You are on page 1of 5

Donald Trump: Raisi Mwenye Mbwembwe Nyingi na Jeuri ya Pesa!

Mwandishi Mtiga Abdalah


Mhariri Denis Mpagaze

Leo tutamzungumzia Rais Donald Trump wa Marekani na ukweli wa aliyenacho huongezewa


hata kama ni mkorofi kiasi gani na asiyenacho hupunguziwa hata awe mwema na mkarimu
kiasi gani, tunamzungumzia Rais Donald Trump wa Marekani na ukweli wa hapa duniani
aliyenacho anaishi na asiyenacho anaisha, tunamzungumzia Rais Donald Trump na ukweli
wa mwenye nacho anakula na asiyenacho anatoa vyombo, Tunamzungumzia Rais Donald
Trump na ukweli wa historia ya mtu inamchango mkubwa katika kutoboa kimaisha au
kutoboka kimaisha kwa sababu maji hufuata mkondo na huo ndio ukweli sema siku zote
ukweli unamarafiki wachache na maadui wengi!
Trump hakuanzia from zero to hero kama matajiri wengi wa bongo, Trump alianzia from
hero to hero. Utajiri wake umeanzia kwa babu yake Frederick Trump ambaye alikuwa
mfanyabiashara maarufu mwenye asili ya Kijerumani. Babu alitoka Ujerumani akiwa na umri
wa miaka 16 baada ya kukwepa kwenda jeshini. Alifika Marekani mwaka 1885 na kuwa
fundi kinyozi. Baadaye mzee alifungua biashara ya restaurant na madanguro huko Canada
akatajirika haraka kwa sababu biashara haramu hazidanganyi. Mwaka 1891 Babu alirudi
Ujerumani akavuta mke lakini wakamtimua kwa sababu alikwepa jeshi, jamaa akasema isiwe
tabu maisha ni popote, akarudi zake Marekani kuendelea na maisha akatajirika mazima
kupitia biashara ya majengo. Sasa mwenzangu umeng’ang’ania kwenu, maisha yamekupiga,
hutaki kutoka ati utaambiwa mkataa kwao ni utumwa.
Katika tumbo la babu yake Trump walizaliwa watoto watano akiwemo baba yake Rais
Donald Trump yaani Mzee Frederick Christ Trump. Baba yake Rais Donald Trump alizaliwa
Oktoba 11, 1905 na kufariki June 25, 1999 akiwa na umri wa miaka 94. Mzee Frederick
Christ Trump aliendeleza kazi ya baba yake Real Estates na kutikisa kwa utajiri katika jiji la
New York. Ni katika familia hiyo ya kitajiri akazaliwa Rais Donald Trump ambaye ndo topic
yetu ya leo. Trump alizaliwa June 14, 1946 na kupokea kijiti cha utajiri na kukimbia nacho
hadi kuandika jina lake kwenye kitabu cha mabilionea duniani kwa sababu ukoo wao
walibarikiwa akili za kuendeleza mali za familia tofauti na huku kwetu matajiri wengi
wanakufa na mali zao na watoto wao kutembelea kucha na wengine kuuana kwa mali
alizoacha baba.
Trump alikulia katika mji ya Jamaica jirani kabisa na jiji la Queens nchini Marekani
alikosoma kuanzia awali hadi la saba pale Kew – Forest School. Amekuwa mtukutu tangu
utoto wake kwa hiyo usidhani anayoyafanya leo yalianza leo. Trump akiwa na umri wa
miaka 13 alihamishiwa shule ya Jeshi walikomnyosha, siunajua jeshi si lele mama?
Waliosoma shule za jeshi wanajua. Kule ni ndiyo afande ndo maana wanajeshi wengi ni watu
wema kweli tatizo ukiwachokoza ndo utajua kumbe nyuki ni nzi aliyeserious na maisha.
