You are on page 1of 2

MALEZI KWA WATOTO WADOGO

Asilimia 80 ya watu wazima wanaishi aina ya maisha ambayo ni matokeo ya malezi waliyopata
utotoni kutoka kwa aidha wazazi/walezi wao au kutokana na mazingira ambayo yaliwazunguka
wakati wa utoto wao. Hii inamaana kuwa kila tukio na uangilizi waliopata wakiwa katika umri
mdogo limekuwa na ushawishi wa kutosha katika kuathiri maisha yao ya baadae wakati wa utu
uzima. Kwa mfano, mtoto anayefundishwa kufanya kazi za nyumbani hata akiwa bado anaumri
mdogo ataendelea kuwa na mazoea ya kufanya hivyo hata afakiapo hatua ya kupevuka kimwili
na kiakili na baadae kuwa mtu mzima.

Hebu jaribu kufikiri, kwa mfano mtoto wa kike ambaye amelelewa katika mazingira ya
kufanyiwa kila aina ya kazi pale nyumbani anapoishi, hata ile kazi ya kutoa vyombo mezani
mara baada ya kumaliza kula chakula... chukua kwamba asifanye kazi ya kuweka chakula
mezani, wala kutoa vyombo mara baada ya kula, wala kusafisha meza aliyoichafua baada ya
kula.

Ni dhahiri kwamba huyu mtoto wa kike ataendelea na tabia hiyo ambayo ilijengeka kwa
kulelewa katika mtindo huo wa maisha hata awapo na umri wa kwenda shule. Endapo atasoma
shule ya kutwa hivyo kurudi nyumbani na kukuta kila kitu kimeandaliwa na dada wa kazi za
nyumbani au mama yake kila siku, utamaduni huo ukaendelea hivyo mpaka kuhitimu sekondari
na baadae kujiunga na masomo ya elimu ya juu...

Fikiri, pia kwamba akahitimu masomo yake ya elimu ya juu, na pengine baada ya hapo akiwa na
umri wa miaka kama 25 akaingia katika majukumu ya ndoa (na kuwa mama wa familia); Je
ataweza kuwa mama mwenye uzoefu wa maswala ya kuendesha familia kama msaidizi wa baba
wa nyumba?...

Tunatambua kuwa mwanafunzi wa elimu ya juu hujiandaa kwa ajili ya kufanya kazi kulingana
na utaalamu na taaluma anayosomea kwa kwenda kwenye mazoezi (practicals/TP/field) akiwa
mwaka wa kwanza, wa pili pia hata na wa tatu kulingana na shahada anayosomea/anayoitafuta.
Hiyo inafanyika kwa jinsi hiyo ili kumuandaa awe bora kwa kuimudu kazi mara baada ya
kuhitimu masomo yake na kuingia katika uwanja wa ajira ili asiwe mgeni wa ile kazi aliyosomea
na hivyo kumudu ushindani wa uzalishaji mali hapo kazini.

… sasa basi, tukirejea tena kwa huyo mtoto wa kike, alisomea wapi kufanya kazi za nyumbani?
alifanyia wapi wazoezi ya kazi ndogo ndogo za nyumbani ili kujizoeza na kumudu majukumu ya
nyumbani ili awe mlezi bora na mwenye weledi afikiapo hatua ya umama?

Ni ukweli usiopingika kwamba huyu msichana aingiapo katika ndoa na kuitwa mama (mke),
ataendelea (kila siku) kuwa mnunua chips-mayai pale mtaa wa pili ili kuyafanya maisha kuwa
rahisi kama vile afanyavyo yule "bachela" ambaye naye ni mteja mzuri wa watengeneza chipsi-
mayai kwa sababu yuko bize na hawezi kutengeneza chakula kwa ajili yake mwenyewe.
Ijapokuwa akina baba wengi wanapokuja na kuingia katika ndoa huwa na mategemeo ya
kumpata mama mbunifu aliyefundishwa kwa usahihi katika kushika nafasi yake ya umama pale
nyumbani, lakini kwa hapo sasa, baba anakuja kukutana na shida…
Hivyo jukumu la huyu mama la kuwalea watoto wake atakaowapata pale nyumbani linaweza
kuwa gumu, na hata kuzalisha kizazi ambacho kitakuwa na mapungufu katika kupata malezi
sahihi kwa ajili ya hatima ya maisha yao ya baadae wawapo watu wazima.

Kwa mazingira yetu ya kitanzani na uafrika kwa ujumla, hali hiyo hiyo kwa watoto wakiume
inatokea pia. Endapo mtoto wa kiume hatapata fursa ya kufundishwa kuwajibika katika
majukumu madogo madogo angali bado katika umri mdogo, yawezekana akaendelea kuichukua
hiyo tabia na mwenendo huo hata awapo mtu mzima.

Matokeo ya kutowafundisha watoto wadogo kufanya kazi pale nyumbani yanaweza kuwa na
athari mbaya sana kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa hapo baadae. Ni rahisi sana hapo baadae
kupata nguvu kazi ya taifa isiyowajibika kwa kiwango cha kutosha kulingana na mahitaji katika
maeneo yao ya kazi kwa sababu ya malezi mabovu waliyopata utotoni wakiwa chini ya malezi
ya wazazi/walezi wao.

Moyo wa kufanya kazi kwa bidii na kwa kujitoa kwa ajili ya kutumikia wengine huwa
hausomewi... yaani, hatusomei kupata cheti/shahada ya bidii ya kufanya kazi ila tunasomea kuwa
na maarifa ya kutosha kufanya kazi. Swala la mtu kufanya kazi na kutimiza wajibu kwa ajili ya
manufaa yake na jamii kiujumla linaundwa toka katika malezi ya utotoni.

Msukumo wa mtendakazi kuwahudumia watu wengi kwa muda mfupi unatokana kwa kiwango
kikubwa na alivyoandaliwa kufanya kazi toka utotoni; unatokana na aina ya malezi ya kimwili
na kiroho na uaminifu ambao amefundishwa kuwa nao katika kutekeleza majukumu anayopewa
ili ayakamilishe kwa kipindi fulani.

Ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha kuwa mtoto yeyote awe wa kike/kiume anashirikishwa
kikamilifu katika majukumu mbalimbali ya mazingira ya nyumbani ili kumuandaa kuwa raia
mwema asiye mvivu; mzazi mtarajiwa atakayekuja kuwa mwenye kupenda kuitumikia familia
yake na jamii nzima na hivyo kutengeneza ustawi bora wa familia yake na jamii kiujumla.

"Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hawezi kuiacha hata awapo mtu mzima"

GEORGE M MYINGA

You might also like