) pia wenye mamlaka ya maamuzi (pasipo siasa) na utekelezaji wa moja kwa moja

unahitajika. Ikumbukwe kuwa “Elimu ni uwekezaji mkubwa, na ili kupunguza tatizo lijalo

5
(kuepusha aibu) ni muhimu kukumbuka kuwa uwekezaji mkubwa zaidi kifedha na rasilimali

watu (nguvu kazi hasa sayansi) unahitajika, hapo.“ Ni kushughulika na maeneo yote

yanayogusa kitu kinachoitwa ‘fedha.‘

Ni ukweli usiopingika kwamba taifa lina mzigo mkubwa wa majukumu yanayohitaji fedha

hasa katika kutekeleza miradi mbalimbali na mikubwa inayoendelea na ijayo - hapo tunaunga

mkono. Lakini ni swala la kipaumbele pia. Eneo la elimu ya msingi na sekondari sio la

kugusa juu juu. Siku zote, misingi ikiharibika, tujue kwamba huko juu na huko mbeleni

tunaenda kuvuna uharibifu. Uwezekano ni mkubwa wa kuwamwaga mitaani hao wahitimu

wote (walioshindwa) na wakakosa mwelekeo kwa sababu hatujaandaa mazingira (kama taifa

na sio wazazi na walezi pekee) ya kuwafanya wawe na faida kwa jamii, ni sawa na kuzalisha

kwa makusudi kitu au kifaa hatari usichokijua na kukiacha au kukitupa na baadae bila kujua

kinakuja kukudhuru mwenyewe.

Endapo kutakuwa na ongezeko kubwa la walioshidwa kidato cha nne, pasipo kuwepo

mikakati mahususi ya jinsi ya kuwaboresha katika ujuzi na maarifa yanayoendana na uhitaji

wa kiuchumi wa dunia ya sasa, hapo tunaandaa taifa lenye watu wasiozalisha na waharibifu

(vibaka, madawa ya kulevya, wezi, waporaji na majangiri). Taifa lenye watu wengi

waliosoma na wenye ujuzi katika maeneo tofauti tofauti litaendelea haraka kuliko kuwa na

wazurulaji wengi, ambao ni ‘wacheza pooltable asubuhi, walewa viroba siku nzima, wapiga

debe wasio rasmi katika vituo vya mabasi masaa 24.’

Kama mtanzania-mzalendo, ninadiriki kuandika hivi kwa sababu mimi sio mwanasiasa, niko

upande wa utendaji zaidi na hapo haihitaji siasa endapo tunataka kuliweka taifa liendelee

kuwa salama. Ni hatari sana endapo taifa halitachukua hatua zenye tija katika kuzuia

ongezeko la watu wasiozalisha kitu katika jamii. Kwa sababu mtoto anatakiwa angalau kwa

jitihada zote zilizowekwa (kwa miaka minne shuleni) basi apate alama ambazo itakuwa rahisi

6
kumuwezesha aidha kuendelea na masomo, kuendelea na masomo ya ufundi stadi au kujenga

mazingira ya mtoto huyo aondoke shulani akiwa na ujuzi katika eneo fulani ili akienda

mitaani basi ikawe rahisi kuwezeshwa. Na hilo ndilo eneo lililo nje ya mkondo wa taaluma

hasa kwa kuzingatia vipawa na karama walizonazo wanafunzi mashuleni. Ikumbukwe kuwa

moja ya mahitaji ya taifa ili liendelee linahitaji kuwa na rasilimali watu (nguvu kazi

iliyoelimika na yenye ujuzi wa kutosha).