Mwaka 1964 Trump alijiunga na Chuo Kikuu cha Fordham na baada ya miaka miwili
alihamia Wharton School, Pennsylvani University. Akiwa chuoni alifanya kazi kwenye
kampuni ya familia, iliitwa Elizabeth Trump & Son. Nchi za wenzetu wana utaratibu mzuri,
unasoma na kufanya kazi, sisi huku ukianza kusoma ni kusoma tu ndo maana tunahitimu ni
maskini sana halafu wanyonge. Mei 1968 alihitimu masomo yake na kujipatia shahada ya
Sayansi na Uchumi. Halafu aliongoza katika mitihani yake ya mwisho lakini jamaa
hakuhudhuria kabisa mahafali na hakutunukiwa zawadi ya kuwa mwanafunzi bora
darasani.Lakini sishangai maana wazungu graduation siyo muhimu kama kule kwenu mtu
akigradate kijiji kizima kinasafiri kwenda kushuhudia.
Halafu Trump hakutaka kabisa matokeo yake yatoke hadharanini na wakati Baba Koku
katundika matokeo yake sitting room. Mwahasheria wake Michael Cohen alitishia kuchukua
hatua za kisheria endapo kama chuo cha Fordham pamoja na New York Millitary Academy
watachapisha matokeo ya mteja wake. Hivyo matokeo ya Donald Trump yakabaki tetesi tu
mara Trump hivi mara vile hadi leo matokeo yake hayajulikani. Hawa jamaa wamestaarabika
sana. Huku kwetu ukitaka matokeo ya mtu yoyote unayapata kirahisi rahisi tu hata kama
ulipata sifuri, ndo maana kama ulichemka darasani ukapata uongozi jitahidi usiwe na
mbwembwe maana watakuvua nguo.
Katika maisha yake Donald trump ilibaki kidogo awe mwanajeshi pamoja na kwamba
alisoma shule ya jeshi. Mwaka 1966 alipimwa afya yake na kuonyesha anafaa kwenda
jeshini lakini alipomaliza shule mwaka 1968 vipimo vilionyesha anahitilafu ya kiafya.
Nadhani ni ule ubabe wake. Imagine kwa akili za Trump angekuwa mwanajeshi siangetafuna
watu? Lakini kitu cha kushangaza pamoja na machachari yote Trump hajawahi kuvuta bangi,
sigara, kunywa pombe wala kutumia madawa ya kulevya. Yeye anasema anayaogopa sana
madawa ya kulevya kwa sababu yalimuua kaka yake mkubwa, Fred Trump. Fred alifariki
akiwa na umri wa miaka 43 familia ikapata pigo. Si kawaida kwa mtu maarufu aliye na pesa
nyingi na shughuli zake nyingi akiwa na wanawake warembo,vinywaji vya kila aina na safari
zake nyingi kutopiga pombe na fegi.
Kilevi chake kikubwa ni wanawake. Mpaka anaingia Ikulu Trump ameweka rekodi ya
mkristo kufunga ndoa mara tatu. Ndoa yake ya kwanza alifunga na mlimbwende Ivana
Zelnickova na kubarikiwa watoto watoto watatu; Donald Trump Jr, Ivanka pamoja na Erick.
Mwaka 1992 ndoa ikavunjika baada ya Trump kujulikana kuwa na mahusiano na muigizaji
mrembo Maria Maples. Mwaka uliofuata akafunga ndoa na mchepuko na kubarikiwa mtoto
mmoja, anaitwa Tiffany Aliana Trump halafu baada ya miaka sita ndoa ikala chali cha
mende, bilionea likakaa bila likakaa single miaka sita, likafunga ndoa na mlimbwende
mwingine, Slovenia Melania Knauss ambaye ndo First Lady Marekani. Trump na Fird Lady
wake wana mtoto mmoja wa kiume, anaitwa Barron. Dogo ndo anafaidi vya Ikulu.
Sasa Trump ni babu wa wajukuu kumi na bado yuko strong. Halafu hafanyi mazoezi kabisa.
