You are on page 1of 1

MOH’D KHAMIS SONGORO (MFALME), VIKUNGUNI CHAKE CHAKE, PEMBA

TUZITUNZE FUNGA ZETU

1. Naona kama ni jana, bada’atu ramadhwani,


Na leo haipo tena, tungoje hadi mwakani,
Na ajuae rabana, ataefika ni nani,
Turidhiwe na karima, tuzitunze funga zetu.

2. La ya ‘arifu insana, kwamba atakufa lini,


Basi atende ya mana, ya wema na ihisani,
Amekhasarika sana, mharibu ramadhani,
Turdhiwe na karima, tuzitunze funga zetu.

3. Laisa lahu dhwamana, hata kwa chumwa amini,


Asietunza amana, hususa ya ramadhani,
Hutembea nayo lana, akhera na duniani,
Turidhiwe na karima, tuzitunze funga zetu.

4. Namuomba subuhana, atuzidishe Imani,


Na siku tukikutana, atuingize peponi,
Amina rabbi amina, tusamehe insani,
Tuzitunze funga zetu, turidhiwe na manani.

5. Ni machache niliyosema, kukumbusha ramadhani,


Sasa naomba karima, Ilahi mola manani,
Naiomba dua njema, ije kwenu waumini,
Awaridhie karima, kwa kufunga ramadhani.

6. Na piya ninayo dhima, kwa swahibu wa moyoni,


Kamuhitaji hashima, sasa yuko kaburini,
Mola mjaze neema, Khalidi awe nuruni,
Umridhiye karima, mithili ya ramadhani.

7. Mwisho beti nasimama, siendi tena usoni,


Songoro nakwama kwama, sijui utunzi nini,
Ila sijakata tama, iko siku nitawini,
Aniridhiye karima, kwa kufunga ramadhani

You might also like