Na hapa ndipo tunaelewa msisitizo wa kufanya kazi unaotolewa mara kadhaa na Raisi, ndugu

John pombe magufuli akisema “mimi nataka watu wafanye kazi.” Ikimaanisha kwamba

tukifanya kazi kwa bidii, hatutasubiri wakati wote misaada toka nje ili tufanye au tupate

maendeleo, hatutaomba chakula cha msaada toka nje, kama ni chakula basi tutazalisha kwa

wingi na kubakiwa na ziada (excess) ambacho kitatoka nje (kwa utaratibu sahihi) ili tupate

fedha za kigeni. Kwa mantiki hiyo, inatukumbusha kuwa rasilimali watu nyingine

inaandaliwa shuleni. Shuleni ndio mazingira yanayotakiwa kupika, kupakuwa na

kuwamwaga hao wataalamu katika maeneo husika. Lakini kama hawakuiva, basi wanatupwa

jalalani (mitaani), nao wanaanza kutafuta mazingira ya kula bila kufanya kazi. Tayari huo ni

mzigo tuliozalisha wenyewe.

Kwa mujibu wa sera ya Elimu na mafunzo (2014) inabaini jitihada na malengo ya sekta ya

elimu (ambayo mimi ninaita “JIKONI” kwa sababu ndio sekta mama katika kuzalisha, kulea

na kukuza rasilimali watu na kada zote zinatoka hapo). Hivyo sekta ya elimu na mafunzo,

kwa mujibu wa dira ya maendeleo ya taifa 2011/2012 hadi 2024/25, ilitarajiwa na inaendelea

kutarajiwa kuleta maendeleo ya haraka ya rasilimali watu kwa kutayarisha idadi ya kutosha

ya watanzania walioelimika na kupenda kujielimisha zaidi ili kulifanya taifa lipate maendeleo

na kuwa lenye uchumi wa kati na baadae iwezekane kuwa na uchumi wa juu.

7
Ninanukuu maelezo ya sera ya elimu, yanasema; ‘kumekuwa na changamoto katika kuinua

ubora wa elimu na mafunzo kutokana na mitaala katika ngazi mbalimbali za elimu na

mafunzo kutokidhi mahitaji ya mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na teknolojia na

hivyo kutoa wahitimu ambao hawana umahiri wa kutosha kuhimili ushindani katika

ulimwengu wa kazi.’

Moja ya mabadiliko katika upepo wa kimaendeleo katika jamii ni msisitizo katika sera ya

viwanda, ambao umetoa fursa kwa wananchi na wawekezaji (ndani na nje) kupatiwa maeneo

(ardhi) kwa masharti nafuu ili kuanzisha na kuendeleza viwanda. Sasa hali hii inaonyesha

umuhimu wa kuweka mabadiliko na mkazo (mitaala) katika utoaji wa elimu inayokidhi

mahitaji hayo ya sasa ili kuandaa taifa lenye mtazamo wa kiviwanda toka wakiwa shule ya

msingi na sekondari.

Na badiliko lingine katika jamii ni ongezeko kubwa la watu na uhaba wa ajira (ajira rasmi).

Kwa mfano walimu wa masomo ya sanaa mpaka sasa hawajaingia katika ajira ya serikali

toka mwaka 2015. Lakini vyuo vinaendelea kuzalisha idadi kubwa ya walimu hao wa sanaa

ambao wanaendelea kuingia mitaani na vyeti na taaluma zao wakitegemea ajira mpya

serikalini na sekta binafsi. Na wakati ajira hiyo imesimama, bado kumekuwa na ongezeko la

idadi ya wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza na pia shule ya msingi.

Hapo pia naweka angalizo. Uandaliwe mfumo wa kuwafanyia usahili walimu wanaohitaji

kuingia ajira ya serikali. Kwa sababu haiwezekani na haiingii akilini kuwa tuna idadi kubwa

sana ya walimu wahitimu wa vyuo vikuu na diploma mitaani lakini bado hakuna utaratibu

wenye manufaa wa kuwachuja ili kuwapata walimu bora na kuwapa ajira. Unajua, hatuhitaji

kuwa na bora walimu, ila walimu bora. Sasa hivi vyuo ni vingi na wengine wameenda

kusomea ualimu na kuingizwa kwenye ajira ya ualimu ili kutafuta riziki tu (watu wa

mshahara) lakini mwito na uwezo wa kumsaidia mtoto hasa kitaaluma hana.