Mara nyingi mazoezi wanafanya wasiokuwa na pesa. Nimesema mara nyingi na siyo mara
zote. Trump anasema mwili wa binadamu ni kama betri hutengenezwa na nguvu ya kiwango
maalumu hivyo kufanya mazoezi kunapunguza nguvu na si kuongeza. Disemba 2015 ilitoka
ripoti juu ya afya yake kutoka kwa daktari wake binafsi ikisema Trump ndiye mtahiniwa wa
urais mwenye afya bora kuwahi kutokea nchini Amerika, miaka mitatu baadae yaani 2018
daktari yuleyule aliyetoa ipoti kuhusu afya yake alisema kuwa ripoti ile ya awali Trump
ndiye alisema iandikwe vile.
Nachompendea Trump ni ili kujikubali kupita maelezo. Kwenye moja kampeni zake za
uraisi aliwahi kusema duniani kuna vitabu bora viwili tu, cha kwanza ni Bibilia na cha pili ni
kitabu alichoandika yeye, kinaitwa ‘Art of the deal.’ Ukiwa na spirit hii huku kwetu watu
watakwambia unajishaua hata kama hawakulishi.
Trump amekuwa milionea tangu akiwa na umri wa miaka nane na wakati sisi katika umri huo
badao unamlilia mama king’amuzi kimeisha unamiss cartoon za Tom na Jerry. Aliwahi
kuazima dola milioni 60 za kimarekani kutoka kwa baba yake mzazi na hakulipa deni hilo.
Lakini yeye huwa anakanusha hilo na kusema utajiri wake wote umetokana na mkopo wa
dola milioni moja kutoka kwa baba yake na mkopo huo alipaswa kurudisha kwa riba. Hapa
nadhani hoja siyo mkopo, hoja ni jinsi alivyotumia pesa hiyo kutoka kwa baba yake na
kuizalisha badala ya kuhonga. Mimi namuheshimu huyu jamaa kwa kuendeleza utajiri wa
familia. Nakumbuka mwaka 1971 alitwaa wa kampuni ya familia na kuibadili jina kutoka
Elizabeth Trump & Son hadi The Trump Organization na mwaka 1978 lilianza kushika kasi
kwenye magazeti ya Marekani. Hizi ndizo akili.
Alitumia kiasi cha dola milioni 400 kukarabati Commodore Hotel na kuipandisha hadhi ya
juu zaidi na kuibadili jina hadi Grand Hyatt Hotel. Alichofanya ni kuongeza thamani ya kitu,
akaongeza mapato. Hapa kuna la kujifunza. Trump akajenga jengo lake maarufu la Trump
Tower katikati mwa jiji la Manhattan na hapo ndipo yalipo makao makuu ya Trump
Organization. Trump aliendelea kujenga manjengo mengine ya kifahari kama vile Trump
Place,Trump World Tower, Trump International Hotel and Tower na mengine kibao kwa
sababu kichwa chake kilichaji sana. Labda kwa sababu hakuvuta fegi na bangi?
Trump aliendeleza akili za babu yake aliyewekeza nchi mbalimbali, maana amejenga
Mumbai, Instabul na Ufilipino, tembelea nchi hizo utayakuta majengo hayo tena kwa jina
lake. Truma kawekeza sana katika burudani, hasahasa katika maswala ya ulimbwende,
mitindo, fasheni na kasino. Mwaka 2003 alianzisha kipindi cha Televisheni katika channel ya
NBC na kulipwa hadi dola milioni 213 na channeli hiyo wakati kipindi chake kinaporuka.
Mshikaji ana biashara hazi za ‘neckties’ na maji ya chupa. Kwake kikupwa utajiri. Trump
anakwambia yeye anautajiri wa dola bilioni 10.
Trump ameandika rekodi ya kuwa Rais tajiri kuliko Marekani wote waliotawala nchi hiyo
lakini mwenye uzoefu mdogo wa kisiasa kuliko marais wote. Trump anamiliki biashara zaidi
ya hamsini zenye leseni ya jina lake anamiliki biashara za fenicha, Vyakula, na vyuo vya
masomo ya watu wazima ambavyo kwa ujumla humuingizia zaidi ya dola za kimarekani
milioni 59 kwa mwaka. Licha ya utajiri wote huo Trump anaandamwa sana na tuhuma za
ukwepaji kodi kwa sababu pesa ni mwanaharamu, pesa haijawahi kutosha.Lakini pia akakesi
kibao za ubaguzi kwenye biashara zake. Mpaka mwaka 2018 kampuni zake zote tayari
zilikuwa zimehusika kwenye kesi 4000.
Licha ya kwamba yeye binafsi hajawahi kuripotiwa kufirisika lakini Casino zake na pamoja
na Hotel katika jiji la New York na Atlantic City zimewahi kufirisika mara 11 kati ya mwaka
1991–2009.
Trump pia ni mwandishi wa vitabu na kupitia uandishi huo ameiga pesa nyingi tu. Kitabu
chake cha ‘The Art of the Deal’ cha mwaka 1978 kiliwahi kuwa kitabu kilichouzwa zaidi
kwa wiki 48 mfululizo. Kitabu hicho kilimpa jina na heshima kubwa sana Trump na
alijulikana sana duniani kama mtaalamu wa kufanya mijadala yenye faida kwenye biashara.
Hata kwenye mieleka nako yumo. Alipewa heshima ya kuingizwa kwenye WWE Hall of
fame. Trump alibakiza kitu kimoja tu, kuwa rais wa Marekani na hiyo imekuwa ndoto yake
kwa muda mrefu na kweli ikatimia pamoja na kwamba hakuwa na uzoefu wa siasa. Katika
hili anatufundisha kwamba kuna muda huhitaji uzoefu kuomba kazi, unahitaji tu kujiamini na
kujitoa kwa moyo wako wote, uzoefu utakutana nao hukohuko kazini.
Ndoto ya Trump kuwa raisi haikubebwa na itikadi ya chama cha siasa, bali ilibebwa na nia
ndani ya moyo wake kwakuwa alishahama vyama vya siasa mara kadhaa. Trump alijiunga
rasmi na chama cha Republican mwaka 1987, ila akaona itikadi zake na zao hazilandani, basi
akahamia Reform Party mwaka 1999, hata hawa akawahama na kujiunga na Demokratic
2001, ila hata Demokratic hakudumu sana mwaka 2009 akarudi Republican.
Mwaka 2000 Trump alithubutu kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni akiwa na
chama cha Reform Party kuutafuta Urais akapigwa chini. Uthubutu wa Trump 2000 ulimpa
ujiko wa kisiasa, ikadhaniwa kuwa angegombea kwenye chaguzi za 2012, lakini
hakugomeba. Harakati za Trump kuutaka urais wa Marekani ziliamka tena kwa kuusakama
utawala wa Barack Obama. Alikosoa sana sera za Barack Obama, hasa swala la uhamiaji,
sera ya mashariki ya kati, swala la afya la taifa la marekani na hata usalama kwa ujumla wea
taifa hilo.
Trump alionekana kujipanga zaidi kutaka kuliongoza taifa la Marekani, inasemekana alitumia
zaidi ya dola milioni moja sawa na bilioni mbili za kitanzania kufanya utafiti juu ya
uwezekano wa yeye kuwa Rais. Oktoba 2013 chama chake cha Republican kilimpendekeza
kugombea ugavana katika jimbo la New York akataa, yeye akasema anautaka urais. Juni 16,
2015 Trump alitangaza rasmi nia kugombea urais wa Marekani. Matangazo haya yaliruka
moja kwa moja kutoka kwenye jengo lake la kifahari la Trump Tower jijini Manhattan.