8
Ushauri wangu kwa Serikali ni kuwa kila halmashauri iwe na kitengo hicho (ikiwezekana

watu wa HR na TSC); usahili ufanyike angalau mara mbili kwa mwaka kwa kila

halmashauri) na kuandaliwa database ya walimu wenye sifa (wanaohitaji ajira) baada ya

kufanyiwa usahili na kupeleka majina na taarifa zao TAMISEMI (hiyo inawezekana kama

kweli tunataka kuingia gharama ambayo inamanufaa kwa hatima njema ya elimu yetu. Hili

pia ni katika kuandaa mazingira yenye tija katika kuandaa taifa lijalo la uchumi wa viwanda.

Maana msingi mkuu ni kuimarisha utoaji wa elimu bora.

Na kama utatumia kigezo cha GPA tu ili kubaini mwalimu bora basi hapo ndio utapotea

kabisa. Ualimu sio GPA peke yake. Humu mitaani kuna waalimu ni darasa la saba wa

zamani, lakini wanauwezo wa kumsaidia mtoto wa darasa la kwanza kwa usahihi kuliko huyu

mwalimu mwenye degree ya kwanza ya ualimu (ijapokuwa tunawatambua hao wa mitaani

kuwa wanawaharibia msingi watoto kwa mfano kwenye kanuni kama za kufundisha

kingereza na hesabu). Lakini ni bora kumchukua huyu wa mitaani na kumpeleka chuo ili

akajue kanuni za ufundishaji na kumjengea uwezo na kumfanya awe mwalimu rasmi. (huo ni

mfano tu).

Kwa swala la kuwafanyia walimu usahili, changamoto inakuja katika kudhibiti rushwa na

undugu. Hapo pia inatakiwa kuwekwa mazingira magumu ya kuchukuana kindugu au kwa

rushwa. Lakini kama zitawekwa sheria kali, inawezekana kulitekeleza hilo (na kupunguza

sana kubebana katika ajira) kwa sababu hitaji letu ni kuona kuwa ualimu sio ‘dampo’ la

kupokea kila mtu aliyekosa kwa kwenda. Ualimu ni taaluma na lazima iheshimiwe, na

serikali iwe na uhakika kuwa imeajiri nguvu kazi yenye kutaka kuleta mabadiliko. Hata

ikiwapa motisha, iwe na uhakika kuwa hiyo motisha imeelekezwa katika mkondo wa watu

sahihi wanaostahili.

9
Zipo sababu nyingi za shule binafsi kufanya vizuri kuliko za serikali kwa sasa, lakini sababu

moja wapo ni kuwafanyia walimu usahili ili kubaini uwezo wao kabla ya kuwapa mkataba au

ajira. Kuna usahili wa kuhojiwa kwa mdomo, wa kuandika na pia usahili wa kuingia

darasani. Yote hayo yafanyike. Hujui kwamba kwa sasa unaweza kuajiri walimu ambao

hawajui kuandika barua ya kuomba kazi. (lakini ile aliyopeleka kuomba kazi aliandikiwa na

mtu mwingine).

Ikumbukwe kuwa elimu ndio nyenzo pekee ya kubadili mawazo, fikra na mitazamo ya watu

ili kuzalisha na kuharakisha matokeo chanya katika jamii na mazingira yanayomzunguka

mwanamchi huyu. Na njia pekee ni kupatiwa elimu kwa njia rasmi na isiyo rasmi ili

kupata/kupanua maarifa na ufahamu kutoka kwa wataalamu na wanataaluma

Sera yetu ya elimu inayotekelezwa sasa inabaini pia kuwa kuna idadi kubwa ya wataalamu

walioelimika kwa kiwango cha juu wanaohitajika ili Tanzania kufikia kiwango cha nchi

yenye uchumi wa kati huku taarifa zinaonyesha kwamba rasilimali watu ya Tanzania, kwa

kiasi kikubwa ni wafanyakazi wenye ujuzi wa chini ambao ni asilimia 84, wakifuatiwa na

wenye ujuzi wa kati asilimia 13 na wenye ujuzi wa juu asilimia 3. Hata hivyo, kwa nchi za

kipato cha kati ngazi ya chini, ulinganifu unaonyesha kuwa nchi hizo zina wastani wa

asilimia 55 ya wafanyakazi wenye ujuzi wa chini, asilimia 33 ujuzi wa kati na asilimia 12

ujuzi wa juu. Hivyo, Tanzania ina changamoto ya kuinua mchanganyiko wa wafanyakazi

wenye ujuzi katika fani mbalimbali ili kufikia mahitaji ya rasilimaliwatu kwa nchi ya kipato

cha kati kufikia mwaka 2025.

Sasa, ili kuweza kuyafikia malengo haya pasipo shida, ni muhimu kushughulika hasa kwa

kuanzia elimu ya msingi na sekondari (hapo ni swala la mitaala). Ijapokuwa watoto wa shule

ya msingi na sekondari, hawapatiwi (kulingana na mitaala) elimu ya kujitegemea inayoweza

kuwaandaa kwa ajili ya kuyakabili mazingira ya kazi yajayo hasa ikizingatiwa kuwa umri

10
wao pia ni mdogo lakini bado tunajukumu kubwa lisilokwepeka la kuanzia msingi na

sekondari kutoa elimu inayoweza kubadili mtazamo na fikra kuwa maisha ya shule

yanatuandaa kwa ajili ya kufanya kazi za uzalishaji mali kwa njia ya kujitegemea (ajira

binafsi). Mwanafunzi ajue kuwa anasoma hata kufikia (kidato cha nne au sita) ili aje

kufanikiwa kuwa fundi cherehani (kushona nguo) na kuwa na kiwanda kidogo cha kuajiri

wengine.

Kazi hata ya kushona viatu na ndala na kubrashi maeneo ya mjini/mitaani inafanywa na idadi

kubwa ya watu ambao hawakupata fursa ya kwenda shule au waliishia darasa la saba la

zamani kidogo. Inaonekana si kazi yenye kufaa kwa wasomi kwa sababu ni matokeo ya

elimu ya nadharia toka shuleni msingi.

Kama ilivyokuwa hapo nyuma, swala la kilimo (mkulima-kushinda kwenye matope),

haikuwa rahisi kufanywa na msomi wa chuo kikuu. Bali na wale waliokosa fursa ya elimu.

Na hata yule mtaalamu wa kilimo (wengine maafisa kilimo) wakijifungia ofisini ili kusubiri

wateja wawafuate, na kusubiri vikao ofisini na si kwenda kushida kwenye mapori, nyasi na

matope ili wakatoa elimu kwa wakulima namna ya kufanya kilimo chenye tija. Hiyo yote ni

mitazamo na fikra ambazo mtanzania ametoka nazo shule ya msingi.

Lakini ukweli ni kwamba kazi ndogo ndogo kama hiyo ikifanywa na msomi inaweza

kufanywa kwa umaridadi wa kiwango cha juu na kuleta mapinduzi katika sekta ndogo ndogo.

Ni kama vile kumchukua profea wa chuo kikuu aende kufundisha shule ya msingi kwa

watoto wanaotoa kamasi. Inakuwa ngumu kidogo (hata kama ataboreshewa mazingira ya

kazi) na kupatiwa mshahara na marupurupu yale yale anayoyapata kule chuoni. Inatakiwa

awe mzalendo. Ingawa tutasema kuwa kutokana na uhaba wa maprofesa chuo kikuu basi

11
awaachie hao walimu wa cheti, diploma na degree wafanye kazi ya kufundisha shule ya

msigni ambayo ni ya kwango chao. Kwa sababu itakuwa ni matumizi yasiyo sahihi ya

rasilimali watu.

Lakini pia mhandisi, akipewa ekari tano (kwa mfano) ili aziendeleze katika kuzalisha zao

fulani, uwezekano wa kumudu hiyo kazi na kuleta matokeo chanya ni mkubwa kwa sababu

tunategemea kuwa ana uwezo mkubwa wa kuelewa na kufuata maelekezo ya wataalamu wa

kilimo. Zaidi ya hayo anafursa ya kujisomea na kujua kanuni nyingi zaidi za kilimo na

kubadilika kulingana na mazingira na mahitaji katika kazi yake ya ukulima. Akienda kwenye

duka la pembejeo kunakuwa na uwezekano mdogo wa kuzulumiwa au kuuziwa viwatilifu

vilivyokwisha muda kwa sababu anauwezo wa kisomi (wa kubaini mambo) na kufanya tafiti

kwa wahusika kama TFDA na kujua ukweli wa bidhaa. Msomi ana ujasiri wa kufuatilia na

kuhoji ili kujua ukweli.