Trump alipigilia msumari kwa Alinadi sera zake kuhusu uhamiaji haramu, kulinda ajira za
Marekani kwa ajili ya Wamarekani, Uislamu na ugaidi pamoja na deni la Marekani. MAKE
AMERICA GREAT AGAIN ndo ilikuwa kaulimbiu yake.
Alitangaza kujifadhili kwenye kampeni zake zote ili kuepuka mashinikizo kutoka kwa
wafadhili mbalimbali. Rais Trump hakuacha kutupa makombora mazito kwa Rais Barrack
Obama,akidai Obama si raia wa Marekani. Lakini baadaye alikiri kuwa hakuna ukweli
wowote kwenye shutuma hizo dhidi ya Obama, ila hakuomba radhi kwa hilo kama
alivyofanya Mchungaji Msigwa kwa Kinana .
Trump alipoonyesha nia ya urais, watu walifukua makaburi ya tangu mwaka 2005 ya
rekodiza vitendo vya manyanyaso dhidi ya wanawake hadi watu wa chama chake wakasema
Trump bado si mtu sahihi kuwa raisi wa Marekani lakini jamaa alilamba urais kwa sababu
aliyenacho huongezewa hata kama ni mshenzi. Walichuana vikali na Hillary Clinton, mwana
mama aliyekuwa na uzoefu mkubwa sana katika siasa. Mama alikuwa anachukua nchi lakini
FBI walimmaliza baada ya kufichua matumizi mabaya ya ofisi ya serikali aliyofanya Hillary
Clinton wakati akiwa Waziri wa mambo ya nje. Hillary alitumia barua pepe binafsi kufanya
mawasiliano ya kiserikali, tena mawasiliano ya siri za hali juu ya taifa hilo, siri ambazo kama
zingedukuliwa na maadui zao basi zingehatarisha usalama wa Marekani.
Kampeni za Trump wakati wa uchaguzi zilzungumzia sana biashara kati ya China na
Marekani, mikataba mikubwa ya kibiashara kama vile NAFTA na TPP, kubadilisha sera na
sheria za uhamiaji hasa kwa watu kutoka nchi za kiislamu na hata kujenga ukuta kati ya
Marekani na Mexico. Sera zake zilizua taharuki na hasira kwa wengi, wamamuita mbaguzi
wa rangi, wengine wakamuita punguani lakini jamaa bado akawa rais wao, yaani
wasiompenda alikuja.
Wakati wa kampeni zake Trump aliweka dhahiri utajiri na mali anazomiliki, lakini aligoma
kutoa hadharani rekodi kodi, alifanya kinyume na ahadi yake ya mwaka 2014 – 2015
alipotamka hivyo ya kwamba atafanya hivyo akigombea uras. Walipozidi kumshinikiza kutoa
taarifa, Trump aliwajibu kuwa taarifa za kodi zake haziwahusu, hivyo watafute kazi nyingine
za kufanya na yeye ataendelea kila siku kutafuta njia za kulipa kodi ndogo kadiri awezavyo.
Novemba 8, 2016 Trump alishinda kiti cha urais na kuapishwa Januari 20, 2017, akaandika
historia ya kuwa Rais Mzee zaidi kuwahi kutokea Marekani, Rais tajiri zaidi kuwahi kutokea
Marekani, Rais wa kwanza Marekani ambaye hajapitia jeshini na Rais wa kwanza ambaye
hajawahi kushika wadhifa wowote serikalini.
Tangu Trump aingie madarakani, urais kwake umekuwa kazi ngumu kutokana na
kushambuliwa kila siku juu ya sera zake pamoja na aina yake ya uongozi. Trump
ameshutumiwa mara nyingi kuwa mbaguzi wa rangi. Januari 2017 CIA, NSA na FBI, walitoa
ripoti ya pamoja kuwa Urusi iliingilia uchaguzi wa marekani kumuweka Trump madarakani.
Pamoja na kelele zote hizo jamaa hayumbishwi na kelele za watu, kwa sababu “Kelele za
chura hazimzuii ng’ombe kunywa maji.”

You might also like