Sasa, elimu ya uchumi wa viwanda inatakiwa kuingizwa katika mfumo rasmi mashuleni ili

tufanikiwe katika harakati hizo na kubadili mtazamo na fikra kuanzia shule ya msingi na

sekondari-hapo siongelei elimu ya nadharia bali kujitegema. Uhamasishaji usiishie mitaani na

kwenye vyombo vya habari tu … hivyo kwa wakati huu, wengi wasiosoma ndio wanaelimu

ya kutosha na kwa kuwa walikuwa na msingi ambao haukuwezeshwa na sera ya taifa ya

viwanda hapo nyuma. Hii inamaanisha kuwa wakati ujao huyo mwenye vyerehani vitano vya

kushonea nguo ndio atakuja kuajiri hao waliokwenda shule na kuhitimu lakini wakakosa sifa,

kwa sababu hao walioshuleni sasa wanafikra kuwa watasoma ili waje kuajiriwa.

Wazo langu pia ni kufikiri namna ambavyo tunaweza kuunganisha elimu ya sekondari na

vyuo kama VETA au vyuo vilivyosajiliwa na VETA. Mazingira hayo yatumike kama sehemu

12
ya kufanya mazoezi kwa kazi ndogo za ujuzi hasa kwa watoto wa sekondari (natambua ni

gumu kutekelezeka.) lakini itambulike kuwa watoto wanauwezo mkubwa wa kushughulika na

vitendo kuliko nadharia endapo tu wataandaliwa mazingira na kujengewa uwezo. Hata kama

mtoto anashida kidogo ya akili lakini ukimpeleka kwenye maeneo ya kushika SPANNER,

uzoefu unaonyesha kuwa anaweza kuendana na mazingira hayo ya ufundi na polepole kupata

ujuzi na baadae kuimudu hiyo na kuifurahia kuliko kushinda kumlazimisha aelewe (kukariri)

sheria za Newton wakati ubonngo wake umegoma.

Hilo nina uhakika nalo (endapo utekelezaji wake ungekuwa rahisi). Hebu jaribu kumchukua

dereva aliyelewa (mlevi) mpaka kufikia kiwango cha kushikwa mikono kwa sababu hawezi

kutembea mwenyewe. Sasa mchukue (kumbeba) na kumuweka kwenye kiti cha gari yake ili

awashe injini na kuendesha. Atafanikiwa kufuata kanuni zote mpaka kuanza kuendesha gari

ingawa usalama utakuwa mdogo akiishaingia barabarani.

Lakini huyo huyo dereva jaribu kumpa maswali yanayohusu taaluma yake ya udereva na

ayajibu kwa kuandika, uhakika ni kuwa atashindwa kuyajibu. Kwa sababu hapo ameingia

kwenye nadharia na sio vitendo.

Hivyo katika kuandaa wanafunzi katika mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, kuna jukumu la

kuendelea kupeleka na kufikisha elimu ya kutosha kwa (jamii) wazazi. Mzazi/mlezi

anapaswa kuandaa mazingira ya kujua mtoto wake anapendelea kufanya nini (kazi gani)

katika maisha. Kwa sababu maono ya maisha yajayo pia hayaanzii ukubwani tu, pia utotoni

(kulingana na mazingira) Na hiyo itasaidia kubaini mwelekeo wa mtoto na pia kuanza

kutengeneza mazingira ya kumwendeleza huyo mtoto. Ijapokuwa sio watoto wote watakuwa

na wazo hilo lakini ni sehemu ya jukumu la wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuanza

13
mapema kutengeneza au kuandaa kipawa kwa mtoto wake. Na shuleni ndio mahali pa

kuviendeleza (mfumo rasmi) pia endapo mazingira yataruhusu (kimtaala na uwekezaji).

Mataifa yaliyoendelea yametushinda hapo, kumuandaa mtoto akiwa bado mdogo katika

kumtengenezea njia aje kuwa mtaalamu au fundi mwenye ujuzi utokanao na kipawa katika

eneo Fulani. Na hii ndio siri kubwa ya mafanikio yao katika sekta ya michezo. Kwa mfano

kumtengenezea bwawa la kuogelea na kumfundisha mtoto wa umri wa miaka 4 ili ajue

kuogelea. Au kumuandaa mtoto huyo awe mchezaji mpira wa miguu. Mtoto huyo akitimiza

umri wa miaka kumi (10) atakuwa tayari ni mchezaji mwenye kipaji ambacho kilianzia

utotoni pale nyumbani kwa wazazi au walezi. Wakati huku kwetu (mataifa mengi ya afrika),

mtoto wa miaka kumi ndio anaanza kuonekana kwa mbali akiwa shuleni kuwa anawezo wa

kuja kuwa mchezaji mpira mzuri. Na hapo wazazi hawajui na hawana taarifa yoyote juu ya

kipaji cha mtoto wao.

Sasa hapo ndio tunategemea kwamba taifa kama letu Tanzania tunaweza kushindana na timu

ya taifa ya wakubwa ya brazil au ujerumani. Wachezaji wetu hawa walioanza kutambulika

kuwa na kipaji cha kucheza mpira walipoanza kusoma shule, tena sekondari. Inakuwa ngumu

kidogo.

Ikumbukwe kwamba mzazi au mlezi anaouwezo wa kuamua kumuandalia mtoto wake awe

mwana sheria, mkandarasi, dereva, mcheza mpira, mwanariadha akiwa bado shule ya msingi.

Na hapo ndio chimbuko la kupata taifa lisilo teteleka katika nguvu kazi kwenye maeneo ya

uzalishaji. Hii ndio maana kama mzazi ni mwana siasa basi asilimia kubwa atakuwepo motto

wake mwanasiasa. Kama mzazi ni mjasiriamali basi atakuwepo mtoto wa kufuata nyayo hizo

14
za ujasiriamali. Kama mzazi ni mkulima basi hivyo hivyo atakuwepo mtoto mkulima katika

wale.

Changamoto kwa watanzanai na waafrika kiujumla ni kuwa hatuna utamaduni huo wa

kumuandaa mtoto katika mazingira ya kutambua (kuibua) vipawa alivyonavyo akiwa angali

katika umri mdogo. Pia hatuna utamaduni wa kujisomea mambo ya msingi (vitabu/hadithi ili

kupanua mawazo), ufukara wa kijamii, kukosa elimu na pia mazingira duni ambayo hayafai

kuandaa watoto wakiwa bado na umri mdogo pale nyumabni (katika jamii). Hayo yote ni

changamoto katika safari ya kuandaa taifa la uchumi wa kati.

Kwa mpango wa miaka mingi ijayo kwa mfano (kuanzia muongo mmoja hivi), mafanikio

katika kumuandalia mwanafunzi mazingira rafiki pale nyumbani (jamii) na shuleni (mitaala)

yatasaidia kuibua vipawa na kuviendeleza na hilo litarahisisha kupunguza idadi ya watoto

wanaokuja kuhitimu kidato cha nne wakiwa hawana mwelekeo wa kufanya kitu (kuzalisha

mali) hasa baada ya eneo la taaluma kushindikana.

Hapo sijagusia swala la kipingamizi cha sheria ya ajira kwa watoto chini ya umri wa miaka

kumi na nne (14), na wale wenye umri kati ya kumi na nne mpaka kumi na saba (14-17),

ambapo kundi hili (14-17), ndilo linabeba wahitimu wengi wa kidacho cha nne kwa sasa.

Ingawa (kwa mtazamo wangu) sheria ya kumbada mtoto wa umri huo (14-17), kufanya kazi

nyepesi unatoa fursa moja kwa moja kuingia katika ulimwengu wa kazi endapo ana ujuzi.

MUNGU LIBARIKI TAIFA LETU LA TANZANIA

0719194900 ////// 0738753217

15

You might also like